Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph Roman Selasini (66 total)

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na matatizo makubwa ambayo wanayo Walimu na nia ya Serikali kuyatatua ipo kada nyingine ambayo ni kama inasahaulika na hii ni kada ya Wakaguzi wa Elimu. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba kada hii nayo inatazamwa ili kwa pamoja na kwa kushirikiana na walimu waweze kusaidiana katika kuboresha elimu ya watoto wetu katika nchi yetu?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali tayari imeshaanza mkakati wa kuboresha ukaguzi wa shule na sasa hivi hata kuna muundo mpya wa wakaguzi, ambapo hata jina la ukaguzi limebadilishwa, wanaitwa Wathibiti wa Ubora wa Elimu, na yote hii ni katika lengo la kuhakikisha kwamba tunaimarisha zaidi ukaguzi wa shule kwa kuangalia wakaguzi wanavyoweza kufanya kazi zao kwa kufanisi zaidi. Ukaguzi umeimarishwa mpaka katika ngazi za Wilaya, na huu muundo unaendana pia na maslahi bora kwa wakaguzi. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi yanasababishwa na mambo mawili. Jambo la kwanza, ni baadhi ya Askari Polisi kupewa taarifa za matukio na kutokwenda kwenye maeneo ya matukio kwa wakati unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ni wahalifu kupelekwa vituoni na baada ya muda mfupi kuonekana wakirandarada mitaani bila kuchukuliwa hatua stahiki na Jeshi la Polisi. Sasa je, Serikali inawaambia nini Watanzania hasa kutokana na uzembe huu ambao unafanywa na baadhi ya Askari Polisi unaosababisha wananchi kukata tamaa na kujichukulia hatua mikononi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwanza tu kueleza jambo tu kwa kifupi sana kabla sijajibu hili swali. Ni kwamba Jeshi letu la Polisi ni jeshi ambalo linajitahidi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na weledi wa hali ya juu.
Hata hivyo, Jeshi letu la Polisi linakumbana na changamoto mbalimbali, kwanza idadi ya polisi ambao tunao hawatoshelezi, kwani sasa hivi Polisi mmoja anahudumia kati ya watu 300 mpaka 350, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na kiwango cha Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo tumeona malalamiko mengi ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na matatizo mbalimbali yakiwemo makazi, usafiri na kadhalika kutokana na hali ya uchumi wa nchi yetu kwa ujumla wake. Kwa hiyo, mbali ya changamoto hizi nyingi ambazo Jeshi letu la Polisi linakabiliana nazo lakini linajitahidi kadri ya uwezo wake kuweza kufanya kazi zake kwa kuzingatia maadili, weledi pamoja na sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hiyo haiondoshi ukweli kwamba wakati mwingine inatokeza baadhi, kama ilivyo mtu mwingine wa sehemu nyingine yoyote, kwamba baadhi ya polisi wanaweza kuwa na upungufu wa hapa na pale. Kadri hali hiyo inavyojitokeza, hatua madhubuti za kisheria zimekuwa zikichukuliwa. Wapo baadhi ya polisi wamekuwa wakichukuliwa hatua za kisheria kupitia Mahakama za Jeshi la Polisi yenyewe, lakini na wale ambao wameweza kutenda makosa ya jinai vilevile sheria imekuwa ikifuata mkondo wake.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo mbalimbali ambayo yamesemwa na muuliza swali lakini vilevile Askari hawa hasa wastaafu nao wana matatizo yao. Kule kwangu Rombo napofanya mikutano ya uhamasishaji, simalizi kuzunguka Jimbo bila kuona mkono wa Askari mstaafu au aliyepigana Vita vya Kagera au wale waliopigana Vita vya Pili vya Dunia, wakilalamika kutopewa haki zao kikamilifu. Swali langu ni kwamba, je, Wizara ina kauli gani juu ya Askari hawa ambao bado wanaendelea kulalamikia mafao yao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao kwa wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania au kwa majeshi yetu kwa ujumla yapo kwa mujibu wa sheria. Tunavyofahamu sisi ni kwamba Wanajeshi wote wenye stahili za kulipwa pensheni wanalipwa pensheni. Wapo wengine ambao hawakufikisha miaka ishirini ya utumishi, wao wanalipwa kiinua mgongo kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inawezekana hao wanaolalamika ni wale ambao walishalipwa kiinua mgongo lakini kutokana na ugumu wa maisha sasa hivi wamekuwa wakiomba waweze kufikiriwa. Ninachoweza kumueleza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, ni vyema tukapata majina maalum ya hao watu, tukaangalia case zao mmoja baada ya mwingine ili tuweze kuwasaidia kwa kadri itakavyowezekana.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa na kesi nimeshinda…! Kwa hiyo nipo tena kazini kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tofauti na Mbinga, wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kilimanjaro hususani Jimbo la Rombo wanaelekea kukata tamaa, wengi wao wanang‟oa kahawa wakibadilisha na mazao mengine. Tatizo ni kwamba gharama ya uzalishaji wa kahawa ni kubwa sana wakati bei ya kahawa ni ndogo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku katika zao la kahawa ili kuwapa motisha wakulima wa kahawa tena kahawa ile tamu ya Arabica ndiyo inayong‟olewa, ili kahawa isije ikafa katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa miaka ya karibuni zao la kahawa limepata changamoto nyingi sana, hususan bei kwa wakulima wetu. Serikali imechukua hatua kadhaa ili kukabiliana na changamoto hii ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Kahawa (CDTF) ili uweze kusimamia zao la kahawa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatoa pembejeo kwa wakulima kwa bei ambayo ni nafuu.
Mheshimiwa Spika, tayari katika mazao mengine, hususan zao la korosho, tumegundua kwamba kwa kuanzisha Mfuko ni rahisi Mfuko ule kuwasaidia wakulima kupata pembejeo kwa bei ambayo ni nzuri na hivyo basi kuwaondolea gharama ambazo katika mjengeko wa bei zinawafanya wapate bei ambayo siyo nzuri. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, tayari Mfuko huu upo, umeanza kazi na mtaji bado unaendelea kujengwa ili uweze kuwasaidia sasa wakulima wa kahawa waweze kupata bei nzuri.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Miradi mingi sana ya maji imeanzishwa nchini na katika Jimbo langu kuna mradi umeanzishwa katika Kijiji cha Shimbi Mashariki, mwingine umeanzishwa katika Kijiji cha Rea, visima vile 10 na vinahitaji kujengewa miundombinu. Sasa kinachosumbua ni fedha zinasuasua kwenda ili kukamilisha umaliziaji wa miundombinu ili wananchi wapate maji. Nauliza je, ni lini fedha zitakwenda ili miradi hiyo ipate kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikuhakikishie kwamba tumeanza Program ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Pili, fedha zimeanza kutolewa. Natoa wito kwa Wakurugenzi wote kwamba kama wana hati ziko mezani, basi waziwasilishe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji. Fedha tunazo na tayari maeneo mengi fedha tumeshapeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama kazi imeshafanyika, hati zipo, hata kesho alete tutampatia fedha.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa majibu ambayo tumeyapata kwa swali hili, kidogo yana mchanganuo ambao unafaa tofauti na mara ya mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza. Dhiki katika Jeshi la Magereza ni uzembe kwa sababu kwa maoni yangu Jeshi hili ni Jeshi tajiri, Jeshi hili lilikuwa na Gereza la Kilimo Songwe ambalo lilikuwa linafanya kazi vizuri sana, Gereza la Karanga lilikuwa na kiwanda kizuri sana cha viatu, Gereza la Ukonga lilikuwa na kiwanda kizuri sana cha nguo; lakini tender zinatolewa kununua nguo za Magereza na za Polisi, tender zinatolewa kununua viatu vya Polisi na Magereza. Kwa nini, Serikali isiboreshe viwanda vya Jeshi hili, ili Jeshi likafanye biashara na likaweza kutatua matatizo yake pamoja na matatizo ya nyumba na hata kuisaidia Serikali, badala yake inatoa kazi ambazo Jeshi hili linaweza likazifanya kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, nashukuru kwa mchanganuo uliotolewa. Naomba kumuuliza Waziri, kwa kuwa Askari Magereza katika Jimbo langu pale Rombo wanaishi katika nyumba zinazoitia aibu Serikali kwa kweli, wanaishi kwenye mabanzi. Je, Waziri yupo tayari kuandamana na mimi akakague nyumba hizo na kwa sababu hiyo, hizi zilizotengwa 390 angalau chache zianze kujengwa Rombo kwa ajili ya kunusuru makazi ya wale Askari pale Rombo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza limepanga kuongeza uzalishaji wa mapato ya kilimo, ushonaji na ufugaji. Kwa hiyo, msingi wa swali lake kwamba Jeshi la Magereza limezembea siyo sahihi, kuna mipango kabambe tu ya kuhakikisha kwamba Jeshi la Magereza linajitegemea kwa chakula, lakini pia linaendeleza ujuzi na rasilimaliwatu ilizokuwa nazo katika kuhakikisha kwamba linachangia juhudi za Serikali za kuweza kuifanya sekta ya viwanda kuchukua sehemu kubwa katika uchumi wa nchi yetu katika miaka inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia utaratibu huo Jeshi la Magereza limeandaa andiko ambalo linaainisha miradi minane. Uzalishaji wenye matokeo makubwa ya haraka (quick win projects) na limeshawasilishwa Serikalini ili kuweza kupata fedha. Miradi hiyo ambayo ni ya kokoto Msalato; unenepeshaji wa ng‟ombe wa nyama Mbigili na Ubena; uzalishaji wa mafuta ya alizeti Ushora, Kongwa na Msalato; ushonaji wa viatu Ukonga na Karanga Moshi ambako ni kwa Mheshimiwa Selasini. Halafu kuna mradi wa samani ambao uko Arusha; kilimo cha umwagiliaji Idete Morogoro na kuimarisha kikosi cha ujenzi ili kiweze kumudu na kufanya kazi kubwa za ukandarasi.
Pia Jeshi hilo limeandika mpangokazi wa kujitosheleza kwa chakula ambalo pia limeshawasilishwa Serikalini ili kupata fedha za uendeshaji. Kwa hiyo, Jeshi linatekekeza sera ya uwezeshaji kwa kuingia ubia pia na taasisi mbalimbali binafsi kupitia utaratibu wa PPP ili kupata mitaji ya kuongeza uzalishaji. Mpaka sasa Jeshi limeshaingia ubia na kampuni ya Tabin ya Uturuki kwa ajili ya kutekeleza kilimo cha mpunga Gereza la Kigongoni. Pia limeainisha maeneo yenye madini na kupata leseni ya uchimbaji karibu 181, hatua za kutangaza maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji zinafanywa. Hilo nadhani lilikuwa ni swali lake la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ametaka kujua kuhusiana na Kilimanjaro. Kilimanjaro tuna aina mbili, mbali ya ile miradi ambayo nimeizungumza, kuhusiana na huo ujenzi wa nyumba 3,500, lakini pia kuna utaratibu ambao Jeshi la Magereza linaenda nao, kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo husika. Kwa Mkoa wa Kilimanjaro tayari nyumba karibu 38 zimejengwa kupitia mradi huo. Kinachofanyika ni kwamba tunatumia rasilimali za nguvukazi zilizopo jeshini pamoja na ujuzi tulionao kuweza kujenga nyumba hizi kufikia katika level ya kuezeka halafu baadaye kupitia fedha za bajeti tunafanya finishing. Kwa hiyo, kupitia utaratibu huo kwa Mkoa wa Kilimanjaro tumeshajenga nyumba 38.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kuambatana na Mbunge wakati wowote kwa ajili ya kwenda kuhakikisha kwamba tunatembelea miradi hii na mipango mingine ambayo atakuwa nayo Mheshimiwa Mbunge na tutashirikiana kwa pamoja. Tunapenda Wabunge wa aina yake ambao wako tayari katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba wingi wa wafungwa magerezani unakwenda sambamba na wingi wa mahabusu waliopo magerezani. Na mara nyingi ni kwamba baadhi ya mahabusu wanakamatwa kwa kupakaziwa makosa na askari wa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, napenda kuiuliza Serikali, ni hatu zipi ambazo Serikali inazichukua za dhahiri, kukomesha kitendo hiki ambacho kinawatesa wananchi lakini kinaitia Serikali hasara kwa kuwashikilia watu ambao hawana hatia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilikuwa nataka nijaribu kuweka kauli yake sawa ambayo ameizungumza kuhusiana na shutuma dhidi ya Jeshi la Polisi. Amezungumza kana kama kwamba Jeshi la Polisi lote kazi yake ni kubambikia watu kesi, ninachoweza kusema ni kwamba kuna matukio machache ya baadhi ya polisi ambao wamekuwa wakilichafua Jeshi la Polisi, lakini ni wachache mno, ambao Jeshi la Polisi limekuwa likiwachukulia hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, na wote ni mashahidi, juzi wakati wa bajeti kuna hoja ilizungumzwa kuhusiana na yule kijana ambaye alibambikiwa kesi pale gerezani. Ninachotaka kulithibitishia Bunge lako Tukufu mpaka sasa hivi ni kwamba askari waliohusika na jambo lile watatu wameshafukuzwa kazi na bado wanaendelea kuchukuliwa hatua za kijinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo si kweli kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likizembea kwa kuwachukulia hatua askari wachache sana ambao wamekuwa wakifanya matendo haya ambayo yanakinzana kabisa na taratibu za sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kimsingi ni kwamba hayo ambayo ameyazungumza Mheshimiwa Selasini kuhusiana na tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi niliona niyaweke sawa kwa statement hiyo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Hospitali nyingi teule hapa nchini zinamilikiwa na mashirika ya dini na katika mikataba kati ya wamiliki na Serikali, Serikali inasaidia madawa pamoja na wafanyakazi. Hata hivyo, hospitali hizi nyingi zimekuwa chakavu na zimekuwa ni mzigo mkubwa sana kwa hawa wamiliki. Je, Serikali iko tayari kuandaa mpango maalum au wa kurekebisha ile mikataba au wa kuweka fungu maalum la fedha ili kusaidia kuhuisha hizi hospitali ziweze kufanya kazi vizuri zaidi ya kuhudumia wananchi wetu, kwa mfano ile hospitali ya Huruma pale Rombo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Selasini na ni kweli. Katika kazi zetu, sana tunafanya kazi na taasisi mbalimbali hasa katika sekta ya afya, lakini sitaki kutoa commitment hapa isiyokuwa na uhakika, nikijua wazi hapa nimetoka kujibu swali kuhusu Hospitali yetu ya Mukandana kule Rungwe hata ukiangalia changamoto katika miundombinu hizi hospitali za Serikali zenyewe vilevile bado tunatakiwa tuziwekee nguvu, isipokuwa tunathamini mchango wa taasisi hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ni kwamba sehemu ambayo ni ya makubaliano yetu kwa mfano kutoa fedha kwa ajili ya madawa, kwa ajili ya watumishi, lazima kwanza tutekeleze kwa kiwango kinachoridhisha. Naamini tutakapofanya hivi vizuri hata taasisi za dini wataangalia na nguvu zao watafanya jinsi gani ili kuboresha hili suala zima la miundombinu, lakini sitaki kutoa commitment hapa, kusema kwamba kesho na keshokutwa tutafanya hili. Litakuwa ni jambo la uwongo na uwongo siyo jambo jema kama binadamu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Ni ukweli usiopingika kwamba wanawake katika nchi hii ndiyo wanaolisha Taifa hili kwa sababu akina mama wengi wanajishughulisha na kilimo na biashara ndogo ndogo. Ni kweli pia kwamba katika baadhi ya Halmashauri akina mama wengi wananyanyasika sana na biashara zao kwa kutozwa kodi mbalimbali ambazo hazina tija.
Je, ni lini Serikali itatoa tamko kwa Halmashauri zote ikiwepo Halmashauri yangu ya Rombo waache kuwatoza akina mama zile kodi ambazo zinawaletea bugudha na hivyo kushindwa kuendesha biashara zao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika kufanya hili nadhani tunafanya rejea, hata Mheshimiwa Rais alipokuwa akizunguka sehemu mbalimbali alikuwa akisema kwamba akina mama hawa wasinyanyaswe.
Naomba niseme wazi kwamba kutokana na agizo hilo la Mheshimiwa Rais, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaandaa marekebisho ya Sheria ya Serikali za Mitaa inayohusiana na mambo ya Kodi, Sura Namba 290 na hivi sasa ipo katika mchakato wa mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuondoa zile kero mbalimbali siyo za akina mama peke yake bali ni pamoja na walemavu na makundi mbalimbali. Katika mchakato huu tutakwenda kuhakikisha tunaondoa kero hii siyo kwa akina mama na vijana tu, lakini na group la walemavu lazima wawezeshwe na Halmashauri.
Hata hivyo, watakapowezeshwa kitafanyika nini ili mitaji yao iende vizuri, ndiyo hiyo sheria inakuja sasa hivi. Imani yangu ni kwamba Wabunge wote kwa pamoja sheria ile itakapokuja hapa tutashirikiana kuipitisha kwa sababu jambo hili lina maslahi mapana sana kwa wananchi wetu lakini kikubwa zaidi lina maslahi katika uchumi wa nchi yetu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, Jimbo la Rombo kama yalivyo Majimbo mengine tuna shida kubwa sana ya maji, shida yetu hasa inatokana na kampuni ambayo inasambaza maji katika Jimbo letu Kili Water kuwa na ukata mkubwa baada ya GTZ waliokuwa wafadhili wake kujiondoa. Halmashauri tangu awamu iliyopita imeleta maombi katika Wizara ya Maji ili tuweze kuanzishiwa mamlaka kwa sababu mamlaka ina uwezo wa kukopa kuanzisha vyanzo vipya vya maji ili iweze kusimamia vizuri hali ya maji katika Jimbo letu. Hivi majuzi nimemkumbusha Waziri kuhusu hitaji hilo.
Sasa nataka nijue, je, Serikali ni lini watatusaidia kwa kushirikiana na TAMISEMI ili tuweze kuwa na mamlaka ya maji katika Wilaya ya Rombo itakayoweza kusimamia vizuri usambazaji wa maji yaliyopo na kuanzisha vyanzo vipya vya maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwenye Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 miradi ya maji ni shirikishi kati ya Serikali na wananchi, Serikali inajenga wananchi wanaiendesha kwa mfumo wa kutengeneza hizi mamlaka ndogo ndogo na mamlaka kubwa.
Kwa hiyo, zipo taratibu naomba nimhakikishie Mheshimiwa Selasini kwamba tutakwenda kuliangalia ombi lake viability ya Halmashauri yake kuweza kuendesha huo mradi badala ya Kili water. Kwa hiyo, hilo tunalichukua na tutakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niseme kwamba, natambua kazi nzuri inayofanywa na baadhi ya askari polisi, lakini kuna baadhi ya askari polisi ambao katika utekelezaji wa majukumu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema, natambua kazi nzuri ambayo inafanywa na baadhi ya askari polisi, lakini kuna baadhi ya askari polisi ambao katika utekelezaji wa majukumu yao wanatumia nguvu kupita kiasi, wanatoa adhabu za kutweza wakati wa kukamata watuhumiwa, kuwasababishia vilema na wengine kuwasababishia maumivu ambayo ni ya muda mrefu.
Sasa Waziri atuambie ni hatua gani ambazo zinachukuliwa ili kuhakikisha kwamba baadhi ya askari hawa wanachukuliwa hatua au kuondolewa kwenye jeshi ili kuondoa chuki ambazo zinaweza zikajengwa na baadhi ya raia kwa jeshi zima la polisi kutokana na vitendo ambavyo vinafanywa na baadhi ya askari polisi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Selasini kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na askari polisi. Nimezunguka nchi nzima nimewaelezea maaskari polisi kuchukua hatua kufuatana na makosa na kufuatana na rika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano vijana walio chini ya miaka 18 wanapokuwa na makosa madogomadogo waangalie namna ya kuyashughulikia, lakini pia na watu wanapokuwa na makosa ya aina hiyo na ni vijana wadogo wasiwekwe sana mahabusu yaliyo na watu waliokithiri kwenye vitendo vya uovu, mfano, kumweka kijana wa miaka 12 ambaye labda alikuwa yuko kwenye magwangala akakaa sehemu moja na watu ambao wameshazoea kwenye uuaji ni kumwandaa kisaikolijia baadaye kuwa mhalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya nguvu; jambo hili lina dhana tofauti. Nimewaambia maaskari wanapopambana na wahalifu watumie nguvu zote kuhakikisha kwamba tunadhibiti uhalifu. Kwa mfano, watu wamekuja wamevamia na wana silaha, wakavamia kituo; ama watu wamevamia eneo kama maeneo ambayo tumeyaona, nimewaelekeza maaskari watumie nguvu zote walizonazo kuhakikisha kwamba tunadhibiti uhalifu. Kwa hiyo, kwenye hilo la uhalifu, kwa wale wanaokuja kihalifu kwa kweli jeshi la polisi tutatumia nguvu zote kwa sababu hatutaruhusu wahalifu waweze kutamalaki katika eneo la nchi yetu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Kwa miaka mingi sana nchi yetu imekuwa ikihamasisha sana utalii kupitia Mbuga zetu za Wanyama, Mlima wetu na Mapori yetu, lakini nchi ina vivutio vingi sana. Sasa nauliza; je, Wizara ina mpango gani wa kujenga makumbusho ili vizazi vyetu viweze kujionea jinsi Machifu wetu kwa mfano Mirambo, Mkwawa, kule Kilimanjaro, Mshumbue Marialle ambao walifanya vitu vingi na kuna vitu vingi vya asili vinavyoweza kuvutia utalii, kule Kusini, Wilaya ya Kilwa ni Wilaya ya zamani sana elfu moja mia nane na kitu, lakini vivutio vyote hivi havizungumzwi.
Je, Wizara ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inajenga makumbusho ili vivutio hivi viweze kuwa kwa faida ya watoto wetu kwa kujifunza na vilevile kutuingizia fedha kutokana na watalii kutoka nje?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze kwa kuweza kutupa hamasa sisi Serikali, hasa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kuongeza jitihada kwenye Sekta hii ya Utalii. Ni kweli na nipende tu kusisitiza kwamba, majukumu manne makubwa ya Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na utalii wenyewe ni misitu, wanyamapori na malikale.
Makumbusho anayozungumzia Mheshimiwa Mbunge yanaangukia kwenye sehemu ya malikale na imo kwenye sera zetu kwamba tunapaswa kuboresha makumbusho maeneo yote ya kihistoria popote pale yalipo ili tuweze kuyatangaza na kuweza kuwafanya watalii waweze kuyafikia pamoja na kutupatia pesa, lakini pia kuweza kutangaza utamaduni wa Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya kwa sasa tumeanza kuorodhesha katika ngazi ya Wizara, pia hivi karibuni tunasambaza barua kwa Halmashauri za Wilaya zote ili waweze kutuambia kwa sababu wao wanafahamu vizuri maeneo hayo halafu tutakwenda kuyakagua kuona kama yatakidhi vigezo vya kuweza kuyafanya kuwa ni maeneo ya utalii.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana lakini napenda kukuthibitishia kwamba niko sawa sawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kila kabila hapa nchini lina aina fulani ya pombe ya asili ambayo inapendwa. Kule kwetu Rombo viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya pombe za aina mbalimbali viko vingi tu. Niliwahi kuomba hapa Bungeni; ni lini Serikali badala ya kupiga vita viwanda hivi ikatuma wataalam wake wa TBS na TFDA wakafanya ukaguzi na wakapima aina ya pombe ambazo zinapatikana huko; na kwa sababu sasa hivi tunajenga Taifa la viwanda tukawa na viwanda ambavyo vinaweza vika-improve zile pombe za asili kwa faida ya watu wetu na kwa ajili ya kuongeza mapato na ajira ya maeneo husika?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imegawana mikoa yote ya nchi hii katika makundi manane, na nitawaagiza timu itakayokwenda Mkoa wa Kilimanjaro kwenye Jimbo la Rombo kwamba wafuatilie suala hilo namna gani tunaweza kutengeneza viwanda vya kuzalisha ile pombe wanayoipenda wananchi kwa kuzingatia ubora na afya; nitazingatia.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Rombo ni moja kati ya Wilaya ambazo zina tatizo kubwa sana la uhaba wa ardhi hapa nchini. Mwaka 1974 Mwalimu Nyerere aliwachukua baadhi ya vijana kuwatafutia ardhi maeneno ya Mpanda kule Mikese na Tanga kule Kilindi. Vijana wa Rombo wana nguvu na wana tamaa ya kujiajiri katika kilimo. Mheshimiwa Waziri yuko tayari nikimletea vikundi vya vijana wa Rombo ambao wako tayari kujiajiri katika kilimo kuwatafutia ardhi maeneo mengine ya nchi ili na wenyewe waweze kushiriki katika kujitafutia ajira kupitia kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika programu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, moja kati ya mkakati mkubwa ambao tumeuweka ni kuwapeleka vijana katika kilimo cha umwagiliaji na kilimo biashara na katika utekelezaji wa programu hii hatuchagui maeneo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kushirikiana naye kwa wale vijana wa Rombo ambao wako tayari kufanya shughuli za kilimo tukawasaidia wakapata maeneo na sisi kama Serikali tukawa sehemu ya kuwawezesha ili haja yao itimie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunao mpango wa kitaifa wa kilimo kati ya Wizara ya Kilimo na sisi Ofisi ya Waziri Mkuu ambao lengo lake kubwa ni kwenda kuyatumia mashamba makubwa ya Serikali yale ambayo hayatumiki, yamekuwa mapori, kwa kuyatengenezea miundombinu ili vijana wengi sana waende kufanya shughuli za kilimo katika maeneo hayo. Kwa sasa tutaanzia eneo la Mkulazi Morogoro ambapo patajengwa Kiwanda cha Sukari kwa ushirika kati ya NSSF na PPF, maeneo yameshatengwa na hivi karibuni tutakwenda kuyasafisha yale maeneo na baadaye vijana watapewa maeneo hayo yakiwa yameshaboreshwa na miundombinu yake imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, vijana wa Rombo wakiwa tayari anione tu niko tayari kumsaidia.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ni miaka saba sasa nikiwa hapa Bungeni swali hili linapoulizwa majibu ni haya haya, hayajawahi kubadilika hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna changamoto kubwa zaidi kwa hao wenzetu polisi kwa sababu kuwalaza polisi uraiani wakati huohuo ukawatuma kwenda kufanya operesheni ambazo zitapelekea kuwapiga wananchi, ni hatari kwao na kwa familia zao. Ni lini Serikali itafanya mkakati wa makusudi kabisa kuhakikisha kwamba imeleta majibu tofauti na haya ili wananchi wa Rombo waone nyumba za polisi zinajengwa, waone nyumba za askari magereza zinajengwa, badala ya majibu haya ya kisiasa yanatolewa kila mwaka?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niliweke sawa swali la shemeji yangu Mheshimiwa Selasini. Suala la majibu kuwa yanafanana ni kwa sababu kila mwaka pia tunaajiri, kwa hiyo tutatarajia upungufu uendelee kuwepo, hiyo ni mathematically. Suala la jibu kuwa lilelile si kwamba Serikali haifanyi kitu, hivi tunavyoongea ukiangalia Dar es Salaam tu kuna nyumba zaidi ya 300 zinajengwa lakini hazitatosha kwa sababu mwaka jana pia tumeendelea kuajiri na kwa kuwa tunaendelea kuajiri maana yake mahitaji yale yataendelea kuongezeka kadri tunavyoajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu iliyopita mmeona imejenga majengo mengi tu tena ya ghorofa, ndiyo mengine kama haya ya Mara ambayo Mheshimiwa Vedastus ameyaongelea. Mwezi uliopita, Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 10 kwa upande wa magereza na ujenzi unaendelea. Kwa maana hiyo ujenzi utaendelea lakini na mahitaji yataendelea kwa sababu tunaendelea kuajiri, hata mwaka huu tunategemea tuendelee kuajiri kwa sababu bado idadi ya askari ambao wanatakiwa haijatosheleza. Kwa maana hiyo tumelipa uzito unaostahili suala hili lakini hatuwezi kuacha kuongeza vijana kwa sababu hakuna nyumba, tutaendelea kuongeza vijana lakini tutaendelea kujenga nyumba ili vijana waweze kupata nyumba hizo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji inayosimamiwa kitaifa inasuasua katika maeneo mengi, katika Jimbo langu la Rombo kuna miradi miwili, Mradi wa Leto na Mradi wa Shimbi Mashariki ni ya muda mrefu sana na upatikanaji wa fedha umekuwa unasuasua. Katika kipindi hiki ambacho hali ya ukame imekuwa kubwa sana ukanda ambao hii miradi ipo una shida kubwa sana ya maji. Sasa je, Serikali iko tayari kupeleka fedha zote za hii miradi ili ipate kukamilika wananchi wa eneo lote la ukanda wa chini katika
Jimbo la Rombo waweze kunufaika na miradi hii ambayo imechukua muda mrefu sasa kukamilika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza anaelezea kwamba miradi kwenye eneo lake inasuasua, lakini tulishatoa maelekezo na nimetoa muongozo namna gani tutakwenda kutekeleza hii miradi hasa kwenye maeneo ya vijijini kwa maana ya utekelezaji wa Programu
Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tunakamilisha miradi inayoendelea na utaratibu ni kwamba wakandarasi wengi wamesharudi sasa, walikuwa wamesimama kwa sababu ya fedha zilikuwa hazipatikani kwa wakati, lakini sasa wamerudi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na sasa hivi kila mkandarasi aliyerudi akileta certificate tumekuwa tunalipa kwa wakati kwa hiyo, tunataka tupate matokeo ya haraka miradi ikamilike kwa sababu hatuwezi kuleta fedha tu zikae kwenye Halmashauri ya Rombo wakati hakuna kazi inayofanyika. Tunapeleka mahali ambapo kazi inafanyika, ili tupate matokeo ya haraka wananchi wetu waweze kupata maji.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa katika swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kwamba baadhi ya askari polisi wetu wanashindwa kutumia sheria ambayo inawaelekeza namna ya kukamata watuhumiwa na mara nyingi sana polisi wamekuwa wakiwahukumu watuhumiwa kwa kipigo kikali sana kabla hawajawafikisha Mahakamani na wakiwafikisha Mahakamani, Mahakama zinawaona watuhumiwa kwamba hawana hatia. Kama Mahakama ilivyoamua hivi majuzi kwenye kesi ya Bwana Mdude, Nyangari na wenzake huko Mbozi.
Je, Serikali iko tayari kwa Wizara hizi mbili; ya Sheria pamoja na Mambo ya Ndani kupiga marufuku na kuchukua hatua dhahiri na za wazi kwa polisi ambao wanaidhalilisha Serikali kwa kuwaumiza raia kwa kipigo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Selasini, naye ana heshima ya kuwa mdogo wangu kwa sababu Lamwai ni kaka yetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu wa Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara na Mambo ya Ndani kukaa chini na kuyapitia mambo hayo. Moja ya msisitizo ambao umekuwepo katika Wizara hizi mbili ni kuendelea kuwapa polisi mafunzo ya juu ya haki za binadamu, lakini pia jinsi ya kutumia mamlaka waliyonayo ya kukamata watu na kuzuia uhalifu kwa namna ambayo inaheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaheshimu Sheria ya Kuanzisha Jeshi la Polisi na inaheshimu sheria zilizowekwa. Kwa hiyo, tutakaa na kulijadili.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, kuna zoezi linaendelea katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Kata za Kitendeni, Tarakea, Reha na Nanjara katika Jimbo la Rombo. Nyumba za wananchi zinawekwa ‘X’ na wameamriwa kuzivunja. Sababu wanayopewa ni kwamba wanataka kuhakiki mpaka wa Kenya na Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nyumba hizi na wananchi hawa wameishi katika maeneo hayo kabla hata ya uhuru. Sasa naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, uko tayari kusimamisha zoezi hili ili wananchi wale wa Kikerelwa, Nayeme na maeneo mengine wapewe maelezo ya kutosha kuhusu zoezi hilo na labda pengine uko tayari tuongozane wewe na mimi kwa ajili ya kwenda kuwapa hawa wananchi maelezo ya kuridhisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunilinda.(Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ni kweli zoezi la uhakiki katika mipaka yetu linaendelea, lakini naomba tukumbuke kwamba usalama wa nchi yetu hii tusipouangalia sisi wenyewe tunaweza tukajikuta tunaiingiza nchi katika matatizo. Kwa sababu wananchi wanapokuwa wanaingiliana katika yale maeneo ndipo hapo hapo uharifu unakuwa ni mkubwa zaidi, huwezi kujua ni nani amefanya zoezi hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kuhakiki mpaka tunakwenda sambamba na ile eneo ambalo ni no man’s land lazima libaki wazi, lakini pia ile buffer zone inayotakiwa kuwepo pale lazima hatua zinazotakiwa zionekane kubaki. Kwa hiyo, lazima tu katika lile eneo pawe wazi ili kuweza kutambua na kuainisha mipaka ilivyo na ile no man’s land imekaa namna gani. Na hili tatizo pia lipo hata upande wa Tunduma, Uganda na Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niwaombe tu kamba tunapofanya zoezi hili kama kuna mtu ambaye amevunjiwa tofauti na utaratibu pengine hakustahili kuvunjiwa hilo ndilo tunaloweza tukalisikiliza. Kwa wale waliojenga kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kujengwa yanatakiwa yabaki wazi zoezi litaendelea kwa sababu ya kuangalia usalama wa nchi yetu ili tuweze kuudhibiti uingiaji holela katika maeneo. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mimi ni muumini wa msemo unaosema kwamba mbwa mzee hafundishwi Sheria. Baadhi ya vijana hatutaweza kuwafundisha uzalendo kwa kwenda tu JKT. Enzi za mwalimu kulikuwa na program za kwata mashuleni, tulikuwa tunafundishwa kwata kwa kutumia Bunduki za mbao. Pia kulikuwa na elimu ya kujitegemea ambapo vijana walikuwa wanafundishwa uzalishaji na stadi mbalimbali ambazo zinafundishwa sasa kwenye VETA. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na Wizara ya Elimu, kwata ikarejeshwa mashuleni, vijana wakafundishwa ukakamavu kuanzia ngazi za chini na wakati huo huo elimu ya kujitegemea ikarejeshwa mashuleni kama zamani? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni wazo zuri, wanafunzi kufundishwa mapema masuala ya kijeshi pamoja na elimu ya kujitegemea ni wazo zuri. Hata hivyo, kama nilivyosema tupo katika mchakato wa kuunda kikosi ambacho kitapitia changamoto zote; na kwa sababu kitajumuisha pia watu wa Wizara ya Elimu suala hili litazingatiwa ili tuone uwezekano wake.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Vijana wengi wanaotumia shisha, bangi, madawa ya kulevya na pombe kali kali hizi, wanatumia kutokana na kukata tamaa katika maisha; nami siamini sana katika kutunga sheria, kuwakamata na kuwaadhibu. Mfano mzuri, juzi Waziri Mkuu Serikali ilipiga marufuku utumiaji wa viroba, lakini sasa kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri kilevi kingine kimeanzishwa. Sasa vijana wanaanza kuvuta gundi kitu ambacho ni kibaya zaidi. (Makofi)
Sasa Je, sisi kama Taifa, Serikali kuna utaratibu gani wa kuwasaidia vijana hawa ambao wengi wamekata tamaa ili waweze kupata matumaini katika maisha na waache mambo hya bila lazima ya kutunga sheria au kuwakamata?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti nimshukuru sana Mheshimiwa Selasini kwa swali lake la nyongeza. Kubwa ambalo tunalifanya sasa hivi ili kuwaepusha vijana wa Kitanzania na matumizi ya tumbaku na vileo ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia Luninga na redio, lakini pia tumechapisha vijarida mbalimbali ili kuonesha madhara ya tumbaku pamoja na matumizi ya pombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, wale ambao walikuwa tayari wanatumia kwa mfano, madawa ya kulevya, tumeanza mpango wa kuongeza vituo vya kutoa dawa (Methodone). Kwa hiyo, siyo tu Dar es Salaam lakini tutaanzisha Mbeya, Arusha, Tanga, Kilimanjaro pamoja na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kubwa ni kwamba leo ni siku ya familia, kwa hiyo, tunatoa wito kwa wazazi, walezi kutimiza wajibu wao wa msingi wa malezi bora kwa watoto wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa sababu nimepata pia fursa ya kusema leo ni Siku ya Familia Duniani. Kwa hiyo, familia bora ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yoyote. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Takataka zinaweza zikasababisha uchumi mkubwa sana kwa wananchi wetu kwa sababu taka zinaweza zikatengeneza matofali, zinaweza zikazalisha umeme, zinaweza zikatengeneza mbolea nzuri sana na sasa hivi kwa sababu maeneo ya kutupa taka yanaendelea kupungua mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali isifanye uamuzi wa makusudi, kabisa ikaleta hii teknolojia nchini, ikaanza na majiji yetu ili kuwafanya wananchi wakapata kipato kwa kukusanya takataka na kuzipeleka kwenye maeneo hayo ambayo yanaweza yakazi-process na kuzalisha vitu vingine kwa faida ya Taifa kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Selasini jambo lako ni zuri sana, ndiyo maana katika ofisi yetu tuna mradi mmoja unaitwa Strategic City Project, katika miji mbalimbali tumetenga utaratibu wa kutengeneza haya madampo ya kisasa, ambapo ukienda Mbeya utayakuta, hapa Dodoma tunajenga na maeneo mbalimbali tunatengeneza madampo kama yale. Lengo letu kubwa ni kwamba taka zitakazozolewa baadaye ziingizwe katika system maalum kuweza ku-convert katika shughuli zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sasa hivi tunakaribisha wawekezaji mbalimbali ambao katika njia moja au nyingine watasaidia ukusanyaji wa hizi taka kuweka katika malighafi nyingine, ikiwemo suala zima la utengenezaji wa mkaa.
Kwa hiyo, ni hilo ni jambo zuri Serikali na wadau mbalimbali tushirikiane kwa mustakabali wa nchi yetu ambao mwisho wa siku taka hizi baada ya kuwa uchafu inaweza ikawa malighafi na zitasaidia kujenga uchumi katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na kusubiri mapitio ya huo mkataba, lakini hapa nchini pana vikundi mbalimbali vya watu vinawakusanya watoto wetu wa nchi hii kwa minajili ya kuwatafutia kazi za ndani nchi za nje. Habari tulizonazo ni kwamba baadhi ya hawa watoto wamekuwa wakinyanyasika, wakiteswa na hata kuuawa. Je, ni hatua zipi za wazi ambazo Serikali inazichukua kwa ajili ya kudhibiti vikundi hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge hapa alikuwa anazungumzia wale mawakala wa ajira ambao kwa namna moja ama nyingine, yamekuwepo malalamiko mengi sana ya kuwapeleka mabinti zetu katika nchi hasa za Uarabuni kwenda kufanya kazi za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alishatoa agizo na tangazo la kwamba wale wote ambao wanakwenda kufanya kazi nje ya nchi wapitie mfumo ambao upo katika Wizara yetu kupitia Wakala wa Ajira wa Serikali ambaye ni TAESA. Sasa tukibaini kwamba wako watu ambao wanafanya kazi hii kinyume na taratibu, sheria zetu ziko wazi, huwa tunawafutia usajili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tumekuwa tukiwachukulia hatua kuhakikisha kwamba hawapati tena registration ili tuhakikishe kwamba nguvu kazi yetu hii wakienda kufanya kazi nje ya nchi tuwe tumewalinda kwa maana ya haki zao za kimsingi, tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo wako baadhi ya Watanzania ambao hawapitii katika Ofisi yetu na wakienda nje ya nchi wakipata manyanyaso tunakuwa hatuna taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata Balozi zetu zimeweka utaratibu mzuri; ile mikataba inayotolewa pale, mwajiri yeyote wa nje ya nchi ambaye anamtaka mfanyakazi wa Tanzania lazima apitie katika Ubalozi na Ubalozi unawasiliana nasi kwa ajili ya kuandaa mikataba ili tumlinde na tulinde haki za mfanyakazi wa Kitanzania.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nauliza swali hili nadhani ni mara ya saba tangu nimekuwa hapa Bungeni. Makampuni ya simu ya nchi jirani kwa mfano MTN ya Zambia na Safaricom ya Kenya yana nguvu kiasi kwamba ukiwa Tunduma huwezi kupata mitandao kutoka kwenye makampuni ya hapa kwetu na ukiwa kule Rombo karibu nusu ya eneo la Rombo Safaricom ndiyo inayosikika na mbaya zaidi hata Redio yetu ya Taifa haisikiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inaonekana kama wananchi wa mipakani tumetengwa fulani hivi na huduma hizi za simu pamoja na Redio ya Taifa. Naomba hii iwe mara ya mwisho, ni lini Serikali itarekebisha tatizo hili ili kutoingiza wananchi wanaokaa mipakani kwenye roaming facility na hivyo kuibiwa muda wao wa maongezi bila wao wenyewe kutaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya Habari mtakumbuka kwamba tuliongelea sana uimarishaji wa TBC. Tatizo ni kwamba mitambo yetu hatujaifikisha katika maeneo ya mipakani kwa kiwango cha kutosha. Tukishaifikisha mitambo yetu katika maeneo ya mipakani frequency haziwezi kuingiliana, uki-tune TBC utapata TBC, ingawa bado ukitaka ku-tune ya upande wa pili nayo utaisikia kwa sababu wenyewe watakuwa wapo kwenye frequency tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutahakikisha tunaimarisha ile miundombinu ya TBC ili isikike vizuri maeneo yote ya mipakani. Vilevile wenzetu wanaotoa huduma za mawasiliano ya simu na internet nao wakiimarisha huduma zao tatizo hili litakwisha. Kwa hiyo, tupo katika mazingira hayo ya kuimarisha na nadhani atakumbuka tulichokubaliana au tulichopitisha kwenye bajeti ile ya Wizara ya Habari. Ahsanteni sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Katika nchi yetu ajali za barabarani zimekuwa nyingi sana na moja kati ya sababu za ajili hizi ni matairi ya mitumba yanayoagizwa kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme Tanzania ni nchi pekee ambayo inaagiza matairi ya mitumba ikijua kabisa kwamba matairi haya yanakuwa yamemaliza muda wake na inaweza ikawa kisababishi kikubwa cha ajali. Sasa wakati tukisubiri kiwanda hiki kufufuliwa, hadithi ambayo imekuwa ni ya miaka mingi, je, Serikali ina mpango gani wa kupiga marufuku uingizaji wa matairi yaliyotumika katika nchi ambayo yanasababisha ajali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ajali za barabarani zimeendelea kuongezeka nchini na inawezekana kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba matairi yasiyo na ubora ni moja kati ya visababishi. Kimsingi suala la ajali za barabarani ni suala ambalo Serikali linalichukulia kwa uzito sana, ni kero kubwa inaondoa maisha ya wananchi wetu. Kwa hiyo, Serikali inaangalia ni namna gani ya kudhibiti ajali hizo ikiwa ni kuangalia visababishi kama hilo la matairi, kwa sababu kuna visababishi vingine mfano uendeshaji usiozingatia utaratibu, uendeshaji kupita speed inayotakiwa, lakini vilevile madereva kulewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Serikali inaangalia suala la ajali katika ujumla wake na visababishi vile itahakikisha inavifanyia kazi ili tuendelee kupunguza ajali barabarani. Kwa hiyo, kama hilo la matairi ni moja ya visababishi kwa vyovyote vile Serikali inalifanyia kazi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Waswahili wana msemo kwamba ukitaka kujua utamu wa ngoma uingie ucheze. Tatizo hili ni kubwa sana na binafsi nilikwishaongea na Naibu Waziri akawa ameniahidi atanipelekea mtaalam kutoka Arusha, hili siyo tatizo la mwaka huu nashangaa jibu linasema kwamba wanaanza kufanya utafiti. Wale wanyama wanaendelea kuzaliana, wanaendelea kuleta usumbufu, sasa hivi wanaingia hata ndani wanaepua chakula kikiwa jikoni na ni hatari sana kwa akina mama na nikisema ni hatari kwa akina mama nadhani kila mtu anaelewa. Sasa nataka nijue huu utafiti utakwisha lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, miaka ya nyuma nyani hawa walikuwa wanadhibitiwa na wananchi wenyewe kwa kuwaua kwa risasi ambazo zilikuwa zinagawiwa kutoka kwenye Ofisi ya Maliasili lakini sasa hivi wamekatazwa kufanya hivyo na Maliasili hawa hawa. Sasa naomba niulize Wizara, kwa kuwa imetamka kwamba inakusudia kuwashirikisha wananchi kwa kutumia silaha za jadi, je, Wizara iko tayari wananchi wenye silaha kama magobole na kadhalika watumie risasi kama utaratibu wa zamani?Mimi Mbunge wao niko tayari kuwanunulia risasi ili tupambane na hawa wanyama vinginevyo watuletee Wa-Congoman waje wawale kule na siyo kutuambia utafiti wakati wanaharibu watu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza Wizara kwa niaba ya Serikali inawapa pole wananchi wa maeneo ya kata zilizotajwa kutokana na usumbufu huo wa wanyama hawa nyani na ngedere na uharibifu wanaosababisha kwenye mashamba yao. Kwenye swali lake la kwanza la nyongeza anauliza utafiti utaisha lini, kwenye jibu la msingi nimesema utafiti huo unakamilika mwezi Disemba, 2017.