Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, ni lini Mradi wa Climate Change utawafikia wananchi wa Tarafa ya Chamriho wanaokabiliwa na tatizo la ukame?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kata zote zilizotajwa hapo saba hazipo hata kata moja ambayo ipo kwenye Tarafa ya Chamriho; na kwa kuwa Tarafa ya Chamriho ina kata ya Nyamanguta, Nyamswa, Kitale, Salama, Bihingo, Mgeta na Unyali. Sasa ni lini Serikali itapeleka mradi huu ambao uko Bunda kwenye hizo kata alizotaja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa mradi huu unaelimisha watu juu ya madhara ya climatic change Serikali ina mkakati gani sasa wa kupeleka semina mbalimbali na warsha katika maeneo haya ili kuelimisha watu juu ya tabia nchi inayotokea kwenye maeneo haya?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi ukiangalia kwenye paragraph ya pili imeonesha kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, tunaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunakaa na wadau na wafadhili mbalimbali ili kuweza kupata fedha twende tukaendeleze mradi huo katika hiyo Tarafa ya Chamriho. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na Subira, lakini pia kama kuna namna ya kufanya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda watuandikie hilo andiko walilete kwetu Ofisi ya Makamu wa Rais, twende tukalipeleke kwa ajili ya kuliombea fedha ili tukakamilishe mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, miongoni mwa kazi yetu kubwa tunayoifanya katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira ni kuchimba visima maeneo mbalimbali ili kunusuru hali hiyo. Kwa hiyo nimwambie tu kwamba tunakwenda kutafuta fedha ili twende tukachimbe visima ili kuweza angalau kuokoa maeneo hayo huku tukisubiria mradi huo uweze kukamilika. Nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nipongeze majibu mazuri sana ya Naibu Waziri. Hata hivyo, kwa heshima ya Mheshimiwa Boniphace Getere na nikifahamu kwamba ameendelea kuwapambania wananchi wake kwa nguvu kubwa sana. Ofisi yetu itafanya kila liwezekanalo mwanzoni mwa mwaka wa fedha katika eneo hilo tutatengeneza borehole moja ya mfano kama kuwafariji wananchi wa Kata ya Chamriho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sambamba na maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri katika majibu ya awali. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Getere kwamba, tutakwenda kuchimba borehole ya haraka sana katika Kata ya Chamriho. Lengo letu ni kuanzia hapo kwanza wakati tukijadili mambo mengine, ahsante sana.
Name
Khalifa Mohammed Issa
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Mtambwe
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, ni lini Mradi wa Climate Change utawafikia wananchi wa Tarafa ya Chamriho wanaokabiliwa na tatizo la ukame?
Supplementary Question 2
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kisiwa cha Mtambwe Mkuu kilichopo katika Jimbo la Mtambwe, Pemba ni kisiwa ambacho kimeathirika sana na tabianchi, maji ya bahari yanaathiri sana makazi ya wananchi wasiopungua 500. Je, ni lini mradi huu wa climate change utawafikia watu wa Mtambwe Mkuu ili kunusuru kaya zao?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Issa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumeona hizo athari za kimazingira ambazo zimetokezea katika Kisiwa hicho cha Mtambwe Mkuu, lakini nimwambie kwamba aendelee kuwa na Subira, tupo kwenye michakato kuhakikisha kwamba maeneo yote ya visiwa ambayo yameathirika kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu, tunaendelea kutengeneza mazingira ili angalau visiwa hivyo viweze kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nitoe wito, visiwa hivi vinakuwa vinapata athari za kimazingira kutokana na shughuli za kibinadamu, watu wanakata miti hasa mikoko, watu wanafanya shughuli za ujenzi lakini na mambo mengine. Kwa hiyo pamoja na kwamba Serikali tunaenda kufanya juhudi ya kukiokoa na kukinusuru kisiwa hiki lakini kwa ushirikiano wa Wabunge na viongozi wengine wa Serikali, tuendelee kuwaelimisha wananchi wetu ili sasa waone namna na umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwenye maeneo haya hasa maeneo ya visiwa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved