Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Vedasto Edgar Ngombale Mwiru (9 total)

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika mjadala wa Taarifa ya Kamati yangu kwa mwaka 2016. Michango mbalimbali mizuri imetolewa na naitaka Serikali sasa kujipanga na kuona namna bora ya kurekebisha kasoro nyingi zilizoainishwa na Waheshimiwa Wabunge ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza ari ya uwajibikaji katika Halmashauri nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na jumla ya wachangiaji 46 ambao wamechangia kwa hoja mbalimbali za Kamati yangu; kati yao 39 wakichangia kwa maneno na saba wakichangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia katika maeneo yaliyogusia matumizi yasiyozingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma, upelekaji usioridhisha wa fedha kwenye Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, asilimia kumi ya mapato kutochangiwa katika Mfuko wa Wanawake na Vijana, Halmashauri kutopeleka asilimia 20 ya ruzuku kutoka Serikali Kuu katika Serikali za Mitaa na Vijiji na Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kwa kuwa sheria hii inakinzana na hali halisi ya bei za bidhaa katika soko na mwisho uwezo mdogo wa kiutendaji wa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie uwezekano wa kutumia chuo cha mafunzo ya Serikali za Mitaa Hombolo kutoa mafunzo kwa Wakurugenzi wapya wa Halmashauri kama ilivyoshauriwa na Mheshimiwa Issa Mangungu, Mheshimiwa Godfrey Mgimwa na Mheshimiwa Abdallah Chikota. Pia Ndugu yangu Mheshimiwa Silinde alisema na kupendekeza kwamba ni vizuri sasa Serikali iangalie uwezekano wa kuwatumia watumishi wanaotokana na Watumishi wa Serikali ili iwe motisha chanya kwa wale Wakuu wa Idara katika utendaji wa kazi, maana kwa hali iliyopo sasa watumishi wengi katika Halmashauri ile ari ya kufanya kazi imeshuka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi kubwa ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa inaitaka Serikali itenge bajeti ya kutosha kwa Bunge ili Wabunge waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuisimamia Serikali hususan kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo badala ya kufanya vikao na mahojiano ya ana kwa ana na Menejimenti za Halmashauri hapa Dodoma. Kimsingi ukaguzi ni moja kati ya shughuli muhimu katika kuhakikisha kuwa kuna nidhamu katika matumizi ya fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia hoja ya ufinyu wa bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi unaosababisha ofisi hii muhimu kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Hili limezungumzwa na ndugu yangu Mheshimiwa Khatibu na kusema kwamba Serikali inazibana Kamati za usimamizi wa fedha za Serikali, lakini inaibana Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Kwa hiyo, mimi situmii ile terminology nyingine aliyotumia Mheshimiwa Khatibu, ila niseme tu kwamba Serikali ilegeze kubana ili basi mambo yaweze kwenda sawasawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati za usimamizi wa fedha zinatekeleza majukumu yake kwa kutumia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, lakini kutokana na ufinyu wa bajeti, mwaka huu CAG ameshindwa kutembelea baadhi ya Halmashauri kufanya ukaguzi na uthibitisho wa majibu ya hoja mbalimbali za ukaguzi. Ufinyu huu wa bajeti usipotatuliwa katika bajeti zinazokuja, kuna hatari ya CAG kushindwa kufanya ukaguzi kabisa na hivyo Kamati hazitaweza kuendelea na majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na michango mizuri inayohusu usimamizi mbaya wa mikataba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo uliobainishwa na Kamati. Naamini kwamba Serikali imeliona hilo na italifanyia kazi hasa kuboresha usimamizi wa mikataba kwa kuwa miradi mingi ya maji katika mwaka wa fedha 2013/2014 na mwaka wa fedha 2014/2015 haikutekelezwa kikamilifu kwa sababu mikataba mingi ilivunjika kabla ya miradi kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Leah Komanya, Mheshimiwa Martin Msuha, Mheshimiwa Richard Mbogo kwa kutoa maelezo mazuri juu ya mfumo wa fedha wa EPICOR. Mfumo huu niseme wazi umegharimu Serikali fedha nyingi katika kuziunganisha Halmashauri nchini, lakini utendaji kazi wake hauna tija. Baadhi ya taarifa kwa mfano, taarifa za mali za Halmashauri zinaandaliwa nje ya mfumo. Ifikie wakati Serikali ione kuwa mfumo huu una changamoto nyingi na hivyo haufai kwa mazingira ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa sasa kupata taarifa za Halmashauri ni mgumu kwa kuwa vitabu vinavyowasilishwa huwa vikubwa mno na mapitio yake huwa magumu mno. Dunia ya sasa inaelekea katika mfumo wa nyaraka laini (electronic filing system). Hili limezungumzwa sana na Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza kwamba Kamati inakutana na malundo ya vitabu ambavyo kuvifanyia upembuzi inakuwa ngumu sana. Hivyo Serikali iangalie uwezekano wa kuanzisha mfumo huu kwa Halmashauri nchini. Hii itapunguza hatari ya gharama za kudurufu vitabu hivi ambavyo ni vikubwa na mzigo mkubwa kwa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mjadala baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walishauri Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kuwa huru na kuwa kipangiwe bajeti ya kutosha ili kiweze kusimamia mwenendo wa fedha za Halmashauri. Wazo hili ni zuri kwa kuwa hata Kamati yangu ilibaini tatizo hili. Serikali iendelee kusisitiza kuangalia namna bora ya utendaji kazi wa kitengo hiki ili kulinda fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Pauline Gekul alifafanua kwa undani namna bora ya Mfuko wa Wanawake na Vijana ambavyo unawabagua wazee ambao nao kimsingi wanayo mahitaji ya fedha kwa ajili ya mahitaji ya biashara ndogo ndogo na shughuli nyingine. Kamati iliona hilo na nichukue tena fursa hii kusisitiza uundwaji wa Sheria ya Mfuko huu ili kuongeza tija, ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto ambazo Kamati imeziainisha katika taarifa yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea pia mchango wa Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kwa maandishi kuhusu suala la Mfuko wa Wanawake na Vijana. Nakubaliana na wazo lake la kuangalia uwezekano wa Serikali kutumia mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuhakikisha usalama wa fedha za umma. Kimsingi ushauri wake ni mzuri kwa kuwa una faida za ziada kwa wanavikundi; kama vile utaratibu wa kujiwekea akiba, kupata fao la Bima ya Afya na kupata fursa ya huduma ya SACCOS ili kupanua wigo wa biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limekuwepo suala la Serikali kuchukua vyanzo vya mapato vya Halmashauri kama vile ushuru wa ardhi na ushuru wa nyumba. Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia wamelalamikia suala hili la Serikali kukusanya ushuru wa ardhi na kutopeleka asilimia 30 katika Halmashauri kama ilivyokubaliwa. Niseme wazi, ushuru huu umefikia wakati kwamba Serikali lazima irudishe katika Halmashauri ili kuongeza wigo wa mapato na kuzipunguzia utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi waliochangia taarifa yetu, wameshauri Halmashauri kufuata utaratibu katika kutekeleza maagizo kutoka Serikalini. Suala la ujenzi wa maabara limegharimu miradi mingi na Kamati ilibaini kuwa ni moja kati ya sehemu zenye walakini mkubwa katika matumizi ya fedha za Serikali. Sasa lipo suala la utengenezaji wa madawati ambalo pia ni agizo kutoka Serikali Kuu. Naendelea kusisitiza kuwa Halmashauri zifuate sheria, kanuni na taratibu za fedha katika kutekeleza maagizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika taarifa yetu na Kamati inataka Serikali kuleta majibu kwa maandishi juu ya utekelezaji wa yale yote ambayo Kamati tumeyaazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho basi niombe sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na mapendekezo yote yaliyomo katika taarifa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kwa mara nyingine tena kwa namna ya kipekee niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Kilwa Kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala zima la uwekezaji wa viwanda katika mazao ya bahari. Mikoa ya Kusini ambayo inapakana na Bahari ya Hindi haina viwanda vinavyosindika mazao ya bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba Mikoa ya Kusini inapitiwa na mkondo wa Kilwa (Kilwa Channel), mkondo ambao unafanya eneo la Kilwa na Mikoa ya Kusini liwe ni miongoni mwa maeneo machache yanayozalisha samaki kwa wingi. Kwa bahati mbaya kabisa mpaka leo baada ya miaka zaidi ya 54 ya Uhuru hatuna kiwanda cha kusindika mazao ya bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi pia unapakana na Mto Rufiji na delta za Mto Rufiji. Delta za Mto Rufiji zimetokana na Mto Rufiji ambao unatiririsha mboji nyingi kutoka Mikoa ya Bara. Maeneo haya yanasababisha bahari hii ya kusini iwe maarufu kwa uzalishaji wa kamba. Tunazalisha kamba wengi, lakini kwa bahati mbaya hatuna kiwanda cha kusindika mazao ya bahari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, sisi watu wa Mikoa ya Kusini tuna mazingira wezeshi ambayo yanaweza kupelekea kuanzishwa kwa kiwanda katika maeneo yetu. Tuna barabara nzuri ya lami, tuna umeme wa uhakika unaotokana na gesi, lakini tuna ardhi ya kutosha. Kwa mfano, katika Jimbo langu maeneo ya Miteja pale, pana ardhi ya kutosha inayowezesha kuanzishwa mchakato wa kuanzishwa kiwanda, lakini kwa bahati mbaya hatuna kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo sasa wavuvi wetu kutokana na kukosa hilo bado wanajihusisha na ku-preserve samaki kwa njia ya kukausha, zile njia za kijima kwamba sasa inalazimika wakaushe ili wapate ng‟onda. Bado tunawafanya wavuvi waendeshe shughuli zao katika njia za kijima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ukianzia maeneo ya Moa - Tanga mpaka Msimbati - Mtwara, kuna viwanda viwili tu vya kusindika mazao ya samaki. Hii haitengenezi ustawi wa wavuvi wetu wa maeneo ya mikoa ya Kusini. Sasa naomba commitment ya Serikali kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuelekeze ana mpango gani wa kujenga kiwanda cha kusindika mazao ya bahari katika maeneo ya mikoa ya Kusini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, niende moja kwa moja kwenye suala zima la uwekezaji katika kilimo cha muhogo. Nilipata kumsikia Mheshimiwa Waziri akisema kwamba Serikali sasa imewezesha kutuletea wawekezaji wa China na wamechagua eneo la mikoa ya Kusini hususan katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini kwamba wataanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya mihogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hilo, naipongeza sana na nichukue fursa hii kuwakaribisha wawekezaji hao, waje, maeneo yapo, tuna ardhi ya kutosha, watu wapo na kwa bahati nzuri sasa tuna umeme huu wa REA. Kwa hiyo, wazo la uwekezaji wa kilimo cha muhogo liende sambamba na kujenga kiwanda cha kusindika mazao ya muhogo. Bila kumung‟unya maneno, napendekeza kiwanda hicho kijengwe katika Jimbo langu katika Tarafa ya Njinjo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala zima la kiwanda cha kuzalisha mbolea Kilwa Masoko maeneo ya Kilamko. Wakati harakati za kusafirisha gesi zinaanza kutoka maeneo ya Kilwa kuja Dar es Salaam, kati ya ahadi zilizotolewa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi wakati wa mfumo wa chama kimoja mwishoni mwa miaka ya 1980 ni kwamba gesi ile ije Dar es Salaam lakini watu wa Kilwa waliahidiwa kujengewa Kiwanda cha Mbolea maeneo yaa Kilamko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ninavyozungumza, hakuna kiwanda zimebakia hadithi. Kilichotokea ni kwamba, watu wa TPDC walichukua zaidi ya hekari 800 maeneo ya Kilwa Masoko na hawajaziendeleza mpaka leo. Kinachotokea sasa ni kwamba wao walisema watawalipa fidia watu 28 tu. Toka mwaka 1989 walipochukua maeneo hayo mpaka leo ninavyozungumza, kuna zaidi ya watu 1,000 wako pale. Kwa hiyo, watu wa TPDC wamekuja lakini kwa msimamo wa kwamba wao watafidia watu 28 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naitaka Serikali ihakikishe kwamba wakati wa mchakato wa kujenga kiwanda kama mlivyotuahidi, wakati tunakumbuka maumivu makubwa ya kuondokewa na gesi yetu kwenda Dar es Salaam, tuwakumbuke pia wale wananchi ambao wapo katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la muhimu ni kwamba sasa hivi sisi watu wa mikoa ya Lindi na maeneo ya Kilwa ni wazalishaji wakubwa wa zao la ufuta. Wilaya ya Kilwa peke yake inazalisha zaidi ya tani 25,000 za ufuta, lakini mpaka leo bei ya zao la ufuta inasuasua kwa sababu hatuna kiwanda cha kusindika mazao ya ufuta. Sijapata kusikia kama kuna kiwanda cha kusindika mazao ya ufuta. Ninaona tu kwamba Serikali inaendelea ku-entertain kwamba zao la ufuta lisafirishwe kama zao ghafi kitu ambacho kinawaumiza wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate maelezo ya Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha sasa zao hili la ufuta linapata viwanda vya usindikaji ndani ya nchi? Nashukuru, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya TAMISEMI na Utawala Bora. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha mimi binafsi kuingia katika Bunge lako Tukufu, lakini katika namna ya kipekee kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini ambao wamenipa dhamana hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miundombinu ya barabara. Jimbo langu kwa ujumla miundombinu ya barabara ni mibovu na kwa sasa barabara nyingi hazipitiki na hasa zile barabara kutoka Nangurukuru kwenda Liwale, haipitiki, ni mbaya. Sasa hivi kutoka Nangurukuru kupitia Njinjo kwenda Liwale, hakupitiki. Hivyo, inalazimika wananchi wanaotaka kwenda huko watembee au wapite katika umbali wa kilometa zaidi ya 400, wakati kutoka Nangurukuru kwenda Liwale ni umbali wa kilometa 230. Naishauri Serikali ione uwezekano wa kujenga barabara hii katika kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna barabara kutoka Njia Nne kwenda Kipatimo, nayo sasa haipitiki, ni mbovu. Barabara hii inapitia katika Tarafa ya Miteja na Kipatimo. Pia naishauri Serikali ione uwezekano wa barabara hii kuijenga katika kiwango cha lami.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu lipo katika ukanda wa Pwani. Ukanda wa Pwani una matatizo makubwa ya maji, lakini tunayo fursa ya uwepo wa Mto Rufiji. Naishauri Serikali ione uwezekano wa kujenga mradi mkubwa wa maji katika Mto Rufiji utakaosaidia vijiji na rarafa zilizopo katika Wilaya Rufiji na Jimbo la Kilwa Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya. Huduma za afya katika Jimbo langu bado zinalegalega; huduma zinazotolewa ni hafifu, hakuna dawa katika zahanati, hakuna wahudumu. Tuna zahanati kama sita ambazo zimemalizika kujengwa, lakini hazina dawa wala wahudumu, kama zahanati ya Mwengei, Luyumbu,Marendego, Kipindindi na Nambondo na Hongwe. Zahanati hizi zimemalizika kujengwa lakini mpaka sasa hivi hazijaanza kufanya kazi. Naiomba Serikali iangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Jimbo langu kuna Hospitali moja tu, hospitali ya Mission. Hospitali hii haina x-ray na tayari wafadhili wa hospitali hii walitoa mashine ya kisasa ya x-ray, lakini kwa bahati mbaya kwa sababu ilichukua muda kupata jengo, ilipata hitilafu na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kusaidia kufanya ukarabati wa x-ray hii. Kwa bahati nzuri ilipofikia mwaka 2013 akatoa shilingi milioni 40 kufanya ukarabati wa x-ray hii. Mpaka sasa ninapozungumza x-ray hiyo haijakarabatiwa na pesa zile zipo. Naiomba Serikali ifuatilie ili basi wananchi wangu waweze kupata huduma ya x-ray.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kilwa Kaskazini ni dampo la mifugo kutoka Mikoa ya wafugaji. Sasa hivi tuna tatizo kubwa la migogoro ya ardhi, lakini mapigano kati ya wakulima na wafugaji na ni kwa sababu tu wafugaji wote wanaotoka katika Mikoa ya wafugaji wanakuja katika Jimbo langu na kusambaza mifugo yao bila kufuata utaratibu wa matumizi bora ya ardhi.
Naiomba Serikali ihakikishe kwamba inaondoa mifugo yote ambayo ipo katika vijiji ambavyo havikupangwa kuwepo kwa mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni elimu. Tunao mpango wa elimu bure. Huu mpango mpaka sasa naona bado ni kama unalegalega. Mimi binafsi nashauri mpango wa elimu bure uendane sambamba na kuangalia maslahi mapana ya walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure inazungumzia namna ya kumsaidia mwanafunzi, lakini bado haijamwagalia mwalimu. Napendekeza, mpango huu uendane sambamba na kuangalia uwezekano wa kutoa teaching allowance kwa walimu. Walimu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, ni vizuri sasa kuangalia maslahi yao. (Makofi)
Mheshimia Mwenyekiti, pia kuna majengo ya Shule na Ofisi za Serikali yanajengwa chini ya viwango. Majengo mengi yanayojengwa sasa, hayawezi kudumu hata kwa miaka kumi, hali ya kwamba majengo ya Serikali yanatakiwa ya kudumu kwa miaka 50 na kuendelea. Serikali iangalie uwezekano wa kusimamia ili majengo yanayojengwa sasa yawe ya kudumu kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uhakiki wa Watumishi. Suala hili katika eneo langu limezua adha na kuna shida! Tayari Serikali ilifanya zoezi hili kwa mara ya kwanza, lakini sasa inaonekana ni lazima warudie tena kufanya tena kwa mara nyingine. Sasa inawagharimu wafanyakazi. Kwa mfano, wananchi wanaotoka Kijiji cha Nandete kwenda Kilwa Masoko ni ziaidi ya kilometa 140. Mtumishi huyu tayari alishakwenda kwa zoezi hilo kwa mara ya kwanza, lakini analazimika tena aende kwa mara ya pili. Hii inawasumbua sana watumishi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu maalum. Naomba Serikali kwanza ibaini idadi ya walemavu tujue kuna walemavu wangapi. Serikali ijielekeze kutoa huduma stahiki za walemavu. Kila mlemavu ana hitaji lake kulingana na aina ya ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mlemavu wa ngozi anatakiwa apate mafuta maalum ambayo yatamwezesha kumnusuru na athari za miale ya mwanga. Mlemavu kiziwi, anatakiwa apate shime sikio (earing aid), itakayomwezesha kupata athari za uelekeo wa sauti na mlemavu asiyeona anatakiwa apate fimbo maalum itakayomwezesha kupata uelekeo. Naishauri Serikali, huduma hizi zitolewe bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwasahau walemavu wa viungo, viungo bandia vimekuwa vikiuzwa kwa bei juu, wananchi wetu hawawezi kumudu. Naiomba Serikali, huduma ya viungo bandia itolewe bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naiomba Serikali ianzishe Kurugenzi ya Elimu Maalum. Walimu wanaoshughulikia watoto wenye ulemavu, wanafanya kazi kubwa lakini mpaka sasa hatujakuwa na Kurugenzi ya Elimu Maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu limepakana na Bahari ya Hindi, lina wavuvi, mpaka sasa wavuvi wanatumia mbinu za kijima kuvua. Naiomba Serikali iwezeshe vifaa vya kisasa kwa wavuvi wale ili waweze kwenda kuvua kwenye maji ya kina kirefu na basi kuweza kupata tija.
Katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini, kuna Tarafa mbili ambazo zinalima kilimo cha michungwa. Katika miaka ya hivi karibuni michungwa imepata changamoto ya ugonjwa ambao unakausha mimea hiyo. Naiomba Serikali ituletee wataalam watakaofanya utafiti wa kugundua ni tatizo gani linaloisibu mimea hiyo kukauka ili basi wakulima wetu waweze kupata tija ya zao hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika utawala bora. Mpaka sasa tunapozungumza, jitihada za kufikia viwango vya juu vya utawala bora bado zinakwamishwa. Bado kuna figisufigisu nyingi katika suala zima la uendeshaji wa utawala bora. Bunge lako Tukufu mpaka sasa linafanya shughuli zake kana kwamba tuko jandoni; kwa sirisiri! Hii nafikiri haipendezi na haiwezi ikawa na mchango mzuri wa ustawi wa demokrasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mpaka sasa maslahi na matakwa ya maamuzi ya chaguzi zinazofanywa na wananchi hayaheshimiwi. Kilichotokea Zanzibar ni kutoheshimu matakwa ya maamuzi ya wananchi. Naiomba Serikali izingatie utawala bora ili basi matakwa ya maamuzi
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, lakini nachukua nafasi hii pia kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa kunichagua kuwa Mwenyekiti wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na uzalishaji wa umeme katika kinu cha Somangafungu. Uzalishaji wa umeme katika mtambo huu kwa kweli umekuwa wa kusuasua, umeme unaozalishwa pale unatumika katika Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Rufiji lakini mpaka sasa umeme umekuwa ni wa kukatika katika kila mara. Tulifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa TANESCO alikuja pale akatuambia kwamba tayari vipuli vimepatikana kwa ajili ya kufanya marekebisho ya mitambo pale, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea alituambia baada ya mwezi mmoja mambo yatatengamaa lakini bado umeme unakatikatika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niongelee kuhusiana na suala zima la umeme vijiji. Katika jimbo langu kuna baadhi ya kata na vijiji havijapata umeme kwa mfano kata ya Miteja - kijiji cha Kikotama, kata ya Mingumbi - kijiji cha Nambondo, kijiji cha Chapita, kijiji cha Nampunga, kata ya Namayuni - kijiji cha Nahama, Namakolo, Naliyomanga, kata ya Chumo - kijiji cha Hongwe, Ingirito na Kinywanyu, kata ya Kipatimo - kijiji cha Mtondowa Kimwaga, Nandete, Pondo, Mkarango bado havijapata umeme, kata ya Kibata kata yote kijiji cha Kibata, Hanga, Nakindu, Mwengehi, Namtende vyote havijapata umeme. Kata ya Kandawale - kijiji cha Kandawale, Ngarambi, Namatewa Natipo havijapata umeme. Kata ya Njinjo - kijiji cha Msitu wa Simba, Kipindimbi havijapata umeme, kata ya Miguruwe - kijiji cha Mtepela na Kingombe na Zinga Kibaoni havijapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika kata ya Kinjumbi kuna vijiji vya Pungutini, Kitope havijapata umeme. Lakini pia katika Jimbo la Kilwa Kusini kwa Mheshimiwa Bwege kuna kata saba yenye vijiji 31 havijapata umeme, kata ya Pande, kata ya Limalyao, kata ya Nanjilinji, kata ya Likawage, kata ya Mandawa, kata ya Kilanjehanje na kata ya Kitole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo pia la kuunganishiwa umeme katika vijiji ambavyo tayari vimeshapata umeme. Watu wa REA bado wanasumbua, vijiji vimepata umeme lakini kuunganisha umeme majumbani inachukua muda wakati mwingine ni zaidi ya miezi sita toka mwananchi alipie umeme, umeme anakuwa bado hajaunganishiwa. Kwa hiyo, naomba pia Mheshimiwa Waziri hilo pia uliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuwa jana kupitia vyombo vya habari tuliona Mheshimiwa Rais akizungumza na Mabalozi lakini pia alizungumza na Katibu wa SADC akieleza nia ya Serikali ya kujenga kiwanda cha mbolea pale Kilwa Masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza, kukupongeza wewe Mheshimiwa Waziri,nimefurahi sana katika hilo na hata kwenye hotuba yako ukurasa wa 37 umeeleza kwamba zimetengwa pesa shilingi bilioni 4.41 kwa ajili ya utengenezaji wa kiwanda hicho, tunashukuru sana. Lakini naomba pia suala hilo liendane sambamba na upanuzi wa…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umekwisha…
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Ahsante!
