Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hassan Selemani Kaunje (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii kwa mara ya kwanza kuchangia katika Bunge hili, lakini nichukue dakika chache kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini vilevile kumpongeza Spika na Naibu Spika kwa ushindi wao, pamoja na wewe mwenyekiti kwa kushinda kuwa Mwenyekiti wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa nafasi ya kipekee, nimpongeze au niwapongeze wote walioteuliwa kuwa Mawaziri katika Baraza la Mawaziri katika Serikali hii ya Awamu ya Tano; lakini na wao niwatume vilevile wafikishe salamu kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba Mheshimiwa Kaunje, Mbunge wa Lindi anahitaji kupongezwa kwa sababu naye alinituma kazi mbili alipokuja kwenye kampeni Lindi na nilizifanya kwa ukamilifu. Kazi ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha natumbua jipu la Mbunge wa Upinzani katika eneo la Lindi Mjini na nilimwondoa. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhakikisha kwamba yeye anapata kura za kutosha na hilo nilihakikisha. Hivyo basi, hana budi naye kunipongeza kwa kazi hizo mbili nilizofanya kwa niaba yake. (Makofi)
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu ya kuchangia.
Kwanza nitachangia yale yanayohusiana na Jimbo langu, halafu kwa ujumla nitakuja tu kuzungumzia biashara ya korosho. Nitamwomba ndugu yangu, Mheshimiwa Mwigulu atakapokuja kufanya majumuisho aniambie kwa nini Lindi Mjini kama Jimbo na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi inakosa fungu la maendeleo ya kilimo wakati wakulima wapo katika Manispaa ya Lindi Mjini? (Makofi)
Pili, aniambie mkakati alionao wa kuwasaidia wananchi wa Kata ya Ng‟apa na Tandangongolo ambao wanazalisha nazi nyingi zinazoliwa Dar es Salaam tangu dunia ilipoanza mpaka leo lakini kiwanda cha kuwasaidia hakipo, na yeye ana mpango gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitamwomba atueleze Wanalindi ambao hatuli nyama ya ng‟ombe wala mbuzi, kwa nini Ranchi ya Taifa ya Ngongo ilifungwa na kama ana mpango wowote wa kuianzisha tena ili sisi ambao tunakosa nyama na kupata maumbo mafupi kama haya, tuweze kupata na warefu watokee Lindi? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anieleze vile vile ana mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa mwani ambao wanapatikana katika Ukanda wa Pwani ya Lindi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee azungumzie kiwanda kilichopo Lindi cha ubanguaji wa korosho ambacho ni kikubwa, atakavyoweza kusaidia kukifungua na wananchi wa Lindi waweze kupata ajira.
Nimkumbushe vilevile eneo la Lindi Manispaa lina ukanda wa bahari wenye urefu wa kilometa 104, lakini ukienda kwenye mapato ya Manispaa ya Lindi Mjini, kutokana na ushauri mbovu au maendeleo hafifu yanayotokana na Idara ya Uvuvi mapato kwa mwaka hayazidi shilingi milioni nne. Kwa maana ya kwamba kwa kila siku mapato ya Bahari ya Lindi hayazidi shilingi 1,000 katika kuchangia pato la Manispaa hiyo. Sasa anishawishi kwa nini tuendelee kubaki na wataalam wake wa uvuvi waliopo pale na namna gani asiweze kuwaondoa akatuletea wengine ambao waka-brand, wakautumia ukanda ule kuweza kuleta mapato katika eneo la Manispaa ya Lindi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza hayo, nichangie sasa kwenye eneo la zao la korosho. Kama ulivyomwomba Mbunge aliyekaa aeleze interest, na mimi nataka ku-declare interest kwamba pamoja na kuzaliwa Lindi kwenye zao la korosho lakini nimefanya kazi katika sekta ya korosho kwa miaka yote kabla ya kuja Bungeni. Kwa hiyo, nataka tu nieleze yale ninayoyafahamu ambayo yatachangia ku-boost hii sekta ya korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinachoitwa Mfuko wa Maendeleo ya Tasnia ya Korosho (CIDTF). Kama walivyoeleza Wabunge wengine Mfuko huu ndiyo ule wenye mamlaka ya matumizi ya almost shilingi bilioni 70 zilizotajwa na Wabunge waliopita. Ukichukulia matumizi ya fedha hizi kwa kila mwaka, unaweza ukakuta zinazotumika haziwezi kuzidi bilioni 30 kurudi kwa wakulima kwa maana ya pembejeo na mambo mengine. Ukija katika mipango yao, kila siku wameendelea kupanga mipango ya kujenga viwanda vya kuendeleza tasnia ya korosho au kubangua korosho zinazopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu nini? Nataka niwashauri, tunapozungumzia maendeleo ya tasnia ya korosho na wakulima wa korosho na wananchi wanaotegemea korosho, haimaanishi tu yanatokana na uwepo wa pembejeo na ubanguaji wa korosho. Wakulima wale wataona korosho ina tija pindi tu korosho ile itakapoweza kuwasaidia kutibiwa, kupata elimu, kuondokana na madhila ya benki, kwa maana ya kwamba uwepo wa fedha wa kuweza kuwakopesha kipindi cha ununuzi, lakini pale inapotokea anguko la korosho, basi fedha ziwepo za kuweza kufidia wakulima. Mambo haya yote yanawezekana katika suala la korosho kwa sababu fedha hizo zipo na vitu hivyo vinaweza kufanyika. Kwa sababu katika Tanzania hili ndilo zao lililo huru linaloweza kujiendesha lenyewe kutokana na fedha zinazopatikana. (Makofi)
Kwa hiyo, nilikuwa ninamwomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na mambo mazuri yanayofanywa na CIDTF hebu awaelekeze wapanue wigo wa maendeleo ya zao la korosho na wakulima wa korosho, haiishii tu kwa kuwapelekea pembejeo na mpango usiokwisha wa kujenga viwanda; waangalie maeneo mengine ambayo yanaweza yakawasaidia. Wakulima wa korosho hawazidi 500,000. Kwa mwaka wakiamua tu kuwachangia katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, shilingi bilioni tano wananchi wote wanaolima zao la korosho watatibiwa katika familia zao. Inawezekana katika shilingi bilioni 70 wanazochukua. Mambo haya tunapaswa tuwashauri na wayafanye kwa ajili ya maendeleo ya zao la korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nilipenda tu nishauri katika sekta ya ushirika. Tumekuwa tunalalamika Wabunge hapa kuhusu ushirika, lakini tujiulize dhana ya ushirika na wanaushirika ni nani ili nao tuwaombe msaada?
Mwanachama wa Chama cha Msingi kilichopo Lindi analeta malalamiko kwa Mheshimiwa Waziri amsaidie kuvunja Bodi ya Chama cha Ushirika, lakini Chama kile cha Ushirika amekiunda yeye katika Mkutano Mkuu. Kwa nini wanachama hawa wasiweze kuziondoa bodi zao? Kwa hiyo, ni lazima tuwaelimishe. Kuna vitu vingine au kuna majipu mengine tunataka watatue wengine wakati sisi wenyewe tuna uwezo wa kuyatatua kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe wito kwa wakulima, nitoe wito kwa wanaushirika katika vyama vyao kujaribu kutatua matatizo yao bila kusubiri Serikali ije kufanya kwa niaba yao kwa sababu watu waliyokuwepo katika Uongozi ule wamewaweka kwa matakwa yao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza haya, nakushukuru kwa kuniona kwa mara ya kwanza kuweza kuchangia. Ndiyo salamu za Lindi zimeanza na ninakuomba kila utakapokalia Kiti hicho usinisahau mimi kuniita na kuweza kuchangia katika Bunge hili. Naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Lakini kwa utamaduni wa Kitanzania unapofanyiwa jambo jema ni vizuri ukatoa shukrani, na shukrani zangu za dhati, ziende kwa Profesa Muhongo, REA, TANESCO Lindi, lakini vilevile TANESCO zone ya Kusini kwa kushughulikia tatizo la umeme katika kata mbili za Ng‟apa na Tandangongoro ambazo zimepitiwa na bombala gesi lakini umeme ulikuwa haujafika. Wamelitatua tatizo hili na ninawashukuru na kuwapongeza sana kwa juhudi hizo walizozifanya.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninataka nizungumze especially kwenye suala moja tu la LNG inayoenda kujengwa Lindi. Na ningemuomba Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa umakini ninayotaka kuyazungumza kwa sababu, kuna ninayotaka kuyashauri ya msingi sana ambayo anapaswa kuyachukua kuanzia sasa anapoanza safari ya kuelekea katika uwekezaji wa kiwanda hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 35 wa hotuba yake ameomba tuidhinishe shilingi milioni 800, anaenda kufanya maandalizi ya uchoraji wa ramani ambayo itaingia katika Mipango Miji katika Manispaa ya Lindi ya kiwanda hiki anachotaka kujenga, lakini vilevile maandalizi ya uwanja wa ndege wa Lindi kwa ajili ya programu inayokuja. Sasa wakati anayafanya haya nimuombe Mheshimiwa Waziri aende sambamba na kulipa fidia kwa wakazi ambao wanaoondoka katika eneo ambalo litaguswa na mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimuombe Mheshimiwa Waziri afanye yafuatayo katika eneo hilo, anaenda kuandaa mchoro wa kiwanda, ila eneo la Lindi Manispaa halina master plan ya Mji, kwa hiyo, aongee na Waziri mwenzie anayehusika na master plan wahakikishe master plan ya Mji wa Lindi inapatikana kabla ya michoro hiyo inayoenda kuandaliwa na kuingizwa haijaweza kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo anaenda kuyafanya hayo anayotaka kuyafanya, atusaidie kutupelekea pesa zetu kwa kumwambia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwamba zoezi la kuandaa mpango kamambe huu ambao ni master plan unakwama kutokana na kuzuiwa kwa zaidi ya shilingi milioni 700 ambazo ni retention money ambazo ziko kwake zinazotokana na