Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa KV 400 kutoka Iringa, Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga utaanza pamoja na kulipa wananchi waliopitiwa na laini hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali na kwa hatua iliyofikiwa na hii itapelekea kukwamua hata makampuni makubwa na viwanda vikubwa ambavyo vilikwama kufunguliwa kutokana na kukosa umeme mkubwa. Pia kuna vijiji kadhaa na vitongoji kadhaa ambavyo vimekosa umeme kutokana na kuchelewa kwa mradi huu vikiwemo Vijiji vya Kata za Ulenje, Kinyara, Vijombe, Swaya, Igale, Iwindi na Bonde la Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme kwenye Vijiji vya Ihango Kata ya Ulenje na Mina na Lusungo Kata ya Iwindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali ina mkakati gani wa kukwamua Mradi wa REA, awamu ya tatu, round ya pili, ambao umekwama kwenye Jimbo la Mbeya Vijijini?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Oran Njeza kwa pamoja, kwa sababu yanahusu umeme vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Njeza pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine wote kwamba Mradi wetu wa Kupeleka Umeme Vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa pili, utakamilika ifikapo Desemba. Vijiji aliyovitaja vilivyo katika kata hizo vyote vitakuwa vimepata umeme kufikia mwezi Desemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi anayepeleka umeme kwenye eneo la Mbeya Vijijini ni mkandarasi wetu ETDCO ambaye ni kampuni tanzu ya TANESCO na ameuliza ni jitihada gani zimefanyika kukwamua mradi kwenye eneo lake. Mkandarasi huyu sasa amewezeshwa zaidi na kampuni mama ya TANESCO, lakini na sisi kama Wizara tumeweka utaratibu mpya wa kusimamia miradi hii ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana kwenye maeneo yetu ya majimbo, lakini kuajiri wakandarasi wahandisi wengi zaidi wa REA kwenye maeneo ya mikoa na kuweka ma - group ya kijamii ya WhatsApp, Waheshimiwa Wabunge wameyaona. Tunaamini kwa njia hizi na jitihada ikiwemo na kulipa pesa kwa wakati, miradi hii yote ya REA iliyokuwa inasuasua, itakamilika kwa wakati ikiwemo kwenye eneo la Mheshimiwa Njeza ambapo mradi utakamilika ifikapo Desemba kupitia makandarasi wetu wa ETDCO.