Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Omary Ahmad Badwel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Primary Question
MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:- Wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye rasilimali mawe, mchanga na maji inapotokea wakandarasi wanachukua rasilimali hizo au mojawapo kwa ajili ya ujenzi huchukua bure au kwa malipo kidogo na hivyo kuwakosesha wananchi haki ya kunufaika na rasilimali hizo; hali hii ni tofauti na maeneo yenye madini ambapo wananchi hunufaika na uwepo wake:- Je, Serikali haioni haja ya kuweka bei elekezi kwa wakandarasi wanaohitaji mawe, mchanga au maji ili wananchi wanaoishi maeneo yenye rasilimali hizo waweze kunufaika?
Supplementary Question 1
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa, Wakandarasi wengi wanaotumia bidhaa hizi hawafuati taratibu hizi ambazo zimeelezwa na Mheshimiwa Waziri, ama kununua mawe na bidhaa nyingine kwa watu wenye leseni, mara nyingine wamekuwa wao wenyewe wakiamua kuchukua hizo bidhaa katika maeneo yetu na bila kulipa mrabaha katika Halmashauri au bila kuwanufaisha wananchi katika maeneo yetu ambako bidhaa hizo zinatoka;
Je, Serikali iko tayari sasa kuangalia utaratibu mzuri ambao utanufaisha hizi Halmashauri zetu pamoja na wananchi husika katika maeneo husika ambayo bidhaa hizi zinapatikana?
Swali la pili, kwa kuwa wakati wa zoezi hili la uchukuaji bidhaa mbalimbali za ujenzi pia hutokea uharibifu wa mazingira katika maeneo yetu ikiwepo uchimbaji wa mashimo makubwa na kuacha hayo mashimo katika maeneo yetu, pia afya za wananchi zinaathrika kwa mavumbi na kadhalika;
Je, Serikali inachukua hatua gani madhubuti kuhakikisha kwamba inadhibiti suala la uharibifu wa mazingira pamoja na afya za wananchi katika maeneo husika?
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa wachimbaji wadogo hasa wanaojihusisha na uchimbaji wa madini ya ujenzi pamoja na viwandani kwa kiwango kikubwa sana hawalipi ada pamoja na malipo mengine Serikalini. Nichukue nafasi hii kuwataka rasmi wachimbaji wadogo wote popote walipo waanze sasa kufanya hivyo.
Hata hivyo, manufaa yanayoweza kupatikana kutokana na uchimbaji wa kokoto pamoja na mchanga ni pamoja na kutakiwa kama ambavyo sheria inawataka kulipa ushuru wa Halmashauri ambao ni asilimia 0.3, haya ni matakwa ya sheria, ni vizuri sana ninakushukuru Mheshimiwa Badwel, nichukue nafasi hii kuwahamasisha viongozi wa Halmashauri ili waanze kukusanya ushuru huo kutoka kwa wakandarasi wanaochimba kokoto pamoja na mchanga kote nchini. Kwa hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Badwel kwa kuwakumbusha wananchi ili wachukue hatua hiyo, ninawaagiza pia wakandarasi wote waanze kufanya hivyo mara moja.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, athari za mazingira, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Badwel kwamba uchimbaji wowote wa madini jambo la kwanza kabisa wanalotakiwa kufanya ni juu ya kutokuharibu mazingira. Huwezi kuchimba madini bila kuharibu mazingira, lakini wana jukumu kwa mujibu wa Sheria za Mazingira na kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, wana wajibu wa kisheria wa kutunza mazingira.
Mheshimiwa Spika, hatua tunazochukua kwa wakandarasi na wamiliki wa leseni wasiotunza mazingira ni pamoja na kuwafutia leseni zao lakini pia kuwachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria hizo mbili.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Badwel pia natoa tamko rasmi, Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira huwa tunachukua hatua za kisheria kwa wale wasiotunza mazingira kwa mujibu wa sheria.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved