Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Innocent Sebba Bilakwate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Primary Question
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwakopesha fedha wakulima wa kahawa ili kuondokana na biashara ya butura?
Supplementary Question 1
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba wakulima wanapata soko la uhakika. Lakini inapofika kipindi cha mavuno ya kahawa kumekuwepo na vitendo vya kuwakamata wakulima wanaotoka kata A kwenda kata B kuvuna kahawa kwa kuwanyang’anya kahawa na kutaifisha ile kahawa;
Je, ni nini tamko la Serikali juu ya vitendo hivi ambavyo havifai?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mibuni mingi mkoani Kagera imekauka kwa sababu ya ugonjwa wa mnyauko. Tumeangalia kwenye bajeti tumetengewa mibuni (miche ya kahawa) michache;
Je, Serikali iko tayari kuongeza miche mingine ya kahawai li kukidhi mahitaji ya wakulima wa Mkoa wa Kagera?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, haikubaliki na hairuhusiwi kumkamata mkulima mwenye mazao yake anayoyatoa sehemu moja Kwenda sehemu nyingine ndani ya Wilaya husika, isipokuwa kama mkulima anayatoa shambani kupeleka kwenye AMCOS kwa ajili ya Kwenda kufanya aggregation hapo ni makosa kumkamata. Vile vile kama kuna mfanyabiashara ambaye pia na yeye anatoa mazao hayo kutoka kwenye AMCOS kupeleka kwenye viwanda lazima tuhakikishe awe ana nyaraka ambayo inamruhusu ili kuondokana na usumbufu. Lakini katika ujumla wake Serikali haiwezi kuwa sehemu ya kuzuia maendeleo ya mkulima; na ninatoa maelekezo katika uongozi wa maeneo husika kuhakikisha kwamba wanawalinda wakulima na wasiwanyanyase wakulima katika mazao ambayo wanayalima wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la kuhusu mibuni. Ni kweli mibuni mingi hivi sasa imeshatimiza zaidi ya miaka 25 na kimsingi imezeeka na inapunguza sana uzalishaji. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa maana ya TaCRI pamoja na Bodi ya Kahawa tunaendelea na uzalishaji wa miche ya kahawa. Mwaka huu tumeendelea kuzalisha miche 20,000,000. Vilevile tutaongeza uzalishaji wa kahawa kupitia teknolojia ya chupa ili kuongeza wigo mpana zaidi na wakulima waweze kupata miche mingi na kwa uharaka zaidi ili kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa.
Name
Flatei Gregory Massay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Primary Question
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwakopesha fedha wakulima wa kahawa ili kuondokana na biashara ya butura?
Supplementary Question 2
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Mwaka jana Jimbo la Mbulu Vijijini na Jimbo la Babati na Mbulu Mji wakulima waliahidiwa kukopeshwa kulima vitunguu, mahindi katika eneo hilo. Kwa bahati mbaya hawakukopeshwa mpaka msimu umeanza mpka leo.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hili?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilichukue jambo hili la Mheshimiwa Mbunge niende kulifanyia kazi na kufahamu nini ilikuwa ni changamoto ili tuweze kulitatua na changamoto hiyo isijirudie tena.
Name
Mwantumu Mzamili Zodo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuwakopesha fedha wakulima wa kahawa ili kuondokana na biashara ya butura?
Supplementary Question 3
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Zao la mkonge ndiyo dhahabu yetu ya Mkoa wa Tanga kwa sasa. Zao la mkonge linachukua miaka mitatu toka kulihudumia mpaka kuanza kuvuna. Wakulima wengi wadogo wadogo wanaoanza wanashindwa pale mwanzo kwa sabbau ya kusubiria miaka mitatu kabla ya kuvuna;
Je, Wizara haioni haja sasa ya kuja na mkakati wa kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ili kuedelea kuleta hamasa kwenye zao hili?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye zao la mkonge Serikali imefanya yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, tumeendelea kuongeza uzalishaji wa miche ya kutosha kupitia TARI Mlingano pale Mkoa wa Tanga, na hivi sasa tunajenga maabara ya tissue culture kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa miche hii ya mkonge ili wakulima wengi zaidi waweze kuhamasika. Pili; tunahakikisha ya kwamba katika mwaka huu wa fedha tunanunua decorticators mbili, ile corona, kwa ajili ya uchakataji wa mkonge ili mkonge mwingi zaidi uweze kuchakatwa na kuongeza hamasa ya wakulima kulima zaidi; na la tatu, tunaendelea kuunganisha wakulima wetu na taasisi mbalimbali za kifedha ili waweze kukopesheka na kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la mkonge. Na la mwisho, kwa sababu katika ulimaji wa mkonge kuna spacing tumekuwa pia tukiwahamasisha pale katikati kulima mazao mengine ya haraka ili yawasaidie kuiongeza tija na kuongeza kipato katika aina ya zao ambalo wanalilima.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved