Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Oran Manase Njeza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Primary Question
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:- Je, ni lini wananchi wa Wilaya ya Mbeya waliopisha mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme mkubwa wa Kilovolti 400 watalipwa?
Supplementary Question 1
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali na yanatia matumaini kwa wananchi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; mradi huu ulitegemewa kuwapatia umeme wa vijiji wanaopitiwa na mradi huu ikiwemo Vijiji vya Wambishe, Ihango katika Kata ya Ulenje na Vijiji vya Rusungomina katika Kata ya Iwindi na Bonde la Songwe ambako kuna viwanda vikubwa sana vinavyohitaji umeme mkubwa kwa ajili ya kuchakata madini. Sasa je, ni lini hawa wananchi watapatiwa umeme kwa mradi mbadala baada ya kuona huu mradi unasuasua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vilevile mradi wa REA III, awamu ya pili na mradi wa Densification umechelewa kwa kiasi kikubwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kunusuru hii miradi miwili ambayo ukiangalia mradi wa densification umepitwa na wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kuendelea kufatilia mradi huu mkubwa tunaouita TAZA wa kupeleka umeme mkubwa katika maeneo hayo. Nimhakikishie tu kwa kauli ya Serikali kwamba mradi huu hausuisui, lakini ni taratibu za kimanunuzi zinazofanya mradi uonekane unachukua muda. Hata hivyo, kama tulivyosema kwenye jibu la msingi tayari taratibu za kufanya fidia zimekaribia kukamilika na kwenye mwaka wa fedha ujao tunatarajia kuanza kufanya fidia. Tayari wafadhili wameshapatikana na fedha ipo na ni taratibu za kukamilisha maandalizi ya utekelezaji wa mradi zinazoendelea na zitakapokamilika mradi utaanza mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee kwamba tayari vijiji hivyo alivyovitaja katika maeneo hayo viko katika program ya kupewa umeme na mradi huu. Tunayo program inayoitwa Land End Connection ambayo tunawaunganisha watu kwenye maeneo ya miradi mikubwa inapopita kama ambavyo wale wenzetu wanaopitiwa na mradi unaotoka Iringa kupita Dodoma, kupita Arusha kwenda Namanga walivyoona tukifanya kwenye maeneo hayo na huku pia tutafanya hivyo hivyo. Kwa hiyo niwaombe tu wananchi wa maeneo hayo wawe na matumaini na Serikali itawapelekea umeme katika maeneo yao baada ya kukamilisha taratibu za mradi ambao unatarajiwa kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, kuhusiana na REA ni kweli REA kama alivyosema siku chache zilizopita Mheshimiwa Waziri alipokuwa akijibu swali tulipata changamoto ya mabadiliko ya bei, lakini suala hilo tumelichukua kwa uzito wake kwa kukaa na wakandarasi na kukubaliana bei mpya zenye uhalisia kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hayo, miradi hiyo katika maeneo mbalimbali inaendelea kwa hatua mbalimbali ya uthamini wa maeneo, ya kusimika nguzo, ya kuvuta nyaya kwa wale ambao walishapata vifaa hivyo kwa ajili ya utekelezaji. Kwa hiyo niwaonye, kuwaasa, kuwaomba, kuwashawishi na kuwashauri wakandarasi wote waendelee na utekeleaji wa miradi hii kwenye maeneo yao kwa sababu mikataba yetu ipo pale pale ili kuweza kufikisha azma yetu ya kukamilisha vijiji vyote vilivyobakia kwa wakati.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved