Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Selemani Said Bungara (10 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amenipa mimi umaarufu na kuwa Selemani Bungara Bwege, pia kwa kukupa Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa mjanja kwa hiyo, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, nawashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Kilwa Kusini, mwaka 2010 nilishinda kwa kura 500 kuna watu wakasema wewe umemuonea tu Madabida nitamwita Mhindi Bin Asineni, mwaka huu nimempiga kwa kura 5,595. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba CCM mjiandae mumlete mgombea mwingine nimpige tena. Kwa mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili mambo mengi yamesemwa hapa, lakini naomba vijana wangu wa upande wa UKAWA msiwe na wasiwasi, humu ndani sasa hivi hatupambani na Serikali ya CCM, humu tunapambana na Serikali ya Magufuli na tunapambana na Serikali ya Mapinduzi, CCM hamna Tanzania sasa hivi, hii ni Serikali ya Magufuli na Serikali ya Mapinduzi.
Sasa mkitambua kwamba tunapambana na Serikali ya Magufuli, tusimlaumu sana Magufuli kwamba ndiyo kwanza anaanza na wamekubali wenyewe Serikali ya CCM kwamba tulifikia hapa na udhaifu huu ni kwa ajili ya Serikali iliyopita ya CCM, hii sasa ni Serikali ya Magufuli. Kwa hiyo, tutamwona Mheshimiwa Magufuli kwa miaka yake hii mitano atafanya nini akishindwa na yeye tutamwajibisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nawashukuru sana vijana wangu wa UKAWA tushirikiane tuzidi ili 2020 tuielekeze kibla Serikali ya Magufuli maana yake CCM tena hakuna nchi hii. Waheshimiwa nimepokea pole, kuna watu hapa wametaka kulia hapa eti kwa sababu…
Bunge lisioneshwe live wanataka kulia, aah, mimi nilifikiri wanataka kulia kwa sababu watu hawapati maji vijijini…
TAARIFA....
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa siipokei kwa sababu anapingana na mwenyewe Mheshimiwa Magufuli, kila siku anasema kwamba Serikali yangu, wakati mwingi anasema Serikali yangu hasemi Serikali ya CCM, kwa hiyo siipokei taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu bado saba ilikuwa tatu tu, narudia kusema kwamba napenda sana Wabunge msililie kwamba Bunge lisioneshwe live mlie kwa kuwa watu hawapati maji, hawapati tiba vizuri, hawapati elimu. Nashangaa sana mtu anayelia anaomba kulia, mimi ninavyojua kulia kuna mambo mawili tu, utamu au uchungu, na ukipata utamu au uchungu huombi kulia unalia tu, ukimwona mtu anaomba kulia au anatamani kulia hataki kulia huyo. Ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naanza na mambo ya viwanja vya ndege, katika kitabu ukurasa wa 99 nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwamba anaanza mchakato katika Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko, nimefurahi sana, lakini Uwanja wa Kilwa Masoko walikuja kutathmini mwaka 2013 na tathmini ya uwanja ili upanuliwe bilioni mbili, milioni themanini, laki nne na sitini elfu mia mbili na sitini mpaka leo, wametathmini watu wale hawajawalipa. Leo wanasema wanafanya mchakato ili wapanue sasa kabla bado hawajafanya mchakato huo wakawalipe wapiga kura wangu, 2,080,460,260, mkawalipe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013/2014, 2015/2016, wanawaambia wasiendeleze majumba wala wasilime mashamba yao mwaka wa tatu sasa hivi au wa nne. Naomba sana katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri aniambie kwamba lini watakwenda kuwalipa wale watu ili waendelee na mchakato wa kuupanua uwanja huo. Kama hawakuniambia lini wanataka kuwalipa nashika shilingi. Najua mtapiga kura nyinyi mko wengi, lakini shilingi mimi nitaishika safari hii isipokuwa katika majumuisho yake akiniambia watawalipa lini kesi imekwisha kwa sababu Serikali ya Magufuli ndiyo kwanza inaanza, sisemi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili barabara, katika ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyepita kulikuwa na ahadi ya barabara ya kwa Mkocho – Kivinje, lakini mpaka leo. Mheshimiwa Majaliwa alikuwa Waziri akasema kabla ya Uchaguzi, uchaguzi umekwisha, naomba Waziri Profesa, Msomi leteni hela hizo barabara ya kwa Mkocho – Kivinje ijengwe, maana yake kuna watu hapa wa CCM wanasema Majimbo upinzani usipeleke hela, jamani ehee mimi nilipata kura elfu kumi na tano, Asineni elfu kumi, Mheshimiwa Magufuli alipata elfu kumi, Mheshimiwa Lowassa alipata elfu kumi na nne, haya hizi elfu kumi za Mheshimiwa Magufuli ndiyo zimemfanya yeye ashinde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukisema kwamba Jimbo la Kilwa huleti maendeleo kwa sababu Magufuli hakushinda mnawaumiza elfu kumi waliomchagua Magufuli, haki sawa kwa wote timizeni. Sina wasiwasi, kama hamkuleta hayo nitashinda zaidi kwa sababu kila ukimuumiza mtu wa Kilwa basi anazidi kupata uchungu anaipiga CCM, leteni Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nangurukuru – Liwale itiwe lami, sisemi sana amesema Mheshimiwa Bi Lulida hapa, Naiwanga – Nainoko – Ruangwa mtengeneze, mjenge. Kilanjelanje na Njilinji mmepanga milioni 85, jamani ehee milioni 85 haifai, haitoshi tuongezeni hela, mvua ya mwaka huu, mafuriko ya mwaka huu barabara yote imekufa tunaomba hela iongezwe, naomba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, siisemi sana Serikali ya CCM kwa sababu tayari ishashindwa na wenyewe Mawaziri mmesema kwamba Serikali yetu ilikuwa dhaifu, ilikuwa haikusanyi hela, ilikuwa hivi, lakini Serikali ya Magufuli inakusanya hela haina udhaifu, wala siilaumu Serikali ya CCM iliyopita, najua nitailaumu Serikali ya Magufuli mwakani siyo mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kuna vijiji kumi havina mawasiliano ya simu Nainokwe, Liwitu, Kikole, nawaomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri watuletee mawasiliano watu wapige simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya, bandari, nimeangalia humu Bandari ya Kilwa haipo, lakini gesi ya Kilwa akisimama Mheshimiwa Muhongo hapa, gesi ya Kilwa italeta mambo, ehee, lakini watu wenyewe wa Kilwa thuma amanu thuma kafara. Naomba bandari nayo muiangalie, sasa gesi hiyo mngeipitisha wapi? Naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, sisi watu wa Kusini mnatuonea, maendeleo yote mnawapa watu wenye maneno mengi tu huku. Sisi wengine hatujui kusema, wanyonge, tunaomba Serikali ituangalie. Kuna mradi wa maji, kuna wafadhili kutoka Ubelgiji, basi mpaka leo hawataki kutuletea, tangu mwaka 2014, Mbelgiji amesema anatuletea maji hamtaki kutuletea maji. Kwa sababu gani, sisi watu wa Kusini tu! Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amani iwe kwa Mheshimiwa Waziri. Awali ya yote napenda kumshukuru Allah (SW) kwa kuniwezesha kuwepo leo hii na nikiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwake ni malipo ya wananchi wa Mji Mdogo wa Kilwa Masoko Sh.3,662,108,122.00 kwa ajili ya fidia. Mheshimiwa Waziri naomba asimamie madai yetu hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini awali ya yote, napenda kukupongeza kwa kuchaguliwa tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Wizara nyeti na muhimu katika Tanzania yetu. Mwenyezi Mungu akuzidishie busara na hekima.
Pia napenda kukupongeza kwa katika hotuba yako ukurasa wa 36 mpaka 37 kwa kuturejeshea mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea, mradi utakaogharimu Dola za Kimarekani bilioni 1.98 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 411.24. Natoa shukrani kwa Serikali kwa kutupatia mradi huu mkubwa kwa maendeleo ya Kilwa na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo, Jimbo la Kilwa Kusini, pamoja na gesi inatoka katika Jimbo la Kilwa Kusini lakini katika mradi wa umeme vijiji REA, kwenye Jimbo la Kilwa Kusini ni Kijiji kimoja tu cha Matanda ndicho kimepata umeme katika mradi wa REA. Mheshimiwa Waziri naomba vijiji vifuatavyo vipate umeme wa REA: Pande, Mtilimita, Namwando, Nakimwera, Nangao Malalani (Kata ya Pande), Rushungi, Kisongo, Ruyaya, Lilimalya Kaskazini na Kusini, Namakongoro (Kata ya Linimalyao), Makangaga, Nakia, Nanjilinji „A‟ na „B‟ (Kata ya Nanjilinji), Likawange, Mirawi, Nainokwe (Kata ya Likawaga) Kilole, Ruatwe, Kisangi, Kimbarambara (Kata ya Kikole).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wilaya ya Kilwa Jimbo la Kilwa Kusini ndilo Jimbo litowalo gesi asili kwa heshima na taadhima lipewe kipaumbele katika mradi wa umeme vijijini. Natanguliza shukrani. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuwezesha wewe kuwa Mwenyekiti wa kikao hiki na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa Urais Mheshimiwa Magufuli na kuapa kwamba atailinda Katiba ya Jamhuri ya Tanzania, lakini kwa bahati mbaya tu Katiba yenyewe kidogo anaipindisha pindisha kwa sababu hatoi haki kwa Vyama vya Siasa kufanya mikutano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si nimetoa shukrani? Mimi nimetoa shukrani tu wala sikumtukana mtu yeyote. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa shukrani hizi kwa Mwenyezi Mungu leo najielekeza kuchangia katika sehemu mbili tu katika hotuba hii. Tunakumbuka 2010 Rais aliyemaliza muda wake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Mungu amzidishie, aliahidi kwamba katika kampeni yake ya 2010 aliahidi kwamba atatengeneza barabara ya Kwa Mkocho – Kivinje barabara ya kilomita 4.2 kwa kiwango cha lami, mpaka leo nisemavyo barabara kwa mvua za jana tu na juzi gari zilikuwa hazifiki katika Hospitali ya Wilaya kutokana na barabara hiyo kuwa chafu na haipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya 2016/2017, tulitenga milioni 800 kwa ajili ya barabara hiyo ili ikamilike kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa hivi nisemavyo ndege zimenunuliwa lakini fedha hizo za bajeti hazijaingia katika Wilaya ya Kilwa ili barabara hiyo itengenezwe. Pamoja na ndege mlizonunua hizo lakini mkumbuke kwamba kuna barabara ambazo ni muhimu sana zinaenda katika hospitali za Wilaya, nazo zikumbukwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naomba hizo milioni 800 zipatikane ili babaraba ile iishe. Tena kwa bahati nzuri tarehe 2 Machi, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Dkt. Magufuli alifika Kilwa na nikamwambia tatizo hilo kwamba kuna kiporo cha Rais aliyepita na nikamwomba kiporo hicho amalizie yeye. Akaahidi na kumuagiza Injinia kwamba hiyo barabara iishe.

Naomba sana naomba, kwa kuwa Mheshimiwa Magufuli hasemi uwongo na alisema kwamba barabara lazima naomba barabara hiyo iishe ili watu wapate kutumia barabara hiyo na kufika katika hospitali kwa njia ya usalama. Bila hivyo watu wa Kivinje na Wilaya ya Kilwa kwa ujumla tutaona kwamba hatutendewi haki tunaonewa bila sababu ya msingi. Naomba Mheshimiwa Waziri barabara hiyo iishe na fedha hizo milioni 800 zipatikane katika mizezi mitatu iliyobaki ili barabara hii iishe. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni uwanja wa ndege. Kilwa Masoko kuna uwanja wa ndege, uwanja huo kulifanywa tathmini kwa wananchi wangu tarehe 19 Machi, 2013 ili walipwe fidia ili uwanja upanuliwe. Mpaka leo ninavyoongea tangu 2013 mpaka leo 2017 wananchi wangu hawajapata fidia. Naomba sana katika kuhitisha hotuba yake Mheshimiwa Waziri atuambie hawa wananchi wangu watapata lini fidia hiyo ya uwanja wa ndege na kama haiwezekani mseme kwamba haiwezekani.
heshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ingawa dakika tano hazijatimia lakini imeeleweka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwingi wa huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Rais katika Serikali ya Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Kikwete aliahidi kujenga barabara ya Singino (Kwamkocho) - Kivinje ya urefu wa kilometa 4.2, barabara hiyo inaelekea katika Hospitali ya Wilaya. Ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kwa umuhimu wa barabara hiyo ya kiwango cha lami, lakini kwa bahati mbaya mpaka leo, hiyo barabara ni tatizo. Katika bajeti ya 2016/2017, ilipitishiwa sh. 800,000,000/= kwa ajili ya kumalizia barabara hiyo lakini hadi leo hakuna kilichopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, mwaka huu wakati alipotutembelea nilitoa kilio changu hiki cha barabara ya kiwango cha lami katika Hosopitali ya Wilaya. Alimwagiza Meneja wa TANROAD Mkoa wa Lindi amalize kero hii ya muda mrefu. Kwa heshima na taadhima naomba fedha ya bajeti ya 2016/2017, sh. 800,000,000/= zipatikane ili mradi huu wa barabara muhimu ya Kwamkocho - Kivinje ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, pia asimamie agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli aliyoagiza Nangurukuru kuwa Meneja wa TANROAD kuwa awasiliane na Wizara ili kero hii imalizike. Naomba kwa heshima na taadhima asimamie barabara hii muhimu kwa ajili ya faida ya kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaona katika bajeti hii mwendelezo wa Uwanja wa Ndege na Bandari ya Kilwa Masoko. Naomba katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri anipatie taarifa ya Uwanja wa Ndege na Bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vile vile Mheshimiwa Waziri anifahamishe, malipo ya wananchi waliotathminiwa katika eneo la Uwanja wa Ndege. Katika majumuisho yake napenda kujua malipo ya wananchi hawa kwa muda sasa wa miaka mitatu hawajalipwa, ni lini watalipwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda kusisitiza:-

(a) Barabara ya Kwamkocho – Hospitali, ambayo ni ahadi ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Kikwete.

(b) Bandari na uwanja wa ndege.

(c) Malipo ya wananchi waliotathminiwa katika eneo la Uwanja wa Ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufafanuzi katika hizo kero zangu na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukurani kwa kunipa nafasi hii ili nichangie. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi ili tuitumie sisi binadamu katika maendeleo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya maji na kila kiumbe ana asili ya maji, sisi binadamu tumepatikana kutoka na asili ya maji. Hata hivyo miaka 56 ya Serikali ya CCM tunazungumzia habari ya maji. Tunakwenda vijijini kuomba kura ajenda yetu kubwa ni kwamba mkinichagua kuwa Mbunge mtapata maji, miaka 56.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema Mheshimiwa wa Mtama hapa, Ilani ya CCM mliwaahidi Watanzania kwamba mtapata maji kutoka asilimia 67 mpaka 85. Mimi Jimbo langu au Wilaya yangu ya Kilwa maji vijijini ni asilimia 48.3. Tunaomba sana maji safi na salama. Tunaomba sana, bajeti ya maji lazima iongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa 2016/2017 tulipangiwa au tulipitisha bajeti ya bilioni mia tisa hamsinitukapata asilimia 19, mwaka huu bilioni mia sita sasa ukipata asilimia 16 utajua mwenyewe itakuwa shilingi ngapi maana itapungua. Naomba sana bajeti hii ya maji irudi iende ikaongezwe fedha kama zilivyoongezwa mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia Mradi wa Maji wa Mavuji. Katika bajeti ya 2016/2017, ukurasa wa 142 kulikuwa na mradi wa maji katika Mji wa Kilwa Masoko. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa chanzo, mitambo ya kusafishia na kutibu maji, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa matanki, ukarabati wa upanuzi wa mabomba ya kusambaza maji. Mahitaji ya fedha euro milioni 61.67. Maelezo, majadiliano ya Serikali na Ubeligiji kupitia kampuni ya Aspec international yanaendelea. Usanifu umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya! Nataka nijue toka kwa Mheshimiwa Waziri, mazungumzo kati ya Aspec na ninyi yameishia wapi? Mradi huu ungesaidia upatikanaji wa maji katika miji midogo miwili ya Kilwa Kivinje na Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, lakini sasa hivi ni miaka mitano maneno tu, maneno tu, kesho, kesho kutwa, kucha maneno tu. Oh haa! Mheshimiwa Waziri leo nataka aniambie mchakato huu umefikia wapi ama sivyo kwa mara ya kwanza nataka nitoe shilingi;.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana. Serikali ya CCM kwa miaka 56 imeshindwa, tunataka kuiangalia Serikali ya Magufuli, maana Serikali CCM haipo, sasa hivi kuna Serikali ya Magufuli. Tunataka tuione Serikali ya Magufuli kwa miaka hii mitano itamaliza tatizo la maji? Kama haikumaliza tatizo la maji katika Tanzania, basi Magufuli bye bye (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali ya Magufuli ikishindwa kutatua tatizo la maji bye bye mwaka 2020, kwa herini. Waheshimiwa maji si mchezo, huwezi kuishi bila maji, huwezi kulala na mama bila maji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, bila maji hakuna kila kitu, watoto hawapatikani bila maji. Tunaomba hilo jambo la maji na hii bajeti lazima irekebishwe ili Watanzania tupate maji. Naunga mkono kabisa; utampata wapi mtoto bila maji? (Vicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kule Kilwa kuna mradi wa maji tangu mwaka 1992, Kilwa sehemu ya Mpala. Watu walitathminiwa lakini tangu 1992 mpaka leo hawajalipwa fidia, mpaka leo! Maji wameyachukua Mpala wameyapeleka Masoko lakini Mpala penyewe pale maji hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana katika majumuisho leo Mheshimiwa Waziri aniambie watu wa Mpala fidia yao watalipwa lini? Naomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji alikuja Mpala na akawaahidi watu wa Mpala kwamba lazima hela zao watapata, nataka nijue leo Serikali sikivu ya Mheshimiwa Magufuli mtoe kauli leo nisikie kama si hivyo sijapata jibu sawasawa nasema kweli Serikali ya Mheshimiwa Magufuli si Serikali sikivu. Kama sikivu kweli nijue kwamba watu wale fidia zao zimetoka au zitatoka lini. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, naomba sana msimtie aibu Mheshimiwa Magufuli, Magufuli ni mzuri pengine wabaya ni ninyi hapo. Magufuli mzuri ana tatizo moja tu, anabinya demokrasia, hapo tatizo analo, lakini mengine hana matatizo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana; kuna matatizo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. Naomba kujua ahadi ya Rais ya barabara ya Kwa Mkocho – Hospitali ya Wilaya ya Kilwa na ahadi ya Rais ya kujengwa kiwango cha lami kilometa nane katika Mji Mdogo wa Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua malipo ya wananchi waliothaminiwa katika maeneo ya mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko. Naomba kwa heshima na taadhima wananchi hao walipwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua Bandari ya Kilwa Masoko upo mpango upi wa kuiendeleza kwa kuwa ni bandari muhimu hasa kwa kuwa upo mpango wa kujengwa kiwanda kikubwa cha mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa kihistoria wa Kivinje miundombinu ya barabara ni mibaya. Mifereji, barabara na madaraja ya Mji Mdogo wa Kivinje, hakuna bajeti wanayopanga. Naomba Mji Mdogo wa Kivinje utengewe fedha za kujenga miundombinu ya barabara, mifereji na madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Masoko tuna kiwanja cha ndege. Kutokana na Mji wa Kilwa Masoko na Kilwa kwa ujumla kukua ni muhimu kuimarishwa na kupanuliwa kwa uwanja huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naomba Mheshimiwa Waziri azingatie maombi na ushauri wangu. Natanguliza shukrani, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimefurahi sana kwa kuwa umerudi salama kutoka katika matibabu, tunakuombea Mwenyezi Mungu afya yako izidi kuimarika na Inshallah itaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia sana habari za siasa na hususan hali ya kisisasa katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye utangulizi pale, misingi ya Katiba na kwa kuwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, undugu na amani. Kwa hiyo, Katiba yetu inazungumzia uhuru na haki ndiyo jambo la kwanza ili nchi yetu tuwe na mapenzi, kupendana, undugu na amani, lakini kama nchi yetu haitokuwa na uhuru na haki undugu na amani hautokuwepo katika nchi yetu, ndiyo msingi kwa Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia yetu ni nchi yetu na jamii yetu ijengwe kwa msingi huo, kwa hiyo kwa msingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake huamini Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na Mahakama iliyowakilisha kwa nchi pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wa saba inasema, nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu ili hali mimi kwa utafiti wangu naona hizi habari siyo za kweli kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina matatizo sana, kama hatukubali kama nchi ina matatizo naomba tutegemee kwamba nchi yetu huko mbele tunakokwenda hali itakuwa mbaya sana. Mimi mwenyewe nilimuandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani, kuna gari Noah ilifika Kilwa tarehe 29 Novemba, ikampigia simu kijana mmoja anaitwa Abdallah Said Ngaranga wakamwambia njoo uchukue mzigo wako hapa Kilwa Masoko, Mheshimiwa Abdallah Ngaranga alifuatana na Mheshimiwa mmoja anaitwa Hamisi Mtori, kufika pale Kilwa Masoko ile gari ya aina ya Noah nyeusi wakamuita yule kijana njoo ndani uchukue mzigo, alipoingia ndani yule kijana, kijana wa pili akawa yuko nje alivyoingia ndani wakamuita na yule wa pili, yule wa pili kaona hata Noah hii nyeusi siielewi akakimbia na askari mmoja akamkimbiza yule kijana akaingia katika makapa akapiga risasi yule askari, lakini jamaa hakusimama, akaondoka akafika Kivinje.

Mheshimiwa Spika, nikaitwa mimi kwamba mtu wetu mmoja katekwa, kwa bahati nzuri nikapiga simu Polisi Masoko nikaambiwa kwamba kweli yule kijana amekamatwa yuko polisi hapa. Usiku huo wakakamatwa vijana tisa, nikaenda polisi siku ya pili nikaambiwa kweli vijana walikamatwa walikuwepo hapa, lakini hatuwezi kuwaandikia kwa sababu walikuwa wamepitia tu. Nikaandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, katika vijana hao 11 wakarudishwa tisa na mpaka sasa hivi wako Kilwa, lakini wawili hawajarudishwa mpaka leo. Mmoja anaitwa Ndugu Ally Mohamed Shali na mwingine anaitwa Ndugu Yussuf Kipuka mpaka leo hawajarudishwa, lakini tuna uhakika walichukuliwa, walikuja kituo cha Polisi Kilwa Masoko mpaka leo hawajarudishwa na wazazi wao hawajulikani wapi walipo.

Mheshimiwa Spika, hii ni ukweli kabisa ninataka leo Waziri atupatie vijana wetu wawili hawa, ushahidi upo tarehe 21 Julai, askari hao hao walikwenda Kijiji kimoja cha Chumo wakaenda msikitini usiku saa saba, wakapiga risasi msikitini mle, wakawachukua watu 10 msikitini. Tumekwenda asubuhi damu zimetapakaa ndani ya msikiti, katika watu hao wakarudi wote 10, katika 10 waliorudi mmoja kafa, mmoja hana jicho, mmoja wakamwambia wewe unafuga ndefu wamemchoma ndevu zake, wamemnyoa ndevu kwa kumchoma moto, watu hawa wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mnatuambia kwamba nchi hii ina amani na utulivu mimi sielewi? Watu hawa wapo na huyo mtu mmoja amekufa tumemzika na majina yao nitakutajia. Samahani kidogo nimeandika aliyefariki anaitwa Ismail Bwela, aliyetoka jicho anaitwa Mbaraka Masaburi, aliyechomwa ndevu anaitwa Muharam Yalife, wapo! Wamepigwa risasi msikitini, mmoja amekufa na Serikali haijasema chochote mpaka leo na wamerudishwa wako Kilwa pale.

Mheshimiwa Spika, unaposema nchi hii ina amani na utulivu sielewi! Ninawaunga mkono waraka uliotolewa na Maaskofu. Nawaunga mkono Maaskofu mlichokisema ni sawasawa na maneno ya Maaskofu ni maneno ya Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii nchi imeharibika leo waislamu lazima wasiseme, tumetengenezewa jambo tunaitwa magaidi, kwa hiyo Mashekhe wote wa kiislam wakitaka kutetea haki zao kuhusu waislam wenzao tunaambiwa aah!Ninyi magaidi mnawatetea magaidi na ndiyo maana waislam hawawezi kusema sasa hivi, watasema vipi wakati wao wanaambiwa ni magaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza Maaskofu sasa hivi matumaini kwa Watanzania ni sehemu mbili tu Mahakama na Maaskofu, lakini waislamu hatuwezi kusema! Akipigwa muislam akisema unaambiwa unatetea magaidi eeh! Waislam wote tumerudi nyuma, tunaomba sana…..

Mheshimiwa Spika, nitunzie muda wangu.

T A A R I F A . . .

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, taarifa nimeipokea. Wewe tulia nitamjibu mwenyewe huyu.

Katika watu wanaolaani kwamba wale watu wamepigwa kwa makosa wale askari pamoja na mimi, lakini siwezi kuacha kusema watu wengine wakionewa haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, polisi wakionewa nitasema, wananchi wakionewa watasema! Nia yetu hapa tunataka amani na utulivu ndiyo hoja, sijasema kwamba waliopigwa risasi polisi sijasema hivyo, nimesema polisi wameiniga msikitini wamewapiga watu risasi sasa mkatae kwamba hamkupiga watu risasi.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Rufiji hiyo ilikuwa watu wanapigwa risasi wanauawa, mkatengeneza mazingira kwamba wale wanaopigwa ni wa CCM na mkahalalisha Viongozi wetu wa CUF wamekamatwa na mpaka sasa hivi hawajulikani walipo, nitawatajia watu sita waliokamatwa katika operation mpaka sasa hatujui walipo, nataka tujue wako wapi.

Mheshimiwa Spika, basi nitakuletea majina ya hao watu sita waliokamatwa tunataka tujue wako wapi, ni wa Rufiji nitakuletea majina. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataalah. Pili, naishukuru Serikali ya CCM kwa kutufikisha hapa tulipofikishwa.

Mheshimiwa Spika, juzi niliwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba hata firauni alikuwa mbaya, lakini watu wake waliokuwa nyuma yake, wanamuunga mkono. Sasa huyu firauni aliota ndoto kwamba ataondolewa katika ufalme wake na akaamua kwamba kila nyumba kumi kuwepo na watu, kila atakapozaliwa mtoto wa kiume auliwe ili ufalme wake uendelee. Bahati nzuri akazaliwa Musa akamlea yeye mwenyewe na ndio yeye akamwangamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ina maana kubwa sana Waheshimiwa, hayo mnayoyatetea katika upande wa Serikali ya CCM, leo Waheshimiwa wawili wamesema CCM tunakufa eeh! Na mimi naamini kwamba CCM itajiua yenyewe kama alivyosema Nyerere. Naomba sana Serikali ya CCM muendele na hayo mnayoyafanya. (Makofi/Kicheko)


