Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, mchakato wa ujenzi wa geti jipya la kuingilia Hifadhi ya Mikumi kutokea Kilangali na Tindiga umefikia hatua gani?

Supplementary Question 1

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Sera ya Ugatuaji ni Sera ya Kitaifa. Suala la mapato ya taasisi zetu na maduhuli ya Serikali kwenda moja kwa moja hazina inaenda kinyume na hii Sera ya ugatuaji. Ndio inayosababisha miundombinu muhimu kwenye hifadhi zetu kutotengenezwa mara kwa mara. Je, Serikali haioni wakati umefika sasa wa kurudisha walau asilimia 20 ya mapato kwenye hifadhi zetu, ili washughulikie miundombinu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Serikali inakiri kufunguliwa kwa geti hili katika Kata ya Kilangali na Tindiga kunaenda kufungua fursa za kiuchumi. Je, wamewaandaa vipi wananchi wa Kata za Tindiga, Dhombo, Masanze na Kilangali, ili wasije kuwa wageni wakati fursa hizi ambazo zitatokana na kufunguliwa kwa lango hili zitakapowadia? Nashukuru. (Makofi)

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya kukamilika kwa miundombinu kwenye maeneo yetu kutokana na kukosekana kwa fedha na mabadiliko tuliyokuwa tumefanya ya mfumo wa kukusanya mapato na kuyapeleka moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Hata hivyo, baada ya jambo hili kujadiliwa kwa kina ndani ya Bunge lako Tukufu na jambo hili kufikishwa Serikalini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kurejesha tozo ya maendeleo ya utalii ambapo tayari Mheshimiwa Rais ameridhia asilimia tatu ya fedha hizi iweze kutumika kwa ajili ya shughuli hizi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili; jukumu la kutoa elimu kwa wananchi wetu sio jukumu la Serikali Kuu peke yake ni pamoja na halmashauri zetu. Nitoe rai kwa halmashauri husika ziweze kutoa elimu kwa wananchi, tukiwepo sisi Waheshimiwa Wabunge, ili wananchi waweze kuchangamkia fursa za kimaendeleo zinazokuja katika maeneo yetu.

Name

Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, mchakato wa ujenzi wa geti jipya la kuingilia Hifadhi ya Mikumi kutokea Kilangali na Tindiga umefikia hatua gani?

Supplementary Question 2

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha lango la kuingia Mlima Kilimanjaro la Kidia kwani lango hili litakuwa linatumiwa na watu maarufu kupanda Mlima Kilimanjaro?

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika kuongeza mapato katika nchi yetu. Kwa hiyo, ni makusudio ya Serikali kuboresha malango katika hifadhi zetu zote za Taifa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, katika hili la Kidia, tayari Serikali inaendelea na kuboresha eneo lile. Tayari tunavyozungumza barabara ya kilometa karibu 28 ya watembea kwa miguu kwenye eneo lile imeboreshwa. Barabara karibu kilometa tisa inajengwa kwa kiwango cha changarawe na katika bajeti ya mwaka huu kupitia TANAPA zimetengwa karibu milioni mia tisa kwa ajili ya kujenga mageti kwenye eneo hilo.