Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Je, ni nini mpango wa Serikali kufanya asilimia 50 ya wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano katika shule za Kata watoke ndani ya Halmashauri?

Supplementary Question 1

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Elimu bila malipo imeweza kuibua vijana wenye vipaji kutoka familia zenye mazingira magumu. Mfano, Bariadi mwaka juzi alitokea kijana aliyepata ‘A’ zote katika masomo yake. Wanafunzi hao wamekuwa wakipangwa shule maalum au shule zilizo mbali zaidi na kushindwa kumudu gharama za kusafiri na zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kuwabaini wanafunzi wa aina hii ili waweze kuwasaidia na kutimiza ndoto zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tumekuwa tukiomba mabweni kwa ajili ya shule zetu za Kata na zinapokamilika shule hizi zinakuwa za Kitaifa. Je, Serikali haioni haja ya kuona kuwa na catchment area kama vile katika Mkoa au Wilaya kuwe na shule ya bweni ili tuweze kuwanusuru vijana wanaokatisha masomo kwa kutembea umbali mrefu. Kwa mfano, mwanafunzi anayetokea Lukale kilomita 40 kwenda Bukundi na kurudi kilomita 40? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba wanafunzi wote wenye vipaji Serikali inawazingatia, na inapotokea wanafunzi waliofanya vizuri kama huyo na bahati mbaya anakuwa ameenda katika maeneo ambayo hakustahili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumefungua dirisha, mnatuletea hayo maombi na tunaweza tukafanya mabadiliko mengine. Kwa hiyo, hilo liko wazi na liko ndani ya uwezo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ujenzi wa shule za bweni katika ngazi ya mkoa kwa kuzingatia hayo; umbali, mahitaji na vipaji, ndiyo maana kwa mwaka huu wa fedha na mwaka 2021, Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ameamua kujenga Shule za Kimkoa kwa wasichana. Mwaka 2021 tumeshapeleka fedha shule 10 na mwaka huu vile vile tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule nyingine 10 za kimkoa ambazo zitapokea wasichana wenye vipaji katika mikoa husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba lengo la Serikali litafikiwa na tunafanya hivyo kupunguza umbali pamoja na kuongeza tija ya elimu katika maeneo husika, ahsante. (Makofi)