Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Primary Question
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:- Mwaka 2013 Serikali iliuza hatifungani ya thamani ya Dola za Kimarekani milioni mia sita (USD 600m) kupitia benki ya Standard yenye tawi hapa nchini (Stanbic); Shirika la Corruption Watch la Uingereza kwa kutumia vyanzo kama IMF imeonesha kwamba hatifungani hiyo imeipa Serikali ya Tanzania hasara ya Dola za Kimarekani milioni themanini (USD) 80.m) na Serikali imelipwa faini Dola za Kimarekani milioni sita (USD Six Million) tu. Je, kwa nini Serikali haiichukulii hatua Stanbic Bank ili walipe faini zaidi?
Supplementary Question 1
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kati ya mwaka 2011/2012 mpaka mwaka 2015/2016, jumla ya fedha amba zo Serikali ilizikopa nje kwa mfumo wa namna hii ni shilingi trilioni 6.8. Katika taarifa ya hukumu ambayo Mheshimiwa Waziri amei-refer kwenye statements of facts ukurasa wa 17 aya ya 113 inaonesha kwamba mtindo huu wa kutumia vikampuni kwa ajili ya kuweza kupata mikopo umekuwa ukitumika na benki nyingi za biashara hapa nchini.
Serikali haioni kwamba imefikia wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aweze kufanya ukaguzi maalum wa mikopo yote ya kibiashara ambayo Serikali imeichukua kati ya 2011/2012 mpaka 2015/2016 ili kuweza kujua kama pia kulikuwa kuna aina za rushwa za namna hii ambazo zilikuwa zinafanyika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwamba DFA ambayo ndiyo hiyo hukumu ya Uingereza ilikuwa ina lengo la kuilinda Benki ya Uingereza ambayo ndiyo iliyotoa hongo kwa maafisa wetu ili iweze kupata biashara. Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa Serikali ifungue kesi dhidi ya benki hii ya Uingereza ili iwe ni fundisho kwa makampuni ya nje yanayohonga kupata biashara katika nchi za Kiafrika?
Name
George Mcheche Masaju
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Answer
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwanza, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anayo majukumu ya Kikatiba ya kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo, naomba kushauri tu kwamba hili ni jukumu lake anaweza akalitekeleza wakati wowote ili kujiridhisha kama mikopo hii ambayo imekuwa ikipatikana imekuwa ikipatikana kwa namna ambayo inaifanya nchi iingie kwenye hasara.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili nirejee tu pia kwenye jibu zuri la Naibu Waziri wa Fedha, kwamba kama Mheshimiwa anazo taarifa zozote zinazoweza kutusaidia sisi, ama kufungua shauri la madai au kufungua shauri la jinai, basi ashirikiane na vyombo vinavyofanya. Kwa mfano, hili shauri la madai sisi tukiletewa litaletwa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tutaliangalia tuone kama linakidhi sifa na sheria na kwa kuzingatia pia mahusiano tuliyonayo na nchi kama ya Uingereza tuone kama tunaweza, moja, kufungua kesi ya jinai au pili, tulifanye kwa namna ambayo tunaweza tukafungua kesi ya madai. Lakini mpaka sasa kilichopo ni kwamba hii benki iliingia makubaliano na Serious Fraud Office ya Uingereza kwa kitu kinachoitwa deferred prosecution agreement, ambayo pamoja na mengine walitakiwa walipe hizi dola kama Naibu Waziri wa Fedha alivyosema. Wakishindwa Serikali ya Uingereza itawachukulia hatua ya kesi ya jinai hii benki na sisi huku kama alivyosema Naibu Waziri wa Fedha, Benki Kuu imewataka Stanbic Tanzania nao walipe hiyo faini na muda huu ambao walipaswa wawe wametoa jibu ilikuwa ni tarehe thelathini. Kwa hiyo, tuupokee tu ushauri wa Mheshimiwa Zitto, Serikali itaufanyia kazi kwa kuzingatia sheria za ndani ya nchi na mahusiano yetu ya kisheria katika Jumuiya ya Kimataifa. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved