Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jitu Vrajlal Soni (67 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake nzima kwa kazi na juhudi kubwa wanayofanya kuleta maendeleo ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchagua timu nzuri, timu ya hapa ni kazi tu, wametuonesha kwa vitendo kasi yao mpaka wengine tunafikiria tunafanyaje na sisi twende na kasi hiyo. Wenzetu wameanza kufikiria na imebidi watoke hapa ndani waende wakajipange huko nje ili na wao waweze kwenda na kasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika maeneo machache. Serikali imedhamiria kuleta maendeleo kwa kasi kubwa. Zile sekta ambazo imeahidi kwamba zitafanyiwa kazi, moja ni sekta ya kilimo tujikite vizuri, bajeti ya kilimo ambayo tutakuja kupitisha hapa wote tuiangalie vizuri iweze kufikia katika lile lengo tulilojiwekea la Maputo Declaration la asilimia kumi. Asilimia kubwa ya wananchi wetu ndiyo wapo huko vijijini na tukitenga bajeti kubwa kwenye sekta hii ya kilimo mambo mengi yatawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Wabunge wote tuunge mkono hoja ya kuongeza fedha ya kutosha katika mambo ya research and development. Bila utafiti hatutaweza kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na-declare interest, nipo kwenye Kamati ya Bajeti, katika hoja za awali tumeona fedha zilizotengwa upande wa utafiti ni ndogo sana, ni vizuri tujipange. Bila utafiti wetu wa ndani ya nchi iwe kwenye kilimo, mifugo, afya au jambo lolote hatutaweza kusonga mbele. Naomba Serikali kwa upande wa utafiti tuwekeze fedha ya kutosha ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia upande wa pili ni kwenye masuala ya mazingira. Tumebaki kusemea tu mambo ya mazingira kama jambo la kawaida, tunalisema linapita, hakuna mpango thabiti. Ni lazima Mfuko huu wa Mazingira tuufanyie kazi. Mfuko upo kisheria ni vizuri tuhakikishe kwamba unapatiwa vyanzo vya uhakika vya mapato ili tuweze kwenda kuboresha mazingira yetu. Hali hii ambayo tunakwenda nayo kwa sasa hivi kutokana na tabia nchi ni vizuri tuwekeze pia kwenye masuala ya mazingira la sivyo sisi kila siku tutakuwa watu wa kuangalia Mfuko wa Maafa kujazia badala ya kuangalia kutibu. Bora kinga kuliko tiba na namna ya kukinga ni kuwekeza kwenye masuala ya mazingira. Kwa hiyo, naomba tujitahidi sana kuwekeza katika masuala yanayohusu mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu zaidi niishauri Serikali juu ya coordination baina ya Wizara moja na nyingine. Mwanzo ni mzuri lakini bado jitihada kubwa inatakiwa baina ya Wizara moja na nyingine coordination ile iwepo zaidi. Wasiwe kama wanashindana, wote mnakwenda kujenga nyumba moja, msishindanie fito. Kwa hiyo, mjitahidi coordination baina ya Wizara mbalimbali iwe ya uhakika na iwe lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naomba katika Mkoa wa Manyara, wilaya zote masuala ya miundombinu yawekewe mikakati. Hii Mifuko yote ambayo tumeiunda tuhakikishe kwamba zile fedha mahali ambapo tumelenga ziweze kwenda. Mimi nishukuru kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu umepunguziwa kazi ya TAMISEMI sasa imepelekwa Ofisi ya Rais. Utakuwa na muda wa kutosha na ni muafaka sasa kuhakikisha unasimamia Wizara nyingine zote na kufanya kazi ya kutembea katika wilaya na mikoa yetu kuhakikisha kwamba kazi inakwenda vizuri, uratibu wako sasa utakuwa wa uhakika zaidi. Badala ya kuwa mezani na ofisini sasa utaweza kutembea na kutoa maamuzi wakati unafanya ziara zako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu naomba Wabunge wote tuunge mkono suala la nishati na maji na hapo hapo tukiunganisha na suala la Mfuko wa Mazingira na utafiti. Bei ya mafuta iliposhuka duniani, leo bei ya mafuta ya jumla kwa diesel ni Sh.1,500. Napendekeza tuipandishe bei mpaka ifike Sh.1,700 ili ile Sh.200 inayopatikana iende kwenye Mfuko wa Maji, Umeme Vijijini pamoja na Mazingira na utafiti ili ile fedha iweze kupeleka nishati, maji na masuala ya mazingira na utafiti kwa haraka zaidi. Baada ya bei kuteremka hakuna Mtanzania aliyenufaika, hakuna nauli iliyoshuka, hakuna bidhaa yoyote iliyoshuka isipokuwa wafanyabiashara wachache wameendelea kupata ile faida kubwa na ile faida hata kodi yake hawalipi kwamba Serikali inapata kodi kutokana na suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ya Fedha pamoja na Mawaziri wa Maji, Mazingira, Nishati na Elimu waangalie Wizara zao zinapokuja kuleta bajeti basi fedha hizo zitumike kuongeza Mfuko wa Mazingira, Mfuko wa Maji na Mfuko huo wa Nishati na utafiti ili kasi ya maendeleo iweze kwenda huko vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bado ni muumini wa maendeleo vijijini zaidi kwa sababu huko vijijini ukiboresha huduma mbalimbali, iwe ya maji, elimu, afya basi wananchi hawatakuwa na hamu ya kuhamia mijini na pia huku mijini tayari kuna maendeleo makubwa. Kwa hiyo, Serikali ijikite zaidi kupeleka maendeleo katika sehemu mbalimbali huko vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nimshukuru Mheshimiwa Lukuvi, nimshukuru Mheshimiwa Mwigulu na Waziri wa Maliasili, Wilaya ya Babati ina matatizo makubwa sana ya ardhi. Tatizo hilo likiisha basi Wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara unaweza kuwa moja katika mikoa ya mfano ambapo maendeleo yatakuwa kwa kasi sehemu kubwa. Tunaomba mjitahidi, tunaomba ushirikiano wenu ili tuweze kumaliza migogoro hii ambayo imedumu kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niendelee kusisitiza kwamba kuna haja kubwa sasa, wenzangu pia walichangia kuhusu suala la kuunganisha utawala kuanzia juu kwenda chini, hii D by D, kwa sasa chain ile kuna mahali inakatika.
Ni vizuri tujaribu kuangalia upya sera namna ya kuunganisha hiyo chain ili maendeleo yakipangwa kuanzia ngazi ya chini kuja huku juu basi yaweze kwenda kwa kasi tunayoitarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kushukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia leo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa juhudi na kazi kubwa wanayoonesha na tumeona ushauri mbalimbali ambao unaendelea kutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuomba Serikali ikubali na Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iwe ndiyo chombo cha kuunganisha Wizara zote, kwa sababu leo hii hakuna chombo cha kuratibu. Kila Wizara inakuwa inafanya kazi kipekee. Muunganike mfanye kazi kama Serikali moja yenye lengo moja. Wizara hii ndiyo iwe mratibu (coordinator), ndiyo iwe kiunganishi, kwa sababu masuala yote ya biashara na uwekezaji inapitia katika sekta hii ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu kuliko yote, tuwe na mabadiliko ya fikra (mind set change) na tukishakuwa na mabadiliko hayo ya kifikra, naamini haya yote tunayotarajia itawezekana. Wote tuondoe ile dhana kwamba Serikali itakwenda kuweka kiwanda kidogo cha nini hapa na cha hii; Serikali iweke Sera nzuri, iweke namna ambayo watu wote tutaweza kwenda kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara, badala ya wataalam wote wa ngazi ya Wizara na ngazi ya Mkoa, kuwa wanaandika tu hizi leseni na kuchukua tozo, wabadilike wafanye kazi ya namna ya kutushauri. Wako Watanzania wenye mitaji yao kuanzia midogo na mikubwa waweze kuwekeza. Kwa mfano, hivi mtu anayewekeza kwenye Petrol Station kwa shilingi milioni 600, ni viwanda vingapi vya alizeti? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kazi ya Wizara ibadilike; badala wale wataalam kukaa na kuandika leseni, hata mtoto wa darasa la saba anaweza kutuandikia leseni. Wao waanze kutushauri, wenye mitaji wapo, mtuambie fursa ziko wapi, Watanzania watawekeza wenyewe. Serikali ibaki kwenye ile ya mradi mikubwa, yaani kwenye zile flagship projects. Iandae miundombinu, sera nzuri, Watanzania waweze kuwekeza kwenye viwanda vidogo na vya kati, wataweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la muhimu ambalo linatakiwa kufanywa ni kuangalia sera mbalimbali; Regulatory Bodies zimekuwa nyingi mno. Leo hii Wizara ingefanya utafiti kwamba kwa nini leo tumesema tupandishe kodi kwenye ngozi ghafi na kwenye korosho ghafi, tumeongeza kodi nyingi za export levy, kwa nini bado tuna-export mali ghafi ambayo bado haijasindikwa? Kwa sababu hata pamoja na kuwa umepandisha kodi, ukijumlisha, ukizalisha ndani ya nchi, kodi zote zile za Regulatory Bodies na tozo mbalimbali ni kubwa kuliko hiyo kodi iliyopandishwa ya ku-export. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wasipokaa na kubadilisha na kuangalia kwa kulifanyia utafiti, bado hii dhana kwamba tutaelekea kwenye uchumi wa viwanda, hatutafikia. Leo hii kwa mfano kwenye mbegu, kwenye madawa ya kilimo, mifugo na chanjo, ukizalisha ndani ya nchi ina kodi zote na ina tozo. Ukitoa nje kuleta ndani vitu hivyo hivyo, havina kodi? Hasa je, hapo unafanya kwamba watu wazalishe ndani ya nchi au tunafanya tuzalishe nje. Kwa hiyo, sera ndiyo kitu muhimu kuliko yote. Sera zikiwekwa vizuri na uongozi (lead) uchukuliwe na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naamini Mheshimiwa Waziri na timu yake ya wataalam wataweza kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la muhimu ni suala la BRELA, tunaomba iwe kwenye kanda na iwe kwenye kila mkoa. Tuanze na kanda ili usumbufu wa kuja mpaka Dar es Salaam kupata huduma hiyo, ingawa mko online lakini bado lazima uje Dar es Salaam. Ni vizuri tuwe kikanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi Regulatory Bodies nyingi zinafanya kazi za aina moja; nashauri kwamba zote zisiruhusiwe kutoza. Tozo iwe sehemu moja; ukishakata leseni, unalipia kila kitu huko, Serikali ndiyo ipeleke OC huko kila mahali. Hapo ndiyo tutaweza. Mfanyabiashara hataki bughudha, siyo kama anakaa kulipa, lakini bughudha ya kila wakati isiwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tulikuwa tunasema tuwekeze kwenye elimu, kwenye masuala ya VETA. Tumeweka kodi ya 5% SDL, tumeigawa ile kwenda leo kulipia mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu. Naomba asilimia yote tano iende kwenye VETA zetu. Tunahitaji kuwa na hawa technical skilled people ili kwenye hivi viwanda vidogo vidogo na kati tuweze kwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine muhimu tena ni Sheria ya Manunuzi. Bila kubadilisha Sheria ya Manunuzi haraka, huo mwelekeo tunaoutaka hatutaweza kuufikia. Ni lazima Serikali iangalie namna ya kulinda viwanda vyake vya ndani. Nchi zote zinatoa ruzuku, zinalinda viwanda vyao vya ndani, leo hii katika bidhaa ambazo tunaagiza kutoka nje, naomba muweke dumping charge kubwa. Kwa mfano, kwenye chuma, nondo na bidhaa nyingine za chuma, iwekwe dumping charge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika mafuta ya kula ambayo yanaagizwa kutoka nje, waweke kodi na ile kodi iwe ring fenced iweze kutumika kwenda kuendeleza mazao ya kukamua mafuta ya ndani. Kwenye VAT wanaozalisha mafuta ndani ya nchi, waondoe ile VAT, kwa sababu wanafanya watu waondoke kwenye formal sector na kurudi kuwa informal. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lingine ambalo wafanyabiashara wengi wangependa ni kuwa na one stop center. Nikilipa sehemu moja, basi sihangaishwi kwenda ofisi mbalimbali na wakati wanapokuja kukagua, wakague wanapotaka, saa yoyote lakini waje kama timu. Kama mtu wa weights and measurement, TFDA, TBS wote wawe humo humo, wakija wataalam wanakuja mara moja, basi siyo kila siku. Leo amekuja huyu, kesho huyu, kwa hiyo, hayo wakiyaweza, naamini huko tunakotaka tutaweza kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ifanye uchambuzi na research. Naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote, tukubaliane, nimependekeza kwamba sh. 50/= kwa kila lita ya mafuta iende kwenye Mfuko Maalum kwa ajili ya utafiti, yaani research. Tukifanya hivyo, tutapata karibu shilingi bilioni 90 kwa miezi sita. Leo tumeweka kama shilingi bilioni nane kwa utafiti Tanzania nzima. Mfuko huu wa utafiti ukiwepo kwenye kilimo, mifugo, afya kila mahali, hata viwanda na biashara, wote watakuwa na hizo fedha za research, kwa sababu bila research nchi hii hatutakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara tungependa wale wenye viwanda, wale wenye biashara, wataalam wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji waje wawashauri kwamba hapa fanya moja, mbili, tatu utapunguza gharama ya uzalishaji, fanya moja, mbili utapata tija zaidi. Hiyo ndiyo iwe kazi ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa sababu wawe regulators, wawe washauri, wawekezaji wapo katika sekta zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia leo hii kwa nini, tujiulize kwa mfano, Sekta ya horticulture ambayo ndiyo sehemu kubwa kwenye kilimo inayoongeza mapato mengi, leo bidhaa zote tunapitishia Kenya kwa malori. Kwa nini hatutumii KIA? Watu wa Nyanda za Juu Kusini, Songwe, tumejenga uwanja kwa mabilioni ya fedha, kwa nini hautumiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kazi ya Wizara hii inatakiwa ndiyo iwe ya kuhakikisha kwamba ushauri unaotolewa, Serikali inakalisha Wizara zote ambazo zinahusika ili ku-regulate na kuangalia namna bora na kuweka mazingira wezeshi kwa watu kuwekeza ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna Taasisi kama TEMDO, CAMATEC, TIRDO, kuna taasisi nyingi ambazo zinafanya utafiti mbalimbali; nyingi katika hizo zinafanya kazi moja. Hebu mziunganishe ziwe moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukija kwenye Bodi ya Mazao, nashauri badala kila zao kuwa na bodi yake, wavunje bodi zote. Hii ni manyanyaso kwa wakulima na kwa walaji. Wekeni bodi moja na kwenye hiyo bodi moja pawe na idara; kama ni tumbaku, kahawa na nyingine, gharama zile zitapungua na kero kwa hao wakulima na hao wanaofanya biashara itapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yao kubwa iwe kushauri namna ya kuboresha biashara, pamoja na hiyo, wakifanya labda kuagiza kama ni pembejeo kwa bei nafuu, faida inayopatikana ndiyo itumike kuendesha zile bodi, isiwe makato kwa wakulima, wavuvi na wafugaji. Kwa hiyo, la muhimu, bado tunarudia pale, ni sera. Kwa hiyo, tunaomba na naamini Mheshimiwa Waziri uwezo huo anao na timu yake kwa kupitia Dkt. Abedi, Katibu Mkuu, waweke Sera bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Awamu ya Tano, kwa kuunda Baraza zuri, Baraza lenye kuleta matumaini kwa wananchi wote. Nimpongeze Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Utumishi na Naibu wake na wataalam wote ambao wako Wizarani kwa juhudi zao walizoonesha ndani ya muda mfupi huu ambao wametuletea matumaini mapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo machache naomba niendelee kuishauri Serikali ambayo wamendelea kuyafanyia kazi ili tuendelee kuboresha. Kazi ya Wabunge siku zote ni kuendelea kuboresha yale ya Serikali na kuisimamia kuhakikisha yale ambayo tunayapitisha basi, Serikali iendelee kufuatilia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja naomba suala la utawala bora. Suala la customer charter ni muhimu sana lirudishwe na huduma ile wananchi wapewe mafunzo, waelimishwe kutokana na suala la customer charter, pia kila mtumishi yale masuala yarudiwe na wananchi wajue kabisa kwamba huduma ambayo wanaenda kuipata kwenye ofisi yoyote au taasisi yoyote wanatakiwa kupata haki gani, lakini muhimu pia muda wa kazi kwamba, ndani ya muda wa masaa nane au ndani ya muda wa kazi wa mtumishi anatakiwa kufanya kazi kiasi gani, ili tuwe na ufanisi, tukifikia huko naamini ufanisi utakuwepo kwa sehemu kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba wataalam kwa mfano hawa wa mipango, wengi wasibakie huku ngazi ya Taifa, tunao mmoja mmoja kwenye Halmashauri, Maafisa Mipango wangetakiwa kuwepo ngazi zote, hasa pangekuwa na timu kubwa ndani ya Wilaya ambapo wangeenda mpaka ngazi za vijiji ili kuibua miradi ambayo wananchi wanataka itekelezwe hasa kwenye huu mpango wa TASAF kwa sababu wananchi wakiambiwa tuchangie basi kwa sababu kero ni darasa, watachangia wataomba kujengewa darasa. Kumbe wangekuwa na mipango wangeomba miradi ambayo wangewekeza kwenye ile miradi, ikawapatia kipato na wakajenga darasa, zahanati na hayo mengine yote. Kwa hiyo, suala la mipango liwekewe umuhimu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaomba suala hili la kumaliza masuala ya watendaji ngazi ya vijiji, kata, wao ni muhimu, ndiyo mahali ambapo pesa zote hizi tutazowekeza asilimia 40 ya maendeleo inaenda kufanya kazi huko. Kwa hiyo, ni jambo muhimu kwamba, awamu hii mmalize hawa wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri alipotoa tamko kwamba mapato yote ya Halmashauri sasa yakusanywe kwa njia ya elektroniki; nakupongeza kwa hilo ni jambo zuri sana. Ombi langu litakuwa moja, kwenye sehemu moja tu kwenye kukusanya ushuru wa mazao, ninaomba hilo sasa lifanyiwe kazi kwa namna yake kwa sababu tukienda moja kwa moja kukusanya ushuru wa mazao kwa kupitia watumishi wetu hatutafanikiwa, kwa sababu leo hii kwanza hatuna watumishi wa kutosha kwa kazi hiyo kwa ngazi zote na ile kazi ni ya saa 24. Ombi lilikuwa ni kwamba kwenye hiyo sehemu moja tu watumike mawakala wa kutumia elektroniki halafu tuelewane na wakala kwamba, asilimia ngapi atakapokusanya, basi Halmashauri ielewane na huyo wakala la sivyo tutajikuta tunapoteza mapato mengi sana kwenye section hiyo moja, mengine yote napongeza ni jambo jema na nina uhakika kwamba, tutapata mapato mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba TAMISEMI itusaidie, makampuni mengi ya simu hayalipi kabisa ushuru ule wa huduma kwenye Halmashauri zetu. Tunaomba TAMISEMI kwa niaba ya Halmashauri zote ikusanye ule ushuru halafu mtugawie kwa uwiano siyo kwamba ambaye hana minara asipate. Ile ni haki yetu wote kwa sababu, simu kila mahali tunapiga. Mkusanye zile pesa, badala ya zile pesa kwenda headquarters pale Dar es Salaam kwenye Wilaya moja, pesa yote nyingi inalipwa pale, ni haki yetu wote tupate hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la hotel levy, kuna suala la hizi tozo mbalimbali kwa mfano ya maliasili, ardhi, zile zikikusanywa na Halmashauri zetu zinachelewa kurudi. Sasa tungeboresha mfumo kwa sababu ni electronic ile tunayokusanya ya Serikali Kuu tuwaachie Serikali Kuu ile ya kwetu tubakinayo kwa sababu, inapoenda mpaka irudi inachelewa sana. Kwa hiyo, jambo hilo kwa sababu, tunaenda na mfumo huu wa TEHAMA ninaomba mlifanyie kazi, ili zile pesa ziende kwenye maendeleo moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine muhimu ni kwa ujumla. Kwa sababu pesa nyingi sana itaenda kwenye maendeleo ni Sheria ya Manunuzi. Naomba sheria ile iletwe mapema tuifanyie kazi, tuibadilishe kwa sababu bila hiyo, utaendelea kuhalalisha wizi ambao unafanywa huko kwa kupitia hii Sheria ya Manunuzi kwa sababu gharama zote ni mara mbili au mara tatu. Hizi pesa zote zikienda tukishabadilisha Sheria ya Manunuzi ina maana maendeleo utayaona mara tatu ya hiyo ambayo tunaiona leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingne ni TEMESA, tunaomba muingalie upya. Kazi ndogondogo ambazo hata dereva anaweza kubadilisha fan belt inabidi upeleke TEMESA! Fan belt ya shilingi 90,000 kwenye cruiser, dereva anaweza kufunga mwenyewe, unachajiwa karibu mpaka shilingi 500,000! TEMESA ni kero, TEMESA ni moja katika majipu ambayo yanatakiwa yatumbuliwe moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kazi ndogondogo za service ya magari na nini, naomba maeneo penye VETA tungewapa VETA ili wale wanafunzi wa pale kwa sababu, wana wakufunzi wapate mafunzo na pia watatusaidia ku-service haya magari kwa bei ya kawaida kabisa. Kwa hiyo, huku tutasaidia kwenye sekta ya elimu, lakini pia itakuwa tumepunguza gharama nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa sababu tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, ninaomba Serikali ikae kwa sababu sehemu kubwa itakuwa inahusika na utawala bora na pia, masuala ya TAMISEMI, hizi regulatory boards. Hizi ndiyo zimekuwa kero na ni matatizo makubwa, tozo nyingi. Hata tukiwekeza kwenye viwanda, siyo kwamba watu hawapendi kuwekeza. Wala huhitaji kutafuta mitaji nje, Watanzania wana uwezo wa kuwekeza, lakini wenye kupiga mahesabu, utaweka kiwanda bado itakuwa rahisi wewe kutoa vitu nje kwa gharama nafuu kuliko hapa kwa sababu, mfano mzuri ni kwenye ngozi; tumepandisha ngozi asilimia 90 ku-export, korosho tumepandisha, lakini bado inaenda ghafi kwa sababu ukizalisha hapa badala ya asilimia 90 utakayolipa export levy unajikuta unalipa asilimia 125 kwa sababu ya tozo mbalimbali na kodi ambayo unatakiwa kulipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuelekee huko Serikali nzima ikae, m-regulate, mhakikishe kwamba, huko tunakoelekea tusije tukakwama kwa sababu ya urasimu na mambo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya nipongeze kazi inayoendelea, kazi inayofanyika ni kubwa na juhudi zimeonekana. Tutakachoomba kuna vitu wananchi mahali ambapo wamejitahidi na Halmashauri zetu vituo vya afya, zahanati, mahali ambapo wamewekeza vizuri, kuna kada za watumishi ambao hawajapangwa kwenda ngazi hizo; kwa mfano Kituo cha Afya Magugu, tuna uwezo sasa hivi kimefanana kabisa na hospitali, sasa tunaomba mtupangie watumishi ambao wataweza kuendesha kituo cha afya hicho kwa sababu vifaa vingi tayari tumeweza kununua. Kwa hiyo, maeneo ambapo wananchi wanajitahidi ngazi ya kijiji, zahanati na vituo vya afya, basi mtuunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni suala la elimu. Mimi ningeomba Serikali ichukue hatua zaidi, tuna vyuo vingi sasa hivi na shule nyingi na nyingi ni private zinadahili watu ambao hawana vigezo, baadae shule hizo hazijasajiliwa, badae tunakuja kupata kesi. Moja ni kama hii St. Joseph. Sasa tayari inakuwa mpira kwa kila mtu. Sisi tumewekeza kwa wanafunzi wetu tumewachangia huko wengi na kwa nini wale Wakaguzi kuanzia siku ya kwanza kama walikosea hawakuchukuliwa hatua?
Kwa hiyo, ni jambo ambalo naomba mlifanyie kazi, wanafunzi wako 504, kama walikuwa hawana vigezo wamefika mpaka mwaka wa nne tulikuwa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale wote waliohusika wapelekwe mahakamani. Kama ni upande wa Serikali, kama ni mwenye chuo, wote wafikishwe mahakamani, muda huu hawa Watanzania waliopoteza hauwezi kwenda bure. Kwa hiyo, naomba kwenye hilo Serikali ijitahidi na tulifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine kulikuwa na suala la maji. Mimi naomba Serikali iwekeze zaidi kwa wataalam kwenye upande wa maji vijijini. Huko katika Halmashauri zetu hatuna wataalam wa kutosha. Pesa inayoenda huko ni nyingi, miradi mingine inakuwa chini ya viwango kutokana na kukosa wataalam, pia ninaendelea kuishauri, kama nilivyosema juzi, kwenye ile shilingi 200 niliyopendekeza iongezwe kwenye mafuta, tena shilingi 70 nyingine iende kwenye maji, shilingi 70 kwenye umeme, shilingi 50 kwenye suala la utafiti na shilingi 10 kwenye suala la mazingira ili tatizo la maji huko vijijini liweze kuisha.
Mheshimiwa pia tunaomba kwamba Sekretarieti ya Utumishi katika Ofisi ya Rais waboreshewe ili waweze kuwa katika kanda zote, waweze kufanya kazi na namna ya kushauri Halmashauri zetu na uko Wilayani ili tuweze kuwa na watumishi bora na wao pia wawe na jukumu hilo la kutoa elimu hiyo ya mambo ya customer chater ili kwenda vizuri, muhimu kwamba watumishi wetu wangekuwa wanatoa hizo huduma vizuri ninaamini kabisa kwamba Tanzania tungesonga mbele na huduma ingekuwa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la TASAF, ninaipongeza Serikali kwa mradi mzuri, lakini bado naendelea kusema mtuletee wataalam wa mipango wakati inapofika ngazi ya kuanzisha miradi, tuwe na wataalam watakaoibua miradi huko chini ili tuweze kufanya vizuri zaidi, wananchi wawe na miradi ambayo itawapatia kipato na uchumi ambao wao baadaye watachangia katika miradi mbalimbali. Huko ndiyo tuanzishe mfumo ambao tuna mifuko mingi ambayo tunapeleka huko, kwa mfano Mfuko wa Wanawake na Vijana, hii ya TASAF zote tuziratibu ziwe moja ili maendeleo yaonekane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue nafasi hii kukupongeza kwa namna unavyoendesha Bunge hili na naamini kwamba kuanzia siku ya kwanza ingekuwa wote tunasimamia kanuni na utaratibu ambao tumejiwekea kisheria, haya mambo yote yasingetokea. Kwa hiyo, uendelee na msimamo huo kwa sababu bado huu ndiyo mwanzo. Kwa hiyo tukianza kuzoea kufuata taratibu, kanuni na sheria huko mbele ya safari tutakuwa tunakuja hapa na kulenga hoja mbalimbali katika kuishauri na kuisimamia Serikali, hizi siasa nyingine zote tutazifanya huko nje ya hapa. Kwa hiyo, nakupongeza sana na naomba uendelee na msimamo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu wake, Katibu Mkuu ambaye anaongoza na timu nzima ya wataalam kwa juhudi kubwa wanayofanya na wametuletea Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Wizara yao, ambapo Wizara hii ndio Wizara mama inasimamia Wizara nyingine zote. Mafanikio yao ndiyo mafanikio ya Wizara nyingine zote. Kwa hiyo, nimpongeze Rais kwanza kwa kuwateua, lakini kwa uzoefu wake Waziri na timu yao na namna wanavyokubali ushauri, niwapongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye masuala mawili muhimu. Moja, wenzangu wengi wamesema, ni Sheria ya Manunuzi. Naomba nisisitize kwa Wabunge wenzangu wote; kama itatokea kwamba sheria hii haijaletwa muda bado tunao wa siku 21 wa kuleta hoja binafsi ya kubadilisha baadhi ya vipengele ili fedha nyingi ambazo tutapeleka kwenye maendeleo, asilimia 40, zikatumike vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama itakuwa tupo nje ya muda basi nitaomba Wabunge wenzangu wote tukubaliane tutakapopitisha Bajeti Kuu ya Serikali tuweke kipengele kwamba pesa za maendeleo hata shilingi isitumike mpaka hapo hiyo sheria itakaporekebishwa. Fedha ziwekwe kwenye akaunti maalum, sheria ije, ikipita ndipo fedha zitumike, kwa sababu hiki kimekuwa ni kilio cha miaka mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nizungumzie juu ya Sheria ya Micro-Finance. Serikali imekuja na mpango mzuri wa kupeleka milioni 50 kwa kila Kijiji. Kule ni masuala ya Village Empowerment, ile milioni 50 kama VICOBA haitakuwa kisheria ambapo inategemeana na Sheria hiyo ya Micro-Finance bado tutarudi pale pale. Kwa hiyo, ningeomba sheria ya Micro-Finance ni muhimu ije mapema ili zile fedha zikienda kule usimamizi wake uwe kisheria na uweze kusimamiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbali na hiyo pia ningeomba Wizara ya Fedha iishauri Serikali ingalie namna ya kuhakikisha kwamba tunapata sheria. Asilimia kubwa ya taasisi zetu za Serikali ambazo zinafanya huduma mbalimbali; kwa mfano huduma za simu na data za TTCL, lakini pia NIC. Hapa tumeoneshwa kwenye kitabu, Waziri ametaja baadhi ya mashirika ambayo yanafanya biashara na NIC; leo NIC haina mtaji mkubwa. Ningeshauri kazi zote za Serikali iwepo sheria kwamba zote ziende NIC. Mashirika mengi ya umma hayapeleki kazi huko, kwa hiyo taasisi zote za umma na Serikali zifanye kazi na TTCL, NIC, kazi nyingi ziende VETA, ziende Magereza. Taasisi za Serikali hakuna haja ya kuwapa fedha za kujiendesha wapewe biashara ili waweze kujiendesha wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ni vizuri Serikali ikaangalia namna ya kuangalia hizi regulatory bodies zote, zote ziunganishwe ziwe regulatory body moja na nyingine zote ziwe idara chini yake. Tuangalie sheria zilizounda hizo regulatory bodies ili zifanyiwe kazi na zote ziunganishwe na iwe moja; hii italeta mazingira mazuri ya kufanyia biashara nchini. Wakati wanakwenda kwenye kukagua viwanda, biashara au shughuli yoyote basi ni taasisi moja inakwenda, tozo inakuwa moja ndogo, itakuwa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara. Huko tunapotaka kuelekea, kwenye uchumi wa viwanda, hiyo body ikiwa moja tozo itapungua na ufanisi wa kazi pia utakuwa ni mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ili kupunguza gharama za kuendesha hizi bodies mbalimbali za Serikali na taasisi zake tungeangalia namna ya kuziunganisha. Kwa mfano RAHCO na TRL zote shughuli ni moja, zingeunganishwa. Mfano mwingine ni kwenye TBS na Weight and Measurements; zingeunganishwa ili shughuli hizi zote zinazofanana zifanywe na moja ili gharama za usimamizi na management yote ipungue na OC nyingi zitapungua. Kwa hiyo, tuhakikishe kwamba tunaweza kufanya namna ya kuziunganisha taasisi nyingi hizi za Serikali ili kupunguza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu nyingine nitakayoendelea kuisisitiza ni kwamba Serikali iangalie na iwe na nidhamu ya matumizi ya fedha. Fedha ambazo ni ring-fenced Wizara ya Fedha ijitahidi isitumie sehemu yoyote nyingine. Pia katika hii Mifuko mitatu; Mfuko wa Bunge, Mfuko wa Mahakama na Mfuko wa CAG, fedha zile ziwe consistent ziende kwa wakati, hasa kwenye huu Mfuko wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali; wao wanakwenda kwa calendar year na wanafuata ratiba. Tunawaomba muwape kipaumbele na zile fedha zihakikishwe kwamba zinaenda kwa wakati kufuatana na kalenda yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tutakapokuja kwenye mid-year review; kwa sababu hawataweza kufanya kazi yao inavyopaswa, ni vizuri tuangalie ili waongezewe bajeti wanayoihitaji. Kwa sababu ya fedha za maendeleo tutazoongeza, hiyo asilimia 40, ni muhimu sana watchdog, ambayo ni Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ipatiwe fedha za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la mid-term review naamini kwamba hiki kidogo ambacho Serikali inacho sasa hivi, basi tukisimamie vizuri na wote tuwe wavumilivu. Nina uhakika kutokana na uwazi na maoni na ushauri unaopokelewa na Wizara safari hii, naridhika kabisa kwamba najua huko tutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningeomba; Wizara ya Fedha kwenye Tume ya Mipango iwawezeshe sana, tena wewe mwenyewe Waziri ulikuwa huko kwa muda mrefu; tunaomba pawe na namna ya kuiunganisha Tume hiyo ifike mpaka ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa sababu huko ndio tunakopanga mipango. Kwa sababu Halmashauri na Mikoa yetu ingekuwa na mipango mizuri basi na huku juu pia hii mipango itakuwa ni endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba Tume hiyo ndiyo iwe inashauri. Kwa mfano, kwenye Halmashauri yangu na Halmashauri nyingi, Afisa Mipango ni mmoja hivyo ni ngumu sana kupanga mipango mingi. Hii mipango ikiwa integrated, yaani wakiwa wanafanya kazi kwa pamoja mafanikio ya Serikali yatakuwa yanaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu nyingine ni suala la kuhakikisha kwamba tunaongeza mapato ya Serikali. Taasisi ambayo inakusanya mapato ya Serikali (TRA) tunawapongeza, lakini kwenye baadhi ya maeneo waendelee kujirekebisha. Kwa mfano, suala la uplifting kwenye bidhaa ambazo zinaingizwa ni kero kubwa ambayo inawakatisha tamaa wafanyabishara. Lakini pia kuna kodi nyingine wanakusanya ambazo tayari sheria ilishafuta, sasa na hizo pia zifanyiwe kazi. Yale ambayo tunaongeza yaongezwe immediately lakini yaliyoondolewa pia yaondolewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu ni kwamba kila Mtanzania ajitahidi kuwa na tabia ya kulipa kodi, bila kulipa kodi sisi wenyewe basi huko hatutaweza kufika na haya malengo ambayo tunajiwekea hatutayafikia. Kwa hiyo, pawe na fair trade competition kila mahali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine muhimu ni ile Tume ya Fair Competition Commission, tunaomba basi bodi yake iundwe mapema ili hizi shughuli nyingine ambazo zinakwama kutokana na shughuli ambayo inatakiwa kufanywa na hiyo Commission basi hizo ziweze kufanywa mapema.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia sehemu nyingine muhimu ni kuhakikisha kwamba kodi na tozo zile ambazo ni kero katika biashara Wizara ya Fedha ingekuwa na timu maalum ambayo itakuwa inafanya uchunguzi, la si vyo hii ndoto yetu ya kufika kwenye uchumi wa viwanda hatutafikia na bado bidhaa za nje sisi hatutakuwa na uwezo wa kuwa kwenye ushindani nazo. Kwa hiyo, zile kodi na tozo ambazo ni kero ambazo zinafanya biashara hizo zisifanikiwe, basi ziondolewe na pawe na mazingira wezeshi ili wafanyabiashara wetu waweze kufanya biashara vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani kubwa na timu nzima ya Wizara ya Fedha na kuna masuala mengi ambayo wameweza kuweka wazi safari hii pia. Hata kile kitabu cha volume one tulipewa kabla ya muda wa bajeti, ambapo huko miaka ya nyuma huwa tunapewa siku ile ambapo Bajeti ya Serikali inasomwa, kwa hiyo hata mwelekeo wa namna ya makusanyo tayari tumeshaanza kuyajua. Muhimu tena naomba Benki hii ya Kilimo ipatiwe fedha ya kutosha ili uchumi uendelee kukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, naomba nishukuru na naunga mkono hoja mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu pia naomba niipongeze Serikali hasa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri wanayofanya kwa kufanya uratibu mbalimbali na kuhakikisha kwamba shughuli zote za Serikali zinaenda. Kuna maeneo mbalimbali ambapo ningependa kushauri na naamini kabisa ushauri utazingatiwa kama ilivyokuwa siku zote unazingatiwa ili shughuli ya maendeleo iende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilikuwa naomba kwanza suala hili la budget process ya kwetu tuangalie namna Serikali iangalie nasi tuendelee kushauri tubadilishe mfumo wetu wa budget circle kwa sababu mengi tunayozungumza leo tayari ceiling zimeshawekwa na maeneo mengi watu wameshapanga bajeti zao, kufumua na kuiandaa upya inakuwa ni ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa ni vizuri sisi tungekuwa tunajadili mambo mengi, nini kipande nini kishuke, mabadiliko gani yaje yawe yanafanyika kuanzia mwezi wa Nane mpaka mwezi wa kumi na moja ili watu wanapoandaa bajeti zao basi shughuli hizi zote ziweze kuendana na budget circle na kama kuna mabadiliko tuweze kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuwe na mfumo, kwanza tujue kabisa mapato yetu ni shilingi ngapi ili kutokana na yale makusanyo ndiyo tupange matumizi yake. Hapo tukiweza kufanya ninaamini kabisa hili suala la kusema fedha hazijatosha, hazijaenda kule kutokana na hii cash budget itakuwa tatizo hilo tumeondokana nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba niipongeze kwanza Sheria ya Manunuzi tumeifanyia mabadiliko mara kadhaa na inaenda vizuri, tumeona mafanikio makubwa katika sekta kwa kutumia force account katika sekta ya elimu, afya. Hata hivyo, bado hiyo hiyo Sheria ya Manunuzi inatumika vibaya na fedha zote tunazokusanya bado matumizi ni mabaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tukienda kwenye manunuzi ambapo tunaendelea kutoa tender na wale wanaopokea zile tender bado bei zao ziko juu. Kwa mfano, ukienda TEMESA, TEMESA ni chaka moja ambapo mahali manunuzi yale bado ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha nyingi za Serikali zinapotea pale TEMESA, TBA na taasisi nyingi za Serikali ambazo zinatoa huduma, unakuta gharama zao ni kubwa kuliko ya private sector na pesa zetu nyingi zinapotea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kwenye viwanda. Naomba kwamba tuna sera nzuri tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda lakini tusipoangalia kwa undani tukafanya uchambuzi wa kina kwamba gharama za uzalishaji ambazo zinakuwa ni kubwa kuliko bei ya bidhaa ambayo inatoka nje, bado hatutaweza kuwa nchi ya viwanda na utakuta bado tutakuwa tunaagiza vitu kutoka nje. Sehemu kubwa inatokana na utitiri wa masuala ya tozo, ushuru, ada na kodi. Hayo yakifanyiwa kazi nina uhakika kwamba viwanda vyetu vya ndani vinaweza vikafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali haswa kwa upande wa miundombinu; huko Babati Madaraja yameendelea kujengwa. Daraja la Magara, daraja la Mtogiheri na madaraja mengine yamejengwa vijijini ambayo hata barabara za trunk roads hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la barabara ningeomba Serikali iangalie upya suala la mgao wa fedha zile ambazo zinaenda TANROAD na ambazo zinaenda TARURA. Ningeshauri kwamba tuwe fifty fifty kwa sababu TARURA ndiyo ina kilometa nyingi za barabara na hiyo ingefanya barabara za vijijini pia ifanye kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwenye suala la elimu hasa elimu stadi. Katika Bunge lililopita tuliweza kupitisha hapa sheria ambayo ilichukua skills development levy ile asilimia nne tukagawa mbili kwa mbili. Mbili zikaenda kwenye Bodi ya Mikopo kwa dharura kwa muda wa mwaka mmoja, lakini naona kwamba sasa bado imeendelea kubaki huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba ile pesa yote asilimia nne irudi iende sasa kwenye ufundi stadi, VETA kwa sababu VETA yetu pia inataka mabadiliko makubwa. Leo tukitaka uchumi wa viwanda, viwanda vyote siku hizi ni mambo ya ICT na tusipobadilika na mfumo huo kwa kufundisha vijana wetu masuala ya ICT bado wale watakaokuwa wanapata mafunzo pale itakuwa hawajafikia hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la maji. Naomba Serikali ijitahidi kuhakikisha kwamba Wakala wa Maji Vijijini ianzishwe mapema ili miradi ya maji iweze kwenda vizuri. Pia pesa ambayo inatengwa kutokana na ile shilingi hamsini tuliyoweka, basi yote ile iende kwa ajili ya maji vijijini, lakini tunaomba kwenye bajeti hii basi Serikali ifikirie kuongeza shilingi hamsini nyingine iwe mia ili Mfuko wa Maji uweze kutuna wananchi vijijini waweze kupata maji. Niihakikishie Serikali wananchi wote hawatajali kupanda kwa gharama zingine ili wananchi wenzao wa vijijini waendelee kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la upande wa Kilimo. Naiomba Serikali sasa ijitahidi kuhakikisha kwamba Benki ya Kilimo iwezeshwe ule mtaji ambao waliahidi kwamba itawezeshwa ili wakulima waweze kukopa kule na suala la utafiti pia tuwe na fedha za kutosha kuhakikisha kwamba tafiti mbalimbali zinaendelea kufanyika, kile chombo ambacho tumeanzisha Tanzania Agricultural Research Institute iweze kuanza kazi yake mara moja na fedha zake ziweze kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni muhimu sana leo hii fedha za OC zinaenda vizuri ambazo zinajumuisha mishahara na gharama zingine za kawaida, lakini fedha za maendeleo zinaenda kutokana na pesa inavyopatikana. Ningeomba kwamba kama kuna uwezekano tuangalie kama tunaweza kupanga kwa uwiano kwamba fedha asilimia fulani zikienda za OC basi na za maendeleo ziwe zinaenda zinafanana. Nasema hivi kwa sababu kama OC imeenda asilimia 100 na za maendeleo imeenda asilimia 10 wanaenda kusimamia nini kwa sababu ile fedha tunaendelea kupoteza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zote ziendane na kama tunaona kwamba hatuna fedha za kutosha kwa maendeleo kwa miradi yote, basi tuweke vipaumbele mwaka huu itakuwa Wizara kadhaa tunawekeza fedha huko zote halafu OC kwenye hizo Wizara ambazo hazipati fedha za maendeleo tupunguze kabisa zote ziende kwenye suala la maendeleo ili value for money iweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningeomba Serikali huko ndani ya Serikali suala la PPP bado halijaeleweka vizuri. Ningeomba kwanza papatikane elimu ya kutosha na semina mbalimbali kwa Wabunge, lakini pia kwa Watumishi wote ili tukikaa pamoja vizuri naamini kwamba suala hili la PPP inaweza kutusaidia na tukapata mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na mifumo mbalimbali kwa mfano kwenye madini. Kwenye Sekta ya Madini ningependekeza niwapongeze Serikali kwa kazi nzuri iliyofanyika, lakini pia kile kituo cha Arusha ambacho kinatoa mafunzo kwa kufundisha watu wa kuchakata madini kutengeneza jewellery na vito, basi fedha za kutosha ziwekezwe ili tuweze kuzalisha wataalam wa humu ndani nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho, ni kwenye masuala ya maafa. Ningeomba Serikali pia tujipange, maeneo mengi haya maafa yangeweze tukaepukana nayo kwa kupanga. Tukiwa na master plan ambayo hasa Miji yetu na katika maeneo ambayo yanakuwa sasa miji midogo tuwe na master plan ili tuweze kuepuka masuala mbalimbali ya maafa. Pia katika maeneo yote ambapo yanatokea mafuriko tuhakikishe kwamba Serikali tujipange na tujue chanzo cha mafuriko ni nini tuweze kuzuia yale mafuriko ili tusitumie fedha nyingi kwenye masuala ya maafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba Taasisi zote za Serikali kwa mfano Fire, watu wa Traffic wakusanye mapato yao yote kwa njia ya kielektroniki na hiyo itaziba mianya hii ya pesa ambazo zinaendelea kupotea na tukipata fedha nyingi Mfuko wa Serikali ukiwa umetuna vizuri nina uhakika kabisa kwamba fedha za maendeleo pia zitakuwa zinatoka na tunaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la muhimu, tuendelee kuangalia suala hilo la Sheria ya Manunuzi na pia suala hilo la viwanda namna ya kukaa pamoja na kuhakikisha kwamba sera yetu inakaa vizuri, lakini pia gharama zote za uzalishaji wote tuzielewe. Tukiwa tunaelewa kwa pamoja naamini kabisa kwamba bidhaa zote ambazo tunaagiza kutoka nje, hasa za kilimo na bidhaa zingine za mifugo nyama, samaki hizo zote ambazo tunaweza kuzalisha nchini tungewekeza basi huko tuzalishe bidhaa zote, sisi ndio tuwe tunapaleka nje na exports ziwe kubwa kuliko imports hasa kwa vitu ambavyo vinawezekana ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, lakini pia Watendaji wote huko Serikalini wanaweza kujipanga na haya yote ambayo tunashauri wakafanikisha kwamba tuweze kupanga na mambo yakaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo naomba ni suala zima la migogoro ya ardhi, Tume mbalimbali zimeundwa, naomba haswa kwa mfano kule Babati, migogoro ya ardhi kwa hifadhi zile mbili za Tarangire na Manyara, Vijiji vya Hayamango, Gedamar, Gedejabong lakini pia Vilimavitatu migogoro ile na yale mashamba ya Kiru tufike mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya migogoro ile ina miaka zaidi ya 25, hivyo tumalize ili watu waishi kwa amani, wafanye kazi ya maendeleo kwa sababu tayari nishati imefika katika maeneo mengi, barabara zimeboreshwa na wapo tayari kufanya kazi, kitu kinachozuia ni hiyo migogoro michache ambapo tukiweza kuwekeza suala zima ya maendeleo huko tutakuwa tunaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala zima la uratibu pia katika ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, suala zima la kusaidia watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum kwamba Mfuko ule wa UKIMWI utafutiwe chanzo cha kudumu cha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi siku ya leo kuchangia. Awali ya yote, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kunijalia kufika hapa leo.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wetu kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya pamoja na watendaji wake wote. Muhimu ni kuelewa dhana nzima na mahali ambapo wanataka nchi yetu ielekee. Mimi nashukuru kwa hii dhana nzima ya kuwa na Sera ya Viwanda ambapo naamini kabisa tukienda vizuri na wote tukachangia vizuri na kila mmoja akaweka mawazo yake pale na tukaangalia changamoto zilizopo na namna ya kukabiliana nazo, mafanikio yapo na uchumi wetu utaendelea kukua.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi uchumi wetu ni mzuri na unaendelea kukua, kuna changamoto ndogo ndogo ambazo naamini Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya Mheshimiwa Mwijage na Naibu Waziri pamoja na timu nzima ikiongozwa na Katibu Mkuu na wote wanafanya kazi nzuri na kubwa. Changamoto bado zipo na tunahitaji kuwapa msaada, kuwapa mawazo mbadala na maeneo ambayo wanafanya vizuri tuwapongeze lakini maeneo ambayo wanatakiwa kuyafanyia kazi wafanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo la muhimu ni kuangalia namna ya kuunganisha Serikali yaani coordination bado haipo. Waziri unafanya kazi peke yako na kila Wizara inajitegemea. Mngefanya kazi kwa kuunganisha Wizara zote ili tupate mafanikio makubwa. Tanzania bado easy of doing business haipo. Bado kuna ukiritimba mkubwa na ukiangalia kila mmoja anajitahidi kuhakikisha kwamba anafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, muhimu ni kuangalia namna ya kulinda viwanda vya ndani. Namna ya kulinda viwanda vya ndani ni lazima muwekeze kufanya utafiti wa uhakika kuhakikisha kwamba bei ya uzalishaji wa viwanda vyetu vya ndani inakuwa ndogo ili isishindane na bidhaa zinazotoka nje, hilo ndilo jambo kubwa kuliko yote. Leo hii wote wanaowekeza kwenye viwanda gharama yao ikiwa ni kubwa kuliko zile bidhaa zinazotoka nje watashindwa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu binafsi tukifanya utafiti tunakuta bado tuna changamoto kwenye regulatory bodies zetu. Tunaendelea kushauri mziunganishe, ziwe moja na watu wasiwe analipa kwenye hizi regulatory bodies, ingekuwa ukishalipa kwenye leseni ya biashara basi huko huko kila kitu kiwe kimelipiwa ili tusipate usumbufu. Wanapokuja kukagua wakague wakati wowote lakini wasisumbuliwe kwa maana kwamba kila mmoja anataka alipwe tozo yake.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine muhimu ni kuwekeza kwenye utafiti. Kwa sababu bila kufanya utafiti wa uhakika, kwenye TIRDO, SIDO na COSTECH ipatiwe fedha bado suala hili la namna ya sisi kuendelea itakuwa ni ngumu. Kwa mfano, ukiangalia viwanda vya ndani bei ya kuzalisha sukari, mafuta lakini pia bidhaa zote zinazoweza kuzalishwa ndani ya nchi, leo tuangalie kwenye pamba (Cotton to Clothing) ni ngumu. Kamati yetu ilitembelea kule MWATEX na viwanda vingine, bado unakuta gharama zao ni kubwa sana ukilinganisha na bidhaa inayotoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa usiangalie tu pale kwenye kiwanda anaajiri watu wangapi na analipa nini, angalia spillover effect kwamba kuanzia mkulima mpaka hapo inapofika kwenye kiwanda na bado ile nguo itakayozalishwa wale washonaji na wengine ni kiasi gani itaweza kuzalisha. Bei ya bidhaa inayotoka nje Serikali ilituahidi kwamba nchi ambazo tunaagiza kutoka kwao kwa wingi mtaangalia bei zao, wengi wana-under declare. Wakisha-under declare kwa mfano kwenye hii Cotton to Clothing mtu wa ndani hawezi kushindana na huyu wa nje.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri tukapata uhakika wa bei ya uzalishaji na ni vizuri mkakaa na wafanyabiashara wakawaeleza bei ya uzalishaji wa viwanda vya ndani. Sehemu nyingine, kwa mfano, kwenye pombe kali, ni mahali ambapo Serikali inapoteza pesa nyingi sana kwa sababu gharama yake ya uzalishaji haijulikani. Wengine wanauza kwa bei ya kodi tu, sasa ile pombe anauzaje? Ina maana kuna mahali ambapo tunapoteza mapato mengi ni vizuri kuangalia. Pia tukiangalia viwanda vyetu kwa mfano vya mbolea, yeye kwa upande wa kodi anatozwa kodi zote hawezi ku-claim kwa sababu end product yake bado haina VAT lakini ile inayotoka nje haitozwi, unakuta gharama yake ya uzalishaji inakuwa kubwa hawezi kushindana na ile mbolea ambayo imetoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni viwanda na biashara mngeangalia pia kwa nini informal sector inazidi kukua? Leo hii asilimia 80 ya watu wako kwenye informal sector (sekta isiyokuwa rasmi), ni kutokana na hizi tozo, kodi na ushuru mbalimbali ambapo mtu anaona ni kero anaona ni bora aendelee kuwa informal na maisha yanaenda. Kama tuki-formalize na tukiangalia namna ya kwenda haraka Serikali itapata mapato mengi zaidi kwa sababu tax base yetu tukiitanua nina uhakika kabisa kwamba unaweza ukapunguza hizo kodi nyingine ili wengi walipe kodi ziteremke na compliance itakuwa ni kubwa. Kwa hiyo, hilo ni jambo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama mngekuwa mnafanya kazi na viwanda vingine, niwape mfano, Manyara tuna Kiwanda cha Kuchambua Pamba, ambapo kwenye sekta nzima ya kilimo wanatumia umeme kwa muda mdogo, ni viwanda kabisa vikubwa vinatumia kwa muda wa mwezi au miezi miwili halafu wanafunga mpaka msimu ujao. Unakuta wanalipishwa capacity charges ya miezi mitatu asilimia 70 ya ile gharama, cost of production lazima iwe juu. Kwa mwendo huo viwanda vingi vitaendelea kufungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukija kwenye maziwa na viwanda karibu vyote msipoangalia, msipokaa na Wizara nyingine ambazo zote ziko kwenye sekta hiyo ya viwanda, kuanzia production mpaka wakati wa kuuza, bado hamtakuwa mmevilinda viwanda vya ndani. Ni muhimu kuangalia namna ya kupata cost of production, faida na kodi. Ni muhimu Serikali iendelee kupata kodi yake sahihi maana isipopata kodi yake sahihi hizi ndoto zetu za kuwekeza kwenye huduma nyingine hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, pia tuangalie viwanda ambavyo vitalenga wakulima, wafugaji, wavuvi, vitu wanavyozalisha vinawezekana kupatikana ndani ya nchi. Kwa nini tunaendelea kuagiza vitu vyote kutoka nje? Bahati nzuri Mheshimiwa Rais pia amelizungumzia mara nyingi, tunaomba sasa muendelee kushirikiana kama Serikali moja, kuwe na uratibu baina ya Wizara zote ili ndoto yetu iweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna jambo lingine ambalo ni muhimu tujue kwamba viwanda haviwezi kujitegemea bila kujua raw material yatakuwa yanatoka wapi. Kwa nchi yetu raw material kwa sehemu kubwa ni sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Tukiwekeza kwenye hizo sehemu tatu na mkaweka mkakati kwamba mwaka huu tunafanya kwenye product mbili au tatu, tukawekeza value chain nzima, yaani mnyororo wa thamani kutokea kwenye uzalishaji, viwandani mpaka kwenye kuuza, nina uhakika kabisa kwamba ndani ya miaka miwili, mitatu, tutaona mabadiliko makubwa.

Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa nchi yetu kuagiza bidhaa ambazo tungeweza kuzalisha ndani ya nchi hii. Mifano ipo mingi, kwanza tuangalie kwenye matunda na mbogamboga, samaki, vitu vyote hivi tunaweza kuzalisha ndani ya nchi. Ni vizuri kama Serikali kwa pamoja tuwekeze kwa ajili ya upatikanaji wa bidhaa hizo. Juice zote tunazokunywa hakuna hata tone moja linalozalishwa hapa nchini zote ni concentrates kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, hata kwenye biashara, kwa mfano kwenye pombe kali, bei ya kodi baina ya pombe inayozalishwa ndani ya nchi na nje ya nchi ni ndogo, hivyo hivyo kwenye juice. Sasa tuangalie, inayozalishwa ndani ya nchi ama tufute kabisa au ipungue kabisa lakini ile inayotoka nje tuipandishe ili watu wawe na incentive ya kuwekeza hapa nchini, waone kwamba ni bora kuwekeza hapa nchini kuliko kuagiza kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, nchi nyingine bado zina mamlaka ya kusamehe kodi kwenye bidhaa zao za export lakini sisi hatuna. Kama Kenya au Zambia wanazalisha wao wanapewa kuingiza nchini bila kodi unakuta bidhaa zao ndio ziko kwenye soko letu badala ya sisi bidhaa zetu kuingia sokoni, kwa sababu sisi hatuna msahama wa aina yoyote. Nchi za SADC tayari tuna ile SADC Protocol ambapo bidhaa zao zinapouzwa kwenye nchi hizi kodi yake ni ndogo, kwa hiyo, ushindani unakuwa mdogo.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri kama Serikali muangalie mambo haya na Wizara hii ya Viwanda na Biashara ndiyo mnatakiwa kufanya utafiti wa uhakika, mshauri Wizara nyingine zote kwa pamoja mfanye nini. Pia tuhakikishe kuna miundombinu muhimu kama barabara na umeme kwa wale wanaohitaji kuwekeza kwenye viwanda. Vilevile tuwaondolee changamoto nyingine, kwa mfano, watu wanaanzisha viwanda halafu unasema barabara hii mwisho tani kumi hatuwezi kufika. Ni muhimu Wizara hii iendelee kushauriana na wengine.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo, lakini pia niendelee kushukuru kwamba nimepata fursa ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la kwanza na kila mwaka naendelea kushauri hivyo; tubadilisheni mfumo wa bajeti yetu, badala ya kupanga matumizi kwanza, tukusanye kwanza halafu ndiyo tupange matumizi, ndiyo tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ndani ya Bunge tubadilishe mfumo wa Budget Cycle yetu. Badala ya kipindi hiki ambacho tunakuja kukaa, hakuna tunachoweza kubadilisha, tungekuwa tunakaa kwanza tunakubaliana kwamba haya yapitishwe, haya yapande, halafu ndiyo tukija huku inakuwa ni kupitisha tu, mambo yote tunakuwa tumewekana sawa. Hapo ndiyo tutakuwa na mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba mwaka huu hawakupandisha kodi katika maeneo mengi, isipokuwa zile ambazo zinatoka nje ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani. Kwenye excise duty hawajapandisha kabisa, lakini lengo ni kuhakikisha kwamba tunakusanya mapato zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri kwamba wangewekeza zaidi kwenye maeneo ambapo watapata mapato yasiyo ya kikodi, hapo ndiyo uchumi wetu utakua. Fedha hizo tungewekeza kwenye maeneo ya miradi ambayo returns zake ziwe zinakuja kwa haraka, tutapata mapato. Hata kwenye ukusanyaji wa kodi, tusiwe tunapandisha viwango vya kodi au tozo badala yake tutanue wigo, watu wengi zaidi walipe kodi. Kila Mtanzania akilipa kodi, nina uhakika tutakusanya kodi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote naendelea kushauri hapa kwamba sekta isiyokuwa rasmi inaendelea kukua.

Zamani ilikuwa asilimia 50, sasa hivi iko asilimia 70. Iko siku tutafika asilimia 100 kutokana na ada, tozo, kodi, ushuru; yaani ni utitiri umejaa. Tumeambiwa wanaleta blue print, lini wataileta? Lini itafanya kazi? Ukiondoa kitu kimoja kwa mwaka mmoja, hujasaidia viwanda vya ndani, wala hujasaidia uzalishaji wa ndani. Kazi ya kwanza ilitakiwa hizi kodi, ada na tozo mbalimbali wangezifanyia kazi wangeona uchumi wetu unakua na uzalishaji wa ndani (local production) ungekua haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyetu havikui, uzalishaji wetu hata huko kwingine haukui kutokana na hizi tozo, kodi, ada na ushuru mbalimbali, ni kubwa sana. Hiyo yote haihusiani na Wizara ya Fedha tu, Wizara zote kila moja ambayo inahusika ilitakiwa wakae pamoja waziondoe. Hii blue print bado wanachelewa sana kuileta, tusitegemee tutakuwa na maajabu kwenye viwanda. Viwanda vyetu haviwezi kukua hata siku moja haya yasipobadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kabla ya hizo Kanuni zote ambazo Mawaziri wamepewa mamlaka, ikiwezekana Bunge tubadilishe sheria au sijui nimefikiri vibaya, ila ilitakiwa Kanuni zije hapa kabla hazijaruhusiwa kwenda kuwa printed kwenye Government Gazette ili kabla Waziri yeyote hajapandisha tozo yoyote, sisi Wabunge tuwe tunajua kwamba hii sasa inaenda kupitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hapa wamekaa kimya wote kwa sababu hata bajeti hii ikiwa ndogo, kwenye tozo kule kwenye Kanuni anaenda kupandisha anavyotaka. Hiyo ndiyo inafanya ukuaji wa uchumi wetu udumae kabisa; badala ya kwenda positive inarudi inakuwa negative. Kwa hiyo, naomba hizo Kanuni sisi kama Wabunge wote tuziangalie upya, kabla ya kufika kwenye Finance Bill, kama kuna marekebisho tufanye hayo marekebisho kwa sababu tutaendelea kumlaumu Waziri wa Fedha, nyingine haziko kwake, ziko kwa Mawaziri wengine wote na kila mmoja anang’ang’ania tozo zake au ada zake asiziteremshe. Kila akiamka kila akipenda anapandisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hiyo ndiyo itafanya uchumi wetu ukue kama hizo kanuni zote zitakuwa zinapitia Bungeni. Ninavyojua, sheria inasema jambo lolote ambalo inahusu kupandisha kodi yoyote au tozo yoyote, lazima lipitie Bungeni. Sasa sijui lini imebadilika? Sasa naomba hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwamba wamekuwa na tax amnesty. Nampongeza sana kwa hilo, watu wengi wataenda kulipa. Ila naomba tunge-extend isiwe tu kwenye tax administration kwa upande wa kodi ambazo wanakusanya kama TRA, wangeweka kwa upana wote, yaani kwenye Regulatory Boards zote, watu wanadaiwa vitu vya ajabu ajabu. Watu wanaamka kule wanadai vitu vya miaka 10 nyuma. Wangeweka kwamba zote wangezisamehe kwa muda wa miezi sita tuanze moja. Nina uhakika tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, hapa tulikubaliana kwamba Local Government Development Grant ambayo Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wote ndiyo tunaitegemea huko kwenye Halmashauri zetu. Tumekubaliana hapa watatoa fedha za Elimu na Afya kutokana na ile miradi tuliyopanga; lakini nimepitia Volume IV, sioni mahali imetajwa kabisa Local Government Development Grant.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya reallocation mwezi wa Saba, Nane na wa Tisa hizi pesa hazitakuja, tutaumia. Lazima wote tukubaliane kwamba hapa ifanywe reallocation na tuone kwenye hii bajeti kwamba Local Government Development Grant iwepo na hizo fedha ziendelee kuja. Hizo ndiyo zinatusaidia huko kwenye kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, kujenga na shule. Tusipofanya hivyo, tutaumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauripia kwenye utafiti, tufanye reallocation tuhakikishe kwamba kunakuwa na pesa kwenye utafiti. Hatuna! Pesa kwenye utafiti tunategemea wafadhili wa nje, tunaweka pesa kidogo sana. Mtu wa nje akikuletea pesa, anapeleka mahali ambapo naye ana maslahi yake, hapeleki mahali ambapo sisi tunapahitaji. Kwa hiyo, kwenye utafiti tuwekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunashukuru wameondoa kodi kwenye taulo za akinamama, animal feeds na kwenye maziwa, lakini wameondoa VAT, yule mtu hawezi kudai import taxes. Naomba tukifika kwenye Finance Bill waje na measures kwamba tunafanyaje ili viwanda vya ndani viweze kupona bila wao kukusanya import taxes au kupata refund, itakuwa importers wanapata faida badala ya wazalishaji wa ndani. Hapa tutakuwa hatujasaidia wazalishaji wa ndani, tutakuwa tumewasaidia wale ambao wana-import ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze kwamba wameweza kupunguza income tax kwa viwanda vipya kwa Sekta ya Ngozi na Sekta ya Madawa. Naomba hata vile vya zamani wangewaruhusu wapate 20 percent. Siyo kwenye hiyo tu, viwanda vyote vipya, sekta zote wangewapa tu hiyo tax incentive ya 20 percent kwa sababu ni ndogo, hakuna kiwanda ndani ya miaka mitano kitakuwa na faida kubwa. Kwa hiyo, hawatapoteza sehemu kubwa. Kwa hiyo, kama ni ndogo, itakuwa ni moja katika maeneo ambayo watapata tax incentive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ETS. Namwomba Mheshimiwa Waziri, ndani ya hizi siku chache apate takwimu sahihi ya idadi ya chupa au idadi ya units ambazo tunazalisha nchini, halafu apige hesabu na hizo bei ambazo tulipewa kama bei elekezi ambayo wanategemea kupiga hizo stamp. Ni bora wangepandisha asilimia tano kwenye ushuru kutokana na inflation kuliko kwa hizo bei ambazo tumepewa. Lengo hapa ni kuhakikisha kwamba wale wote ambao hawaoneshi records zao vizuri au wana- under declare tuweze kuwapata. Ila lengo siyo kwamba hao tuwakomeshe na kupandisha gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la ETS tumeifanyia kazi vizuri, naye ana uwezo wa kupata units ngapi tunazalisha kwa mwezi na kwa mwaka halafu kutokana na hiyo, sisi tulivyopiga hesabu, stamp haitakiwi kuzidi shilingi moja au shilingi mbili. Kwa hesabu zetu, tunazalisha zaidi ya units bilioni tano kwa mwezi. Ukipiga kwa miezi 12 ni bilioni 60 mara shilingi mbili ni 120 billion, inatosha hiyo kurudisha uwekezaji wake pamoja na kupata faida. Kwa hiyo, kwenye stamp hii kwenda shilingi kumi na tatu, ni bora angepandisha asilimia tano kwenye inflation kuliko hizo rates. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye pombe kali. Bado huko kuna udanganyifu mkubwa unafanyika kwenye suala la uzalishaji na ndiyo maana kuna watu wanaweza kuuza bei ya chini kuliko gharama za uzalishaji kwa sababu kuna upotoshaji. Hapo sisi tunaamini kuna zaidi ya shilingi bilioni 400 au 500 zinazopotea. Ni eneo ambalo nashauri walifanyie kazi na wataweza kupata kodi nyingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naendelea kusisitiza Sh.50/= kwa kila lita ya mafuta yanayoingia nchini, hiyo ndiyo itakuwa ukombozi wetu. Naomba Waheshimiwa Wabunge wote safari hii tuifanyie marekebisho sheria na tuombe hiyo Sh.50/=, ndiyo mahali ambapo tumeona kuna mafanikio kwa ile Sh.50/= tuliyoiweka mara ya kwanza na REA imefanikiwa kutokana na hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na team yake nzima ya wataalam inayoongozwa na Katibu Mkuu mzoefu Dkt. Meru. Nawapongeza kwa kutuletea Mpango mzima na mzuri wa mwaka huu 2016/2017. Hotuba yako imefafanua vizuri kwa muhtasari kabisa mwelekeo wenu kwa bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze Serikali yetu kwa kuona umuhimu wa kuwa na uchumi wa viwanda. Mimi binafsi naona ni hatua kubwa sana na mwelekeo ni mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri masuala machache ili yafanyiwe kazi katika kuboresha dhana nzima ya uchumi wa viwanda. Tanzania suala la viwanda linawezekana sana. Tuna rasilimali nyingi na fursa ya malighafi za aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni muhimu, Wizara ya Viwanda, Biashara iwe ndiyo Wizara inayoratibu masuala yote ya biashara na uwezeshaji. Iwe ndiyo kiunganishi (coordinator) baina ya Wizara zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi na tozo zinazotozwa na Serikali na taasisi za udhibiti (Regulatory Bodies) pamoja na Serikali za Mtaa. Nyingi hujirudia na shughuli za taasisi za udhibiti hujirudia. Tunashauri nyingi ziondolewe au kupunguzwa na pawe na One Stop Center wakati wa malipo na wakati wa ukaguzi wote kama team moja ya Serikali na siyo kila taasisi kwa wakati wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Regulatory Bodies zisitoze na badala yake Serikali itoe bajeti za kuziendesha na itoze kwa wafanyabiashara sehemu moja na kugawa kwa taasisi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nashauri pia tuwe na mfuko maalum wa kupata fedha za utafiti. Fedha za utafiti kila mwaka ni ndogo sana. Bila utafiti katika sekta zote hatutasonga mbele. Nashauri kwa kuanzia tutoze shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta kwenda kwenye mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wa ndani wapo na wanahitaji msaada wa utafiti ili waweze kuwekeza katika viwanda vidogo na kati. Mitaji kwao siyo shida bali ushauri wa kitaalam na msaada wa kufuata sheria na kanuni ili waweze kuwekeza. Wizara ya Viwanda na Biashara inaweza kusaidia kufanya kazi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni katika eneo la uwekezaji wa kimkakati (strategic flagship investments) ya 2015 - 2020. Nashauri suala la Kiwanda cha Mbolea inayoendana na gesi asilia (Urea plant) ili tuweze kuzalisha aina zote za mbolea hapa nchini badala ya kuagiza urea ambayo ni moja kati ya msingi (foundation compound) ya mbolea zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali iangalie namna ya kukuza Sekta ya Biashara ya Mbegu ndani ya nchi. Tulikuwa tumefikia katika hatua nzuri sana kabla ya miaka ya 2004. Baada ya sera kubadilika na kutotoa fedha za kutosha katika taasisi zetu za utafiti na kuondoa kodi na tozo zote katika uagizaji wa mbegu za nje na kuendelea na kutoza uzalishaji wa ndani kwa aina zaidi ya kodi na tozo 26, sekta hii ilidorola na wazalishaji wengi wa nje walihamia nchi zinazopakana na sisi kuzalisha mbegu huko na kuleta nchini bila kodi na tozo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii pia ni kwa Sekta ya Madawa ya mimea na mifugo ambapo uzalishaji wa ndani hutozwa kodi na tozo nyingi lakini bidhaa hiyo hiyo kutoka nje haina kodi wala tozo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Wizara iangalie namna ya kuwa na Ofisi za BRELA kimkoa, tuanze na ofisi katika Kanda. Leo hii ingawa ipo online lakini bado ni lazima ufike ofisi za Dar es Salaam kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishauri Serikali iangalie namna ya kuboresha huduma katika viwanja vya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Songwe. Leo hii mazao ya Sekta ya Mboga Mboga (horticulture) ya Kanda ya Kaskazini yote hupitia Kenya (Nairobi) badala ya KIA. Je, utafiti umefanywa kuwa tatizo ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninashauri kama sababu ni biashara, tuangalie namna ya kuunganisha bodi zote za mazao kuwa moja na kila zao liwe na idara katika bodi hiyo. Hii itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa bodi hizo na pia wataalam waliobobea katika biashara ndio waongoze bodi na siyo uwakilishi wa kisiasa na uwakilishi sababu tu ya uwakilishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba bodi hiyo moja iangalie namna ya kusaidia sekta husika bila kuwatoza. Gharama za kuendesha itokane na uwekezaji na faida itakayotokana na biashara ya kuhudumia sekta hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali iangalie namna ya kuondoa kodi kwenye vifaa na mitambo ya ujenzi na kuchimba maji zinapoagizwa (import duty and VAT on earth moving equipment and drilling equipment) na itoze kwenye shughui za kazi na siyo kwenye uagizaji. Hii itafanya ziwe nyingi nchini na zikiwa nyingi ushindani utakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri ili kulinda viwanda vya ndani, tutoe kodi ya VAT kwenye mafuta yanayozalishwa ndani ya nchi na tutoze mafuta ya kupikia yanayoagizwa kutoka nje. Pia tutoze tozo maalum kwenye concentrates za juice zinazotoka nje na tozo hiyo itumike kuboresha kwa kuagiza miche ya matunda tuzalishe ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutoze dumping charge kwenye chuma. Leo hii viwanda vyetu vitafungwa kutokana na mzalishaji mkubwa duniani kuleta chuma kwa bei nafuu. Wanafanya dumping kumwaga kwa bei ya chini ya gharama za uzalishaji wa viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie upya sera ya kulinda viwanda vya ndani badala ya kuangalia upatikanaji wa kodi inayotokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Wizara ya Viwanda na Biashara ibadilike na wataalam wake badala ya kuwa wakusanyaji wa kodi na tozo tu, wawe washauri wa wafanyabiashara na wanaotarajia kuwekeza; wawe washauri katika kila sekta kwa kufanya utafiti na kushauri jinsi ya kuboresha sekta hiyo; jinsi ya kupunguza gharama, kupata mitaji, kupata teknolojia mpya na masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, coordination and advice hii iwe katika kila ngazi kuanzia Wilaya, Mkoa na Taifa. Wafanye utafiti katika gharama mbalimbali na tozo na kuishauri Serikali namna ya kuboresha biashara ya ndani na nje ya nchi.
na elimu ya kodi. Wizara pia inaweza kusaidia kutoa elimu hiyo. Muhimu hapa ni mindset change kuwa na mabadiliko katika fikra.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itumie Sheria ya PPP (Public Private Partnership) kufanikisha maendeleo ya biashara nchini na kuboresha mfumo ili uwekezaji ufanyike kwa tija. Naamini Waziri na team yake nzuri ya wataalam wanaweza na wataongoza mabadiliko ya kuelekea katika uchumi wa viwanda. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kufanya kazi kubwa na kuleta mabadiliko makubwa katika sekta hii ya madini. Pia kwa kuona Wizara hii inastahili kuwa peke yake na Wizara ya Nishati kuwa peke yake ambapo kwa Wizara zote mbili tutapata manufaa makubwa na ufanisi mkubwa wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Waziri, Naibu Mawaziri wote wawili pamoja na timu yao nzima kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya kuhakikisha kwamba sekta hii sasa inasimama vizuri na nchi yetu iweze kunufaika na rasilimali hii ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia. Naweza kusema kwamba kila aina ya madini yaliyopo duniani na Tanzania yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la kwanza na siku zote huwa nasema hapa, kwenye bajeti hii nimeona pale mmeandika kwamba Oktoba mtaanza mafunzo katika Kituo cha TGC pale Arusha, kituo ambacho kitakuwa kinafundisha Watanzania jinsi ya kuchonga vito lakini pia na kupata mafunzo mbalimbali ya madini yaani vito pamoja na usonara lakini vifaa vinavyotakiwa pale bado havijatosheleza. Badala ya mashine 45 ambazo wanazo mngeongeza mashine zifike 100 na gharama yake siyo kubwa sana. Hii programu ya Diploma ni ya miaka mitatu (3) lakini bado mnaweza kuwa na certificate ambapo inafanyika International College Gemstones - Marekani, Bangkok na maeneo mengine ni miezi sita. Mtanzania ambaye hajui kusoma na kuandika kwa sababu kuchonga vito ni art yaani ile ni sanaa, kwa hiyo, mngeweze kufundisha watu 100 kwa kila miezi sita kwa muda wa miaka miwili (2) mtakuwa na watu 400 na hata mkipata asilimia 20 tu ambao watakuwa wazuri pale tayari madini mengi ya Tanzania tutaweza kusanifu hapa nchini na tutaweza kuongeza thamani na pia ajira itaongezeka kwa wingi sana. Kwa sababu tuna madini kwenye vito aina ya precious na semi-precious, zote hizo zitapata thamani na biashara hiyo itakuwa nzuri. Kwa hiyo, tunaomba kwenye bajeti hii mhakikishe kwamba mmeweka fedha ya kutosha ya kuwezesha kituo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, siku za nyuma tulishafanya mabadiliko kwenye hizi leseni kubwa za Prospecting License (PL) ilikuwa unaruhusiwa kuwa na leseni nyingine za madini ya ujenzi lakini imefika mahali ukienda unanyimwa kuchukua leseni hizo za madini, kwa mfano, ya mawe kwa ajili ya moram au kwa ajili ya mchanga. Mtu akishachukua square kilometer 100, 200, 300 huko ndani nyie wengine wote sasa mnafanya kazi kienyeji, hamruhusiwi kupata hizo leseni. Nina uhakika kwamba hapa Bungeni tulipitisha sheria, tunashindwa kuamini kwa nini hiyo sheria haitekelezwi na huko chini kwa mfano kwenye Ofisi za Kanda wanashindwa kutupa leseni hizo za madini ya ujenzi ili watu katika Halmashauri zetu na maeneo mbalimbali waweze kuwa na fursa na haki ya kutumia hayo madini bila kubughudhiwa na huyo mwenye leseni kubwa ya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama alivyozungumza mwenzangu ni vizuri pia tukayaangalia haya madini aina ya chumvi, kwa sababu huyu mwenye leseni ya madini ya chumvi anatozwa sawa kabisa na yule wa dhahabu au wa madini mengine ambayo yana thamani kubwa. Kilo ya chumvi na kilo ya dhahabu ni vitu viwili tofauti, sasa kwa nini leseni zao zifanane? Kwa hiyo, mngeangalia hii leseni ya chumvi mngewaondolea kabisa au mngeweka ada ndogo tu ili chumvi yetu ambayo tunazalisha Tanzania iweze kuzalishwa kwa wingi na tushindane kwenye soko la Afrika Mashariki na Kati. Kwa hiyo, hilo naamini kabisa Wizara mtalichukulia maanani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, naomba Wizara pamoja na Wizara ya Fedha zifanye kazi kama Serikali kwa kusaidiana . Leo hii Arusha au Tanzania tungekuwa center of gemstones kwa Afrika. Jambo hili limeshindikana kwa sababu ya mifumo yetu ya kikodi kwa sababu mtu akitoka na madini katika nchi hizi ambazo zinatuzunguka kuja kuuza Tanzania anabanwa sana mipakani au kwenye viwanja vya ndege na anashindwa kuingiza mzigo wake. Vilevile kama akiingiza na hajaweza kuuza siku akitaka kuondoka na mzigo bado inakuwa ni kero na tatizo pale mipakani kutokana na mifumo yetu ya kikodi. Sasa ni vizuri tungeangalia mfumo huo ili watu wote wawe na urahisi wa kuingiza madini yao na wakitaka kuondoka na madini ambayo hawajauza waweze kuondoka nayo kiurahisi ili center ile ya Afrika ambapo ilikuwa ni Arusha wanafanya show kila mwaka iweze kukua na Tanzania iwe kama Bangkok na Brussels ili nasi kwa Afrika ndiyo tuwe kituo kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie kwenye mfumo wa kodi. Leo hii tunalalamika kwa nini tanzanite au madini yetu ni mengi lakini yanauzwa kwa bei nafuu nje ya nchi. Leo hii ukitaka kuuza tanzanite nje ya nchi, uki-export officially, kihalali kabisa unalipa asilimia 5 tu ya royalty. Ukipeleka tu Kenya hapo asilimia 5 halafu ukitaka kuuza hiyo tanzanite iliyochongwa hapa nchini unatozwa asilimia 18 ya VAT, ina maana tanzanite itakuwa rahisi Kenya badala ya hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo kwenye dhahabu, bei ya dhahabu sisi hatupangi inapangwa kwenye World Market Stock Exchange, metals zote. Unakuta dhahabu yetu ukitaka kuuza hapa ni plus 18 percent locally, 18 percent kwenye VAT una-calculate pamoja na faida na gharama zote, ukipiga hesabu ni zaidi ya asilimia 25 mpaka 30. Sasa unakuta bei ya dhahabu hapa nchini locally itakuwa bei ya soko la dunia plus 25 percent. Ukienda Dubai ni asilimia 5 tu juu ya ile bei ya soko la dunia, ina maana watu wengi kwa sababu dhahabu hainunuliwi na watu wa kawaida, ni middle na upper class. Kwa hiyo, mtu anayenunua vitu vya Sh.10,000,000 ukiongeza asilimia 25 ni Sh.12,500,000, hiyo
Sh.2,500,000 inatosha kununua tiketi ya ndege kwenda Dubai, kulala five star, kufanya shopping na kurudi na unakuwa hujaingia gharama, ndiyo maana hapa biashara hiyo haikui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya dhahabu Tanzania inayochimbwa na wachimbaji wadogo ni kubwa kuliko ile ya migodi mikubwa. Sasa mgeweka tu royalty kama Dubai ilivyoweka asilimia 5, siyo lazima iwe asilimia 5, mnaweza kuweka asilimia 7/8 ili biashara ifanane. Ungekuta biashara halali ingefanyika hapa nchini na watu wengi sana wangekuwa wananunua na Serikali ingepata mapato ya kutosha na huu usonara na nini ungeweza kukua kwa sehemu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi pia tumebadilisha ile sheria kwamba haturuhusiwi kuuza madini ambayo hayajawa processed. Naomba Wizara itoe definition ya uhakika kabisa ya maana ya raw mineral kwa sababu raw mineral haijulikani, ina maana itafika mahali tutashindwa kutuma nje ya nchi madini ya aina yoyote au metal yoyote ambayo haijawa processed. Sasa ile definition mngeiweka vizuri kwa sababu hata kwenye dhahabu ya kawaida kama ni carat 24 ni ngumu, unakuta inakuwa na madini mengine ambayo yapo kidogo humo ndani. Sasa utakuta hiyo ni raw tutaanza kuingia kwenye mgogoro mwingine. Ni vizuri definition zote zikakaa vizuri ili suala hili sasa liweze kusaidia nchi yetu. Muhimu ni kwamba Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Wizara ya Madini zikae kwa pamoja waangalie Tanzania inawezaje kuwa center ya Afrika kwenye suala hili la vito na pia kwenye jewellery na madini yote tunayo hapa gold, silver pamoja na fedha yote yanapatikana hapa nchini ili Watanzania waweze kunufaika na nchi iweze kupata kodi na mapato mengine kutokana na madini hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa hawa wachimbaji na wafanyabiashara wadogo zile gharama za leseni na ada wanazotozwa mngeangalia iwe ni fixed rate ili hata kwa mfano sonara anapoambiwa kwamba biashara hiyo wakitaka kufanya ni lazima wakate leseni ya dola 2,000, lazima awe na gemstone dealers license au gold dealers license ndiyo maana watu wanaingia kufanya biashara ya magendo. Mngeweka vitu kwa bei nafuu na isiyo na urasimu kila mtu angekuwa anafanya biashara halali na Serikali ingekuwa inapata mapato kama nchi nyingine zinavyofanya. Nchi ambayo haina hata madini ya aina moja inanufaika kuliko Tanzania ambayo tuna madini ya kila aina lakini niwapongeze Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambapo watu wanaendelea kugundua tatizo kubwa ambalo lipo na wenzangu wamelisemea ni mfano wewe unamiliki eneo lako, kwa mfano, Halmashauri yetu tuna watu ambao wana primary license hatujawahi kuwaona, hatujui wanalipa nini na wanalipia wapi, sisi hatupati hayo mapato na siku wakitaka kuanza kufanya kazi tayari wanaingia mgogoro na wanakijiji. Kwa mfano, Halmashauri ya Babati tulipotaka crusher ya mawe tulinyimwa kutokana na sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu siku ya leo kunipa fursa ya kuchangia hapa.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya Wabunge wote ambao wanatokana na maeneo ya ufugaji lakini pia wafugaji Tanzania nzima kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa maamuzi ya busara na makubwa aliyofanya hivi karibuni. Katika maeneo mbalimbali nchini, ni furaha kubwa sasa watu wamekuwa na matumaini makubwa na tunaamini kabisa kwamba suala hili sasa litafika mwisho na hii migogoro baina ya hifadhi mbalimbali, baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi yote sasa itafika kilele. Tunampongeza Mheshimiwa Rais na tunaomba sasa watendaji wote ambao watafuatilia wafanye kazi kwa umakini ili patokee matokeo mazuri na pande zote ziwe na mafanikio makubwa. (Makofi)

Mhesheshimiwa Spika, naomba pia nikumbushe kuwa haya maeneo mengi ambapo wafugaji wapo watu wengi sasa hivi hata humu ndani baadhi ya Wabunge wamechangia kwamba ni waharibifu wa mazingira, kama sio wafugaji wa asili hizi hifadhi zote zisingekuwepo. Kwa mfanom Kanda ya Kaskazini kama siyo wafugaji wale wametunza hayo mazingira na yamekaa vizuri na wanyamapori, hizo hifadhi zote zisingekuwepo.

Mheshimiwa Spika, tunapongeza na tunajua kabisa sasa katika maeneo ya Ayamango, Gedamag, Gidejebong ambayo tumeyasemea kwa muda mrefu lakini pia kwa maeneo ya WMA ya Burunge katika Wilaya ya Babati, changamoto zote hizi sasa zitapata ufumbuzi. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Ulega, kwa kufika pale, alitolea ufafanuzi mzuri na kila upande ulifurahi na sasa wanasubiri utekelezaji lakini naamini kwamba na wengine wote watafuata nyayo za Mheshimiwa Ulega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikijikita kwa upande wa kilimo, nipongeze Kamati zote kwa kazi na ripoti nzuri na nikiwa mmojawapo katika Kamati ya Kilimo. Nimpongeze Waziri wa Kilimo na Naibu wake wote wawili, Waziri wa Maliasili na Utalii lakini pia Waziri wa Ardhi kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya, changamoto zitaendelea kuwepo, ni kawaida lakini naona mafanikio ni mengi ziadi kuliko changamoto. Kwa hiyo, tuendelee kushirikiana, tuendelee kufanya kazi ili changamoto zote ziishe.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kubwa kwa upande wa kilimo, ili tuwe na usalama wa chakula ambao tunaimba kila siku, jambo la kwanza kabisa naomba tuwe tunazalisha mbegu zetu. Asilimia 75 ya mbegu zetu zinatoka nje ya nchi hasa mbegu ambayo ni ya chakula chetu kikubwa yaani mahindi lakini pia mbegu za mbogamboga zote asilimia zaidi ya 90 zinatoka nje ya nchi. Nashauri tuiwezeshe ASA ambao ni Wakala wa Mbegu nchini pamoja na mashamba yao waweze kuzalisha mbegu ya msingi (foundation seed) ili tuwe na uhakika wa mbegu ndani ya nchi ambazo zitakuwa zinafanya vizuri badala ya kuagiza mbegu kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tunaagiza bidhaa kutoka nje ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini kwa mfano sukari, mafuta ya kula, mchele, ngano, mbogamboga, matunda, maziwa pia nyama na samaki. Hizi zote tuziwekee muda kwamba ndani ya muda fulani, ndani ya miaka mitatu au mitano itakuwa hatuagizi tena kutoka nje badala yake tutakuwa tunazalisha ndani ya nchi, fursa zipo na tuwekeze katika hayo maeneo ili tuweze kuzalisha vya kutosha lakini pia ziada tuwe tunatuma nje na uwezo huo upo kabisa.

Mheshimiwa Spika, lingine naomba tuwekeze kwenye utafiti hasa katika masuala ya bioteknolojia na vituo hivi 17 vya utafiti hapa nchini. TARI ambayo inafanya kazi kubwa isipowezeshwa, haya mambo ya mbegu lakini pia utafiti mbalimbali wa udongo na mambo mbalimbali, hatutaweza kufikia malengo ambayo tunatarajia. Jambo la muhimu ni kwamba ile bajeti ambayo tumetenga kwenda kule TARI iende. Lengo ilikuwa tutenge asilimia 1 ya bajeti yetu nzima iweze kwenda katika masuala mbalimbali ya utafiti kwa ujumla, siyo kilimo peke yake.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye kilimo, mbali na kuchanganya bajeti zile nyingine ambazo zinaingiliana ambazo ni mtambuka, bajeti ya kilimo peke yake tu kama kilimo iwe ni asilimia 10.

Mheshimiwa Spika, lingine ni uzalishaji wa mbolea, tunaagiza mbolea nyingi sana kutoka nje ya nchi. Tunacho kiwanda kimoja ambacho mbolea yake hatuitumii hapa nchini inavyotakiwa badala yake mbolea nyingi ya Kiwanda cha Minjingu inapelekwa nchi za jirani. Serikali za huko zinanunua kama Bodi ya Mazao Mchanganyiko Kenya ndiyo wananunua tani zaidi ya 20,000. Mheshimiwa Rais alishatolea maelekezo kwamba mbolea hiyo inunuliwe katika maeneo ambayo inafaa itumike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbolea ni sawa na binadamu, unapoumwa ndiyo unaenda unapimwa, ukipimwa ndiyo unapewa dawa, tusichukulie tu kwamba mbolea ya Minjingu kila mahali itafanya kazi. Mahali mbolea ya Minjingu isipofanya kazi hata hiyo DAP inayotoka nje ya nchi haitafanya kazi kwa sababu haitakiwi hiyo DAP. Kwa hiyo, tuendelee na utafiti na masuala ya kitaalam, kwa hiyo, tutumie viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Spika, tuliambiwa kwamba kuna suala hili la kujenga kiwanda kule Lindi ili tuzalishe urea nchini. Tukiwa na urea na phosphate, NPK itapatikana hapa nchini. Baada ya hapo ni kuchanganya ratio kwamba unahitaji asilimia ngapi ya aina moja ya N, P au K unapata mbolea za aina mbalimbali, hakuna zaidi ya hapo, hiyo ni baseline nyingine zote ni nutrients za ziada ambazo zinatakiwa zinatokana na upimaji wa udongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la maji, nipongeze Wizara inafanya kazi nzuri sana, wamekuwa na mpango mzuri na niwapongeze kwa kupitisha sheria hii mpya juzi ambayo italeta mabadiliko makubwa kwa upande wa maji. Nikirudia kwa upande wa maji vijijini, napongeza na naomba suala hili la uanzishwaji wa RUWASA, uwe wa haraka lakini pia kwenye jambo hilo kanuni zake zitoke mapema.

Mheshimiwa Spika, ombi langu lilikuwa ile shilingi 50 ambayo tulikuwa tunasema iende kwenye Mfuko wa Maji, narudia tena kwamba iende kwenye RUWASA yaani maji vijijini. Ikienda huko ambapo kuna changamoto kubwa huu Mfuko mwingine wa Maji mkubwa utaendelea kupata kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado naendelea kuomba tuongeze na shilingi 50 nyingine ili iwe 100. Hata ukiangalia kwenye mtiririko, fedha nyingi ambazo zimekwenda huko vijijini ndiyo hiyo shilingi 50 ambayo tulitenga kwenda huko na bajeti ya kawaida pesa iliyoenda ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia Serikali iangalie tutakapofika kwenye bajeti iendelee kuondoa kodi na tozo mbalimbali katika kuagiza mitambo ya uchimbaji maji, mitambo ambayo inaweza kutengeneza mabwawa na malambo mbalimbali ili tuwe na uvunaji wa maji. Tukivuna maji katika maeneo mbalimbali kwanza tutaondoa uharibifu unaotokea kwenye miundombinu ya barabara, reli, lakini yale maji yatatumika kwenye kunywa binadamu na mifugo, ufugaji wa samaki na kwa matumizi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema pia watu wa Maliasili, ni muhimu sana tuhakikishe kwamba Mto Ruaha Mkuu unaendelea kutiririka. Njia pekee sisi kwenye umwagiliaji lazima twende na mambo ya kisasa, mambo ya teknolojia mpya, tukitumia teknolojia ile ya zamani ya kumwagilia kwa kujaza ardhi yote ijae maji iwe kama bwawa ndiyo upande mpunga au mazao mengine, tuondokane na huko tutumie drip irrigation.

Mheshimiwa Spika, tukitumia drip irrigation, mahali ambapo una maji ya eka tano kwa kumwaga kwenye shamba zima kwa drip irrigation utamwagia eka 20. Kwa hiyo ukiwa na eka moja ya kawaida utafanya eka tano. Kwa hiyo, tunaweza kutumia maji kidogo lakini kwa kutumia teknolojia tukapata mashamba makubwa mengi zaidi ambapo kutakuwa na ufanisi mkubwa na ule mto ukiendelea kutiririka, Stiegler’s Gorge pia itaweza kufanikiwa kwa sababu lazima tuhakikisha maji yanatembea ili Stiegler’s Gorge iweze kupata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na hiyo, kwa upande wa utalii, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa na naomba hizi ndege ambazo tumenunua sasa ziendelee kufanya kazi na ziweze kutangaza nchi yetu ili kuleta mafanikio. Ombi moja tuangalie charges mbalimbali ambazo zipo katika viwanja vyetu, kwa nini bado gharama zetu za usafirishaji, hasa kwenye mazao ya kilimo, maua zinakuwa juu na badala yake kupelekea kupitia Kenya. Kwa hiyo, Wizara zote zikishirikiana naamini tutapata mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi lingine kwa ujumla kwenye kilimo, mifugo na maji huko kote tuangalie. Blue print ile tuliyoileta hapa Bungeni na Serikali iliahidi itaifanyia kazi bado uzalishaji wetu gharama yetu iko juu sana; regulatory bodies zina-charge gharama nyingi sana na ndiyo maana inafanya biashara zetu zote hazikui, haswa viwanda ambavyo vinachakata mambo mbalimbali ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye utalii bado wamekuwa na changamoto kubwa, wameendelea kupigwa faini za ajabu. Mtu akikutwa na nyama ambayo haina label ambapo sisi tunahamasisha wafugaji wadogo wadogo wafuge kuku, samaki wakiuzwa kwenye zile hotel wanapigwa faini ya shilingi milioni moja, milioni tano, milioni 20, hilo jambo naomba lifike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi tu, halina siku mbili jirani na Jimbo la Babati Vijijini hoteli moja imepigwa faini ya shilingi milioni moja kwa ajili ya kutoa nyama kwenye fridge ili iyayuke (defrost). Wamekata tamaa wanauliza wawe wanaagiza kutoka sokoni au buchani mtalii akija ndiyo tuweze kuwapikia watu? Naomba tusifike huko, naamini Serikali hii itaweza kuleta mabadiliko. Juzi kwenye briefing tuliambiwa kwamba suala hili limesitishwa lakini naweza kuleta ushahidi kwamba bado linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze kwamba sasa tuna Waziri wa Uwekezaji. Naamini Waziri huyu akikaa pamoja na Mawaziri wote wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi tutaweza kufanya kazi kubwa na kuleta mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo, lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri na Wizara yake inavyofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Wizara ya Uwekezaji, lakini pia kuhamisha Kituo cha Uwekezaji (TIC) katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Jambo hili tulikuwa tumelisemea kwa muda mrefu sana kwamba lazima pawe na chombo Serikalini ambacho kitakuwa kinaratibu, kinaunganisha Wizara mbalimbali na ndiyo kinaelekeza ili Serikali iweze kufanya kazi kama Serikali moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote tulikuwa tunasema huko nyuma hakuna uratibu ndani ya Serikali, kila Wizara ilikuwa inajitahidi ifanye mema katika sekta yake, lakini bila kuwa na uratibu na kufanya kazi kwa pamoja, Serikali kama Serikali isingefanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote katika Ofisi ya Waziri Mkuu, tena ni akina mama wote wawili, Mheshimiwa Jenister na Mheshimiwa Kairuki. Ni akina mama ambao wanajiamini na wanaweza kuchukua maamuzi magumu. Pia Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na timu nzima kwa kazi nzuri wanayofanya. Mimi ombi langu ni moja, naomba Waziri wa Uwekezaji ndio awe mratibu mkuu kwa shughuli zote hasa katika biashara inayofanyika hapa nchini katika sekta zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa sababu hili suala tunalozungumza kuhusu urahisi wa kufanya biashara Tanzania, umekuwa mgumu kutokana na kodi, tozo, ada na urasimu mwingi. Hiyo inaweza kuondolewa na Wizara ya Uwekezaji; siyo kwa wawekezaji wa nje tu, lakini pia kwa uwekezaji wa ndani uwe mkubwa au mdogo. Wizara hii inaweza kufanya kazi kubwa.

Mhshimiwa Naibu Spika, nilipitia bajeti yao lakini bado naona bajeti waliyopewa ni ndogo. Nilikuwa naomba kama inawezekana Wizara hii iongezewe bajeti ili wawe na fedha ya kutosha kufanya utafiti lakini pia waweze kufanya kazi ambazo zinaweza kuunganisha Wizara nyingine zote. Ni vizuri sasa Mawaziri wengine kupitia Wizara zao watoe ushirikiano wa karibu sana na Waziri wa Uwekezaji ili mambo yetu yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu kwenye suala hili, ili pawe na urahisi wa kufanya biashara, tunahitaji kuwa na One Stop Center. Sheria inasema, kutokujua sheria siyo kinga. Hivi kila Mtanzania, kama wako milioni 20 wanafanyabiashara, hivi kila mmoja atajua sheria zote? Leo hii tunakwama kwa sababu sekta ambayo ni rasmi inazidi kupungua na sekta isiyokuwa rasmi inazidi kuongezeka kutokana na urasimu na utaratibu ambao ni mbovu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta isiyokuwa rasmi inazidi kukua kutokana na tozo, ada, kodi mbalimbali ambazo zinatokana na taasisi za udhibiti (Regulatory Boardies) charges zao zimekuwa kubwa. Leo hii wote sasa wanashindana kukusanya mapato kwa kupitia fine au tozo mbalimbali ili kuonekana Wizara zao zinakusanya mapato makubwa. Mapato yalitakiwa yatokane na faida inayopatikana na kodi ya hiari watu walipe, hapo ndiyo utaona uchumi umekua na watu wanafanya biashara na wanaridhika kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zile tozo ni kubwa mno. Mheshimiwa Rais juzi alisema kwamba liangaliwe na kama ni sheria ziletwe. Huu ndiyo wakati wa kubadilisha hizo sheria na tozo mbalimbali ili ziendane na viwango. Cost of production ikiwa kubwa hata tukiwekeza; kama sukari yetu au mafuta gharama ya kuzalisha ndani ya nchi ikiwa kubwa, hatuwezi kushindana na ile inayotoka nje. Mtu akitoka nje, akilipa kodi zote hata ukiweka mara mbili, bado ni rahisi kuliko ile ya ndani. Ni vizuri sasa ile blueprint tuifanyie kazi; na siyo kuifanyia kazi kwa kuleta tu Bungeni kwa kuturidhisha sisi, lakini ifanyiwe kazi ili iwe na mafanikio makubwa, ili biashara zetu zikue, viwanda vikue na hali ya ufanyaji wa biashara uwe mzuri hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu ni kuangalia namna ya kupunguza zile tozo na kodi mbalimbali. Sasa tukija kwenye kila sekta, tutaleta hasa kwenye Finance Bill kwamba hivi ni vitu ambavyo vinatakiwa viondolewe au vipunguzwe ili tuweze kuzalisha bidhaa zetu kwa gharama nafuu, bidhaa ambazo tunaweza kuzalisha humu humu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia Wizara ya Uwekezaji, sisi tuna bidhaa kama nne au tano, tungeweka muda kwamba ndani ya miaka mitatu tunataka tuwe tunazalisha nchini na tusiagize kutoka nje, tutakuwa na mafanikio makubwa, moja ni mbegu ambayo kwa asilimia 76 tunaagiza kutoka nje ya nchi ambayo hata usalama wa chakula hakuna; lakini pia mafuta ya kula, sukari, maziwa, nyama, samaki lakini pia mboga mboga na matunda. Ni vitu hivyo tu ambavyo tunaweza kuzalisha hapa nchini, hivyo ni vizuri kwa kupitia Wizara ya Uwekezaji tufanye hiyo kazi na Serikali iwekeze katika hayo maeneo tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali isipowekeza kwenye utafiti, bado hatutafanikiwa kwa sababu bila utafiti hatutakuwa na maendeleo. Ni vizuri tuwekeze kwenye suala la utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia asilimia kubwa ya Watanzania wako kwenye Sekta ya Kilimo, zaidi ya asilimia 75. Vijana wetu wanaosoma, wengi sasa hivi ajira hakuna kutokana na fani walizosomea ajira hizo hakuna. Ni vizuri Serikali sasa ikubali maombi yetu ya muda mrefu kwamba huko nyuma tuliondoa Skill Development Levy, ile 4% tukaipungua 2% kwenda kwenye Loans Board. Naomba asilimia mbili ile ambayo tumeipeleka kwenye Loans Board sasa irudi kwenye Skills Development Levy iende VETA ili tuwekeze kwenye shule zetu hizi za ufundi ili watu wengi waweze kusoma ufundi kwa kuwa ajira zao zipo na hizo kazi uhitaji wao ni mwingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo namna ya kuongeza ajira ni kuwekeza kwenye shule zetu za ufundi ili tupate vijana wengi ambao wanaweza wakapata ajira za kawaida ambao uhitaji ni mkubwa; iwe kwenye sekta yoyote, iwe kilimo, mifugo, hata kwenye Sekta ya Madini, tukitaka value addition bila kuwekeza kwenye Vocational Training watu ambao watajua kusanifu na kuchonga madini yetu ili tuzalishe bidhaa hapa hapa, hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba ile 2% ambayo tuliipeleka katika kipindi tulichokuwa na dharura, hatukuwa na fedha ya mikopo, basi turudishe irudi kwenye VETA. Mbali na hiyo, ni vizuri pia tukaangalia namna ya kuhakikisha kuwa hiyo One Stop Center iwe na mafanikio makubwa kwa biashara kubwa na ndogo, lakini pia Ofisi ya Uwekezaji iweze kukaa na Wizara mbalimbali. Leo hii ili waonekane wanafanya kazi kubwa, wanaanza kudai tozo na ada ya miaka kumi nyuma. Unakuta mtu wa TFDA anakuja anakudai vitu vya miaka kumi nyuma. Unakuta OSHA, Regulatory Boardies, yaani Taasisi za Udhibiti, zinakuja kukudai vitu vya miaka 10 nyuma. Je, siku zote walikuwa wapi? Sasa ni vizuri tukafutilia mbali madeni ya nyuma, wakaanza leo kwa sababu waliolala usingizi walikuwa ni wao, sio wafanyabiashara. Mfanyabiashara kutokujua sheria, siyo kosa lake. Sasa ni vizuri haya yakafanyiwa kazi na ninaamini kabisa kwamba hali ya ufanyaji biashara itakuwa na unafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hiyo, ni vizuri pia sekta binafsi kwa kupitia Baraza la Uwezeshaji lakini pia kwa kupitia Baraza la Biashara Taifa ambalo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, liweze kufanya kazi kubwa na kuunganisha na kuangalia kwamba nini kinahitajika ili kazi iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika watu wamezungumzia urasimu, namshukuru Waziri wa Uwekezaji, juzi kulikuwa na vibali ambavyo vilitakiwa vitolewa ili mtu aanze kuwekeza kwenye Kiwanda cha Sukari. Aliweza kupiga simu mbili na ndani ya wiki moja kibali kikatoka, lakini yule mtu alihangaika zaidi ya miezi sita, ilikuwa hapati. Sasa ni vizuri pawe na mfumo au website ili hata kama mtu anaomba katika Wizara nyingine aweze kutoa taarifa hiyo kwa Waziri wa Uwekezaji ili Ofisi yake iweze kufanya kazi ya uratibu kwamba kwa nini hiki kitu hakijatoka kwa muda maalum? Kwa sababu watu wakipata vibali kwa muda maalum, nina uhakika watu watawekeza na mambo yetu yataenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo ni muhimu sana, kwamba tukija kwenye Finance Bill kwa kupitia Waziri wa Uwekezaji na Waziri wa Kazi, ni vizuri tukaangalia hizi kodi mbalimbali ambazo ni kubwa, tuzipunguze lakini tukizipunguza hatutapata tatizo lolote kwenye ukusanyaji kwa sababu compliance itakuwa kubwa. Leo hii kama kodi ni kubwa watu wengi wanaendelea kukwepa, juzi Mheshimiwa Rais amezungumza vizuri sana, naamini muda huu ni muafaka, amezungumzia kipindi cha Bunge la Bajeti, tutaweza kufanikiwa kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hiyo, wengi wamezungumzia suala la vibali; upatikanaji wa permit. Kwa watu ambao wanawekeza, kuna aina mbili; kuna wale ambalo ni skilled labour ambao wana vyeti vyao vyote, lakini pia kuna unskilled labour, lakini ana uzoefu mkubwa. Vile vile mwangalie wale ambao ni unskilled lakini wana uzoefu, vibali hivyo viwe vinatoka kwa urahisi zaidi ili biashara hizo ziweze kufanyiwa kazi na Serikali itapata kodi kubwa na watu wetu wa humu ndani pia wataweza kujifunza kutokana na suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hayo, napongeza tu kwa kuanzishwa kwa Wizara hii ya Uwekezaji na ninaamini kabisa kwamba kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara zote hizi zikifanya kazi vizuri kwa ushirikiano, tutakuwa na mafanikio makubwa na tutaweza kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata viwanda vingi, biashara inakua na uchumi wetu unakua. Wananchi wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wote wa Jimbo la Babati kwa kunirudisha kwa awamu ya pili kuwa mwakilishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikiongozwa na Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa mwendo na kasi na matumaini mapya ambayo wameonyesha kwa Watanzania wote. Vile vile nishukuru uongozi mzima uliochaguliwa ikiwa pamoja na wewe Mwenyekiti, Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wenzako na Mawaziri wote waliochaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Dkt. Mpango, Waziri wetu wa Fedha kwa kuja na mpango mzuri, mpango ambao unaonyesha na umeangalia sekta zote. Mpango huu ukitekelezwa vizuri nina uhakika kabisa kwamba yale malengo ambayo tunayo ya kufikia miaka mitano ijayo na huu wa mwaka mmoja ya kufikia kuwa nchi ya kipato cha kati, tutafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika Mpango huu inabidi Serikali ijipange vizuri sana, kwanza kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana kwa kutekeleza yale yote ambayo yamepangwa na ambayo yako kwenye Mpango. Pia Watumishi wengi ambao wako Serikalini kubadilika fikra zao, yaani mindset change. Tusipobadilika hayo yote yataendelea kubaki kama yalivyokuwa huko nyuma, mipango inakuwa mizuri lakini haitekelezeki.
Muhimu kuliko yote pia ni kuhakikisha kwamba suala lile la nidhamu kwenye matumizi ya fedha iheshimiwe hasa zile fedha ambazo ni ring-fenced. Yale yakiheshimiwa nina uhakika kabisa zile fedha ambazo zimepangwa kwenda kutekeleza miradi mbalimbali itakuwa inaenda. Kwa mfano, miradi ya REA na ule mpango wa maji. Yale pia tutaomba wakati wa majumuisho, basi tupatiwe taarifa rasmi ili tuweze kujua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la muhimu lingine ni kuhakikisha kuwa suala zima la PPP linafanyiwa kazi kwa undani kabisa. Serikali ikubali, hasa wale Watumishi wa Umma wajue kabisa kwamba Serikali haiwezi kutekeleza haya mambo yote yaliyoko kwenye Mpango. Sehemu kubwa hasa huko tunakoelekea kwenye viwanda, viwanda vidogo, vya kati, viwanda vikubwa na hata mambo mbalimbali ya miundombinu ya huduma, wakishirikiana na sekta binafsi, yaani PPP, tutaweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ni muhimu Serikali ijipange katika uratibu baina ya Wizara moja na nyingine, ile coordination iwe ya hali ya juu. Kila Wizara isiwe na mpango wake, kila Wizara ifanye kazi, Wizara zote zishirikiane ili mpango kama ni wa kutekelezwa basi coordination iwe ya hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kabisa kwamba safari hii, sekta kubwa imelengwa ni sekta ya kilimo. Kilimo kwa mapana yake. Kilimo, mifugo, uvuvi yote hayo yapo kwenye mpango huu. Muhimu naomba tujipange. Kulikuwa na ile ambapo Tanzania ilikubaliana kwenye Maputo Declaration kwamba asilimia 10 ya bajeti nzima. Kwa hiyo, bajeti ambayo tunategemea kwamba itapangwa safari hii 10% yake itaenda kwenye sekta hiyo ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia asilimia moja (1) ya bajeti nzima pia itaenda kwenye sekta ya utafiti kwa sababu bila utafiti hatuwezi kuendelea. Tukiangalia vituo vyetu vya utafiti vina hali mbaya sana, tukiangalia watafiti wetu wana hali mbaya. Sasa tukiwatengea bajeti, mengi tunaweza kuyafanya humu humu nchini kutokana na mazingira yetu na kutokana na hali yetu tunaweza kwenda tunapotarajia kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine muhimu ni suala la kwenye bajeti itakayopangwa hiyo ya asilimia 10 kwenye kilimo, suala zima lile la fedha ya kununua mazao, lisiwe kwamba ni moja katika asilimia inayoongezwa pale. Leo unaambiwa bajeti ya kilimo ni kubwa sana lakini utakuta zaidi ya nusu ya ile fedha inakwenda kununua chakula ya hifadhi. Sasa ile siyo maendeleo ya kilimo ile ni pesa tu imewekwa kwa ajili ya kununulia mazao, hiyo iwe kwenye kitengo tofauti kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine muhimu ni nidhamu ya matumizi na matumizi mabaya ya fedha. Ni muhimu sasa tujikite huko. Kila mwaka tunasikia na Wabunge wote hapa wamechangia, reli ya kati, unakuta barabara, kila mwaka fedha ya maafa inatumika kwa mabilioni. Kila mwaka sehemu hiyo hiyo. Ni vizuri sasa wale ambao wanaosimamia hayo maeneo kwa nini wanasubiri tu kwamba haya maafa yatokee kila mwaka wapate hizo fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu naona kwamba, labda ni mradi wa namna ya kula hizo fedha, lakini muhimu ilitakiwa kwamba kama haya mafuriko yametokea sehemu fulani, tukaangalia chanzo chake ni nini, kama ni maji yanatokea sehemu fulani tuweke mabwawa huko juu, maji yasije yakaharibu huku chini ili yale maeneo ya huko juu maji yakivunwa yatumike kwenye umwagiliaji, maji ya kunywa, maji ya mifugo na hii fedha badala ya kwenda kila mwaka kwenye maafa itapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka kuna mikoa ambayo tunapeleka chakula cha msaada ni mabilioni ya shilingi, lakini hayo mabilioni ya chakula yanayopelekwa kule kwenye mikoa hiyo, ingepelekwa miundombinu wa umwagiliaji, kuvuna maji na umwagiliaji. Baada ya mwaka mmoja mikoa ile ingezalisha chakula kingi, kuliko hii mikoa ambayo tunapeleka chakula huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la matumizi ya fedha Serikali ijikite, tuangalie maeneo yote yale ambapo tunaweza kubana matumizi. Tuweze kubana lakini kabla ya hiyo bajeti pia natarajia kabisa kwamba sheria ya manunuzi tutakuwa tumeifanyia kazi. Hata tungekusanya mabilioni ya shilingi asilimia yote inakwenda kutumika vibaya kwa sababu sheria mbovu, sheria kandamizi, sheria hiyo ya manunuzi. Nashukuru kwamba, miaka minne nilipigia kelele hiyo sheria, sasa italetwa na naamini Wabunge wote tutashirikiana kwa kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningeendelea kushauri, ni kwamba tumeambiwa safari hii katika ile Sheria ya Bajeti, Maafisa Masuuli wa sasa watakuwa wanapanga bajeti kutoka kila Mkoa, kila Idara. Ni vizuri basi ushirikishwaji wa wadau wote katika kila mkoa, katika kila Taasisi, uanze mapema ili maoni ya watu wote namna ya kwenda, namna ya kufanya ufanyiwe kazi mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine tunaposema tunaanza kuwekeza kwenye sekta nzima hii ya kilimo, ili tuweze kuwa na viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa ni vema tujikite maeneo ambayo tayari yanazalisha. Kwa mfano, sukari kuna maeneo ambayo tunazalisha miwa, kwa mfano kule Babati, lakini utakuta kwenye mpango mpya huu wa kuanzisha viwanda vipya, Wilaya ile haipo. Tunataka kuzalisha labda mafuta ya mawese, utakuta Wilaya husika haijahusishwa, kwa hiyo, vizuri yale maeneo husika yafanyiwe kazi na yawe kwenye mpango kwa awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwenye suala la namna ya kukusanya mapato zaidi ili Serikali iwe na wigo mpana wa kukusanya kodi. Suala la kutumia mashine za EFD’S tunashukuru na tunasema kila Mtanzania ambaye anafanya biashara atumie mashine ya EFD. La muhimu tulipendekeza kwamba, badala ya kuwa centralized, kwamba kampuni chache ndiyo ziruhusiwe kuleta hizo mashine na kusambaza, kila Mtanzania ambaye ana nia ya kuwa na mashine hizo na kufanya biashara hiyo, kwa mfano hapa Dodoma, unaweza kuwa mtu anataka mtaa fulani kama zile za cable aweze kuwa na bishara yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke viwango vya zile mashine zinavyotakiwa kutumika ili service ya ile mashine pia ziweze kupatikana katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi Serikali iangalie namna ya kupunguza kodi na tozo mbalimbali, ili viwanda vya ndani viweze kukua. Leo niwape mfano, kwenye sekta ya mbegu tunaagiza asilimia 75 ya mbegu toka nje ya nchi. Ni kutokana na huko nyuma, ilikuwa asilimia 70 inazalishwa ndani 30 inatoka nje.
Baada ya Serikali kuweka kodi na tozo mbalimbali, kwa wingi tayari sekta hiyo imekufa kabisa leo tunaagiza mbegu kutoka nje, ambayo haina kodi kabisa. Madawa ya mifugo kutoka nje, hayana kodi lakini ukizalisha ndani ya nchi ina kodi. Kwa hiyo, mfumo mzima wa utozaji wa kodi, uangaliwe ili sekta binafsi na sekta zote ziweze kukua ndani ya nchi. Viwanda hivi, kama tusiporekebisha, mfumo mzima na tozo mbalimbali haitakua, na watu hawatawekeza katika suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia maeneo mengine tuangalie mbinu mbadala, tushirikishe watu, kwa mfano, kwenye Sekta ya Uvuvi, tulishapendekeza huko nyuma. Tunaweza kutumia nishati mbadala kama gridi ya Taifa haifiki, katika maeneo ya Pwani, katika maziwa mbalimbali, mahali kuna uvuvi tupeleke nishati mbadala, solar na hii ya upepo, ili wakulima wetu, wafugaji wetu, wavuvi kule wawekewe ghala/friji ndogo ndogo za kuhifadhi mazao yao ili badala ya kuuza samaki kwa vikapu, waweze kuhifadhi hawa samaki, waweze kuwauza kwenye soko ili waweze kupata bei nzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo madini mengi, sasa Serikali ijikite kwa mfano, tuna madini ya gemstones vito vya thamani ya chini. Tuna kituo pale Arusha cha Kanda ya Kaskazini, ambapo Serikali ingewekeza fedha za kutosha….
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na fursa ya kuwepo hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kasim Majaliwa pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mheshimiwa Abdallah Possi na Mheshimiwa Anthony Mavunde, wote kwa pamoja kwa kuunda timu ya uhakika ya kuleta maendeleo. Niipongeze pia timu ya wataalam wa ofisi zote chini ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nipongeze hotuba nzuri ambayo ilisomwa na Waziri Mkuu ambayo imegusa nyanja zote. Niipongeze Serikali kwa kuja na mpango wa kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti,kwanza kabisa naomba niishauri Serikali na wataalam, ijipange kuangalia suala zima la sera na sheria pamoja na kanuni mbalimbali ili tufanikiwe katika mipango yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naona kutakuwa na tatizo katika mfumo wetu wa gharama za juu kwenye uzalishaji. Viwanda vingi nchini vimeshindwa kupata mafanikio kwa sababu ya sera yetu ya kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa na Taasisi za Udhibiti (Regulatory Bodies), ndiyo maana hata baada ya kuongeza kodi ya kusafirisha nje malighafi, mfano ngozi au korosho ghafi, lakini bado zinasafirishwa ghafi kutokana na gharama mbalimbali za tozo na kodi zinazotozwa katika usindikaji ndani ya nchi kuwa kubwa kuliko hiyo export levy.
Pia bidhaa nyingi huingizwa nchini bila kodi yoyote, kama mbegu, madawa ya kilimo (viuatilifu) na mifugo (dawa za chanjo na zinazozalishwa nchini kutozwa kodi na tozo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali iangalie namna ya kuondoa tozo hizo zinazotolewa na wadau kwa ajili ya huduma zao na badala yake Serikali igharamie gharama za uendeshaji wa taasisi hizo. Leo hii zimebaki kufanya kazi ya kukusanya tozo zaidi badala ya huduma. Baadhi ya tozo hizo ziondolewe kabisa kwa sababu zinaleta ushindani usio wa haki (no fair trade practice); waliosajiliwa hutoza zaidi kuliko wasiosajiliwa. Taasisi nyingine hufanya kazi zinazofanana. Pia Serikali iangalie namna ya kuondoa urasimu na kupunguza muda wa kutoa maamuzi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine muhimu ni kuongeza bajeti ya utafiti. Utafiti ndani ya nchi unatakiwa kuboreshwa sana. Njia pekee ni kuwekeza katika rasilimali watu, vifaa na kutoa taarifa za utafiti huo (dissemination of information).
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba tuishauri Serikali kama Bunge, itangaze bila kukosa mafanikio yote yaliyofanywa na Serikali. Serikali haitangazi yote yaliyofanywa kutoka miaka mingi iliyopita. Hii inatoa fursa kwa Wapinzani wa Serikali yetu kutusema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na kunipa uwezo wa kuchangia leo. Naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa na imani kubwa kwa kumteua Mheshimiwa Profesa Muhongo kuwa Waziri na Mheshimiwa Dkt. Matogolo kuwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, uamuzi wa kupeleka asilimia 40 kwenye maendeleo kwa Wizara ya Nishati na Madini; napongeza kwa juhudi kubwa katika sekta zote za nishati na madini. Naomba nianze na suala la nishati; kwanza nishukuru kwa mradi wa REA, katika Wilaya ya Babati maeneo yanayotarajiwa kupata nishati hii tayari wananchi wameanza kujipanga kutumia kwa maendeleo. Katika REA II maeneo mengi yameachwa, tunaomba na nashauri, katika Mpango wa REA III hayo maeneo na taasisi muhimu yapatiwe umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara kupitia TANESCO itusaidie kupitisha design ya nguzo za cement za umeme ili tuweze kuanza kuzalisha. REA III itahitaji nguzo nyingi sana, tukiruhusiwa sasa uzalishaji baada ya design kukubalika itatusaidia kufanya matayarisho mapema.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Wizara isaidie kufuta (charges) gharama ya kutotumia umeme katika mradi wa kilimo na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yetu ambayo viwanda hivyo hufanya kazi kwa miezi miwili au mmoja tu pamoja na umwagiliaji. Tozo hiyo inaua viwanda na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iangalie namna ya kuongeza tozo kwenye mafuta, napendekeza iongezwe sh. 200/= kutokana na bei ya mafuta ya dunia imeshuka sana. Hakuna nauli, usafiri au bidhaa iliyoshuka, hawana kodi iliyoongelea kutoka kwa wafanyabiashara, ikiongezwa sh. 200/= kwa lita, sh. 70/= iende REA, Umeme Vijijini, sh. 70/=; Maji Vijijini, sh. 40/= iende Mfuko wa Utafiti na sh. 10/= Mazingira. Bei ya mafuta ikipanda duniani, basi tozo hii ipungue kidogo kidogo. Tunaweza kupata takribani shilingi bilioni 330 kwa miezi sita. Kwa hiyo, wastani wa shilingi bilioni 110 kwa Nishati Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nashauri Serikali iondoe Kodi ya VAT kwenye vito na vidani (germstone and jewelry) vinavyouzwa ndani ya nchi (local sale). Kama bei ya dunia ya dhahabu inajulikana na vito kuweka VAT inafanya sekta isikue. Nashauri kituo cha Arusha cha Mafunzo kiboreshwe na mafunzo ya kuchonga vito na kutengeneza vidani (jewelry and lapidary) ianze mapema. Napongeza juhudi za Wizara kwa sasa. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya kuchangia leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa kazi nzuri inayofanya, vile vile niwapongeze Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yake ya wataalam wote kwa kazi nzuri wanayofanya. Pia niishukuru Serikali kwa kukubali kuanzishwa kwa Wakala wa Maji RUWASA yaani chombo ambacho kitakuja kusaidia na kuondoa kero zote ya maji, tunaamini hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu kwenye RUWASA ni kuwa na chanzo cha uhakika cha mapato ambapo itakuwa inatekeleza miradi. Huku kote tulikuwa tunalalamika kwamba miradi inasimamiwa vibaya, miradi imesanifiwa vibaya naamini RUWASA wakianza, wataanza na wataalam waliobobea wataalam wazuri na kutakuwa na usimamizi mzuri. Kwa hiyo RUWASA tunaamini itakuwa sawa na REA kwa upande wa maji. REA imepata mafanikio makubwa kutokana na usimamizi mzuri, lakini pia upatikanaji wa fedha wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, leo hii tumepata Sh.50 ambayo tulitenga kama Bunge kwa ajili ya kwenda kwenye Mfuko wa Maji. Kwa sehemu kubwa bilioni 106 ambayo ni sawa na asilimia 67 ya fedha iliyotakiwa kwenda ya bilioni 158 ndiyo fedha ya Mfuko wa Maji. Fedha ya bajeti ya kawaida ni bilioni 333, bilioni 443 ni asilimia 17 tu iliyoenda yaani bilioni 43 ndiyo zimeenda. Sasa ukizijumlisha zile zote mbili ya Mfuko wa Maji iliyoenda na bajeti ya kawaida iliyoenda, bado haijafikia fedha zote ingekuwa imepatikana asilimia 100 ya Mfuko wa Maji ambayo ni ring fenced. Sasa tunapoomba iongezwe shilingi 50 iwe shilingi 100 au tutafute na vyanzo vingine iwe ni kwa kutokana na mitandao yaani kutokana na DART au EWURA au vyanzo vingine zikipatikana bilioni 150 nyingine ya ziada itakuwa tunapata karibu bilioni 300 na ndiyo fedha zote zilizoenda leo kwenye miradi yote ya maji ya fedha ya ndani, ya nje yote jumla imeenda bilioni 343 ambayo ni asilimia 51 tu ya fedha iliyotengwa kwa ujumla wake. Kwa hiyo sehemu kubwa ya hii fedha ni huu Mfuko wa Maji lakini pia Mfuko wa Maji unapeleka maji mijini pamoja na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri tukaboresha Mfuko huu ukapatiwa, tusiogope kuweka hata hiyo ya mafuta watu ambao wanasema italeta inflation. Kipindi hicho bei ya mafuta imeshuka mpaka Sh.1,400, hakuna nauli iliyoshuka, hakuna bidhaa iliyoshuka wala hakuna kodi ya ziada, walikusanya kutoka kwa wafanyabiashara waliopata super profit kutokana na hiyo bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mfuko huu wa Maji unapeleka maji mjini na pamoja na vijijini. Ni vizuri tukaboresha mfuko huu, tusiogope kuweka tozo kwenye mafuta ambapo watu wanasema italeta inflation. Kipindi bei ya mafuta yameshuka mpaka 1,400 hakuna nauli au bidhaa iliyoshuka bei wala hakuna kodi ya ziada mlikusanya kutoka kwa wafanyabiashara waliopata super profit kutokana na bei hiyo. Sisi kama Wabunge tutawaelimisha Watanzania kwamba tumefanya hivyo ili wapate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu sana ni suala la uvunaji wa maji ya mvua na mito ili tuweze kuyatumia vizuri. Kwenye hilo la uvunaji wa maji tulishapitisha sheria kwamba majengo yote yanayojengwa mjini na sehemu nyingine kama huna mfumo wa kuvuna maji basi usipewe kibali cha kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia huko tunapopoteza maji mengi kwenye mito na maji ya mvua, Serikali iondoe kodi kwenye mitambo ya kuchimba maji na kutengeza mabwawa. Siyo lazima kila kitu kifanywe na Serikali mitambo ikiwa ya bei nafuu wananchi wa kawaida (private sector) itawasaidia kujenga mabwawa kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaposema tumtue mwanamke ndoo kichwani ni vizuri Serikali ikaondoa pia kodi kwenye solar pumps. Leo hii miradi mingi ya maji ambayo inatumia diesel au umeme, wananchi vijijini wanashindwa kulipa bili tungetumia solar pumps. Solar pumps ukileta leo ina kodi lakini solar pump hiyo hiyo ukiileta kwa njia ya irrigation haina kodi, ni controversial. Anayetaka kuleta pumps kwa ajili ya umwagiliaji haina kodi ila ukileta kwa ajili ya matumizi ya kawaida ina kodi. Ni vizuri Serikali ikaweka msimamo ikaondoa kodi jumla ili hata yule mwananchi wa kijijini pump hiyo imsukumie maji mita 400 sawa na yule wa mjini inawezekana ikidhamiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hizi mashine za kuchuja maji (water purifiers? Mkiondoa kodi kwenye water purifiers bajeti ina maana tunayotumia zaidi ya shilingi bilioni 45 ya kutibu magonjwa ambayo yanatokana na maji hiyo pesa tungeweza kuitumia kupata maji safi na salama, ni bora kukinga kuliko kutibu. Kwa hiyo, tungeweza huku kuondoa kodi ndiyo utapoteza kidogo lakini ile shilingi bilioni 45 unayopeleka kwenye afya utaweza kuiokoa na wengi wanaopata shida hiyo ni watu wanoishi vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye mitambo ya kuchimba maji, nchi zote za Afrika Mashariki hazina kodi isipokuwa Tanzania. Kwa wale wakandarasi wakubwa ambao wanaleta vifaa vya kuchimba maji pamoja na Drilling and Dam Construction Agency wote wanapata msamaha wa kodi lakini mwananchi wa kawaida akitaka kuleta mashine yake moja hata kama ni mtumba bado anatozwa kodi ndiyo maana gharama za uchimbaji maji zimekuwa kubwa na uvunaji wa maji umekuwa mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Wakala wa Maji katika maeneo mbalimbali katika wilaya ambazo zina Bodi ni vema tungeziunganisha. Kwa mfano, Bodi moja inaweza kuhudumia wilaya tatu, nne hata mkoa mmoja kwa sababu ndiyo tutapata ufanisi kuliko kila kata na tarafa kuwa na Bodi yake ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukajipanga na naamini tukijipanga vizuri haya yote ambayo tunayazungumza tutafanikiwa. Maeneo mengi ambapo mashine zinatumia diesel au umeme tufunge solar na hasa katika taasisi mbalimbali za Serikali. Tukiweza mifumo hiyo gharama ya uendeshaji itakuwa ndogo na pia upatikanaji wa maji ni mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya maji tusipoyavuna ndiyo yanakwenda kuharibu miundombinu ya barabara na reli. Tukiweza kuvuna maji hayo na tukayatumia vizuri tutapata maji ya kunywa, ya umwagiliaji na mabwawa ya kufugia samaki na pia tutaweza kuzalisha zaidi hata maji ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa tunalopata uzalishaji wetu unakuwa mdogo hata upande wa umwagiliaji kutokana na kwamba hatuna vifaa vya kuchimbia mabwawa haya. Ondoeni hiyo kodi kidogo wenye kustahili kupata msamaha tayari wanapata ni hao wachache wachache ndiyo hawapati. Kwa hiyo, mngeruhusu hata kwa private sector pia maana itaweza kusaidiana na Serikali katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tozo mbalimbali ambazo zinachajiwa na Mabonde kwa watu ambao wanatumia maji. Ni vizuri tukaangalia zile chaji katika Mabonde yote bei zifanane. Ni vizuri tukawezesha haya Mabonde zikasaidia upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ambao naomba Serikali izingatie, leo hii kwa sehemu kubwa tumeanza kutumia maji ya ardhini lakini hatujawekeza hata shilingi moja wala hatuna asilimia hata moja ambayo inaenda kwenye kutunza vyanzo vya maji na maeneo ya catchment (vidaka maji) ambavyo vita-recharge aquifer za kule chini. Tusipo-recharge zile aquifer baada ya muda hata hivi visima ambavyo leo tunapata maji kwa mita 80 mpaka 100 tutakuja kujikuta tunatafuta maji kwa mita 200 au 300 ambapo hatutakuwa na uwezo wa kutoa hayo maji huko chini. Kwa hiyo, suala la mazingira nashauri Serikali kwenye kila mradi ambao tunaanzisha angalau asilimia moja ya fedha yote mradi iende kwenye kutunza mazingira, kuboresha vyanzo vya maji na vidaka maji (catchment area) ili tuweze ku-recharge aquifer za huko chini ili tuweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Serikali ni moja ingeangalia bajeti tunayotumia upande wa afya kutibu magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji lakini vifo vinavyotokea kwa kutumia maji machafu na ambayo siyo salama, hayo tungeweza kuepuka kama tutaondoa baadhi ya kodi. Najua Serikali inasita kuondoa hizi kodi kwenye water purifier kwa sababu tutakosa kodi kwenye viwanda zinavyouza maji ya chupa lakini ni vizuri tukose kodi hiyo afya ya Watanzania iwe salama haswa huko vijijini ambapo sehemu kubwa tunakosa maji. Tukiboresha huduma za maji, umeme kama inavyoenda sasa hivi na miundombinu huko vijijini hakuna mtu yuko tayari kukaa mjini kwani maisha ya vijijini ni mazuri. Tukiboresha huko vijijini watu hawatarundikana mijini na kukosa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea kuboresha huduma mbalimbali huko vijijini na maji ni uhai na maji ndiyo maisha, kwa hiyo, kilimo mifugo, uvuvi haya yote tunaweza tukafanikiwa kama Wizara hii ya maji itashirikiana na kuratibu masuala mbalimbali ya namna ya kuboresha miundombinu ya maji kwa njia zote, iwe ni uvunaji wa maji na kusimamia. Pia Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha zikae pamoja ili kuangalia na kuondoa baadhi ya hizi kodi ambazo zitakuwa ni chache sana. Mimi naamini kwa data ambazo tunazo ni kodi kidogo sana ambazo tutapoteza kutokana na msamaha tutakaotoa ambapo multiply effect yake hii mitambo yote ikiletwa kwa bei nafuu watu wengi sana watachimba maji wenyewe na itaisaidia Serikali maana siyo lazima kila kitu kifanywe na Serikali. Kwa hiyo, dhana nzima ya PPP (Public Private Partnership) tutakuwa tumeifikia kama private sector na Serikali watashirikiana kufanya jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji kama ilivyo Babati Mjini ndiyo hivyo hivyo ilivyo katika wilaya zote Tanzania. Hakuna sehemu yenye nafuu, iwe mjini au vijijini kote kuna tatizo la kubwa la maji. Hakuna mahali hata huko mijini unaweza kufungua bomba la maji ukanywa yale maji bila uhakika kama ni safi au salama kwa sababu upatikanaji wa maji ni jambo moja lakini maji safi na salama ni jambo lingine. Kwa hiyo, ni muhimu tupunguze bajeti ya kwenye matibabu turudishe huku kwenye maji hata namna ya kutibu maji ili Watanzania wapate maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika Serikali hii ni sikivu huu ushauri ambao tumeutoa kwa muda wote huu mtauzingatia vizuri na haswa hii ya kuongeza bajeti ya Mfuko wa Maji ili iweze kufika agalau shilingi bilioni 350 maana pesa yote iliyoenda kwa ujumla wake ni shilingi bilioni 343. Kwa hiyo, ingekuwa tumeongeza mwaka jana au mwaka juzi badala ya shilingi 50 iwe 100 ungekuta pesa yote asilimia mia moja ingetokana na huo Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tujue hii miradi mingine, iwe ni mradi wa zile fedha za Exim Bank ya India au fedha nyingine tunayopata kutoka kwa wafadhili mbalimbali hailengi Watanzania wote bali inaenda kwenye specific project. Kama ni miradi ya miji 28, kama ni ule Mradi wa Ziwa Victoria yaani ni miradi ambayo imetengwa na imechaguliwa, je, sisi ambao hatuko kwenye hiyo miradi tunapata wapi hiyo bajeti na ukiangalia ni shilingi bilioni 41 tu ndiyo imeenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima muweke utofauti kati maji mjini na maji vijijini. Percent kubwa ya Watanzania wanakaa vijijini, kwa hiyo, asilimia kubwa ya fedha inatakiwa kwenda vijijini. Ni sawa na hii ya TANROADS na TARURA ilivyowekwa kwamba asilimia 70 ni ya TANROADS na asilimia 30 ni TARURA, hapa pia kwenye huu Mfuko wa Maji asilimia 20 ndiyo iende mjini na asilimia 80 iende kuwasaidia Watanzania wanaoishi vijijini kwa sababu huko ndiko kwenye shida kubwa ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho tutumie E-water. Mfumo wa E-water itasaidia maji kupotea na ni eneo ambapo Serikali itaweza kukusanya mapato yake kabla. Hata kama ni zile Kamati za Maji zinazosimamia gharama ya usimamizi wa maji inakuwa ndogo, Serikali itaendelea kupata unafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuendelee kuboresha vyuo vyetu ambavyo vinafundisha hawa wataalam wa maji na naamini kabisa RUWASA ndiyo itakuja kuwa mkombozi wa sekta ya maji Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kuweza kupata fursa ya kuchangia. Pia nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri na kubwa na kwa nia ya dhati ya kuonesha kwamba, kutakuwa na mabadiliko katika sekta nzima ya kilimo. Nimshukuru Waziri, Manaibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ambayo iko Wizarani kwa kazi kubwa na nzuri na taasisi zote zilizoko chini yao kwa kazi kubwa wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote tunaendelea kushauri na ningeomba Wabunge wengi badala ya sehemu kubwa kutumia muda wetu kuelezea changamoto, changamoto kila mtu anazijua. Tuendelee kutoa ushauri mbalimbali ili kwenye dakika 10 kama dakika nane kila mtu atatoa ushauri, kwa Wabunge 300 angalau moja au mbili ikichukuliwa hapo tayari tutakuwa na mageuzi makubwa kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza ningeendelea kuomba kwamba bajeti ya Serikali tuendelee kuiongeza. Najua wataalam wanaweza kusema kwamba bajeti hii kwa kilimo peke yake inajitosheleza kwa sababu bado kuna mengi huko kwa sababu ni mtambuka, bajeti inaenda kubwa yaani inaenda kwa Wizara nyingine nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa utafiti wangu binafsi, naweza kuwa nimekosea, nikiangalia bajeti ya mwaka jana na mwaka huu ya kilimo utaona imepanda kidogo lakini ukiirudisha (convert) kwenye bei ya USD bado imeteremka haijapanda. Lakini ukiichukulia kwa ujumla wake, kwamba trilioni 33, ukichukulia 10 percent yake ambayo ilikuwa ndiyo makubaliano kwamba iende kwenye kilimo, inatakiwa angalau kwenye trilioni tatu au zaidi. Hivi nikichukulia Wizara zote ambazo zinaenda vijijini ambako kilimo kwa sehemu kubwa kinapofanyika hiyo trilioni tatu sikuiona; yaani mimi nilivyojumlisha jumlisha tu sioni hiyo trilioni tatu. Kwa hiyo, bado bajeti ya kilimo inazidi kushuka na mchango wake katika Pato la Taifa bado nao unaendelea kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba sekta nyingine zinaendelea kukua, lakini asilimia kubwa ya Watanzania walipo ndipo huko kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kwa ujumla tunasema kilimo; kwa hiyo ni vizuri tukaangalia namna ya kuboresha bajeti yake. Serikali isiangalie tu namna ya kuongeza bajeti kwa kupitia Serikali yenyewe, iweke mazingira wezeshi ili na sekta binafsi pia iweze kuchangia kwa sehemu kubwa na kama ilivyokuwa kwenye ASDP II, asilimia 65 inatakiwa fedha zitoke kwa sekta binafsi; lakini pasipokuwa na mazingira wezeshi, Serikali isipoweza kufanya kama timu moja, pakawa na uratibu, bado haya mambo yote hayatawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusitegemee Wizara ya Kilimo, wanafanya kazi nzuri na wana mpango mzuri ila Wizara nyingine zote zisiposhirikiana bado tutaendelea kupata changamoto hiyo. Kwa hiyo, naomba mfanye kazi kama timu na wote mkae mezani mnapojadili kilimo basi kama ni kodi, tozo na ada mbalimbali mshirikiane namna ya kuzipunguza au kuziondoa. Huku kukiwa na tija huko kwingine utaendelea kupata kodi kwa njia nyingine ambayo ni indirect tax. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuomba; tunaendelea kutegemea umwagiliaji, bila umwagiliaji hatutaweza kusogeza kilimo mbele. Sasa kwenye umwagiliaji tulikuja hapa na wazo kubwa tukaanzisha sheria na ikaanzishwa Tume ya Umwagiliaji; lakini tangu imeanzishwa bado haijawahi kupewa fedha yoyote, yaani ni sifuri, kwenda kushughulika na umwagiliaji. Sasa nilikuwa naomba tuiwezeshe Tume ya Umwagiliaji ili kwenda kushughulika kwenye umwagiliaji. Sasa nilikuwa naomba tuiwezeshe Tume ya Umwagiliaji ili iweze kufanya kazi yake. Pamoja na hiyo ningeomba kwamba Benki ya Kilimo na Mfuko wa Pembejeo nao wawezeshwe vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila kwenye hiyo pesa ambayo wamepata pawe na mkakati maalum, kwamba asilimia 20 ya fedha wanayopewa kukopeshwa kwenye sekta ya kilimo basi 20 iweze kutumika kwenye umwagiliaji tu, hapo pia utaiona sekta binafsi kwa sababu ni pesa ambayo watakopa watarudisha. Kwa hiyo, Benki ya Kilimo na Mfuko wa Pembejeo watenge asilimia 20 ambazo zitaenda kwenye umwagiliaji tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye umwagiliaji bado kuna changamoto nyingi. Kwa mfano ukitaka leo kuchimba visima, ukitaka kuleta mitambo ya kuchimba visima, kutengeneza mabwawa, solar pump za irrigation zote zina kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukishirikiana, kama Serikali mkikaa pamoja, ondoeni hizo kodi, wekeni mazingira wezeshi ili watu waweze kuchimba visima, kutengeneza mabwawa, na private sector itafanya. Kwa hiyo Serikali iweke tu mazingira mtaona kwenye kilimo jambo hilo la umwagiliaji litaendelea kukua. Pia mboreshe na kuandaa wataalam wa kutosha kwa upande wa umwagiliaji ili wao wakiweza kufanya kazi vizuri kwenye umwagiliaji ndiyo tutakuwa tunaweza kuokoa Watanzania badala ya kutegemea mvua, tuweze kufanya kilimo cha uhakika zaidi, na badala ya kufanya msimu mmoja, tufanye misimu miwili au mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru kwamba kuna wazo la kuwa na Sera na Sheria mpya ya Kilimo ambayo tunaamini itakuja kulinda ardhi za kilimo. Leo hii maeneo mengi ya kilimo yanachukuliwa kuwa makazi na kubadilishwa matumizi; na hayo sisi si kama wenzetu, uwezo wetu ni mdogo. Leo Mji wa Dodoma tu kila mahali itakuwa makazi, hii zabibu na mvinyo wa Dodoma utapotea. Vivyo hivyo, maeneo ya makazi yamechukua hayo maeneo ya kilimo. Kwa hiyo, sheria ije ya dhati, tunaweza kwenda kujenga milimani, tukajenga maeneo ambayo hakuna rutuba na ardhi ambayo siyo nzuri kwa uzalishaji, tukapeleka tu maji, barabara na nishati makazi yatakuwa mazuri, lakini maeneo ya kilimo yalindwe kwa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija pia kwenye sekta ya mbogamboga (horticultural) inafanya vizuri. Huko pia tulikuwa tunaomba cold storage ili wakulima waweze kuhifadhi mazao yao kabla ya kwenda kusafirisha, hasa kwenye maeneo ambayo Serikali itawekeza. Vilevile sekta binafsi iweze kuwekeza kwenye cold storage na kwenye mambo ya chillers pia muangalie namna ya kusaidia kupunguza na kuondoa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Upande wa Ushirika. Tulishakubaliana kwamba leo tunaweka nguvu kubwa kwenye shirika, na ndiyo njia pekee ya kwenda mbele kwenye kilimo. Kwenye ushirika bado ile Sheria ya 2013 tulipobadilisha kuliwa na dhana kwamba pale lazima tuhakikishe kwamba fedha ambayo ushirika itakuwa inachukua hakutakuwa na makato ya wakulima, tulisema ushirika kazi yao ni kuhudumia wanachama wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanapotafuta masoko, wanapoleta pembejeo tofauti ya kwenye bei na nini wanaponunua kwa wingi ile tofauti ya bei ndiyo iwe inaendesha ushirika. Ushirika usimkate mkulima hata shilingi moja, ndiyo maana wakulima hawapendi kupeleka mazao yao kwenye ushirika. watu wapendelee kwenda kwenye ushirika badala ya kukwepa kwenda kwenye ushirika. Kwa hiyo, ni jambo ambalo naamini tukikaa tukaelezea vizuri, tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, luna jambo linguine. Leo hii tunaagiza vitu vitano; mbegu, asilimia kubwa ya mbegu zetu hasa mahindi, asilimia 65 ya mbegu inatoka nje ya nchi, usalama wa chakula na mbegu haupo. Kwenye mbegu kuna alizeti na mbegu hizi ambazo zinazalisha mafuta, tunaangiza sisi, baada ya mafuta ya magari mafuta haya ya kula ndiyo sehemu kubwa ya fedha yetu inakotumika. Kwa hiyo mbegu, sukari, mafuta, mchele, mbogamboga, matunda na hivi vyote ambavyo tunaagiza kutoka nje tuwekeza. Muwe na timeframe, kwamba ndani ya miaka mitatu hakuna kitu kitakachoagizwa nje, tutazalisha ndani ya nchi na sisi ndio tutapeleka nchi nyingine. Hayo yanashindikana kutokana na mazingira wezeshi kwenye sekta hii ya kilimo na Wizara zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mfano, juice zote tunazokunywa hapa Tanzania asilimia 99.5 ni concentrates kutoka nje, ni asilimia 0.5 ndiyo inazalishwa hapa nchini, kwa nini? Tukizalisha hapa nchini kwanza tutapata lishe bora, fedha kwenye uchumi wetu na tutapata mazingira bora kwa ajili ya miti hiyo mingi. Kwa hiyo itakuwa na trickling effect kwenye Wizara nyingine zote. Kwa hiyo, naomba tuifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni muhimu ni kwamba bajeti ya TARI ni ndogo sana, na tunapanga wakati mwingine tunaweza kupitisha hapa lakini fedha zinazokwenda ni ndogo. Bila utafiti kwenye kilimo hakuna uwezekano kwa kwenda popote kwa sababu kilimo ni sayansi, kilimo ni biashara kama biashara yoyote nyingine. Wekezeni kwenye TARI ili vituo vya utafiti vizalishe mbegu, viangalie namna ya kudhibiti magonjwa lakini pia tuangalia namna ya kuboresha ASA. ASA ina mashamba mazuri sana, wanahitaji uwekezaji wa kwenye umwagiliaji na uwekezaji kwenye zana za kilimo (matrekta na zana zake). Mkiwawezesha wale wala siyo kwa kuwapa bajeti, wakopesheni wataweza kulipa kwa sababu wanafanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia TPRI na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JITU V. SONI: Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kupata fursa ya kuchangia. Vile vile nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yao nzima kwa kuandaa mpango mzuri ambao tulivyokubaliana huko nyuma mpaka sasa hivi unakwenda vizuri sana, pia mkakati ambao umewekwa wa kukusanya mapato na kuhakikisha kwamba yale yote ambayo yamepangwa kwenye Mpango na bajeti iliyopangwa basi inatekelezeka vizuri. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru Serikali kwa juhudi kubwa ambayo inafanya katika kuhakikisha kwamba maendeleo sasa yanaonekana kwa uwazi kabisa na tumeanza kuyaona. Lengo kuu ni kukuza uchumi wetu na tufikie katika uchumi wa viwanda, lakini hapo hapo tukifungamanisha uchumi wa Watanzania wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niweze kushauri katika maeneo machache. Lengo kuu hapa na kwenye mpango huu imeelezwa vizuri kabisa kwamba kutakuwa na eneo, hasa kwenye elimu kuendelea kufundisha kwa wingi wataalam ambao ni wa ngazi ya ufundi ambao ni adimu, hawapatikani ili waweze kuja kusaidia kuendeleza mahali ambapo tunahitaji wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwamba huko huko tuweke nguvu kubwa zaidi kwa sehemu kubwa. Kama tunataka kuwa na uchumi wa viwanda, tunahitaji kuboresha Sekta ya Skills Development, yaani upande wa ufundi mchundo (technicians). Huko ndiko ambako tukiwa na viwanda vingi itawasaidia Watanzania wengi ambao uhitaji wao mkubwa zaidi ni kuingia kwenye soko la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie tutakapofika kipindi cha bajeti iwepo kwenye huu Mpango kama ilivyowekwa wazi hapa kwamba wataalam ambao ni adimu watafundishwa kwa wingi, basi pia tufundishe wataalam wetu wa kawaida, hawa mafundi mchundo (technicians) kwa kupitia VETA zetu. Kwa maana hiyo itafanya kwanza ajira ziwepo ambazo ni blue collar jobs, yaani kazi ambazo zitafanywa kwenye viwanda vyetu vyote. Pia viwanda vinavyotakiwa ni vya kisasa, vinavyokwenda na mfumo wa teknolojia ya kisasa kwa kutumia mifumo ya IT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huko kwenye VETA kunahitajika kuwekezwa zaidi mbali na ile mifumo ya zamani. Tu-phase out mifumo ya zamani, tuondokane na mifumo hiyo iliyokuwepo ili twende na mfumo huu wa teknolojia kwa kutumia IT kwa sababu siku hizi hata mashine ya kushona ya kawaida hii ya cherehani ina programming ambapo unatakiwa uwe nayo; na huhitaji kuwa na degree wala Ph.D kwenye hilo. Ni basic skills kwenye IT ili uweze kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri ili tuweze kwenda kwenye uchumi wa viwanda tuwekeze zaidi kwa upande wa VETA na hasa wataalam ambao watakuwa hands on, yaani watakuwa na uzoefu tayari. Akitoka pale chuoni tayari ana uzoefu wa kutosha kwa kupitia mpango wa ufundi wa dual apprenticeship au wa DATS, yaani anasoma kwa miezi miwili, miezi miwili anakuwa yuko anafanya kazi kwenye yale aliyofundishwa, anakwenda ku-practise ili ndani ya miaka mitatu akitoka pale tayari yeye amebobea katika fani hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hivyo hivyo kwenye kilimo, mifugo na uvuvi, hawa wote tukiweza kuwekeza zaidi katika elimu hiyo, ajira kwa Watanzania waliokuwa wengi itapatikana kwa sababu ajira ya watu wenye degree na Ph.D ni chache na ukiangalia Watanzania wengi ni vijana. Kwa hiyo, ni vizuri kuangalia mahitaji ya soko ni nini? Wanaotakiwa kwenye ajira ya aina hizo kwa kujiajiri au kuajiriwa, basi tuwekeze zaidi katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kuanzisha miradi ile ya kimkakati. Mmoja ni huu wa kufua umeme wa kutosha kwa kupitia Stiegler’s Gorge ambapo tutakuwa na umeme wa kutosha, kwa sababu ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote Tanzania tutakuwa tuna umeme. Huko huko ndiyo tunahitaji kuwa na viwanda vidogo vya kusindika mazao yetu na viwanda ambavyo tutaongeza thamani mazao yetu ili tuweze kupata kipato kikubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kuu ni kuhakikisha kwamba tunafungamanisha ukuaji wa uchumi pamoja na watu. Ukuaji wa uchumi wa watu ni kuwa na spending power. Yaani hawa wakulima, wafugaji na wavuvi ni vizuri tukawekeza zaidi kwenye Sekta hii ya Kilimo. Tukiwekeza kwenye Sekta ya Kilimo kwa mapana yake; kilimo, mifugo na uvuvi ambapo asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania wako huko, basi tutaweza kufanya vizuri na uchumi utakuwa kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni muhimu tuangalie namna ya kuondoa informal sector ili iendelee kupungua ili formal sector iendelee kukua. Leo hii trend iko tofauti. Sekta isiyokuwa rasmi ndiyo inaendelea kukua. Kwa hiyo, ni vizuri tukajipanga kuhakikisha kwamba tunarudisha mfumo ili sekta iliyokuwa rasmi ndiyo iendelee kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwa na viwanda ambavyo vitaweza kuzalisha na tukazalishe bidhaa ambazo zitakuwa na ushindani, katika soko la ndani, soko la kanda na soko la Kimataifa ambalo liko kwenye Mpango, ni vizuri suala lile la blue print tukalifanyia kazi. Leo hii gharama ya uzalishaji Tanzania ni kubwa kutokana na hizi regulatory authorities. Gharama ya uzalishaji kwa bidhaa zetu, zinakuwa kubwa kwa sababu hizi charges ambazo ziko kwa upande wa regulatory authorities ni kubwa mno. Kwa hiyo, hatuwezi kushindana. Hata viwanda vinavyozalisha ndani, ni bora utoe mali nje, itatoka China, itatoka nchi nyingine kwa gharama nafuu kuliko ile ambayo inazalishwa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili uchumi wetu ukue na bidhaa zetu zipate masoko, hasa bidhaa zinazotokana na kilimo, mifugo na uvuvi, ni vizuri suala la blue print lisifanyiwe kazi kwa taratibu. Yaani mngehakikisha blue print mnaileta mara moja, sheria ije na yale yote ambayo yanatakiwa yafanyiwe kazi; zile tozo na ada zote ziondoke. Tulishawahi kupendekeza mara nyingi, mngekuwa na Tanzania Regulatory Authority ambapo kunakuwa na upper stream na lower stream. Jambo hilo mkilifanyia kazi, nina uhakika kabisa kwamba bidhaa tutakazozalisha hapa nchini zitakuwa zinaweza kushindana kwenye soko la ndani, soko la kanda, lakini pia soko la Kimataifa. Bila kufanya hivyo, nina uhakika kabisa kwamba bado Tanzania itakuwa net importer wa bidhaa kutoka huko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata bidhaa zetu nyingi ambazo tunazalisha hapa nchini, zinapelekwa nje wanakwenda kuzalisha kule halafu bidhaa hizo hizo zinarudi nchini kwa kupitia pamba, kwa kupitia mazao yetu mengine. Bidhaa zinatoka nje halafu zinarudi ndani ya nchi kutokana na gharama za uzalishaji wa hapa ndani ya nchi kuwa kubwa. Sehemu kubwa ni kutokana na hiyo blueprint ambayo tulisema kwamba Serikali tayari imeifanyia kazi, tunashukuru maeneo mengi mmeweza kuyafanyia kazi lakini mngeleta kwa ujumla wake ili ianze kazi mara moja kabla hatujafika kwenye bajeti ya mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika haya yote yakifanyiwa kazi, mtaona kasi ya ukuaji wa uchumi wetu itaongezeka mara dufu na itaweza kufanya ajira nyingi zaidi ziweze kupatikana kwa sababu malighafi ambayo tunazalisha hapa nchini itakuwa inasindikwa hapa hapa nchini au kuongezewa thamani hapa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwamba kwenye mpango huu mmesema kwamba mtawekeza zaidi kwenye utafiti kwa kupitia vituo mbalimbali, kwa kupitia COSTECH lakini Vituo vya Utafiti vya Mifugo, yaani TALIRI au TARI kwa upande wa kilimo. Ni vizuri tuongeze nguvu kubwa zaidi katika utafiti kwa sababu hakuna nchi inayoweza kufanya vizuri bila kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile utafiti siyo kwa upande wa kilimo na mifugo tu, kwenye sekta zote; iwe ni afya, hata biashara, kwenye huu Mpango ni vizuri fedha za kutosha ziwekwe, utafiti ufanyike ili tunapotekeleza huu Mpango na tunapopanga bajeti zetu, basi tunakuwa tuna uhakika na jambo ambalo tunakwenda kulifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni muhimu upande wa huduma kwa wananchi, kwa sehemu kubwa ni Sekta ya Maji. Sekta ya Maji hapa kwenye Mpango mmeiweka lakini bado haijapata kipaumbele kinachostahili. Ni vizuri tukaangalia namna ya kuhakikisha kwamba kwa upande wa maji tuweke mkakati na Mpango kuiwezesha RUWASA kupata fedha nyingi zaidi ili miradi ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ambayo ndiyo changamoto namba moja kwa sasa hivi ziweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa Sekta ya Afya, Elimu, kwa Sekta ya Miundombinu, huko kote tumefanya vizuri mno. Sasa cha muhimu ni kuangalia namna ya kuongeza uchumi kwa watu wetu ili wawe na uchumi wa kununua bidhaa. Wakiwa na spending power, Serikali itaendelea kukusanya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia cha muhimu zaidi, badala ya kufikiria namna ya kuongeza kodi tu na mapato, ni vizuri vile vile tuangalie namna ya kupunguza matumizi ambayo siyo ya lazima. Bado kuna maeneo yanatakiwa kufanyiwa kazi ili tupunguze matumizi yasiyo ya lazima ili fedha inayopatikana hiyo hiyo kidogo iweze kufanya kazi kubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Malizia Mheshimiwa Jitu.

MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Njia kubwa ni kwa kutumia force account katika miradi yetu yote.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wenyeviti wote wawili kwa kutuletea taarifa nzuri, lakini pia na kamati kuchambua kazi walizofanya ndani ya mwaka mzima. Ni taarifa ambazo zinatupa dira lakini kuna maeneo ambayo tungependa kuchangia ili kuboresha zaidi ili na wao katika Kamati zao waendee kuishauri Serikali ili kufanya mabadiliko makubwa zaidi na tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia Kamati zote mbili. Moja, naomba nichangia kwa upande wa Kamati ya Bajeti. Nishukuru kwamba taarifa yao kwa sehemu kubwa inaonesha kazi ambazo zilipangwa na ambazo wamefanya, lakini bado naomba niendelee kusisitiza Kamati iendelee kuifanyia kazi sekta nzima ya kilimo kwa mapana yake; kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu ndio inachangia kwa 27% kwenye pato la Taifa, lakini ukuaji wake bado ni 4.3%. Bado ni mdogo sana, tulitegemea sekta ya kilimo ukuaji wake ungekuwa angalau 20% au 30% kutokana na watu wengi kuwa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo yote inatokana na kutokuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo. Pia, siyo kuwekeza tu kwa Serikali au kuweka labda fedha ya kutosha na bajeti zilizopangwa, yaani budget approval na zile disbursed kuendana sawa kwenye fedha za maendeleo, lakini bado kuna changamoto nyingi ambapo Kamati hii ya Bajeti pamoja na Kamati ya Uwekezaji inaweza kutusaidia kwa kuhakikisha kwamba ile blueprint for regulatory authorities yaani reforms zile ziletwe haraka, kwasababu kwa mwendo tunaoenda, bado itatuchukua labda miaka mitano au kumi kufikia huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo hakiwezi kukua kwa sababu bado kuna kodi, tozo na ada nyingi sana ambazo zinazuia sekta hiyo kukua. Tunaondoa kitu kimoja kwa mwaka wakati ilitakiwa viondolewe vitu zaidi ya 50 au 60 ambavyo itafanya Sekta ya Kilimo kukua sana. Moja kwa wale ambao ambao wamesajiliwa kwenye sekta ya kilimo ni kuwa rasmi (formal sector). Wale ambao wana kampuni wanalipa kodi, ada, tozo nyingi sana ambapo yule ambaye hajasajiliwa (informal sector) halipi chochote zaidi ya ushuru; kama ni ushuru, ni ushuru wa mazao. Hiyo inafanya wengi waondoke kwenye formal sector na kurudi kwenye informal sector.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye taarifa nzima utaona Sekta ya Kilimo, kwa mfano horticulture ambayo inaingiza zaidi ya dola milioni 680 kwa mwaka, hiyo bado hujajumuisha mboga mboga na matunda ambayo yanauzwa humu nchini ambayo ni zaidi ya mazao mengine yote au bidhaa yoyote nyingine yoyote inayozalishwa nchini, lakini sekta hiyo inachukuliwa kama ni sekta isiyokuwa rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili sekta hii iweze kuwa na nguvu zaidi, ni vizuri zile kodi, tozo, ada na ushuru mbalimbali ambazo ndiyo kikwazo zingeendelea kuondolewa. Nami napendekeza, ili tuendelee kuwa vizuri kwenye umwagiliaji, mitambo ile ya kuchimba mabwawa ya maji ingeondolewa kodi, kwa sababu bidhaa wanayozalisha huwezi kutoza kodi ya VAT. Kwa hiyo, wale wakileta hawapati ile exemption kutokana na mitaji (Capital goods). Kwa hiyo, bado kwa wao hiyo kodi inakuwa ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sekta nyingine, kwa mfano, ya madini au ya viwandani, akileta hiyo bidhaa wao hawajali. Wanalipa hiyo kodi kwa sababu au watapata hiyo exemption on capital goods kwa sababu bidhaa zao ziko vatable watasamehewa. Sasa kwenye Sekta ya Kilimo, hiyo haipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumesamehe kwa mfano kwenye majokofu, kwenye cold rooms kwa ajili ya horticulture, lakini tungeenda mbali zaidi, hiyo hiyo gari ndiyo inatumika kwenye maziwa na samaki. Kwa hiyo, wangeangalia kwa mapana yake. Ni vizuri Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo, Wizara Mifugo zote zikae pamoja na kuangalia kwa mapana yake. Pia nyingine hazipo Wizara ya Fedha. Unakuta tozo na ada mbalimbali zipo katika taasisi mbalimbali kwa mfano OSHA iko sekta nyingine, fire, yote haya wanalipwa kwenye Sekta ya Kilimo. Ndiyo maana hata tukiondoa kodi yote kwa upande wa Wizara ya Fedha ikawa sifuri, bado hizi nyingine zikitozwa bidhaa ya nje bado itaendelea kuwa bei rahisi na hatutaweza kuendeleza kilimo hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri kwenye Sekta hii ya Kilimo na Mifugo Serikali ingekaa na Wizara nyingine zote wahakikishe kwamba ile blueprint for regulatory authorities, ile reform ifanyike haraka; na kwenye bajeti hii tunatarajia itakuja vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali iangalie kwamba watakuwa wanapata indirect taxes. Siyo lazima upate direct tax, tuangalie indirect tax ambayo itafanya Serikali ipate mapato makubwa zaidi na huduma kwa wananchi itaongezeka sana. Vile vile coordination baina ya Wizara moja na Wizara nyingine zote, jambo hilo pia lazima lifanywe vizuri na ninaamini Kamati hii ya PIC inaweza ikatusaidia kwa kuunganisha pamoja na Kamati zote ili chini ya Waziri wa Uwekezaji, jambo la uwekezaji wa ndani na wa nje yote iende sambamba