Mheshimiwa Spika, pia Serikali ya CCM mnatutaka Wapinzani lakini hamtutaki, lakini sisi hatuwataki lakini tunawapendeni. Tukiwaambieni maneno mazuri ndiyo tunawapenda hivyo, mfanye. Mkifanya tu mambo mazuri tu Tanzania, naomba sana Serikali ya CCM muwe wasikivu, moja hiyo.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie habari ya mifugo kwanza, Kilwa mmetuletea mifugo, tulikuwa hatuijui mifugo tunashukuru sana sasa hivi tunapata maziwa mengi, lakini hamjawatendea haki wafugaji walikwenda kule, hawana malambo wala hakuna majosho. Naomba sana Serikali ya CCM kwa kuwa mliwatoa mlikowatoa kuwaleta Kilwa hebu tuleeteeni malambo na majosho ili wakae vizuri wale wafugaji, hilo ni ombi la kwanza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi la pili kwetu Kilwa tuna maeneo ya ng’ombe wale, kuna vijiji vingine vimeambiwa wafuge ng’ombe wengine wawe wakulima Mheshimiwa Ulega najua. Kwa mfano, kijiji cha Nakiu ni kijiji cha wakulima lakini kuna ng’ombe siyo chini ya 2000 tunawaomba kila siku ng’ombe hao waende katika sehemu husika hawaendi, tatizo kubwa inawezekana viongozi wa Mkoa na Wilaya kama wamepata rushwa hivi, Mkuu wa Mkoa huyu na Mkuu wa Wilaya ninawasiwasi wamepata rushwa, kwa sababu Mkuu wa Wilaya kaandika barua kwamba ng’ombe wa kijiji cha Nakiu watolewe mwezi wa Novemba waondoke, lakini mpaka leo hawajatolewa na ukimuuliza Mkuu wa Wilaya anasema hela za kuwatoa sina. Ukiwaambia polisi wakawatoe wanasema hela hatuna na kijiji cha Nakiu kimewahi kutoa shilingi 1,500,000 kuwapa polisi kwamba hawana posho, hela wamechukua ng’ombe wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali hii sasa Jeshi la Polisi hawana uwezo mpaka kijiji kitoe hela kiwape polisi, hela wamechukua na ng’ombe mpaka leo wapo, kweli hii Serikali, kwamba polisi hawana hela mpaka wanakijiji watoe hela na wanatoa hela halafu ng’ombe hawajatolewa? Mkuu wa Wilaya kala rushwa, Mkuu wa Mkoa kala rushwa, polisi wamekula rushwa na kama hawakula rushwa tuwaone ng’ombe watoke, leo bila hivyo wamekula rushwa! (Makofi/ Kicheko)

T A A R I F A . . .

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kusema na nipe dakika moja tu nisema. Nimesema kijiji kimetoa fedha kwa ajili ya kuwapa polisi kuja kutoa ng’ombe, lakini fedha wametoa na ng’ombe hawakutolewa kwa mazingira haya nina wasiwasi watu wamepewa rushwa na kama kutoa rushwa basi ng’ombe wale watoke, kama hawakutoka wamepewa rushwa. Ndiyo hoja yangu mimi, nina uhakika kijiji kimetoa hela na ng’ombe hawajatoka. Sasa kama hawajatoka hela ile ndiyo rushwa, sasa kama wewe unasema habari hizi ni za uongo thibitisha wewe, tuende kijijini mimi na wewe kama hela hazikutolewa.

Mheshimiwa Spika, mimi mwanasiasa eeh!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kufanikisha malipo ya wapiga kura wangu walio katika Chanzo cha Maji Champala, kwa kweli nakushukuru kwa hili, Mwenyezi Mungu akujalie afya, busara na hekima.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mheshimiwa Waziri naomba sana tatizo la maji katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje ambapo ipo Hospitali ya Wilaya ambayo ina upungufu wa maji kwa muda mrefu. Nakuomba sana Mji Mdogo wa Kivinje uangaliwe kwa jicho la huruma sana, tena sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, napenda kukukumbusha Mradi wa Maji wa Mavuji ambao upembuzi yakinifu umekamilika lakini tatizo ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo. Mradi wa Mavuji utakapopata fedha na kukamilika hilo ndilo suluhisho la upatikanaji wa maji katika Mji Mdogo wa Kivinje/Masoko. Nakuomba sana usimamie mradi huu wa Mavuji ambao upembuzi yakinifu ulifanywa na Wabelgiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba fedha zilizopangwa mwaka 2017/2018 zitolewe katika miradi ya maji na pia fedha zilizolengwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019 zipatikane ili matatizo ya maji yapungue. Natanguliza shukrani, ahsante. Tunakuelewa na tunakukubali.