Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kubadilisha utaratibu wa utoaji vibali vya kuvuna miti ili kuhusisha Kamati za Maendeleo za Kata na Vijiji?

Supplementary Question 1

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na uwepo wa mwongozo huo wa mwaka 2017, bado kumekuwepo na ongezeko kubwa la kuvuna miti kiholela. Hata wale ambao wanapatiwa vibali, anapewa kibali cha kwenda kuvuna miti mifu anakwenda kuvuna miti hai. Yametokea kwenye Vijiji vya Mshara na Uswaa, na Mto wote wa Makoa ule unaharibika: -

Je, hamuoni ni wakati sahihi sasa wa kuongeza nguvu wa kushirikisha ODC na mikutano mikuu ya vijiji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa mwongozo huu ni wa muda mrefu sasa, hamuoni ipo haja ya kufanya maboresho ya mwongozo huu ikiwa ni pamoja na kuongeza kipengele kwamba wale wanaopewa vibali vya kuvuna miti na wao wapewe miti kadhaa ya kupanda kwenye maeneo ambayo wanavuna miti?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuhusu hili ongezeko la ukataji miti hovyo, hususan kwa hawa wavunaji, ni kweli kumekuwa na ongezeko hili, lakini kwenye ile kamati tulitarajia kwamba mwongozo huu usimamiwe vizuri kwa sababu Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji ni mjumbe wa kamati ya uvunaji ya wilaya. Kwa hiyo tunatarajia anapoitisha vikao vya vijiji tayari wanakijiji wote wanakuwa wanajua kwamba eneo lao linakwenda kuvunwa, na ujumbe unaotoka kwa wanakijiji anauchukua mwenyekiti na anaingia kule kama mjumbe anaufikisha.

Mheshimiwa Spika, wakati huohuo kuna kamati ya mazingira na kamati ya maliasili ambazo ziko chini ya Serikali ya kijiji, zote hizi zinapitisha utaratibu wa namna ya kuvuna. Kwa hiyo sisi hatuoni kama kuna haja ya kubadilisha mwongozo, isipokuwa usimamizi wa ule mwongozo ndio tunatakiwa tuuboreshe zaidi, kwa maana ya kwenda chini na kufuatilia zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili suala la pili la kuangalia kipengele kwa wale wanaovuna, kwamba kuwepo na haja ya kurejesha, kwa maana ya kupanda miti; kuna asilimia tano ya mvunaji; anapokuwa ameshapata kibali cha kuvuna anarejesha asilimia tano na inarudishwa kwenye halmashauri ya wilaya. Ile asilimia tano ya fedha zinazotokana na uvunaji inakwenda kurudisha uoto wa asili kwa kupanda miti. Kwa hiyo tunazielekeza halmashauri kwenye ile fedha inayorudishwa ya uvunaji wahakikishe kwamba inakwenda kwenye matumizi ya upandaji miti ili kurudisha uoto wa asili.