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi pia kwa upande wa uwekezaji, nashauri kwa mfano kwenye shirika letu, kama tulivyopendekeza Serikali iwekeze, tunaipongeza kwamba TTCL sasa inafanya vizuri, lakini mngeiongezea mtaji wa kutosha. Kwa sababu leo kampuni binafsi ambayo wanachukua data kutoka TTCL na kuuza kwa wateja ambao ni raia wa kawaida, ni vizuri TTCL pia ingepata mtaji wa kutosha nao waendelee kusambaza mawasiliano, data pamoja na voice ili iweze kuwa na nguvu kama tulivyosema kwa upande wa NIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingi ambazo ziliunda haya mashirika zimepitwa na wakati. Ni vizuri zingeangaliwa upya ili zifanyiwe marekebisho ili mashirika haya pia yaweze kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa lakini pia wananchi kuendelea kupata huduma vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo, kama nilivyosema kule kwenye Sekta ya Kilimo, ni vizuri tukaangalia bajeti ambayo imekuwa approved na bajeti ambayo inakuwa disbursed bado haijakaa vizuri. Ni muhimu wakaangalia nini kitapunguza gharama ili uzalishaji wa ndani uweze kukua na viwanda vya ndani viweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiagiza viwanda vidogo vidogo ya vya thamani ya shilingi milioni 10, 20 au 30, vinatozwa kodi kama kawaida na wakati wa kuingiza hawapati ule msamaha wa capital goods ambayo ingesaidia viwanda hivi vidogo na Watanzania wengi wangeweza kuwekeza huko kwa sababu umeme umeenda katika maeneo mengi, pongezi kwa Serikali. Hiyo ingetusaidia kuwa na viwanda vidogo ambapo bidhaa zinazoenda viwandani zingekuwa zinatoka kwenye sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na ingetusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine muhimu ambalo Kamati inaishauri Serikali ni suala hili la informal sector na formal sector. Leo hii tumeona informal sector inaendelea kukua na hiyo ni kutokana na kwamba formal sector ndiyo wanakamuliwa, wanatozwa kodi, ada, tozo na ushuru mbalimbali ambayo inawafanya wengi sasa kukata tamaa na wengi sasa wanarudi kuwa informal sector. Lengo la Serikali ni kuwa na formal sector ambayo ni strong.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuwaandikisha hawa walipa kodi kuongeza wigo ni muhimu sana kwa sababu wengi wakilipa, Serikali itaweza kupunguza kodi na ushuru mbalimbali ili jambo hili liweze kufanikiwa. Ombi langu ni kwamba Serikali ikubali kuunda taasisi moja, Tanzania Regulatory Authority ambayo taasisi zote hizi zitakuwa chini yake ili sasa mfanyabiashara alipe mara moja halafu sasa huko ndani wanagawana ili tuweze kudhibiti watu kwenda kudai fedha na kupiga faini za ajabu ajabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba nishukuru na kupongeza Kamati zote mbili kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na kwa kunipa fursa siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri Mheshimiwa Lukuvi kwa kazi nzuri na inayoendana na wakati, lakini la muhimu kwa kuwa muwazi kabisa. Sifa yake imemtangulia. Pia nimpongeze Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzuri kwa kazi nzuri na kurudisha matumaini ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri maeneo machache ili kuboresha huduma hiyo ya Wizara. Ardhi ndiyo kila kitu, hakuna jambo linaloweza kufanyika bila ardhi, uwazi katika kazi ya Wizara ndiyo mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwanza Wizara iangalie namna ya kudhamini Halmashauri zetu kupata vifaa vya kupima ardhi na kuandaa hati za kimila. Maeneo mengi nchini ujengaji holela unaendelea kwa sababu ya uwezo wa Halmashauri zetu kutokuwa na vifaa vya kisasa vya kupimia viwanja na miji pamoja na mashamba. Pia vifaa vya ofisini ili kuwa na uwezo wa kutoa hati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itafanya tupate hati kwa wakati na pia kuongeza mapato ya tozo la ardhi (land rent)kwa kila mtumiaji.
Pia naomba nishauri Wizara iweze kutumia mfumo ule wa kutumia satellite imaging kwenye hati. Pia elimu zaidi itolewe kwa umma juu ya satellite imaging ili kuondoa fidia Serikali inayolipa bila sababu kwa wanaojenga maeneo tunapotaka kujenga miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze jitihada ya Wizara kumaliza mgogoro. Naomba iunde sheria ya kulinda ardhi ya kilimo bila ya kuwa chini ya mikono ya Halmashauri zetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuchangia Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya, nimpongeze Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri na pia kwa uteuzi wa viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Nimpongeze Waziri Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe na Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Ramo Makani na Katibu Mkuu - Meja Jenerali Gaudence S. Milanzi kwa kuongoza Wizara hii nyeti na maalum katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika baadhi ya maeneo na kushauri kutokana na maoni yangu na mengine ya kutoka kwa viongozi wa Wilaya na Mkoa wetu wa Manyara. Niombe Wizara ya Maliasili na Utalii isaidie Halmashauri zetu ambazo zina hoteli za kifahari na camp sites ambazo kisheria wanatakiwa kulipa ushuru wa huduma (service levy) asilimia 0.3 ya mapato yao hadi leo wamekataa na walienda mahakamani na kushindwa kesi, wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Mapato mengi tunapoteza na hasa Halmashauri zetu zinazotegemea mapato hayo. Wizara inaweza kukaa na chama cha wenye Hoteli Tanzania (HATS) na kuleta suluhisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika WMA nyingi tunapokusanya mapato ya utalii, fedha hizo ambazo hugawanywa kwenda Taifa, Halmashauri na vijiji husika WMA huenda baada ya kukusanywa katika WMA zetu na kupelekwa hadi Taifa, baada ya hapo hurudishwa chini tena. Tunaomba zile za Halmashauri na WMA zibadilishwe na gawio la Taifa ndiyo pekee liende.
Tatu, leo ni mwaka wa tatu, kifuta jasho na kifuta machozi wananchi wa Babati hawajalipwa pamoja na kufuatilia Wizarani mara kadhaa nikiwa na Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri hadi leo shilingi milioni 12 tu kati ya hizo zimelipwa. Nashauri badala ya Wizara kupitia kitengo cha wanyamapori kulipa hizo gharama za kufuta machozi na vifuta jasho, hifadhi husika mfano, TANAPA, Ngorongoro Conservation Authority ndiyo walipe. Tubadilishe sheria yetu ili malipo haya yaende kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, naomba miradi ya kusaidia vijiji vinavyopakana na hifadhi zetu mfano, TANAPA, NCA, KINAPA ziwe zaidi ya kulenga mtu mmoja mmoja katika miradi ya kuwaongezea mapato. Wakiwa na uchumi mzuri basi wao wataweza miradi ya sasa kwa mfano, ujenzi wa madarasa, mabweni, zahanati na wataalam wamenufaika moja kwa moja, watu kuwa walinzi wazuri na watetezi wa hifadhi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, tunashauri matokeo ya Tume ya Kimahakama au Kijaji kufuatilia suala la mauaji ya Operesheni Tokomeza yatolewe mapema. Imani ya wananchi kuwa sheria itachukua mkondo wake na haki itendeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, tunaomba suala la vijiji vya Ayamango, Gedemas na Gidejabung, Wilayani Babati sasa vipatiwe ufumbuzi wa kudumu. Wananchi waliopewa ardhi hiyo kisheria na baadaye kujikuta wako ndani ya Hifadhi ya Tarangire. Aidha, walipwe fidia ya ardhi, wapewe fedha ili wajitafutie ardhi wenyewe. Wapatiwe ardhi mbadala na kama haiwezekani wapewe hiyo ardhi yao waliyotumia miaka zaidi ya 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, eneo la Tarangire na vijiji vya Ayamango, Gedemas na Gedejabung wapewe wafugaji kwa malisho kwa mkataba maalum. Miundombinu ya josho na malambo yawekwe, idadi maalum ya mifugo iruhusiwe hapo (carrying capacity) na wachunge kwa miezi sita, Januari hadi Juni na kutoka Julai hadi Disemba mifugo irudi vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, eneo la kisheria la Burunge Game Controlled Area na zingine kama hizo zifanyiwe marekebisho yanayoendana na wakati. Leo hii kuna vijiji na miji mingi kutoka Manyoni, Minjingu, Mdorie, Magugu, Mamire, Galapo, Kash hadi maeneo ya Kondoa yapo humo, kisheria imekaa vibaya na itaweza kuleta athari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tisa, Tanzania Forest Service Agency inakusanya mapato mengi yanayotokana na maliasili ya misitu, magogo, mkaa, mbao, nta, asali na kadhalika. Kwa mwaka takribani bilioni 45 hadi bilioni 50, lakini hakuna fedha hata kidogo inayoenda kupanda miti na kurudishiwa pale palipovunwa. Nashauri asilimia 30 ya mapato hayo yaende kwenye Mfuko wa Taifa wa Mazingira ili itumike kupanda miti, kuboresha upatikanaji wa mbegu za miti mbalimbali na utoaji wa elimu kwa jamii. Taasisi ya Taifa ya Miti (National Tree Centre) pia wana hali mbaya kifedha hii michango itaweza kusaidia kueneza elimu na mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumi, nashauri uwindaji wa kitalii upigwe marufuku kwa muda angalau miaka kumi ili wanyamapori wetu waweze kurudi kama zamani. Nashauri hadi kwenye zana na vifaa vya ufugaji wa nyuki na kusindika asali iondolewe ili kukuza sekta hii na kupata viwango vizuri (quality).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumi na mbili, tozo mpya ya maliasili kwenye vinyago katika viwanja vya ndege iondolewe.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia siku siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya. Pia nipongeze taarifa za Kamati zote mbili; mimi ni mjumbe wa Kamati ya Kilimo, Maji na Mifugo, nimpongeze Mwenyekiti wetu na Kamati nzima kwa kazi kubwa na nzuri na ushirikiano mzuri na mkubwa ambao unafanywa na Wizara ambao tunazisimamia. Pia nishukuru Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa taarifa nzuri na kazi kubwa ambayo wamefanya na mabadiliko yote tumeweza kuyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika badhi ya maeneo. Nikianza na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utlii; naomba nitoe maoni machache ambayo yangeweza kuboresha shughuli, najua Kamati itaweza kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kuna sheria mbalimbali ambazo tumepitia na tumefanya semina mbalimbali pamoja na Kamati hiyo, sheria ambazo zinakinzana kwenye sekta nzima ya ardhi, maliasili na utalii; kuna sheria za maliasili, lakini pia kuna sheria za ardhi na sheria za mifugo. Ziko sheria tumezibainisha ambazo zinakinzana na hiyo ndiyo unaleta changmoto kubwa na ndiyo inasababisha migogoro mingi. Tukiweza kuziweka vizuri sheria hizi na zisiwe zinakinzana naamini migogoro mingi itakuwa imepungua.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, napendekeza kwa upande wa National Haousing, sehemu kubwa siku za nyuma walikuwa kazi zao nyingi wanazi-outsource. Ni vizuri kila jambo wangekuwa wanafanya in house, kwa mfano kutengeneza madirisha ya aluminum wangekuwa na kiwanda chao wenyewe, kama ni kufyatua blocks wafyatue wenyewe yaani shughuli nyingi ziwe in house badala ya kuwa outsource ambapo gharama inakuwa kubwa na faida ndogo. Kwa hiyo, wakifanya kazi nyingi bei za nyumba zitapungua sana na wataweza kuwauzia Watanzania nyumba ambazo zitakuwa na gharama nafuu. Kwa hiyo, hilo jambo ni muhimu kwa upande wa National Housing. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa upande wa migogoro mbalimbali ya ardhi, tungeomba sasa Kamati itusaidie. Yale yote ambayo Tume iliyoundwa na Mheshimiwa Rais wetu kumaliza ule mgogoro basi yafanyiwe kazi sasa na vile vijiji vitangazwe rasmi ili ile hofu na wananchi kuishi bila kujua hatma yao haswa katika vijiji kwa mfano Jimbo la Babati kuna Vijiji vya Ayamango, Gedamar, Gedejabong na eneo lile ambalo lina tatizo kubwa la WMA basi ingewekwa wazi ili kila mmoja ajue ni nini kimetokea. Jambo hilo likifanyiwa kazi naamini kabisa kwamba migogoro mingi itaisha. Pia kwenye Land Use Plan basi tuweze kuangalia ushirikishwaji katika maeneo mengi ya sekta mbalimbali ili ziendane kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, napendekeza kamati itusaidie, matumizi ya ardhi yanabadilika kila siku na hasa leo tunaangalia Mji kama wa Dodoma, kuna mashamba yako ndani ya Mji huu wa Dodoma hasa ya zabibu na nchi nyingi duniani zinakuwa na mashamba ndani ya miji. Ni vizuri hii sheria ikawekwa la sivyo tutajikuta mashamba yetu ya zazibu ambayo ni eneo pekee Tanzania ambalo tunaweza kupanda zabibu ya uhakika na ambayo ina sifa kubwa duniani itatoweka. Kwa hiyo, jambo hilo pia lizingatiwe, Land Use Plan kwenye miji pia izingatie kulinda mashamba mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija pia kwenye utalii, naomba Serikali kwa kupitia Kamati ishauri, najua maoni hayo tuliwaletea na mmeyafanyia kazi, lakini kwenye hii bajeti tunayoelekea maeneo mengi, hasa katika maeneo ya hifadhi ambayo yanaingiza fedha za kutosha ambapo zinalisha hizi hifadhi nyingine hasa kwa mfano Tarangire, kuna barabara tatu zinazoingia zingetengenezwa. Tumeomba kwa muda mrefu sasa barabara ile ya Minjingu kuingia getini, ile ya Kibawa Tembo kwenda Sangaiwe na ile ya Babati Mji kwenda kule Mamire zote zingetengewa fedha ili kukuza utalii katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Spika, pia Kamati iweze kusaidia kuangalia miradi mbalimbali ambayo inachangiwa na hizi hifadhi katika jamii isiwe miradi ambayo kwa mfano ya kujenga shule au ya kujenga zahanati na kadhalika lakini waangalie mahali ambapo wanaweza kuchangia miradi ambayo itanyanyua uchumi wa watu ili watu wakishakuwa na uchumi mzuri wao wenyewe watajenga hizo zahanati na shule. Kwa hiyo, iwe ni miradi ambayo itanufaisha wananchi wanaokaa jirani na hizi hifadhi. Pia, nipongeze kwamba mahusiano sasa yamekuwa mazuri sana baina ya hifadhi nyingi na wananchi wanaozunguka na usimamizi umeendelea kuwa mzuri.

Mheshimiwa Spika, nikirudi sasa kwenye sekta ya kilimo, niipongeze Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanafanya, lakini pia Wizara ya Maji ambayo Kamati yetu inasimamia. Nishukuru kwamba wamekubali lile ombi letu la kufanya miradi mingi kwa kupitia Force Account. Tumeona Force Account imekuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya elimu na sekta ya afya. Sasa hivyohivyo tukitumia kwenye sekta hii ya maji, nina uhakika kwamba tutaona mafanikio makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi letu kwa kupitia Kamati ni Serikali wakati tunapokuja kwenye bajeti iweze kuondoa kodi kwenye mitambo ya kuchimba maji, mitambo ya kuchimba mabwawa, ili badala ya Serikali kutegemea bajeti yetu ndogo basi sekta binafsi iweze kufanya kazi hiyo. Leo hii bidhaa nyingi ambazo zinatokana na sekta ya kilimo hazina VAT kwa hiyo, hawapati ule msamaha wa capital goods kwa sababu bidhaa zao hazina VAT. Wakiondoa hilo katika sekta ya kilimo watu wengi wataweza kuleta hii mitambo na kutengeneza mabwawa wenyewe na kuanzisha miradi ya umwagiliaji ambayo itakuwa ni kilimo cha uhakika zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini muhimu zaidi ni maoni ambayo pia Kamati imeiomba Serikali na nasisitiza kwamba ilete ile Sheria ya Blue Print Regulatory Reforms mapema kwa sababu bila hiyo sekta nzima hii ya kilimo itaendelea kuwa na changamoto. Tumeainisha kwenye ripoti yetu utaona ada, tozo, ushuru na kodi nyingi kwenye sekta moja tu ndogo ya horticulture hivyohivyo iko katika karibu sekta nzima ya kilimo na mifugo, kuna utitiri wa kodi na tozo na ada mbalimbali ambazo zinafanya bidhaa zetu zinakuwa ghali kuliko bidhaa zinatoka nje. Tunaendelea kuishauri Serikali kwamba ni vizuri bidhaa ambazo tunaagiza kutoka nje kwa mfano matunda na mboga ambazo tuna uwezo wa kuzalisha nchini basi Serikali iweze kuwekeza zaidi. Sehemu kubwa tunachohitaji ni kuwa na mazingira rafiki, siyo lazima Serikali iwekeze fedha, wakiweka mazingira wezeshi basi sekta binafsi itaweza kuchukua fursa hiyo na kuifanyia kazi ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na kuzalisha ndani ya nchi na kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, hivyohivyo kwa upande wa mbegu tumeona asilimia 60 ya mbegu tunaagiza kutika nje ya nchi. Ni vizuri sasa Serikali iangalie namna ya kupunguza gharama mbalimbali ambazo zinafanya uzalishaji wa mbegu hizo hapa nchini kuwa wa chini ili tuzalishe wenyewe hapa nchini na fursa hiyo ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu ni kwamba sekta hii ya kilimo inakua kwa asilimia 4.5 ingawa ni sekta ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania lakini kwenye bajeti haipewi umuhimu wake. Tunaomba tuangalie namna ya kuongeza bajeti angalau ifikie asilimia 10. Ndiyo tunakubali kwamba Serikali inasema miradi yote ambayo inatekelezwa mjini iwe ya elimu, afya, maji, barabara, miundombinu, nishati, yote hiyo inachangia kwenye sekta ya kilimo lakini ukichukua budget approved na Bunge na budget disbursed kwa upande wa maendeleo huko vijijini bado haifikii asilimia 10.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri ile asilimia 10 ili iweze kufikiwa yote hiyo, tunakubali ni sekta ya kilimo na mifugo kwa mapana yake, ni vizuri budget disbursed ambayo tunapitisha hapa Bungeni, ile approved basi ilingane na asilimia 10 tutaona maendeleo huko kwenye sekta ya kilimo. Kwa sasa hivi bado haijafikia iko kwenye asilimia 8.2, ni vizuri tukahakikisha kwamba hiyo miradi yote tunayosema iko vijijini bajeti hizo ziende kwa sekta zote tutaweza kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwa upande wa maji tungeomba Serikali iangalie namna ya kuboresha. Kuna mitambo ya kusafisha maji, water purifiers, wangeweza kuondoa kodi ili gharama za kupata maji safi na salama vijijini iwe ndogo. Pia solar water pumps zikiondolewa kodi watu wengi zaidi watapata maji safi na salama na bajeti kwa upande wa afya ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa magonjwa yanayotokana na maji itapungua na watu watakuwa na afya njema na Watanzania wengi wataendelea kupata maji. Serikali inafanya kazi kubwa na nzuri, lakini hizi reforms tunahitaji ziende kwa haraka zaidi kwa wakati mmoja ili tupone haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, naunga mkono hoja moja kwa moja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kunipa fursa ya kuchangia leo lakini nitumie fursa hii kwa kuzipongeza Kamati zote tatu kwa kuwasilisha report ya Mwaka ambayo imeeleweka vizuri sana na tumeona maoni yao na tunaunga mkono kwa asilimia kubwa maoni yao waliyotoa lakini kuna baadhi ya meneo ningependa kuchangia ili tuweze kuboresha vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; nilikuwa naomba Kamati ya Sheria Ndogo lakini pia Kamati ya Sheria wakati wanapofanya mapitio katika Sheria mbalimbali kwa sababu sasa tunatumia teknolojia basi wawe wanaweza kuweka na Bunge liangalie utaratibu wa sisi kupata hizo Sheria mbalimbali wanazopitia kwa sababu kipindi wao wanapitia Sheria hizo na Kanuni na sisi tuko kwenye Kamati zingine tunafanya shughuli zingine. Lakini kama kuna eneo ambalo ninahitaji kuja kuchangia basi niweze kujua ni lini itakuwa ni sehemu ya kupatia taarifa vizuri niweze kupitia hizo Sheria lakini ombi langu moja na nimekuwa nikilisema mara nyingi Bungeni; Sheria zote ziwe online ambazo ziko updated, Sheria na Kanuni. Leo tukitaka kufanya marejeo yoyote hizi Sheria ni ngumu kuzipata na nyingi haziko updated kwenda na wakati lakini pia Kanuni mbalimbali pia zote ziwe updated, ziwe online ili iwe rahisi kwetu sisi kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na moja katika mifano naweza kutoa; kipindi nimehangaika kuleta hapa Sheria ile na kuleta kwenye Kanuni, suala la force account tulichukua miaka minne kwa sababu kupata tu nyaraka zile mbalimbali hazikuwepo. Nimshukuru Mheshimiwa Chenge kama siyo yeye, bado hili jambo la force account ingekuwa bado ni ndoto kwetu na yeye amesaidia kutoa kwenye archive yake zile document na leo sifa kubwa ya mafanikio ya Serikali yetu ni kwa kutumia force account.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lingine ni suala la upande wa uwekezaji kwa Waziri wa Uwekezaji pamoja na timu yake; wanafanya kazi kubwa na nzuri lakini bado naona kuna Sheria mbalimbali ambazo zinawapa ugumu wa kufanyakazi. Leo siyo kweli kwamba ni one stop center, bado changamoto ziko nyingi. Leo vibali vingi ambavyo viko pia TIC, kwa kupata tu vibali vile vya muwekezaji wa class A hatuzungumzii yule mfanyakazi ni nani lakini yule wa Class A tu bado inasumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu amewekeza ana jengo lake lina thamani labda ya ghorofa 10 lakini baada ya miaka miwili au mitatu kupata ile Class A anahangaika kupata ile permit ya labor, bado aende kule kupata resident permit sasa mngeunganisha na ingekuwa rahisi kwamba mtu amewekeza hivi yule ukimnyima permit, hiyo mali yake inakwenda kwa nani? Lakini mbali na hilo, kuna biashara nyingine nyingi tu ambazo zimeendelea kufungwa na zimeendelea kudorora kutokana na watu kunyimwa vibali.

Leo kwa mfano; kwenye sekta ya hotel; unapomnyima mpishi wa aina mbalimbali kama ni Mchina au kama ni M-mexico unapowanyima vibali na wale watu wanakwenda kula pale kutokana na aina ya yule mtu kufanya hiyo kazi, unapomnyima kibali leo chakula kinapikwa na Jitu ambaye hajui kupika chakula Kichina kweli ni jina tu la Kichina lakini ile ladha na nini haipo. Tuangalie kwamba wale wakiwepo biashara kiasi gani inaongezeka na tunayo mifano mingi tunaweza kuwapa biashara zilizofungwa, kudorora kabisa kwa ajili ya watu kunyimwa vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya TIC inasema vile vibali vitano vya mwanzo yaani hamtamuhoji yule Muwekezaji kwa sababu hata akileta Ndugu yake, amemleta pale ili asimamie kwa ajili ya imani na kuwa na uaminifu na yule Mtu. Sasa tunapoanza kuhoji mambo mengine ya kwamba je, hiyo kazi inaweza kufanywa na Mtanzania na haiwezi kufanywa kwenye uaminifu hakuna cha Utanzania hata mimi na Ndugu yangu wote Watanzania hatuaminiani kwa hiyo inaweza kuwa Mtu mwingine ambae ninamuamini anaweza kuwa anasimamia ile mali kuliko Ndugu yangu ambae anaweza kunirusha sasa ni vizuri haya mambo tuyaangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huko zamani kwenye incentives kulikuwa na mambo mengi leo hayo yote hayapatikani. Kwa mfano; tukitaka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo na ndiyo hiyo katrika kila mchangu wangu hapa naisemea. Leo sekta ya kilimo bidhaa yake yote siyo veritable kwa hiyo sisi tukitaka exemption kwenye capital goods hatuwezi kupata hata tukiwa kwenye TIC hatuwezi kupata kwa sababu VAT on deferment bidhaa zetu hazipo veritable kwa hiyo tunanyimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ya pili; unaambiwa ni lazima VAT kiwango kile kiwe ni milioni 10 na kuendelea. Milioni 10 ina maana ile bidhaa ni zaidi ya milioni 50 sasa capital goods kwa Watanzania ambao wanaanzisha viwanda vidogo vidogo kama haikufika hiyo milioni 10. Je, hawana haki ya kupata hiyo VAT on deferment hata kama bidhaa yao iko veritable? Kwahiyo, Sheria hizo zinafanya watu wengi wanaona kama TIC ni sehemu tu nyingine ya kupata vibali vingine vingi zaidi. Ni vizuri lengo la kuanzisha TIC, lengo la kuanzisha Wizara ya Uwekezaji ni kuangalia mahali tuwe na one stop center na sisi tukisema mbali na TIC, local content ni wangapi wamewekeza Watanzania TIC? Ni vizuri pia Watanzania wa kawaida wajue fursa zilizopo ili na sisi wengine ambao ni Watanzania tupate hizo fursa kupitia hizo incentives za TIC na tuweze kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine naomba nichangie kwa upoande wa Serikali za Mitaa, kwa upande wa TARURA; ni vizuri tungeendelea namna ya kuongeza bajeti ya TARURA lakini pia Waziri akae, TARURA ni agency inayojitegemea pamoja na TANROADS lakini matatizo mengi tunayoyapata barabarani sasa hivi katika barabara za vijijini ni matokeo ya athari za kujengwa kwa barabara za TANROADS.

Sasa ni vizuri wale wawili wakae kwa pamoja ili waweze kutatua na kusaidia katika kuboresha amzingira mbalimbali huko chini lakini TARURA mngeruhusu kazi nyingi angalau isiyozid milioni 200 zifanywe kwa mfumo wa force account. Force account leo hii barabara inayopangiwa milioni 30 au 40 huko kijijini itachongwa kilometa mbili au tatu, Morum wataweka mita 500 na labda kujenga culvert moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia force account tunaweza kutengeneza Kilometa 10 yote iliyojazwa vizuri kwasababu kukodisha mitambo yote kwa siku moja haizidi milioni tisa. Sasa tukienda kwa mfumo huo kwa force account, barabara nyingi amabzo ni za milioni 30 tutaweza kutengeneza sehemu kubwa na hasa kipindi hiki ambayo karibu barabara zote zimeharibiwa na mvua, kwa kutumia force account tutaweza kutengeneza barabara nyingi zaidi huko vijijini kwa hiyo, nilikuwa naomba muiruhusu TARURA kwa kipindi hiki iweze kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo lingine ni vizuri suala la blueprint, ili uwekezaji uendelee kukua wa ndani na wa nje, blueprint bidhaa ya Kitanzania kama isipokuwa na bei ambayo itakuwa ya ushindani ndani na nje, bado bidhaa za nje zitaendelea kutawala ndani ya masoko yetu. Ni vizuri suala hili lisije kidogo kiodgo, lije kwa wakati mmoja ni sawa na mtu ukitaka kupona malaria lazima uchomwe sindano ya Quinine, hivyo hivyo itakuwa na madhara mengi, mapato yanaweza kushuka kwa mwaka mmoja lakini long run tutakuwa na mapato mengi zaidi na ajira kwa watu wengi zitaongezeka kwa hiyo jambo hili la blueprint ninaomba sana lifanyiwekazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Utawala Bora; nilikuwa naomba nikushauri kwamba Kamati iendelee kusisitiza customer charter iendelee kuhimizwa katika Idara zote, katika Taasisi zote za Serikali ili kila mmoja aweke wazi customer charter yake. Lakini humo humo nilikua naomba sasa tumeingia kwenye mfumo wa kidigitali na kielektroniki, kila mtu anapopeleka barua au nyaraka apewe risiti ya kielektroniki ya ku-acknowledge kwamba barua tumepokea tarehe hii na nyaraka fulani ili haya mambo ya kusumbuana Mwaka mzima hupewi majibu hayatakuwepo, mtu unakuwa na ushahidi kwamba vitu vyangu vimepokelewa na yote haya ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi uwe na ushahidi kwa sababu unaweza kuacha barua baada ya mwaka unaambiwa barua yako haijulikani mahali ilipo zaidi ya wewe kusainiwa kwenye kile kitabu chako ambacho siyo ushahidi wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kila Taasisi itoe acknowledgement ya barua au nyaraka ambazo watakuwa wanapokea ili twende na numbering na kila first come, first save ndiyo iwepo. Hiyo ndiyo italeta Utawala Bora na huduma nyingi zitaendelea kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nishukuru, ninaomba Kamati zote zinafanyakazi zao vizuri lakini haya mambo tukiyasimamia vizuri nina uhakika kwamba katika Utawala Bora lakini pia hii ya TARURA itafanya vizuri lakini kwenye uwekezaji hilo ndiyo eneo pekee na ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameunda tena Wizara hii ya Uwekezaji ili kuweza kupata uwekezaji wa ndani na nje na tuweze kupata mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wka kazi kubwa anayofanya lakini ni vizuri semina hizi pia msitutolee sisi Wabunge tu, nendeni mkatoe Wizara ya Fedha kwa sababu changamoto ya Wizara zote ziko Wizara ya fedha. Kwa hiyo, naomba huko Wizara ya fedha mtuite hata sisi tutakuja kutoa hiyo semina tukawasaidia changamoto na experience ambazo tunapata kutoka huko kwa raia na kwa Wananchi kwa sababu ndiyo wawakilishi wao, nina uhakika hizi zote tutaweza kuzitatua na tukapata mafanikio na tusiangalie kupata mapato ya moja kwa moja. Inawezekana usipate direct tax lakini indirectly ukawa unapata mara 10 ya hiyo na ajira kwa Watanzania ikawa ni kubwa zaidi. Kwa hiyo ni vizuri tukaangalia hayo.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Jitu.

MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru wka nafasi uliyonipa, lakini nizipongeze Kamati zote tatu, naunga mkono hoja zote, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na fursa ya kuchangia leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri na pia kwa kuteua viongozi wenye uzoefu katika Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na bajeti ndogo katika Wizara hii, tunashauri Serikali ipeleke fedha kwa wakati ili majukumu yatekelezwe vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ifanye juhudi na kukaa na Wizara zingine (Coordinate) katika kuboresha huduma za Wizara na pia kuongeza fursa ya kiuchumi na kimahusiano ya nchi yetu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri masuala machache ya kuboresha huduma na fursa kwa Watanzania. Kwanza, naomba Watumishi wetu, Waheshimiwa Mabalozi wetu wapatiwe mafunzo ya kiuchumi na marketing namna ya kuitangaza nchi yetu (economic diplomacy), Mabalozi wa nchi nyingi hufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze wachache niliopata fursa ya kukutana nao mfano, Balozi wetu wa China na Netherland, pia wapate uwezo wa kutafuta masoko ya bidhaa zetu na pia tunapohitaji bidhaa huko watupatie maelezo au vielelezo. Ni muhimu Wizara iwe na dirisha la kuhudumia Watanzania wanaotaka kuagiza bidhaa nje na fursa ya kuwekeza nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Tanzania iangalie namna ya kutumia Watanzania wanaoishi nje na waliokuwa Watanzania na sasa ni raia wa nchi zingine kutokana na mazingira diaspora. Nashauri tuwe na pass au utambulisho maalum ambao utawapa fursa waliokuwa Watanzania na sasa raia wa nchi zingine ili warudi kutembelea nyumbani wapate haki zote sawa na Watanzania isipokuwa kufanya kazi za umma (Serikalini), kuchagua na kuchaguliwa mfano, ni nchi ya India. Tuangalie pia hao raia ambao watoto wao pia wawe na hiyo haki, ambapo leo hawana (Persons with Tanzania Origin).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Wizara iboreshe Chuo cha Diplomasia na pia ishirikiane na Wizara ya Elimu kuboresha mitaala na mafunzo ya International Relations. Leo hii wanafunzi wetu wa International Relations hawana viwango kabisa, lugha ni shida, wacha lugha nyingine hata kiingereza ni shida. Vijana wetu wangekuwa wanajua lugha nyingi hata ajira ya ukalimani wangepata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Diplomasia kiongezewe bajeti kuboresha huduma mbalimbali ili wanaotoka au kuhitimu hapa, waweze kupata ajira kokote katika mashirika ya Kimataifa na pia taasisi za ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, tunashauri pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iwatumie Mabalozi wetu kufanya jitihada ya kuunganisha Taasisi za huko waliko ili kuboresha Taasisi zetu. mfano, vyuo kama SUA, Chuo cha Nelson Mandela, vituo vya utafiti mbalimbali, tuwe na Program za kushirikiana (Exchange).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutufanyia semina Wabunge wote juu ya masuala ya Itifaki, namna ya sisi kuweza kufanya mawasiliano na viongozi mbalimbali. Suala zima la kuweka heshima yetu na namna ya kutuwezesha kufanya mawasiliano (Etiquette and Diplomacy) (Manners and Presentation).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na fursa ya kuchangia leo. Nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na timu yake ya wataalam kwa kazi nzuri sana waliyofanya. Naomba masuala machache yafanyike ili kuboresha huduma ya Wizara ya Ardhi inayoendana na maendeleo ya makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jimboni kwangu, Serikali iharakishe kupitia mgogoro wa ardhi ya miaka mingi iliyotutesa na kusababisha migogoro hii kutumika kisiasa wakati wote. Migogoro ya Vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gidejabong na TANAPA Tarangire, Serikali ndio iliweka vijiji hivyo hapo katika eneo la hifadhi. Wapatiwe eneo mbadala na pia shamba la Galapo Estate pia lisitolewe viwanja na badala yake iwe eneo la kuwapa hao wanaondolewa katika hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba suala la mashamba ya Bonde la Kisu, migogoro ya ekari 25. Tunaomba pale mapendekezo ya Wilaya na Mkoa zifanyiwe kazi pia Serikali itoe tamko la kuvamia mashamba na kuharibu mali ya wawekezaji ambayo wana haki na wanatimiza wajibu kisheria. Pia tunaomba ardhi ya kilimo ilindwe kisheria ili matumizi ya ardhi ya kilimo isiweze kubadilishwa bila Bunge kupitisha mabadiliko hayo kuwa ya makazi, viwanda au matumizi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba Wizara iandae program ya kila Halmashauri kupata vifaa vya kupima kwa mkopo pamoja na vifaa vya kuweka kumbukumbu ya hati na vifaa vya kuchapa hati. Kwanza tutaweza kulipa ndani ya muda mfupi. Leo Halmashauri nyingi hawana bajeti ya kununua kwa fedha taslim.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba Wizara ya Ardhi iangalie namna ya kulipia gharama ya matumizi ya satellite. Hii itafanya upimaji kwa ramani iliyopo inakuwa bora na wa uhakika. Leo hii ramani nyingi zina tatizo sababu hawana fursa ya kutumia hiyo huduma ya satellite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pia tuwe na sheria ya kuzuia kuuza kiholela kwa ardhi hasa yenye hati ya kimila ili wenye uwezo wasinunue ardhi nyingi na wasiokuwa na uwezo kukubali kuwa vibarua na mbele ya safari tutakuwa na hatari sawa na Afrika Kusini na nchi zingine kama Kenya ya wachache kuwa na ardhi. Leo kila Mtanzania ana uwezo wa kuwa na ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba Serikali itumie fursa hii kutoa tamko kwa umma na sisi wanasiasa kutumia ardhi kisiasa na kuhamasisha vurugu kwa maslahi ya kisiasa na hasara kwa umma na wamiliki wa ardhi, hifadhi mbalimbali na vyanzo vya maji.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba nichukue fursa hii kwanza kuipongeza Serikali kwa kuleta hii Sheria ya Manunuzi. Mimi kwangu na ninaamini kwa Wabunge wote hii sheria ndiyo sheria muhimu kuliko sheria zote kwa sababu manunuzi yote ndiyo yanaenda kufanywa huko. Hii ndiyo sheria ambayo italeta taswira kwamba uchumi wetu utakua au hautakua, kwa hiyo nawapongeze kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba Waziri wakati mnaandaa kanuni, mjitahidi sana kuhakikisha mnaweka dirisha. Moja, kwenye suala la PPP kwa sababu ile Sheria ya PPP bado inafanyiwa marekebisho ili isije ikawa kwamba mahali ambako Serikali sasa inataka kuingia ubia na private sector acha kwenye hii miradi mikubwa mimi nazungumzia hasa hizi za kwetu za ngazi ya Halmashauri/ngazi za chini ambapo 80% ya maendeleo inaenda huko pawe na dirisha ambapo Halmashauri ikitakiwa kuchangia na sekta binafsi kwamba, wale wadau wa maendeleo pawe na fursa kwamba, Halmashauri ichangie kiasi fulani, wadau wanachangia kama ni vifaa ili kazi zionekane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niendelee kushauri kwamba huko ngazi ya Halmashauri tunakuwaga nasuppliers kwamba, mwanzo wa mwaka tunachagua wale watu ambao watakuwa wanatoa huduma kumi ambao watakuwa wana-supply kwenye Serikali, naomba hiko kifungu kiondolewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila tender inapotoka au kila tunapotaka kufanya iwe wazi yeyote yule ambaye anataka kuingia kwenye huo mfumo wa kuomba kutoa huduma au kufanya kazi waruhusiwe kwa sababu inawezekana kipindi fulani Januari mnachagua watu kumi mwezi Machi tayari sasa dira au yule mtengenezaji akaweka godown yake pale kwamba unaweza kununua moja kwa moja kwa bei ya kiwandani kwa mfano kwa cement yaani agent wake akawa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ni vizuri kwenye vikundi vidogo vidogo ambavyo havijasajiliwa kuwe na dirisha sisi tutaenda kuhamasisha vikundi vijisajili hata kama ni wale wamama wanaouza sokoni basi wawe na mashine yao moja ya EFD. Yeyote anaye-supply pale risiti ikitoka pale sokoni ili zile supplies na wale wapate riziki ambayo wanastahili kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu leo hii wanao-supply chakula, wanao-supply bidhaa ndogo ndogo katika hizi tender ndogo ndogo unakuta gharama ni kubwa sana wakati tungeweza kupata kwa bei ya chini. Yule mtu wa chini hapati kwa sababu hajasajiliwa, ni muhimu sasa twende kuwashawishi waendelee kusajiliwa ili na wao wapate fursa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini muhimu nyingine kwenye suala la standards; kila Wizara unakuta inakuwa nastandards zake, Wizara ya Mambo ya Ndani inaruhusu kujenga majengo yao kwa hydraform blocks, lakini Wizara ya Elimu ukitaka kujenga darasa kwa hydraform blocks hairuhusiwi wanakuwa na standards zao. Sasa tungekuwa na uniform standards kwamba standard moja kwenye Serikali ikikubalika kote basi iendelee kukubalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nilikuwa nashauri yale maoni yote ya Kamati ya Bajeti basi pia yachukuliwe kwa uzito wake na pawe na special provisions kwa zile public entities ambazo zinafanya biashara competitive business kwa mfano TTCL na nini muiwekee special provision kwamba wao pia wakitaka kufanya manunuzi basi wasifate ule mlolongo wa kawaida ni ili taasisi zetu zifanye kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye life saving health commodities and equipment nilikuwa naomba hiyo iwekwe. Lakini pia kwenye kile kifungu cha kununua vifaa vilivyotumika ambapo tuna ndege, meli na reli lakini viongezwe vifaa vya afya hizi life saving health commodities. Kwa sababu kuna vifaa vingi vya tiba ambavyo ni used kwa mfano vitanda vya akina mama kujifungulia. Hata ingekuwa kimetumika mara ngapi bado ile kwetu kijijini itaweza kuokoa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya vifaa ambavyo sio electronic basi vile vifaa baada ya kupitishwa na Waziri husika viruhusiwe kununuliwa ikiwa used pamoja na vifaa vya kilimo. Kuna vifaa vingi sana vya kilimo ambavyo Serikali kwenye mashamba yake ambayo tunataka kuanzisha uzalishaji wa mbegu.Wanaweza kununua vifaa vingi ambavyo ni used kwa mfano ma-rippers na nini. Bei yake mpya ni dola 65000 ya used unapata hata dola 10,000; sasa pawe na dirisha kwa vifaa vile ambavyo havina mwisho katika maisha yake basi viruhusiwe kununuliwa vifaa ambavyo vimetumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ningeshauri kwamba tuangalie katika kanuni, muhimu kuliko yote manunuzi yote nimeona katika sheria hii ya Halmashauri zetu zinaenda kule kwenye kanuni. Sasa wakati wa kanuni tutaendelea kumuomba Waziri, sisi tutaendelea kuleta input zetu ili ziweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninaomba ombi lingine kwa Serikali, naomba hii sheria tukiipitisha mwakani muirudishe ili ndani ya huu mwaka mmoja haya majaribio yote tunaenda kufanya, mapungufu yote ndani yamwaka mmoja tuje tuzibe ile mianya yote, tusije tukakaa miaka minne kama tulivyofanya 2011, tukarudia mwaka 2014 mwishoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kila wakati tukiweza kurekebisha ninaamini huku tunakotarajia kufika tutaweza kufika. Muhimu kuliko yote pia ni kuangalia namna wakandarasi yaani Watanzania wanaweza kushiriki katika manunuzi iwe katika nanii kubwa au ndogo. Ninashukuru kwamba Serikali imekubali kwamba, hata katika ukandarasi mahali ambapo wanatakiwa kwenda kufanya tathmini na nini kuna namna ambapo watu wetu wa ndani wakishiriki basi na wao watakuwa wanapata fursa ya kupata ile elimu na fursa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye Halmashauri naomba muendelee kuangalia kwa mfano kama TEMESA magari yetu yanatakiwa tupeleke pale kutengeneza. Kama tunaweza kutengeneza kwa bei nafuu hapo hapo ndani ya mji huo sisi tufanye quotation TEMESA ikiwa juu kuliko hao basi turuhusiwe kupeleka kwingine ili na TEMESA wafanye kazi yao iwe competitive. Nanii yoyote isiwe kama tunapeleka kwenye taasisi ya Serikali basi watu- charge bei yeyote na wao pia waingine kwenye tender kama mtu yeyote mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama bei zao zikiwa nafuu tupeleke huko kama sio nafuu basi tupeleke mahali ambapo sisi kama Halmashauri au taasisi ya Serikali itaona kwamba inapata unafuu na inaweza ikaokoa fedha nyingi. Lengo kubwa hapa ni kuokoa fedha lakini sio kupunguza ubora wa kazi na huduma ambayo inatakiwa. Tupate huduma na ubora wa kazi ile ile tunayotakiwa kwa standards zinazotakiwa lakini kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, procurement zingine zote kwa mfano kwenye ununuzi wa tiketi na nini yote hayo Serikali iangalie mifumo ambayo serikali itaendelea kufaidi na itapata discount kwa sababu unapofanya bulk procurement kwenye jambo lolote bado unaendelea kupata discount.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendelee kushukuru na niendelee kuipongeza Serikali kwa kuleta sheria hii. Tunaomba Waziri wakati wa kuandaa kanuni basi maoni ya Wabunge wengi ambapo tutaendelea kusimamia kule kwenye Halmashauri zetu uyapokee na uyafanyie kazi, kwa sababu kila Halmashauri inakuwa ina jambo lake la kipekee tofauti na Halmashauri nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ambayo yako Dar es Salaam tofauti na Babati, mazingira ambayo yako Kigoma au kwingine yanaweza kuwa tofauti. Pia wakati wa kuweka standards ya bei kwa mfano jengo la darasa linalojengwa Dar es Salaam na Babati na nyingine ambayo iko Mwanza au kule Kigoma ni tofauti.
Kwa hiyo mtakapoweka wastani wa bei pia katika Mkoa huo basi wao wamekaa na waangalie kwamba ndani ya Mkoa wetu wastani wa bei itakuwa ni jambo fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukishaweza kufanya hivyo na mahali ambapo wadau wengine wa maendeleo wanaweza kuchangia. Pawe na dirisha ambapo pesa za Serikali, pesa za umma ziweze kutumika kwa kibali maalum. Nasema tusivunje kanuni, tusivunje sheria lakini pawe na vibali, pawe na authority ambayo itatoa hiko kibali. Lakini ili tuweze kuokoa fedha na tuweze kufanya shughuli ambayo italeta manufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu kila Mkoa na kila Wilaya kabla ya kutoa kazi basi wawe wanaangalia bei ambazo ziko sokoni. Bei kama ni barabara, nyumba, ujenzi, kama ni supplies za vitu wawe wanatoa. Lakini muhimu wanasemaga pesa za Serikali zinachelewa bei inakuwa mara mbili, hapana! Hata kama umekopa benki basi ile bei ipande kutokana na interest rate. Umekopa CRDB kwa 21% basi weka asilimia 25 kwamba wewe umekopa hizo pesa ukicheleweshewa wewe utalipa riba ya benki iwe ni kiasi hicho sio bei iwe mara mbili au mara tatu alafu unasema kwamba pesa za Serikali huwa zinachelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukiwa na uwazi katika shughuli hizi zote mimi naamini tutaokoa fedha nyingi sana na ubora wa kazi utaendelea kuwepo. Lakini Wizara ya Fedha naomba kile kitengo chenu ambacho siku zote tunaendelea kuomba kwamba Planning and Development kitengo hiki kiweze kutoa elimu lakini pia waweze kuwa wanapita kila wakati kuangalia mazingira ya eneo moja na eneo lingine ili shughuli hizi zote basi ziweze zikafanikiwa na tukapata manufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache naomba nishukuru na niipongeze Serikali kwa kuleta sheria hii, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuja na Miswada hii yote miwili kwa muda muafaka, ilitakiwa ije mapema, lakini niipongeze sasa kwamba zimekamilika. Hii itatusaidia sana kusonga mbele katika Sekta ya Kilimo, Mifugo pamoja na Uvuvi na zote zinaingiliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo machache ambayo ningependa nichangie, moja tunaendelea kuunda hizi Taasisi mbalimbali. Tayari tunazo nyingine nyingi upande wa mifugo hata hii upande wa uvuvi, lakini ningependekeza tuwe na Tanzania Research Institute moja, hizi zote zingeunganishwa tuwe na Institute moja tu ambapo huu chini sasa pawe na Idara mbalimbali ya Kilimo, ya Mifugo, ya Misitu na nini ili kupunguza gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaunda hizi Bodi, tutaunda muundo mzima ambao tumependekeza hapa na matokeo yake kila mwaka tutakuwa tunapeleka fedha kwenye bajeti za OC, lakini hatutakuwa na pesa za development ambapo tungekuwa na Taasisi moja tu, nina uhakika kwamba tungeweza kuwa na timu ndogo, kila sekta ingekuwa inatoa mtu mmoja kuingia kwenye ile Bodi, basi gharama zingekuwa zinapungua, halafu fedha nyingi ziwe zinaenda kwenye kufanya utafiti yaani kwenye development.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hapa bado kila mmoja atakuwa anashindana hivyo hivyo. Kilimo atataka, wa Mifugo atataka, wa Uvuvi atataka, ukija kwenye Misitu kila mmoja anataka fedha tofauti tofauti. Sisi hatuna fedha hizo na hata leo hii COSTECH ndiyo ambayo inasimamia utafiti karibu wote. Hao wote wanategemea pesa kutoka huko, ni bilioni nane tu ambazo zimetengwa mwaka huu ambayo haitoshi hata kwenye chuo kimoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo fedha sasa ni vizuri tuanze kufikiria pamoja na hii itakuwepo lakini ziunganishwe sasa tuwe na Tanzania Research Institute ambayo itakuwa inasimamia sasa mambo ya utafiti mbalimbali na hapo patakuwa na coordination nzuri, hapo ndiyo patakuwa mahali ambapo unapofanya utafiti labda kwenye Ziwa fulani siyo lazima aende mtu wa samaki tu. Huyu wa mafuta ataenda kuangalia madini kama yapo, kama kuna masuala ya maji, ubora wa maji wote watakuwa wanashirikiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependekeza, kwa baadaye tufikirie kuwa na Tanzania Research Institute moja ambapo taasisi zote hizi zitakuwa chini yake, itakuwa ni umbrella kwa ajili ya taasisi zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwenye hii ya uvuvi, ningependekeza taasisi zetu badala ya kuwa na vituo vyao ambavyo wanafanyia kazi zao wako peke yao na tafiti zao nyingi hazifiki kwa walengwa, tungeunganisha na Vyuo Vikuu vyetu na tungeunganisha na vyuo vingine. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Sokoine, basi Taasisi hii ya Utafiti ya Kilimo ingekuwa humo ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulienda na Kamati ya Kilimo Holland, unakuta Chuo Kikuu huwezi kutofautisha nani ni mwanafunzi, nani ni mfanyakazi wa chuo na nani mtu wa utafiti. Mwanafunzi anayeingia wakati anafanya utafiti wake hahitaji kusubiri kupewa fedha ya kwenda field, anapoanza tu shughuli tayari hapo anakutana na Watafiti, anakutana na vifaa mbalimbali ambavyo asingeweza kuviona angekuja kuvipata baada ya miaka mitatu, minne wakati anakaribia kumaliza elimu yake ya chuo ndiyo atakutana na hivyo vitu, lakini hapa kuanzia siku ya kwanza anakuwa tayari anapata on job training na hapo anakuwa Msaidizi wa hao Watafiti na lingeweza kuwa ni jambo ambalo lingetusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganda wenzetu tayari wameshaanza hivyo. Unakuta University ya Kampala tayari iko imeunganishwa na vituo vya utafiti, kwa hiyo wanafanya kazi under one roof, lakini kila mmoja anakuwa kwenye Idara yake ndani ya ofisi moja. Unakuta wengine ni watu wa wanafunzi na wengine ni watu wa utafiti ambayo itatusaidia katika tafiti mbalimbali na wanafunzi wetu watakuwa wanapata exposure na watakuwa wanapata on job training hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nashukuru kwamba ikishaundwa basi tafiti mbalimbali ambazo zimefanyika sasa matokeo yake na namna ya kufanya majaribio yatakuwa yanaenda sasa kwa walengwa. Muhimu tafiti hizi wakati zinafanyika basi tungehakikisha kwamba kwa mfano kama ni za kilimo ziende kufanywa katika mashamba ya wakulima ili wakati wanafanya majaribio, basi wakulima pia yule ambaye hata kama hajasoma atajifunza jambo moja au mawili pale na yeye anaweza kushika yale mazuri na tukawa tunaboresha kilimo chetu na pia katika masuala ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uvuvi sehemu kubwa Tanzania tumebarikiwa kuwa na maji ya kutosha; Mito, Maziwa lakini hatuna industrial fishing yaani ufugaji wa samaki ambao ni commercial, hiyo yote inatokana kwa sababu hatuna suala zima la utafiti ambao umefanyika na ni muhimu sasa tuunganishe nguvu zetu kwamba utafiti wowote ambao unafanywa uende ufanywe huko kwa walengwa na nina uhakika kwamba matokeo yake walengwa watakuwa wananufaika, kama ni wakulima, kama ni wafugaji, kama ni wavuvi, wote watanufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala la Board Member nilikuwa napendekeza pia iongezwe na nitakuja na amendment kwamba pawe na Board Member mmoja kutoka private sector ambaye yuko kwenye kazi hii ya utafiti, kama ni Researcher, kama ni wa mbegu, kwamba anafanya biotechnology mambo ya tissue culture nini, kama wana association yao, basi mmoja wao pia tofauti na yule anayetoka kwenye farmers group ambaye ni mkulima wa kawaida, yeye atakuwa anapeleka mahitaji, lakini huyu ambaye yupo kwenye field moja kwa moja na ni mtaalam, basi mmoja wao pia aunganishwe kwenye hiyo Bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingine ambaye pia ningependekeza awepo kwenye Bodi na iwe katika Bodi zote ambazo tutaunda ni mtu kutoka Idara ya Mipango. Mara nyingi hapa tunaweka watu mbalimbali, lakini watu wa Idara ya Mipango hatuwaweki na tusipowaweka watu wa Idara ya Mipango na watu wa Fedha matokeo yake huko tutajiandaa vizuri, planning inakuwa vizuri, lakini mwisho wa siku ambaye anaamua kwamba fedha ziende wapi kama hajui na haelewi, fedha hizo hatutapata. Kwa hiyo, ningependekeza mtu wa mipango na fedha wawepo pia katika Bodi hii ili wawe na uelewa kwamba nini kinatakiwa na wakati tunapopanga bajeti zetu wawe wanahakikisha kwamba mpango unawekwa kwamba bajeti hiyo itapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependekeza kwamba tafiti zimefanywa nyingi, sasa namna ya kusambaza zile tafiti iwe katika kilimo, mifugo iangaliwe namna ya kutumia pia vijana wetu kuanzia ngazi ya sekondari, kama utafiti mbalimbali unafanywa wangekuwa wanafanya pia katika shule zetu za sekondari, wanafanya pia katika vyuo mbalimbali, nina uhakika kwamba tungekuwa tunafika mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu hapa kuliko yote ni namna ya kupata fedha ya uhakika. Kipindi cha bajeti hapa tulipendekeza kwamba shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta iwekwe iende kwenye utafiti ambayo tungepata karibu bilioni 100. Hapa kwenye Kamati wameandika kwamba Serikali imetenga chini asilimia 0.5 ya Bajeti nzima, siyo 0.5 ni 0.0005 kwa sababu bilioni nane kwa trilioni 29 haionekani wala haipo kwenye mahesabu ni sawa na hatujatenga fedha yoyote kwenye utafiti. Lazima tuwe na chanzo cha uhakika ambacho fedha zake zitakuwa zinakwenda kwenye utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Uganda leo asilimia 40 ya fedha kwa ajili ya kuendeleza mambo ya utafiti iko kwenye bajeti yao. Majengo pamoja na vifaa, Serikali inanunua asilimia100 na ukienda pale unakuta vijana wadogo wenye umri wa miaka 25 mpaka 35. Ukienda kwenye vituo vyetu kwakweli inasikitisha kwa sababu wako watu waliosoma sana wana Masters, Phd, Doctorates mbalimbali, mwingine amesoma katika kozi tatu, nne kwa sababu pesa za kufanya maendeleo ya kufanya kazi hamna, kwa hiyo anabaki pale anajiendeleza kusoma, mwisho wa siku anakuja kustaafu hajatumika kabisa na mifano mingi tunayo hapa Tanzania. Sasa watu wale badala ya kugharamia kuwasomesha tungehakikisha kwamba tafiti mbalimbali ziendelee kufanywa na Watanzania wanufaike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuje kwenye suala la biotechnology ambayo inakuja kwenye kilimo, inakuja kwenye mifugo, inakuja kwenye uvuvi, ni vizuri sisi wote tukapata uelewa mpana kuhusu masuala ya biotechnology, wengi hapa wanapinga na wanapiga vita masuala ya biotechnology.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipojiendeleza kwenye masuala ya biotechnology Watanzania tutakuja kupitwa na wakati kwa sababu wenzetu Waganda 2020 wataanza kutoa ndizi na mazao mengine ya GMO na sisi hatuna ukuta wala hatuna namna ya kuzuia vile vitu kuja hapa. Tayari leo Watanzania tunakula vitu vingi ambavyo ni GMO bila kujijua. Kwa hiyo ni vizuri tupate uelewa.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nitumie fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu na pia nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuishukuru Wizara ya Fedha na wataalam wake wote ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kazi ambayo wanafanya, lakini muhimu kuliko yote ni namna tunavyoshirikiana kuhakikisha kwamba tunaelewana ili mambo mengi yaende. Siku zote kwenye mambo ambayo ni magumu, lazima pawe na mvutano, lakini kwa mambo mengi tumeweza kukubaliana. Tunamshukuru kwa hilo Mheshimiwa Dkt. Mpango pamoja na timu yake mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nishauri jambo moja na ikiwezekana tukija kwenye Bunge lijalo tubadilishe timing zetu kwa sababu muda huu ambao tunasoma bajeti na Wajumbe wanachangia, halafu mara baada ya hapo inakuja Finance Bill, muda unakuwa ni mdogo sana kuweza kukaa na kuleta mabadiliko ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na hiyo, napenda pia kushauri kwamba badala ya sisi kusubiri kufanya mabadiliko na kukutana na wadau hiki kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kufikia kwenye bajeti, process hii tungeanza mara baada ya mwaka mpya wa fedha kuanza, Bunge kwa mfano hili la mwezi wa Nane tungeanzia hapo kukaa na wadau ili yale
mabadiliko ambayo tunataka kuyafanya tuweza kuyaangalia vizuri, kushauri vizuri, tukae na Serikali, tukae na wadau ili tunapofikia huko, maamuzi yote yawe tumeshamaliza. Hiyo ndiyo itakuwa njia pekee, kwa sababu kuna mengi ambayo tumependekeza.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano nikiangalia kwenye hii Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kuna mengi nimependekeza leo ni mwaka wa saba, unakuta kila mwaka unaambiwa basi tutaangalia mwaka ujao. Haya yote yasingetokea kama ingekuwa tunakaa mapema na kujadiliana.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa naomba tuangalie ni jambo muhimu sana. Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla iwe na timu maalum, iangalie nini kinafanyika kwenye nchi zinazotuzunguka ili kabla ya kwenda kwenye Kikao cha Afrika Mashariki, yale yote ambayo yanahusiana na East African Customs Union ambapo Bunge hili hatuna uwezo, wala kubadilisha chochote, tutaongea hapa yanapelekwa mwakani ili maoni mengi yawe yanachukuliwa mapema na wakifika huko wajue nini kinaendelea kwenye nchi zinazotuzunguka ili nasi tuje na mabadiliko kwa sera yetu ya kodi na tozo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia wamekuja na blue print. Nashukuru kwamba wameiandaa, lakini hii blue print imesubiriwa kwa muda mrefu na kwa sasa hivi hakuna mabadiliko yoyote yaliyokuja kwenye huu Muswada wa Sheria. Kwa hiyo, bado kwa mwaka nzima ujao hatutaona mabadiliko yoyote kwenye sekta hii ya viwanda wala kilimo wala nini kwa sababu mengi kuhusu kero ambazo zinafanya sekta zetu zote zisiendelee ikiwemo viwanda yapo kwenye ile blue print. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na hilo, kuna suala la double taxation ambayo pia ilibidi tukae mapema tuangalie nini kifanyike ili kuondoa huu utitiri wa kodi, tozo na ada? Pia mahali ambapo mtu analipa mara mbili au mara tatu;
kwa mfano, mtu anayelipa ushuru wa mazao, yakisindikwa analipa 0.3% Service Levy, lakini yale mazao ambayo ni by product kwa mfano mashudu yanaendelea kutozwa ushuru wa mazao ambapo mashudu siyo mazao, ni by product ya huko viwandani.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ni muhimu, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuleta katika Muswada huu mabadiliko ya sheria ambayo itamruhusu Waziri kusamehe kodi ya mapato na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye masuala mbalimbali ya Kiserikali.

Mheshimiwa Spika, Kamati imekuja na pendekezo, tunashauri kwamba pia Serikali iangalie katika eneo la VAT kwamba maeneo ambayo yana miradi ya kijamii hasa katika Halmashauri zetu na miradi mbalimbali ambapo tunapata ufadhili, Serikali iweze kusamehe hizo kodi ili tuweze kutekeleza miradi. Vile vile marafiki ambao wanataka kutuchangia wawe huru kutuchangia na tusitozwe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia maeneo mengi kwa mfano vituo vya utafiti ambavyo ni vya Kiserikali pia vinatozwa kodi. Halmashauri zetu pia zinatozwa kodi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri angetanua wigo huo, nina uhakika kwamba hapo tungeweza kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tungeangalia kwa mfano, kwenye mitambo ya kuchimba maji, kutengeneza mabwawa na kadhalika, tungeondoa kodi ili iwe mingi nchini tuondokane na hii kero ya maji kabisa na hasa katika hii Sekta ya Kilimo katika umwagiliaji na uvunaji wa maji tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Sekta ya Madini, pia tunaishukuru Serikali imepiga marufuku kupeleka nje madini yetu. Tukija kwenye Sekta ya Vito, kama hatuna mashine za kutosha hapa nchini za kuchonga na kusanifu, wangeweka incentives kwamba waondoe kodi kwenye zile mashine za kuchonga ili zije kwa wingi nchini kwa bei nafuu zaidi, kwa sababu kama kodi ya asilimia 18 wakiondoa, tayari kutakuwa na mabadiliko karibu asilimia 30 kwenye bei ili watu wengi waweze kutumia.

Mheshimiwa Spika, mbali na hiyo, Serikali bado haijawa na mkakati wa kusaidia viwanda vya ndani. Bado kabisa. Tunashukuru, kwa mfano, kwenye taulo za akina mama wamefuta kodi, lakini hii itakuja kusaidia zile zinazotoka nje ya nchi. Hawa wa ndani ya nchi hawataweza kudai import tax na bei kwa viwanda vya ndani itakuwa hatujavisaidia.

Mheshimiwa Spika, mbali na hiyo, hata kwenye viwanda vingine kwa mfano chakula cha mifugo, nashukuru kwamba tumeweza kuongeza bidhaa nyingine kwa mfano mashudu, lakini bado tungefikia mwisho kwamba zile zote ambazo zinazalisha chakula cha mifugo na masuala yale yote yangefutiwa kodi ili tuweze kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinalindwa.

Mheshimiwa Spika, leo tuna viwanda vingi vinashindwa kushindana na viwanda ambavyo viko kwenye nchi za Afrika Mashariki. Bidhaa zetu ukipeleka nje, yaani uki- export hakuna kodi. Kwa hiyo, ukirudisha ndani inakuwa haina kodi nchi za jirani. Kwa hiyo, sisi tutakuwa tunaendelea kubaki kuwa soko badala ya kuwa wazalishaji na kuwa tunatuma huko nje.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine muhimu ni kwamba Serikali na Waheshimiwa Wabunge tungekaa na wataalam kuangalia zaidi kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Utalii tuone kikwazo ni nini kwenye sekta hizo? Ili tuweze kuwekeza zaidi humo kwa asilimia 80 ya wananchi ambao wako huko. Tukiwawezesha kiuchumi tukajua vikwazo ni nini na kuwasaidia katika usindikaji wa mazao yote hayo, nina uhakikika, wananchi wakiwa na uchumi mzuri na spending power, Serikali pia itakuwa inakusanya kodi nyingi zaidi na tayari mapato yetu yataendelea kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tusiangalie kwenye sekta ya kikodi tu. Serikali ingewekeza kwenye maeneo pia ambapo moja kwa moja hawatapata kodi au mapato, lakini watakuwa wamekuza uchumi na kutokana na indirect tax yaani kodi ambazo hawakusanyi moja kwa moja, watapata mapato mengi.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuomba jambo la mwisho. Binafsi nilikuwa bado naona katika Serikali hakuna coordination, yaani Wizara moja na nyingine bado haziongei vizuri. Idara na Idara haziongei vizuri. Leo tunapata matatizo kwa sababu kila mmoja anakurupuka.

Mheshimiwa Spika, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba ni vizuri na Bunge sasa likakaa imara kwa sababu hii mamlaka tunavyoiachia Serikali kwamba kila Waziri akitaka kwenye kanuni akabadilishe ada, tozo na mambo mbalimbali, tuibane hiyo. Tunatakiwa turudishe kwetu, Bunge ndiyo liwe linapanga. Kwa sababu baada ya hapo tunakuta tuwe na guided frame lines kwamba kwenye kanuni awe na uwezo wa kubadilisha mambo fulani fulani tu, siyo kila siku akiamua anapandisha tozo na ada. Hii blue print itakuwa haina maana kama hatutaweza kuibana Serikali na kuhakikisha kwamba mambo yote yanaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo ni muhimu sana, Serikali iunde timu ya kudumu ambayo itashirikiana na Bunge lako kwamba kila wakati tuwe tunapata mawasiliano kutoka kwa wadau, lakini tukae na Serikali tupate mifano halisi na hai ili kuangalia sekta zote, kwa sababu leo ukisema kwenye sekta fulani tuwaondolee msaada wa kitu kimoja tu inakuwa hujaisaidia hiyo sekta.

