Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joseph Roman Selasini (4 total)

MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:-
Kumekuwa na usumbufu na uharibifu unaosababishwa na ongezeko la nyani ambao wanavamia mashamba ya wananchi na kula mazao kama mahindi, ndizi na sasa wanaingia katika majumba ya watu na kubeba chakula katika Kata za Ushiiri, Mrao – Keryo, Kirua – Kei, Katangera – Mrere, Kirongo – Samanga na Olele.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapunguza au kuwahamisha nyani kwenye maeneo hayo?
(b) Je, kuna utaratibu gani wa kuwafidia wananchi hasara waliyoipata kutokana na uharibifu wa nyani hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge wa Rombo, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii inatambua uwepo wa tatizo la wanyamapori wasumbufu na waharibifu ambao wanaharibu mazao katika kata zilizotajwa ambazo zinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro. Wizara kupitia Taasisi yake ya TAWIRI imepanga kuendesha zoezi la utafiti wa wanyamapori aina ya nyani, ngedere na kima katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2017 ili kubaini idadi na mienendo yao na kuwianisha na shughuli za kilimo zinazofanyiwa na wananchi katika maeneo ya vijiji vya kata zilizotajwa. Kwa sasa Wizara imeandaa utaratibu wa kushirikisha jamii husika katika kulinda mazao yao kwa kutumia mbinu mbalimbali za kitaalam na za kijadi, hatua ambayo itatekelezwa kuanzia mwezi Oktoba 2017 kwa Wizara kuwashauri wananchi kuanzisha vikundi, kuendesha mafunzo na kuwapatia silaha za jadi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kufidia hasara, kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kufidia mazao yaliyoharibiwa au kuliwa na wanyamapori na badala yake Kanuni za Dangerous Animals Damage Consolation za mwaka 2011 chini ya Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 zinaelekeza ulipaji wa kifuta jasho. Hata hivyo, katika kanuni hizo, jamii ya nyani siyo miongoni mwa wanyama wanaotambulika kisheria katika ulipaji wa kifuta jasho. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:-
Wananchi wa Kata za Mahinda, Ngoyoni, Mengwe na Kirongo – Samanga walifanya uamuzi wa kujenga vituo vya polisi kwa nguvu zao na vituo hivyo vimefikia hatua mbalimbali za ujenzi, lakini kutokana na kuwepo na shughuli nyingine zinazohitaji michango ya wananchi kama vile ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na maabara wameshindwa kumalizia vituo hivyo.
Je, Serikali iko tayari kuchukua hatua za kumalizia ujenzi wa vituo hivyo njia ya kuwatia moyo wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge wa Rombo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kupongeza sana juhudi za wananchi wa Mahida, Ngoyoni, Mengwe na Korongo kwa uamuzi wao wa kujenga vituo vya polisi kwa nguvu zao wenyewe. Kutokana na ujenzi wa vituo hivyo kuwa katika hatua mbalimbali. Serikali kupitia jeshi la polisi itafanya ukaguzi wa vituo hivyo ili kupata tathmini ya gharama zitakazohitajika katika kukamilisha ujenzi huo. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:-
Wapo wananchi wengi waliotuhumiwa na kushtakiwa katika Mahakama tofauti na kutozwa faini na baada ya kulipa faini hizo wakakata rufaa Mahakama za juu kulalamikia hukumu hizo na Mahakama za juu zikawaona hawana hatia.
(a) Je, Serikali inayo kumbukumbu ya taarifa za wananchi wa namna hiyo?
(b) Na kama Serikali inazo taarifa hizo, je, ni lini wananchi hao watarejeshewa fedha zao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge wa Rombo, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inazo kumbukumbu zote na taarifa za wananchi wanaolipa faini na baadae kushinda rufaa za kesi zao na hivyo kustahili kurejeshewa faini walizotoa kwani mashauri yote na hukumu zinazotolewa kumbukumbu zake zinatunzwa na Mahakama. Urejeshaji wa fedha hutegemea upatikanaji wa nyaraka zinazothibitisha malipo ya faini kupokeleawa na uwepo wa nakala ya hukumu kwani mara nyingi rufaa inaweza kuwa imetolewa baada ya muda mrefu tangu hukumu ya kwanza kutolewa.
Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumiwa na Mahakama ni kuwasilisha hazina nyaraka husika kwa ajili ya uhakiki na uidhinishwaji wa malipo kabla ya fedha zao kurejeshwa tena Mahakamani ili mwananchi husika aweze kulipwa. Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya shilingi 60,152,487.65 zililipwa na Mahakama kama fidia kwa mashauri 16 yaliyohakikiwa na kuthibitishwa na Mahakama baada ya kupokea fedha kutoka Hazina.
Mheshimiwa Spika, madai 24 yenye jumla ya shilingi 87,046,649.38 yameshachambuliwa na kuwasilishwa Hazina na tayari yanasubiri malipo na wakati huo huo jumla ya madai 12 yenye thamani ya shilingi 6,920,000 miongoni mwao yakiwemo madai mapya yamewasilishwa Hazina. Mara uhakiki utakapotengamaa na Mahakama kupokea fedha kutoka Hazina malipo hayo yatafanyika bila kuchelewa.
Mheshimiwa Spika, kama kuna mtu yeyote ambaye amecheleweshewa malipo yake nashauri awasiliane na Wizara au Mahakama ili kutatua tatizo hilo.
MHE. SAED A. KUBENEA (K.n.y. MHE. JOSEPH R. SELASINI) aliuliza:-
Vipo vyanzo vya maji kutoka Mlima Kilimanjaro ambavyo vinasemekana vinapeleka maji nchini Kenya kupitia msitu wa Rongai:-
Je, Serikali haioni sababu za kudhibiti vyanzo hivyo ili kuhakikisha kwamba maji hayo yanatumika katika Halmashauri ya Rombo badala ya kwenda nchi jirani ya Kenya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Raman Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ipo miradi ya maji kwa upande wa Kenya inayotumia vyanzo vya maji vilivyopo katika msitu wa Rongai ambapo kuna mito na chemchem 14 inayopeleka maji Loitokitok nchini Kenya. Maji hayo yanachukuliwa kwa vibali vya Bonde la Mto Pangani. Kijiografia wananchi wa Loitokitok hawana sehemu nyingine jirani ambayo wangeweza kupata maji. Upelekaji wa maji Mji wa Loitokitok ni wa kihistoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufuatiliaji uliofanywa na wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo umebaini kuwa maji hayo yalianza kuchukuliwa tangu miaka 1960 ambapo ipo miradi ya maji yenye vibali vya mwaka 1960, 1990, 2000 na baada ya 2010. Baada ya ufuatiliaji huo, watumiaji wote wametakiwa kuomba vibali upya kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya 2009. Maji yanayochukuliwa ni kutoka kwenye vyanzo vidogo ambavyo haviwezi kutumika katika mji mdogo wa Tarakea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na vyanzo hivi kuwa na maji kidogo, kuna uwezekano wa kuchepusha ili kuwasaidia wananchi wetu wa mpakani hasa maeneo ambapo mabomba yanapita ili kudumisha ujirani mwema wa pande zote mbili. Kwa sasa Kampuni ya Kiliwater ambayo ndiyo inayotoa huduma ya majisafi Wilayani Rombo imeomba kibali cha kuchukua maji kutoka Mto Naremuru na tayari kibali cha ujenzi kwenye chanzo hicho kimepatikana.