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Mchango wangu nitaanza kujielekeza kwa ndugu zangu wa TAMISEMI. Serikali ya Awamu ya Tano toka iingie madarakani haijaongeza nyongeza ya mishahara, lakini pia watumishi wamepandishwa madaraja lakini hakuna mabadiliko ya mishahara kutokana na madaraja waliyopandishwa. Sasa naomba Serikali iwaangalie watumishi ambao watastaafu katika kipindi hiki, kwamba wao walistahili wapate nyongeza hizo kwa mujibu wa sheria, lakini kwa kuwa sasa Serikali imeamua kutofanya hivyo maana yake kuna uwezekano wa watumishi hawa kukosa haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali watumishi wataostaafu katika kipindi hiki basi lazima wazingatie kwamba watastaafu kwa kukokotoa kwa hesabu zipi? Kwamba watakokotolewa kwa hesabu zile ambazo kabla mshahara haujabadilishwa au mpaka hapo sasa ambapo Serikali itaamua kuongeza nyongeza hizo za mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la waraka uliotolewa na Serikali kuhusiana na vigezo vipya vya namna gani sasa shule zinaweza zikapata usajili. Kuna waraka mpya umetolewa kwamba ili shule iweze kusajiliwa lazima shule hiyo iwe na madarasa 10, nyumba tatu za Walimu, matundu 10 ya vyoo. Suala hili nafikiri Serikali haijafanya utafiti wa kutosha kwa sababu mazingira ya maeneo ya vijijini ni ngumu sana kwa shule kuwa na uwezekano wa kujenga vyumba 10 vya madarasa, nyumba tatu za Walimu ili waweze kufikia vigezo vya kuweza kupata usajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima ikumbuke pia wana jukumu kubwa la kuhakikisha linafuta ujinga, linaondoa vijana ambao watakuwa na matatizo ya kushindwa kuhesabu, kusoma na kuandika, sasa kama hili halitazingatiwa maana yake upo uwezekano wa Serikali kuzalisha vijana wengi wenye shida ya kupata ujuzi huo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado haijawaangalia Wenyeviti wa vijiji na vitongoji, wanafanya kazi kubwa lakini bado Serikali haijawaona. Naishauri Serikali ione uwezekano wa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji waweze kupata posho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mahusiano mazuri kati ya watendaji wa Serikali na wawakilishi wa wananchi kwa maana ya Madiwani pamoja na Waheshimiwa Wabunge. Katika Halmashauri Wakurugenzi wengi wapya walioteuliwa hawana mahusiano mazuri na Waheshimiwa Madiwani na hoja kubwa katika utendaji wao wa kazi, wanasema sisi ni wateule wa Rais, kwa hiyo mara zote, hata katika mambo ambayo yanahitaji kutumia hekima na busara msingi mkubwa unakuwa kwamba sisi ni wateule wa Rais kwa hiyo tunafanya vile tunavyoona. Niishauri Serikali itoe semina kwa Wakurugenzi hawa, lakini pia inatakiwa wawashauri watumie hekima na busara ili kuona kwamba haya mambo yanakwenda katika utaratibu unaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la TASAF ambalo limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, mimi pia kwa msisitizo niseme, Serikali imefanya makosa na lazima ikubali kwamba imefanya makosa. Kwa sababu, wananchi hawa hawakwenda kwa Serikali kuomba msaada kwamba wasaidiwe katika kaya maskini hapana, ilikuwa ni utaratibu wa Serikali. Kama hivyo ndivyo Serikali ilijipanga na ikaweka taratibu zake kwa kutumia Maafisa wake. Kwa hiyo, Maafisa wa TASAF wanapokwenda katika kijiji fulani na kuhitaji kupata vigezo vya nani anastahili apate usaidizi huu, hilo lilikuwa ni jukumu la hao Maafisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichotokea sasa hivi wakasema kwamba Serikali imeleta agizo la kwamba vigezo havikufuatwa ili wananchi husika waweze kupata hizo stahili, matokeo yake, kwa mfano katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini katika Kijiji cha Miteja, Mkurugenzi ameagiza kwamba fedha zile ambazo zilipelekwa kwa wananchi ambao hawakustahili zilipwe na Serikali ya Kijiji na Serikali ya Kijiji sasa inatakiwa itoe zaidi ya milioni tano, hii imefanyika katika Kata ya Mandawa na Kata nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niitake Serikali izingatie tena haya maagizo yake, haikuwa ni ombi la wananchi kupata hizo pesa, ulikuwa ni utaratibu wa Serikali, kwa hiyo Serikali lazima hili iliangalie kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vitambulisho vya Taifa; hili suala imefikia mahali kwamba wananchi wanashindwa kuelewa, walikuja hawa watu wa NIDA, wamefanya zile process zote za kupata taarifa kutoka kwa wananchi lakini mpaka sasa hivi, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Kilwa Kaskazini wananchi hawafahamu vitambulisho hivyo watavipata lini, Serikali nalo hilo iliangalie ili wananchi wapate vitambulisho hivyo vya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni suala la Mabaraza ya Ardhi; chombo hiki cha baraza la ardhi ni chombo kizuri sana na kimesaidia wanyonge kupata haki zao. Niishauri Serikali ihakikishe chombo hiki kinakuwepo katika ngazi zote. Kwa sasa, chombo hiki kinapatikana katika ngazi ya kijiji na ngazi ya Kata, baadaye ngazi ya Wilaya huwezi kupata chombo hiki, uende mpaka kwenye ngazi ya Mkoa na kule kwenye ngazi ya Mkoa kuna Mwanasheria mmoja tu. Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe panakuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya ili basi kupeleka huduma hizi kwa wananchi. Pia sisi watu wa Kusini katika Mahakama Kuu Kanda ya Kusini kuna Jaji mmoja tu, kwa hiyo, utoaji wa haki unacheleweshwa kwa sababu Jaji mmoja hawezi kukidhi haja ya usaidizi wa sheria kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili basi na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Miundombinu.
