Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Primary Question

MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya kuchelewesha mafao kwa wastaafu?

Supplementary Question 1

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali kuhusiana na wastaafu kulipwa mafao kwa wakati, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko ya kuchelewa kulipwa mafao yao mapema na malalamiko makubwa yamekuwa kwamba kuna baadhi ya wastaafu makato yao yanakuwa hayajapelekwa kwenye mifuko hiyo. Nini kauli ya Serikali kwenye eneo hili kwa sababu limekuwa na usumbufu mkubwa ambao hauna sababu kwa sababu wamekuwepo kwenye utumishi kwa miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wastaafu wamekuwa wakiombwa taarifa zao upya baada ya kuwa wameshastaafu. Serikali inakuwa ina taarifa zao zaidi ya miaka 30 haioni kwamba ni usumbufu wa kuwaomba wastaafu ambao wamekuwa nao kwa miaka yote ya umri wao? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusiana na malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo tayari tumekwishakufanyia kazi, unakumbuka katika Bunge lako hili yalitolewa maelezo mahsusi na Waziri mwenye dhamana, wakati huo Mheshimiwa Mhagama, na sasa Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, tumekwishakuanza kufanya tathmini na mapitio upya kuweza kuhakikisha kwamba wanalipwa kwa wakati na tayari kuna mifumo mbalimbali ya kitehama ambayo imeanzishwa, ikiwemo mfumo wa MAS pamoja na CFM, hii yote ni kwa ajili ya kutengeneza ile membership administration system ambayo ni mfumo wa ki-TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo hivi karibuni tutaanza ziara ya mkoa kwa mkoa kuweza kuanza kusikiliza changamoto za wastaafu ikiwa ni pamoja na kuhakiki taarifa mbalimbali ili kuweza kuhakikisha kwamba wanalipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ameulizia kuhusiana na hawa wastaafu wanapoombwa taarifa mpya. Utakumbuka kwenye Bunge lako hili tulitoa taarifa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba hili suala la uombaji wa barua za wastaafu limefikia mwisho, kwa sababu taarifa hizi sasa ni wajibu wa mifuko yenyewe kuweza kuhakikisha zinatunza kumbukumbu sahihi za wanachama wake ikiwa ni pamoja na ndani ya huo mfumo wa membership administration service system, pamoja na mfumo wa NSSF weyewe ambao ni core fund management system zote hizi taarifa zitakuwa mle.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kutumia fursa hii kuwasihi waajiri kote nchini kuwasilisha michango kwa wakati ya wanachama ili wasihangaike. Pili kuhakikisha mfuko wenyewe unahakiki taarifa za wale wastaafu hata mwaka mmoja kabla ya kustaafu ili kupunguza usumbufu kwa watumishi hawa waliotumikia Taifa vizuri. (Makofi)

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya kuchelewesha mafao kwa wastaafu?

Supplementary Question 2

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Wafanyakazi wa TAZARA wamekuwa wakiidai Serikali mafao yao na wamechangia michango yao yote katika kipindi cha utumishi wao, TAZARA ilikuwa haipeleki michango kwa wahusika.

Je, Serikali inawasaidia vipi hao wafanyakazi ambao wengi wao wamefariki?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama alivyokwisha kuuliza kuhusiana na wafanyakazi wa TAZARA ambao wamekuwa na changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari jambo hili linaendelea kushughulika nalo lakini kwa nia njema ya dhati kabisa ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, ilitokana na ile mifuko minne ambayo iliunganishwa. Katika ile mifuko minne ilirithi deni la Shilingi Trilioni 1.02 ya wanachama hawa ambao walikuwa wanadai katika maeneo mbalimbali. Nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba nina furaha kwamba fedha hizo zimelipwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameongeza pia fedha zaidi ya Trilioni 2.17.

Name

Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya kuchelewesha mafao kwa wastaafu?

Supplementary Question 3

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, kiwanda cha nyuzi Tabora mpaka kinafungwa wafanyakazi wengi walikuwa hajalipwa mafao yao ya kustaafu. Ni lini Mheshimiwa Waziri upo tayari tuiongozane kwenda kuwasikiliza wale wastaafu?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwakasaka kama alivyouliza kuhusiana na wastaafu wa kiwanda hicho cha Tabora, nipo tayari kumpa ushirikiano kuwasikiliza, pia Serikali itatoa fursa hiyo kuweza kuhakikisha kwamba haki zao hazipotei. (Makofi)