Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jeremiah Mrimi Amsabi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Primary Question
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara Jimbo la Serengeti hasa za vijijini ambazo hutumika kusafirishia mazao?
Supplementary Question 1
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi tena. Nishukuru majibu ya Serikali yaliyotolewa kwa swali, lakini niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza jumla ya barabara ambazo zilijengwa 2021/2022 na zitakazojengwa mwaka wa kesho zinaonesha wastani wa kilomita 100 tu kwa mwaka. Sasa basi jumla ya barabara zinazohudumiwa na TARURA ni zaidi ya kilomita 900, hii maana yake ni kwamba itatuchukua zaidi ya miaka tisa kujenga barabara zote zilizo chini ya TARURA katika Jimbo la Serengeti. Sasa basi Serikali haioni haja ya kutafuta fedha za ziada kwa ajili ya kuongezea Jimbo la Serengeti kwa sababu barabara ni nyingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tarehe 25 Julai, 2021, Naibu Waziri wa TAMISEMI aliwaahidi wananchi wa Serengeti kwamba barabara ya lami inayozunguka soko la Mugumu ingejengwa na kukamilishwa. Mpaka sasa hivi mkandarasi ameshasaini mkataba toka mwanzo wa mwaka huu lakini barabara ile haijengwi. Tunaomba commitment ya Serikali ya kujenga barabara ile ya lami ya kuzunguka soko la Mgumu? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Msabi kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuwakilisha ipasavyo wananchi wa Jimbo la Serengeti. Pili, kuhusiana na fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri ya Serengeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii imeendelea kuongeza fedha ambazo zinakwenda kufanya matengenezo na ujenzi wa barabara vijijini na mijini. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2020/2021, bajeti ya Serikali kupitia TARURA ilikuwa bilioni 255, lakini 2021/22 Serikali iliongeza kutoka 255 mpaka bilioni 722, zaidi ya mara tatu ya bajeti. Pia mwaka ujao wa fedha tumeongeza kutoka 722 mpaka bilioni 822 plus.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii yenyewe inaonyesha namna Serikali ambavyo ina commitment kubwa ya kuongeza fedha kupitia TARURA ili barabara zetu ziendelee kujengwa. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata wao mwaka 2020/2021, bajeti ilikuwa ndogo, lakini imeendelea kuongezeka na tutaendelea kuhakikisha tunaongeza bajeti ili barabara za Serengeti zijengwe vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na barabara ya lami inayozunguka Soko la Mugumu, naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi na Watendaji wote wa Mamlaka hii ya Barabara TARURA kuhakikisha mkandarasi huyu anaanza kazi haraka iwezekanavyo na vinginevyo tutachukua hatua mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha barabara inakamilika mapema. Ahsante.
Name
Mohamed Lujuo Monni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Primary Question
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara Jimbo la Serengeti hasa za vijijini ambazo hutumika kusafirishia mazao?
Supplementary Question 2
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Lahoda ndio kata maarufu sana kwa uzalishaji wa ufuta na alizeti kwa Kanda ya Mashariki, lakini barabara yao ya kutoka Ilasee, Lahoda hadi Handa na kuunganisha na Singida ni mbovu sana. Naomba kujua nini mkakati wa Serikali wa kuboresha barabara hii? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kwa kazi nzuri anayoifanya kwa Jimbo la Chemba na nimhakikishie kwamba Serikali imeweka mkakati mzuri sana kuhakikisha maeneo yote yenye mazao ya kimkakati kama alizeti, ufuta na kata ambazo amezitaja, kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara zile zinajengwa vizuri zinapitika vizuri ili wananchi waweze kusafirisha vizuri mazao yao. Kwa hiyo nitoe maelekezo kwa Meneja wa TARURA Chemba, wafanye tathmini ya bajeti iliyopo na kuweka kipaumbele kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa kama haya ili barabara ziweze kupitika vizuri. Ahsante.
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Primary Question
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara Jimbo la Serengeti hasa za vijijini ambazo hutumika kusafirishia mazao?
Supplementary Question 3
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ya swali la nyongeza. Barabara ya Chombe, Kaoze ni barabara muhimu sana na mvua za mwaka jana zilipelekea uharibifu mkubwa na ombi maalum lipo tayari Wizarani. Nataka kujua je, ni lini Serikali itaijenga barabara hii ya Chombe, Kaoze ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Kata ya Kaoze?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sangu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kufuatia mvua barabara zetu nyingi zimeathirika na Serikali imefanya tathmini, lakini wataalam wote Mameneja wa Mikoa na Halmashauri wameelekezwa kuleta maandiko maalum ya mapendekezo, lakini na gharama ya utengenezaji wa barabara hizo. Niwapongeze halmashauri hii wameshaleta andiko hilo, tunalifanyia kazi na mapema iwezekanavyo tutaona uwezekano wa kwenda kufanya matengenezo ili barabara ipitike vizuri. Ahsante.
Name
Dr. John Danielson Pallangyo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Mashariki
Primary Question
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara Jimbo la Serengeti hasa za vijijini ambazo hutumika kusafirishia mazao?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Changamoto za barabara Arumeru Mashariki zinasababishwa na hali ya kijiografia ambayo sio rafiki wananchi wengi wako milimani. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo ya barabara hizi kwa kiwango cha lami au kwa teknolojia nyingine yoyote ambayo itafanya barabara hizi zihimili mafuriko wakati wa mvua?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Pallangyo kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa Jimbo la Arumeru Mashariki. Pia nimhakikishie kwamba tunafahamu na tumefanya tathmini ya barabara ambazo ziko milimani katika Jimbo la Arumeru Mashariki na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tumeweka mpango kazi wa kutenga fedha kulingana na uhitaji. Kuna maeneo yenye milima yenye mvua nyingi na changamoto kadhaa. Kwa hiyo bajeti zetu sasa pamoja na vigezo vingine itazingatia sana hali ya hewa, lakini pia na uhitaji mkubwa wa barabara hizo. Kwa hiyo nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili tunalifanyia kazi.