uuzwaji wa viwanja. Tupelekee fedha hizi katika Manispaa ya Lindi, ili tuweze kuandaa mpango kamambe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, anapeleka mradi huu ambao unatarajiwa kupeleka zaidi ya wafanyakazi na watu wengine watakaokadiriwa kuwa 20,000 na Mji wa Lindi una watu takribani 100,000 kwa hiyo, unapopeleka watu 20,000 ni idadi kubwa ya watu. Lakini wananchi wa Lindi wana matumaini makubwa na mradi huu unaenda kutatua, historia yao inaenda kufutwa ya umaskini uliokithiri kupitia ajira zitakazotokana na mradi huu, lakini watu wa Lindi wana tatizo moja kubwa la kihistoria, umaskini wao ni pamoja na kukosa elimu, hawana elimu, yanayoendelea katika mradi huu hata yaliyoanza sasa hivi ajira zile ndogo ndogo za maandalizi wanashindwa kupata kutokana na kukosa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, anapopeleka kiwanda hiki ambacho ujenzi wake utakamilika sio chini ya miaka kumi kutoka sasa hivi, basi aungane na Waziri wa Elimu kuweza kuandaa mpango utakaowafanya wananchi wa Lindi waweze kuwa na sifa hitajika na kuingia katika ajira zitakazotokana na kiwanda hiki pale kitakapokamilika. Nasema hivi mpango uwe maalum kwa sababu Serikali kwa mara nyingine au mara zingine imeshawahi kuchukua hatua stahiki za kusaidia baadhi ya maeneo kutatua kero zinazowasumbua especially za elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona maeneo yale ya Wamasai ilipelekwa programu maalum ya kuwafanya wasome, lakini vilevile kwenye maeneo ambayo ukeketaji kulikuwa na shida, Serikali ilichukua jukumu maalum la kuhakikisha kwamba tatizo hili linaondolewa. Nimuombe yeye na Waziri husika na Serikali kwa ujumla, wananchi wa Lindi walio wengi hawana elimu na uwezo wa kuweza kufanya kazi katika kiwanda hiki kitakapokamilika, tuwasaidie kwa kuanza na programu hii anapoanza sasa kuelekea kule kukitengeneza kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tulisimama hapa Mbunge mwenzangu wa Nachingwea, aliomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda apeleke wawekezaji watakaoweza kuwekeza processing ya samaki kwa sababu tuna ukanda wa kilometa 112 Lindi Mjini ambazo ni za bahari. Na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alisema tusiwahishe shughuli anatuletea kwanza viwanda vya mihogo; lakini lengo letu la kuzungumza viwanda vya samaki tunamaanisha kwamba kuna wavuvi ambao watahitaji soko lile na kwa sababu tunapeleka watu ambao watakuwepo katika kiwanda hiki, tunapaswa tujipange na tuwawezeshe wavuvi hawa waweze kuwa na soko la uhakika, ili waweze sasa na wao kuingia katika uchumi unaoenda wa kiwanda hiki cha gesi. Nimuombe basi, amwambie Waziri pamoja na kiwanda cha mihogo ambacho anatupelekea, basi atusaidie kutupelekea watu watakaowekeza katika sekta ya samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika eneo lingine. Eneo hili nataka nishauri kwa ujumla katika mambo yanayohusu uchumi wa Taifa ambao unaendana na Wizara hii ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ununuaji wa mafuta wa jumla ambao kwa kifupi unaitwa BPS. Na katika uagizaji ule wa mafuta makampuni yanayoleta mafuta ambayo yana zabuni ile mengi yamekuwa registered nje ya Tanzania.
Matokeo yake kwamba makampuni yale yanakwepa baadhi ya kodi ambazo zingepaswa kulipwa kama tu wange-register BRELA, Tanzania. Nimuombe Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi jambo hili, ili kampuni hizi zinazoingiza mafuta ziweze kulipa kodi stahiki ambazo zitaendeleza Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo kuna jambo la vinasaba vya mafuta vinavyowekwa katika mafuta tunayoyatumia. Jambo hili linapigiwa kelele na wadau tofauti, wazo langu ni lifuatalo; Mheshimiwa Waziri lengo la kuweka vinasaba katika mafuta tunayoyatumia ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na mafuta salama kwa ajili ya vyoimbo vyetu. Kuna wadau wanaozungumza kwamba jambo hili si zuri. Tunaweza tukaungana nao mkono, lakini tutaungana nao mkono tu pale tutakapohakikishiwa usalama wa vyombo vyetu, hivyo nimshauri Mheshimiwa Waziri jambo hili liendelee mpaka suluhu yake itakapopatikana na kuonekana jambo hili linaweza kutatuliwa kwa namna nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyazungumza haya nimuombe Mheshimiwa Waziri asiponijibu vizuri lini atawalipa fidia wananchi wa Mbanja, wananchi wa Likong‟o, wananchi wa Kikwetu kupisha ujenzi wa kiwanda chake, nakusudia kuondoa Shilingi katika bajeti yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa wasaa huu wa kuchangia katika Wizara hii. Ahsante sana.