Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe (4 total)

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:-
Miradi ya REA I na II katika Wilaya ya Mwanga haikukamilika na fedha zilizokuwa zimepangwa hazikutumika:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia umeme wananchi waliopitiwa na umeme huo bila kufungiwa?
(b) Je, Awamu ya III ya REA iliyozinduliwa Mwanga, mwezi Septemba, 2017 itaanza kutekelezwa lini?
elezaji wa REA Awamu ya I na II Wilaya ya Mwanga
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:-
Miradi ya REA I na II katika Wilaya ya Mwanga haikukamilika na fedha zilizokuwa zimepangwa hazikutumika:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia umeme wananchi waliopitiwa na umeme huo bila kufungiwa?
(b) Je, Awamu ya III ya REA iliyozinduliwa Mwanga, mwezi Septemba, 2017 itaanza kutekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Jumanne Abdallah Maghembe, Mbunge wa Mwanga, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vijiji 38 kati ya vijiji 44 vya Wilaya ya Mwanga vilipata umeme kupitia Awamu ya II ya Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini ambapo wateja zaidi ya 2,241 waliunganishiwa umeme. Aidha, vijiji sita vilivyosalia havikuweza kupatiwa umeme kutokana na Mkandarasi, Kampuni ya SPENCON, aliyekuwa anafanya kazi hiyo kushindwa kukamilisha kazi hiyo na mkataba wake kusitishwa mwezi Disemba, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imempata Mkandarasi Kampuni ya M/S Octopus Engineering Limited atakayeikamilisha kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vilivyosalia kwa awamu ya pili. Kazi hizo zimeanza rasmi mwezi Januari, 2018 na zitakamilika ndani ya miezi sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu katika Wilaya ya Mwanga ulianza mwezi Oktoba, 2017 chini ya Mkandarasi Kampuni ya Urban and Rural Engineering Services Limited. Kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 10.98; njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 urefu wa kilometa 24; ufungaji wa transformer 12 za kVA 50; pamoja na kuunganisha wateja wa awali 347. Gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 1.7 na shilingi bilioni 12.3; mradi huu utakamilika mwezi Juni, 2021.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:-

Awamu ya III ya REA ilizinduliwa Wilayani Mwanga mnamo Julai, 2017 lakini hadi sasa utekelezaji wake haujaanza;

Je ni lini utekelezaji wa mradi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Jumanne Abdallah Maghembe, Mbunge wa Mwanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini katika Wilaya ya Mwanga kupitia REA awamu ya tatu ulianza mwezi Oktoba, 2017 ukifanywa na Mkandarasi Kampuni ya Urban and Rural Engineering Service Limited. Katika mzunguzuko wa kwanza vijiji 14 vya Wilaya ya Mwanga vitapatiwa umeme vikiwemo Vijiji vya Ndorwe, Kinghare, Kigoningoni, Kiriche, Mangulai, Kirya, Lungurumo, Mangara, Kiverenge, Kichwa, Chang’ombe, Vuchama Ngofi na Ngujini.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme katika Vijiji vya Wilaya ya Mwanga inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 10.98, njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 24, ufungaji wa transfoma 12 za KVA 50 pamoja na kuwaunganisha wateja wa awali 347. Kwa sasa mkandarasi anaendelea na kazi za awali ikiwemo uchimbaji wa mashimo na kusimika nguzo katika Kata ya Kirya. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo itakamilika mwezi Juni, 2019. Gharama ya mradi ni Sh.1,350,000,000.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:-

Kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa Shule za Msingi Wilayani Mwanga:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu 384 wanaohitajika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Jumanne Abdallah Maghembe, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna changamoto ya upungufu wa walimu wa shule za msingi nchini, na Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ina jumla ya shule za msingi 110, za Serikali zenye jumla ya walimu 590, hadi kufikia Novemba, 2018 kulikuwa na upungufu wa walimu 384.

Mheshimiwa Spika, Mwezi Aprili, mwaka 2019, Serikali imeajiri walimu 4,549 wa shule za msingi na sekondari ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Halmashauri ya Mwanga, na kati ya walimu hao 3,089 ni kwa shule za msingi na walimu1,460 ni shule za sekondari. Walimu hawa wameshapangwa katika halmashauri mbalimbali nchini na walipaswa kulipoti kuanzia jana mpaka tarehe 21 na wale ambao hawataripoti, nafasi zao zitapewa watu wengine ambao wana uhitaji kama huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri ya Mwanga imepelekewa walimu 21 wa shule za msingi nawalimu watano wa shule za sekondari. Serikali itaendelea kuajiri walimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:-

Serikali inafanya juhudi katika kuendeleza elimu hapa nchini kwa kutoa elimu bure na hata kujenga Shule nyingi zikiwemo za kata.

Je, lini sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha Maabara za Sayansi katika Shule zote za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMIESEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Jumanne Abdallah Maghembe, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi katika shule za sekondari kwa kushirikisha wananchi na wadau wa maendeleo wa ndani na nje. Katika mwaka wa fedha 2019/ 2020, Serikali imetenga kiasi cha jumla shilingi bilioni 107.1 zikiwemo shilingi bilioni 58.2 kupitia mpango wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) na shilingi bilioni 48.9 kupitia mgango wa kuboresha shule za sekondari (SEQUIP) ambapo sehemu ya fedha hizo zitatumika kukamilisha ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kwa shule za sekondari za kata nchini. Ahsante.