Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Primary Question

MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:- Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Uyui - Tabora katika Kata ya Tura na Wilaya ya Ikungi – Singida?

Supplementary Question 1

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwa na migogoro mingi sana katika maeneo mbalimbali ya Kata kwa Kata, Kijiji kwa Kijiji, Mkoa kwa Mkoa, Wilaya kwa Wilaya. Sasa na wataalam wetu wamekuwa wakisoma hizi ramani kwa muda mrefu sana.

Je, kupitia Wizara yako hauoni kutoa maagizo mahsusi kwa wahusika wakamalize migogoro hii kwa haraka?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili. Kwa kuwa, mgogoro huu mahsusi wa Kata ya Tura na Wilaya ya Singida (Ikungi). Je, hauoni haja ya mimi na wewe Naibu Waziri tukaenda tukaumaliza ili sasa wananchi wabaki na amani na wajue nini wanachotakiwa kuenda na wapi ni mpaka wao? Ahsante. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Venant Protas, Mbunge wa Igalula:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna mgogoro wa muda mrefu katika eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelizungumzia na hasa kuna vijiji viwili vya Makene ambayo ipo katika Kata ya Iyumbu, Wilayani Ikungi na Kijiji cha Nkongwa kilichopo Kata ya Tura, Wilayani Uyui. Tayari jitihada za Serikali kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya hizi mbili ya Uyui na Ikungi, vilevile Mikoa hii miwili zimekuwa zikifanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nitumie Bunge lako Tukufu hili kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuwaelekeza, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wa Wilaya hizi mbili kukutana mara moja wiki hii, kwa ajili ya kupata suluhu ya mgogoro huu na kufanya majadiliano haya yafike mwisho ili mipaka ya Mikoa hii miwili iweze kujulikana na wananchi wajue wanapata huduma kutoka upande gani wa maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, mimi nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kadri tutakapopata tu taarifa ya Kamati za Ulinzi na Usalama hizi mbili za Wilaya ya Ikungi na Uyui, nitaongozana na Mheshimiwa Mbunge ambae amekuwa mstari wa mbele katika kuwapigania wananchi wake wa Uyui. Nitaongozana nae kwenda kuhakikisha tunafanya mkutano na wananchi hawa na kuwaeleza mipaka iliyopo kwa mujibu wa GN.