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa nini tunafanya utafiti wakati ni dhahiri kwamba wanyama wapo na wanasumbua na wanaharibu. Mimi nafikiri utafiti ndiyo njia nzuri ya kuweza kufika mahali kupata jibu au suluhisho. Ni sawasawa na mtu anayeumwa malaria ambaye hataki damu itolewe iende kwanza ikapimwe, nafikiri hiyo haitakuwa njia sahihi. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumedhamiria na tunakusudia na mimi na wewe tunaweza tukapata nafasi kabisa kupeana taarifa ya mara kwa mara katika kipindi hiki kabla ya hiyo Disemba ili tuweze kuona tunasonga mbele namna gani.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya silaha, matumizi haya yapo kwa mujibu wa sheria na kama ni matumizi ya risasi za moto sheria zinakuwa kali zaidi. Katika eneo hilo hao Serikali inashughulikia masuala hayo kwa kushirikisha Wizara zaidi ya moja, si suala la Wizara ya Maliasili na Utalii tu.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kwamba utafiti sasa ndiyo unaweza ukatuwezesha tuone ukubwa wa tatizo, uzito wake, kama utaainisha kwamba matumizi ya silaha za moto ni lazima basi labda tunaweza tukaenda huko kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo lakini kama kwenye utafiti tukiona tunaweza kutumia njia nyingine ambayo siyo silaha za moto basi itakuwa ni vema tutumie njia hizo ambazo tutazipata.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, LEKIDIA imekuwa ikishirikiana na wananchi katika kuibua vipaumbele vya maendeleo katika Kata ya Kirua Vunjo Mashariki kwa muda mrefu na kipaumbele cha sasa ni hii barabara ya Uchira - Kisomachi - Kolaria ambao wamejitahidi kuchanga fedha na sasa wana lami pipa 300. Kipaumbele chao ni kwamba hii barabara ijengwe kwa kiwango cha lami.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kusaidia ili lami hii isije ikaharibika kujenga walau hatua kwa hatua kilometa tano na baadaye kilometa nyingine tano ili hatimaye hii barabara iweze kukamilika kwa kiwango lami badala ya kutumia fedha nyingi kwa ukarabati mara kwa mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wamekuwa wakishiriki sana katika kuchangia maendeleo, wamekuwa wakichangia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, shule na kadhalika. Katika Jimbo langu la Rombo karibu kila kijiji kuna miradi ya maendeleo inayoendelea kwa michango ya wananchi lakini kwa upande wa Serikali fedha zimekuwa haziendi kwa wakati jambo ambalo sasa linawavunja moyo wananchi.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu upelekaji wa fedha za maendeleo jinsi ambavyo zimekubaliwa kwenye bajeti ili kuwatia moyo wananchi hao waendelee kuchangia shughuli za maendeleo ambazo tayari zimeshaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli LEKIDIA wamechanga wamenunua mapipa takribani 340 kwa rekodi niliyokuwa nayo. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema kwa sababu sasa hivi tumeunda Wakala mpya wa TARURA na bahati nzuri tumepata Meneja maalum wa mradi katika Halmashauri ya Rombo na katika Halmashauri zote Tanzania. Meneja hawa jukumu lao sasa ni kufanya needs assessment katika kila Halmashauri. Tuagize Meneja wetu apitie barabara hiyo then ataleta tathmini halafu tutajua nini cha kufanya katika barabara hiyo. Kwa hiyo, ni jukumu kubwa la Serikali kuhakikisha barabara hizi zote zinafanyiwa matengenezo. Kwa hiyo ni commitment yetu Serikali kwa Tanzania nzima, hili jambo tutaenda kulifanya nikitambua juhudi kubwa ya wananchi wanayoendelea kuifanya, lazima tuwaunge mkono. Kwa hiyo, kazi itafanyika baada ya tathmini ya Mameneja wetu walioko site kuangalia kipi kilichopo na kipi kifanyike katika utaratibu gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala zima la upelekaji wa fedha, nimesema hapa kwa mfano fedha za barabara tumetenga karibuni shilingi bilioni 263 lakini hizi kuna fedha za barabara zenye vikwazo lakini zingine za road fund na maeneo mbalimbali. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha tunapata fedha hizi na bahati nzuri jana tulikuwa na Waziri wa Fedha katika kikao chetu cha mambo ya lishe amesema commitment ya Serikali katika mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha fedha zote za maendeleo zinafika katika maeneo husika. Kwa hiyo, ondoa hofu, jukumu letu sasa hivi naomba tuungane mkono wote kwa pamoja tukusanye mapato, tulipe kodi na mwisho wa siku kwamba fedha hizo zitapelekwa katika vijiji vyetu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma nzuri katika maeneo mbalimbali.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika jambo ambalo wanafunzi wetu wanahimizwa sasa hivi ni kuondokana na dhana kwamba elimu yao ni kwa ajili ya kujipatia ajira rasmi Serikalini na hivyo waingie katika mtazamo kwamba elimu itawasaidia kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muktadha huo, benki ni chombo muhimu sana cha kuwasaidia vijana wetu wanapomaliza shule kuweza kukopa ili kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo linalowakwamisha ni dhamana. Vijana wetu wanaambiwa wapeleke hati za mashamba, majumba na vyombo visivyohamishika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaiagiza Benki Kuu iweze kurekebisha sheria zake ili kuwasaidia vijana hawa wanaomaliza vyuo vikuu waweze hata kutumia vyeti vyao kama dhamana kwa ajili ya kukopa ili waweze kupata fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali ya kuwasaidia katika maisha yao? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana. La kwanza, ni muhimu sana kutambua kwamba benki zetu zinafanya biashara. Ni lazima benki hizi zipate faida kama mfanyabiashara yeyote ili shughuli za benki hizi ziweze kuwa endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba vijana wetu walioko shuleni wanakwamishwa na baadhi ya masharti ya mabenki yetu ikiwemo hili la dhamana ambalo Mheshimiwa Selasini anasema, lakini tumeanza kupiga hatua kuelekea huko ambako tunataka kwenda. Mathalani, vijana walioko Igunga walipomaliza masomo yao Chuo Kikuu cha Sokoine, kitu cha kwanza walijiunga pamoja wakaunda kikundi wakakiandikisha na wakaanza shughuli yao katika kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya CRDB ni moja ya benki ambayo ilijitokeza na kuwakopesha kufanya shughuli zao. Kwa hiyo, pole pole tunakwenda kuangalia, ni vyombo gani ambavyo vinaweza vikatumika kama dhamana kulinda mabenki yetu yasipate hasara, lakini wakati huo huo kuwawezesha vijana wetu waweze kupata mikopo. Kwa hiyo, hilo ni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni muhimu sana niendelee kusisitiza kwamba vyombo hivi sisi wenyewe tunao mchango. Mara nyingi baadhi ya wakopaji wanakuwa na historia mbaya, hawalipi. Sasa wasipolipa maana yake ni kwamba zile benki nazo zitapata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu nao wakopaji wakalinda ile credibility yao, ndio, maana tulianzisha Credit Reference Bureau kuhakikisha kwamba wakopaji wanakuwa na historia ya ukopaji. Wale ambao wana rekodi nzuri vyombo vyetu vya fedha viko tayari kuwakopesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko benki ambazo sasa hivi zimeanza hata kutoa mikopo kwa watu wasio na dhamana. Zipo benki ambazo zinakopesha kwa mfano vikundi vya akina mama, ikiwemo CRDB na NMB, vikundi vya walemavu, bila dhamana lakini sharti ni kwamba kiwepo kile kikundi credible kimeandikishwa ili fedha zinazokopeshwa zisipotee. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kuna mambo mengine Serikali haitakiwi hata iyaseme, kwa sababu yanaitia Serikali aibu. Wavuvi wanasema wanawafahamu, ni Waganda. Sasa ni kitu rahisi, kwa nini Serikali isikae na wavuvi, wavuvi wakasaidia kuwa- identify hawa watu? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Selasini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hizi kwamba kuna majambazi kutoka mje ya nchi wanavamia wavuvi huko ziwani, hata mimi nimepata kuzisikia, lakini baada ya kufanya verification kwa kuongea na wavuvi wenyewe, mimi naongea nao wengi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea na wavuvi wenyewe hasa katika visiwa vya huku Mara, kilichothibitika ni kwamba ni Watanzania hawa hawa ambao wanajifanya kwamba ni wageni wanapoenda kwenye visiwa jirani kwa kujifanya wanaongea lugha ambayo kama siyo Kiswahili sawa sawa. Ajenda ya kwamba ni majambazi kutoka sijui nchi za jirani, siyo sahihi. Hawa watu wanafahamika na tumeshatoa taarifa kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza wawatafute kwa sababu at least identity zao sasa zinafahamika. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niipongeze Serikali kwa mkakati wake wa kusambaza maduka ya dawa sehemu mbalimbali za nchi na nimpongeze Waziri wa Afya na Naibu wake kwa kazi nzuri ya kusimamia maduka haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, kumekuwa na kauli ya kuwatia matumaini wazee kwamba wataendelea kupata tiba bure, lakini wazee wengi katika nchi hii hasa wazee wa Jimbo langu la Rombo bado kero ya matibabu ni kubwa sana kwao.
Ni lini Serikali basi itamaliza kero hii ili wazee waliotumikia nchi hii kwa shida sana waweze walau kumaliza maisha yao hapa duniani wakiwa na matumaini kwamba wanapendwa na Serikali pamoja na wananchi ambao wamekuwa wakiwahudumia miaka yao yote?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi tu nimshukuru Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge wa Rombo kwa swali lake kuhusu wazee na nimhakikishie tu kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa mara ya kwanza inaweka commitment kubwa sana kwenye masuala yote yanayohusu mambo ya wazee na ndiyo maana katika ngazi ya kitaifa Mheshimiwa Rais mwenyewe ametengeneza Wizara ndani yake ameweka mahsusi portfolio inayohusu mambo ya wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la wazee tuna vipaumbele sana sana cha kwanza ikiwa ni kwenye eneo hili la afya ambapo tunashukuru kwamba Sera ya Afya ya mwaka 2007 inatoa msamaha wa matibabu kwa wazee wote wenye miaka 60 (ambao hawana uwezo). Ili kutekeleza hilo, nakubali kumekuwa na changamoto kadhaa lakini kwa sasa tumeweka utaratibu wa kuzitaka Halmashauri zote ziweze kuwakatia kadi ya CHF wazee kuanzia mwezi wa 12. Kwa hiyo, Halmashauri zimeanza ku-respond na nikuombe na wewe kwenye Halmashauri yako uhamasishe wenzako kwenye Baraza lenu muweze kuwakatia kadi za CHF wazee ili waondokane na adha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mkakati huo, tumesema mzee kwanza na wazee wenyewe wanafurahi sana, juzi nimetoka kwenye mkutano wa wazee wanafurahi sana kwamba Serikali hii inawapa kipaumbele na kweli hospitali zote nchi zimeweka kibao kwamba mzee apite kabla ya mtu mwingine na hilo linatekelezeka. Kwa hiyo, tuendelee tu kwa pamoja kutekeleza mikakati hii.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Sera ya Elimu Bure imewasaidia baadhi ya wazazi wasio na uwezo kuandikisha watoto shuleni, lakini wakati huo huo bado kuna michango kadhaa inayoendelea kwa baadhi ya shule na michango hii imerudisha nyuma morali ya wazazi kuchangia kwa juhudi katika maendeleo mbalimbali ya shule.
Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa elimu kwa wananchi kwamba sera ni elimu bila ada na siyo elimu bure ili kuwafanya wananchi waweze kuchangia kwa nguvu kama ilivyokuwa zamani? (Makofi)
Swali la pili, shule za Sekondari za Keni, Shimbi na Bustani katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ni shule ambazo zimejengwa kwa mtindo wa ghorofa kwa sababu ya uhaba wa ardhi katika Wilaya ya Rombo na sasa zina muda karibu wa zaidi ya miaka 10 wananchi wameshindwa kuzikamilisha.
Je, Serikali ipo tayari katika bajeti ijayo katika bajeti
ijayo kuzipokea hizi shule na kuzikamilisha ili kuweza kuunga mkono nguvu za wananchi katika jitihada zao za kufanya maendeleo mengine kama kumalizia maabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubalina na Mheshimiwa Selasini kwamba kuna michango ambayo inaruhusiwa. Lakini michango ile ina utaratibu kwamba ili kusudi mchango uweze kukubalika kisheria ni lazima Kamati ya Shule au bodi ya shule iwe imeujadili na kupeleka kwa wadau ambao ni wazazi, wakipitisha wanaomba kibali kwa Mkuu wa Mkoa, wakipata kibali basi hapo wanaweza wakaendelea na kuchangishana. Huo ni utaratibu ambao ni mzuri, namshauri Mheshimiwa Mbunge autumie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake
la pili, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu tupo tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujadili namna ambavyo tunaweza tukaboresha utaratibu wa kuzikamilisha hizi shule ambazo anazizungumzia. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina vivutio vingi sana vya utalii ukiacha mbuga zetu na mlima na kadhalika, wazee wetu wa zamani, machifu wana vitu vyao ambavyo walikuwa wanatumia. Tuna ngoma zetu na vitu hivi vinaaza kupotea. Sasa Wizara hii ya Maliasili na Utalii ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vivutio kama hivi, miji yetu kama Mji wa Kilwa vinahifadhiwa kwa ajili ya vizazi vinavyokuja?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nchi yetu na ina vitu vingi ambavyo ni vivutio vya utalii. Ni azma ya Wizara yetu kuhakikisha kwamba hivi vyote vinahifadhiwa ili viweze kutumika na vizazi vijavyo viweze kuvielewa na viweze kufaidika na matunda ya hivyo vitu vyote. Kwa hiyo ni azma ya Wizara yetu, itaendelea kulishughulikia, kuvilinda na kuvihifadhi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kamati ya Mheshimiwa Chenge iliyokuwa inapendekeza kodi mbalimbali mpya ilitoa mapendekezo ya kutumia uvuvi wa bahari kwa ajili ya kuongeza mapato na mara zote ni kwamba Serikali inasema boti za kisasa ambazo zinaweza zikadhibiti wavuvi wa kina kirefu hazipatikani.
