Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Makete?

Supplementary Question 1

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Wilaya ya Makete ni moja kati ya hospitali chakavu sana. Ni hospitali ambayo imetembelewa na Mawaziri tofauti, Mheshimiwa Ummy akiwa TAMISEMI amefika, Mheshimiwa Bashungwa, Mheshimiwa Jafo amefika na Kamati ya Bunge ya TAMISEMI imefika wamejionea hali ya Hospitali ya Wilaya ya Makete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipi ni kauli ya Serikali mimi kama Mbunge ningeomba msifanye ukarabati mjenge. Je, ipi ni kauli ya Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tuna vituo vya afya cha Kitulo, tunayo zahanati ya Nungu, Kisungilo na Unyangogo, hizi zahanati zimekamilika hazina vifaatiba. Je, ni lini Serikali itapeleka vifaatiba ili huduma zianze kutolewa kwa sababu wananchi wangu wa Makete, wametoa nguvu kazi yao wamejenga zahanati hizi na vituo vya afya lakini vifaatiba hamna. Ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Sanga kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa wananchi wa Jimbo la Makete, nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kumpa ushirikiano ili kuhakikisha wananchi wa Makete wanapata maendeleo ambayo yanatarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Makete ni kweli ni hospitali chakavu, Mheshimiwa Mbunge ameuliza hapa mara kadhaa Serikali hii sikivu ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ikamuahidi kupeleka fedha na sasa tumetenga mwaka ujao wa fedha milioni 900. Hii ni miongoni mwa hospitali 19 ambazo mwaka ujao wa fedha zitakabarabitiwa au kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali ni kwamba tunafanya tathmini na kuona hospitali zile zenye uchakavu mkubwa beyond repair tunafanya ujenzi mpya, lakini zile ambazo zinaweza kukarabatika, tutakarabati. Kwa hiyo, kauli ya Serikali ni kwamba kufuatia tathmini ambayo tutaifanya katika hospitali ya Makete tutatoa maelekezo rasmi kwamba Shilingi Milioni 900 inakwenda kujenga ama inakwenda kukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Vituo vya Afya vya Kitulo, Zahanati ya Nungu na nyingine kuhitaji vifaatiba. Katika mwaka wa fedha ujao, Serikali imetenga milioni 450,000 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati katika Jimbo la Makete ili vituo hivi viweze kupata vifaatiba. Ahsante.

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Makete?

Supplementary Question 2

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumuuliza swali la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, wananchi wa Kata ya Gale, na Kata ya Makanya, wamejenga viuo vya afya kwa nguvu zao wenyewe.

Je, ni lini Serikali itatoa milioni 250 kama ilivyokuwa inatoa fedha hizo kwenye vituo vingine? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka mkakati ambao umeendelea kutekelezwa na Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi kwamba Serikali imeendelea kupeleka fedha Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, tumeendelea kupeleka Milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati na hospitali za Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi vituo ambavyo wananchi wameanza ujenzi, Serikali itapeleka fedha ili tuweze kukamilisha ujenzi huo, ahsante. (Makofi)