Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Je, kwa nini Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo mpakani mwa Ziwa Tanganyika havina Usafiri wa uhakika?

Supplementary Question 1

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Waziri unajua kwamba kumekuwa na changamoto sana ya uvamizi kwa wavuvi kuchukuliwa vifaa vyao ikiwemo injini pamoja na fedha na tunaposema boti tunazungumzia speed boti kwa ajili ya kuendana na wale wahalifu wanaotoka nje za jirani. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuwapa speed boti kwa maana ya fiber askari polisi ili waweze kuwalinda wananchi wetu na kupambana na wale wahalifu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili Askari Polisi wa Nkasi wanapata changamoto kubwa sana kulingana na jiografia. Ni lini mtawapa gari pamoja na mafuta ya kutosha siyo kama hivi wanavyofanya sasa hivi ili waweze kuwajibika katika majukumu yao? Ahsante.

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba wakati mwingine wananchi wetu wanaathiriwa na majambazi hawa wanaopita maeneo ya ziwani kwa sababu wanakuwa na vifaa bora zaidi kuliko walivyokuwanavyo vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwenye maeneo hayo. Kwa kulitambua hilo ndio maana nimeeleza katika boti tutakazonunua ni fiber zinazokwenda mwendokasi ili kukabiliana na hao majambazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vijana wetu ambao wanahitaji magari, nimesema yatakapotoka tutawagawia na Wilaya yako ya Nkasi itanufaika na pamoja na Jimbo la mwenzio Nkasi Kusini ambaye ni Mjumbe wa Kamati yetu ya NUU wote tutahakikisha kwamba tunapata magari. Baada ya kupata magari hayo katika mwaka ujao pia tutaongezea vitendea kazi vingine zikiwemo pikipiki ili kuimarisha uwezo wa vijana wetu wa doria kwa magari na madoria kwa pikipiki, nashukuru sana.