Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Asia Abdulkarim Halamga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana wakati wote katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini?
Supplementary Question 1
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nichuke nafasi hii kuipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini pia nina maswali yangu mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikinunua dawa MSD na inapokosa inanunua kwa mshitiri; je, Serikali inamkaguaje mshitiri ili kuwa na dawa za kutosha pale inapokosekana MSD?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; ni hatua gani zinachukuliwa kwa watoa huduma wa vituo vya afya ambao wanathibitika na upotevu wa madawa? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri ambayo yanalenga kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma. Ni kweli kama anavyosema Mbunge kwamba, wakati mwingine inapokuwa MSD hakuna dawa, basi watu wetu wanapewa OS na wanakwenda kununua kwa mshitiri, lakini kuna mikoa ambayo wamemweka mshitiri ambaye ni mmoja na wataalam wetu hawaruhusiwi kunua dawa nje ya yule mshitiri. Kwa hiyo, anapokuwa amekosa MSD, anafika kwa mshitiri, naye mshitiri akiwa hana dawa, kwa hiyo, inafika mahali watu wetu wanateseka hawana dawa na huku fedha wanazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii na hili swali la Mheshimiwa Mbunge kuagiza kwamba, kwanza tusilazimishe hospitali zetu kununua kwa mtu fulani dawa. Ni kwamba tutengeneze biashara huria, duka lolote lenye dawa ambalo limetimiza vigezo, watu wetu waweze kununua kwenye duka lolote la dawa bila kulazimishwa kununua kwa mtu fulani. Kwa sababu nayo hiyo ni aina ya ufisadi mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge, hakika tutakapokuwa tunapita, tutashirikiana naye kushughulikia suala hilo, kwa sababu ukiona mtu mmoja analazimishwa kwenye mkoa mmoja kwamba yeye ndio auze dawa, hiyo ni aina mwingine wa ufisadi na tutausimamia na ku-control.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu tunafanya nini kwa wale wanaobainika kwamba wameiba dawa, kwa kweli kuna sheria na taratibu za utumishi wa umma. Kama unavyojua, nasi ni Wabunge ambao tunatunga sheria hapa, kuna baadhi ya sheria tumetunga ambapo mwizi anakuibia mara moja, lakini ikifika mahali wakati wa kumshughulikia mwizi ambaye una hakika kwamba ameiba, inabidi ufuate taratibu na sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi tutafakari kwa kina namna gani tutawashughulikia watu ambao wanafanya ufisadi kwa sababu wakati mwingine sheria zinawalinda sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved