Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, lini Serikali itaongeza posho za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji?
Supplementary Question 1
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina mwaka wa nane hapa Bungeni, sijawahi kuona mjadala wowote wa kupandisha posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Napenda Mheshimiwa Waziri atueleze, ni lini mara ya mwisho Serikali ilipitia…
SPIKA: Mheshimiwa, hujawahi kuona nini? Samahani.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, sijawahi kuona mpango wa Serikali kupandisha posho za viongozi hawa. Napenda kujua, ni lini mara ya mwisho Serikali ilipitia posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Mama Samia amepeleka fedha nyingi sana vijijini na zinahitaji umakini wa usimamizi ili miradi iweze kukamilishwa kiukamilifu.
Je, kwa mwaka wa fedha ujao 2024/2025 Serikali ipo tayari kuongeza posho ya Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa ili kupunguza kelele za viongozi hawa? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza namuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwamba katika Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Ofisi ya Rais - TAMISEMI katika mjadala ambao Waheshimiwa Wabunge waliujadili kwa kina sana, ilikuwa ni uwezekano wa kuongeza posho za Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti, na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, Bunge hili limeshajadili sana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tulipokea, nimhakikishie kwamb lini posho hizi zilipandishwa, posho za Waheshimiwa Madiwani zilipandishwa. Nitakwenda kuona exactly ni lini lakini nafahamu kwamba zilipandishwa kutoka zilipokuwa, kidogo lakini sasa angalau ziko na hali nzuri.
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba zinahitajika kuongezeka zaidi ili ziweze kukidhi mahitaji na safari ni hatua. Serikali inaendelea kulitazama na kuona uwezekano huo wa kupandisha posho za Waheshimiwa Madiwani.
Mheshimiwa Spika, pili, katika mwaka ujao wa fedha, kama tutaongeza posho hizo au vinginevyo. Tumelichukua, Serikali itafanya tathmini na kuona uwezekano huo na itatoa taarifa rasmi kama linawezekana ama tunahitaji kuijengea uwezo ili kuweza kuongeza posho hizo, ahsante sana.
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, lini Serikali itaongeza posho za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji?
Supplementary Question 2
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa uzoefu ambao nimeupata kujifunza kwenye halmashauri mbalimbali nchini, kumekuwa na halmashauri nyingi ambazo zinavuka na bakaa kwa maana ya salio.
Je, Serikali haioni ni wakati sahihi kuzielekeza halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kuwaongeza Madiwani kwa sababu sehemu kubwa Serikali imechukua mzigo huo na halmashauri nyingi zimekuwa zikivuka na bakaa na salio?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kweli kuna baadhi ya halmashauri zimekuwa zikivuka na fedha katika mwaka wa fedha unapoisha kwenda mwaka mwingine kwa maana ya bakaa na Mheshimiwa Mbunge anapendekeza kwamba salio lile litumike kwa ajili ya kuwalipa nyongeza posho Waheshimiwa Madiwani, lakini niseme zile fedha ambazo zinavuka mwisho wa mwaka wa fedha mara nyingi ni fedha za miradi ambayo inasubiri kutekelezwa. Kwa hiyo, ni fedha ambazo tayari ziko committed, lakini zinakwenda kutekeleza miradi ile katika first quarter ya mwaka wa fedha unaofuata.
Mheshimiwa Spika, jambo la msingi ni kwamba tunajua kuna umuhimu wa kuongeza posho Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni jambo ambalo tutaendelea kulifanyia kazi na kadri uwezo wa Serikali utakapoongezeka suala hilo litaendelea kushughulikiwa, ahsante.
Name
Neema Kichiki Lugangira
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, lini Serikali itaongeza posho za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji?
Supplementary Question 3
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ningependa kufahamu je, Serikali ipo tayari kupitia upya posho kwa ajili ya vikao vya Madiwani kwa kuzingatia umbali wanakotoka kwa sababu kama Wilayani Muleba tunazo Kata tano Boziba, Kerebe, Rubale, Ikuza na Mazinga ambazo ni za visiwani lakini Waheshimiwa Madiwani wakienda kwenye vikao wanalipwa posho sawa na wale ambao wanatoka pale pale mjini wakati wao wakienda kwenye vikao inawalazimu walale kutokana na umbali? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishatoa mwongozo wa posho za kujikimu kwa Waheshimiwa Madiwani wanapohuduhuria vikao vya mabaraza na mwongozo ule ulizingatia wale ambao wanatoka mbali wanahitaji kulala, rate zao zilikuwa ziko tofauti na wale ambao wanatoka eneo la jirani hawahitaji kulala rate zao ziko tofauti.
Kwa hiyo, nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwasisitiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Halmashauri zote kuzingatia mwongozo ambao uko very clear na unaelekeza wanaotoka mbali wanatakiwa kulipwa kiasi gani na wale wanaotoka jirani wanatakiwa kulipwa kiasi gani, ahsante.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, lini Serikali itaongeza posho za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji?
Supplementary Question 4
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona, kwa kuwa Serikali imeondoa mzigo ule wa kulipa posho za Madiwani kutoka kwenye Halmashauri na Serikali Kuu sasa ndio inayolipa hizo posho; je, Ofisi ya Rais, TAMISEMI iko tayari sasa kuelekeza kwamba zile posho zilizokuwa zinalipwa kwa Madiwani sasa zielekezwe kuwalipa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 alichukua jukumu la Serikali Kuu kulipa posho za Halmashauri 168 kote nchini na kazi hii inaendelea.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba halmashauri hizi siku za nyuma zilikuwa zinalipa posho za Madiwani, lakini zile fedha zimeendelea pia kupelekwa kwenye maeneo ya miradi mbalimbali. Naomba tuchukue wazo la Mheshimiwa Mbunge kwamba tuone kama zinaweza zikapelekwa kwenye malipo ya Serikali za Vijiji na Mitaa, tutafanya tathmini tuone kama inaweza kutekelezwa ama vinginevyo na tutaleta taarifa rasmi, ahsante.
Name
Boniphace Nyangindu Butondo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, lini Serikali itaongeza posho za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji?
Supplementary Question 5
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na ukiukwaji wa kikanuni na hasa kuhusiana na suala zima la ziara ya Kamati za Kudumu za Madiwani na kwamba kila robo ya mwaka Kamati za Kudumu zinatakiwa kutembelea na kuona miradi iliyotekelezwa katika kipindi hicho, ili kuona kwamba fedha zinazotumwa na Serikali chini ya Mama Samia Suluhu Hassan zinasimamiwa na kuona ile value for money. Sasa Finance Committee peke yake imekuwa ikienda kwenye ziara hii kinyume na kanuni na Kamati nyingine za kudumu zisiende…
SPIKA: Swali lako.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nini tamko la Serikali kuhusiana na changamoto hii?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ziara za Kamati za Kudumu za Waheshimiwa Madiwani katika Baraza la Madiwani zimewekwa kwa mujibu wa mwongozo ambao umeelekeza Kamati ya Fedha kutembelea miradi, lakini pia Kamati za Kudumu nyingine kama Huduma za Elimu, Afya na Maji na nyingine kutembelea miradi pia kuona utekelezaji wa miradi ile.
Kwa hiyo, nitumie fursa hii pia kuwasisitiza Wakurugenzi na Mabaraza kuzingatia Mwongozo wa Serikali ambao umetolewa ili kuweza kuwa na ufatiliaji wa karibu wa thamani ya fedha katika miradi ambayo inatekelezwa, ahsante.