Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Geoffrey Idelphonce Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Masasi Mjini
Primary Question
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge kati ya Mtwara - Mbamba Bay na Songea – Ludewa?
Supplementary Question 1
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu ni sehemu ya mpango ambao upo kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya nchi yetu Awamu ya Tatu ambao mwezi Julai unafikia hatua ya miaka mitatu ya utekelezaji. Ni maandalizi gani ya awali ambayo Serikali imeyafanya kuonesha kwamba ina dhamira ya dhati kujenga mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mradi huu ni sehemu ya mradi funganishi wa Mtwara Development Corridor ambayo makubaliano ya mradi huo ulifanyika Lilongwe - Malawi Novemba, 2004 na marais wanne wa hizi nchi nne.
Je, ni lini Serikali sasa kama mnufaika mkuu utarudisha utaraibu wa marais hao wanne kukutana na kuweza kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huu wa reli pamoja na miradi mingine ndani ya Mtwara Development Corridor? (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mbunge wa Masasi Mjini, Mheshimiwa Idelphonce Mwambe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa mradi huu na Wabunge wote wa Mkoa wa Mtwara na kwa swali la kwanza anapenda kujua maandalizi ya awali ya mradi huu.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali tumeanza maandilizi ya awali, kwanza tumeanza vikao ndani ya Serikali pamoja na kufanya vikao na wadau mbalimbali na hivi ninavyosema tutakuwa na kikao kingine ambacho kimeitishwa na Mamlaka ya Bandari nchini kitakachofanyika tarehe 22 hadi 23 pale Mtwara na Waheshimiwa Wabunge mnakaribishwa katika mkutano huu kwa sababu ndio unaenda kuifungua Mtwara Corridor yote na wadau wengine ni pamoja na RAS kwa maana ya Mamlaka ya Mkoa wa Lindi, Mtwara yenyewe pamoja na Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi, ni kwamba mradi huu kwa kuwa kwanza kuna makampuni zaidi ya matano kutoka nchi mbalimbali kutoka nchi ya Uingereza, Canada, Marekani, Afrika Kusini, Croatia, Morocco wameonesha nia katika uwekezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na kwa maana hiyo, changamoto kubwa ilikuwa katika kikwazo ambacho kilichokuwepo kupitia Sheria ya PPP ambayo Bunge lako tukufu wiki iliyopita imepitisha na kufanya mabadiliko madogo kwenye sheria hiyo.
Kwa hiyo, tunaamnini mapatano na mikutano itakayofuata sasa katika makampuni kutoka nchi hizi watakuja moja kwa moja kuwekeza kwa kuwa tayari tulishaanza kufanya nao mikutano hiyo, ahsante.
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge kati ya Mtwara - Mbamba Bay na Songea – Ludewa?
Supplementary Question 2
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwamba hivi karibuni Bunge lako tukufu limefanya marekebisho ya Sheria ya PPP ili kuwezesha miradi kama hii kutekelezwa kwa urahisi.
Je, Serikali inatoa kauli gani sasa katika kuharakisha utekelezaji wa mradi huu ambao unasubiriwa kwa hamu kwa wananchi wa maeneo hayo husika? (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chikota kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina hamu kubwa sana katika kutekeleza mradi huu na ndio maana Serikali imeanza pia kulipa fidia. Nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya takribani shilingi bilioni 15 katika kulipa huu mradi wa Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, Serikali inaona umuhimu mkubwa wa mradi huu na ndio maana pia tumeitisha vikao hivi mara moja mara baada ya kubadilisha sheria yetu ya Public Private Partnership kwa maana ya ubia, ahsante. (Makofi)
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge kati ya Mtwara - Mbamba Bay na Songea – Ludewa?
Supplementary Question 3
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kwamba kazi ya mshauri ilifanyika toka mwaka 2016 ikiwa ni pamoja na uthamini kwenye eneo ambalo reli hii itakwenda kupita.
Ni lini sasa Serikali itaanza kulipa fidia kwa wananchi waliopo kwenye eneo ambalo reli hii ambapo mradi unaenda kutekelezwa? (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekwisha kusema kwamba upembuzi yakinifu ulikwishafanyika tangu miaka hiyo ya 2016 na Serikali hatua iliyofikia sasa ni kumuajiri Transaction Advisor kwa maana ya Mshauri wa Kifedha ambaye ndiye atakayetupa miongozo yote hadi kulipa fidia, lakini pia kupitia mthamini mkuu kwa sababu hili jambo lilishafanyika miaka mingi kwa vyovyote vile kutakuwa na haja ya kurudia kupitia daftari ambalo lilikuwa limeandaliwa kipindi hicho, nashukuru.
Name
Omari Mohamed Kigua
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Primary Question
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge kati ya Mtwara - Mbamba Bay na Songea – Ludewa?
Supplementary Question 4
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, miaka mitatu iliyopita Serikali katika mpango wake wa maendeleo ilijielekeza kwamba itajenga SGR kwa reli hii ya kuanzia Tanga – Moshi - Arusha hadi Musoma. Je, mpango huo bado upo? Ahsante. (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali itajenga reli hiyo ya Dar es Salaam – Tanga - Moshi mpaka Arusha, lakini kwa sasa tuna awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni kujenga reli ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza na awamu ya pili kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma. Mara tutakapokamilisha hizi ndipo tutakapokuja katika hii reli ya kutoka Dar es Salaam – Tanga - Moshi mpaka Arusha na mpango huo uko vilevile.
Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo kwamba Serikali ina nia hiyo, lakini kwa sasa tunakamilisha hizi ambazo tumekwishaanza, ahsante.