Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Willy Qulwi Qambalo (38 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ushirika wa Wafugaji (Ayalabe Dairy Cooperative Society) na Ayalabe SACCOS Wilayani Karatu ni vyama vyenye usajili na viliingia katika mgogoro mkubwa mwaka 2014 na Serikali imetumia muda mwingi na rasilimali nyingi kuutatua, lakini bila mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, ngazi mbalimbali zikiwemo: Afisa Ushirika Wilaya na Mkoa; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Ushirika - Mei, 2015; na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika – Aprili, 2015 walitoa ushauri kunusuru ushirika huo lakini viongozi na baadhi ya wanaushirika huo wameendelea kupuuza na kukaidi yote. Mali ya ushirika huo zimeendelea kuharibika na Halmashauri ya Wilaya ilitoa sh. 500,000,000/=.
Mhshimiwa Naibu Spika, tangu Machi, 2015, Naibu Waziri alipotembelea vyama hivyo, hakuna kinachoendelea hadi hivi sasa na vyama hivyo viko kinyume na sheria, kwa kuwa muda wa viongozi umeshakwisha. Mgogoro huu uko ofisini kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania ili atoe maamuzi au ushauri kulingana na sheria na kanuni za Vyama vya Ushirika. Namwomba Waziri wa Kilimo na Mifugo, achukue hatua stahiki sasa kabla mali za ushirika huo hazijapotea zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna dhambi kubwa anafanyiwa mkulima ni kumfikishia mbegu wakati wa msimu wa kilimo/kupanda imeshapita.
Misimu ya kupanda inafahamika katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kwa nini mbegu zinachelewa? Hatujasikia hatua iliyochukuliwa kwa uzembe huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wetu wanajua aina ya mbegu inayofanya vizuri katika maeneo yao. Baadhi ya mawakala wamekuwa na tabia ya kupeleka mbegu zisizofaa, kwa mfano mbegu za mahindi za muda mrefu (miezi 3 - 4) kupelekwa katika maeneo yenye mvua haba. Maoni ya walengwa/wananchi yaheshimiwe na wapelekewe mbegu za uchaguzi wao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo wa sasa wa kushughulikia masuala ya elimu nchini unaofanywa na Wizara mbili (TAMISEMI, na Wizara ya Elimu) umeleta mkanganyiko mkubwa sana. Elimu yetu siku za nyuma ilisimamiwa na Wizara moja na ndiyo maana tulifanya vizuri. Ninashauri Serikali kurudisha mfumo na muundo wa awali wa Wizara moja tu kama kweli tunataka kupiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao uhaba mkubwa sana wa walimu wa sayansi kwenye shule zetu hasa za sekondari za Kata. Mwalimu ana nafasi kubwa katika kumsomesha mtoto. Iweje mtoto anaanza form one hadi form four hajapatwa kufundishwa na mwalimu wa sayansi kisha watoto hao tunawapa mtihani baada ya miaka minne.
Ninashauri Serikali kufanya jitihada za maksudi kuhakikisha walimu wanapatikana. Serikali pia itoe motisha ya mishahara mizuri kwa walimu ili walimu wakae kwenye kazi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za sekondari za Kata, mfano; Endallah, Endabash, Baray, Mangola, Upper Kitete, Kansay, Orbochand, Getamock zina walimu pungufu sana wa masomo ya sayansi. Ninaiomba Wizara ipeleke walimu hao Karatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ada elekezi huu siyo muda wake. Serikali iboreshe shule zake badala ya kutaka kupunguza ada kwa shule binafsi. Niulize, hivi humu ndani ya Bunge nani ana mtoto wake katika hizi shule za Kata? Tumepeleka watoto shule za binafsi baada ya kuona elimu inayotolewa huko ni bora kuliko ile inayotolewa katika shule za Serikali. Serikali iachane na ada hizo na kama kuna wazazi wanaona hizo shule za binafsi ni ghali basi wapeleke watoto wao kwenye shule ambazo ada zake wanazimudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ilitoa majengo na maeneo yake Ayalabe karibu na Mji wa Karatu ili kuanzisha chuo cha Ualimu, miundombinu ya chuo hicho iko tayari. Nimwombe Waziri wa Elimu afike, akague chuo hicho ili kianze kutumika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kuendelea kukamilisha zoezi la usanifu wa kina wa barabara ya Oldeani Junction - Matala - Mwanuzi - Kolandoto. Barabara hii ndiyo barabara ya kuunga Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu hadi Mwanza. Hii barabara ni fupi sana na ujenzi wake hautasumbua maana inapita katika maeneo mepesi kufikika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inapita katika maeneo yenye vitunguu, mpunga, mahindi na pia eneo muhimu sana kwa ufugaji. Barabara hii ni rafiki wa mazingira na ndiyo maana inaitwa Serengeti Southern By pass.
Naomba Serikali itafute fedha za ujenzi haraka sana ili kutimiza sera ya kuunga mikoa, lakini pia ahadi ya viongozi wa juu wa Awamu ya Nne na ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara ya Karatu - Mbulu - Haydom - Matala iliyoingia mwaka huu kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na baadaye usanifu wa kina. Ni imani yangu kuwa baada tu ya maongezi hayo kazi ya ujenzi itaanza mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba barabara ya Manyara - Kitete - Losetele ipandishwe hadhi kutoka barabara ya Halmashauri kwenda kuwa barabara ya Mkoa; barabara hii inaunganisha Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Monduli. Ni barabara inayopitisha mazao mengi kuelekea soko lililoko Arusha. Nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa fursa niweze kuchangia katika sekta hii muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, lakini pia kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaongea juu ya sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 65.5 ya wananchi wetu. Suala la ajira nchi hii limekuwa ni jambo ambalo halijawahi kupata suluhu; lakini hapa tunayo sekta ambayo inaajiri asilimia 65 ya watu wetu, lakini ni sekta ambayo pia tunaipa fedha kidogo kiasi hicho. Takwimu zimetuambia Sekta ya Kilimo mwaka 2015 na mwaka 2016 imechangia asilimia 29 ya pato la Taifa. Nadhani tuna kila sababu ya kuitizama sekta hii ili iweze kuchangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea asilimia 65 ya Watanzania, Watanzania waadilifu, watiifu ambao wamebaki vijijini wanazalisha, siyo wale waliokimbilia mijini, lakini Watanzania hawa ni wale ambao wanakumbana na changamoto mbalimbali za kimaendeleo. Ukija ukame ni wao; wadudu waharibifu ni wao, kwelea kwelea ni wao, tatizo la maji linaandama kundi hili, lakini bado ni kundi ambalo mimi kwa mtazamo wangu naona hatujalitendea haki kikweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tumeanza kujadili bajeti za Wizara ni kama tumefika nusu ya safari. Sasa mimi sijui hizi fedha pengine hizo Wizara zinazokuja ndiyo zitapewa asilimia hizo nyingi 70%, 80% na 90%, lakini tangu tumeanza ni 3%; sana sana tumekwenda mbele asilimia 50 na kitu. Hizi fedha zinasubiri kupangiwa Wizara ipi, kama Wizara nyeti kama hii inapewa fedha kidogo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kilimo cha zao la mahindi. Zao la mahindi ni zao la biashara lakini pia ni zao kuu la chakula kwa maeneo mengi ya nchi yetu. Zao hili kwa takwimu za kitabu cha Waziri linachangia karibu tani milioni sita kwa mwaka. Tukiwa serious tunaweza kuzalisha zaidi ya mara tatu au nne ya kiasi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa kwenye kilimo cha zao la mahindi ni suala la mbegu. Utafiti unaonesha kabisa ukilima mahindi ukatumia zile mbegu zetu za asili, zile za kuchukua tu, utavuna kidogo, lakini ukipanda mbegu zile zilizoboreshwa, utapata angalau kiasi cha kutosha kwa heka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu wamesema, mbegu za mahindi ambazo zimeboreshwa ni ghali sana na sehemu kubwa inatoka nje ya nchi. Sasa Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, mimi sijui wataacha legacy gani mtakapoondoka katika eneo hili la kilimo cha mahindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tunaomba ili tuwakumbuke mtuambie Kampuni ya TANSEED iliyokuwa inazalisha mbegu nchini miaka ya nyuma, imekwenda wapi? Mtuoneshe hilo kaburi mahali lilipo tukafufue ili tuzalishe mbegu ndani ya nchi yetu ili bei ya mbegu iwe rahisi.

Wakulima wengi wanajitahidi sana, wanalima kwa muda, lakini linapokuja suala la kupanda, kwa kweli mbegu inawakwaza. Mwisho wa siku wanaishia kwenye kupanda kile chochote ambacho ama amenunua dukani au amepewa chakula cha msaada na matokeo yake kwa heka anaishia kupata gunia mbili au tatu. Tunao uwezo wa kuongeza uzalishaji wa zao la mahindi kama tutazingatia suala la mbegu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye zao la mbaazi. Kwa miaka ya karibuni, zao la mbaazi limekuwa ni mkombozi kwa wakulima wengi kwenye zile kanda ambazo zao hili linalimwa. Msimu wa mwaka 2015 zao hili lilikwenda kwa kilo karibu shilingi 3,000, msimu wa mwaka 2016 zao hili likashuka hadi shilingi 900; wakulima wamechanganyikiwa, wamekosa hamu ya kulima zao hili kwa sababu bei hailipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba ndugu zangu mliopo kwenye dawati la Wizara
hebu mtusaidie kutuunganisha na masoko ya zao hili yalioko ndani au nje ya nchi ili wakulima wetu waweze kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwenye eneo hili ni suala la wanunuzi wa zao hili. Wapo wanunuzi ambao hadi leo tunapoongea, bado hawajawalipa wakulima fedha zao baada ya kuchukua mbaazi zao. Tunaomba Mawaziri mtakapokuwa mnahitimisha mtuambie, wanunuzi wa mazao kama hawa, ambao wanawakopa wakulima mwaka mzima, wachukuliwe hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye eneo la pembejeo. Wenzangu pia wamelisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imejaa wataalamu wa kila aina na wa kila rangi, hivi inawezekanaje pembejeo zinachelewa kwenda kwenye maeneo yanayohusika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnajua watu hawa wanahitaji mbegu kwa ajili ya kupanda; msimu wa kupanda ni Januari, lakini mbegu zinaenda mwezi wa tatu za kazi gani? Kwa hiyo, nadhani kuna vitu vingine tunapopiga kelele, sijui tatizo lipo wapi? Kwa nini hayo marekebisho yasifanyike? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hata kabla sijaingia Bungeni, suala la ucheleweshaji wa pembejeo limekuwa ni jambo ambalo halijapata ufumbuzi. Nadhani ni vitu vidogo sana. Suala la kalenda ya kilimo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu inafahamika; na pembejeo hizi kwa bahati nzuri au mbaya inawalenga watu wachache. Hivi inashindikana nini kupeleka tani tano au kumi kwenye Wilaya X kwa muda ili wananchi wale waliolengwa walime pia na kupanda kwa muda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hili jambo linawezekana. Hebu mzizi huu sasa ukateni, fitina kwenye eneo la ucheleweshaji iishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani ni watu muhimu sana kuwasaidia wakulima wetu, lakini tunao wachache sana.

Kwa hiyo, nilikuwa nadhani katika Wizara hii kama kuna eneo ambalo mnaweza kuwatendea haki wananchi wetu ni kuwapeleka Maafisa Ugani wa kutosha. Wale wachache walioko vijijini, sasa hivi ndiyo wamekuwa Acting WEOs na Acting VEOs hawafanyi zile kazi zao ambazo zimewapeleka kule. Kwa hiyo, naomba Maafisa Ugani pia wapewe uwezeshwaji wa vifaa vya usafiri ili waweze kuwafikia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amechelewa kupiga marufuku uchinjwaji wa punda. Amechelewa kabisa! Nilitegemea angesema kesho. Wanyama hawa wanaisha na wanyama hawa wanazaliana kidogo kidogo sana. Kule vijijini wanyama hawa ambao walikuwa wanatusaidia kusafirisha vitu, kuchota maji na kupeleka vitu sokoni, sasa hivi wanaibiwa hovyo.

