Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, kuna mkakati gani wa kufufua zao la kahawa nchini?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mkakati wa Serikali unaonekana hawajafanya utafiti wa kuweza kujua ni kwa kiasi gani uzalishaji wa mbegu unahitajika nchini: -
Je, Serikali ipo tayari sasa kutengeneza mkakati, angalau wa miaka mitano, wa kuhakikisha kwamba wanafanya utafiti wa kujua ni idadi kiasi gani ya mbegu zinatakiwa ili uzalishaji huo wa miche milioni 20 kwa mwaka angalau upande hadi kufikia miche milioni 50?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa TaCRI na Bodi ya Kahawa peke yao hili zoezi hawaliwezi: -
Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuhakikisha kwamba inaihusisha sekta binafsi katika eneo hili la uzalishaji wa mbegu ili sasa hili zao la kahawa tuweze kulifufua kote nchini? (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utafiti kwenye kahawa ndiyo kazi ambayo imekuwa ikifanyika muda wote kupitia TaCRI ili kuwezesha kuongeza uzalishaji katika zao letu la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa miche ya kahawa unaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na mahitaji. Kwa hivi sasa tumetoa maelekezo kwa wenzetu wa TaCRI pamoja na wakulima pia kuhakikisha ya kwamba tunang’oa ile mibuni yote iliyofikisha zaidi ya miaka 25 ambayo imezeeka na kupanda miche mipya ili kuongeza uzalishaji. Hivyo, itatulazimu kuongeza uzalishaji mkubwa sana wa miche ya kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sisi kama Serikali peke yetu hatuwezi kufanya, tumewahusisha pia sekta binafsi ili kwa pamoja tuweze kuzalisha miche mingi zaidi, na lengo hapa ni kuwa na miche mingi ya ziada ili wakulima wetu waweze kuipata kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tumeongeza mkakati mwingine wa kuhakikisha kwamba tunatumia teknolojia ya chupa (tissue culture) kwa ajili ya kuongeza uzalishaji miche mingi zaidi ya kahawa, iwafikie wakulima kwa wakati, na tuweze kuongeza uzalishaji wa zao hili la kahawa hapa nchini.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved