Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Primary Question

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:- Je, Serikali ina uhakika gani na usalama wa nchi yetu katika mpaka wa Pori la Akiba la Kimisi na Burigi na Mto Kagera?

Supplementary Question 1

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mpaka wa Tanzania katika eneo la Rusumo mpaka unapoenda Kagera ni hifadhi, lakini mpaka huo kwa upande wa Rwanda ni vijiji ambavyo viko mpaka kwenye Mto Kagera, kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba changamoto zilizopo katika hifadhi hiyo ni pamoja na hifadhi hiyo kutumiwa na wahamiaji haramu, watu wanaopitisha silaha na ujambazi.
Je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atahakikisha kwamba eneo hilo linalindwa kwa usalama wa nchi? Hilo swali la kwanza.
Swali langu la pili, katika hifadhi hizo za Burigi na Kimisi kuna Maziwa Ngoma na Maziwa Burigi, ambayo miaka yote yamekuwa yakitumiwa na watu kutoka nchi za jirani kwa uvuvi katika maziwa hayo na kwa ulinzi mkubwa wa askari wa wanyamapori. Ni lini Serikali itaanzisha seasonal fishing kwa Watanzania ili waende kuvuna maliasili hiyo?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza lini Serikali itaimarisha ulinzi kwenye maeneo hayo, nimejibu kwenye swali la msingi, kwamba mpaka sasa hvi tunavyozungumza, changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika eneo tunalolizungumzia zimekuwa zikishughulikiwa kwa pamoja kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamati ya Ulinzi ya Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ameeleza kwamba yapo mashaka ambayo yanaendelea kuongezeka kila siku, basi Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mkoa kuweza kuona namna gani tunaweza kuboresha vizuri zaidi au kufuatilia zaidi ambazo zinaonekana kujitokeza upya kwa sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala ni lini, napenda pia nimkumbushe Mheshimiwa Kanyasu kwamba tumesema mara tu baada ya Bunge hili tunapita maeneo yote ambayo yana changamoto za kiulinzi na usalama kuhusiana na masuala ya mipaka ili tuweze kuboresha vizuri zaidi changamoto za ulinzi na usalama na changamoto za migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mabwawa yaliyopo ambayo yana samaki na kwamba kwa sababu yapo ndani ya hifadhi basi kwa mujibu wa sheria wananchi hawaruhusiwi kufanya uvuvi. Napenda kujibu kwamba sababu za kuzuia kufanya uvuvi zitakuwa ni sababu za kiuhifadhi, lakini kwa kuwa kuhifadhi maana yake siyo kuacha kutumia maana yake ni kutumia kwa busara na hekima, kuhifadhi maana yake ni kutumia ukijua kwamba ipo kesho na kwamba unaweza ukatumia leo ukijua kabisa kwamba kesho utahitaji kutumia kitu kile unachokitumia leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwa maana ile ya kufanya uhifadhi endelevu tutaliangalia suala hili kuona ni namna gani tunaweza tuka-engage wananchi waliopo katika maeneo haya waweze kufanya uvuvi kama taratibu za kisayansi za uhifadhi zitaruhusu. Lakini tunakwenda kufanya jambo hili kwa pamoja liwe shirikishi ili wote tuone ukweli sasa kwamba kitakachofanyika kiwe kwa maslahi ya Taifa.