Mheshimwia Naibu Spika, kabla sijaanza nichukue nafasi hii kutoa pole kwa majirani zangu wa Rufiji kwa mafuriko maana kuanzia jana Mto Rufiji umefurika, kwa hiyo, nitoe pole sana, hata yale maghorofa yetu yote yameanguka chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mawasiliano. Katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini kuna kata ambazo bado hazijapata mawasiliano ya simu; kuna Kata za Kibata, Kandawale na Kijumbi hazijapata mawasiliano ya simu, lakini pia kuna vijiji vya Namakolo na Chapita katika kata ya Namayuni havijapata mawasiliano ya simu. Katika kata ya Kipatimu kuna kijiji cha Nkarango na kijiji cha Nandete havijapata mawasiliano ya simu. Niishauri Serikali ijitahidi maeneo hayo niliyoyataja yaweze kupata mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara; nianze na barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale ambayo ina kilometa 230. Barabara hii ina umuhimu katika mambo makuu matatu; kwanza ni barabara ambayo imepitia katika majimbo matatu, Jimbo la Kilwa Kusini, Jimbo la Kilwa Kaskazini na Jimbo la Liwale, lakini la pili ni barabara ambayo imepita katika Hifadhi yetu ile ya Selous. Kwa hiyo, barabara hii kama ingekuwa imetengenezwa ingetusaidia sana katika utalii. Pia la tatu Waheshimiwa Wabunge tusijisahau, nyakati zile za uchaguzi Wabunge wengi huelekea maeneo ya Liwale, maeneo ya Ngende kwa sababu ya mambo yetu yale, mimi nafikiri ninyi mnayafahamu, lakini cha kushangaza ni kwamba barabara hii inasahaulika. Kwa hiyo, niiombe Serikali, barabara hii ni muhimu sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine nashangaa ni vigezo gani vinatumika kuamua sasa ni barabara ipi ijengwe kwa kiwango cha lami? Kutoka Nangurukuru mpaka Liwale ni mbali sana, Wilaya ya Liwale iko pembezoni kabisa na katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilieleza kwamba ingefanya upembuzi yakinifu lakini nimeangalia katika hotuba hakuna chochote kilichopangwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nikuombe basi uwafikirie wale watani wangu Wangindo na sisi Wamatumbi ili basi na sisi tufaidi matunda haya ya uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kwankocho – Kivinje. Barabara hii ni ya urefu wa kilometa tano na ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Barabara hii inaunganisha barabara inayokwenda Kilwa Masoko na Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga pamoja na Mji wa kitalii wa Kilwa Kivinje. Barabara hii imeahidiwa lakini mpaka sasa hakuna chochote kilichofanyika. Niiombe Serikali iijenge barabara hii kwa kiwango cha lami ili basi tupate urahisi wa kwenda katika hospitali ile ya Wilaya ya Kilwa Kivinje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Njianne – Kipatimu. Barabara hii inahudumiwa na wenzetu wa TANROADS lakini inapita katika miinuko ya milima na kuna milima ambayo kama itatengenezwa katika kiwango cha changarawe basi tutaendelea kupata matatizo tu. Niishauri Serikali milima ile kwa mfano Milima ya Ndundu pale Namayuni, Ngoge, Kinywanyu pamoja na na Mlima wa Karapinda pale darajani basi ingewekwa katika kiwango cha lami ili kuhakikisha kwamba barabara ile inapitika kwa wakati wote. (Makofi)
Lakini isitoshe, nikumbushe pia, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika sherehe za kumbukumbu ya Vita ya Majimaji mwaka 2010 kule Nandete aliahidi kujenga barabara kutoka Nandete mpaka Nyamwage, ahadi ile imeota mbawa sijui kama utekelezaji wake unakwenda vipi. Niikumbushe Wizara, Mheshimiwa Rais aliahidi na ningependa kuona utekelezaji wake unafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo yanayotoka kwamba Mkoa na Mkoa utaunganishwa kwa barabara ya lami, lakini sisi Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Morogoro hatujaunganishwa kwa barabara. Niishauri Serikali ione uwezekano sasa wa kujenga barabara kutoka Mkoa wa Lindi kwenda Mkoa wa Morogoro, na hii pengine inatengeneza uwezekano mwingine wa kwenda katika Mikoa ya Kusini, isiwe lazima ukitokea Dodoma uende Dar es Salaam, ufike Rufiji, uende Kilwa kwenda Kusini basi ukifika Morogoro uingie Liwale - Nachingwea uende Kusini. Naomba ombi hili lishughulikiwe kwa sababu na sisi watu wa Lindi tuna haki ya kuunganishwa na wenzetu wa Morogoro ili basi kuleta ustawi wa watu hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sasa suala zima la ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko. Kwenye bajeti ya mwaka jana tulichangia bajeti lakini hakuna chochote kilichofanyika. Niishauri Serikali iufanyie ukarabati uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko kwa sababu ni muhimu sana kwa shughuli za utalii, kama ambavyo mnafahamu Mji wa Kilwa ni mji wa kitalii, ni mji wa kale, watalii wengi wanakuja lakini hatuna uwanja wa uhakika wa ndege, kwa hiyo Serikali ishughulikie suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la upanuzi wa Bandari ya Kilwa Masoko. Kilwa Masoko tuna bandari ya asili, lakini mpaka sasa ile bandari haijafanyiwa chochote. Niishauri Serikali ione uwezekano wa kupanua bandari ya Kilwa Masoko ili basi meli kubwa ziweze kutia nanga pale na sisi watu wa mikoa ya Kusini au watu wa Kilwa mazao yetu basi yauziwe pale pale Kilwa, maana Meli kubwa zikija hatutakuwa na sababu ya kupeleka mazao Dar es Salaam. Tunalima korosho, tunalima ufuta, bandari ya Kilwa ikifanya kazi basi mazao yale tunaweza tukayauzia Kilwa na hivyo kupandisha bei ya mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa masikitiko makubwa nizungumzie suala zima la stand ya mabasi kwa Mikoa ya Kusini. Mikoa ya Kusini kwa jiografia yake, barabara inayosafirisha abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Kusini inatokea maeneo ya Mbagala Rangi tatu, lakini mpaka sasa hatuna stand inayoeleweka ya mabasi kutoka Mikoa ya Kusini. Tunapata shida kubwa maana stand zinazotumika