Je, Serikali haioni kwamba kwa kutopatikana kwa boti hizo Serikali inakosa mapato makubwa sana kutokana na wavuvi haramu wa nchi mbalimbali duniani wanaokuja kuvua katika bahari yetu? Ni lini sasa boti hizo zitapatikana? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Selasini anaulizia juu ya uboreshaji wa sekta ya uvuvi na akihusisha na Kamati ya Chenge One ambapo mimi nilikuwa mjumbe wa Kamati hiyo tukiwa na Mheshimiwa Selasini. Nimwambie tu Mheshimiwa Selasini kwamba sasa kwa sababu mapendekezo yale tuliyapendekeza ili Waziri wa Uvuvi akayafanyie kazi na mimi ndiye Waziri wa Wizara hiyo sasa hivi aniachie ili tukamilishe mapendekezo hayo ambayo tulipendekeza kwa Waziri wa Uvuvi ambaye leo ni mimi. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ni kweli baadhi ya halmashauri zimetekeleza agizo la Serikali la kutenga shule moja kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, lakini ni kweli pia kwamba shule hizi hazina vitendea kazi pamoja na Walimu wa kutosha na matokeo yake hata ufaulu wa watoto umekuwa ukitia shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano Shule ya Sekondari ya Viziwi Njombe ambayo matokeo ya Form Four ya mwaka uliopita shule nzima wamepata division zero. Sasa je, Serikali iko tayari pamoja na agizo hili kuhakikisha kwamba shule hizi zimepata Walimu wa kutosha na vitendea kazi ili hawa watoto waweze kuangaliwa kwa uzito ule ule wa watoto wengine ambao hawana mahitaji kama hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru amerejea kauli yangu kwamba agizo hili la kila Halmashauri kuwa na angalau shule moja ambayo watasoma watoto wenye mahitaji maalum. Napenda kumhakikishia kwamba agizo lile lililotolewa tangu mwaka jana lilienda sambamba na maagizo kwamba wahakikishe shule hizo zinakuwa na vifaa na vitendea kazi pamoja na Walimu ambao watawafundisha watoto hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wake wa Njombe alioutoa, namwagiza Mkurugenzi wa Elimu pale ofisini kwangu afuatilie hiyo shule ya Njombe kuona je, ni ukosefu wa vifaa au ukosefu wa Walimu au ni tatizo la wanafunzi wenyewe lililosababisha wote wapate division zero? Hata hivyo, tunafuatilia na naagiza kwamba kila Halmashauri inapoteua shule ya watoto wenye mahitaji maalum wahakikishe kwamba kunakuwa na vifaa vya kutosha vya kuwafundishia. Ndiyo maana tunaita ni mahitaji maalum kwa sababu mtu ambaye ana ulemavu wa macho anahitaji vifaa maalum vya kusomea. Mtu ambaye ana ulemavu wa akili anahitaji vifaa malum vya kusomea. Kwa hiyo wahakikishe vifaa vyote vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni wakati wa kupanga bajeti, kwa hiyo wahakikishe kwamba ikifika mwezi wa Saba tarehe moja, utekelezaji uanze kufanyika kwa mujibu wa maelezo ya Serikali. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo taarifa kwamba wako Walimu wa kufundisha shule za walemavu wamehitimu hawajaajiriwa bado. Tumefanya mazungumzo na Ofisi ya Waziri Mkuu, nimezungumza na Naibu Waziri anayeshughulika na walemavu, tuletewe orodha ya mahitaji ya Walimu kwa ajili shule za walemavu, tutapata kutoka Wizarani orodha ya wale ambao tayari wamehitimu. Tutawaajiri mara moja ili wanafunzi hao nao wapate elimu kama wanafunzi wengine. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, akina mama wengi wajawazito wanapata madhara na kufariki hasa wanapokuwa na referral kutoka zahanati kwenda vituo vya afya na hospitali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma ya ambulance ili hawa akina mama wanapopata matatizo vijijini waweza kufikishwa haraka kwenye vituo vya afya na zahanati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatambua kwamba kumekuwa na changamoto ya kuwasafirisha akina mama wajawazito kwenda katika sehemu za kupata huduma, na kwa kiasi kikubwa kwa kweli kumekuwa na muitikio mkubwa sana wa akinamama kujifungulia katika vituo vya afya, hivi tunavyoongea sasa hivi ni zaidi ya asilimia 60 ya akina mama wajawazito wanajifungulia katika vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuboresha vituo vya afya na fedha kama alivyosema Naibu Waziri TAMISEMI, zaidi ya vituo 205 vimefanyiwa maboresho kwa kujenga theater, wodi ya akina mama kujifungulia ili hizi huduma za kujifungulia ziweze kuwa karibu zaidi. Lakini sambamba na hilo, Serikali imeendelea kutoa magari (ambulance) katika vituo vya afya na hospitali za wilaya, na kadri muda unavyokwenda tutakuwa tunaziongeza ili tuweze kufikia vituo vyote.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu ya swali hili na niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyakati ambazo mlima Kilimanjaro unapata ajali ya moto na kwa sababu hiyo wananchi wanaotokana na halmashauri zinazozunguka mlima wanafanya kazi ya kuzima moto huo, hususan wananchi wa Wilaya ya Rombo na kikubwa wanachoambulia ni nusu mkate. Sasa kwa kuwa kuna utaratibu wa kutoa mrabaha kwa halmashauri ambazo zina madini; je, Serikali haioni kwamba umefika wakati sasa mapato yanayotokana na mlima Kilimanjaro kiasi fulani kitolewa kama mrabaha kwa halmashauri zinazozunguka mlima ili iwe kama incentive na kuwafanya wananchi hao waweze kuulinda mlima wakati majanga ya moto yanapotokea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna vijana wapagazi (porters) ambao wanabeba chakula, maji, gesi na kadhalika kwa ajili ya kuwasaidia watalii kupanda mlima. Vijana hawa wana malalamiko makubwa sana kwamba malipo yao ni ya kinyonyaji. Je, Serikali iko tayari kuchunguza malalamiko haya na kuwasaidia hawa vijana ili waweze kupata stahiki zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakishiriki katika kuzima moto pale unapojitokeza katika hifadhi ya Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mrabaha hasa kwenye Halmashauri zile ambazo zinazozunguka mlima Kilimanjaro, naomba niseme kwamba hilo tutalifanyia kazi, tutangalia kama hilo linaweza likafanyiwa kazi. Kwa utaratibu uliopo hivi sasa ni kwamba katika bajeti nzima ya hifadhi za Taifa (TANAPA) asilimia tano mpaka saba huwa zinatengwa kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali inayoibuliwa na wananchi walioko katika maeneo yaliyo jirani na hifadhi mbalimbali. Kwa hiyo, katika hili ambalo amelisema basi tutalifanyia kazi tuone kama nalo linaweza likafanyiwa kama tulivyofanya madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la kuhusu wapagazi, kama atakumbuka hapo tulipokuwa tunajibu swali lililokuwa linahusu maslahi wapagazi na waongoza utalii tulisema; katika kikao kilichofanyika Arusha kati Serikali wapagazi na vyama vyao pamoja; katika utatu huo tulikubaliana kabisa viwango ambavyo vimependekezwa na ambavyo tulifikia muafaka. Tukaagiza kwamba sasa wale wote, mashirika yote, taasisi zote, kampuni zote za kitalii lazima ziingie mikataba na hao wapagazi ili angalau kuhakikisha kwamba kwa siku kila mmoja anapata fedha zisizopungua dola elfu kumi kwa siku. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukisubiri sungura mdogo huyu wa Serikali kugawanywa nchi nzima sisi watu wa Rombo tumeamua kujiongeza, na tumejenga Kituo cha Polisi Useri kimeshaanza kufanya kazi, Kituo cha Ngoyoni kiko kwenye rooffing, kituo cha Kirongo Samanga pamoja na nyumba ya polisi karibu inafika kwenye linta na kituo cha Mahida kiko kwenye msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa jibu la hakika ili wananchi wa Rombo waamasike kuchangia zaidi ujenzi wa hivi vituo. Ni lini mtakuja kufanya hiyo tathimini ili kuwatia moyo wananchi wakamilishe hivi vituo kwa sababu kazi ya kuchangia vituo vya polisi ni ngumu kuliko hata kuchangia zahanati na shule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa sababu ya urefu wa mpaka wa Rombo na Kenya na njia za panya kuwa nyingi, Jeshi la Polisi Rombo lina magari ya zamani sana na chakavu.
Je, Serikali iko tayari kuweka katika bajeti ijayo gari kwa ajili ya kusaidia shughuli za polisi katika Wilaya ya Rombo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue furusa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, na hii ndiyo aina ya Wabunge wakutolewa mfano. Kazi waliyoifanya ni kubwa ya kushirikiana na kuhamasisha wananchi wake kujenga vituo vitatu hivi kituo cha Ngoyoni, Mahida na Kirongo si kazi ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie mbele ya Bunge hili Tukufu kwamba jitihada za aina kama hii za Mbunge Selasini na Wabunge wengine wengi tu wamo katika Bunge hili wanafahamu wamefanya kazi nzuri kama hii. Serikali itaziunga mkono na mimi nimuhakikishie kwamba nitahakikisha tathimini hii imekamilika haraka na natarajia kufanya ziara hiyo karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda kushuhudia hii kazi mimi mwenyewe na ndiyo maana nazungumza kwa kujiamini sana. Nilikwenda nilifanya ziara Rombo na nikaona kazi hii inafanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa hiyo basi namuhakikishia kwamba nitakuja tena Rombo karibuni ili tushirikiane kwa pamoja. Kuna mambo mawili ambayo tutafanya; la kwanza tutatoa kipaumbele katika bajeti ambayo inakuja ili kuhakikisha vituo hivi vinakamilika; lakini la pili nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili kuendelea kuhamasisha wadau zaidi ili tumalize vituo hivi ili viweze kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kulingana na kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Mbunge anaifanya nina uhakika kabisa tutaangalia uzito wa changamoto ya gari katika Mkoa wa Rombo ili tuone katika gari ambazo tunatarajia kuzipokea wakati wowote tuweze kupeleka huko zisaidie kupunguza changamoto za askari.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwwenyekiti, Serikali inapochelewesha kupeleka fedha ambazo ziko kwenye bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi mbalimbali za Serikali kama Ofisi za Wakuu wa Wilaya na za Halmashauri inasababisha variation katika ujenzi wa ofisi hizi na kwa sababu hiyo Serikali inaingia katika matumizi makubwa zaidi katika kumalizia.
Je, kwa nini Serikali isitoe kwa mkupuo fedha hizo ofisi hizo zikamalizika zote kwa pamoja ili Halmashauri pamoja Wilaya hizo zikawa na ofisi na Serikali ikaokoa kiasi kikubwa cha fedha kwa njia ya variation?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la Mheshimiwa Selasini ni wazo zuri na ndiyo maana nimesema mwaka huu tumetoa karibu shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi huo, lakini unaangalia jinsi gani kila sehemu ina eneo lake la kimkataba la ujenzi. Ndiyo maana hapa tukusema kila Mbunge ataanza kupinga kelele.
Kwa hiyo, ni wazo zuri tutaenda kulifanyia kazi lengo kubwa ni kwamba tumalize haya matatizo yote ya ofisi wananchi na wataalam wetu waweze kupata huduma kwa hiyo ni wazo zuri na Serikali tunaendelea kupeleka fedha kwa kadri tunavyokusanya na mimi naamini kwamba utafika muda ofisi nyingi zitakamilika na Watendaji wetu watakuwa katika mazingira mazuri ya kufanya kazi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Takataka zinaweza zikasababisha uchumi mkubwa sana kwa wananchi wetu kwa sababu taka zinaweza zikatengeneza matofali, zinaweza zikazalisha umeme, zinaweza zikatengeneza mbolea nzuri sana na sasa hivi kwa sababu maeneo ya kutupa taka yanaendelea kupungua mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali isifanye uamuzi wa makusudi, kabisa ikaleta hii teknolojia nchini, ikaanza na majiji yetu ili kuwafanya wananchi wakapata kipato kwa kukusanya takataka na kuzipeleka kwenye maeneo hayo ambayo yanaweza yakazi-process na kuzalisha vitu vingine kwa faida ya Taifa kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Selasini jambo lako ni zuri sana, ndiyo maana katika ofisi yetu tuna mradi mmoja unaitwa Strategic City Project, katika miji mbalimbali tumetenga utaratibu wa kutengeneza haya madampo ya kisasa, ambapo ukienda Mbeya utayakuta, hapa Dodoma tunajenga na maeneo mbalimbali tunatengeneza madampo kama yale. Lengo letu kubwa ni kwamba taka zitakazozolewa baadaye ziingizwe katika system maalum kuweza ku-convert katika shughuli zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sasa hivi tunakaribisha wawekezaji mbalimbali ambao katika njia moja au nyingine watasaidia ukusanyaji wa hizi taka kuweka katika malighafi nyingine, ikiwemo suala zima la utengenezaji wa mkaa.
Kwa hiyo, ni hilo ni jambo zuri Serikali na wadau mbalimbali tushirikiane kwa mustakabali wa nchi yetu ambao mwisho wa siku taka hizi baada ya kuwa uchafu inaweza ikawa malighafi na zitasaidia kujenga uchumi katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na kusubiri mapitio ya huo mkataba, lakini hapa nchini pana vikundi mbalimbali vya watu vinawakusanya watoto wetu wa nchi hii kwa minajili ya kuwatafutia kazi za ndani nchi za nje. Habari tulizonazo ni kwamba baadhi ya hawa watoto wamekuwa wakinyanyasika, wakiteswa na hata kuuawa. Je, ni hatua zipi za wazi ambazo Serikali inazichukua kwa ajili ya kudhibiti vikundi hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge hapa alikuwa anazungumzia wale mawakala wa ajira ambao kwa namna moja ama nyingine, yamekuwepo malalamiko mengi sana ya kuwapeleka mabinti zetu katika nchi hasa za Uarabuni kwenda kufanya kazi za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alishatoa agizo na tangazo la kwamba wale wote ambao wanakwenda kufanya kazi nje ya nchi wapitie mfumo ambao upo katika Wizara yetu kupitia Wakala wa Ajira wa Serikali ambaye ni TAESA. Sasa tukibaini kwamba wako watu ambao wanafanya kazi hii kinyume na taratibu, sheria zetu ziko wazi, huwa tunawafutia usajili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tumekuwa tukiwachukulia hatua kuhakikisha kwamba hawapati tena registration ili tuhakikishe kwamba nguvu kazi yetu hii wakienda kufanya kazi nje ya nchi tuwe tumewalinda kwa maana ya haki zao za kimsingi, tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo wako baadhi ya Watanzania ambao hawapitii katika Ofisi yetu na wakienda nje ya nchi wakipata manyanyaso tunakuwa hatuna taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata Balozi zetu zimeweka utaratibu mzuri; ile mikataba inayotolewa pale, mwajiri yeyote wa nje ya nchi ambaye anamtaka mfanyakazi wa Tanzania lazima apitie katika Ubalozi na Ubalozi unawasiliana nasi kwa ajili ya kuandaa mikataba ili tumlinde na tulinde haki za mfanyakazi wa Kitanzania.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya sheria ya zamani ya mita 60 kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji, ilianza katikati ya mto mita 60 mpaka pembezoni mwa mto na mwaka jana tukairekebisha ikaanza mwisho wa mto na kuendelea, iliwaathiri wananchi wengi sana waliokuwa na mashamba ya asili wakati huo, ambao sasa hivi ndio wanakumbwa na hili tatizo la kuondolewa katika maeneo yao ya asili kama walivyofanya kwa Mheshimiwa Mbowe ambaye amekaa kwenye hilo shamba karibu miaka 80 iliyopita.
Je, Serikali imejipanga namna gani kufidia hawa wananchi kwa sababu marekebisho ya sheria ya mwaka jana yaliwakuta wananchi wakiwa wanaishi katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu katika utaratibu wa kisheria, mambo haya katika vyanzo hivi, maeneo chepechepe, maeneo oevu, yanakuwa defined katika mazingira mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu kuna sheria ambayo imetungwa, kwa sababu tunajua kwamba kuna Waziri mwenye dhamana katika Ofisi ya Makamu wa Rais na bahati nzuri alipita mpaka Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa mingine, wakifanya ufafanuzi wa hizi sheria na utaratibu wake ukoje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu maamuzi yote yanaenda katika suala zima la mipango shirikishi, imani yangu kuwa ni kwamba, zoezi hili linapokwenda na ndio maana nirejee jibu langu la msingi, linapokwenda sasa kufanyika kubaini maeneo mbalimbali, kwamba hawa watu uhalisia wake ukoje, naamini maamuzi sahihi yatafanyika lakini baada ya kufanya jambo hili kuwa shirikishi zaidi kama tulivyoelekeza katika suala zima la Jimbo la Arumeru Magharibi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mvua zinazoendelea zimeharibu barabara nyingi sana za vijijini karibu nchi nzima mfano katika Jimbo langu la Rombo barabara nyingi sana za vijijini hazipitiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua TARURA inafanya kazi nzuri sana sasa hivi katika baadhi ya majimbo. Natambua pia kwamba kuna bajeti itasomwa hapa kwa ajili ya kuiwezesha TARURA kuendelea na kazi zake. Je, Serikali ina mpango wowote wa dharura wa kuisaidia TARURA ili iweze kuwezesha barabara ambazo zimevunjika vijijini kupitika kwa sasa hivi ili wananchi waweze kupeleka mazao yao katika masoko na kadhalika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mvua zimenyesha kubwa katika maeneo mengi na kila neema inavyokuja huwa inakuwa na adha yake. Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba barabara zote zinapitika kwa vipindi vyote. Ni vizuri tukapata fursa ya kufanya uthamini maeneo ambao yameharibiwa na mvua ili hatua za dharura ziweze kuchukuliwa na wananchi wetu wasiweze kuendelea kupata shida.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wafanyabiashara kote nchini hivi sasa wanalalamika biashara zao kuyumba na ukweli uliopo ni kwamba tatizo hili bado linaendelea katika Manispaa hii ya Mpanda. Je, Serikali iko tayari kuiagiza Halmashauri kwa spirit ya utawala bora kukaa tena na wafanyabiashara hawa ili kuweza kwa pamoja kujadili kiwango ambacho Halmashauri na wafanyabiashara watanufaika ili sasa pande zote mbili ziweze kufanya kazi bila manung’uniko?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika utendaji bora na ushirikiano na Halmashauri ni kwamba maeneo mengi utendaji unaonekana kukwama kwa sababu wakati mwingine mabavu yanatumika katika kuweka hivi viwango vya kodi na kadhalika. Ni lini Serikali itatoa maagizo ya hakika kabisa ili Halmashauri zisigombane na wateja wao ambao ni hawa wafanyabiashara na sasa hivi tunavyohimiza Halmashauri ziweze kuongeza vyanzo vipya vya mapato ili mapato ya Serikali kokote katika nchi yetu yasipotee tu kwa sababu ya uhusiano mbaya kati ya Halmashauri pamoja na wafanyabiashara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, nafarijika swali kama hili kutoka kwa Mheshimiwa Selasini na bahati nzuri yeye ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI. Katika nafasi niliyopata kushiriki katika vikao vyake amekuwa akihimiza Halmashauri zihakikishe kwamba zinakusanya mapato yake ili ziweze kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, umenisaidia. Sisi Waheshimiwa Wabunge ni Madiwani tukiwa kwenye halmashauri zetu. Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ilishirikisha wafanyabiashara, zimeundwa Tume zisizopungua tatu na katika jibu langu la msingi nimeeleza hawa ambao wamekuwa wanapangishiwa wamekuwa wakilipa Sh.100,000 mpaka Sh.150,000.
Mheshimiwa Spika, sasa halmashauri katika kuona katika vyanzo vyao ambavyo ni vizuri wakavisimamia iko katika kupandisha kutoka Sh.15,000 ambayo imekuwa ikitozwa zaidi ya miaka 30 na kwenda mpaka Sh.40,000 which is very fair.
Mheshimiwa Spika, ameelezea juu ya suala zima la kutokuwa na migongano baina ya wafanyabiashara na halmashauri. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, ushirikishwaji umekuwepo na hata ninavyoongea leo hakuna hata kibanda kimoja ambacho kimefungwa katika Manispaa ya Mpanda kwa sababu ushirikishwaji umekuwepo. Zimekuwepo Tume zaidi ya tatu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba maridhiano yanakuwepo na halmashauri inapata chanzo chake cha pesa na kinatumika sahihi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza mmomonyoko wa maadili kwa vijana mara nyingi tunazungumza habari ya vijana wasanii, wanaocheza filamu, wanamuziki na kadhalika. Lakini mmomonyoko pia mkubwa sana upo kwa vijana wa mitaani na hawa mara nying ni kwa sababu ya kukata tamaa.
Sasa naomba niiulize Serikali, pamoja na mifuko mbalimbali ya kuwaendeleza vijana, ni mkakati gani ambao Serikali inao ili kuwasaidia kisaikolojia na namna vilevile ya kuweza kuona matumaini katika maisha yao vijana waache kuingia kwenye tabia ambazo kwa kweli zinasababisha mmomonyoko mkubwa sana wa maadili? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na ninakushukuru kwa kujibu sehemu ya hilo swali kwamba huu ni wajibu wa jamii nzima. (Makofi). Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imekuja kwa nguvu sana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu ili Watanzania wathamini kazi. Kazi ndiyo ufunguo wa kila kitu ningeomba Watanzania wote tushirikiane kuhakikisha kwamba kila mtu Tanzania anafanya kazi, mambo ya njia za mpito kuweza kuishi hayana nafasi tena ndiyo yanayozua matatizo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili wazazi tuna nafasi kubwa sana kuweza kubadilisha hii hali kwa upande wa watoto wetu tukiweka mbele suala la kazi kama tulivyokuwa tunafanya wakati wa uhuru ambapo tulikuwa tunasema uhuru ni kazi na leo ni hapa kazi tu. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kwanza niungane na Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe kwa kukubaliana naye kwamba suala la kubadilisha utaratibu wa mfumo wa maisha kwa vijana pamoja na kwamba ni suala la jamii kwa ujumla, lakini napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba pia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeandaa programu mbalimbali ambazo tunashirikiana na Halmashauri za Wilaya kuhakikisha Halmashauri zetu Idara za Vijana zinajipanga kutoa elimu ya kubadilisha mawazo na mtazamo kwa vijana ili kuwasaidia kujenga mtazamo mpya wa kujiajiri na kuondoka katika tabia za kupoteza muda kwenye vijiwe na kuingia kwenye shughuli ndogondogo za kuweza kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tusaidiane kwa pamoja na Halmashauri zetu, hasa wale vijana ambao wamekuwa wakipoteza muda mwingi kwenye vijiwe. Wageuze vijiwe vyao kuwa ni shughuli za kiuchumi badala ya kutumia vijiwe kuwa ni maeneo ya kupoteza muda. Mifuko ya kuwawezesha hao vijana kupitia Idara ya Vijana kwenye Halmashauri zetu ipo na Serikali tumeshajiandaa na Wabunge ambao wapo tayari tutafanya nao kazi hiyo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri haya ya kaka yangu Profesa Kabudi, nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wengi sana wanakosa haki zao, kwanza kwa kutojua kwamba wanapaswa kudai fedha zao walizolipa kama faini baada ya kushinda kesi na pili kwa sababu nakala za hukumu custodian wake ni Mahakama yenyewe.
Je, Serikali haioni kwamba kwa kutotoa maelezo kwa hawa warufani wakati rufani zao zikiwa zinasomwa kwamba wanatakiwa wafuatilie zile faini walizolipa baada ya kushinda, Serikali haioni kwamba inawadhulumu na au inaendelea kuwaadhibu kutokana na kutowarejeshea fedha zao?
Swali la pili, kwa kuwa Mahakama huwa inatoa muda maalum wa kukata rufaa na mtuhumiwa yule anapokata rufaa Mahakama inakuwa inajua. Je, ni kwa nini Mahakama inapopokea fedha zile isiziingize kwenye akaunti ya akiba kwa ajili ya kusubiri rufani itakapoamuliwa na badala yake inaingiza kwenye akaunti ya mapato na hivyo kusababisha fedha zile zinatumika, zinapohitajika inakuwa shida kupatikana?(Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, moja ni kweli inawezekana wananchi wengi hawafahamu kwamba mara baada ya kuwa wameshinda rufaa zao wana haki ya kurejeshewa faini ambayo walikuwa wamelipa. Kwa hiyo, Wizara pamoja na Mahakama tutafanya jitihada kutoa elimu na maelezo kwa wananchi kwamba mara wanapokuwa wameshinda rufaa zao za mwisho basi waweze kufuatilia malipo ya rufaa zao kwa sababu ni haki yao. (Makofi)
Kuhusu swali la pili, kwa kuwa utaratibu wa Serikali ni kwamba, faini zinachukuliwa kama maduhuli na zinakatiwa risiti ya Hazina, basi jambo hilo tutakaa na Hazina ili tuweze kuona utaratibu unaoweza kutumika ili kuhakikisha kwamba malipo ya faini yanarejeshwa kwa haraka iwezekanavyo ili wananchi ambao wamelipa fedha hizo waweze kuzipata hela zao kwa wakati. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nnakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza naomba tu jina la muuliza swali lisomeke kama Pascal Yohana Haonga siyo Pascal Yohana Hasunga. Baada ya masahihisho hayo kidogo naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mara nyingi Serikali imekuwa ikizungumzia na kutoa matamko kuhusu ada zinazopangwa na shule za binafsi ikionesha kana kwamba Serikali ina mpango wa kuweka kiwango fulani cha ada bila kuzingatia gharama ambazo shule hizi zinaingia katika kusomesha wale watoto na kuendesha shule zao. Je, kwa nini Serikali isiwaachie wamiliki wakapanga hizi ada wenyewe ili wazazi ambao wanaweza wakamudu ada hizo waenda kwenye shule bila kikwazo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara nyingi shule zinapanga taratibu zao za namna ya kuwafanya hawa watoto waweze kufaulu, kwa mfano, kuwawekea mitihani kutoka kwenye daraja fulani kwenda kwenye daraja fulani, lakini Serikali pia inaonesha haifurahishwi na jambo hili. Je, kwa nini Serikali isiache hizi shule zikapanga utaratibu wa kuwafanya hawa watoto waweze kufaulu kulingana na sera na taratibu za shule zenyewe? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Serikali kutoingilia maamuzi ya shule za binafsi katika kuamua ada. Naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na sekta binafsi ya namna bora ya kuratibu suala hilo badala ya Serikali yenyewe kutoa maelekezo ya gharama ambazo zinatakiwa zilipwe.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu shule za binafsi zinaendeshwa na watu binafsi, lakini vilevile kwa sababu ni biashara na ni biashara ambayo maana yake mtu anayetaka kwenda kununua au kupata hiyo huduma yeye ndiyo aangalie uwezo wake, tunafikiri bado kuna busara ya kuendelea kujadiliana nao namna bora ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na gharama ambazo zinahimilika badala ya Serikali yenyewe kuanza kutoa bei au gharama elekezi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili kwamba Serikali isiingilie taratibu za shule binafsi za kuweka viwango vya ufaulu. Wakati tunatambua kwamba ni kweli ni vizuri sekta binafsi katika uendeshaji wa shule ikaachiwa nafasi ya kuamua wenyewe namna wanavyodhibiti ubora. Ni kweli kwamba udhibiti wa ubora ni suala la kisera na kisheria, kwa hiyo, haiwezekani Serikali ikakaa moja kwa moja ikaruhusu kila mtu ajiamulie namna anavyodhibiti ubora katika shule yake.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa ilichoamua ni kwamba tutaendelea kushirikiana na Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi ili kuangalia namna ya kuboresha sheria na taratibu zilizopo ili ziwawezeshe kupata ubora ule, lakini bila kuvunja sheria za elimu kwa sababu hata kama shule ni za binafsi, lakini ni nchi moja, Serikali ni ile ile, sheria ni zilezile, hatuwezi tukaruhusu kila mtu akajiamulia anavyotaka kwa sababu siyo kila mwenye shule binafsi amekuwa akitumia uhuru huo vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya wanafunzi wamefukuzwa shule kinyume na sheria, kuna wengine wanakaririshwa kwa kuonewa, kuna wanafunzi unakuta wa Form Four wanafukuzwa shule tu kwa sababu hajafikia kiwango fulani. Tunachosema ni kwamba tutaendelea kuwaruhusu kuboresha hayo mazingira, lakini sheria na taratibu lazima tuzifuate na ndiyo maana tunaendelea kufanya nao mjadala kwa pamoja.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Maji mengi sana ya mvua yanapotea katika nchi hii kiasi kwamba tungekuwa na utaratibu wa kuyavuna yangeweza kusaidia katika shughuli za umwagiliaji na shughuli za wanyama. Kwa mfano katika Jimbo langu la Rombo kuna mito ya msimu kama Ungwasi, Marwe, Tarakea, Uashi pamoja na Nana ambapo maji ya mvua ambayo yanakwenda nchini Kenya wale wameyazuia wanafanya nayo umwagiliaji halafu wanatuletea tena bidhaa huku kwetu.
Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari utakapopata nafasi twende wote Rombo ukayaone haya mabonde ya mito hii ya msimu ili tuweze kuangalia uwezekano wa kuyazuia ili tuweze baadae kuyatumia kwa ajili ya umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Selasini Mzee wangu, mimi kama Naibu wa Waziri wa maji nipo tayari baada ya Bunge twende pamoja Rombo ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Vyama vya Siasa imeweka masharti ya wazi na yaliyo kamilika namna ambavyo vyama vitapata wanachama wake na vitaeneza sera na itikadi yake, lakini kwa sasa polisi wamekuwa na desturi ya kuzuia vikao vya vyama vya siasa hata vikao vya ndani vinavyopanga mipango ya uendelezaji wa chama. Sasa Serikali haioni kwamba badala ya kusimamia sheria Serikali yenyewe kwa kutumia vyombo vyake inavunja sheria; na kama inataka hayo masharti ya sasa yaendelee ilete hiyo sheria hapa Bungeni ili kuweza kuweka hayo masharti mapya, badala ya kutumika kwa ajili ya kuwapiga wanasiasa mitaani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea majibu yangu ya awali kwamba si kweli kwamba Serikali inazuia harakati za kisiasa na hata sheria aliyoisema, sheria hii imetoa uhuru kwa vyama kutafuta wanachama na kufanya mikutano, lakini iko subject na sheria zinginezo ikiwepo sheria ya Police Force na Auxiliary Service Act ambayo pia imeweka masharti katika section namba 44 na 45 ya namna vyama vya siasa vinaweza vikafanya kazi zao hasa katika mikutano na maandamano mbalimbali.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa miaka 54 sasa Serikali hizi mbili za Chama cha Mapinduzi zimeshindwa kutatua kero za Muungano na Tume ya Warioba ilileta pendekezo katika mchakato wa Katiba ambao ungeondoa hizi kero za Muungano kwa kuunda Serikali tatu. Sasa je, ni lini Serikali watarejesha ule mchakato wa Katiba ili kuweza kupata Katiba ambayo itaondoa kero za Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Baba Paroko, Mheshimiwa Selasini. Si kweli kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaongozwa na Chama cha Mapinduzi kwamba imeshindwa kutatua changamoto za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa katika majibu ya kumjibu Mheshimiwa Mbarouk kwamba mpaka sasa changamoto ambazo tunashughulika nazo zimebaki nne tu katika nyingi zilizokuwepo. Sasa kusema kwamba Serikali imeshindwa katika uwiano huo nafikiri Mheshimiwa Selasini itabidi tukae mahali fulani tufundishane mahesabu yale ya wingi na uwiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa wapo baadhi ya Watanzania na Waheshimiwa Wabunge hata yale masuala ambayo si changamoto za Muungano, wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kuonesha kwamba masuala hayo ni changamoto za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwasihi Mheshimiwa Selasini (Baba Paroko) tusifike mahali ikawa kama Kanisani ambapo kanisani kila siku lazima tunahubiri kwamba shetani yupo, tuendelee kupambana naye. Sisi kwenye masuala ya kisiasa yapo mambo tunapambana nayo yakiisha, hayo yameisha hayapo tena si kama tunavyopambana na shetani. (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa mujibu wa sheria, uthamini ukishafanyika, ndani ya miezi sita waathirika wote wanapaswa wawe wameshalipwa fiidia zao. Wako wananchi wa Arusha na wananchi wa Rombo, Lotima na Holili, ambao bado wana malalamiko ya kutolipwa fidia zao. Je, Serikali iko tayari kupokea majina ya wananchi hawa wanaolalamika na kuwalipa fidia zao?
Swali la pili, barabara kutoka Mamsera Jimboni Rombo mpaka Mahida KNCU na kwa Abiola ilichukuliwa na TANROADS mwaka 2014/2015 lakini TANROADS wameitelekeza hadi sasa, Halmashauri, TARURA na TANROADS hawaiangalii.
