Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Primary Question

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa wanashiriki mafunzo ya JKT ya muda mfupi?

Supplementary Question 1

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naipongeza Serikali kwa nia yake ya kuwa tayari kwa mafunzo haya, na Wabunge wengi tulioenda katika yale mafunzo tulikuwa tunapata maswali mengi sana ya Wakuu wa Idara na baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wanaotaka kwenda kwa kujitolea, walikuwa wanauliza ni utaratibu gani ambao wanaweza kuufuata ili kushiriki mafunzo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Kambi ya Makutupora hapa, imetupa mafunzo mazuri sana na tunatoa ombi kwa Wabunge ambao hawajaenda waende kwa sababu kila siku wanatuambia kwenye group kwamba vifaa vyao viko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili ya nyongeza. La kwanza: Je, ni lini intake nyingine ya Wabunge na viongozi wa wilaya ambao wako tayari itaenda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kama nilivyosema, Kambi ya Makutupora iko hapa Dodoma, ni kaibu: Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha ya bajeti kwa sababu JKT ni taasisi ya Kiserikali ili Kambi ile jirani ya Makutupora iweze kutoa mafunzo vizuri zaidi na kwa ufanisi zaidi, ikiwemo kujenga mabweni, vitanda na kadhalika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara kadhaa wamekuwa wakienda kwenye kambi hizi kwa ajili ya kushiriki kwenye mafunzo haya ambayo yana nia ya kuwajenga Waheshimiwa Wabunge. Ni kweli kwamba wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hawajapata fursa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa niwaambie tu kwamba mara nyingi sababu zinazosababisha hizi, kwanza ni nafasi yetu sisi kama Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ya majukumu ambayo tunayo. Lingine kubwa ni kutokana na utaratibu. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kupitia Bunge hili, kama tulivyoeleza katika jibu la msingi, iombwe ruhusa, kwa maana ya kwamba tuombwe kibali maalum ili Jeshi la Kujenga Taifa liweze kutoa fursa hiyo ya Wabunge wengine kuweza kuendelea ama kupata mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme tu kwamba, kwa kuwa mafunzo haya yamelenga katika kuwajengea uzalendo, kuwajengea utayari, ukakamavu na ujasiri Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine wa taasisi nyingine, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyoelezwa katika jibu langu la msingi, kwamba suala la uchangiaji gharama ni jambo la msingi; na kwa sababu tunatakiwa tuchangie gharama hizi kwa sababu ya mahitaji maalum yakiwemo afya, matibabu, chakula na vifaa vingine, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayofuata tutajitahidi tuongeze fungu maalum kwa ajili ya kutoa huduma hizi za mafunzo kwa Waheshimiwa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.