Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Willy Qulwi Qambalo (9 total)

MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Barabara ya Oldeani Junction - Mang‟ola – Matala - Manuzi ni kiungo muhimu sana kwa kuunganisha Kanda ya Kaskazini (Mkoa wa Arusha) na Mikoa ya Kanda ya Ziwa (Simiyu):-
Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika muda wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Oldeani Junction - Mang‟ola - Matala - Manuzi ambayo pia hujulikana kama Kolandoto - Oldeani Junction yenye urefu wa kilometa 328 umeanza na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami zitaanza baada ya kukamilika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaoendelea na kupatikana kwa fedha za ujenzi.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y MHE. WILLY Q. QAMBALO) aliuliza:-
Pamoja na kuwa katika Kata ya Qurus zipo Ofisi ya Kituo cha TANESCO, Vijiji vingi vya Kata hiyo vikiwemo Gongali, Qurus, Qorongaida, Genda na G/ Lambo havijafikiwa na umeme na vichache vyenye umeme, kwango cha usambazaji ni kidogo sana:-
Je, ni lini Serikali itawapaia wananchi wa Kata hiyo huduma hiyo muhimu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Willy Qulwi Qambalo, Mbunge wa Karatu linaloulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Flatei Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jina la Kata iliyoko Wilayani Karatu ni Qurus yenye vijiji vya Bashay, Doffa G‟Lambo, Gendaa, Gongali, Qorong‟aida na Qurus. Aidha, hakuna Ofisi ya kituo cha TANESCO katika Kata hii. Vijiji vyote 23 vilipangwa kupatiwa umeme katika mradi wa REA awamu ya II Wilaya ya vimewashiwa umeme na hivi sasa Mkandarasi Angelique International Ltd anaendelea na kazi ya kuwaunganishia umeme wateja. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 99 na utakamilika ifikapo tarehe 30 Juni, mwaka huu. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 53.24.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyotajwa na Mheshimiwa Mbunge G‟lambo, Gongali, Qorong‟aida na Qurus vimewekwa kwenye mpango wa REA awamu ya III unaoanza Julai, 2016. Kazi ya kupeleka umeme katika Vijiji hivi itahusisha pia ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 8, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 12, ufungaji wa transfoma 5 zenye ukubwa mbalimbali lakini pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 236. Gharama ya kazi hii ni hsilingi milioni 740.
MHE. WILLY Q. QAMBALO aliuliza:-
Katika kupunguza tatizo sugu la maji Wilaya ya Karatu baadhi ya vijiji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamechimba visima virefu 12 katika maeneo ya Basodawish, Endabash, Rhotia Kainani, Endamarariek, Getamock, Karatu Mjini, Gongali na kadhalika, visima hivyo vinaendeshwa kwa kutumia mashine za dizeli jambo ambalo linasababisha gharama kubwa za uendeshaji.
Je, Serikali itawasidia lini wananchi hao kwa kuwaunganisha na nishati ya umeme katika visima hivyo ili kupunguza gharama za uendeshaji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kabla sijatoa maelezo ya kuhusiana na swali la Mheshimiwa Mbunge niombe kwa ridhaa ya kiti chako Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge nichukue nafasi moja ya kuwapa pole sana wananchi wa Jimbo langu Chato kwa kupata msiba mkubwa ambao umetokea juzi baada mvua kubwa kunyesha kwenye Jimbo la Chato na kusababisha wananchi wawili kupoteza maisha yao na wananchi wengine 17 kujeruhiwa vibaya sana. Kwa heshima ya kiti chako basi kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge tujumuike na wananchi wa Chato katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sasa kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Willy Qulwi Qambalo, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kufikisha umeme katika maeneo yote nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Wilaya ya Karatu. Kipaumbele katika kutekeleza miradi ya umeme ni pamoja na kufikisha umeme katika miundombinu inayotoa huduma za kijamii ikijumuisha visima vya maji, shule, zahanati, makanisa, misikiti na maeneo ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Basodawish, Endabash, Endamarariek, Getamock pamoja na maeneo ya Karatu Mjini yamefikishiwa huduma ya umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Pili. Hata hivyo huduma ya umeme haijafikishwa katika visima vya maji vilivyopo katika maeneo niliyoyataja. Kazi ya kupeleka umeme katika visima hivyo itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 12.6 na ufugaji wa transfoma tano za KVA 100 kila moja. Gharama ya kazi hizi ni shilingi milioni 467.16. Visima vyote katika vijiji vilivyotajwa hapo juu vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika kisima kilichopo Karatu Mjini inahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 1.2 na kufunga transfoma ya ukubwa wa KVA100. Gharama ya kazi hii ni shilingi milioni 33.81 kazi imepangwa kutekelezwa kupitia bajeti ya TANESCO ya mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha vijiji vya Gongali, Gyekrum Lambo, Kainam Rhotia na Kambi Faru vitapata umeme kupitia mradi wa REA awamu ya Tatu. Kazi za kuvipatia umeme vijiji hivi itahusisha pia upelekaji umeme kwenye visima vya maji vilivyopo katika vijiji hivyo.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliluliza:-
Wilaya ya karatu ina umri wa zaidi ya mika 20 lakini bado haina Hospitali ya Wilaya jambo ambalo linawatesa wakazi wengi hasa wazee, akinamama na watoto.
Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya cha Karatu kuwa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Qulwi, Mbunge wa Karatu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kupandisha hadhi kituo cha afya kuwa hospitali yanaanza katika Halmashauri yenyewe kupitia Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa. Taratibu hizi zikikamilika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa kibali baada ya kujiridhisha kupitia timu ya ukaguzi hivyo Halmashauri unashauriwa kuanzisha mchakato wa kujadili suala hilo katika vikao vya kisheria na kuwasilisha katika mamlaka husika kwa maamuzi.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Bei kubwa ya pembejeo hususan mbegu bora ya mahindi imesababisha wakulima wengi kupanda mbegu zilizo chini ya kiwango na hivyo kusababisha uzalishaji hafifu sana, mfano msimu wa mwaka 2015/2016 kilo moja ya mbegu ya zao hilo iliuzwa kati ya shilingi 5,000 hadi shilingi 6,000.
(a) Je, ni nini kinafanya bei ya mbegu bora kuwa ghali sana?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa zao hilo kupata mbegu hizo kwa gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Jimbo la Karatu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, bei ya mbegu bora inakuwa ghali kutokana na gharama halisi za uzalishaji wa mbegu hizo. Mbegu bora zinatokana na tafiti mbalimbali zinazofanywa na watafiti na huchukua muda mrefu kuweza kupata aina mpya ya mbegu.
Pia mbegu bora zinapozalishwa hupitia hatua mbalimbali kama vile usajili wa mashamba, ukaguzi wa mashamba, uchukuaji wa sampuli na upimaji wa mbegu maabara kabla ya kuanza kuziuza kwa wakulima, hatua hizo zote zinachangia mbegu bora kuwa ghali ikilinganishwa na mbegu ambazo sio bora.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia tija inayopatikana kutokana na matumizi ya mbegu bora utaona kuwa bei ya mbegu bora sio ghali. Mfano, ukitumia mbegu bora za mahindi kilo kumi inayotosha ekari moja pamoja na kanuni bora za kilimo inaweza kutoa gunia 25 hadi 30 ikilinganishwa na gunia tano hadi kumi zinazopatikana kwa kutumia mbegu isiyokuwa bora.
(b) Mheshimiwa Spika, katika kukabaliana na changamoto ya bei ya mbegu bora na kwa kutambua uwezo mdogo wa wakulima kuweza kumudu gharama hizo, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija. Aidha, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuimarisha utafiti wa mbegu bora na kuwahamasisha wakulima kuzalisha mbegu za daraja la kuazimiwa ubora (Quality Declared Seeds) ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora katika maeneo ya vijijini.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Miaka ya karibuni zao la mbaazi limechangia kipato kwa wakulima baada ya kupata bei nzuri katika masoko. Katika msimu wa 2016/2017 bei ya zao hili ilishuka hadi kufikia shilingi 900 kwa kilo moja ukilinganisha na bei ya shilingi 2,800 kwa kilo moja kwa msimu wa 2015/2016.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaunganisha wakulima wa zao hilo na masoko yaliyoko ndani na nje ya nchi ili waweze kupata bei nzuri?
Wapo wanunuzi wa zao hilo, mathalani Kampuni ya Kilimo Market wanachukua mazao ya wananchi na kuchelewa kuwalipa fedha zao. Je, ni nini kauli ya Serikali dhidi ya makampuni ya namna hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya mbaazi iliporomoka katika msimu wa 2016/2017 katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na ongezeko la uzalishaji wa zao hilo katika nchi za China, Brazil, Myanmar, Canada, Msumbiji na Sudan kuliko mahitaji ukilinganishwa na msimu wa mwaka 2015/2016. Ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata soko la uhakika la mbaazi, Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko iliandaa Mkataba wa Makubaliano (Memorandum of Understanding – MOU) na Serikali ya India ambao ndiyo wanunuzi wakubwa wa mazao ya jamii ya mikunde hapa nchini ili kuweka mfumo rasmi wa soko la mazao ya jamii ya mikunde hapa nchini. Mkataba huo ulipelekwa India ambako kwa mujibu wa Ubalozi wa India nchini bado wanaufanyia kazi kabla ya kusainiwa na pande zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hatua zinazochukuliwa za kuuza mbaazi nchini India, Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambao umeleta matokeo mazuri kwa zao la korosho ili pia utumike kwa zao la mbaazi. Ili mfumo ho utumike ipasavyo na kwa ufanisi, Serikali itawahamasisha wakulima kujiunga katika vyama vya ushirika kwenye maeneo yao na pia kuwa na utaratibu wa kupanga bei elekezi yenye kuzingatia gharama zote za uzalishaji kama ilivyo kwa zao la korosho.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wanunuzi kuchukua mazao ya wananchi na kuchelewa kuwalipa fedha zao, Serikali itaendelea kutoa maelekezo na kuhakikisha kuwa wanunuzi wote wa mazao nchini wanawalipa wananchi fedha zao mapema iwezekanavyo mara tu wananuapo mazao hayo. Hata hivyo, mfumo rasmi wa soko la mazao ya jamii ya kunde ambao utakuwa chini ya usimamizi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko utaziba mianya ya wanunuzi holela hivyo kuepusha udanganyifu wakati wa kununua mazao ya jamii ya kunde ikiwa ni pamoja na mbaazi kutoka kwa wakulima.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa ardhi yote ya Tanzania inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kisheria kama namna mojawapo ya kuondoa migogoro hususan ya wakulima na wafugaji nchini?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kupanga na kupima ardhi yote nchini kama namna mojawapo ya kupunguza migogoro baina ya watumiaji wa ardhi, hususan wakulima na wafugaji na watumiaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya Mwaka 2007, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni jukumu la mamlaka ya upangaji ambazo ni halmashauri za wilaya na vijiji. Aidha, kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya Mwaka 2007 kinaelekeza kuwa jukumu la upangaji na uendelezaji miji lipo chini ya mamlaka za upangaji ambazo ni Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji, Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo. Wizara yangu imekuwa ikizihamasisha na kuzijengea uwezo mamlaka za upangaji katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kuandaa mipango kabambe ambayo ndiyo dira ya kuongoza uendelezaji wa ardhi katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa ardhi yote ya Tanzania inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kisheria. Mikakati hiyo ni pamoja na kuandaa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha kila Kipande cha Ardhi Nchini ambayo itahusisha halmashauri zote nchini; kusajili makampuni binafsi ya kupanga na kupima ardhi yenye weledi wa kufanya kazi hizo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo na kununua vifaa vya kisasa vya upimaji vitakavyosambazwa kwenye kanda nane za usimamizi wa ardhi kwa lengo la kuharakisha upimaji wa ardhi katika wilaya mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la upimaji wa ardhi ni endelevu, natoa rai kwa halmashauri zote nchini kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao kila mwaka kwa ajili ya kurahisisha na kuharakisha zoezi la kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na mipango kabambe na hivyo kuwezesha kukamilika kwa azma ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini kwa wakati.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Matukio ya Wanyamapori kutoka nje ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo Wilayani Karatu na kuharibu mazao ya wananchi na kujeruhi watu yamekuwa yakijirudia mara kwa mara:-
• Je, ni nini mkakati wa Serikali kuwadhibiti wanyama hao ili wabaki katika maeneo waliyotengewa;
• Fidia/Kifuta jasho kinachotolewa pindi wanyama wanapofanya uharibifu ni kidogo sana na imepitwa na wakati. Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya kifuta jasho, ili kuendana na mazingira ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uharibifu wa mali na maisha ya binadamu kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu unajitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Ngorongoro. Katika Eneo la Ngorongoro uharibifu unajitokeza zaidi katika maeneo ya mashamba na makazi ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hiyo.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu inakabiliana na changamoto ya uharibifu wa mali na maisha ya binadamu kwa kufanya doria za pamoja. Aidha, Mamlaka ya Ngorongoro ina vituo vitano katika maeneo ya Kilimatembo, Elewana, Nitini, Bonde la Faru na Masamburai kwa ajili ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, vilevile magari mawili yamenunuliwa kwa ajili ya madhumuni hayohayo.
Mheshimiwa Spika, juhudi nyingine zinazofanyika ni kuendelea kutoa elimu ya namna ya kujihami na kudhibiti wanyamapori, hususan tembo. Elimu hiyo, inahusisha matumizi ya pilipili, mafuta machafu na mizinga ya nyuki kuzunguka mashamba kama njia ya kufukuza tembo.
Mheshimiwa Spika, fedha za kifuta jasho na kifuta machozi hazitolewi kama fidia bali hutolewa kwa ajili ya kuwafariji wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu. Hivyo, fedha hizo kuwa ni kidogo na hazilingani na hali halisi ya uharibifu.
Mheshimiwa Spika, kulingana na wingi wa matukio pamoja na ufinyu wa bajeti Serikali imeamua kupitia Kanuni za Kifuta Machozi na Kifuta jasho ili kuondoa changamoto zilizopo kiutendaji.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Eneo la Mang’ola katika bonde la Eyasi, Wilayani Karatu ni maarufu sana kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia chemchem za Qangded. Chemichemi hizo ziko katika hatari ya kutoweka kutokana na kuingiliwa na shughuli za kibinadamu:-
Je, ni lini Serikali itaweka mpango madhubuti wa uhifadhi wa chemchem hizo ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka kwa kutumia sheria zilizopo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Kati kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, mwaka 2017 ilifanya tathmini ya uharibifu wa mazingira, matumizi ya maji na mipaka ya chanzo hicho ambapo yafuatayo yalibainika:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha Qang’dend kimehifadhiwa kwa kuwekewa mpaka tangu mwaka 2006 na baadaye mwaka 2014 kwa umbali wa kuanzia mita 145 hadi mita 595 kulingana na eneo lilivyo katika maeneo yenye chemchem na umbali wa kuanzia mita 84 hadi mita 303 kwa baadhi ya maeneo ya kandokando ya Mto Mang’ola ambayo chanzo chake ni chemchem ya Qang’dend. Alama za mipaka zilizosimikwa haziheshimiki na wananchi katika baadhi ya maeneo kutokana na kwamba zingine zimejificha chini ya ardhi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, pili, pampu zote za umwagiliaji zimeondolewa kwenye mto na kuwekewa nje ya mto kwenye umbali ambao hazina athari kwenye chanzo. Pia tathmini imebaini kuwa tatizo la chemchem kukauka limechangiwa na mchanga ama udongo mwingi uliosafirishwa kutoka maeneo ya juu ya chemchem na mito midogo iliyoingiza maji katika mto Mang’ola ambapo imesababisha kuziba kwa macho ya chemchem hizo.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, tatu; hatua zilizopangwa kutekelezwa na Wizara yangu ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo, kuweka mipaka madhubuti katika maeneo yote muhimu ya chanzo na kuondoa michanga iliyoziba chemchem hiyo.