Kwa hiyo, naomba suala la kupiga marufuku ikiwezekana punguza huo muda. Siku 45 zinatosha kumaliza punda katika nchi hii. Hao wanaofanya biashara ya punda, sasa hivi wamebadilisha mbinu nyingine, wanawachinja huko huko na ngozi wanazichukua na wanapeleka huko wanakopeleka. Wanyama hawa ili wasiishe, hiyo marufuku naomba ipunguze muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme juu ya suala la kilimo cha umwagiliaji. Kilimo chetu kwa muda mrefu kimekuwa ni kilimo kinachotegemea mvua. Hebu tuchukue jitihada za makusudi za kuelekea kwenye kilimo cha umwagiliaji. Nchi hii, leo mvua inanyesha, baada ya wiki mbili, tuna shida ya maji. Tuwekeze kwenye miradi mikubwa mikubwa ambayo itachochea kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Olenasha jirani yangu, anafahamu kwamba sisi Mang’ola ni wakulima wazuri sana wa vitunguu na tunazo chemchemi zenye uwezo mkubwa wa kumwagilia mwaka mzima, lakini tatizo letu mifereji ile ya kumwagilia haijajengewa. Hebu wekeni mpango tusaidieni wananchi wa Mang’ola waweze kumwagilia vizuri baada ya ile mifereji kujengewa ili maji yafike kwa wakulima walioko upande wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee juu ya migogoro ya wakulima na wafugaji. Migogoro hii imekuwa ni ya muda mrefu. Jitihada mbalimbali zimefanyika, lakini jambo hili naishauri Serikali, hebu lifike mwisho. Hawa watu wawili wote ni Watanzania; hebu tuwekeni pamoja kwenye meza moja tuongee, tusiwe tunagomba kila siku. Nchi hii imetawaliwa na migogoro ambayo haiishi. Kila mmoja hapa anachangia kwenye pato la Taifa. Huyu mfugaji kwa sehemu ni kama alikuwa ameachwa achwa, ni kama hakulindwa. Ifike mahali tutambue kwamba hata ndugu zetu wafugaji wana mchango kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya kuchungia hayapo. Serikali sasa hivi inasema tutenge maeneo, hivi tutatenga kutoka wapi? Hivi ukisema Wilaya ya Karatu tutenge maeneo ya kufugia, yako wapi? Hebu mje mtembee mwone, hakuna eneo la kufugia! Pia mje na mpango ambao utatusaidia hata yule ng’ombe moja au wawili tuwafuge kwa ubora ili watupe kile ambacho tunataka. Mkisema tuuze ng’ombe, hivi mnadhani wafugaji hawajui mahali minada ilipo? Tunajua mahali minada ilipo, lakini hatuuzi kwa sababu ng’ombe ni benki yetu. Sasa ukiniambia niuze, wewe mbona accounts zako za NBC na CRDB hufungi? Kwa hiyo, suala siyo kuuza mifugo, suala ni kumsaidia mkulima ili afuge kwa kisasa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwenye eneo la hifadhi ya chakula. Tunapoteza chakula kingi kwa sababu ya uharibifu unaofanywa na wadudu. Takwimu zinasema, karibu asilimia 40 ya tunachokivuna, kinapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Muda wangu nitagawana na jirani yangu Mheshimiwa Japhary, kama atawahi, asipowahi nitaendelea mimi mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya mwanzo jioni hii ya leo. Tunapoongelea uchumi wa viwanda, ni jambo la kufurahisha kwamba bajeti tunayoijadili jioni hii ina mchango mkubwa sana katika kutufikisha kwenye uchumi huo wa viwanda. Naomba nijielekeze katika eneo la kwanza la upembuzi yakinifu, mara nyingine usanifu wa kina na wakati mwingine wanapenda kutumia maneno Mhandisi Mshauri na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua sana umuhimu wa zoezi hilo la kabla ya miradi kutekelezwa, lakini niseme kwamba, zoezi hili limekuwa ni kichaka cha kujifichia kwenye Wizara hii, Mawaziri wakijibu asubuhi maswali utaambiwa mradi huo uko kwenye upembuzi yakinifu; baadaye utaambiwa uko kwenye usanifu wa kina; baadaye utaambiwa Mhandisi Mwelekezi anaendelea. Kwa hiyo, nataka kushauri, wananchi wetu kule nje wanachotaka kuona, ni miradi inatekelezwa. Pamoja na kwamba hatua hii haiepukiki na ni muhimu sana, nashauri hebu tupunguze muda wa mazoezi haya, ili hatimaye tuingie kwenye masuala ya utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingine mazoezi haya yamechukua miaka ya kutosha miaka mitano, upembuzi yakinifu siku nyingine miaka mitano, usanifu wa kina na kadhalika, kwa hiyo, mradi utakuja kutekelezwa baada ya miaka 10, 15 mpaka 20. Tuna mfano hapa uwanja wa ndege wa Msalato, ukienda pale Msalato hadi leo ni pori tupu, lakini miaka kadhaa iliyopita mazoezi haya yalifanyika, yakatumia mabilioni ya fedha zetu. Pia baadaye zoezi kama hilo hilo likafanyika, kwa hiyo, ni kama duplication ya jambo hilo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la pili, la madeni ya wakandarasi, nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha hotuba yake, bado Serikali inadaiwa. Huwa najisikia vibaya sana napodaiwa, wanasema dawa ya deni ni kulipa, kwa nini Serikali hii isiwalipe hao Wakandarasi? Miradi mingi iliyotekelezwa huko nyuma tunadaiwa, iwe kwenye maji, iwe kwenye eneo hili la ujenzi na kadhalika na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Serikali ili kulinda heshima yake ikwepe jambo hili na tunaingia kwenye matumizi ya ziada ya kulipa fedha za hawa wakandarasi kwa kuwa tumekaa na fedha zao. Kwa hiyo, nashauri kama Serikali hii kweli iko makini, kama Serikali hii ni Serikali ya “Hapa Kazi” hebu tuwalipe wakandarasi ili pia pale wanapokosea tuwe na nguvu ya kuwasukuma na kuwasahihisha. Wakati mwingine hawa wakandarasi wanaishia kufanya kazi zetu vibaya kwa sababu tu wanatudai. Kwa hiyo, nataka kushauri, hebu haya madeni ya wakandarasi tuyalipe kwa muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ni eneo la zile barabara zilizoko kwenye ngazi ya Halmashauri. Barabara hizi ziko nyingi sana na barabara hizi zinahitaji fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo, lakini fedha tunazopelekewa ni kidogo, hazitoshi. Nimesikia hapa ndani Waziri amesema yapo maombi zaidi ya 3,000 ya kupandisha hizi barabara. Nashauri hebu maombi haya yafanyiwe kazi ili hizi barabara kweli ziweze kuchukuliwa na TANROAD ambao wana nguvu kubwa kuliko sisi Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la kuunganisha mikoa, hili ni jambo la kisera na kwa kuwa ni jambo la kisera linahitaji kuwa ni jambo la kutekelezwa. Iko mikoa mingi ambayo mpaka sasa hivi bado haijaunganishwa; ukiwa Arusha ukitaka kwenda Musoma, inabidi upite nchi ya jirani; ukiwa Arusha ukitaka kwenda Mwanza inabidi upite barabara ndefu ya kupitia Singida na Shinyanga, lakini zipo barabara ambazo unaweza kupita ukafika mapema.
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, dakika tano hizo.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa usambazaji umeme vijiji unaotekelezwa na REA katika Awamu ya Pili uligusa vijiji vichache sana katika Wilaya ya Karatu. Serikali inatamka kuwa Awamu ya Tatu itaelekezwa katika vijiji vyote vilivyobakia nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni habari njema kwa ananchi wote. Nimwombe Mheshimiwa Waziri agawe orodha ya vijiji kwa kila Wilaya ili sisi Wabunge tuweze kufuatilia utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Karatu inavyo visima virefu 13 vya maji ambavyo vinaendeshwa kwa mashine za Diesel.
Mheshimiwa Naibu Spika, uendeshaji wa visima kutumia Diesel Engine ni gharama kubwa unafanya wanachi kushindwa kuendesha miradi hii. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii apeleke umeme katika miradi hii ya visima vilivyoko Vijiji vya Basodamsh (2), Emaranek (3), Kiviwasu (2), Rhotia Kainan (1), Endabash (1), Gilambo (1), Gendaa (1), Getamoa (1), Kambi Faru (1).
Mheshimiwa Naibu Spika, tukifikisha umeme katika visima hivi pia kwa vijiji ambavyo visima vipo vitanufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Madini. Serikali imeteua mawakala kukusanya kodi au tozo ya madini ya ujenzi Example mchanga, kokoto, mawe, moram na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limeleta vurugu na mkanganyiko mkubwa. Kwa muda wote wa nyuma madini hayo yamekuwa chini ya Halmashauri za Vijiji kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya. Mfano, huko nyuma tozo zilizokuwepo ni; kijiji sh. 5,000/=, Halmashauri sh. 5,000/= na wapakiaji Sh. 10,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakala huyo aliyeletwa sasa naye anachukua sh. 5, 000/= na Serikali Kuu sh. 3, 000/=. Jambo hili limeongeza gharama ya kupata mchanga. Lori tani saba kutoka Sh. 20, 000/= hadi Sh. 28, 000/=, huyu Wakala anapata sh. 5, 000/= kwa kila tani saba kwa sababu gani? Hivi Halmashauri zetu haziwezi kukusanya mapato?.
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu bwana hachangii matengenezo ya barabara, jambo hili halikubaliki kabisa na litaleta mgogoro mkubwa. Tunaomba Waziri amuondoe wakala huyu na ushuru huo ukusanywe na Halmashauri ya Wilaya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nichangie Wizara hii muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuonesha masikitiko yangu kwa Mheshimiwa Waziri. Nimeona kwenye kile kitabu cha migogoro ya ardhi, Wilaya ya Karatu haipo. Nilimkabidhi mmoja wa wahudumu wa hapa ndani orodha ile na nikamsindikiza kwa macho yangu, Mheshimiwa Waziri alikuwa amekaa pale, alimkabidhi na aliisoma. Simlaumu, nimemwandalia orodha nyingine hii hapa ambayo ni more comprehensive. Nitampatia baadaye, ikibidi nipige picha ili nipate ushahidi kwamba nimemkabidhi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri imeainisha mamlaka tatu ambazo zinashughulikia masuala ya ardhi. Ziko mamlaka za Halmashauri za Vijiji, iko mamlaka za Halmashauri ya Wilaya na Mji na iko pia Wizara yake. Namwomba Mheshimiwa Waziri asiogope, asihofu. Akiona tunakuja kwake iwe ni kiashiria tosha kwamba wale walioko kule chini wameshindwa. Pia ionekane kwamba inawezekana wale walioko kule chini pia wanachangia katika matatizo yaliyopo. Kwa hiyo, tunakuja kwake kwa kuwa tumeshakata tamaa na wale ambao walipaswa kutusaidia kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo migogoro mingi ya ardhi na migogoro hii mingine imesababishwa na sera. Tunayo ile sera iliyokuja mwaka 1975 ya Operesheni Vijiji, imeleta mkorogano mkubwa sana. Pia migogoro mingine imesababishwa na sisi viongozi wa kisiasa. Pia iko migogoro mingine na ndiyo mingi zaidi, imesababishwa na baadhi ya Watendaji katika ngazi mbalimbali za utendaji wao; Mabwana Ardhi wa Wilaya na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, akiona tunakuja kwake awe na amani kabisa. Tuna nia njema, amejaribu, nami naamini hatabadilika, aendelee na kasi hiyo. Tuna imani kiasi fulani kwamba amejaribu na ataendelea na kasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo migogoro mingi sana ya ardhi. Wamesema Wabunge wengine, shida kubwa ya ardhi ya nchi hii, haijapimwa. Kuna shida gani kupima ardhi ya nchi hii na kuwamilikisha wale ambao wanayo? Kitabu cha Waziri kimesema ni asilimia 15 ya ardhi ya Tanzania ndiyo imepangwa na imepimwa, nami naamini hii ni ardhi iliyoko mijini, ardhi kubwa iliyoko vijijini inaonekana haina mwenyewe, lakini ile ardhi ina mwenyewe, yuko yule ambaye ameikalia hadi sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba na naishauri Serikali, kama kweli tuna nia ya dhati ya kumaliza migogoro hii au kuipunguza kwa kiwango kikubwa, Serikali ije na mpango madhubuti wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kisheria. Bila kufanya hivyo, migogoro ya ardhi, leo utatatua, kesho utazaliwa mwingine. Kwa hiyo, kila kukicha utaendelea kupata migogoro hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana mpango mzuri anaoufanya kule Ulanga na Kilombero; program ya upimaji wa ardhi katika zile Wilaya tatu, ni mpango mzuri, lakini atamaliza Tanzania baada ya miaka mingapi? Kama kwa miaka mitatu anafanya mpango wa majaribio katika Wilaya tatu. Anahitaji zaidi ya miaka 50 kupima ardhi ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri na ameandika pale, amesema mpango ule ukifanikiwa utasambaa katika nchi nzima. Majibu anayo, mpango ule lazima ufanikiwe, ikibidi akahamie kule yeye mwenyewe asimamie ile kazi ili ule mpango ufanikiwe ili ardhi ya wananchi ipimwe na wamilikishwe kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la mashamba ya wawekezaji, nchi hii inawaabudu sana hawa watu wanaoitwa wawekezaji. Nimeangalia kwenye kile kitabu iko jumla ya karibu ekari milioni 5.6 ambazo hawa waheshimiwa wamezikalia. Sisi kule Karatu tunayo mashamba 40 ambayo yana jumla ya ekari 45,000 hainingii kwenye akili kwanza kwa nini hawa watu walipewa mashamba haya? Kwa sababu, mashamba mengi wamepewa kwa ajili ya kulima na kufuga, wengi wa hawa ni watu waliotoka nje, hivi tulikuwa tunahitaji mtu atoke Ulaya kuja kufuga hapa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wafugaji wazalendo ambao sasa hivi maisha yao ni kutangatanga na kuhamahama kutafuta malisho kwa sababu, ardhi kubwa imechukuliwa na hawa waheshimiwa. Hawa wawekezaji wamepewa maeneo ambayo ni very prime, yana maji, yana rutuba na yana mvua za uhakika. Wananchi wetu wamesukumwa wamekaa maeneo ambayo mvua ni kidogo sana na nimeona mashamba mengine karibu muda ule wa miaka 99 au 71 unakaribia kwisha, naomba hiyo miaka ikiisha mtushirikishe sisi watu wa maeneo hayo wasipewe tena maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hebu atusaidie hivi hawa wawekezaji wanailipa Serikali shilingi ngapi kwa kuwa na maeneo hayo? Kwa sababu, baadhi ya wawekezaji hao badala ya kufanya yale ambayo wamekubaliana kufanya, leo wameyapangisha au kukodisha mashamba hayo kwa watu wengine na wana-charge hela nzuri tu! Kule kwetu Karatu eka moja ya shamba hilo lililoko kwenye maeneo mazuri unalikodisha kwa sh. 200,000/= kwa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikipiga mahesabu ya harakaharaka kwa eka 45,000, ungeweza kupata shilingi bilioni tisa kutoka Karatu tu. Mheshimiwa Waziri mashamba yale 40 ya Karatu yanakuletea shilingi ngapi? Nadhani watakuwa wanaletea kidogo sana. Kwa hiyo, niombe na wengi wa hawa wawekezaji wanakaa nje ya nchi, yaani wanakuja tu kupumzikia kule wakati wa baridi kwenye nchi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mashamba mawili ambayo yamekuwa ni tatizo katika Wilaya ya Karatu; liko shamba la mwekezaji anayeitwa Acacia Hill au Ndamakai Estate. Mheshimiwa Waziri nina uhakika anayo taarifa ya shamba hili, Mkuu wa Mkoa anazo taarifa, Mkuu wa Wilaya anazo taarifa na hata Mheshimiwa Waziri alipopita Karatu kwa muda mfupi aliambiwa habari ya shamba hili. Huyu bwana ni mbabe, ni katili, ni mkorofi na hata haijui Serikali. Ni mtu wa ajabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu bwana anamiliki zaidi ya eka 3,840 lakini robo tatu ya eneo hilo halijaendelezwa, limekuwa ni mapori bubu ya kufugia wanyama tembo na wale wengine. Sasa siku hizi ni lazima asubuhi wototo wa shule wasindikizwe ili wasikutane na wanyama hao. Sasa mtu ana eka 3,840 ameendeleza tu robo, tena ameendeleza kwa kahawa ambayo imekwishazeeka, maeneo mengine yote ni pori! Mheshimiwa Waziri lile shamba ni size yake naomba aje autengue umiliki wa yule bwana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huyu bwana pia, kwa ukorofi niliousema amediriki kuwanyima wananchi barabara. Barabara ya mita sita kwa kilometa tano ukifanya mahesabu ya eneo ni karibu eka sita. Barabara ambayo inaokoa muda na gharama ya kwenda kijiji cha jirani ambacho ingebidi utumie karibu muda wa masaa mawili kwa umbali wa kilometa karibu 50, yaani kwa kukatiza pale unahitaji dakika 20, lakini huyu bwana kwa ukorofi wake amewanyima wananchi eneo hilo. Kwa hiyo, inabidi wazunguke kutoka Kijiji cha Mang‟ola Juu kwenda Kijiji cha Makumba, mtu anaingia gharama ya kwenda kilometa 40 kwa sababu ya ubabe na ukatili wa bwana huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba huyu bwana ashughulikiwe kabla wananchi hawajachukua hatua, kwa sababu yeye anapotaka kwenda mjini anapita kwenye maeneo ya wananchi. Tutamfungia kule kwenye kisiwa na ataishia kule! Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri achukue hatua za haraka kumnusuru huyu bwana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko shamba lingine jirani na hapo Mang‟ola Juu linaitwa Tembotembo, lina matatizo hayo hayo ni mashamba ambayo yameendelezwa kwa kiwango kidogo sana. Kwa bahati mbaya taarifa ambayo halmashauri imeandaa na taarifa ambayo iko kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri zinakinzana, lakini naamini tutashirikiana, ili kupata taarifa ambazo ni sahihi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri haya mashamba mawili naomba ayachukulie hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la uhakiki wa mipaka ya Ngorongoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yale niliyochangia kwa kuongea, naomba kwa sababu ya muda haya nayo yaunganishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imesababisha migogoro ya ardhi katika vijiji vinavyowazunguka. Mipaka ya NCAA iliyowekwa miaka ya 1950 inafahamika na alama bado zipo na pia GN inaonesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2002 Mamlaka ya Hifadhi ilifanya uhakiki wa maeneo yake na hapo ndipo migogoro ilipoanza. Mamlaka ilichukua maeneo ya wananchi ya kufugia mifugo katika vijiji vya Endramaguang na kijiji cha Lositete bila ya kuwashirikisha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa NCAA inahakiki mipaka yake kazi inayofanywa na Wizara ya Ardhi. Naomba kutahadharisha kuwa haki itendeke na uhakikiwe mpaka wa zamani na si ule wa mwaka 2002 ambao NCAA walijiwekea. Najua uhakiki huo umelipiwa na NCAA na isije kuwa sababu ya kupindisha haki. Hatutakubali hata mita moja ya ardhi ya wananchi wetu ipotee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utata wa mipaka halisi kati ya Wilaya ya Karatu na Wilaya za Ngorongoro Monduli na Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karatu iligawanywa kutoka Wilaya ya Mbulu na wakati huo mpaka ulikuwa pale juu view point. Eneo la msitu wa Great Northern Forest lilikuwa Mbulu. Baadaye eneo hilo la msitu lilipandishwa hadhi na kuwa msitu ndani ya hifadhi ya Ngorongoro. Hili haliondoi mpaka wa Karatu kuwa pale juu view point. Naiomba Wizara ilete majibu ya mpaka sahihi kati ya Wilaya za Karatu na Ngorongoro na pia kuleta timu ya wataalam ili kuonyesha mpaka sahihi kati ya Wilaya za Karatu na Monduli na pia Karatu na Mbulu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. QULWI W. QAMBALO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imejaaliwa sana kwa kuwa na vivutio vya utalii hadi kushika nafasi ya pili duniani. Hii ni zawadi na heshima kubwa aliyotupa Mwenyezi Mungu. Si watu wote nchini wanafurahi na kuwepo hifadhi za wanyama katika maeneo yao kutokana na manyanyaso na uonevu wanaofanyiwa na hifadhi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) haitendei haki wananchi wa vijiji vinavyozunguka. Mipaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliwekwa tangu mkoloni na inafahamika na beacons zipo katika mazingira ya ajabu sana. Mwaka 2002/2003 NCAA walifanya uhakiki wa mipaka yao na hapo ndipo walipopora maeneo ya wananchi ya malisho ya mifugo yao katika vijiji vya Endamaghang na Losetete. Tangu muda huo migogoro imeshamiri. Ikumbukwe wakazi wa kijiji cha Losetete walihamishiwa Lositete miaka ya 1950. Kuchua maeneo yao waliyopewa ni unyanyaswaji wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Wizara ya Ardhi imefanya uhakiki wa mipaka ya NCAA. NCAA ndiyo waliolipa fedha ya zoezi hilo na nitahadharishe Wizara kuwa isije ikawa uhakiki unaofanywa sasa ni kutaka kuhalalisha haramu iliyofanyika mwaka 2002/2003 walipohakiki. Nawataka NCAA wahakiki mipaka yao ya awali na siyo mipaka ya mwaka 2002/2003 waliyojiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni uharibifu unaofanywa na wanyama kutoka Ngorongoro (ndovu na nyati) kwenye mashamba ya wanavijiji katika vijiji vya Lositete, Kambisimba, Kambi ya Nyoka, Oldeani na Makulivomba. Wananchi wanajitahidi kulima lakini wanyama wanawatia umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la ajabu ndovu wanatoka crater hadi barabara ya lami iendayo Ngorongoro, askari wa doria hawatoshi na pia hawajawezeshwa. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha, aliambie Bunge hili Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa uharibifu wa mashamba ya wananchi unaofanywa na wanyama unadhibitiwa?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ilikuwa na mzozo wa mpaka na nchi ya Malawi ndani ya Ziwa Nyasa. Naomba Waziri aliambie Bunge hili mzozo huo umefikia hatua gani maana kwenye hotuba yake hajaugusia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni kati ya nchi zenye vivutio vya utalii vinavyopendwa duniani. Sijui ni kwa kiasi gani Ofisi zetu za Ubalozi zinasaidia kutangaza vivutio hivyo. Nchi ya China hivi sasa inakuja juu sana kuleta watalii, nimshauri Mheshimiwa Waziri na Maafisa wake wajipange kutangaza nchi yetu ili tupate fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema kuwa na utangamano wa Afrika ya Mashariki lakini isiwe ni kigezo cha kuwanyima watu wetu fursa za kiuchumi. Ni jambo lisilopendeza kabisa kuona hata kazi zile ambazo vijana wetu wanaweza kufanya zinafanywa na wageni toka nchi za nje. Mfano ukienda kwenye hoteli za kitalii na mashamba ya wawekezaji kazi za kuhudumia wageni hotelini au kusimamia vibarua mashambani zinafanywa na watu kutoka nje. Mbaya zaidi wageni hao wanawanyanyasa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpaka wa Kenya pale Namanga kuna urasimu mkubwa upande wa Tanzania. Wakati wenzetu wa Kenya upande wao wa mpaka mambo yanaenda haraka, ukija upande wa Tanzania hata kule kugonga muhuri inachukua muda sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali ili kuongeza ufanisi. Wabunge kwa nyakati mbalimbali wanashauri, ni vizuri Serikali ikawa sikivu na kuchukua ushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge la Bajeti, Wabunge walipigia sana kelele masuala ya VAT kwenye utalii; VAT on transit, single customs territory kuunganisha RAHCO na TRL na kadhalika. Nchi imeendelea kupoteza mapato ya mabilioni ya fedha na hakuna hatua zinachukuliwa, kama nchi sasa tumekuwa mawakala wa kukusanya kodi kwa nchi ya DRC.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, uwekezaji kwenye sekta ya kilimo haukwepeki ikiwa kweli tumeamua kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati. Mpango utoe kipaumbele kwa agro-processing industries. Watanzania asilimia 80 wasiwe watazamaji tu katika mpango huu bali wawe ni sehemu muhimu ya mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo chetu kimekuwa tegemezi kwa mvua ambazo hazitoshelezi. Ni muhimu sana tufanye mapinduzi katika kilimo ili kilimo cha umwagiliaji wa kutumia mabwawa na visima virefu kipewe kipaumbele. Pia, masoko ya mazao hayana uhakika, msimu wa 2015/2016 kilogramu moja ya Mbaazi ilikuwa sh. 3,000 na msimu huu wa 2016/2017 bei ya kilogramu moja ni sh. 800. Wakulima wa Mbaazi wamekata tamaa kabisa, ruzuku ya kilimo haipatikani kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo Benki ya Kilimo ambayo iko Dar es Salaam, benki hii iongezewe mtaji na ikopeshe wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya huduma za afya nchini ni mbaya sana, hakuna dawa kwenye vituo vya afya, hakuna vifaatiba na pia watalaam hawatoshi, ni vema mpango huu uhakikishe hospitali za Wilaya, vituo vya afya na dispensary vinatoa huduma stahiki kwa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuleta mageuzi ya uchumi wa viwanda nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Waziri Mkuu kwa kufanya ziara ya kihistoria mwishoni mwa mwaka jana Wilayani Karatu. Ziara hiyo ilileta matumaini mapya ya maisha kwa wakulima wadogo wadogo wa Bonde la Ziwa Eyasi wanaotumia kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia chemchem zilizoko Qangded.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu kwa kusikiliza malalamiko ya wananchi wa bonde hilo kupitia mabango waliyomwandikia na kwa kuzingatia misingi bora ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, Waziri Mkuu aliagiza mashine zote zilizoko mtoni ziondolewe na mipaka ya chanzo ihifadhiwe kwa mita 500 kila upande.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kauli hiyo ya kiongozi mkubwa ambayo pia imezingatia sheria; viongozi wa chini yake waliopaswa kusimamia maagizo hayo wameshindwa kuchukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea baadhi ya mashine bado ziko mtoni kabisa. Upimaji wa mipaka ya chanzo ulifanyika hivi karibuni lakini bado mipaka hiyo haizingatiwi na watu wanalima ndani ya eneo lililopimwa. Uhifadhi wa vyanzo vya maji ndiyo njia pekee ya kuinusuru
nchi hii kugeuka kuwa jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Waziri Mkuu akamilishe kazi hii njema aliyoianza kule Karatu kwa kutoa tena tamko kwa uongozi wa chini yake wasimamie kauli yake ambayo ni kauli ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania walio wengi wanajishughulisha na kilimo ili kupata chakula na pia mazao ya biashara. Kilimo chetu kimekuwa tegemezi kwa mvua jambo ambalo limepunguza mapato na mavuno pindi tunapokuwa na mvua chache. Niishauri Serikali kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga mabwawa makubwa ambayo yatakinga maji nyakati za mvua. Nchi kadhaa duniani na hata hapa Afrika wamefanikiwa kwa kuwekeza katika miradi ya aina hiyo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
HE. QULWI W. QAMBALO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karatu ina umri wa zaidi ya miaka 20 na bado haina Hospitali ya Wilaya. Wananchi wengi na hasa wazee, akinamama na watoto wanapata shida sana kufuata matibabu mbali. Tunacho Kituo cha Afya Karatu ambacho kina miundombinu ya kutosha na kama Wilaya na Mkoa tumekubaliana kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya.

Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Afya aone umuhimu wa kupandisha hadhi kituo hicho ili kichukue nafasi ya Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo sera katika Wizara hii inayosema kuwa na dispensary kila kijiji na Kituo cha Afya kila Kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karatu ina Kata 14 na ni Kata tatu tu zenye Vituo vya Afya. Huu ni upungufu mkubwa sana. Hata hivyo, vitatu vina upungufu mkubwa wa vifaa tiba na watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko dispensary zimefungwa kwa kukosa watumishi mfano Zahanati ya Makhomba Endashangwet na kadhalika. Suala la afya ya wananchi wetu ni suala muhimu sana. Nchi yetu ni ya wakulima na ili mtu alime anahitaji afya timamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la maendeleo ya Jamii limesahaulika kabisa. Kitengo hiki kinapaswa kuwa injini katika Halmashauri zetu maana hawa ndio wanapaswa kufanya maandalizi ya jamii ili mradi iweze kufanikiwa. Huko nyuma tulikuwa na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, mfano Tengeru, Monduli na kadhalika. Vyuo hivi vimetoa wataalam wazuri sana wa kuwahamasisha wananchi kupokea miradi na kuwaandaa ili mradi iwe endelevu. Hali ilivyo sasa, kitengo hiki kimemezwa na Idara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwawezeshe watumishi wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii ili wawafunze wananchi kwa utekelezaji wa miradi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo ili nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana katika maendeleo ya watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na eneo hili la kisera. Suala la kuunga mikoa limesemwa jana katika hotuba zote tatu, wachangiaji tangu jana na leo na hata ripoti zote hizo zimebainisha kwamba kuna mikoa yetu mingi bado haijaungwa. Ukienda Kaskazini, ukienda Magharibi, ukaenda na Kusini hali ni hiyo hiyo. Kwa hiyo, naishauri Serikali kama tulikubaliana tuanze na kuunga mikoa hebu tuunge hiyo mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina uhakika kama miradi yote iliyopo kwenye vitabu hivi ni ya mikoa, kuna miradi ya Wilaya, tusichanganye kama tulikubaliana tuunge mikoa tumalize kuunga mikoa kwanza halafu tushuke kwenye hizo ngazi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiingii akili ya kawaida mtu uko Mahenge, uko Ifakara unataka kwenda Lindi na Mtwara urudi Morogoro, uende Dar es Salaam ndiyo ushuke kwenda kule chini, haiingii akilini kwa kawaida. Mnavyofahamu barabara ya kwenda Dar es Salaam jinsi ambavyo ina changamoto zake nyingi. Hivyo, naishauri Serikali hebu tufanye jambo hilo kwanza. Watanzania wengi tena wale wa hali ya chini usafiri wao siyo ndege, usafiri wao siyo meli, usafiri wao ni treni na barabara. Treni haipiti maeneo yote, twendeni tukajenge hizo barabara zinazounga mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Chenge asubuhi ya leo, ameongea vizuri sana kuhusu barabara inayounga Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Arusha. Ukiwa Arusha ukitaka kwenda Musoma ni budi upitie Singida
- Mwanza - Musoma. Hakuna barabara inayounga Arusha na Musoma, hakuna barabara inayounga Arusha na Simiyu, hakuna barabara inayounga Manyara na Simiyu, hakuna barabara inayounga Manyara na upande huu wa Tanga.

Tunafanya nini? Kwa hiyo, nadhani tufanya jambo hilo la kisera ambalo tumekubaliana. Barabara ya Oldeani Junction, Mang’ola, Matala hadi Mkoa wa Simiyu na baadae Mkoa wa Shinyanga ni barabara ya siku nyingi sana. Mzee wangu asubuhi ameiongelea vizuri. Mheshimiwa Chenge ule muziki uliousema wa kuucheza, wewe ukianza kucheza huko Simiyu na sisi tutaanza kucheza huku Arusha, halafu Mheshimiwa Mbarawa utatuona. Tufanye mambo ambayo tumekubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mbarawa barabara ya Oldeani Junction, Matala hadi Simiyu siyo barabara ya Karatu - Mbulu - Haydom kwenda Simiyu, hizi ni barabara mbili tofauti. Barabara hii kwenye vitabu vyenu mmeiita The Southern Serengeti bypass. Southern Serengeti bypass hata siku moja haiwezi kupita Mbulu ni hii ambayo Mzee Chenge asubuhi ameiongelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri juzi nikiwa Jimboni nimekutana na vijana wa ofisini kwenu, hii taarifa sijui wameitoa wapi, sasa wakati mnahitimisha mtuambie hili badiliko la kwamba barabara sasa ni kama inataka kutelekezwa, barabara ambayo imetumia mabilioni ya pesa kwenye upembuzi yakinifu, sasa wanaanza upembuzi yakinifu mwingingine utakaotumia mabilioni ya hela mnapitisha Mbulu - Haydom, Huku ni kuchezea hela.(Makofi)

Mmetumia over bilioni tano kwa ajili ya upembuzi yakinifu na hata sasa hivi pamoja na kwamba kazi ile ya upembuzi yakinifu ilikamilika, bado mmeipa hela iendelee kutumika vibaya. Kwa hiyo, barabara ya kuunga Arusha na Simiyu ni Oldeani Junction - Matala - Mwanhuzi - Lalago na kwenda huko kwingine siyo hii ya Mbulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Karatu - Mbulu - Haydom na kwenda Mto Sibiti, Mheshimiwa Waziri Mbarawa ni barabra iliyochelewa nayo pia kujengwa kwa kiwango cha lami. Wale Wabunge wa siku nyingi mlioko kwenye jengo hili mmesikia, tangu enzi ya Marehemu Mzee Patrick Qorro, akaja Mzee Philip Marmo akaja Mheshimiwa Dkt. Wilbrod Slaa na hawa wengine wa majuzi wameendelea kuongea barabara hiyo lakini hadi leo barabara hiyo ni ya vumbi. Viongozi wote tena wengine wameanzia awamu ya akina Kikwete, barabara ya Karatu - Mbulu - Haydom Marehemu Mzee Rashid Kawawa alipokwenda Maghang miaka hiyo ya 1980 alisema barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami, hadi leo ni barabara ambayo kupitika kwake wakati wa mvua ni shida kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nakushauri Mheshimiwa Mbarawa, haya mambo nadhani mengine mnayapata mkiwa ofisini, hebu mje field, sijakuona ukija Kanda ile na Naibu wako pia sijamuona, hebu mtembee ili muone jiografia ili muweze kujua hiki ambacho tunakiongea. Naomba barabara hizo mbili mzitambue ni barabara mbili tofauti na zote zina umuhimu wa tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kuhusu suala la kupandisha hadhi barabara. Mheshimiwa Waziri tunaomba barabara zipande hadhi ili zipunguze mzigo kwenye Halmashauri zetu. Fedha zinazokuja kwenye Halmashauri kwa ajili ya matengenezo ya barabara ni fedha kidogo sana.

Mwaka jana Karatu tulipitishiwa shilingi bilioni 1.5, lakini hadi sasa tunavyoongea tumeletewa shilingi milioni 300, thirty percent na tuna mtandao wa barabara unaozidi kilometa 500, hivi utafanya nini kwa shilingi milioni 300? Kwa hiyo, tunaomba zipande juu ili huu mzigo utoke kwetu uende huko kwako ambako kuna fedha nyingi, huko ambako unapata asilimia kubwa ya fedha.

Kwa hiyo, tunaomba hizi barabara zipande hadhi ili mtusaidie ndugu zetu kubeba mzigo huu, siamini sana kama hoja ya kuanzisha Wakala ndiyo itakuwa suluhisho la kumaliza tatizo hili, tuleteeni fedha, Halmashauri zetu zina uwezo na wataalamu wa kutosha wa kufanya kazi ya barabara. Jambo hili leo mkilitoa pale Halmashauri, wale wataalamu tulionao watakuwa redundant. Kwa hiyo, nadhani suala hili tuleteeni hela sisi tuwasaidie kufanya hizo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema kidogo kuhusu Reli ya TAZARA, miaka ya 1970 nchi hii ilipata neema ya kupata reli ya kisasa kwa wakati ule. Ilikuwa reli pekee katika Ukanda huu wa Kusini iliyojengwa kwa usasa wa kiasi kile, yaliyoendelea TAZARA tunayafahamu, yanayoendelea TAZARA tunayafahamu. leo kama Nchi tumejitwisha kubeba kujenga reli nyingine ya standard gauge hii inayopita katikati ya nchi. Naomba hayo yaliyotokea kwenye reli ya TAZARA yawe ni somo na darasa kwa ajili ya uendeshaji wetu kwenye reli hii ya kati tunayokwenda kujenga. Tusipoangalia miaka 40 mingine inayokuja tutaimba muziki huu huu ambao leo tunauimba kwenye reli ya TAZARA.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, naamini nchi hii bado inaihitaji reli ya TAZARA, tena inaihitaji reli ya TAZARA sana. Reli ya TAZARA kwa sasa kinachohitajika ni uwekezaji na kupata viongozi wenye weledi basi reli ile inaweza ikajiendesha. Machimbo ya makaa ya mawe yaliyopo pale Songwe yanatosha kabisa kuendesha reli hii. Kwa hiyo, Serikali ikubali kuwekeza fedha kidogo ili reli hii iweze kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo tena kuhusu reli ya kati….

MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ili na mimi niweze kuchangia juu ya sekta hii muhimu katika maisha na maendeleo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kutoa pole nyingi sana kwa wazazi, wanafunzi na Walimu na Watanzania kwa ujumla kwa ajili ya ile ajali mbaya iliyotokea kule Karatu, iliyochukua maisha ya wanafunzi wetu wengi na Walimu. Mwenyezi Mungu aweke roho zao mahali pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna ubishi juu ya suala la umuhimu wa maji. Kila mtu anafahamu, wanyama wafugwao wanafahamu hata wale wa porini wanafahamu umuhimu wa suala hili. Hata Vitabu Vitakatifu vya Mungu vimeeleza juu ya umuhimu wa maji kwa maisha ya mwanadamu tangu uumbaji. Kwa hiyo, naomba tusilifanyie mzaha na mchezo suala la maji kwa maisha ya watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kitabu cha Waziri. Ukienda ukurasa wa saba imeandikwa 72.5% ya Watanzania waishio vijijini wanapata maji safi na salama katika umbali wa mita 400. Mheshimiwa Waziri takwimu hizi amezitoa wapi? Uhakika wa takwimu hizi ameufanyia kazi kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe pia umekuwa ukikaa kwenye Kiti hicho mara nyingine asubuhi, katika Kipindi cha Maswali pale asubuhi, kukiwa na swali la maji, Wabunge tunabanana kupata nafasi hiyo, hicho ni kiashiria cha kutosha kwamba eneo hili la maji lina matatizo makubwa. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, hizi takwimu zake hebu azirejee kama kweli ziko sahihi. Haiwezekani kama 72% ya Watanzania waishio vijijini wanapata maji, Wabunge wangepaza sauti zao kiasi hiki humu ndani, isingewezekana! Kwa hiyo, takwimu hizi nina wasiwasi hazina usahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tena wanasema ndani ya mita 400. Wengi tulioko humu ndani tunatoka vijijini, hizi mita 400 zimesemwa kwenye sera lakini nadhani si kweli kwamba asilimia hiyo inapata maji kwa kiasi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tumewasilishiwa bajeti hapa ambayo mwaka jana tulipoipitisha, leo hadi mwezi wa tatu utekelezaji wake ni 19.8%. Naamini kwenye jambo hili kuna mkono wa mtu. Haiwezekani kwenye bidhaa muhimu kama maji tunapata asilimia ndogo kiasi hicho. Nawaomba ndugu zangu Mawaziri hapo mjitizame na mjipime kama kweli mko sahihi kuwa hapo kwenye Wizara hii muhimu namna hii, hii asilimia ni ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,kwa hiyo, Watanzania tujiandae kushuhudia sasa migogoro mingi ikitokea kwenye vyanzo vya maji kwa sababu vyanzo vya maji ni vichache. Watoto wetu waende shule asubuhi wamebeba vidumu vya maji kwa sababu shule hazina maji. Akinamama wetu watembee kilomita nyingi kutafuta maji kwa sababu maji hakuna. Afya ya Watanzania iendelee kuwa rehani kwa sababu ya kutumia maji yasiyo safi na salama na yale mengine ambayo yanafanana na hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na wale ambao wanasema tuongeze tozo kwenye fedha za mafuta. Ukiangalia katika zile fedha ambazo zimetolewa shilingi bilioni 181, asilimia 57 ya fedha hii imetokana na Mfuko wa Maji. Kama tumeweza kupata asilimia 57 kutoka kwenye Mfuko wa Maji, naamini tukiongeza mara mbili tunaweza kupunguza tatizo hili la maji kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia najiuliza tulikuwa tumetoka kwenye ule Mpango wa Progamu ya Maji - WSDP I sasa tumeingia kwenye WSDP II na tumeaminishwa siku za nyuma kwamba hizi ni fedha za Benki ya Dunia. Hizi fedha za Benki ya Dunia zipo wapi kama miradi tunatekeleza na fedha za Mfuko wa Maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika bajeti ya mwaka 2017/2018, asilimia ndiyo hiyo imeshuka kutoka shilingi bilioni 900 sasa tumekwenda shilingi bilioni 600. Bajeti ya mwaka jana, Wilaya ya Karatu tulikuwa tumetengewa shilingi bilioni 1.4 lakini hadi sasa tunavyoongea tumepata shilingi milioni 540, bado shilingi milioni 610. Mheshimiwa Naibu Waziri yuko kwenye Kiti hapo naomba sasa wakati wanajumuisha watuambie, naamini tatizo hili la kutokupeleka fedha za mwaka jana haliko kwenye Jimbo la Karatu peke yake bali ni maeneo yote, katika miezi hii miwili iliyobaki fedha hizi wanazipeleka lini. Miradi haikamiliki kwa sababu fedha hawazileti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye jedwali 5(a) ambapo fedha zimetengwa kwa kila wilaya au kwa kila jimbo, pale utaona mambo ya ajabu sana. Ziko wilaya mwaka jana zilipewa shilingi bilioni mbili, tatu na kadhalika na safari hii zimepewa hivyo hivyo. Ziko wilaya zimepata mgao wa shilingi milioni 500, 600 au 700, kwa nini tunatofautiana namna hii? Kama sungura ni mdogo basi tugawane wote ili kila mtu apate hicho kidogo. Mbona wakati wa vile vijiji kumi vya ule Mradi wa Benki ya Dunia tulipewa kila mtu vijiji kumi kumi! Kwa nini leo hii wengine wana mabilioni na wengine wana milioni tena chache sana? Hili ni jambo ambalo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sitakuwa nimewatendea haki wananchi wa Bonde la Eyasi kama sitasema kuhusu mradi wao wa umwagiliaji. Nashukuru Naibu Waziri upo hapo na ulifika katika bonde lile, tuna mgogoro mkubwa wa uhifadhi wa chanzo cha maji Qangded.Bahati nzuri Waziri Mkuu alifanya ziara kule Mangola mwezi wa kumi na mbili, wananchi walimlilia kiongozi wao na kiongozi wao akawasikiliza. Waziri Mkuu alitoa kauli ya Serikali kwa kusema chanzo kile cha Qangded kihifadhiwe kwa umbali wa mita 500 na mashine zote zilizowekwa kwenye mto ziondolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha hadi leo tunavyoongea bado mashine zile ziko kule mtoni zinachukua maji mengi na wananchi wanaokaa chini hawapati bidhaa hiyo. Bado zile mita zilisemwa na Waziri Mkuu hazijafanyiwa kazi. Naomba kufahamu, hivi ni nani wa kutekeleza kauli hii ya Waziri Mkuu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mangola walimsifu na walimpongeza sana Waziri wao Mkuu kwa kutambua kero yao lakini viongozi wale wa chini wameshindwa kufanya kazi ya kupima mita zile zilizowekwa kuanzia kwenye chanzo hadi kwenye ziwa. Kwa hiyo, wakati watakopojumuisha naomba walizungumzie hili suala la chanzo cha Qangded katika Bonde la Eyasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati ambao unategemea uimarishaji wa viwanda. Tanzania tulikuwa na viwanda vingi miaka ya nyuma lakini tulifika mahali tukauza au kuvibinafsisha vingine, tena kwa bei ndogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kurudi nyuma katika kipindi kile cha uuzaji wa viwanda, kuangalia mikataba ile yote ili kubaini ni vipi tunaweza kurejesha viwanda mikononi mwa Serikali. Ujenzi wa viwanda ni ghali sana na ni bora na rahisi kufufua vile vya zamani kuliko kuweka viwanda vipya.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda maana yake ni ajira kwa vijana wetu. Serikali hii ina mipango mizuri kwenye makaratasi, lakini kwa kweli kiuhalisia bado kabisa viwanda havionekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuanzisha viwanda vile ambavyo malighafi yake inaweza kupatikana nchini. Tunayo mazao ya mashambani, tunayo mifugo mingi sana na pia tunayo madini mengi. Viwanda pia vilenge katika kukuza uzalishaji wa mazao hayo ya hapo juu. Ni jambo la kuhuzunisha, kwani mazao yanalimwa hapa nchini lakini yanasindikwa nje. Mfano, nchi yetu inazalisha korosho nyingi lakini inabanguliwa nje. Huku ni kukosesha Watanzania ajira na pia kupoteza mapato ya Serikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye eneo la uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji. Ni jambo lisilopingika kuwa vyanzo vyetu vingi vya maji vimeingiliwa na shughuli za binadamu kama kilimo, utalii, ufugaji na kadhalika na hivyo kutishia uhai wa vyanzo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, chemchemi za Qangded katika Bonde la Ziwa Eyasi, Wilayani Karatu ni chanzo muhimu sana kwa kilimo cha umwagiliaji ambako zaidi ya kaya 35,000 katika vijiji saba vya Kata za Baray na Mangola wananufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka ya hivi karibuni chanzo hicho kimeshindwa kabisa kuwahudumia wananchi hao baada ya maji mengi kuchukuliwa na watu wachache karibu na chanzo, wanaochukua maji yote katika mashamba yao na hivyo kusababisha zaidi ya wakulima 30,000 walioko chini ya chanzo (down stream) kutokufikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa K. Majaliwa alitembelea Bonde la Eyasi na baada ya wananchi kumlilia juu ya hifadhi ya chanzo cha Qangded, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza na kutoa Kauli ya Serikali kuwa chanzo hicho kihifadhiwe kwa umbali wa hadi mita 500 na kwamba mashine zote zilizoko mtoni ziondolewe mara moja. Kauli hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ilishangiliwa sana na wananchi wa Bonde la Eyasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kauli hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu haijatekelezwa hadi leo. Bado mashine za kunyonya maji zipo mtoni na pamoja na kuwa alama za mipaka ya chanzo zimewekwa majuzi, bado mipaka (beacons) haijawekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, huku ni kumdhalilisha Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni kuidhalilisha Serikali. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja hii awaambie wakulima wa Bonde la Eyasi wanaotumia chanzo cha Qangded ni lini watatekeleza Kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu? Wizara kwa kushirikiana na wadau wavitambue na kuviwekea mipaka na kuvitangaza vyanzo hivyo vya Qangded kuwa maeneo tengefu ili kuvilinda na kuvihifadhi vyanzo vya Qangded.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Wizara hii na Waziri wake kuongeza uwazi na umahiri katika ukusanyaji wa kodi. Wananchi wetu hawakatai kulipa kodi ila iko mianya mingi ya ukwepaji wa ulipaji wa kodi sahihi. Wapo watumishi wa TRA wanapokisia kodi wanachukua asilimia kubwa na Serikali inapata kidogo. Serikali izibe mianya ya wizi wa kodi ili ipate mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Maji ya KAVIWASU (Karatu Villages Water Supply) ni chombo cha wananchi (COWSO) kilichosajiliwa kwa sheria ya nchi Cap.375 kutoa huduma ya maji katika Mji wa Karatu na vijiji vinavyozunguka mji huo. KAVIWASU hawafanyi biashara bali wanatoa huduma ya maji kidogo wanachopata kutokana na mauzo ya maji kinatumika kuendeleza mradi katika maeneo ambayo mtandao wa maji haujafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mshangao wa wengi wameshtuka TRA Karatu wameitaka KAVIWASU ilipe kodi yenye jumla ya Sh.200,000,000/= na zaidi la sivyo watakatiwa huduma na kukamatiwa mali. Mheshimiwa Waziri, DAWASCO, AWASA, DUWASA na bodi nyingine nyingi tena za daraja A hazilipi kodi hiyo iweje KAVIWASU tena chombo cha wananchi ambacho hata hakipati ruzuku yoyote kinalazimishwa kulipa kodi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii aangalie suala hili kwa kuwaelekeza TRA Karatu wasitishe madai yao hayo yanayokiuka sheria. Ikiwa sheria inawataka KAVIWASU kulipa kodi basi Waziri kwa mamlaka aliyonayo asamehe kodi hiyo ili wananchi wa Karatu waendelee kunufaika kwa huduma ya maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi nchini ni moja ya kero kubwa inayokwamisha maendeleo ya kiuchumi na ya watu wetu. Migogoro hii imedumu muda mrefu na kama nchi lazima tunatakiwa kuchukua hatua sasa. Ili kumaliza migogoro hii Serikali ni lazima ihakikishe ardhi yote imepangwa, imepimwa na kumilikishwa kisheria. Kuhusu migogoro ya mipaka kati ya Mkoa na Mkoa, Wilaya na Wilaya na Kijiji na Kijiji, nishauri Serikali kufanya utaratibu wa kutafsiri GN zilizounda maneno hayo ili haki itendeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karatu inayo mashamba 40 ya wawekezaji (Mikataba). Mengi ya mashamba hayo hayajaendelezwa kwa kiwango cha kuridhisha na yamekuwa chanzo cha migogoro. Shamba la Tembo na Tembe lenye ekari 562 na 545 ambayo yote yametekelezwa kwa chini ya 50% yamekuwa kero kubwa katika Wilaya ya Karatu. Naomba Serikali ichukue hatua ya kuyachukua mashamba hayo au hata sehemu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba la Acacia Hill, lenye ekari 1556, nalo tunaomba sehemu yake irudishwe kwa wananchi maana nalo limeendelezwa kwa chini ya asilimia 50%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba la Bendhu Limited lenye ekari 472 limetelekezwa baada ya mmiliki wake kufariki. Tayari Halmashauri ya Wilaya imeshaomba shamba hilo kufutiwa umiliki na lipewe wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niiombe Wizara iongeze wataalam wa ardhi na vifaa katika Wilaya ya Karatu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu huu wa kilimo zao kuu la chakula mahindi linapata pigo kubwa kutokana na kushambuliwa na viwavi (fall army worms). Wadudu hao wavamizi wameshambulia zao hili katika maeneo mengi ya Mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Simiyu, Mara wakati mimea iko katika hali ya kuota na palizi na cha kutisha ni kuwa dawa nyingi zimeshindwa kuwatokomeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karatu wakulima wake wengi wameathirika hadi hivi sasa wakati mahindi yako katika stage ya kutoa maua bado hao viwavi ni tishio kubwa. Hali hii isipodhibitiwa uzalishaji wa zao hilo utapungua sana na upungufu wa chakula utakuwepo. Naiomba Serikali ipeleke timu ya wataalam ili kupambana na wavamizi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chemchem za maji za Qangded zilizoko Mangola - Karatu ni chanzo muhimu sana cha kilimo cha umwagiliaji kwa wakulima wa bonde la Eyasi (vijiji saba). Chemchem hizo zipo katika hatua ya kutoweka kutokana na kuingiliwa na shughuli za kibinadamu. Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Wilaya ya Karatu mwishoni mwa mwaka 2016 wananchi hao walimlilia na hatimaye aliagiza chemchem hizo zipimwe mipaka yake kwa mita 100 na zihifadhiwe. Hadi wa leo chemchem hizo hazijapimwa na ziko katika hali mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa agizo lake bado halijatekelezwa na chemchem za Qangded bado zinaathirika sana. Mvua za mwaka huu zimesababisha mafuriko ambayo yameziharibu sana chemchem hizo. Niombe Serikali ipeleke timu ya wataalam kushauri namna bora ya kuhifadhi vyanzo hivyo lakini fedha pia kwa ajili ya kukarabati miundombinu iliyoharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro ya ardhi inayosababishwa na mipaka tatanishi hasa kati ya wananchi na hifadhi za wanyama ambayo imeendelea kuwa kero. Kutokana na agizo la Serikali wataalam wameendelea kuweka alama za mipaka katika maeneo bila kuwashirikisha wananchi, malalamiko ni mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kumaliza mgogoro wa mpaka kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (WCAA) na Wilaya ya Karatu hususani katika maeneo ya Lositete, Endamaghang, Upper Kitete, pia mgogoro kati ya TANAPA na wananchi wa Bugei katika Wilaya ya Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA imeanzishwa kuwa mtengenezaji wa barabara za vijiji na mjini. Katika umri wake wa karibu mwaka mmoja bado hatujaona sana matunda. Barabara nyingi katika Wilaya ya Karatu hasa katika kipindi hiki cha mvua zimeharibika na TARURA wameshindwa kurudisha mawasiliano. Naomba Serikali kutenga fedha za kutosha kuwezesha TARURA kufanya kazi yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. WILLY Q. QAMBALO: Mheahimiwa Mwenyekiti, nianze na eneo la Vyuo vya Ufundi (VETA). Tanzania imedhamiria kuwa na Chuo cha VETA katika kila Wilaya na hili ni jambo jema. Wilaya ya Karatu kwa kushirikiana na wadau wake wa maendeleo wamejenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na majengo ya msingi yamekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyonayo Karatu ni msajili wa chuo hicho na hatimaye uendeshaji wake. Tunashukuru tumepata usajili wa muda miezi sita na tayari fani mbili zimeanza. Naomba Serikali kutupatia usajili wa kudumu na kisera kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kuendesha Chuo hicho kwa kutupatia walimu na vifaa vya ufundishaji. Tunao upungufu mkubwa sana wa watumishi. Wilaya ya Karatu ina upungufu wa walimu wa msingi 546 na sekondari 66. Idadi hii ya upungufu ni kubwa mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya msingi Endamaghang Wilayani Karatu ni maalumu ya bweni kwa watoto wa jamii ya Wahadzabe na Wabarbaig ambao kwao bado mwamko wa elimu ni mdogo sana. Shule hiyo ina changamoto na upungufu mwingi sana. Shule hiyo haina umeme japo nguzo zimepita hapo. Pia walimu hawatoshi kabisa, nyumba za walimu hazipo na mabweni kukosa vifaa kama magodoro na mashuka. Wahudumu mfano wahunzi na wapishi hawatoshi na hawapati mafao yao kwa muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wetu nchini wanazo changamoto nyingi sana ikiwemo mishahara midogo, kupandishwa madaraja na pia nyumba zao. Naishauri Serikali kuondoa changamoto hizi ili watumishi katika sekta ya elimu wapate moyo wa kufanya kazi kwa bidii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejitahidi kujenga maabara na changamoto kubwa iliyopo sasa ni watumishi wa kada ya laboratory technicians. Serikali ipeleke watumishi wa ngazi hii Wilaya ya Karatu. Tumejitahidi sana kujenga shule za sekondari 31 kwenye kata 14. Serikali sasa itupe upendeleo wa kukamilisha maabara katika shule 18 ili hatimaye watoto wetu wapate kujifunza kwa vitendo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kuchangia Wizara hii muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na wananchi wetu na eneo la kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sera ya makusudi iliyokuwa imefikiwa ili makao makuu ya mikoa yote yaweze kuunganishwa kwa barabara za lami. Kamati kwenye hotuba yake imesema vizuri sana iko zaidi ya mikoa 15 ambayo bado haijaunganishwa. Niunganishe kwenye orodha ile Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara haujaunganishwa na Mkoa wa Arusha na Mkoa Mara haujaunganishwa. Malengo ya sera hii ilikuwa ni mwisho iwe 2017/2018, leo tunaingia 2018/2019 karibu robo ya mikoa haijaunganishwa, nadhani tunapaswa kuongeza kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni ukweli kwamba bado kuna barabara nyingine ndogo ndogo labda ndani ya wilaya, barabara za kwenda hata kwenye vitongoji, hata njia za ng’ombe zinawekwa lami lakini mikoa bado haijaunganishwa. Kama kweli tumedhamiria kuunganisha mikoa hebu tuanze kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kuunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu ni barabara ya Oldeani Junction - Mang’ola - Matala - Mwanhuzi. Barabara inayosemekana ya Karatu - Mbulu – Haydom - Mto Sibiti - Mwanhuzi hiyo ni barabara nyingine na barabara hizi zote mbili zina umuhimu wake tusichanganye. Pale Mang’ola ambako barabara hii inapita kuna gesi muhimu sana ya helium ambayo imegundulika, utaisafirisha kwa barabara hii ya Oldeani Junction - Mang’ola - Matala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama ni kweli hiyo reli wanayoisema ya Tanga – Arusha - Musoma itajengwa hiyo ndiyo barabara ya kupitishia vifaa vya ujenzi. Kwa hiyo, barabara ya Oldeani Junction - Mang’ola ni barabara muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, pale Mang’ola kila siku inayotoka kwa Mungu kuna tani 150 za vitunguu maji vinasafirishwa kuja Arusha. Kwa hiyo, ni barabara ambayo naomba isiachwe kwa sababu tu tunasema barabara ni hii ya Karatu – Mbulu – Haydom, hiyo ni barabara nyingine na ni muhimu na kila barabara ina umuhimu wa aina yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye eneo la uwanja wa ndege, nashukuru Benki ya Dunia imeweka hela na naamini itakuja kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Lake Manyara. Wananchi wako tayari, miaka miwili imepita Wizara wameshaweka alama za uwanja lakini mpaka sasa hivi wananchi hawajui kinachoendelea. Kwa kuwa fedha zile zimetengwa na nina uhakika ni fedha za uhakika basi waende wakawaambie wananchi juu ya kile ambacho kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo pia kuhusu Uwanja wa Ndege wa Songwe ni muhimu sana kwa maendeleo ya Nyanda za Juu Kusini. Hata hivyo, uwanja huu haukamiliki zaidi ya miaka 10, kuna tatizo gani? Tumetoka juzi pale Kamati ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma, mambo yanayoendelea kwenye Uwanja wa Ndege wa Songwe ni aibu. Mkandarasi ameshabadilishwa zaidi ya mara tatu, hivi taratibu za manunuzi ya hawa wakandarasi zikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi wa kwanza hovyo, wa pili hovyo, wa tatu naye ameshamaliza pesa kazi imesimama, tunawateuaje hawa makandarasi? Mkandarasi wa mwisho huyu Shapriya ameshindwa kumaliza kazi lakini ameshalipwa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.4. Wanawezaje kumpa mkandarasi fedha ambazo siyo za kwake na leo ameshindwa kufanya kazi? Kwenye kitabu wametenga shilingi bilioni tatu ya kwenda Songwe, huyu mtu aliyechukua hii shilingi bilioni 1.4 wana mpango gani naye? Pana shida kubwa sana pale Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo kuhusu reli. Tunashukuru sana, ni mkakati mzuri lakini tusiishie kwenye reli ya kati. Hii reli inayosemwa ya Tanga – Arusha - Musoma imekuwepo tangu mimi niko mtoto wa shule. Kila siku upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na mabilioni yanakwenda. Kuna hiyo reli ya Kusini, yuko mwenzangu amesema kama inawezekana na kama tuna sifa hebu twendeni tukakope ili hizi reli zote zikajengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri atusaidie, alikuja mbele ya Bunge hili akasema deni la Taifa limekuwa kubwa kwa sababu pia tunakopa fedha za ujenzi wa reli ya standard gauge lakini pia kuna kauli inasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. QAMBALO W. QULWI: Tunajenga kwa fedha za ndani, hebu atuambie kauli ya Serikali ni nini juu ya ujenzi wa reli hii?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vya maji katika nchi hii vinahitaji kuhifadhiwa kwa nguvu kubwa kwani kasi ya kuharibiwa ni kubwa mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa alipofanya ziara Bonde la Eyasi mwaka 2016 alitoa kauli za Serikali zifuatazo:-

(a) Chanzo cha Qangded kihifadhiwe kwa radius ya mita 500 pande zote.

(b) Mashine zote zilizoko mtoni ku-pump maji ziondolewe na ziwekwe nje kabisa ya chanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi leo miezi 17 tangu tamko litoke hakuna lililofanyika. Nimuombe Waziri wa Maji na Umwagiliaji afike Bonde la Eyasi ili kutekeleza maagizo hayo ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Kijiji cha Getamvua uliojengwa chini ya WSPP kwa zaidi ya shilingi milioni 600 haufanyi kazi kwa kujengwa chini ya kiwango. Wataalam wa Wizara walienda kufanya tathmini na hadi leo fedha za ukarabati bado hazijaletwa. Nimuombe Waziri awakumbuke wananchi wa Getamoa ili mradi ule wa maji ufufuliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Karatu kwa kushirikiana na Shirika la Kidini la CRS wamefanya mradi wa maji katika kijiji cha Qaru kwa kutumia mfumo wa prepaid water meters. Mfumo huo una mafanikio makubwa sana kwani hata mapato yameongezeka mara tatu. Tunamuomba Waziri afike azindue mradi huo ili kutoa hamasa kwa wadau wengine.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii adhimu ambayo nimeipata ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri mwanzo mwisho, mara mbili, mara tatu.

Kama kweli haya yalioandikwa humu yatakwenda kutekelezwa nchi hii itakuwa paradiso nyingine. Hata hivyo, inaonyesha miaka yote mitatu iliyopita Waziri hakuwa na hela hivi atafanya maajabu gani ili yote haya mazuri aliyoandika humu yaende kutekelezwa? Sioni tofauti kubwa kati yake Waziri na Waziri Kivuli ambaye hana mafungu, sana sana Waziri anatembelea gari la Serikali. Kwa sababu miaka yote anapata chini ya asilimia 20, atakwendaje kutekeleza haya yote yameandikwa humu ndani? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii tulikuwa na historia ndefu ya ukulima uliotukuka wa mazao ya kahawa, mkonge, ngano na mazao mengine leo mazao hayo yameangukia pua. Sasa mahindi tunakwenda kuangukia pua, mbaazi tumekwishaangukia pua, ngano tunaangukia pua, hivi mkulima wa nchi hii alime nini ili awe salama? Sioni wapi yupo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye masoko ya mazao. Mwaka jana mahindi tuliangukia pua, mbaazi tukaangukia pua, safari hii tunakwenda kuvuna, hivi mnatuambia nini sisi wakulima? Tunakwenda kuangukia pua au sasa tunaangukia mdomo ili meno yaishe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge mwaka jana wakati Serikali imekuja kutoa kauli ya zuio la kupeleka mahindi nje, Waziri Mkuu alikuwa amekaa pale alipotoa kauli hii ni sisi wenyewe ambao tulimshangilia na upande huu ndiyo mlimshangilia zaidi, wale wanaojiita the big five ndiyo walishangilia kuliko wengine. Kweli wanasema mzigo mzito mbebeshe Mnyamwezi, leo Tizeba ataubeba mzigo huu kwa sababu haikuwa kauli yako. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakulima tunalima ili tuzalishe chakula na tukauze ziada. Nimelima mahindi ya kutosha halafu unaniambia nisiuze, hivi unanizuia nisiuze nimekopa shamba niko mwenyewe, nimelima niko mwenyewe, nimenunua mbegu niko mwenyewe, palilia mwenyewe, navuna mwenyewe, halafu unakuja unasema usiende kuuza kule. Sasa kama hutaki nikauze huko basi nunua wewe, sasa na wewe huna uwezo wa kununua si uniche huru nikauze? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati mwingine huyu mkulima tumuache huru auze. Tuko kwenye utengamano wa Afrika Mashariki haya mambo ya kuuziana mazao ni ya kawaida. Mimi nikivuka Namanga naona soko zuri unaniambia nisiende, hasa nunua wewe basi unipe hela nzuri huwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumefika mahali wakulima wa mbaazi wameacha mbaazi shambani wanachungia ng’ombe, mahindi yanaoza kwenye maghala yetu, mnataka tupeleke watoto shule, mnataka tujenge madarasa, mnataka tuchangie hospitali, fedha hizi tunapata wapi? Mimi nadhani kwa kweli hatuwatendei haki wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa kwenye semina ya kilimo masula ya viwavijeshi vamizi. Wabunge tulipata semina lakini imekuja kwa kuchelewa sana, huko vijijini watu wanavuna halafu ndiyo mnatufanyia semina. Pia ilikuwa semina ya Wabunge na wakulima je? Wakulima wamehangaika mwaka mzima hakuna mtu anayewasaidia si Mkurugenzi na si Waziri ni mateso matupu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tishio la viwavijeshi huyu ni kubwa sana, hili kwa kweli ni janga la nchi. Bahati mbaya sana sijui kama nchi hii haina mfuko wa kuhangaika na majanga, kwa sababu hakukuwa na namna ya kumsaidia mkulima. Hata wale wa Maafisa Ugani hawana uhakika wa dawa ambayo inaweza kupambana na mdudu huyu, wakulima wameachwa tu. Kwa hiyo, tusipoangalia mwaka huu hata mavuno yatakuwa chini sana lakini pia ubora wa mahindi yatakayozalishwa utakuwa chini kwa sababu huyu mdudu ametusumbua sana. Kwa hiyo, nafikiri tuwe na mfuko imara ambapo likitokea janga kama hili wananchi waweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Maafisa Ugani ndiyo wamekuwa Watendaji wa Kata na Vijiji. Nakubaliana kabisa na pendekezo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ubadhirifu wa mali za vyama vya ushirika uliofanywa na baadhi ya viongozi na wanachama wasio waaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ayalabe SACCOS Wilayani Karatu, fedha za ushirika zilifujwa miaka zaidi ya sita iliyopita na hadi sasa hakuna majibu. Waliohusika kupoteza fedha hizo wanafahamika maana fedha zilitoka benki ya TIB na kuingia kwenye account zao. Hapa wezi si wako wazi lakini kwa kuwa wezi wana mtandao ndani ya Wizara bado wameendelea kulindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachama wa SACCOS hii pamoja na viongozi wa Wilaya wamelalamikia sana na SACCOS hii kwamba imeendelea kudorora na wananchi wanakosa imani kabisa na vyama vya ushirika. Leo hii Serikali inajitahidi kufufua ushirika lakini wananchi hawaelewi kutokana na mifano hii mibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika anatuhumiwa sana na wanachama wa Ayalabe SACCOS kama ndiye anayewalinda wezi hao. Najua jambo hili liko mezani kwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Niishauri Wizara ilifanyie kazi tatizo hili ili haki itendeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo ardhi nzuri na hali ya hewa nzuri kwa zao la alizeti. Hatuna kabisa sababu ya kuagiza mafuta nje wakati tungeweza kulima wenyewe na kuwasaidia wananchi wetu. Serikali iwapatie wananchi mbegu bora ya alizeti.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, migogoro kati ya hifadhi za wanyama na vijiji vinavyozunguka hifadhi hizo ni ya muda mrefu na inaumiza sana. Mgogoro kati ya Vijiji vya Losilete, Upper Kitete, Slahamo, Makuromba na Endamaghang Wilayani Karatu na Hifadhi ya Ngongoro ni ya muda mrefu. Pia mgogoro kati ya TANAPA (Lake Manyara National Park) na wananchi wa kata ya Buger umekosa wa kusuluhisha.

Mheshimiwa Spika, askari wa wanyamapori wamekuwa na ubabe wa kuwanyanyasa na kuwapiga wananchi. Mipaka ya hifadhi hizi imewekwa siku nyingi tangu ukoloni na bila kumung’unya maneno mipaka halisi inafahamika, inaonekana na ni ubabe tu wa hifadhi kuyaongezea maeneo ya wananchi. Serikali iachane na tabia ya kuvamia maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, wanyama wamekuwa chanzo cha kutia umaskini wananchi wetu. Tembo na mbogo wamekuwa wakitoka hifadhini na kwenda vijijini kuharibu mashamba ya wananchi na hata kusababisha vifo. Uongozi wa hifadhi hizi hauko makini kuwazuia wanyama hao. Niishauri Serikali kuhakikisha timu za doria zinaongezwa na kupewa zana za kuwadhibiti wanyama hao.

Mheshimiwa Spika, sheria ya kutoa kifuta jasho na pole kwa uharibifu na mauaji yanayofanywa na wanyama hao imepitwa na wakati na inahitaji marekebisho makubwa. Pole ya shilingi 1,000,000 haitoshi kabisa hivyo inafaa iongezwe.

Utaratibu wa kukamata na kutaifisha mifugo ya wafugaji pale inaposemekana wameingia hifadhini haufai kabisa na ni unyanyaswaji wa wananchi. Ng’ombe wamekuwa wakitaifishwa kwa uonevu mkubwa. Utaratibu huu ubadilishwe, haufai kabisa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia uhai hadi kuona siku hii ya leo. Jeshi la Polisi ni taasisi muhimu kwa ajili ya ulinzi wa raia na mali zao. Jeshi hili liachwe huru kabisa lifanye kazi yake kwa mujibu wa taratibu na sheria zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi lisitumike kisiasa na watawala wote waache kutoa maagizo kwa jeshi hili lifanye kwa matakwa yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Wilaya wanapofanya ziara zao vijijini wanaandamana na magari ya polisi kiasi cha kuwatia wananchi hofu. Mbona sisi Wabunge tunafanya ziara bila polisi na usalama upo wa kutosha? Kutembea na mapolisi ni matumizi mabaya ya Jeshi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kuhusu vitambulisho vya uraia (NIDA). Mradi huu ulitengewa fedha za kutosha lakini wakati wa utekelezaji wake wananchi wetu katika Wilaya ya Karatu walichangishwa fedha kwa kila mmoja Sh.1,000/= kama sharti la kupata kitambulisho. Kwa nini wananchi wachangishwe wakati Serikali ilitoa fedha kwa mradi huu? Naomba kupatiwa ufafanuzi wa jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ilitoa ardhi eneo la Njiapanda (Bashay) ekari 60 kwa Jeshi la Magereza ili kujenga Magereza ya Wilaya ya Karatu. Hadi leo bado magereza hayo hayajajengwa. Jeshi la Magereza kama halihitaji lirudishe eneo hilo kwa halmashauri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karatu ina mashamba ya mikataba 42 na mengine yamekuwa hayajaendelezwa ipasavyo na kugeuka kuwa mapori ya kuishi wanyama. Mashamba ya Tembo Tembo na ACACIA yaliyo Kijiji cha Mangola juu yameendelezwa kwa chini ya asilimia 40 na yanakosa sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilishapelekwa Wizarani na hata wananchi walimsimamisha kwa mabango Waziri Mkuu alipotembelea Karatu. Tunaomba Serikali iwarudishie wananchi wa Mang’ola juu sehemu na mashamba hayo hapo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmiliki wa shamba la ACACIA amekataa kutoa njia ya wananchi wa Mang’ola Juu kwenda Kijiji cha jirani cha Makhomba. Huu ni ukatili wa hali ya juu na kuwanyima wananchi haki ya kutembeleana; mmiliki huyo haitambui Serikali. Tunaomba Waziri awasaidie wananchi wa Mangola Juu kupata njia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karatu ambayo iligawanyika kutoka Wilaya ya Mbulu ya zamani ina utata wa mpaka kati yake na Wilaya ya Ngorongoro. Kihistoria eneo la msitu wa kutoka gate la Ngorongoro hadi View Point lilikuwa eneo la Wilaya ya Mbulu. Tunaomba Serikali isaidie kupata ukweli wa mpaka sahihi kati ya Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi ya Kata yanafanya kazi kubwa na muhimu sana ya kusimamia haki. Bahati mbaya Mabaraza haya ya Kata bado yanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Suala la posho zao, nauli pindi wanapokuwa kazini bado ni shida kubwa sana. Tunaomba Serikali iweke mpango wa wajumbe hao kuwa na posho ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka kati ya Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Ngorongoro uhakikiwe. Mpaka kati ya Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Mbulu eneo la Maseda nao uhakikiwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana kwa ajili maisha na uhai wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, nianze na eneo la uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji. Yapo mambo ambayo tunaweza kusema yanahitaji fedha nyingi lakini yako mambo ambayo pengine hayahitaji fedha kiasi hicho ni suala tu la umakini na utekelezaji wa sera na taratibu ambazo tumejiwekea.

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa alifanya ziara ya kikazi katika Bonde la Eyasi mwishoni mwa mwaka 2016. Wananchi walieleza kero zao nyingi ikiwemo uharibifu wa chanzo cha maji cha Mto Qangded. Baada ya Waziri Mkuu kuwasikiliza wananchi hao na kuona ukubwa wa jambo hilo alitoa maagizo mawili yafutayo; jambo la kwanza; eneo la chanzo cha Mto Qangded lihifadhiwe kwa mita zisizopungua 500 kila upande. Jambo la pili, mashine zote za ku-pump maji zilizoko kwenye
mto na kwenye chanzo ziondolewe jioni ya siku hiyo na zisirudi kwenye chanzo hicho. Jambo la kushangaza hadi leo mwaka na nusu maagizo ya Waziri Mkuu bado hayajatekelezwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Maji unisikilize kwa sababu naongea na wewe, naona unaongea pembeni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni jambo kidogo la kusikitisha kama Kiongozi Mkuu wa Pili wa nchi anatoa maagizo na maelekezo halafu mwaka na nusu unapita hakuna jambo ambalo limefanyika. Mbaya zaidi hawa watu wenye kiburi, wenye jeuri wanaoharibu vyanzo hivyo sasa wamevuta na umeme wa gridi kuupeleka kwenye vyanzo vya maji ili wa-pump vizuri maji hayo na wale walioko chini hawapati maji, tunakwenda wapi? Ni jambo ambalo haliingii kwenye akili ya kawaida huku tunasema hatuna fedha za kufanya miradi lakini hata hili la kusimamia sheria tumeshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri juzi uliulizwa maswali mawili ya nyongeza hapa na Mheshimiwa Paresso na dada yangu Mheshimiwa Catherine kuhusu chanzo hiki hiki na ukasimama, ukalidanganya Bunge kwamba chanzo kile kimepimwa. Mimi naomba nikuhakikishie chanzo kile bado hakijapimwa. Wataalam wako wa Bonde la Kati walikwenda Bonde la Eyasi, wamekaa kwa siku moja lakini wakakwamishwa na viongozi walioko chini yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni suala la athari za mafuriko. Ukiongelea chanzo cha Qangded, Bonde la Eyasi unaongea juu ya uhai wa wananchi wasiopungua 70,000. Chanzo kile kikipotea wanachi hao maisha yao yako hatarini. Juzi wananchi wa Mang’ola baada ya chanzo kile kuharibika wamejichangisha zaidi ya shilingi milioni 21 na Halmashauri ya Karatu ikaweka shilingi milioni 35 ili kunusuru chanzo hicho. Nikuombe sasa na wewe uweke mkono kwa sababu wewe uko kwenye chungu kikubwa ili kuhakikisha chanzo hicho kinaendelea kutoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri ulipokuwa Mang’ola kabla kidogo ya ziara ya Waziri Mkuu ulitoa ahadi ya kuboresha miundombinu katika eneo hilo. Nikukumbushe tu kwamba bado wananchi wanakumbushia utekeleze ahadi yako ya kuboresha baadhi ya miundombinu ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nimesoma katika kitabu cha Waziri, mwaka 1962, kiwango cha maji kwa mtu katika nchi hii ilikuwa ni mita za ujazo 7,862 lakini mwaka huu ni mita 1,800 za ujazo kwa mtu kwa mwaka. Tunakwenda chini kwa kasi kubwa sana. Nadhani kama nchi tuna kila sababu ya kuchukua hatua. Kama miaka 50 kumekuwa na tofauti kubwa kiasi hicho, miaka 50 inayokuja nadhani tutakwenda chini ya mita 100 za ujazo. Kwa hiyo, mimi nishauri hebu Serikali fanyeni jitihada za makusudi za kuhakikisha vyanzo vya maji nchi hii vinalindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015/2016 asilimia 28 ya fedha ambazo tulipitisha ndiyo zimekuja, mwaka uliofuata asilimia 25, mwaka huu ambao tunamalizia asilimia 22. Mheshimiwa Waziri una jeuri gani kuja mbele yetu leo na mabilioni ya hela wakati siku zilizopita umekuwa unapata hizo asilimia chache? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia mimi simuoni Waziri kama anasikitika, simuoni Waziri kama analia, Waziri unataka tukusaidiaje? Hebu lia tusikie halafu na sisi tukusaidie. Mimi naona wewe unaridhika tu na hicho unachopewa. Pambana kama wenzio upate hela za kutosha, maana yake hapa tutakurushia madongo na mawe ya kila aina lakini mwisho wa siku kama ulikuwa unashuka na ukafika 22, bajeti hii hata 20 haitafika. Kwa hiyo, mimi nadhani ndugu zangu suala la maji halina mbadala, mtu aitaka maji unampa maji. Kwa hiyo, mimi niombe hebu tuweke jitihada za makusudi nchi hii tuhakikishe eneo hili linapewa fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda nichangie Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari hususani mabweni, madarasa na majengo ya utawala katika Shule ya Msingi Gongali na Sekondari za Endabash, Banjuka, Welwel na Mangola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu hawapati mikopo na hivyo kuhangaika sana. Niishauri Serikali kuboresha mifumo ya utoaji mikopo ili kweli wale wanaostahili wapate mikopo hiyo. Wako wanafunzi wameacha masomo baada ya kukosa ada, vipo pia vyuo vikuu vinawakaririsha wanafunzi mwaka endapo atashindwa kukamilisha ada, hii si sawa kabisa. Wanafunzi wote wa elimu ya juu wapewe nafasi ya kukopa kisha utaratibu wa kulipa uimarishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi na mafunzo ya VETA hayaepukiki katika Tanzania ya Viwanda tunayojenga. Serikali imesema itajenga Chuo cha Ufundi katika kila Wilaya. Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imejenga Chuo cha Ufundi cha kisasa. Tunashukuru Chuo kimesajiliwa lakini bado kinakosa wakufunzi na vifaa. Tunaomba Wizara itusaidie kupata wakufunzi na vifaa vya ufundishaji katika Chuo cha Ufundi cha Christimac Tree, Bashay Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri pia Serikali irudishe mfumo wa zamani wa shule zote za msingi na sekondari kuwa chini ya Wizara ya Elimu badala ya kuwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa muundo wa sasa, shule hizi ni kama hazina mwenyewe, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ina mambo mengi sana na hivyo kupelekea eneo hili la elimu kutozingatiwa ipasavyo.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kusema yangu machache kwenye mpango huu wa Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hotuba ya Waziri anayehusika lakini pia hotuba ya Kamati ya Bajeti, lakini pia hotuba ya Kambi ya Upinzani. Hotuba zote hizi zimekiri mapungufu ya kibajeti, ndio maana katika mipango yote iliyopita hatukufikia malengo. Sasa sielewi awamu hii katika mpango huu wa nne ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango anakuja na miujiza gani ili aweze kutekeleza yale yote ambayo ameyaweka kwenye mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia takwimu katika mipango iliyopita hasa kile kipengele cha bajeti ya maendeleo, utekelezaji umekwenda kwa asilimia kati ya 50 na 60, mimi ninatafsiri matokeo haya kama sio yenye afya sana kwa sababu kama ni kule shuleni hiyo bado ni B wala sio B+; kwa hiyo tuko chini ya wastani. Kwa hiyo nilikuwa nataka niliseme kwamba hapa kinachotakiwa ni pesa ili mipango hii iweze kufanikiwa kinachohitajika ni pesa, lakini pia kingine kinachohitajika ni dhamira ya dhati ya kutekeleza yale yote ambayo tumekusudia kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri maeneo machache, Mheshimiwa Waziri naomba nikushauri umwezeshe Msajili wa Hazina afanye kazi yake vizuri, Msajili wa Hazina ana makampuni au mashirika yasiyopungua 250 ambayo yanapaswa kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, lakini mengi ya mashirika haya, yamekuwa yakitenda kwa kusuasua, mengine hayajui kabisa kutoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, mashirika mengine hata kama yanatoa gawio, yanatoa gawio kwa kile kiasi ambacho wao wanajisikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia yako mashirika ambayo kwa kweli yanahitaji kuondolewa kwa sababu yanachukua ruzuku Serikalini lakini mwisho wa siku hayazalishi kitu chochote, kwa hiyo nilikuwa nafikiri msaidie Msajili wa Hazina na huyu bwana ukimsaidia naye atakusaidia sana kupata pesa. Msaidie kupata watumishi, lakini pia mpatie vitendea kazi ili aweze kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ni ukusanyaji wa kodi. Mheshimiwa Waziri, wewe ndio mkusanyaji mkuu wa kodi nchi hii, na nchi hasa awamu hii ya tano, imedhamiria kujiendesha kwa kukusanya kodi na kutumia kodi kwenye maendeleo, kwa hiyo unapokutana na wakwepaji wa kodi hawa watu naomba usiangalie sura yao, usiangalie dini yao, usiangalie na kabila yao, na usiangalie na vyeo vyao. Miezi michache iliyopita kulikuwa na lile sakata la makontena ya Makonda, ambayo yalikuwa na sura ya ukwepaji wa kodi, ulijaribu, ulijaribu kutoka hadharani na Watanzania tukakusifu na Watanzania tukasema tunaungana na wewe, sijui mwisho wa siku lile jambo limeishaje, umeshinda au ulishindwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uje utuambie baadae, jambo lile liliisha namna gani, lakini kama tumekubaliana kuendesha nchi kwa kodi basi wale wote wanaostahiki kulipa kodi halali walipe na kusiwe na mianya ya watu kukwepa kodi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la kilimo, wengi wameongelea eneo hili na mimi naomba nipite pia huko huko. Nchi hii karibu asilimia 60/70 ya watu wake ni wakulima, na kwa hiyo kama tunahitaji mipango yetu ifanikiwe ni lazima tujielekeze kwenye namna ya kusaidia kundi hili kubwa liweze nayo kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo, chetu bado ni duni, wakulima wetu wengi wanatumia jembe la mkono wachache wanatumia majembe ya kukokotwa na mifugo, wachache sana wanatumia matrekta, tunahitaji kufanya mapinduzi makubwa kwenye kilimo chetu, ili kilimo kiwe na tija.

