Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanzisha Tawi la Chuo Kikuu Huria katika Halmashauri ya Ifakara?
Supplementary Question 1
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninaishukuru Serikali kwa majibu hayo, lakini swali la kwanza; kwa kuwa Ifakara ni katikati ya Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga, na mahitaji ya kuwepo kwa tawi ama kituo cha mitihani ni makubwa mno: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Tawi dogo la Chuo Kikuu Huria?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; endapo halmashauri itatoa eneo kwa sasa: -
Je, Serikali iko tayari kujenga Tawi la Chuo Kikuu Huria ama tawi la chuo kikuu kingine chochote? Ahsante.
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha jibu katika majibu ya swali la msingi, lakini Mheshimiwa Asenga anataka kufahamu, japo kuwa pale tuna Kituo cha Chuo Kikuu Huria ambacho wanafanyia mitihani bado ana msisitizo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Asenga; Chuo Kikuu Huria kinao utaratibu wa kuwa na vituo vya mitihani katika ngazi za wilaya pamoja na kata kulingana na uhitaji wa maeneo hayo. Lakini vilevile kina utaratibu wa kuweza kuanzisha matawi au vituo hivyo vya kuratibu mitihani katika makambi yetu ya majeshi pamoja na kambi mbalimbali za wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Asenga naomba tu nikuhakikishe kwamba Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina katika eneo hilo ulilolitaja la Kilombero, Ulanga na kule Malinyi na maeneo mengine nchini, na kuweza kuona kama uhitaji huo upo ili tuweze kuanzisha ama vituo au matawi ya Chuo Kikuu Huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la pili, kwanza tuishukuru Halmashauri ya Ifakara, lakini tukushukuru wewe binafsi kwa jitihada zako za kutenga eneo kwa ajili ya Chuo Kikuu Huria. Naomba nikuhakikishie kwamba Serikali itaendelea kufanya tathmini, pamoja na uwepo wa maeneo haya, lakini vilevile kuna uhitaji wa rasilimali fedha pamoja na uhitaji wa rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivi vyote vikichanganywa ndipo tunakwenda kuanzisha matawi haya ya chuo kikuu, lakini vilevile uhitaji wa hilo tawi katika eneo hilo. Kwa hiyo, baada ya tathmini hii tutajihakikishia sasa kama upo umuhimu wa kwenda kuanzisha tawi katika eneo la Ifakara au la, nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved