Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cosato David Chumi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Primary Question
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Wavunaji na watumishi wa msitu wa Taifa Sao Hill wanapata huduma za kijamii na mahitaji yao katika Jimbo la Mafinga Mjini na kwa kuwa msimu uliopita hakuna kijiji au mtaa hata mmoja uliopata kibali cha kuvuna msitu katika Jimbo hilo:- (a) Je, Serikali iko tayari kutoa kibali cha kuvuna msitu kwa kila kijiji au mtaa ili fedha zitakazopatikana kutokana na vibali hivyo ziweze kusaidia shuguli za kuboresha huduma za jamii kama vile kuchonga madawati na kumalizia ujenzi wa zahanati? (b) Je, Serikali iko tayari kutoa vibali vya kuvuna misitu kwa vikundi rasmi vya wajasiliamali ili kuwasaidia kukuza mitaji yao na kujipatia maendeleo ya kiuchumi? (c) Je, ni kiasi gani cha fedha kimetolewa kama sehemu ya kurejesha hisani kwa jamii kutoka kwa kampuni ya misitu na viwanda vikubwa vya mazao ya misitu vilivyopo kwenye Jimbo la Mafinga na maeneo ya jirani?
Supplementary Question 1
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali inawauzia kiwanda cha Mgololo nusu ya bei 14,000 badala ya 28,000; je, Wizara iko tayari sasa kuwauzia pia wavunaji wadogo wadogo wa Mafinga na Wilaya ya Mufindi kwa ujumla nusu ya bei kama inavyouzia MPM?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kumekuwa na ujanja ujanja mwingi katika suala zima la utoaji vibali na kama nilivyosema jana tuko karibu na waridi lazima tunukie waridi; je, Wizara iko tayari sasa katika kutoa vibali, itoe by name and by location ili kusudi wakazi wanaozunguka msitu waweze pia na wenyewe kunufaika kwa kupata vibali hivyo badala ilivyo sasa orodha inaonesha kuna watu wanapata vibali lakini majina ya watu hao sio wanaozunguka msitu. Ahsante.
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusu nusu bei kwa kiwanda cha Mgololo na uwezekano wa kuuza kwa bei hiyo hiyo bidhaa hiyo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo au mwananchi mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili hoja yake ni miongoni mwa hoja kubwa, nzito zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti jana na kwa sababu hiyo maandalizi ya majibu ya kina yapo kwenye majawabu ya ufafanuzi wakati Mheshimiwa Waziri atakaposimama na nitakaposimama mimi. Sasa kwa kuokoa muda namwomba Mheshimiwa Mbunge asubiri wakati tutakapokuwa tunahitimisha hotuba jioni. Atapata majibu ya kina kuhusu swali hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la ujanja ujanja na uwezekano wa kutoa vibali kwa majina na kwa maeneo; jawabu ni kwamba jambo la msingi hapa linalohitajika ni uwazi. Wananchi wangependa kuona uwazi zaidi kuliko ilivyo sasa kwamba tutakapotoa takwimu kwamba watu gani wamepata mgao, basi ni vyema watu hao wakaonekana miongoni mwa jamii wazi wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nimetembelea kwenye shamba la msitu la Sao Hill moja ya mambo ambayo nilisema ni kwamba, kuanzia baada ya ziara yangu wakati utakapofika licha ya ule utaratibu wa kusubiri kupitia mwongozo mzima, hili moja ni la wazi kabisa kwamba tunakwenda kushirikisha Serikali tangu kwenye ngazi ya vitongoji na vijiji si tu kwamba kumtaja mtu mmoja mmoja lakini Serikali kwa ujumla wake kwa kutumia mfumo wake utashirikishwa katika zoezi zima la ugawaji wa malighafi hizi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved