Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Raphael Michael Japhary (11 total)

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-
Viwanda vingi vya Moshi vilibinafsishwa havifanyi kazi, badala yake vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali na vimechakaa sana; aidha mafao ya wafanyakazi waliostaafishwa katika Kiwanda cha Magunia na Kilimanjaro Timber Utilization hayakulipwa inavyostahili na hivyo kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu ya madai yao bila mafanikio:-
(a) Je, kwa nini Serikali isivikabidhi viwanda hivyo kwa kampuni nyingine zenye uwezo wa kuviendeleza na hivyo kupunguza tatizo la ajira katika Mji wa Moshi?
(b) Je, ni lini madai ya mafao ya wafanyakazi waliostaafishwa katika viwanda hivyo yatalipwa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na zoezi la kufanya Ufuatilliaji na tathmini katika viwanda na mashirika ya umma yaliyobinafsishwa ili kubaini kama masharti ya vipengele vya Mikataba ya mauzo iliyoingiwa kati ya Serikali na wawekezaji yametekelezwa ili kuchukua hatua stahiki. Katika utekelezaji wa zoezi hilo, pamoja na mambo mengine mikataba yote ya mauzo inapitiwa na endapo itagundulika kuwa masharti ya mikataba husika yamekiukwa, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo Serikali kuvirejesha viwanda hivyo. Pia wawekezaji mahiri wenye nia ya kuwekeza nchini watatafutwa. Vilevile viwanda ambavyo vitaonekana wamiliki wana nia na uwezo wa kuvifufua, makubaliano mapya yatafikiwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wote katika viwanda vilivyotajwa walilipwa stahiki zao. Hata hivyo, baada ya malipo hayo kutolewa wafanyakazi waliendelea kudai zaidi madai yanayotokana na Mikataba ya Hiari. Serikali ilishatolea ufafanuzi suala hili kuwa madai yanayotokana na Mkataba wa Hiari yanapaswa kulipwa kutokana na hali ya uzalishaji wa kiwanda au kampuni kwani yanalenga kugawana ziada ambayo kiwanda kama cha Magunia (Tanzania Bag Corporation –TBCL) hakikuwa nayo, wakati kile cha Kilimanjaro Timber Utilization kiliuzwa kwa ufilisi.
Aidha, wakati zoezi la ubinafsishaji linatekelezwa, kiwanda cha Magunia cha Moshi kilikuwa na malimbikizo ya mishahara ya Wafanyakazi wake kwa zaidi ya miezi 18 hivyo hakikuwa hata na uwezo wa kulipa malipo ya kisheria, hivyo madai ya nyongeza hayakuwa na msingi. Serikali haiwajibiki kulipa mafao yoyote kwa wafanyakazi waliokuwa katika viwanda vya Magunia na Kilimanjaro Timber Utilization.
MHE. ANTONY C. KOMU (K.n.y. MHE. RAPHAEL J. MICHAEL) aliuliza:-
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ilianza mchakato wa kuifanya Jiji tangu mwaka 2012 baada ya kupata baraka za Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro (RCC) na Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Moshi (DCC) na sasa mchakato huo umekamilika katika hatua zote za kikanuni.
Je, ni lini Serikali itatangaza Manispaa ya Moshi kuwa Jiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika vikao vyote vya kisheria vimekaa na kuridhia pendekezo la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Jiji. Hapo awali, maombi hayo yaliwasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya maamuzi. Hata hivyo, maombi hayo yaliyejeshwa ili yafanyiwe marekebisho kutokana na upungufu uliobainika kulingana na vigezo na taratibu zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa timu ya uhakiki kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ipo katika uhakiki wa maombi ya maeneo mapya ya utawala yakiwemo maeneo kutoka Manispaa ya Moshi ili kuhakiki vigezo vilivyozingatiwa katika kuanzisha maeneo hayo. Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo nchi nzima, Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa atashauriwa ipasavyo kuhusu maombi haya.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA (K.n.y MHE. RAPHAEL J. MICHAEL) aliuliza:-
Hospitali ya Mawenzi ambayo ni ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uchakavu wa miundombinu yake, samani, mlundikano mkubwa wa wagonjwa kwa sababu Manispaa ya Moshi haina Hospitali ya Wilaya, upungufu wa Madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya:-
(a) Je, ni lini hospitali hiyo itafanyiwa ukarabati ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuiongezea watumishi niliowataja?
(b) Je, ni lini Serikali itakubali ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi la kujenga Hospitali ya Wilaya?
(c) Je, Serikali itasaidiaje Hospitali ya Mawenzi iweze kupata mkopo kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili iweze kuboresha miundombinu yake?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mkoa umejiwekea utaratibu wa kufanya ukarabati wa Hospitali ya Mkoa kupitia fedha za uchangiaji wa gharama za matibabu. Hadi sasa zimeshatumika Sh. 14,700,000/= kwa ajili ya ukarabati wa mfumo wa maji, jengo la wagonjwa wa nje pamoja na jengo la Madaktari waliopo mafunzoni (intern doctors). Mkakati uliowekwa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili kujenga uwezo wa kuihudumia hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la watumishi, hospitali hiyo imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya 79, katika mwaka wa fedha 2015/2016 na watumishi 65 wamepangwa kuajiriwa katika mwaka ujao wa 2016/2017 ili kukabiliana na upungufu huo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wilaya ya Moshi imeingia ubia wa utoaji huduma na Hospitali ya Mtakatifu Joseph (DDH) ambayo itatumika kama Hospitali ya Wilaya. Ili kuendelea kuboresha huduma za afya, Halmashauri imeamua kukiboresha Kituo cha Afya cha Msaranga ili kukiongezea uwezo wa kutoa huduma zenye hadhi ya hospitali.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ya Mawenzi unafanyika, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.35 katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, kuhusu suala la mkopo kutoka TIB, Mkoa unashauriwa kukamilisha mazungumzo yanayoendelea na yatakapowasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutatoa ushirikiano baada ya kuridhishwa kama mkopo huo umekidhi vigezo vinavyozingatiwa katika tathmini ya mikopo ya aina hii.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:- Uwanja wa ndege wa Moshi ni muhimu sana kwa kukuza masuala ya utalii kwani unatumiwa na watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro lakini uwanja huo unahitaji kufanyiwa ukarabati ili uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa. Je, ni lini Serikali itaufanyia ukarabati uwanja huo ili uweze kufanya kazi yake kwa ufanisi hasa kuendeleza sekta ya utalii na uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuhusu umuhimu wa kiwanja cha ndege cha Moshi kwa sekta ya usafiri wa anga na mchango wake katika uendelezaji wa sekta ya utalii na uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu huo wa kiwanja cha ndege cha Moshi, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia. Kazi hii ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inahusisha pia viwanja vya ndege vya Iringa, Njombe, Songea, Lindi, Kilwa Masoko, Tanga, Lake Manyara, Singida, Musoma na kiwanja kipya katika Mkoa wa Simiyu na inatarajiwa kukamilika ifikapo Machi, 2017. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ifikapo Machi, 2017 Serikali itaendelea na hatua inayofuata ya kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa kiwanja hicho. Aidha, mamlaka ya viwanja vya ndege imekuwa ikifanya matengenezo ya miundombinu ya kiwanja mara kwa mara ili kiweze kutoa huduma katika kipindi chote cha mwaka. Vilevile katika mwaka 2016/2017, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imetenga shilingi milioni 350 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio na maegesho ya ndege.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:- Mkoa wa Kilimanjaro una tatizo la uhaba wa magari ya zimamoto; gari linalofanya kazi mpaka sasa ni moja tu, hivyo kufanya huduma ya zimamoto kuwa duni sana.
(a) Je, ni lini Serikali itaongeza magari mengine mawili ili kusaidia shughuli za zimamoto na kuepusha hasara zinazowakabili wananchi wanaopata majanga ya moto?
(b) Je, Serikali haioni kwamba uamuzi wa kuhamishia Kitengo cha Zimamoto Wizara ya Mambo ya Ndani umeiongezea mzigo Wizara hiyo na kupunguza ufanisi wa shughuli za zimamoto?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mkoa wa Kilimanjaro una gari moja kubwa la kuzima moto ambalo lina uwezo wa kubeba maji lita 7,000 na dawa za kuzimia moto wa mafuta lita 400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa sasa kuna magari mawili madogo ya kuzimia moto yasiyo na matanki ya kubeba maji na madawa. Pamoja na magari haya, hufanya kazi kwa kupata maji kutoka gari lingine au kutoka katika vituo maalum vya maji ya kuzimia moto (fire hydrant). Hata hivyo, kwa sasa ni gari moja tu linalofanya kazi na lingine linahitaji matengenezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kununua magari ya zimamoto na uokoaji kwa ajili ya Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa mingine. Katika kutekeleza mpango huo, Serikali inafanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za nje ya nchi ambazo zimeonyesha nia ya
kutukopesha fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya zimamoto pamoja na uokoaji na mazungumzo yatakapokamilika mkataba utasainiwa na kuanza utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhamishwa kwa Kitengo cha Zimamoto kutoka katika mamlaka mbalimbali na kuwekwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kulifanyika baada ya tathmini hususan ya utendaji kazi za kila siku, ambapo ilibainika kuwa utendaji kazi wa Vikosi vya Zimamoto
katika Halmashauri ulikuwa dhaifu kutokana na vikosi hivyo kuwa chini ya Wahandisi wa Majiji, Manispaa na Miji ambapo hawakuwa na utaalam wa masuala ya Zimamoto na Uokoaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ilibainika pia kuwa vikosi vikiwa chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vihamishiwe Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuleta ufanisi zaidi wa kazi na viwe chini ya kamandi moja ili viweze kupokea amri kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba uamuzi huo uliongeza ufanisi na siyo mzigo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. RAPHAEL J. MICHAEL) aliuliza:-
Hospitali ya KCMC inamilikiwa na taasisi ya kidini ikishirikiana na Serikali na imekuwa ikitoa huduma bora zinazofanya wagonjwa wengi kutoka ndani na nje ya nchi kukimbilia hospitali hiyo hivyo kuifanya hospitali hiyo izidiwe na uwezo wake wa kuhudumia wagonjwa hususani miundombinu na samani za hospitali.
(a) Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuisaidia hospitali hiyo ili iweze kutoa huduma bora zaidi kulingana na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaokwenda kutibiwa hapo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiasi cha pesa inachopeleka katika hospitali hiyo na kuhakikisha kuwa kile kiwango kilichotengwa kwa sasa kinapelekwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaipa uzito mkubwa Hospitali ya KCMC na inaipongeza kwa huduma bora za afya inazozitoa kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na wengine kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, Wizara inafanya jitihada za makusudi za kuiwezesha Hospitali hii kuendelea kutoa huduma bora, ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ilitenga kiasi cha shilingi 12,202,942,000 kwa ajili ya hospitali hii. Kati ya fedh hizo, shilingi 11,275,224,000 zilikuwa nikwa ajili ya Mishahara ya watumishi, na shilingi 427,718,000 zilikuwa kwa ajili ya matumizi mengineyo (Other Charges) na kiasi cha shilingi 500,000,000 zilikuwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwenye wodi ya dharura kupitia bajeti ya Miradi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ili kuzipunguzia mzigo wa wagonjwa hospitali za rufaa za Kanda ikiwemo KCMC Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaboresha huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, hospitali za Wilaya pamoja na vituo vya afya na zahanati ili kupeleka huduma bora karibu zaidi na wananchi ili wale wachache tu wenye kuhitaji huduma za rufaa basi wafike katika Hospitali za Rufaa za Kanda, hospitali maalum pamoja na hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mheshimiwa Spika, ili kuziwezesha hospitali na taasisi nyingine zote zilizo chini ya Wizara kujiendesha kiuendelevu, Wizara inatekeleza mkakati wa kuhakikisha hospitali na taasisi zote zilizo chini yake zinafunga na kutumia mifumo ya kielektroniki ili hospitali hizo ziweze kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma. Vilevile katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Wizara imetenga kiasi cha shilingi 11,004,329,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo na mishahara, lakini pia shilingi 500,000,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-
Gereza la Karanga ni chakavu na lina uhaba wa samani:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kulikarabati gereza hilo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za kutosha za uendeshaji ili kununua samani pamoja na vifaa vingine vitakavyosaidia kutoa huduma kwa wafungwa na mahabusu gerezani hapo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba Gereza la Karanga linakabiliwa na uchakavu wa miundombinu na hali hiyo imetokana na majengo na miundombinu ya gereza hilo kuwa ya tangu mwaka 1949 likiwa na uwezo wa kuhifadhi wahalifu 814 na wahalifu waliopo sasa ni takriban 1,200. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatekeleza mpango wa muda mrefu wa kuyaboresha majengo hayo kwa kuyafanyia ukarabati mkubwa unaolenga kuyaimarisha na kuyaboresha pamoja na kuyafanyia upanuzi.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mpango wa kupeleka fedha za maendeleo kwa ajili ya ukarabati na ununuzi wa samani katika magereza yote nchini likiwemo Gereza la Karanga. Aidha, kutokana na ufinyu wa bajeti, fedha hizo zimekuwa zikitolewa kwa awamu katika magereza mbalimbali nchini.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-
Je, Serikali imejipanga vipi kumaliza madai ya msingi na ya muda mrefu kwa waongoza watalii, wapagazi na wapishi kutambuliwa kwa kima cha chini cha mishahara, mikataba ya kazi inayoendana na kazi zao, malipo ya posho kwa huduma wanazotoa kwa siku, sera shirikishi katika kutatua matatizo yao na utalii wa nchi kwa ujumla na malipo ya huduma za jamii kama vile afya na majanga?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MAJIBU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya wapagazi, wapishi na waongoza watalii yameshughulikiwa na Wizara kwa kushirikiana na Vyama vya Tanzania Association of Tour Operators (TATO); Kilimanjaro Association of Tour Operation (KIATO); Tanzania Tour Guides Association (TTGA); Kilimanjaro Guides Association (KGA); Tanzania Porters Organization (TPO); Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi Ajira, Vijana na Ulemavu) na Vyama vya Wapagazi na Wapishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkutano uliofanyika Arusha tarehe 12 Desemba, 2015 Wizara na wadau walikubaliana kuhusu viwango vya chini vya ujira kwa wapagazi wapishi na waongoza watalii. Viwango vinavyopendekezwa kwa siku ni shilingi sawa na dola za Marekani 10 kwa wapagazi 15; kwa wapishi na 20 kwa waongoza watalii kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika makubaliano