Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Primary Question

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari cha Muhalala – Manyoni?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, na kwa kuwa mradi huu umechukua miaka sita sasa tangu ulipositishwa, ninayo maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa Serikali itakamilisha mchakato wa kupitia hasara zilizosababishwa na kusimamishwa kwa mkataba huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kumpata mkandarasi mpya ili kazi ya ujenzi wa mradi wa Mhalala uweze kuanza? Ahsante sana.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyonyeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza, Benki ya Maendeleo ya Ulaya iko tayari, na fedha zipo kwa ajili ya kuendeleza. Kilichokuwa kinachelewesha ni kwamba baada ya kuingia mgogoro wa kimkataba ilikuwa ni lazima Serikali ihakikishe kwamba wanakaa pamoja na mkandarasi huyu ili waweze kukamilisha changamoto zote zilizokuwepo, wakishakubaliana sasa ndiyo waingie mkataba kutafuta mkandarasi mwingine wa kukamilisha.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni imani ya Serikali kwamba kwa mwaka tunaoanza wa fedha tutahakikisha kwamba mkandarasi anapatikana, na kazi iliyobaki, Kituo cha Ukaguzi hiki cha Muhalala pamoja na kile cha Nyakanazi, kwa sababu vyote vilisimama kwa pamoja vinaanza kujengwa na kukamilika kwa sababu ni muhimu sana kwa ajili ya kulinda barabara zetu, ahsante.