pale Mbagala Rangi tatu ni stendi za watu binafsi, na kwa sasa kuna ubaguzi mkubwa unafanyika kwa magari yanayotokea Kilwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumelazimishwa kwa magari yanayotokea Kilwa tuka-park uchochoroni huko ambako zina-park daladala hali ya kwamba Kilwa ni mkoa wa Lindi na kuna mabasi mengine ya Mkoa wa Lindi yana- park katika stand ambayo iko barabarani sasa tunashindwa kuelewa ni kwa nini watu wa Kilwa tutengwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue nafasi hii pia kuishauri Serikali ijenge stand kwa ajili ya mabasi ya mikoa ya Kusini; kwa sababu kwa jiografia ya Jini la Dar es Salaam haiwezekani mtu anayetoka Mtwara, Kilwa au Lindi kwenda Ubungo, haiwezekani. Kwa hiyo Serikali ifikirie kujenga hiyo stendi ili kuondoa adha hii kwa wananchi wa mikoa ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu wa maandishi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango ya Waheshimiwa Wabunge katika Wizara hii, wameeleza tatizo kubwa la ukosefu wa X-Ray katika Hospitali zetu. Katika Jimbo langu ambalo lina Hospitali moja ya Shirika la Dini, hatuna huduma ya X-Ray. Jitihada nyingi zimefanyika zikiwemo pamoja na mchango wa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuchangia Shilingi milioni 40 mwaka 2010. Nasi Halmashauri kwa upande wetu katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018, tumetenga Tanzania Shilingi milioni 20. Hivyo tunaomba Wizara itusaidie kuwasiliana na wenzetu wa Bima ya Afya ili waweze kutukopesha kifaa tiba hicho, kwani tayari tunazo shilingi milioni 60 mkononi ambazo zitaweza kuwashawishi wenzetu kutukopesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 127 inaonesha hali ya Halmashauri. Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa hali yake ya upatikanaji ni asilimia 77. Ukilinganisha na Halmashauri nyingine, Halmashauri hii ni miongoni mwa Halmashauri chache ambazo upatikanaji wake wa dawa bado uko chini. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha, atuambie ni kwa nini Kilwa? Je, kuna mikakati gani ya kutatua tatizo hili ili kuhakikisha tunapata dawa kama zinavyopata Halmashauri nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha zaidi ya Tanzania Shilingi bilioni nne zimepotea kutokana na miradi iliyokamilika lakini haifanyi kazi. Katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini, kuna zahanati sita ambazo majengo yake yameshakamilika, lakini bado hazijafunguliwa. Ni Zahanati ya Hongwe, Mpindimbi, Nambondo, Miyumbu, Marendego na Mwengei. Naomba kwa usimamizi wa Serikali izifungue zahanati hizi kwani nguvu za wananchi na Serikali zimepotea bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, katika sakata la vyeti feki, uhakiki wa vyeti, Wilaya yangu imeathirika sana hasa katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga na Hospitali ya Kipatimu. Madaktari tegemezi wamekumbwa na tatizo hilo. Naomba watakapopanga mgawanyo wa Madaktari kutokana na tatizo hili, Wilaya yangu iangaliwe kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niseme yangu katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kutoa pole zangu kwa wenzetu wa Arusha kutokana na msiba wa wanafunzi. Namwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuunga mkono wale wote wanaosema kwamba bajeti ya Wizara hii iongezwe. Kwa ukweli kabisa kama tuna kusudio la kutaka kuwatendea haki wananchi wa Tanzania, basi tuna kila sababu ya kuongeza bajeti ya Wizara hii ili wananchi wakapate maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, falsafa ya kumtua mama ndoo kichwani, ililenga zaidi kwa wananchi wanaoishi vijijini. Kwa mazingira yetu, sehemu nyingi za mijini zina maji na ikiwezekana miundombinu yake, maji haya yanaenda kabisa mpaka majumbani. Sehemu ambazo bado akinamama wanabeba ndoo kichwani ni sehemu za vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia bajeti, bado imekuwa na upendeleo zaidi kwa maeneo ya mijini kuliko maeneo ya vijijini. Jimbo langu ni la kijijini na hakuna mradi wowote wa maji uliotengwa katika bajeti hii. Nimesoma kwenye kitabu hiki hakuna chochote kilichowekwa kule. Sasa ina maana kwamba mwaka huu wa fedha unanipita hivi hivi. Namwomba Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini awaangalie, hakuna chochote alichotenga kwa ajili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimeangalia pale, Mkoa wa Lindi umetengewa pesa kama 1.1 billion fedha za wafadhili. Basi naomba zile pesa ziwaangalie pia wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nachukua nafasi hii kupendekeza kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini, kwa sababu vinginevyo basi mgawanyo wa keki hii, wenzetu wa mijini au wenzetu wa baadhi ya Majimbo watakuwa wanapata zaidi kuliko sehemu nyingine. Kwa hiyo, basi uanzishwe Wakala wa Maji Vijijini ili vile vijiji ambako ndiko Watanzania wengi wanaishi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, nijielekeze katika matatizo ya maji katika Jimbo langu. Jimbo langu ambalo lina Kata 13, kuna Kata kama sita hivi, bado hazijawa na mradi wowote wa maji. Kuna Kata ya Somanga ambayo iko pale barabarani haina mradi wa maji, Kata ya Kinjumbi, Kata ya Kibata, Kata ya Chumo, Kata ya Namayuni na baadhi ya vijiji katika Kata ya Kipatimu; kuna Vijiji vya Nandete, Intikimwaga, Nandemo, Mkarango na Kijiji cha Nasaya; vyote hivi havina mradi wowote wa maji. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri ayaangalie maeneo hayo nao waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza utekelezaji wa Wizara kwa Mradi wa Maji wa Mingumbi Mitete. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukishirikiana na ule mradi umeelekea kukamilika. Ule mradi unapitia katika Kijiji cha Njia Nne. Namwomba Mheshimiwa Waziri wananchi wa Kijiji cha Njia Nne wapate maji katika mradi ule kwa sababu haiwezekani likapita bomba tu pale halafu wao waliangalie. Ule mradi unaopeleka maji katika Vijiji vya Mingumbi, Poroti, Nangambi na Ipuli, Tingi, Mtandango na Miteja, lakini wale wa Njia Nne wamesahaulika. Kwa hiyo, naomba pia na wale wa Njia Nne waweze kupata maji katika ule mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, nijielekeze katika matumizi ya chanzo cha Mto Rufiji. Tumekuwa tukiona hapa, vyanzo vyote vikubwa vya maji tayari vinatumika kwa ajili ya matumizi ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo. Kuna chanzo cha Ziwa Victoria, Mto Malagarasi na sehemu nyingine; lakini mpaka sasa na nimekuwa nikishauri mara kadhaa, Serikali haijakiangalia chanzo cha Mto Rufiji kwa ajili ya wananchi wa Rufiji na Kilwa. Mpaka sasa yale maji yanapotea tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji wanaita RUBADA. Wapo pale, lakini sioni kama kuna jitihada zozote zinazofanyika, maana hakuna mipango yoyote ya umwagiliaji inafanyika pale; yale maji yanatupita tu hivi hivi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie ana mpango gani wa kuhakikisha kile chanzo cha Mto Rufiji kinatumika kwa manufaa ya watu wa Rufiji, Kibiti, Kilwa, Kilwa Kusini na maeneo ya jirani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nijielekeze katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali anaeleza kuwa kuna zaidi ya pesa shilingi bilioni nne zinapotea kutokana na miradi kukamilika, lakini kutotumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na tumefanya ziara za ukaguzi wa miradi maendeleo katika sehemu mbalimbali za nchi hii. Tulichojifunza huko, kuna miradi mingi inakamilika, lakini haitumiki na moja ya miradi hiyo ni miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna mradi kule Nachingwea, kuna mradi kule Tabora, miradi ile imekamilika lakini haitumiki. Tatizo kubwa, kuna shida kubwa kwa Ma-planner wetu wa Halmashauri. Wasanifu wetu, wanasanifu miradi ambayo baada ya kuja kukamilika wananchi wanashindwa kuitumia. Kwa mfano, kuna mradi pale Nachingwea, ili wananchi waweze kutumia ule mradi, basi inahitaji ndoo moja ya maji inunuliwe kwa sh.300/= kitu ambacho wananchi hawawezi kumudu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna shida kubwa kwa wataalam wetu wa Halmashauri kusanifu hii miradi. Naomba wataalam wanapokaa na kusanifu hii miradi wawe makini sana na wawashirikishe wananchi kuona namna gani wao wanaweza wakaimudu hiyo miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu katika muda huu wa dakika tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya kuhamisha mifugo kutoka katika Mikoa ya wafugaji kupeleka Mikoa ya Kusini na hasa Mkoa wa Lindi yameleta athari kubwa za mazingira. Na kimsingi hakukufanyika upembuzi yakinifu wa namna gani mazingira yataathirika, maamuzi yale yamepelekea kuathiri sekta ya utalii, mazingira lakini pamoja na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kijiji cha Ngea kuna zaidi ya mifugo 10,000 iko pale, lakini kijiji hiko hakiko katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya mifugo. Lakini ndicho kijiji ambacho kina hifadhi ya misitu ya Likonde na Mitalule na mifugo ile ipo ndani mle mle. Kwa hiyo sasa hivi kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika hifadhi ile.
Lakini isitoshe katika kile kijiji kuna Bwawa la Maliwe, bwawa ambalo linatunza viboko wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya ziara kule kina cha maji katika Bwawa la Maliwe kinapungua kwa sababu lile bwawa liko jirani kabisa na Hifadhi za Misitu ile. Hivyo basi kutokana na uwepo wa mifugo maana yake mifugo inapelekea mmomonyoko wa ardhi na hivyo kina cha bwawa lile la Maliwe kinapungua. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuiomba Wizara ifuatilie katika maeneo hayo ninayoyaeleza kwa sababu vinginevyo mazingira ya uhifadhi wa misitu ni kama yanaenda kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la wakulima na shughuli zao za kilimo. Wakulima katika msimu wa mwaka huu katika kijiji cha Ngea na vijiji vya jirani ni kama hakuna watakachovuna kwa sababu mazao yote yameharibiwa na mifugo. Kwa hiyo, niiombe Serikali pia iangalie suala hilo ili basi wakulima wetu waweze kuepukana na baa la njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza katika jitihada za kuhakikisha kwamba ile mifugo inatolewa pale Serikali ya Wilaya ya Kilwa ilifungua kesi mahakamani ili basi kuwaondoa wale wafugaji. Lakini katika hali ya kushangaza kwenda mahakamani Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilwa imeshindwa mahakamani na wananchi wanalalamika kwamba inaonekana kuna dalili ya rushwa. Wananchi wanalalamika iweje vyombo vya ulinzi na usalama vimeenda kuwakamata wafugaji katika maeneo ambayo hawakupasa wawepo, lakini wanapoenda mahakamani wanashindwa. Kwa hiyo niombe Wizara ifuatilie suala hilo wananchi wa maeneo hayo wanapatashida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna suala la fidia kutokana na uharibifu unaofanywa na wanyama au kwa mazao au kwa binadamu. Katika jimbo langu la Kilwa Kaskazini tunapakana na Hifadhi ya Selous kuna wananchi wamejeruhiwa na wanyama, lakini taratibu zote zinazofanywa ili basi kupata fidia inachukua miaka mingi kupata fidia kutoka Wizarani. Kwa hiyo, niiombe Wizara kwamba kama ambavyo ninyi mnachukua hatua za haraka pale mwananchi anapomjeruhi mnyama au anapoua mnyama, basi iwe hivyo hivyo pale mnyama anapomjeruhi mwananchi zile fidia zipatikane kwa haraka. (Makofi)

Lakini sio hivyo tuu kuna suala zima la mashamba, kuna ekari nyingi za wananchi zimeharibiwa na ndovu, lakini taratibu zimefuatwa kupitia Maafisa wenu wa Maliasili lakini hakuna chochote kinafanyika baada ya taarifa kufika kwenu. Naomba sana hayo myazingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mipaka kati ya hifadhi hizi na wanavijiji. Kuna tatizo kubwa la mipaka katika kijiji cha Namatewa na kijiji cha Ngarambe. Wananchi wako pale toka siku nyingi lakini sasa hivi inaonekana wenzetu wa Selous wanaidai katika eneo ambalo wananchi wapo wanadai kuwa ni eneo la kwao, kwa hiyo, tayari kumekuwa na migogoro baina ya hifadhi ya Selous na wananchi. Kwa hiyo, niiombe Wizara na hilo lishughulikiwe ili mgogoro uweze kuisha. Ahsante sana, nashukuru.