Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaweka Kituo kidogo cha Forodha katika Kata ya Itiryo – Bikonge Tarime Vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba alienda Bikonge na Nyamuhonda; wananchi wa Jimbo zima walienda kwake wakitaka kujua ni lini wataweka pale kituo kwa sababu kitasaidia kuokoa fedha za Serikali na kufanya biashara mpaka watu wa Serengeti watanufaika hapa. Kwa hiyo niliomba nijue ni lini kituo hicho kitajengwa kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliahidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninapozungumza hapa Kanda ya Ziwa yote Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Mara biashara ya mazao imesimama kwa sababu Sirari kuna vurugu kubwa kwa zuio ambalo limetolewa na Mheshimiwa Waziri kwa Niaba ya Serikali. Watu wa Sirari na kanda ya ziwa wangependa kujua ni lini zuio hili litaondolewa kwa sababu wakati wanatoa tamko la kuzuia tayari wafanyabiashara wa mazao walikuwa na mazao kwenye maghala yao, hawafanyi biashara; na ulikuwa ukipeleka mazao Kenya unaleta bidhaa nyingine kutoka Kenya. Kanda imesimama biashara haifanyiki;

Je, ni nini kauli ya Serikali katika jambo hili?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwita kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimpongeze sana kwa namna anavyofatilia kituo hiki kidogo cha forodha pale mpakani. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo hiki mara tu upatikanaji wa fedha utakapopatikana basi kituo hiki kitajengwa, asiwe na hofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili naomba tulipokee kwa sababu limechanganya Wizara tofauti, Wizara ya Kilimo, Biashara na Fedha. Naomba tulipokee tukakae kama kamati tutakutana na wewe Mheshimiwa Mbunge tuone namna gani tutatatua changomoto.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa majibu ya ziada katika swali alilouliza Mheshimiwa Waitara. Mimi na yeye tumeshaongea zaidi ya mara moja mara mbili, naomba nirejee na Watanzania wanielewe. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijazuia watu kufanya biashara ya mazao na kuuza mazao nje ya nchi. Serikali ilichokizuia ni watu kufanya biashara bila kufuata utaratibu wa Kisheria. Haiwezekani mtu unanunua mahindi Songea unapakia kwenye malori huna business license ya aina yoyote, hata business name kusajili ambayo ni huduma inayotolewa. Huna tin number, huna tax clearance, huna export permit, huna phytosanitary halafu unataka nchi ikuruhusu kwenda kuuza nje mazao hayo. Malipo hayaonekani katika mfumo rasmi wa fedha, hatuzipati data katika export statement zetu za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Mheshimiwa Rais yako wazi, Mtanzania yeyote anayetaka kufanya biashara ya mazao kwa ajili ya kuuza nje ama kuuza ndani ya nchi akate leseni ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipitie kwenye Bunge lako Tukufu kuwaambia wafanyabiashara wa mazao, nendeni kwenye halmashauri kateni leseni za biashara, nendeni TRA chukueni Tin Certificate ili muingie kwenye mfumo rasmi na formalization ya biashara ya mazao ya kilimo. Hatuwezi kuendelea katika mfumo huu unao endelea. Na nia ya Serikali ni kurasimisha shughuli za kilimo na shughuli za biashara za mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana mtu yupo tayari apigwe penalty ya shilingi laki nane au milioni moja kwa sababu hana leseni avuke upande wa pili. Wiki iliyopita tumeruhusu malori Sirari, wiki hii tumeruhusu zaidi ya malori 506 na wote wamelipa faini ya shilingi milioni moja. Hatuwezi kuruhusu mfumo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wafanyabiashara, mazao ya kilimo yatauzwa popote, nendeni mkajirasimishe muwe na business license, muwe mna TIN, mna tax clearance. This is how we formalize economy. (Makofi)

Name

Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaweka Kituo kidogo cha Forodha katika Kata ya Itiryo – Bikonge Tarime Vijijini?

Supplementary Question 2

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha forodha Oloika katika kata ya Ololosokwan Wilayani Ngorongoro ili kupunguza usumbufu kwa wananchi lakini kuongeza mapato ya Serikali?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Serikali kupitia TRA walifanya utafiti nchi nzima. Kwa hiyo upatikanaji wa fedha katika nchi yetu basi kituo alichokitaja Mheshimiwa Mbunge kitajengwa.

Name

Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaweka Kituo kidogo cha Forodha katika Kata ya Itiryo – Bikonge Tarime Vijijini?

Supplementary Question 3

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kulikuwa na ujenzi wa vituo vikubwa vitatu vya forodha, kipindi inajengwa Vigaza kulikuwa na cha Manyoni halikadharika kulikuwa na Kituo cha Nyakanazi Biharamulo ambacho kilikuwa kimeshaanza kujengwa na tayari majengo yako pale, lakini kimetelekezwa kile kituo na kiko chini ya Wizara ya Fedha.

Sasa nilitaka kujua ni lini ujenzi wa Kituo cha forodha Nyakanazi Biharamulo ambacho kilishaanza ujenzi utafufuliwa ili uweze kukamilika kwa manufaa ya Biharamulo?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ezra kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki kilikuwa na mgogoro kati ya Mkandarasi na upande mwingine lakini tumechukua hatua na ninacho mhakikishia Mheshimiwa Mbunge, hivi karibuni tutapata mwafaka wa jambo hilo na kituo hicho kitaendelea na ujenzi kama kilivyopangwa.

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaweka Kituo kidogo cha Forodha katika Kata ya Itiryo – Bikonge Tarime Vijijini?

Supplementary Question 4

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwaka 2021 Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango alifanya ziara kwenye Jimbo la Momba kumwonesha mahali ambapo tunapendekeza kujenga kituo cha forodha. Mwaka huu mwezi wa pili Mheshimiwa Waziri Mkuu pia tulimshirikisha wazo hilo na akaona ni jema;

Je, Serikali imefikia hatua gani kujenga kituo kipya cha forodha ndani ya Jimbo la Momba ili kunusuru kituo cha forodha kilichopo Tunduma kwa sababu kimezidiwa ili kiweze kutoa huduma kwa ufasaha?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRII WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hicho ni kweli Mheshimiwa Waziri wa Fedha alienda lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda. Tuna mpango wa kujenga kituo hicho. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subra mara tu fedha zitakapopatikana tutajenga kituo hicho.