Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Samweli Xaday Hhayuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Primary Question
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:- Je, lini barabara ya Hilbadaw – Bashnet itahamishiwa TANROADS?
Supplementary Question 1
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara hii ambayo inapita Lukhumeda – Setet kwa upande wa Babati, ambayo kwa Hanang inapita Bassodesh – Dang’aida – Hilbadaw, lakini ukienda upande wa Singida inaenda Singa – Ilongero – Singida, imejadiliwa kwenye kikao cha Bodi ya Barabara mwaka 2021. Hapa Bungeni nimeshaisema hii barabara zaidi ya mara tano; je, Serikali ina kauli gani juu ya nini kifanyike ili barabara hii iweze kufanyiwa kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022, tuliongeza bajeti ya TARURA kwa uwiano kwa majimbo yote, lakini kwa majimbo yale makubwa ambayo mtandao wa barabara ni mkubwa, fedha hizi ni kidogo; kwa mfano kwa Hanang tuna kata 33 na vitongoji 414; je, Serikali ina kauli gani kuziongezea bajeti zile Halmashauri kubwa au majimbo makubwa?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Hhayuma, hili la kwanza la kauli ya Serikali juu ya barabara hii ya Hilbadaw – Bashnet iliyopo kule Hanang kupandishwa hadhi; kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi, hili ni takwa la kisheria la kupitisha barabara hii kwenye vikao hivi. Mheshimiwa Mbunge ameshasema barabara hii ilipitishwa mwaka 2021, hivyo basi, kwa sasa litakuwa chini ya Waziri mwenye dhamana na barabara ambaye ni Waziri wa Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitakiwa timu ije kufanya tathmini ya barabara hiyo kabla ya kuipandisha hadhi na kumshauri Waziri wa Ujenzi. Kwa hiyo, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi na kuona hili limekwamia wapi? Pale lilipokwamia basi hatua ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu uwiano wa bajeti ya barabara za TARURA katika majimbo mbalimbali hapa nchini, ikiwemo na Jimboni kwake Hanang; hapa wakati najibu swali mojawapo la nyongeza, nilisema tayari kuna timu ambayo inafanya tathmini ya maeneo yetu hapa nchini juu ya bajeti ya barabara ambayo inatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa TARURA ilirithi mfumo ule ule uliotoka kwenye Bodi ya Barabara wakati taasisi hii inaanzishwa. Tathmini ile itakapokamilika kuangalia maeneo ya kijiografia, kiuchumi na masuala ya kilimo yanayotokana na maeneo mbalimbali hapa nchini, basi formula mpya itatolewa. Kama nilivyosema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, analifanyia kazi na timu yake muda siyo mrefu itamshauri.
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:- Je, lini barabara ya Hilbadaw – Bashnet itahamishiwa TANROADS?
Supplementary Question 2
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Manispaa ya Moshi, barabara inayotoka YMCA kwenda KCMC ni barabara ambayo ina msongamano mkubwa sana. Kuna Chuo cha Ushirika, kuna Chuo cha CCP Moshi na kuna Chuo Kikuu cha Katoliki, lakini kwenda pale hospitali kwenyewe watu wanaoenda kuona wagonjwa wanachelewa na wakati mwingine pia wanapata matatizo; bajaji zimo humo humo, bodaboda zimo humo humo, vi-hiace na hata magari binafsi; kutokana na majibu ya msingi, kwamba vikao vifanyike na ni matakwa ya sheria, vyote vimeshafanyika: ni lini Serikali itaona umuhimu na udharura wa kubadilisha barabara hiyo kutoka TARURA kwenda TANROADS? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya YMCA kwenda KCMC katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi. Tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kuona hatua zipi ambazo wamezifikia katika kwenda kupandisha hadhi barabara hii kuwa barabara ya mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo awali kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba haya ni matakwa ya kisheria, na yakishapita kutoka kwenye vikao hivi vyote na vikipitishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa ambaye ni Mkuu wa Mkoa, sasa yanakwenda kwenye mamlaka ya Waziri wa Ujenzi ambaye ndiye mwenye dhamana ya barabara. Kwa hiyo, Serikali inalichukua na tutakaa na wenzetu wa barabara kuona imefikia wapi?
Name
Noah Lemburis Saputi Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Primary Question
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:- Je, lini barabara ya Hilbadaw – Bashnet itahamishiwa TANROADS?
Supplementary Question 3
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Arumeru Magharibi hivi karibuni mvua kubwa zimenyesha na kuharibu miundombinu kweli kweli yakiwemo madaraja, barabara na sasa wananchi hawana mahali ambapo wanapita katika maeneo haya ambapo yalitakiwa kujengwa maradaja mapya.
Ni lini sasa Serikali itapeleka hizo fedha za dharura ambazo tumeziomba kwa ajili ya kuokoa wananchi ambao hawana jinsi ya kwenda shambani, hospitali au popote wanapohitaji kupata huduma?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) inaangalia namna ya kupata fedha za ziada za dharura. Bajeti ya TARURA kwa ajili ya dharura kwa mwaka ni shilingi bilioni 11. Kama nilivyosema hapo awali, tayari Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Kairuki, ameshakaa na Waziri wa Fedha kuona ni namna gani TARURA inaweza ikaongezewa fedha za dharura kwenda shilingi bilioni 46 ili barabara hizi zilizoharibika katika kipindi hiki cha mvua ziweze kutengenezwa, zikiwemo hizi za kule Arumeru Magharibi kwa Mheshimiwa Lemburis. Pale ambapo Wizara ya Fedha itaridhia TARURA kuongezewa fedha hii, basi barabara hizi zitaanza kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nimalizie tu kwa kusema kwamba tunakwenda kuanza kutekeleza mwaka mpya wa fedha mwezi mmoja na siku kadhaa zijazo (mwezi Julai), hivyo basi, wataona barabara hizi zitengenezwe katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:- Je, lini barabara ya Hilbadaw – Bashnet itahamishiwa TANROADS?
Supplementary Question 4
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika kikao cha Barabara cha Mkoa wa Kilimanjaro na Kikao cha RCC cha Mkoa wa Kilimanjaro, tulipitisha barabara kadhaa tangu mwaka juzi kupandisha hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS; na tayari kikoa cha mwisho cha RCC Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alituambia ameshawasilisha Wizarani ili barabara hizi ziweze kupandhishwa hadhi.
Je, ni lini sasa barabara hizi za majimbo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro na Hai zitapandishwa hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni takwa la kisheria kwamba barabara hizi na vikao vyote vinavyokaa kule vya kisheria katika ngazi ya wilaya na mkoa zinafikishwa kwa Waziri mwenye dhamana na barabara ambaye ni Waziri wa Ujenzi. Hivyo, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kuona ni hatua zipi ambazo zimefikiwa na kupandisha hadhi barabara hizi za Mkoa wa Kilimanjaro, na Jimbo la Hai kule kwa Mheshimiwa Saashisha.