hayo, Serikali ilisisitiza juu ya umuhimu wa kuingia mikataba ya kazi baina ya waajiri na waajiriwa. Serikali ilitoa miongozo ya mikataba ili izingatiwe kwa mujibu wa matakwa ya kila kundi na ilianza kutumika katika Sekta ya Utalii. Waajiri na wajiriwa wanatakiwa kisheria kutekeleza wajibu wao wa kusaini mikataba na kuzingatia viwango vilivyokubaliwa. Endapo makubaliano yao hayatazingatiwa, ni wajibu wa waajiriwa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kima cha chini cha mishahara na malipo ya posho kwa huduma za jamii kama vile afya na majanga, Serikali inaendelea kuhimiza kuwa waajiri wazingatie kima cha chini cha mishahara kilichotolewa na Serikali na michango inayopaswa kutolewa kwenye mifuko mbalimbali kama vile Shirika la Taifa la Hifadhi wa Jamii (NSSF), Bima ya Afya na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-
Mheshimiwa Rais katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 aliahidi kujenga kilometa 10 za barabara ya lami katika Manispaa ya Moshi.
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kusaidia Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kujenga mitaro katika barabara zake za lami ili kuzifanya zidumu muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napensa kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli, barabara zenye urefu wa kilometa 16.57 zimejengwa katika Manispaa ya Moshi kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Machi, 2018 ambapo kati ya hizo kilometa 6.06 zimejengwa kupitia fedha za Mfuko wa Barabara kwa gharama ya shilingi 2,076,497,094 na kilometa 10.51 zimejengwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Kuimarisha Miji 18 (ULGSP) kwa gharama ya shilingi 8,384,872,640.87. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri inaendelea na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 2.79 kwa kiwango cha lami kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara unaotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi 1,178,201,860.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mradi wa Kuimarisha Miji 18 (ULGSP) katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2018 Serikali imejenga mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 11.57 kwa gharama ya shilingi 1,833,520,330. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kujenga mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 9.47 na mradi huu utagharimu jumla ya shilingi 1,612,952,130 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara, ujenzi huu upo katika hatua za awali.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi haina Hospitali ya Wilaya na kuifanya Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi izidiwe na idadi ya wagonjwa:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili kujenga Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Moshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha taratibu za kukabidhi majengo na ardhi ya Kituo cha Afya Moshi Arusha kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ili kipanuliwe na kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Halmashauri. Baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu inayohitajika kwa hadhi ya Hospitali ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa sasa wananchi wa Manispaa ya Moshi wanapata huduma katika Hospitali Teule ya Mtakatifu Joseph ambayo inafuata miongozo ya Serikali kwa kutoa matibabu bure kwa wazee, watoto chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa muda mrefu imekuwa na maombi ya kupandishwa hadhi kwa Zahanati za Msarango, Longuo B na Shirimatunda kuwa Vituo vya Afya:-

Je, ni lini Zahanati hizo zitapandishwa hadhi kuwa Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Moshi ina jumla ya Zahanati 31, 12 za Serikali, tatu za Mashirika ya Dini na 16 binafsi. Vituo vya Afya viko 10. Viwili vya Serikali, kimoja cha Shirika la Dini na saba ni vya watu binafsi; na Hospitali nne zote za Mashirika ya Dini ambapo Serikali imeingia mkataba na Hospitali ya St. Joseph kuwa hospitali teule kwa maana ya CDH.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mwongozo wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) Kituo cha Afya kinapaswa kuhudumia wakazi kati ya 10,000 hadi 60,000. Zahanati inapaswa kuhudumia wakazi wasiozidi 10,000 na hospitali ina wakazi kuanzia 50,000 na kuendelea. Zahanati ya Msarango inahudumia wakazi 7,699, Longuo B wakazi 6,632 na Shirimatunda wakazi 4,485, hivyo, zinakosa sifa ya kupandishwa hadhi kuwa vituo vya afya.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inasisitiza kujenga Vituo vya Afya vipya badala ya kuhuisha Zanahati izopo ili kuendana na ubora wa miundombinu inayohitajika na pia kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya na siyo kupunguza zahanati zilizopo ili kuongeza Vituo vya Afya.