Sasa ninajua uko mradi wa Matrekta na mengi yameanikwa pale Kibaha, takwimu zinasema nchi hii, nchi hii ya Tanzania inazo kilometa za mraba karibu laki nne zinazofaa kwa kilimo na kwa kilometa hizo unahitaji walau kiasi cha matrekta milioni mbili ili ulime vizuri, lakini Tanzania ya leo, ina matrekta yasiyozidi 30,000 yakiwemo yale ya pale Kibaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa wewe utaona jinsi ambavyo kwa kweli, tunahitaji mapinduzi makubwa ili kilimo kiwe na tija, lakini pia suala mbegu, wakulima wetu wengi wanapanda zile mbegu ambazo sio zile zilizoboreshwa na matokeo yake wanavuna kiasi kidogo. Miaka ya nyuma tulikuwa na Kampuni inaitwa Tanseed iliyokuwa inazalisha mbegu ya mahindi, kampuni hii imetoweka, mbegu nyingi tunazopanda sasa hivi kwenye zao la mahindi ama zimezalishwa Kenya au Msumbiji au Malawi au Zambia zinazalishwa katika mazingira tofauti kabisa na haya ya kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zinapokuja nyumbani zinauzwa kwa bei ghali mno, ni wakulima wachache wanaweza kupanda hizi mbegu ambazo zimaboreshwa.

Turudishe mashirika yetu ya Kitanzania yaweze kuzalisha mbegu hapa nyumbani ili wakulima wetu wapate mbegu kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye mbolea, maeneo mengi ya nchi hii kama hujaweka mbolea huvuni kitu, lakini tunayo Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ambayo mimi naweza kusema ni kama kampuni inayoelea kuzimuni, kampuni hii inashindwa hata kujiendesha, zamani kampuni hii ilikuwa inazalisha mbolea pale Tanga, kiwanda kimekufa, sasa hivi wanaagiza, wanasambaza na wanauza mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kampuni hii, inaonekana haina uwezo kabisa wa kufanya kazi hii, kimsingi kampuni hii ya TFC inakosa mtaji wa uendeshaji yaani working capital. Mheshimiwa Dkt. Mpango, shirikiana na Waziri mwenzako wa Kilimo na Waziri mwenzako wa Viwanda, ili kuisadia Kampuni ya TFC iweze kufanya kazi yake vizuri, vinginevyo nchi hii suala la mbolea tutalisahau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la Mchuchuma, Mchuchuma na Liganga imekuwa ni wimbo ambao hauna mwisho, hapa ndio nataka kusema kama kweli kama nchi tuna dhamira ya dhati hebu mradi huu ukamilike, miaka 25 ndani ya Bunge hili watu wanaongea habari ya Mchuchuma na Liganga, lakini miradi hii haikamiliki, kuna tatizo gani? Mimi nadhani kama tuna dhamira ya dhati jambo hili linawezekana, tuifanye Mchuchuma kama tulivyofanya kwenye reli, kama tulivyofanya kwenye ATC na kama tulivyofanya kwenye hiyo Striglers Gorge...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Maji ni hitaji la msingi na ni haki kwa kila mtu, kwa hiyo tunapochachamaa na kudai huduma hii muhimu ya maji tunadai jambo ambalo ni la msingi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miradi ya maji ambayo inajengwa chini ya kiwango. Mwaka jana wakati tupo kwenye hotuba kama hii, Wabunge wengi walitaka kuazimia Tume huru ya Bunge ili kwenda kuchunguza mingi ya maji iliyojengwa siku za nyuma hasa ile ambayo iko kwenye ule mpango wa WSDP, lakini baadaye Wizara ikasema tuwape nafasi ya mwisho wenyewe waende wakafanye kazi hiyo ili watuletee ripoti. Sijui na sidhani mpaka leo kama ripoti ile imeweza kupatikana. Kwa hiyo naomba Wizara hii itupe taarifa ya wataaam wao walipokwenda kukagua miradi ile, tatizo hasa ni nini ya ujenzi ule kuwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana mimi natokea Karatu, timu hiyo ilikuja Karatu, walipokuja Karatu badala ya kupelekwa kwenye miradi ambayo ina hali mbaya sana, walipelekwa kwenye miradi ambayo ina unafuu mkubwa. Ukipata Daktari Bingwa anakutembelea kwenye hospitali yako nadhani namna bora ni kumpeleka kule kwenye wagonjwa walioko ICU sio kwa wale wagonjwa wa nje wanaokuja na kurudi, lakini wale wataalam kwa baadhi ya maeneo walipelekwa kwenye miradi ambayo walau inafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Miradi ya Vijiji Kumi kila Wilaya, pale Karatu tuna miradi 10 lakini miradi mitano kati ya 10 haifanyi kazi hadi sasa. Ukijumlisha fedha zilizotumika ni zaidi ya shilingi bilioni nne, Mradi wa Matala, Kansay, Buger, Getamock na Mradi wa Endonyawet, miradi hiyo yote haifanyi kazi. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Karatu tukamweleza kwenye kikao cha wilaya na aliahidi kupita kwenye miradi hiyo, lakini tangu wakati ule mpaka leo hajaweza kurudi. Jambo hili sisi Viongozi wa Wilaya limetushinda, Viongozi wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa ameshakwenda mara kadhaa imemshinda, sasa tunaomba huu mzigo hebu wakaubebe wao. Watu hawa wameiibia Serikali, wakandarasi na wataalam hawa wamewaibia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuombi fedha mpya, tunataka fedha zilizotumika, ziende zikafufuliwe ili wananchi wapate huduma ambayo ilikuwa imekusudiwa. Kwa kweli haipendezi mradi unakaa miaka saba, miaka kumi haufanyi kazi na huku wananchi bado wanahangaika na shida kubwa ya maji iliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, niwaombe hili suala la miradi ya Benki ya Dunia ambayo imechakachuliwa kwa sehemu kubwa, tunaomba walivalie njuga, wafike kwenye maeneo hayo ili watusaidie kuwaleta site wale Wakandarasi waliofanya kazi hiyo, wale Wahandisi, Washauri waliosimamia lakini pia wale Wahandisi wa Halmashauri ambao na wenyewe walikuwa na nafasi kwenye kuhakikisha miradi hiyo inafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni suala la vyombo vya watumia maji. Naamini kujenga mradi wa maji kimiundombinu ni jambo moja, lakini jambo la pili ambalo nalo ni muhimu sana ni kuhakikisha miradi ya maji inakuwa endelevu. Kwa maeneo ya mjini tunazo Mamlaka za Maji Mijini, lakini kwa maeneo ya vijijini kwa sehemu kubwa vyombo hivi vya watumia maji ndivyo ambavyo vinasimamia na kuendeleza miradi hii ya maji. Vyombo hivi, vinatambuliwa katika nchi hii. Sera ya Maji ya Mwaka 2002 inavitaja, hata kwenye hotuba ya Waziri vinatajwa, lakini pia Sheria mpya ya Maji Na.5 ya Mwaka 2016 pia imevitaja. Ni vyombo ambavyo tukivisimamia vizuri vinaweza vikapunguza matatizo ya maji kwenye badhi ya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwetu Karatu tuna vyombo vitatu vinavyotoa huduma. Tuna Mamlaka ya Maji ya Mji wa Karatu ambayo imeundwa ina karibu miaka mitano, ambayo inatoa huduma ya maji kwa asilimia 6.7, lakini tuna Bodi ya Wadhamini, chombo ambacho kimeundwa na wananchi, kilichosajiliwa kisheria ambacho kimekuwepo kwa muda wa miaka 20 na ambacho kinatoa huduma kwa zaidi ya asilimia 76 kinaitwa KAVIWASU. Pia tuna watoa huduma wachache, watu binafsi ambao wana visima vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa naomba nieleze kwamba hivi karibuni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, barua hii hapa, ameandika barua kusitisha zoezi la kisheria la kupata wawakilishi wa wananchi ili waweze kusimamia mradi huo wao nilioutaja wa Karatu Villages Waters Supply. Kama kweli tuna nia njema ya kuona miradi ya wananchi inayofanya kazi, mradi wa Karatu ni wa mfano. Ukitaka kuona mradi wa PPP ambao pia wananchi wameusimamia kwa ufanisi mkubwa ni huo mradi wa Karatu lakini Mkurugenzi ameandika barua kusimamisha uchaguzi kwa sababu Bodi iliyokuwepo muda wake umeisha, sasa wanataka kuchagua bodi nyingine lakini Mkurugenzi anasimamisha eti kwa maelekezo kutoka juu. Eti kwa sababu Wizara sasa hivi inatunga kanuni kwa ajili ya hizi sheria mpya, hivi vinahusiana wapi na wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Karatu tuna machungu, Karatu tuna makovu ya matatizo ya maji ya miaka iliyopita. Naomba msiturudishe huko. Inawezekana kwenye jambo hili kuna siasa, lakini siasa inaingia wapi kwenye huduma ya maji. Niseme tu wazi, Mheshimiwa Humphrey Polepole, Katibu Mwenezi wa CCM alikuja Karatu na ndiye aliyetoa maagizo ya kusimamisha uchaguzi huo, inaumiza sana. Inaumiza sana kwa sababu wananchi mradi huo wameuendesha peke yao miaka 20 bila hata kupata ruzuku ya senti moja kutoka Serikalini. Leo zoezi la kisheria ambalo wananchi wako tayari kuendesha mradi wao, linasimamishwa kwa hisia tu za kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache niseme kwamba, mradi huo wakati wadau wa maendeleo pamoja na wananchi wameumaliza na Bodi ilipokabidhiwa miaka 20 iliyopita, walikuwa na mtandao wa bomba wa kilomita 57, leo wana kilomita 421. Wakati huo walipokabidhiwa wana vituo vya umma 37 leo wana 86. Walipokabidhiwa walikuwa na kisima kirefu kimoja leo wana visima saba. Walipokabidhiwa walikuwa na matenki 10 leo wana matenki 23. Walipokabidhiwa walikuwa na private connections sifuri (1) leo wana 2,661. Walipokabidhiwa walikuwa hawana mfumo wa kulipia kabla (prepaid) leo wana vituo karibu 15 vya prepaid na mambo mengine mengi. Ndiyo maana nilisema kama kuna mradi unaweza kuona jinsi wananchi wanavyosimamia miradi yao na kuiendesha ni mradi wa Karatu lakini leo mradi ule unataka kuzimika kwa sababu tu ya hisia ambazo siyo za kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu jambo hili inasemekana limetoka ofisini kwenu Mheshimiwa Waziri, hebu niwaombe mtuache Karatu tuendeshe mradi wetu kwa namna ambayo tunaweza. Wananchi wako tayari, fomu za kugombea wamechukua lakini sasa zoezi limesimama na matokeo yake hata mishahara ya watumishi hawawezi kulipa kwa sababu wale watendaji wamebaki wenyewe, wale wawakilishi wa wananchi kwa maana ya Wajumbe wa Bodi hawapo. Leo hata madeni ya maduka ya vifaa hawawezi kulipa kwa sababu ya kusimama kwa zoezi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa vile inasemekana jambo hili limeanzia kwenu naomba mruhusu wananchi wa Karatu na vijiji vya jirani waweke viongozi wao. Kama kuna matatizo mengine, hata muende mkautembelee na mtaona, Naibu Waziri nashukuru ulikuja Karatu lakini hata ulivuyokuja, hata kuambiwa kwamba kuna mradi unahudumia asilimia 76 ya maji katika Mji wa Karatu na vijiji vya jirani haukuambiwa. Kwa hiyo, ujue katika sura hiyo jinsi ambavyo kuna tofauti na harufu ya kisiasa kwenye jambo hili. Kwa hiyo, naomba kadri itakavyowezekana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii kuchangia pia kwenye Wizara hii, asubuhi nilipata fursa ya kuuliza swali la nyongeza juu ya mpango wa ujenzi wa reli ya Standard Gauge Kaskazini mwa nchi hii na Mheshimiwa Waziri majibu yake yalikuwa ni kwamba tusiwahishe mambo tusubiri wasilisho lake mambo mazito yanakuja. Sasa na mimi kama alivyoongea

