Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Primary Question

MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitangaza ndani na nje ya nchi bidhaa zinazotokana na Zao la Mwani?

Supplementary Question 1

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia matumaini hususan kwenye Balozi zetu. Ila tukumbuke kwamba tuna takribani zaidi ya miaka 30 sasa tokea mwani huu uletwe hapa kwetu Tanzania ambayo ni nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha mwani mwingi, lakini bado hatujaona jitihada kubwa za kuhakikisha mwani utambulika nchini na kuwa na thamani kwa wakulima wetu: Je, ni upi mpango wa Serikali sasa wa kushirikiana na taasisi ya sayansi na teknolojia iliyokuwepo Dar es Salaam pamoja na ile taasisi ya Zanzibar ambayo inashughulika na masuala ya mwani ili kuhakikisha mwani unakuwa na thamani nzuri na unatambulika? Hilo swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wizara imejipangaje sasa ili kutoa elimu kwa wakulima wetu ili wafahamu faida zinazopatikana kwenye huo mwani? Ahsante. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kwa ukaribu zao la mwani. Zao la mwani ni moja ya mazao ya kimakakati katika Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi ambayo yanatokana na mazao ya bahari. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni pamoja na kuzitumia hizi taasisi ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge hapa kwa maana ya COSTECH pamoja na ZSF iliyoko upande wa Zanzibar. Malengo haya tutaendelea kuyasisitiza kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha sasa huu mwani unakuwa maarufu siyo kwa Tanzania peke yake, ni mpaka nchi za pembezoni ili kuongeza biashara kubwa na pato la Taifa kwa ujumla kwa pande zote mbili; Tanzania Bara pamoja na Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, hilo ndiyo mpango wetu wa sasa kuhakikisha kwamba tunaongeza engagement ya watu katika zao hili la mwani ikiwemo vijana, akina mama pamoja na wanaume ambao watahitaji kuingia katika zao hili. Kwa hiyo, tutatoa elimu na tutaongeza wataalam kwa ajili ya kusaidia zao la mwani. Ahsante. (Makofi)

Name

Khalifa Mohammed Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Mtambwe

Primary Question

MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitangaza ndani na nje ya nchi bidhaa zinazotokana na Zao la Mwani?

Supplementary Question 2

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwani ni zao ambalo likisanifiwa linaweza likatoa bidhaa nyingi ambazo zinatoa faida kwa wakulima: Je, ni lini Serikali itawapelekea viwanda vidogo vidogo katika yale maeneo ambayo yanazalisha mwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Moja ya mpango wa Serikali ni pamoja na kuwawezesha wakulima wa mwani na ndiyo maana ukifuatilia katika Hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambayo aliitoa hapa Bungeni, moja ya mikakati tuliyonayo ni pamoja na kuwanunulia vifaa vya kisasa na kuongeza tija katika zao la mwani ikiwemo kuwapatia viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuzalisha kama sabuni, mafuta yanayotokana na mwani. Kwa hiyo, hayo ni sehemu ya mpango ambao Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunayo. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitangaza ndani na nje ya nchi bidhaa zinazotokana na Zao la Mwani?

Supplementary Question 3

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina swali dogo tu la nyongeza. Tunafahamu kwamba mwani ni muhimu sana na unaleta fedha za kigeni lakini mwani unalimwa sana na wanawake na hata kule Jimboni kwangu Mchinga, wanawake wanalima mwani, lakini bei yake ni ndogo ndogo sana. Serikali ina mpango gani juu ya hili jambo? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nampongeza Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa Jimbo la Mchinga kwa kuwa Halmashauri yake ya Mchinga hapa nchini ni moja ya halmashauri ambazo zinaongoza kwa uzalishaji wa zao la mwani. Kwa hiyo, hilo linafahamika, na ni kweli zao la mwani wakulima wakubwa ni akina mama. Sisi kama Serikali tunakiri kwamba bado changamoto ya bei ipo chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati yetu tuliyonayo ni pamoja na majibu ya swali la msingi kama tulivyojibu kwamba, ni kutangaza zao la mwani, kutafuta masoko nje ya nchi hususan katika nchi ya China ambapo ndipo wanunuzi wakubwa wa zao hili ili kuhakikisha kwamba sasa tunaongeza bei kwa wakulima wetu wa ndani ili kupata tija na kuongeza pato la Taifa kwa nchi nzima. Kwa hiyo, hilo liko ndani ya mipango yetu, ahsante. (Makofi)