Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Luhaga Joelson Mpina
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Primary Question
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza:- Je, Serikali imejiimarisha vipi kukagua miamala ya uhamishaji bei ya mauziano ya bidhaa/huduma za makampuni ya Kimataifa?
Supplementary Question 1
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza niipongeze sana TRA kwa hatua walizozichukua kuongeza uwezo wa kukagua hii miamala ya transfer pricing, ikiwemo ununuzi wa Kanzidata ya Orbis na kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki. Sasa ninayo maswali mawili ya nyongeza:-
Swali la kwanza; hizo hatua ambazo amezizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri zimesaidia kwa kiwango gani kuongeza mapato ya Serikali?
Swali la pili; ni kauli gani Serikali inatoa juu ya ongezeko kubwa la taarifa shuku juu ya fedha haramu ambapo miamala ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya kielektroniki na fedha taslimu imeongezeka kutoka trilioni 123 hadi trillioni 280 mwaka wa 2023. Sasa ishara hii inaonesha kwamba, kuna ongezeko kubwa la rushwa, ufisadi, transfer pricing, elicit financial flow, capital flight, sasa haya matukio haya kwa ongezeko hilo la hizi takwimu Serikali inatoa kauli gani kama FIU ilivyotoa taarifa? (Makofi)
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote kabla ya kujibu maswali naomba kumpongeza Mheshimiwa Mpina pamoja na Wabunge wengine kwa namna wanavyopigania kuona kwamba, ukusanyaji wa mapato unapatikana kwa ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kwa kweli, hatua hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa sana. Ndiyo maana inadhihirika hata hivi karibuni tumeona TRA wamevunja rekodi katika ukusanyaji wa mapato hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kupitia TRA Serikali imeimarisha mifumo ambayo itadhibiti mianya yote ya rushwa na hata njia nyingine za ukwepaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Serikali kupitia TRA imeongeza rasilimali watu kwa kiasi kikubwa sana na hata hivi karibuni nafasi 524 zimetangazwa na mchakato unaendelea.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, pamoja na hayo Serikali imekwenda mbali sana, iko sasa hivi kwenye FATAF (Financial Action Task Force), anti-money laundering, anti-terrorism financing, Serikali iko vizuri sana. Mimi niko kwenye kikao cha European Union na tumeona namna European Union wanavyoisifia Serikali ilivyodhibiti utakatishaji pesa na ku-finance terrorism katika Taifa letu.
Mheshimiwa AG.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, nilitaka tu kuongeza ya kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Anti-Money Laundering, taarifa shuku zinapowasilishwa kwa FIU, baada ya kufanyiwa analysis hupelekwa na kufanyiwa kazi na vyombo vyenye dhamana ya kuchunguza na baadae kuchukua hatua za kisheria. Kwa hiyo, taarifa ambazo zimekwishatolewa kwa sasa zinaendelea kufanyiwa kazi na vyombo vyenye dhamana hiyo vilevile. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved