Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa ithibati kwa baadhi ya pombe za kienyeji ambazo zimekidhi viwango?

Supplementary Question 1

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nataka kumweleza Mheshimiwa Waziri kwamba suala la pombe za kienyeji ni kwa lengo la kulinda viwanda vyetu vya ndani pia kulinda ubunifu wa watu wetu, kuongeza ajira na kuongeza uchumi kwa ajili ya kulinda mawazo ambayo yamezalishwa na wananchi wetu. Naomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka nimechangia hoja yangu ni mwezi umepita sasa. Je, ni upi mkakati wa Serikali kwa mwezi huu mmoja mmeshaanza kuzipatia leseni zile pombe ambazo mmezikataza kutumika kwenye jamii, mfano gongo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Je, kwa nini Serikali isiongeze kodi kwenye pombe zote ambazo zinaingizwa kutoka nje mithili hiyo ya spirit na pombe zingine ili kuzipa thamani pombe zetu za ndani na kuwavutia wawekezaji wote waje wawekeze kwenye pombe zetu za ndani ili tulinde soko letu la ndani na mawazo ambayo yametokana na watu wetu wa ndani? Ahsante. (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli tunajua mchango mkubwa sana wa sekta hii ya pombe na hasa pombe za kienyeji ambazo akina mama wengi ndiyo wanashiriki huku kama wajasiriamali kutengeneza pombe hizi za kienyeji na ndiyo zimekuwa nguzo na msingi mkubwa kulea familia katika kaya nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati madhubuti na ndiyo maana nimesema tumeshaweka mikakati mojawapo ni kuona namna gani tunawasaidia kuwafundisha na kuwawekea teknolojia sahihi ili waweze kuzalisha pombe za kienyeji zinazokidhi viwango na ambavyo vitakuwa havina madhara kwa wanywaji. Kupitia TBS kwa maana ya shirika la viwango na SIDO tumeshaweka fedha katika bajeti ambayo itatumika kama ruzuku kuwafundisha, kuwafuata kwanza wazalishaji wa pombe hizi za kienyeji kule waliko vijijini lakini kuwafundisha namna ya kuzalisha pombe ambazo zinakidhi viwango ili ziweze kuendelea kutumika katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zile pombe ambazo zilikuwa na madhara ambazo ndiyo wanasema zimepigwa marufuku tunataka tuwasaidie ili athari ile isijitokeze na baada ya hapo zitaruhusiwa kuendelea na kupewa ithibati ya ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali inafanya juhudi mbalimbali na hili ni dhahiri kwamba katika kuhakikisha tunafungua uchumi wa nchi yetu ni pmoja na kuruhusu biashara huru kulingana na taratibu na kanuni zilizopo, kwa maana ya kurusu pia bidhaa kutoka nje ya nchi kama vile ambavyo sisi tunauza nje ya nchi bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vyetu. Kwa hiyo, tunaendelea kuweka mkakati madhubuti kulinda viwanda vya ndani pale ambapo tutaona kwamba vinatakiwa kufanya hivyo na tumeshaanza kufanya na katika sekta hii ya pombe pia tutafanya hivyo ili kuwasaidia wananchi kunyanyua kipato lakini kuinua uchumi wa nchi yetu. Nakushukuru.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nilitaka tu nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge kwamba tumelipokea wazo lake la kuongeza kodi kwenye pombe na tutakamilisha kufanyia kazi na tutatoa majibu tutakapokuwa tunatoa kauli ya Serikali kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka huu. (Makofi)