Naomba kauli ya Serikali, barabara ile imerudishwa TARURA ili waitengeneze au TANROADS wako tayari kuendelea kuihudumia hiyo barabara? Kwa sababu, imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Mahida, Chana na maeneo mengine ambayo hiyo barabara inapita? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Selasini kwa kufuatilia na anajua kwamba ziko harakati na juhudi kubwa ambazo zinafanyika kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza niseme tu kwamba suala hili la kulipa fidia ni kwa mujibu wa sheria. Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba sheria hii namba 13 ya 2007 inatoa mamlaka ya kufanya fidia kwa wananchi pale ambapo mradi wa barabara unapita na hususan ukiangalia section 16 inasema pamoja na mambo mengine, Sheria ya Kutwaa Ardhi (Land Acquisition Act), pia iko Land Act na Village Land Act ambapo zinatumika sambamba na sheria hii ya barabara ili kufanya wananchi waweze kupata haki zao. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kama wapo wachache kama nilivyosema, wengi wamelipwa, basi tutatazama, lakini sambamba na sheria, haki zao watazipata kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili amezungumza juu ya hii barabara ambayo anasema inatoka Mamsera, kulikuwa na sintofahamu labda kuhamishwa kwenda TARURA. Cha muhimu ni kuhakikisha barabara inaboreshwa. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zinavyojengwa, ziko kwenye mpango, kwa maana ya kwamba sisi upande wa TANROADS iko strategic plan ambayo ina-monitor ujenzi. Tutazama tu kuona kama inakwenda TANROADS au TARURA lakini lengo itaweza kutengenezwa kwa mujibu wa taratibu zilizokuwepo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali imechukua baadhi ya vyanzo vya mapato katika Halmashauri na kurudisha Serikali Kuu na vilevile imechukua baadhi ya watumishi kama watumishi wa Idara ya Ardhi na sasa watumishi wa Idara ya Maji. Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo inakwenda kinyume na sera yake ya D by D na mwisho wake ni kuziua kabisa hizi Halmashauri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Selesini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumwambia kwamba, uchukuaji wa vyanzo vile vya mapato ilikuwa kwa lengo moja na Bunge lako Tukufu liliridhia kwamba vichukuliwe ili ufanisi uonekane kwenye makusanyo na hatimaye fedha hizi ziweze kutekelezwa kulingana na bajeti za kila Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili la kuchukua watumishi, tuitendee haki Serikali yetu ya Awamu ya Tano, hakuna mtumishi aliyehamishwa kutoka Halmashauri moja kupelekwa kwenye Wizara yoyote. Watumishi wamebaki kwenye Halmashauri husika, lakini wanatakiwa kuripoti kwenye Wizara zao za kisekta. Kwa hiyo, hakuna mtumishi yeyote aliyeondolewa ndani ya Halmashauri. Tunachokifanya kama Serikali ni kuboresha tu utendaji kazi wa watumishi hawa kwa manufaa mapana ya Taifa letu wananchi wetu kwa ujumla.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ukweli utabaki pale pale kwamba TARURA inahitaji nyongeza ya fedha. Pamoja na ubovu wa daraja liko tatizo la barabara ambazo zina mawe hazipitiki, kwa mfano katika Jimbo la Rombo, Kata za Handeni, Shimbi, na Makiidi ni Kata ambazo zilikumbwa na volkano na kwa hiyo mawe ni mengi barabara hazitengenezeki. Sasa, je, ni mkakati gani Serikali itakayofanya ili barabara kama hizi ziweze kupitika kwa sababu Vijijini ndiko kwenye uzalishaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na yeye kwamba kuna baadhi ya ameneo ambayo uhitaji wa pesa ni mkubwa. Kwa hiyo iko case by case, naomba Mheshimiwa nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa ikichukua case by case, pale ambapo kuna uhitaji maalum kuna fedha ambazo zimekuwa zikitengwa ili kutatua changamoto ambazo zinakuwa zinawakabili wananchi wa maeneo husika.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro inategemea sana upandaji miti wa wananchi wanaozunguka Mlima Kilimanjaro na unyevunyevu wa ile miti ndiyo unasaidia theluji mlimani iweze kuendelea kukaa na ikae kwa muda mrefu. Sasa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri au Serikali, fedha hizi zitakapopatikana maeneo muhimu kama haya yenye Hifadhi za Taifa kama mlima wetu, mko tayari hizi fedha zisaidie wananchi wale ili waweze kupanda miti kwa wingi kwa ajili ya kuhifadhi theluji katika ule mlima wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi ni kwamba tuko tayari kutoa fedha kwa kushirikiana pia na wezentu wa Maliasili hasa Wakala wa Misitu ambao pia watatusaidia kupata miti inayoweza kuhimili maeneo hayo. Ahsante.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza mimi nikiri kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI na kwamba Kamati ilikwishafanya ziara mara kadhaa kwa ajili ya kukagua miradi ya TASAF na nikiri kwamba kuna maeneo ambayo TASAF inafanya vizuri tulitembelea Maswa pale tukakuta mama mmoja amejenga kajumba kake kwa njia hiyo vizuri, lakini sasa ni ukweli pia kwamba fedha hizi zinagawanywa kibaguzi na katika ziara tulielezwa na hofu inakuja jana tumemsikia Mheshimiwa Rais anasema ukiwa na chakula chako unawapa kwanza watoto wako halafu ndio unawapa jirani. Sasa mimi naiomba Serikali isipuuze hili suala la ubaguzi kwa sababu litagawa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Wizara iko tayari kubeba hili dukuduku, haya mashaka na kuyafanyia kazi kwa ajili ya mtengamano wa nchi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachompenda Mheshimiwa Selasini ni mtu mkweli, maana utangulizi wake amesema maeneo mengine TASAF wanafanya vizuri, mimi nampongeza kwa kuwa mkweli, lakini tulivyo sisi binadamu katika matarajio ya utendaji hawaweze watoto wote 100 wakafanya vizuri kama unavyotaka wewe. Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya TASAF nakubali rai yake kwamba yale maeneo yenye malalamiko niyafanyie kazi na kwa uzoefu wangu mnavyo nifahamu hili jambo tutaliweka vizuri na naomba Mbunge yeyote ambaye ana ushahidi kwamba mahala fulani hizi pesa zinafanyika kwa upendeleo mimi nitalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkazo uliwekwa vizuri sana katika elimu ya msingi na elimu ya sekondari tulipojenga shule nyingi sana za kata. Mkazo pia umewekwa kwa elimu ya juu kwa maana ya vyuo vikuu. Hata hivyo vijana wengi sana baada ya kumaliza form four na form six wana-hang hapa katikati hawana pa kwenda na viwandani wanahitajika sana…
… kama mafundi mchundo na kadhalika. Sasa, je, Serikali ina mkakati gani na vijana hawa kuwapa elimu ambayo baadae itawasaidia kuwa mafundi mchundo na kazi nyingine za viwandani badala ile elimu ya chuo kikuu ambayo inatengeneza mameneja zaidi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika ngazi za kati hatuna mafundi wa kutosha kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Selasini, lakini niseme tu kwamba jitihada zimeendelea na kama tutakumbuka mara ya mwisho kupitia Bunge lako tukufu tuliweza hata kupitisha uwezekano wa makundi hayo kupewa mkopo ili kuweza kuziba hayo mapengo. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kufanyiakazi ili kuweza kuona kwamba maeneo hayo yanaimarishwa na vijana wengi zaidi wanapatikana kutoka katika makundi hayo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi na naomba uniruhusu nimpongeze Naibu Waziri Mheshimiwa Stella Ikupa. Tangu amechaguliwa, amekuwa ni faraja na sauti yenye matumaini kwa walemavu wenzake na bidii yake ya kazi hapa Bungeni sote tunaiona. Kwa hiyo, namwombea Mwenyezi Mungu aendelee hivyo hivyo kwa sababu hata sisi walemavu watarajiwa tunawiwa kwake. (Makofi)
Sasa swali langu, katika jimbo langu kuna Chama cha Walemavu na kilikuwa kinapata ufadhili kutoka kwa mama mmoja Elizabeth kutoka Sweden. Chama hiki kiliingia kwenye mgogoro wa uongozi na kusababisha yule mfadhili akarudi nyuma, na baadhi ya walemavu pia wakarudi nyuma, kwa sababu ya kugombea baadhi ya vitu ambavyo walikuwa wanafadhiliwa.
Sasa nataka nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri, je, uko tayari utakapopata nafasi kuja Rombo ili tusaidiane kutatua ule mgogoro na kuwaweka wale walemavu vizuri katika chama chao. Ili wale wafadhili waweze kurejea na kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo ameeleza kwamba anashughulikia masuala ya watu wenye ulemavu kwenye jimbo lake. Nimhakikishie kwamba baada ya Bunge hili nitaendelea na ziara, na miongoni mwa ziara ambazo nitafanya kama alivyoniambia au kama alivyoniomba, nitafika kwenye jimbo lake kwa ajili ya suala ambalo amelieleza mbele yako. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi na nimpongeze tu Waziri anavyojua hii miradi ya maji na scheme za maji na jinsi anavyoifuatilia, hongera sana Mheshimiwa Waziri.
Kuna Ziwa la Chala pale kwetu Rombo na Wabunge wote wa Rombo waliopita Mzee Mramba, Ngalei na wengine tumekuwa tukiomba maji yale yametumike kwa ajili ya wananchi wa vijiji 28 vya Ukanda wa chini na nashukuru sasa ruhusa imetoka kwa sababu yale yalikuwa maji ya kimataifa. Sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri Halmashauri tumeleta andishi, tunaomba shilingi milioni 130 kwa ajili ya kufanya usanifu ili vijiji vyote vya Ukanda wa chini katika Jimbo la Rombo viweze kupata maji.
Je, Wizara iko tayai kulishughulikia andishi hili ili litatue kabisa moja kwa moja shida ya maji katika Wilaya ya Rombo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa natambua kwamba Ziwa Chala lipo na tumeanza kulifanyia kazi. Lakini kufuatia matamshi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais mwezi uliopita kwamba sasa wahandisi kutoka Halmashauri watatekeleza miradi yao wakiwa wana ripoti kwa Katibu Mkuu. Kweli andiko tumeshalipokea naomba unipe siku mbili, siku mbili hizi tutatoa taarifa kwenye Serikali kwamba sasa…
...utekelezaji wa miradi utakuwaje, lakini ninayo taarifa kwamba lazima tutumie Ziwa Chala kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji pale Kilimanjaro kupitia ziwa hilo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, urithi mkubwa wa Taifa letu unapotea. Ngoma zetu zinapotea, lugha zetu za asili zinapotea, vyakula vyetu vinapotea. Wewe ni Chifu, unafahamu hazina kubwa ambayo Machifu walikuwa nayo, mavazi yao, vyombo vyao vya nyumbani, samani zao na vyote hivi vinaweza vikavutia utalii kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni kwa nini usiwepo mkakati wa kila Halmashauri au kila Wilaya kujenga jumba la makumbusho na kwa sababu hiyo Viongozi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kuhamasisha wananchi ili vitu vyote vya asili vikakusanywa, kwanza kwa ajili ya elimu ya watoto wetu, lakini kwa ajili pia ya kuvutia utalii ikiwa ni pamoja na kuleta mashindano ya ngoma za asili ambazo zina mafunzo mengi sana kwa Taifa letu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge mzuri sana ambaye amekuwa akifuatilia sana mambo ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niseme tu kwamba kama ulivyosema ni kweli kabisa tunayo mikakati mingi ambayo tunataka kuitekeleza. Lakini kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, kwa utaratibu wake aliyoanzisha wa kuhakikisha kwamba anashindanisha ngoma za asili, na hili ndilo tunalolitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi katika mkakati wa kuhakikisha kwamba hili tunalitekeleza, tumeamua kwamba mwezi wa Septemba kila mwaka, nchi ya Tanzania Mikoa yote, Halmashauri zote, zitakuwa zinasherehekea Mwezi wa Urithi wa Utamaduni wetu. Kwa hiyo, ngoma mbalimbali zitashiriki katika Kanda, katika Mikoa, kuhakikisha Watanzania wanakumbuka utamaduni wao. Nami ninaamini kabisa tukitekeleza hili kwa pamoja basi vitu vyote vile, mali kale zote zitaweza kubainishwa na kuweza kuelimishwa na wananchi wote wataweza kuvibaini vizuri kabisa. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Migogoro kati ya hifadhi zetu na wananchi itaendelea kwa muda, kwa sababu wananchi wanaongezeka, wanyama wanaongezeka, ardhi iko pale pale. Wanyama hawawezi kufanya uzazi wa mpango, lakini sisi tunaweza. Je, ni lini Serikali yetu itakuja na sera na mpango kabambe wa uzazi wa mpango kwa wanadamu ili tuweze kudhibiti ongezeko hili la watu ambalo linaweza likaathiri hata shughuli nyingine za kiuchumi kama afya, elimu na kadhalika? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba idadi ya wananchi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Wakati tunapata uhuru mwaka 1961 idadi ya Watanzania walikuwa ni milioni 10.3, sasa hivi mwaka 2018 idadi ya Watanzania tunakadiriwa kufika milioni 54.2. Kwa hiyo utakuta kwamba sasa idadi imeongezeka kwa kiwango kikubwa wakati ardhi imebaki vilevile haijaongezeka. Kwa hiyo na hii ina maana gani, ina maana tuje na mipango madhubuti ya kuhakikisha moja, tunadhibiti idadi ya ongezeko la watu lakini la pili, matumizi bora ya ardhi yetu tuliyonayo, ndiyo maana tumeweka mkazo katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili wazo la mpango wa uzazi wa mpango, naomba nilichukue kama Serikali tutalifanyia kazi kuhakikisha kwamba tunawahimiza Watanzania wote tuwe na uzazi wa mpango ili kusudi tuzae idadi ya watoto inayolingana na ardhi ile tuliyonayo. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Migogoro kati ya hifadhi zetu na wananchi itaendelea kwa muda, kwa sababu wananchi wanaongezeka, wanyama wanaongezeka, ardhi iko pale pale. Wanyama hawawezi kufanya uzazi wa mpango, lakini sisi tunaweza. Je, ni lini Serikali yetu itakuja na sera na mpango kabambe wa uzazi wa mpango kwa wanadamu ili tuweze kudhibiti ongezeko hili la watu ambalo linaweza likaathiri hata shughuli nyingine za kiuchumi kama afya, elimu na kadhalika? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba idadi ya wananchi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Wakati tunapata uhuru mwaka 1961 idadi ya Watanzania walikuwa ni milioni 10.3, sasa hivi mwaka 2018 idadi ya Watanzania tunakadiriwa kufika milioni 54.2. Kwa hiyo utakuta kwamba sasa idadi imeongezeka kwa kiwango kikubwa wakati ardhi imebaki vilevile haijaongezeka. Kwa hiyo na hii ina maana gani, ina maana tuje na mipango madhubuti ya kuhakikisha moja, tunadhibiti idadi ya ongezeko la watu lakini la pili, matumizi bora ya ardhi yetu tuliyonayo, ndiyo maana tumeweka mkazo katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili wazo la mpango wa uzazi wa mpango, naomba nilichukue kama Serikali tutalifanyia kazi kuhakikisha kwamba tunawahimiza Watanzania wote tuwe na uzazi wa mpango ili kusudi tuzae idadi ya watoto inayolingana na ardhi ile tuliyonayo. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Migogoro kati ya hifadhi zetu na wananchi itaendelea kwa muda, kwa sababu wananchi wanaongezeka, wanyama wanaongezeka, ardhi iko pale pale. Wanyama hawawezi kufanya uzazi wa mpango, lakini sisi tunaweza. Je, ni lini Serikali yetu itakuja na sera na mpango kabambe wa uzazi wa mpango kwa wanadamu ili tuweze kudhibiti ongezeko hili la watu ambalo linaweza likaathiri hata shughuli nyingine za kiuchumi kama afya, elimu na kadhalika? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba idadi ya wananchi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Wakati tunapata uhuru mwaka 1961 idadi ya Watanzania walikuwa ni milioni 10.3, sasa hivi mwaka 2018 idadi ya Watanzania tunakadiriwa kufika milioni 54.2. Kwa hiyo utakuta kwamba sasa idadi imeongezeka kwa kiwango kikubwa wakati ardhi imebaki vilevile haijaongezeka. Kwa hiyo na hii ina maana gani, ina maana tuje na mipango madhubuti ya kuhakikisha moja, tunadhibiti idadi ya ongezeko la watu lakini la pili, matumizi bora ya ardhi yetu tuliyonayo, ndiyo maana tumeweka mkazo katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili wazo la mpango wa uzazi wa mpango, naomba nilichukue kama Serikali tutalifanyia kazi kuhakikisha kwamba tunawahimiza Watanzania wote tuwe na uzazi wa mpango ili kusudi tuzae idadi ya watoto inayolingana na ardhi ile tuliyonayo. (Makofi)
MHE. JOSEPH R.SELASINI: Mheshimiwa Spika, katika awamu hii umezuka mtindo kwa baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwavua vyeo baadhi ya Walimu kutokana na sababu za shule zao kutofanya vizuri, kuwavua vyeo Madaktari na hata wengine kuwaondoa kazini. Sasa mtindo huu unavyoendelea tafsiri ya jamii inaonekana kwamba ni hatua ambazo ni mahususi zilizoagizwa na Serikali. Je, Serikali iko tayari kupitia maamuzi yote haya na kuwarejeshea hao Walimu au Madaktari haki yao kama ikithibitika kwamba walionewa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wako Walimu hasa ajira mpya na hawa wengi wako katika jimbo langu. Wanapoingia kazini hawapewi zile fedha subsistence allowance za kuwasaidia kabla hawajapata mishahara yao na nadhani hata maeneo mengine katika nchi yetu iko namna hiyo. Je, ni utaratibu gani ambao Wakurugenzi au Serikali inao wa kuhakikisha kwamba hao Walimu hawapati mateso wanapoanza kazi zao kwa mara ya kwanza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, ametaka kujua je, kuwavua vyeo kunakoagizwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Serikali iko tayari sasa kuwarudisha. Nilipojibu swali la msingi nilieleza kwamba nchi hii inaendesha kwa mujibu wa Sheria, taratibu na kanuni.
Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili ni kwamba yule aliyekuajiri wewe ndiye mwenye madaraka ya kukufukuza. Kwa hiyo, utaona kwamba mara nyingi wakigundua kwamba kuna makosa wanamsimamisha wakati wanasubiri yule mwenye madaraka ya ajira achukue hatua za mwisho.
Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge hili kama kuna mahali mtumishi amefukuzwa na Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya wakati yeye siye aliyemwajiri niletewe suala hilo nitalishughulikia mara moja, kwa sababu kwa taratibu zetu za kiutumishi yule aliyekuajiri ndiye anayekuadhibi na ndiye anayekufuza. Nimeeleza hapa jamani sisi siyo malaika, nimeeleza kwamba wakati mwingine tunapowateua tunawapa mafunzo. Hao wanaozungumzwa tumeshawapa mafunzo, naamini nadhani hata Bunge hili kama mnafuatilia maji yametulia katika mtungi siyo kama tulivyoanza huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, Walimu hawapewi subsistence allowance kabla, moja nataka niseme, Wizara yangu ya Utumishi kazi yake ni kuajiri, nikishaajiri nakwambia wewe nenda Wizara ya Maji, Wizara ya Ushirika na kadhalika, sasa yule tajiri wako ndiye anayekushughulikia. Hata hivyo, siku za nyuma imetokea ilifanyika miaka ya nyuma namna hiyo, watu wakawa wanafanya ndivyo sivyo anakwenda anachukua hela anasema anakwenda kuripoti halafu haendei.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tu kwamba kwa utaratibu tulionao sasa huingizwi wewe kwenye mfumo wa mishahara mpaka umefika, umeripoti, tuna uhakika kwamba huyu mtu kafika. Huo utaratibu unatuwezesha kupunguza udanganyifu mkubwa katika masuala ya ajira.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mara nyingi Mawaziri wetu hapa Bungeni wamekuwa wakituambia kwamba ahadi ya Rais ni sheria na lazima itekelezwe. Sasa kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Palestina kuwa Hospitali ni ahadi na agizo la Mheshimiwa Rais. Sasa ni kwa sababu gani badala ya Serikali kutekeleza ahadi hii, inafanya maboresho?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kituo cha Afya cha Tarakea katika Wilaya ya Rombo kinachukua wagonjwa wengi sana kutokana na eneo kubwa na wagonjwa wengine kutoka nchi jirani ya Kenya, lakini hakina incinerator, hakina mortuary, vilevile kilikuwa hakina uzio lakini Mbunge akajitahidi kwa fedha za Mfuko wa Jimbo kujenga uzio.
Sasa je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufika Rombo kutembelea kituo kile ili tushauriane naye namna ya kukiboresha kiweze kuhimili idadi kubwa ya wagonjwa ambao wanakwenda kwenye kile kituo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, Serikali tunakiri juu ya umuhimu wa Kituo cha Afya cha Sinza pale Palestina, lakini ni ukweli usiopingika kwamba ili Kituo cha Afya kiwe Hospitali ya Wilaya kuna suala zima la eneo ambalo katika jibu langu la msingi nimemwambia kwamba tunahitaji ekari 25. Sasa ukienda katika kile Kituo cha Afya cha Palestina, eneo hilo halipo na ndiyo maana katika maboresho ambayo yanaendelea ni pamoja na kutenga shilingi milioni 160 ili kuweza kuwa na hadhi ya kufanana na Kituo cha Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba tunapata changamoto katika Vituo vya Afya vilivyo Mijini, kitu ambacho kinakosekana ni jina lipi tutumie? Kwa sababu vinakuwa na hadhi zaidi ya Vituo vya Afya, lakini vinakuwa havijafikia kuwa Hospitali za Wilaya. Ndiyo maana nimesema kwamba ni vizuri Manispaa wakatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, kama Serikali tuko tayari na wala hatupingani na kile ambacho Mheshimiwa Rais alielekeza kwa wakati ule, lakini changamoto ya ardhi ndiyo inayotusababisha tuseme kwamba ni vizuri likatengwa eneo lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, Mheshimiwa Selasini anataka utayari wangu kwenda kutazama Kituo cha Afya Tarakea. Naomba nimhakikishie, kama ambavyo nimefanya ziara kwenda Kituo cha Afya cha Kiaseri kule, niko tayari kufika hata Tarakea kwa kadri muda unavyokuwa umeruhusu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pia niruhusu nimshukuru na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilimpelekea shida ya mpaka wa Kenya na Tanzania kule Tarakea, alikwenda kule amesaidia sana kuleta utulivu kule mpakani. Mheshimiwa Waziri namshukuru sana.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa sana eneo la Holili, viwanja vimegawanywa hovyohovyo, vimechukuliwa kiholela kabisa na ni tatizo la miaka zaidi ya 10. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, akipata tena nafasi, kama timu yako inaweza kwenda pale kuangalia uhalali wa namna ambavyo vile viwanja vimegawanywa kwa sababu, ni tatizo ambalo limeshindikana, Wakuu wote wa Mikoa wamejaribu wameshindwa. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikwenda Rombo, lakini tulikuwa na zoezi la kuangalia mpaka. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua kuweka mpaka wenye alama zinazoonekana kwa wananchi kati ya nchi ya Tanzania na Kenya, Wilaya ya Rombo ni Wilaya ya mpakani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli nilikwenda huko na nimekwenda mpaka Mkoa wa Mara na zoezi hili litazinduliwa na viongozi wa nchi hizi mbili hivi karibuni. Tumeweka mipaka ya alama mia mia, ili wananchi waweze kuona alama zile waweze kujua nchi yao ya Tanzania inaishia wapi. Kama tunavyojua kwamba, alama hizi zilikuwa zimewekwa kwa umbali wa kilometa elfu moja, mpaka elfu mbili, nyingine mpaka kilometa mia mbili mpaka mia tatu. Kwa hiyo, zilikuwa hazionekani na watu walikuwa wanaingiliana, wananchi wa upande mmoja walikuwa wanaingia upande mwingine bila kujua na wananchi wa upande mwingine walikuwa wanaingia.
Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa pongezi zake na tutaangalia hayo maeneo mengine, sina taarifa kamili hizo alizoniambia nitafurahi zaidi kama Mheshimiwa Selasini akiniandikia vizuri ili nipate message vizuri. Amezungumza kwa haraka sana lakini kwa kadri tutakavyolielewa,
tutalishughulikia. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kama sikosei taarifa ya mwisho ya Bodi hii ilitolewa katika kipindi cha pili cha Awamu ya Nne. Hii ni bajeti ya tatu tunaijadili katika Awamu ya Tano na tunasema katika awamu hii uchumi umekua. Naomba niiulize Serikali, ni lini Bodi hii itatoa ripoti yake ili kuwezesha kupandishwa mishahara ya wafanyakazi ambao hivi sasa hata morali yao inashuka kwa sababu ya hali ngumu ya maisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na mishahara, statutory increments ambazo ziko kisheria nazo hazitolewi. Ni lini takwa hili la kisheria litatolewa ili Serikali isionekane kwamba inavunja sheria ambayo tumejiwekea wenyewe? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la kwanza la lini ripoti ya Bodi ya Mishahara itatoka. Kwa mujibu wa kifungu cha 35(1) cha Sheria Namba 7 ya Mwaka 2004, Sheria ya Taasisi za Kazi imeelezwa uundwa wa Bodi ya Mshahara ambapo watapewa teams of reference na Mheshimiwa Waziri na baadaye kuwasilisha kwa ajili ya maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, navyozungumza hivi sasa kwa muda wa tangu mwaka 2015 Bodi hii imeshaundwa na taratibu ambazo zimewekwa ni kuhakikisha kwamba Bodi hii inapewa kwanza mafunzo na kwa mujibu wa sheria wanapewa nafasi ya kufanya kitu kinaitwa investigation kabla ya kwenda kumshauri Mheshimiwa Waziri. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, tumetenga fedha kwa ajili ya Bodi hii iweze kufanya kazi, kwa hiyo, naamini fedha hii ikitoka na wakimaliza kazi yao ripoti hii itawasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu annual increment, ni dhahiri kwamba na Mheshimiwa Mbunge anafahamu limekuwepo zoezi la uhakiki wa wafanyakazi ambalo kwa kiwango kikubwa sana lengo lake lilikuwa ni kujaribu kutengeneza mfumo mzuri wa utumishi wa umma na kujenga utaratibu mzuri wa Serikali katika kufanya mambo ambayo wamepangwa kwa ajili ya watumishi wa umma na mojawapo likiwa ni hilo la ongezeko la mshahara. Kwa hiyo, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu taratibu hizi zimeshafanyika na zinaendelea basi pale Serikali itakapokuwa tayari kwa maana kibajeti hilo takwa la kisheria litafanyika.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu katika nchi za nyingine Afrika Mashariki wako makini sana katika jambo hili na mashauri mengi yamekuwa yakiamuliwa kwa haraka tofauti na sisi. Kucheleweshwa kwa maamuzi ya mashauri haya kunaweza kukapelekea fikra kwamba rushwa inatumika zaidi katika kuamua haya mashauri. Sasa, je, ni lini Serikali itakamilisha huo mchakato wa kuongea na wadau ili maamuzi haya yaweze kufanyika haraka iwezekanavyo kunusuru maisha ya watoto wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sheria inataka mali za watuhumiwa wa madawa ya kulevya zitaifishwe. Uwezekano wa kuzitaifisha ndani ya nchi upo, lakini ni utaratibu gani unaotumika kutaifisha mali hizi kama ziko nje ya nchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu ya msingi, kinachofanyika hivi sasa ni wadau wa haki jinai ambao ni mhimili wa mahakama na pamoja na sisi upande wa Serikali kutafuta namna bora ya kuanza utekelezaji wa shughuli ya kushughulikia masuala ya kesi za madawa ya kulevya katika maeneo ya viwanja vya ndege na mipaka ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu jambo hilo ni la kisheria tunalifanya kwa umakini mkubwa. Hivi sasa ninavyozungumza tayari Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya na Jaji Kiongozi Feleshi wameshaanza mazungumzo ya kuja na namna bora ya kuweza kuwa na mahakama hizi ambazo zitakuwa tembezi, ili inapotokea kwamba kuna mhalifu yeyote amekamatwa na madawa ya kulevya basi aweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa utaratibu ambao unakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugumu unakuja kwa sababu ukiangalia kesi hizi nyingi za madawa ya kulevya zina masharti yake pia kwa maana ya kisheria. Kwa sababu ni kesi ambazo zinatakiwa zipitie hatua moja mpaka nyingine; kwa maana zinakwenda Mahakama Kuu na zikienda Mahakama Kuu maana yake ni kesi ambazo utaratibu umewekwa kwa mujibu wa sheria zianzie katika Mahakama za Mwanzo. Kwa hiyo si rahisi sana kufanya maamuzi hayo ya kiharaka, ndiyo maana tukasema kwamba kupitia utaratibu huu utarahisisha sana mashauri haya yaweze kusikilizwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge, imeanzishwa Mahakama ya Mafisadi kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria Na.3 ya Mwaka 2016 ambayo imeonesha tija sana na mpaka hivi sasa ninapozungumza tayari kesi 7,517 zimeshaamuliwa kwa uharaka sana na tunaamini kabisa zoezi hili likikamilika basi tutaweza kuwahudumia Watanzania kwa kuhakikisha kwamba wale wahalifu wote wanakamatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameuliza kuhusu namna ya utaifishaji wa hizi mali nje ya nchi. Nchi yetu imesaini makubaliano na tulishirikiana na baadhi ya nchi na tumekuwa na ushirikiano mzuri na nchi nyingi ambazo kupitia utaratibu wa makubaliano hayo, ikitokea suala la namna hiyo basi mamlaka zote mbili zinafanya kazi kuhakikisha kwamba mhusika ambaye mali zake ziko nje ya nchi pia utaratibu ufuatwe wa kisheria ili ziweze kutaifishwa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wabunge na Madiwani ni wawakilishi wa wananchi lakini mara nyingi baadhi ya Wabunge na Madiwani wamekuwa wakitoa taarifa za migogoro kati ya wananchi kwenye maeneo yao lakini matokeo yake ile migogoro inageuzwa Wabunge au Madiwani wanaonekana ni wachochezi wanakamatwa na kuwekwa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize Serikali, ni lini tabia hii itakoma Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wanapotoa taarifa ionekana kwamba taarifa hizo ni taarifa muhimu na za kufanyiwa kazi na ziheshimike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Vitongoji na Mitaa ni viongozi wa umma. Wanapotoa taarifa huwa zinapewa uzito unaostahili, isipokuwa tu kama kuna taarifa zingine ambazo zinakuja ku-counter kwamba labda wao wamehusika kwa njia moja au nyingine katika kusababisha mitafaruku iliyojitokeza hapo ndiyo hatua nyingine huwa inachukuliwa. Hata hivyo, taarifa zao huwa zinachukuliwa kwa uzito unaostahili na kwa heshima kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sema tu kwamba wenzetu wa Jeshi la Polisi kupitia Sheria ya Kanuni ya Adhabu wanao uwezo wa kufanya counter intelligence research kujua kwa kina tatizo hasa ni nini. Sasa wanaweza wakamshikilia kiongozi kwa muda ili waweze kupata taarifa za ziada, lakini kwa kweli kama watazidisha muda ambao wanaruhusiwa kukaa na viongozi kwa ajili ya mashauriano hiyo itakuwa wanafanya kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali lake ni la msingi na kwa kweli tutaliangalia kwa umakini zaidi ili kusudi kuweza kuweka mazingira mazuri zaidi. Sheria ya Kumlinda Mtoa Taarifa ipo na ilipitishwa na Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi wowote.