Mheshimiwa Mzee Nsanzugwanko nimecheki kwenye kitabu hiki nimekuta hadithi ni ile ile upembezi yakinifu, usanifu wa kina muhandishi mshauri, mhandisi muelekezi. Hizi hadithi zinatakiwa zifike mahali sasa zikome. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka kuona ni vitu vinajengwa miundombinu ijengwe hadithi ya kujenga reli hii ya Kaskazini ya kuanzia Tanga Musoma imekuwepo tangu nikiwa mtoto mdogo wa shule leo kichwa kimekuwa cheupe bado kipande cha Arusha Musoma hata haijawahi kufanyiwa kazi. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri kama haiwezekani kujenga ni bora tukae kimya tusihamasishe hivi vitu wananchi wapate moyo kwamba kuna kitu kinakuja. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, wenzetu wakoloni waliotutawala miaka hiyo ya 1890 walikuwa na maono wakajenga reli ya mwazo Tanga kwenda Usambara sisi leo miaka 100 baadaye bado tuna mipango ambayo bado haieleweki. Niishauri Serikali tufike mahali tuwe wa kweli kama hatuwezi tuseme hatuwezi. Imeongelewa sana hii reli ya standard gauge sasa hivi tunajenga vipande viwili lakini kwa uhakika kama ambavyo Wabunge wengi wameshauri na makundi mbalimbali yameshauri kipande cha kutoka Tabora kwenda Kigoma ni kipande ambapo hakiepukiki kama kweli tunataka kujenga reli hii iwe na faida ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli inabeba abiria na mizigo tutamaliza kujenga reli hii huko tunakotaka kujenga lakini mwisho wa siku tutakosa mizigo ya kubeba kama hatutakuwa na mikakati ya kutafuta mizigo iko wapi, nadhani ni muda muafaka sasa Serikali ijielekezi hivi hi mizigo ya kubeba iko wapi? Imesemwa sana tuna soko DRC , tuna soko Burundi lakini tufahamu kwamba kuna wenzetu wa Kenya na wenyewe wana reli ya aina hii na wenyewe wanaelekea huku huku na hivi majuzi tumesikia Marais wa nchi hizo mbili wameingia mkataba wa mashirikiano, sasa kama hiyo mizigo tunayoilenga DRC itakwenda kwa wenzetu wa Kenya hivi hii ya kwetu mizigo ya kubeba itatosheleza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tuwe na mpango wa nini tunakwenda kubeba hata kama tunakwenda kuijenga reli hii. Nafikiri sasa pia ni vizuri reli hii ya sasa ya kati tumeijenga kwa kutumia vyuma kutoka nje ya nchi, lakini sisi tunaambiwa tuna-deposite ya vyuma huko Mchuchuma miaka mingi, hivi hata hatuoni fahari tunaona fahari kutumia ndege kwa sababu tuna Twiga pale nyuma hivi kwa nini tusione fahari kujenga reli hizi kwa kutumia chuma ambacho tunacho ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuna nia njema ya kukuza uchumi wa nchi hii hebu hizo reli mbili ambazo tunaambiwa ziko kwenye upembuzi yakinifu, usanifu wa kina kwa maana ya reli ya Mtwara na kuendelea na hii ya Tanga tuijenge kwa kutumia chuma ambacho kinapatikana ndani ya nchi yetu. Kwa namna hiyo nadhani huo uzalendo ambao tunausema kila siku tutakuwa tumeuona vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihame kwenye eneo la pili, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL). Shirika hili ni kati ya mashirika machovu nchi hii. Sote tunafahamu historia ya Shirika la TTCL, shirika hili lina shida kubwa ya upungufu wa mtaji, halina mtaji na ndio maana mambo yake hayaendi. Shirika hili limeshindwa kuingia kwenye soko la ushidani na mashirika mengine ya mawasiliano ambayo tunayo nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo ambalo linasikitisha Taarifa ya CAG imebaini kwamba, mmoja wa wadaiwa sugu wa shirika hili, yaani watu wanaodaiwa na shirika hili ni Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo Mheshimiwa Eng. Kamwelwe wewe ndiye Waziri wake. Unadaiwa shilingi bilioni 20.6 fedha ambazo TTCL wametumia kulipa shughuli na kazi za mkongo wa Taifa, wakati huohuo Wizara yako imeshikilia akaunti ya mapato ya mkongo wa Taifa. Sasa TTCL kwa sura hiyo itawezaje kujiendesha kama wewe mwenyewe baba hutaki kulipa fedha ambazo wao wenyewe wamezizalisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tunaomba kama TTCL kweli tunataka liwe shirika ambalo litaingia kwenye soko la ushindani tuwape fedha zao. Walipeni bilioni zao 20 halafu washindane na hao wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la tatu, Uwanja wa Ndege wa Lake Manyara. Uwanja wa ndege wa Lake Manyara umekuwepo katika vitabu vyetu tangu mwaka juzi, mwaka jana hata mwaka huu, lakini sioni dalili ya uwanja ule kujengwa. Wananchi wamekubali kutoa maeneo yao, wananchi wamekubali kupisha ujenzi wa uwanja ule, lakini mpaka leo hawajalipwa fidia na uwanja haujengwi. Sasa kama Serikali haina fedha muwaambie wananchi waendelee na shughuli zao za kimaendeleo kuliko maeneo ya wananchi mmeyachukua halafu bado hakuna kitu kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom, tumeiongea mara nyingi sana. Mheshimiwa Waziri imetengwa shilingi bilioni 1.4 na imeegeshwa tu kwenye Barabara ya Mto wa Mbu, Loliondo na Nata, shilingi bilioni 1.4, barabara ya kilometa 389 zinakwenda kufanya nini? Nadhani wakati mwingine mnaturidhisha tuone vitu vimeandikwa, lakini kwa uhakika hakuna kitu unaweza kwenda kufanya kwenye barabara ile kwa hiyo, utuambie hii barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom inakwenda kujengwa lini? Na hii bilioni 1.4 ni za kujenga lami au ni kwa ajili ya kuendelea na upigaji uleule wa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina nambo mengine kama hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeona kwenye barabara ile fedha hizi umezielekeza kwenye kipande cha Mbulu – Haydom, yaani unakwenda kujenga katikati fulani, mwanzo umeacha na mwisho umeacha. Mheshimiwa Waziri hata ukiingia saluni hata kichwa hakianziwi huku katikati unaanzia huku pembeni; sasa wewe kwa nini umeenda kuanza hii barabara pale katikati? Kama kweli tunataka kujenga barabara hii na tuone ina manufaa ya kibiashara na kiuchumi kipande cha Karatu – Mbulu nashauri uanzenacho ndio kipande ambacho kina magari mengi, lakini ndiyo kipande ambacho udongo wake wakati wa mvua unateleza sana; hata muwa Mheshimiwa Engineer Kamwelwe unaanza kule mwisho au huku mbele, lakini wewe unapiga muwa katikati, una lako jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwamba, kwa kweli, barabara hiyo kama mna nia ya kuijenga muanze kuijenga kuanzia Karatu kwenda Mbulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Barabara ya kuunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu ilikuwa Barabara ya Oldian Junction – Matala – Mto Sibiti na kwenda Mkoa wa Simiyu, lakini sasa ni kama barabara hii imehamishwa ndio hii ya Karatu – Mbulu – Haydom. Hebu Serikali itoe kauli na Wananchi wajue, Waziri Mkuu alikuwa Mang’ola aliulizwa swali hilo akasema barabara imeshafanyiwa usanifu na baada ya usanifu tutapata fedha na kujenga barabara hiyo. Sasa barabara ya kuunganisha Arusha na Simiyu ni barabara ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali muwaambie wananchi, wananchi wasisubiri kitu ambacho hamuwezi kujenga. Nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania na hivyo ni vyema sekta hii ambayo ndiyo imeajiri watu wengi wa hali ya chini iangaliwe kwa umuhimu mkubwa na ipelekewe fedha za kutosha. Upelekaji wa fedha kwenye Wizara hii bado uko chini sana.

Mheshimiwa Spika, kama nchi tunatakiwa kujitafakari juu ya hali isiyotia matumaini ya baadhi ya mazao nchini. Wakulima wa katani/mkonge wamekata tamaa, kahawa nao wamekata tamaa, alizeti, mbaazi, mahindi, hali ni mbaya, korosho ndiyo hiyo inayoyoma.

Mheshimiwa Spika, ni vyema tujiulize tumekosea wapi? Hivi mkulima wa Tanzania alime nini ili apate kunufaika?

Mheshimiwa Spika, mahindi ni zao linalolimwa kama chakula na biashara. Mbegu bora ya mahindi inauzwa ghali sana na hivyo kufanya wakulima wengi kushindwa kuzipanda. Serikali iangalie namna bora ya kuwapatia wakulima mbegu bora. Huko nyuma tulikuwa na mashamba ya kuzalisha mbegu kupitia kampuni ya TANSEED ambayo yalizalisha mbegu tena katika mazingira ya kwetu. Mbegu kwa sasa nyingi zinatoka nje na ndiyo maana zinauzwa ghali.

Mheshimiwa Spika, zao la mbaazi nalo lina hali mbaya sana. Mwaka jana zao hili lilipoteza thamani na halikuuzika mwanzoni na baadaye liliuzwa kwa bei ndogo sana. Serikali iwatafutie masoko ya mbaazi.

Mheshimiwa Spika, kama kweli kilimo kinathaminiwa Serikali iwaajiri maafisa wengi wa ugani ili wakulima wapate mafunzo na ushauri wa kitaalam kwa karibu sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio ya wanyama waharibifu hasa tembo na nyati waliharibu mazao ya wananchi katika Vijiji vya Rhotia, Kilimatembo, Ayalabe, Kitete, Kamba ya Nyoka na Oldeani Wilayani Karatu yamekuwa ya kujirudia rudia na mwaka huu yamekithiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tembo wengi wanashinda mashambani na kula mahindi ambayo bahati mbaya mwaka huu yako kidogo sana; wanyama hao wanatoka Hifadhi ya Ngorongoro. Niishauri Serikali iwaelekeze mamlaka hiyo kuongeza doria ili kuwadhibiti wanyama hao.

Tembo hawasikii lolote, wananchi wanahangaika sana na mazao yao yanaharibiwa sana. Katika ukanda huo wa msitu kuna kambi tatu tu. Kambi hizo hazitoshi na pia askari wawe na mafuta na silaha zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, wako baadhi ya askari wa wanyamapori ambao wanaendeleza uonevu na ukatili kwa mifugo inayoingia kwenye hifadhi kwa bahati mbaya. askari hao wamekuwa wakiua au kujeruhi ng’ombe. Hivi majuzi askari wa hifadhi ya Ziwa Manyara waliwaua ng’ombe watatu na kujeruhi wengine watano na pia kumvunja mguu mwananchi kwa kumpiga risasi mguuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ng’ombe hali wanyama wala hashambulii wala kudhuru miti kwanini wapigwe risasi? Askari hao si waadilifu kabisa na wamekuwa wanapokea rushwa ili mtu aingize mifugo. Huo ni unyama dhidi ya mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku za nyuma NCAA na TANAPA walikuwa wanasaidia miradi mbalimbali ya maendeleo; tangu mwaka 2016 miradi hiyo imepungua sana. Ili waone kuwa na wao ni sehemu ya hifadhi hizo ni vyema miradi ya maendeleo ya wananchi iweze kutekelezeka, kama vile miradi ya shule, afya, maji na kadhalika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada nyingi anazofanya Waziri Kalemani katika kuhakikisha kwamba Tanzania yote inawaka umeme ifikapo 2021 bado jitihada hizi zinakwamishwa na baadhi ya watendaji na wakandarasi. Mawaziri wa Wizara hii wameongea mara nyingi kuwa umeme ukifika kwenye kijiji chochote utafika kila taasisi, kitongoji, lakini kinachofanyika Tanzania hii ni tofauti na kauli za Mawaziri. Katika Wilaya ya Karatu Vijiji vya Huduma, Khusumay, Kauam, Rhotia, Losetete umeme haujaenda kwenye vitongoji bali umeishia kwenye centers za vijiji wananchi wanalalamika sana kwani imeme haujafika kwenye vitongoji.

Mheshimiwa Spika, tatizo hili limesababishwa wa timu za survey ambazo hazikuwasilishwa viongozi wa wananchi. Timu hii maeneo mengine walikwenda hata siku za jumapili na walifanya wenyewe bila kushirikisha viongozi wa wananchi. Niishauri Serikali itoe maelekezo ya kutosha ili survey inapofanyika viongozi wa wananchi washirikishwe ili maeneo yote yafanikiwe.

Mheshimiwa Spika, leo ni mwezi wa tano mwishoni na bado katika Wilaya ya Karatu, Vijiji vya Bugeu, Ayalaliyo, Endanyawe, Kambifairu, Umbang Laja, Quvus. Lositete, Endalals, Bawakta, Mangola Juu pamoja vitongoji vyake bado umeme haujafika. Wananchi wameshajiandaa katika maeneo hayo na wanasubiri wakandarasi. Niombe Waziri uwaelekeze wakandarasi ili wakamilishe kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Waziri, Dkt. Kalemani kwa kutoa transformer tisa ili kuunga visima tisa vya maji kwenye umeme. Kwa niaba ya wananchi wanaotumia visima hivyo nimshukuru sana Waziri. Hata hivyo, nimuombe Waziri afuatilie transformer moja ambayo haijafungwa katika kisima cha Endamavamek, kijiji hiki kiliombewa transformers mbili lakini imefungwa moja tu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Takwimu zinaonesha kwamba nchi hii takriban asilimia 65 ya wakazi wake wanajihusisha na shughuli ya kilimo wengi wao wakiwa maeneo ya vijijini ukilinganisha na karibu asilimia 97 ambazo tulikuwa nazo miaka ile tunapata uhuru wetu. Sasa hii inatuambia nini, hii inatuambia kwamba kila mwaka asilimia ya watu wanaojihusisha na kilimo inazidi kupungua na matokeo yake tutafika mahali kama ambapo wenzetu USA wamefika asilimia mbili ya wakazi wake ndiyo wanaojihusisha na kilimo na masuala ya ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii 65% ya Watanzania inazalisha chakula kwa ajili yake lakini pia inabidi izalishe chakula kwa ile 35% iliyobakia. Pia hii asilimia 65 inatakiwa izalishe mazao ambayo tunataka yaende viwandani. Vilevile hii asilimia 65 inatakiwa izalishe kwa ajili ya mazao ya kuuza nje ili tuweze kupata fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri ni muhimu sasa tujiulize swali, hii asilimia 65, je, itaweza kufanya haya yote ambayo tunakusudia iende ikayafanye? Takwimu za Serikali bado zinaonesha kuwa asilimia 53 ya Watanzania inalima kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 ndiyo inayotumia matrekta, asilimia 27 ndiyo inayotumia wanyama kazi. Kwa hiyo utaona ni dhahiri kwamba kwa asilimia hizi jinsi zilivyo kwa sasa ni vigumu sana kufikia hicho ambacho tunakitaka. Ni wazi kwa kutumia jembe la mkono hatutatoka hapa tulipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa nataka kuishauri Serikali hii, kwamba kama kweli inajali wananchi wake wananchi wake hawa ambao asilimia kubwa wameajiriwa na sekta ya kilimo ni lazima ifanye mapinduzi kwenye kilimo hiki ili basi wazalishe kile ambacho tunatarajia wazalishe. Leo katika nchi hii hakuna mkulima anafuraha; wakulima wa korosho wamenuna, wakulima wa alizeti wamenuna, wa kahawa walikwisha kununa wa mahindi ndiyo hivyo halikadhalika. Kwa hiyo ili mazingira haya ya kilimo yaweze kuvutia ni sharti wakulima wapate kile ambacho kitawasaidia ili waweze kwenda kuzalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado bei ya mazao ya wakulima hali ni mbaya sana. Hebu Serikali tuishauri ikubali kuwaunganisha wakulima na masoko ili waweze kupata fedha ambazo zitawasaidia katika mambo yao lakini pia kuchangia kwenye uchumi wa taifa. Hapo nyuma tulikuwa na mikopo ya matreka kupitia Shirika la SUMA JKT, lakini mikopo ile sasa imefutwa, ukitaka trekta inabidi ulipe cash milioni 48, milioni 50. Hivi ni Watanzania wangapi wa vijijini wanauwezo wa wa kulipa shilingi milioni 48 ili waweze kumiliki trekta? Mheshimiwa Mpango wewe ni mkopaji mzuri sana, unakopa nje na unakopa ndani na ndiyo maana Deni la Taifa hadi sasa ni trilioni 51.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba na tunashauri wakulima wakopeshwe matrekta ili wakazalishe vizuri. Kwa majembe yetu ya mikono na kwa kutumia wanyama kazi hatuwezi kutoka hapa ambapo tumefika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala zima la madeni ya Serikali, kama ambavyo nimesema hapa mbele. Walimu, kada ambayo inafanya kazi katika mazingira magumu sana wanaidai Serikali shilingi bilioni 61. Hizo hela za walimu wapewe. Tunafahamu mazingira ya kazi ni magumu miundombinu na kazi ya ni kidogo, tunaomba Serikali ilipe hela za walimu ili walimu wakafanye kazi na wazalishe elimu ya watoto wetu. Ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu umechukua zaidi ya miaka 20 kufika hatua hii ya leo kujadiliwa Bungeni. Waziri alikuwa na nia njema kuwashirikisha wadau wa Tasnia ya Habari kutoa mawazo yao. Ni bahati mbaya Muswada huu haujasheheni mawazo ya wadau wa habari. Hakukuwa na ulazima wa kuingiza Bungeni haraka hivi ukiwa haujachangiwa na wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 5(e); Kutoa Leseni kwa Machapisho. Kifungu hiki nashauri kifutwe na badala yake msajili wa magazeti aendelee na kazi ya kusajili magazeti kwa sababu kuna hatari ya leseni kutumiwa vibaya kuvinyima vyombo vya habari haki ya kuchapisha.
Mheshimiwa Spika, vifungu vya 50(2 -11), vifungu hivi vinaadhibu wasomaji na wachapishaji wa magazeti. Nashauri vifungu hivi vifutwe vyote, vifungu hivi vinatishia maisha ya wasomaji na uwekezaji katika mitambo ya uchapishaji kwa kumpa ruhusa Mkuu wa Jeshi la Polisi kukamata na kuharibu mitambo.