Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Selemani Said Bungara (4 total)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu lililotolewa na Mheshimiwa Waziri. Hata hivyo, namwomba sana, kwa kuwa Mheshimiwa Rais Magufuli ameagiza hii barabara ijengwe na mpaka sasa hivi anasema kwamba wanatafuta fedha ili ijengwe, naomba sana waitafute hiyo fedha barabara hiyo ijengwe. Pamoja na hilo, nataka niulize swali la nyongeza; kwanza; je, tathmini hiyo ni shilingi ngapi katika barabara hiyo iliyotathminiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika kampeni ya mwaka 2015, Rais Dkt. Magufuli alipokuja Kilwa aliwaahidi watu wa Kilwa kama atashinda Urais atajenga kilometa tano katika Mji Mdogo wa Kilwa Masoko. Sasa pamoja na kwamba ahadi za Rais hizi hazitekelezwi kwa wakati. Je, ni lini ahadi hii ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa sababu Urais alishaupata, na yule Bwana akisema jambo basi linakuwa hivyohivyo anavyosema. Je, ni lini itatimizwa ahadi hii ya kilometa tano katika Mji wa Kilwa Masoko?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wetu wa TANROADS walikwenda kufanya tathmini ya barabara hiyo na tukagundua kwamba inahitajika takribani bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha barabara hiyo. Mwezi huu uliopita tu Halmashauri zilipelekewa takribani milioni 400, sasa tunaamini kazi iliyopo mbele yetu ni kutafuta bilioni 2.6 kwa ajili ya kukamilisha barabara hiyo. Mheshimiwa Rais alinipa jukumu hilo na nitahakikisha kwamba pesa hizo tunazitafuta ili barabara hiyo iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kuhusu ujenzi wa kilometa tano Mjini Kilwa Masoko. Ahadi zote alizotoa Mheshimiwa Rais tumezichukua na tunazifanyia kazi na tutahakikisha hivi karibuni tutaanza kuzitekeleza moja baada ya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na Kituo cha Kipatimo ambacho amesema Mbunge mwenzangu wa Kilwa Kaskazini, Mbunge wa Kilwa Kusini kuna kituo cha Polisi ambacho kimejengwa na wananchi lakini bado kumalizika kule Kijiji cha Nanjilinji. Je, Mheshimiwa Waziri, unaweza kutusaidia ili kituo hicho kimalizike?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Nanjilinji ni miongoni mwa vituo vingi ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi ambavyo vinahitaji kukamilika. Hiyo ni dhamira ya Serikali, kuhakikisha kwamba vituo vyote hivyo nchi nzima ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi vinakamilika, siyo tu kwa sababu ya faida na manufaa ya matumizi ya vituo hivyo, lakini pia kwa kuweza kutokuwavunja moyo wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Kituo cha Nanjilinji, pale ambapo hali ya kifedha itakaa vizuri, tutakimaliza pamoja na vituo vingine, lakini Mheshimiwa Mbunge vilevile anaweza akatumia fursa hiyo kusaidia kuweza kufanikisha ujenzi huo kwa kuhamasisha wananchi wake ama wadau kuendeleza jitihada hizi za Serikali na Serikali pale ambapo uwezo utakuwa tayari basi tutavimaliza.(Makofi)
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje kuna vitongoji tisa ambavyo vyote havina maji; na kuna mradi mkubwa wa maji ulikuwa wa kutoka Mavuji kuja Kilwa Kivinje, mpaka sasa hivi hatujajua hatima yake. Je, Waziri anazungumzia vipi upatikanaji wa maji katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kivinje naufahamu uko baharini, lakini juzi nilimpa Mheshimiwa Mbunge shilingi milioni 500, tumetoa fidia kwa ajili ya kutunza eneo la chanzo cha maji. Kwa hiyo, chanzo hicho sasa tutatekeleza mradi mmoja mkubwa wa kuchukua maji yaliyo baridi pale na kuyapeleka katika eneo la Kivinje. Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi Ilani ya Chama cha Mapinduzi iko makini, itatekeleza huo mradi kuhakikisha wananchi wa Kivinje wanapata huduma ya maji.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jibu lisilokamilika kutokana na kwamba mimi niliulizia Kilwa lakini amejibu kwa pamoja. Ni lini sasa uchambuzi wa kina na hali ya halisi utakamilika ili vyuo hivyo vipate huduma inayohitajika? Hilo ni swali langu la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Chuo cha Maendeleo cha Wilaya ya Kilwa kina mafunzo ya udereva, lakini mpaka sasa hivi hakuna gari la kujifunzia. Ni lini Wizara itapeleka gari katika Chuo cha Maendeleo Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bungara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zoezi litakamilika lini, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, zoezi hilo litategemea kukamilika mwezi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chuo kupatiwa gari, kama tulivyosema tunafanya tathmini ya kuangalia vitu vinavyohitajika ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Kama gari ni moja kati ya vitu vitakavyoonekana kwamba vinahitajika basi Serikali itajipanga ili kuweza kuhakikisha kwamba linapatikana kadri uwezo utakavyoruhusu.