Mheshimiwa Spika, inatakiwa tuje na mabadiliko makubwa (total reform) kwenye Sera ya Kodi lakini pia mambo mbalimbali ambayo yanatozwa na Regulatory Boards na kadhalika. Tukifanya hivyo, tutaona uchumi wa Tanzania unakua na Sekta zote za Kilimo, Mifugo na Utalii zitaweza kukua vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado naendelea kushauri kwamba yale ambayo Kamati imekuja nayo kwenye schedule of amendments, Serikali ifikirie kwa sababu tumeyachambua kwa muda mrefu na mengi ya hayo mawazo yanatokana na miaka miwili, mitatu, minne ambayo Serikali ilishaahidi kuyafanyia kazi na bado haijafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa fursa ya kuchangia leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii kuwapongeza Wizara ya Fedha, Kamati ya Bajeti kwa kazi nzuri na kubwa waliyofanya na angalau awamu hii bajeti hii ni nzuri sana, huko tunakotarajia kuelekea naona sasa tuko kwenye mstari sahihi kabisa na kazi inaenda vizuri kabisa. Pia niwapongeze kwa jitihada kubwa kwenye kuondoa zile tozo angalau mmeanza kuondoa tozo mbalimbali kwenye lile suala la blueprint. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuwa productive yaani tuwe tunazalisha bidhaa Tanzania ambapo itakuwa bidhaa zenye gharama nafuu ambazo zitaweza kushindana kwenye soko la ndani na la nje ni lazima blueprint ianze kufanya kazi kwa asilimia 100. Bahati mbaya blueprint ni taasisi mbalimbali za udhibiti pamoja na Wizara mbalimbali ambazo zinatoza ushuru, tozo, ada na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kama nilivyoshauri siku zote tungeunda Tanzania Regulatory Authority ambapo taasisi zote hizi zitakuwa chini ya mwamvuli mmoja. Zikiwa chini ya mwamvuli mmoja kazi yao iwe ni ku-regulate yaani kuboresha na kudhibiti yale ambayo wanatakiwa kufanya na wakienda kwenye viwanda, biashara mara ya kwanza wawe wanatoa onyo, elimu na watoe muda wa kufanya marekebisho lakini mara ya pili karipio na mara ya tatu ndiyo wapige faini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ni kupiga faini tu imekuwa chanzo cha mapato. Lengo siyo hilo bali ni kuhakikisha kwamba tunafanya kazi vizuri na tunadhibiti ubora na viwango vya bidhaa zetu lakini pia itasaidia sisi tuweze kuzalisha vizuri. Niombe Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha na Wizara ya Uwekezaji mkifanya kazi kwa pamoja nina uhakika jambo hili tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze kwamba mmepunguza ile presumptive tax kutoka Sh.150,000 kwenda Sh.100,000 ina maana compliance itakuwa kubwa, watu wengi wataweza kulipa na watalipa kwa hiari bila kulazimishwa. Changamoto inakuja moja, sehemu zote mmepeleka ni kwenye hii formal sector, hawa ni wale ambao hawaweki record, tunawatoza tu kutokana na mauzo yao. Kwa upande wa wale ambao wanatunza rekodi na wamejisajili inawezekana biashara yao imefanana kabisa ila mmoja aliamua kuwa formal yaani alimua kuwa rasmi na akasajili kampuni yake kwa sababu kusajili kampuni siyo kazi kubwa, sasa hawa hamjawasaidia ina maana wengi tutaondoka huko kwenye sekta ambayo ni rasmi tukarudi kwenye sekta ambayo sio rasmi. Ingetakiwa vivutio vingi viwe kwenye sekta rasmi, huko ndiyo mngepunguza zaidi ili watu wengi waondoke huko kwenye sekta isiyokuwa rasmi na warudi kwenye sekta rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwamba suala hili la vitambulisho, lengo la kuwa na vitambulisho hivi naamini kwamba mtaendelea kurekebisha ili zile fomu wanazojaza kabla ya kupewa vitambulisho viwe vimekamilika wengi wao tuna uhakika wataondoka huko kwenye hivi vitambulisho vya Sh.20,000 na waanze kulipa kodi stahiki ambayo wanatakiwa kulipa, yaani wengi wao bado wanafanya biashara zaidi ya shilingi milioni 4 lakini wanalipa hiyo Sh.20,000. Sasa ili kutanua wigo wa walipa kodi ni vizuri kila mtu alipe kodi stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu kubw anyingine Wizara ya Fedha itusaidie kupitia TRA pawe na usawa katika kufanya biashara. Unakuta mtu anafanya biashara analazimishwa kuwa na mashine ya VAT kwa sababu ameweka rekodi yake wenzake waliomzunguka wanafanya biashara kubwa zaidi ya yeye hawako kwenye VAT, yule mtu mnamuua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo mtu anakuwa na mashine ya EFD wengine wanaofanya biashara zaidi ya yule wala hawana mashine ya EFD, hutakaa ujue nani anatakiwa kulipa kodi kiasi gani. Kwa hiyo, suala la EFD tuendelee kusisitiza ili kila mmoja alipe kodi anayostahili kulipa ndiyo tutakuwa na wigo mpana wa kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwamba Kamati pia mlishauriana na Serikali na safari hii Serikali imekubali, kwenye bajeti hii mmeweza kuondoa tozo nyingi kwa viwanda vya ndani lakini mmeweza kupandisha kwa bidhaa zinazotoka nje ili kulinda viwanda vya ndani. Hongereni sana kwa jambo hilo lakini sasa muendelee kuangalia namna ya kulea viwanda hivi. Suala siyo kodi peke yake mkijumlisha na hili suala zima la blueprint na mazingira mengine, nina uhakika biashara itakuwa nzuri na kwa sehemu kubwa mtapata kodi katika uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu, mmeweza kuondoa ile shilingi milioni 100, mtu asiandae mahesabu kwa kupitia wahasibu ambao wamesajiliwa. Tulikuwa tunaomba pia kwa wale ambao wako kwenye sekta rasmi ambao pia wanafikia tu hiyo shilingi milioni 100 au chini ya shilingi milioni 100 wao sasa sheria inawalazimisha kuwa na mhasibu kwa sababu yeye amejisajili tu kuwa rasmi pia na huyo mngemuondolea kwamba na yeye pia kama hajafikia shilingi milioni 100 asiwe anaandaa mahesabu ile pawe na usawa na kuwa kivutio cha watu kwenda kuwa sekta rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kama walivyosema wenzangu wote pamoja na Kamati Serikali ingeangalia namna ya kuondoa kodi kwenye mitambo ya kuchimba maji na kutengeneza mabwawa na solar water pumps. Kwenye jambo hilo la mitambo ya maji kuna hoja kwamba wale ambao wako kwenye VAT wao wanapata msamaha moja kwa moja kwa sababu akiingiza kama capital goods anapata exemption kwenye VAT on deferment. Sisi ambao tuko kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi bidhaa zetu hatuwezi kupata huo msamaha wa kodi kwa sababu bidhaa zetu baadaye hazina VAT, kwa hiyo, hatupati huo msamaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi tunataka kutengeneza mabwawa kwa ajili ya maji ya kunywa, umwagiliaji, mabwawa ya kufugia samaki lakini pia itapunguza mafuriko. Tija ikiwa kubwa huko kwenye kilimo, watu wakizalisha kwa wingi zaidi spending power ikiwa kubwa consumptation itakuwa kubwa na mtapata indirect tax badala ya direct tax. Kwa hiyo, Serikali tunaipongeza ninyi mbaki kutekeleza miradi ile mikubwa ya kimkakati kwa mfano Stigler’s Gorge, SGR lakini hii ya maji mtuachie private sector pia tusaidiane na Serikali kwa kuondoa baadhi ya kodi ambazo tunasema na mtaona mtapata faida kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilikuwa naomba nikumbushie kuna kodi nyingi ambazo tumeshazifuta na zimepunguzwa au kuondolewa lakini zinaendelea kutozwa tofauti na tulivyokubaliana. Kwa mfano, kwenye bidhaa zingine za solor tunatoza kodi wakati imeshafutwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kwenye property tax, mwaka jana tulikubaliana kwamba property tax itakuwa tunalipa kwenye zile miji yote na makao makuu ya halmashauri ya miji na maeneo ambapo Waziri atatangaza kwa kushauriana na Waziri wa TAMISEMI kwenye miji midogo lakini leo hii mpaka vijijini property tax tunaendelea kutozwa ambapo sio utaratibu ambao tulikubaliana. Kwa hiyo, naomba na hilo muweze kuliangalia ili tuweze kulitolea tamko ili watu wasiendelee kupata tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilikuwa nashauri kwamba cycle yetu ya bajeti tungeibadilisha kwa sababu leo hii kwa sehemu kubwa hatutaweza kubadilisha jambo lolote. Ni vizuri sisi bajeti tungekuwa tunapita kama kawaida lakini hivi vikao vya kuangalia nini kipande nini kishuke ili watu wajipange, taasisi mbalimbali zisiweke tozo au ada na kuweka kwenye bajeti zao kabla ya mwezi Novemba. Kwa hiyo, ingeanza mwezi Septemba mpaka Novemba kabla ya bajeti za kuanzia ngazi za chini kuja juu hazijaanza kuandaliwa ingekuwa inarahisisha tusingekuwa tunapata shida na huko ndiyo tungekuwa na uhakika kwamba sera ya kodi na tozo ingekuwa ya uhakika zaidi na watu wengi wangependa kupata ushauri kutokana na jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia taskforce ingeweza kufanya kazi badala ya kukaa ofisini na kusubiri wangekuwa wanatembea ku-insight, watu wanapotoa mifano basi waende waonyeshwe kwamba hapa biashara inaenda hivi, kwa sababu wegi wao wamefanya tu kazi wamesoma baada ya kumaliza shule wamepanda vyeo na wamefikia hapo walipofikia lakini hawajawahi kufanya biashara. Sasa wakiweza kwenda kwenye mazingira ya biashara, wakaona wafanyabiashara wanavyofanya kazi hapa ndiyo wataelewa kwamba kumbe hili jambo tukifanya hivi, unaweza ukakosa direct tax lakini indirectly ukapata ajira na kodi nyingine nyingi badala ya wanavyofanya kazi leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilitegemea kwamba tungekuwa kwenye vifungashio vya mbegu, lapidary equipment na pia bidhaa hizi za kukaushia mazao na yale makasha ya jokofu. Pia wangetanua wigo kidogo kwa mfano kwenye majokofu yawe ya maziwa, samaki na nyama kwa sababu kazi ni ileile, ile itasaidia watu wengi kununua.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie, ni jambo moja tu namalizia. Kuna jambo hili la kuagiza kwa mtu ambaye anafanya hiyo biashara. Naona wangeondoa na wangeweka pia hata wale Mawakala wanaouza wapate msamaha wa kodi, kwa sababu leo hii mkulima yupi ana uwezo wa kuagiza vitu hivyo moja kwa moja kutoka nje ya nchi. Kwa mfano halmashauri yetu, ukitaka kununua kwa mikopo kwa vikundi, hawataweza kwa sababu Sheria ya Manunuzi haiwaruhusu kutuma fedha nje kabla hiyo bidhaa haijangia nchini, kwa hiyo mpaka iingie nchini ina maana tayari itakuwa imeshatozwa kodi. Kwa hiyo sasa ni vizuri, walengwa ni hao watu wadogo na huu ushirika wetu, kwa hiyo naomba pale wakati wa marekebisho watuondolee kwamba ni agent wa hiyo bidhaa kama ni majokofu, ni agent wa hapa hapa Tanzania au kama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba nichukue fursa hii kukupongeza tena, kwa jitihada zako na namna unavyosimamia Bunge letu. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yao ya Wataalam kwa kutuletea hotuba nzuri, ambapo baada ya sisi wote kuchangia ninaamini kwamba tutakapoelekea kwenye Finance Bill yale mapendekezo ambayo Wabunge wengi wamependekeza, watayazingatia ili tuelekee huko sasa kufanya shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze sana Serikali kwa kutuletea Sheria ya Manunuzi, binafsi nimefarijika na ninajua hilo sasa litakuwa jambo ambalo litatusaidia wote. Niendelee kusisitiza kama wenzangu wote walivyosema suala la shilingi 50 kwenye maji. Lakini kwenye maji pia nigeomba niwapongeze kwa kuondoa gharama za dawa isitozwe kodi, pia ondoeni vile vifaa muhimu ambayo vya ku-filter maji ili na zenyewe katika hospitali zetu na sehemu za shule ambazo gharama yake ni kubwa ina import duty na VAT iondolewe ili watu wapate maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niendelee kuomba Serikali ihakikishe kwamba wafanye kwa hati ya dharura kuanzisha wakala wa maji. Fedha hizi mtazipata, anzisheni huo wakala ili ifanye kazi tunavyotarajia.
Ninaomba tena niwaombe Wizara ya Fedha wajaribu kuangalia suala la motor vehicle muiondoe. Hivi tunavyoenda sasa hivi kwa kukata kwa kupitia TRA wekeni kwenye mafuta, ili wale wanaokwepa wote wasiweze kukwepa. Ukiweka kwenye mafuta watayatumia mafuta atakuwa analipa na yule ambaye atumii atakuwa na gharama ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo mzima ulivyokaa, ukiweka kwenye mafuta itakuwa ina unafuu kwetu. Hata mambo ya uendeshaji wake na namna ya gharama za ku-print itapungua, itakuwa mtu akiweka mafuta ameshamaliza kila kitu. Lakini pia kwa wale ambao wako nje ya wigo wa hiyo kodi, wakiweka Serikali itakuwa inapata mara mbili ya hii mnayopata leo. Kwa nini wakati tukiwaelekeza mtapata mapato mnakwepa kuweka? Tunaomba huo ushauri mchukue, ili suala la motor vehicle lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tena tuangalie namna ya kupata fedha ya uhakika ya utafiti na masuala ya mazingira. Leo hii hakuna dunia, haya mambo yote tunayosema tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, bila utafiti ni hakuna kitu, na utafiti tumetenga fedha kidogo sana. Tuangalie namna ya kupata fedha za utafiti na suala la mazingira, kwa sababu mazingira pia ni muhimu sana huko tunakoelekea gharama tutakazotoza kuboresha hali ya mazingira itakuwa mara kumi ya hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, bBado kwenye suala la Sheria ya Finance Bill, mmeondoa msamaha kwenye vifaa vya natural gas lakini pia mimi ningependekeza ongezeni hata gesi ya kawaida liquid petroleum gas ili tuache kutumia mkaa, haya majiko na nini; ikiwa bei ni ndogo tutaacha kuharibu mazingira na pia itakuwa ni nafuu kwetu. Kwa hiyo, muondoe hizo kodi huwezi kupata kote kote. Huwezi ukapata kote kote, sehemu moja lazima upoteze nyingine upate. Kwa hiyo, kama mnapenda mazingira ondoeni hiyo kodi kwenye majiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ningeomba ni katika suala la EFD hii Electronic Fiscal Devices ndiyo njia pekee tutapa kodi yote tunayostahili kupata, leo hii mliahidi mtaleta mashine za kutosha, sijaona kwenye bajeti mashine za kutosha, naomba tulishawahi kupendekeza ruhusuni watu binafsi walete mradi vile viwango mnavyotaka zile specification wapeni. Mtu akiamua hapa Dodoma siyo lazima ununue mashine shilingi 700,000, mtu kama hizi decoders anaweza akakukodishia kila mwezi ukamlipa shilingi 30,000, shilingi 50,000 na service anakufanyia. Kwa hiyo muangalie mfikirie nje ya box, hili suala bila kuwa na EFD za kutosha mashine hizo 12,000 mnazosema hata Dar es Salaam peke yake Wilaya moja hazitoshi, kwa hiyo tukitaka kukusanya kodi zaidi hakikisheni suala la EFD mnalifanyia kazi kwa mapema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine suala la formal sector na informal sector. Mfumo huu na hizi tozo za penalty mlizokuja nazo za kodi kwamba mtu akichelewa kidogo, penalt kila mwezi asilimia tano itafanya watu wengi zaidi warudi kwenye informal sector, teremsheni kodi, compliance iwe kubwa iwe tax friendly, watu walipe kodi vizuri zaidi, lakini hapa mnawatisha watu. Hivyo ningeomba sana hili suala la kwenye kodi tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo mzima wa kodi wetu bado haujakaa vizuri. Kwa mfano, leo bidhaa zile ambazo tunazalisha ndani ya nchi, mbolea, net ukiwa ndani ya nchi raw material yake inatozwa kodi na hawapati refund. Kwa zamani ilikuwa zero rated tumeondoa zero rated, aki-export hiyo bidhaa mbolea na net akipeleka tu Kenya anarudishiwa zile kodi zake, aki-import tena hiyo hiyo bidhaa akiirudisha hana kodi, sasa mtafanya watu wasizalishe ndani ya nchi bora mtu atoe nje na kurudisha ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wetu wa kodi bado haujakaa sawa na ninaomba tu tuangalie la sivyo hii ndoto yetu ya kwenda kwenye viwanda, hatutafikia kama mfumo wetu wa kodi tusipouangalia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza kwamba TRA iwe ni one stop center, kodi zote na zile tozo ambazo siyo za kodi zote zikusanywe na TRA, na pia ingeanzishwa huduma center, kila mtu ambaye anataka huduma mbalimbali kuna Wabunge hapa tena Mheshimiwa Makamba alishawahi kuisemea. Tuanzishe one stop center easy of doing business iwe vizuri, ikiwa hivi hata wale watu ambao wako nje ya wigo wa kodi labda anafanya biashara zingine lakini leseni yake akitakiwa kukatia TRA, huyu mtu atalipa angalau kidogo, na tutaweza kupata mapato yetu yote vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tunaomba kwamba hizi kampuni za simu zote ziwe listed kwenye stock exchange. Kwa nini makampuni madogo yawe listed na haya ambayo wanafanya biashara kubwa hawawekwi humo. Ningeomba sana kampuni zote, ziwekwe humo, lakini muhimu kuliko yote, tufanye reseach na statistics hatutumii kabisa statistics na ndiyo maana hatuendi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu sana ni kwenye sekta ya kilimo. Sekta ya kilimo tuliahidiwa kwamba kodi nyingi na ambazo ni kero mngeziondoa kwa kweli mimi nilisikitika baada ya kuona kwamba kwenye Bodi ya Pamba mmeondoa shilingi laki nne na nusu hata mngeacha isingeleta tofauti yeyote. Hata hizo kodi kwenye angalau kwenye korosho mmejitahidi kuondoa asilimia kadhaa kwa mwaka mzima inaondoa kiasi fulani lakini hizi zingine na sekta yetu ya kilimo haitaweza kukua, kama tutakuwa tunaendelea na utitiri wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningeomba kwamba mngeunganisha Regulatory Board zote ziwe chini ya bodi moja iitwe Tanzania Regulatory Board na hizi zingine zote ziwe taasisi chini yake ili wanapoenda kufanya ukaguzi au wanapoenda kufanya shughuli mtu analipa mara moja basi, wale watu wanatakiwa kama ni sekta fulani wataalamu wa sekta hiyo kutokana na zile idara wataenda kwenye hiyo bodi, hata wafanyabiashara wataona kuna unafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache niendelee kupongeza jitahaa hizi zilizopo, mindset change na nina uhakika kwamba tunaweza kufanikiwa Tanzania ya viwanda. Ahsante, hongereni sana.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na kunipa uwezo wa kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais kwa kazi nzuri sana ya kuendeleza uongozi bora katika nyetu. Ni mfano wa kuigwa katika uongozi wake kwa kuwa mfuatiliaji mzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuonesha nia na njia ya kuboresha masuala ya mazingira kwa ujumla na pia kuonesha na kutekeleza vyema uboreshaji wa Muungano wetu, kuendelea kuboresha kwa kutatua changamoto za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri katika masuala mawili muhimu na yote yanalenga mazingira. Kwanza napongeza uzinduzi wa Mfuko wa Mazingira Kitaifa ulioanzishwa 2004, tumechelewa lakini tunasema unapoamka ndipo pamekucha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Mfuko huu tuangalie namna ya kupatia vyanzo vya kudumu ili uwe endelevu na malengo yake yatimie. Suala la athari za Mazingira linajulikana na hakuna hatua ya uhakika inachukuliwa, tunabaki kulalamika wote bila kuchukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuhitaji Sheria mpya, zilizopo zinakidhi na pia urasimu wa kubadilisha Sheria na Kanuni zake itachukua muda. Tuhakikishe tunafuata sheria zilizopo, nashauri agizo litolewe na mmoja kati ya vigezo kwa kiongozi yoyote na mtumishi wa Serikali katika ufanisi wa kazi yake iwe masuala ya mazingira, tuzo itolewe kwa kila ngazi kwa taasisi na binafsi katika usimamizi wa mazingira na sheria zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuongelee na kuhakikisha kuwa Bunge lipitishe sheria ya kuweza kupata vyanzo vya kudumu katika Mfuko wa Taifa wa Mazingira. Pia napendekeza kuondoa kodi katika uagizaji wa majiko yote yanayotumia gesi (LPA) au majiko banifu. Hii itafanya kushuka bei ya gesi na majiko yake na kupunguza uharibifu wa misitu kwa asilimia mbili au tatu. Pia tuhamasishe utumiaji wa nishati mbadala au jadilifu (renewable energy). Kodi ipunguzwe katika uagizaji wa vifaa hivyo nje ya sola ambayo haina kodi kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri gharama za ukaguzi na leseni kibali cha NEMC ipunguzwe ili Watanzania wengi zaidi waweze kutafuta hivyo vibali badala ya kusubiri kupigwa faini ambayo wanaona ni ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vyanzo nashauri asilimia kumi ya tozo zote au leseni zinazotolewa na zinahusiana na masuala ya Mazingira. Mfano; leseni ya Viwanda vyote, leseni za Madini, Leseni za Ujenzi, Leseni za Utalii, Leseni za huduma za Afya Mawasiliano, Uvuvi, Mifugo, Kilimo na Leseni za uzalishaji wa Nishati. Pia tozo tunayopata kutokana na (TFS - Wakala wa Misitu Tanzania) ambayo ni uvunaji wa misitu yetu asilimia ishirini ya mapato hayo yarudi kuboresha mazingira. Leseni au vibali vya watumiaji maji asilimia kumi pia zirudi kuboresha vyanzo vya maji katika Mfuko wa Mazingira pia tuliweka kodi ya kuingiza magari na bidhaa chakavu huwa zinaharibu mazingira, asilimia ishirini ya mapato hayo yaende katika Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza shilingi kumi ya kila lita ya mafuta pia iende kwenye Mfuko wa Mazingira. Pia shughuli zote zinazofanyika ambazo zinaharibu mazingira, pawe na asilimia kumi ya tozo kwenye vyanzo hivyo vinavyopatikana ili mfuko uweze kuwa endelevu na mipango itimizwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Fedha za EWURA, pia asilimia kumi ziende kwenye kuboresha au kutunisha mfuko. SUMATRA pia katika leseni zote ichangie asilimia kumi ya mapato yake katika mfuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuleta hamasa incentive pawe na ruhusa kuweka angalau asilimia tatu au tano kama gharama expenses ambayo itatozwa kodi (allowed expense) katika balance sheets (Income Tax Act) na itafanya makampuni yachangie katika masuala ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaoshughulika na utalii wapewe maeneo maalum ya kuboresha mazingira na hivyo hivyo viwanda, migodi na biashara zote zipewe maeneo maalum ya kusimamia na kuboresha mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi iondolewe katika mitambo ya kusafirisha na kurudisha bidhaa sokoni recycling na pia katika mitambo ya kufua umeme unaotokana na taka ngumu. Tuwe na tozo ya shilingi hamsini kwa kila mfuko wa mbolea ya dukani inayoagizwa kutoka nje ya nchi. Tunaweza kujadili na pakawa na Tume Maalum ya kuangalia vyanzo vya Mfuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie taarifa ya Kamati ya kwanza kwa kuwapongeza sana kwa kazi nzuri na kubwa wanayofanya. Naomba nishauri Bunge iangalie namna ya kuwa na mfumo wa Kamati za Kudumu kufanya kazi ya pamoja coordination, uratibu baina ya Kamati mbalimbali kwenye masuala mtambuka. Kwa sasa kila Kamati inajitegemea na sio rahisi kufanya kazi ya pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niendelee kushauri Kamati ichukulie kwa umuhimu suala la kulinda ardhi za kilimo, mifugo na pia maeneo ya uvuvi zisibadilishwe matumizi kiholela na pawe na sheria itakayowezesha Bunge kuridhia kubadilishwa matumizi ya ardhi hasa za kilimo, mifugo na uvuvi. Leo hii nyingi zenye rutuba za kilimo zimegeuzwa kuwa makazi, viwanda na matumizi mengine. Pia kuishauri Serikali kutatua mgogoro wa ardhi baina ya Hifadhi mbalimbali na wakulima, wafugaji na hata ushoroba mbalimbali zinapovamiwa ambazo ni muhimu kwa uendelevu wa hifadhi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeshauri tuangalie namna ya kuchangia kuboresha misitu na hifadhi zetu ili mchango wake uwe endelevu kwa Taifa letu. Ni vyema mapato yanayotokana na maliasili sehemu yake mfano asilimia 10% yarudishwe kuboresha mazingira. Kwenye kufanya
uratibu na Kamati zingine tuishauri Serikali kuangalia kilimo, hifadhi, kulinda vyanzo vya maji na pia kuzuia mmomonyoko wa udongo kwenda kwenye maziwa. Sheria zipo ila hamna ufuatiliaji na usimamizi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Kamati ikubali kufanya utaratibu wa karibu na Kamati zingine na kupokea maoni ya Wabunge na wadau wengine ili kuboresha utalii. Tumejaliwa na Mwenyezi Mungu kupata vivutio vingi vya aina mbalimbali lakini hatujafikiria hata asilimia 10% kufaidi rasilimali tuliyonayo. Tunashauri tuangalie mfumo wa kuishauri Serikali namna ya kufuatilia na kusimamia sheria zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Kamati pia iweze kushirikiana na taasisi ya Wabunge uliopo Bungeni ya TAPAFE ili kuendelea kupata tija. Ahsante.
Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nichukue furasa hii kwanza kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na kuleta matumaini makubwa. Migogoro mingi imeendelea kupungua na tunaendelea kuomba kwamba waendelee kufanya kazi hiyo kubwa ili migogoro ya ardhi sasa hapa nchini iishe. Tunaomba ile migogoro hasa ile ya Babati ambayo Wabunge wenzangu wote tumekubaliana kila anayepata fursa aisemee, ile ya vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gidejabug wale wananchi wapatiwe maeneo mbadala kuna mapendekezo tumeshaleta, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ifanyie kazi ili Wizara ya Ardhi iweze kutoa vibali, lakini pia ile migogoro ya mashamba ya kule Kiru yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu Mheshimiwa Waziri ninaomba utuletee sheria mpya hapa ndani ya hii Sheria ya Ardhi kipengele cha kuzuia matumizi ya ardhi ya kilimo ilindwe kisheria ili ukitaka kubadilisha matumizi ya ardhi ya kilimo ije hapa Bungeni kwa sababu maeneo mengi yenye rutuba Tanzania yamebadilika matumizi sasa yamekuwa makazi, viwanda na matumizi mengine ambapo hayo matumizi mengine tungeweza kuyapangilia yakawa katika maeneo mbadala na italinda ardhi yetu ya kilimo, kwa sababu hatuna uwezo kama Serikali kuandaa maeneo mapya ya kilimo katika maeneo ya jangwa au maeneo ambayo hayana rutuba kuwa ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba kwamba la Wabunge wote wamelalamikia suala la kupatiwa vifaa, mpango wenu mzuri wa kuweka vifaa vya kupima kwenye Kanda haitoshelezi, tunaomba muwe na mpango, mtukopeshe wala hatuhitaji kwamba Serikali iweke bajeti ituletee bure, kila Halmashauri tukopeshwe vifaa ili sisi tutaendelea kulipa hilo deni la vifaa vya kupimia ardhi zetu, ili tupime viwanja vya watu, mashamba ya watu lakini pia vifaa vya kutolea hati miliki zile za kimila huko katika Halmashauri zetu. Hiyo itatupunguzia sehemu kubwa ya matatizo ili wananchi wote waweze kupata huduma ile muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hapo naomba kwamba kuna ile asilimia ambayo kodi ya ardhi inapolipwa ile Wizara basi iwe badala ya kufika Hazina na huko Halmashauri iweze kukata moja kwa moja ili tuweze kuyapangia matumizi ya ile fedha ambayo tunawasaidia Wizara kukusanya ile kodi ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna migogoro mingi ambayo sasa hivi kwa sababu Serikali haijatoa tamko maalumu kwamba watu kuvamia maeneo ya hifadhi, kuvamia maeneo mbalimbali na katika mali za watu Serikali iweke msimamo kwamba nini maamuzi ya Serikali na mahali ambapo Serikali huko nyuma tayari ilishakosea kwa kuanzisha vijiji ndani ya maeneo ambapo ni hifadhi au ni mashamba mengine ya lease, basi mgogoro huo utatuliwe mapema ili kila mmoja aweze kuishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pia naomba iangaliwe namna kwa wale waliokuwa Watanzania ambao sasa wamebadilisha uraia wao kwenda nchi zingine ili huko wapate haki, pawe na mpango maalum. Najua Wizara ya Ardhi mnao mpango masuala ya derivative rights, lakini waweze kurudi nyumbani angalau kama wanataka kuwekeza kujenga nyumba na kadhalika, waweze kuwa na haki hiyo kwa sababu kuna diaspora kubwa ambao wana uraia wa kule lakini ni Watanzania kiasili na wao waweze kupata haki yao kuja kuwekeza hapa nyumbani bila kuwa kupitia TIC. Labda anataka kuweka nyumba tu ya kuishi na nini na wengine wana ndugu zao ambao wapo hapa, lakini wakirithishwa ile mali ni haki yake kurithi ya mzazi wake au baba yake au babu yake, akija hapa inakuwa ni mgogoro kwa sababu yeye tayari anao uraia wa nchi nyingine. Watanzania wengi wanakosa fursa hiyo naomba muangalie namna kwa wale ambao walikuwa Watanzania wameenda wamebadilika sasa kuwa raia wa nchi nyingine aendelee kuwa na haki maalum, kuna haki zingine wasipewe lakini angalau hii ya kwao ya kuja kuwekeza humu nchini basi pawe na mfumo mzuri waweze kuja na kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu na ninaendelea kusisitiza kwamba hivi vifaa tumeona pale nje mmetuletea aina nyingi, pawe na mpango maalum tuweze kukopa kila Halmashauri kwanza itakuwa fursa ya kumaliza migogoro ya watu kupatiwa hati miliki na hati za kimila, lakini pia maeneo mengi yatakuwa yamepimwa, muhimu ni coordination baina ya Halmashauri zetu na Wizara, namna ya kuelekeza Maafisa Mipango Miji na namna ya kupanga makazi hata huko vijijini tunahitaji kupanga matumizi bora ya ardhi ili huko mbele tunakoelekea migogoro isiendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwanza kumshuku Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo. Nilichangia kwa kuongea, naomba nichangie kwa maandishi kwa eneo ambalo sikumalizia na kuweka kwa muhtasari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashauri Waziri wa Fedha aweze kupatiwa fursa tena ya kutoa msamaha wa kodi katika eneo la miradi ya kitaifa na miradi mbalimbali ya jamii ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; marekebisho ya sheria yaje mapema Bungeni turekebishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nashauri Serikali iangalie namna bora ya kuweka vyanzo vya mapato vya uhakika katika Mfuko wa Mazingira. Si tozo mpya bali kutokana na ada, tozo, ushuru na leseni mbalimbali asilimia fulani ziende katika Mfumo wa Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la kuwa na vyanzo vya mapato kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI na watu wenye mahitaji maalum. Pia halmashauri zitoe mikopo kutokana na ile asilimia 10 ya vijana na wanawake kwa wenye mahitaji maalum na wenye Virusi Vya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Serikali iangalie ushauri wa kuongeza Sh.50/= kwa kila lita ya mafuta ili iwe Sh.100/= kwa kila lita ya mafuta. Pia kuondoa kodi kwenye mitambo ya kuchimba maji, pampu za maji zenye mita na pampu za maji za sola. Hii itafanya gharama za vifaa hivyo na huduma ya uchimbaji kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sheria ya Manunuzi, Serikali iboreshe kwa kutoa waraka wa kuangalia value for money pamoja na bei halisi. Maeneo ya kuangalia ni eneo la TEMESA, TBA, Taasisi ya Uchimbaji wa Mabwawa na Visima pamoja na maeneo yote tunapopata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nashauri maeneo yote ambako Serikali inapata mapato au maduhuli zitozwe kwa njia ya kielektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali, kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana anayoifanya pamoja na Serikali yake yote. Nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na timu yake nzima kwa kazi nzuri wanayofanya, tunaendelea kukuombea na tunasema endelea na mfumo huo huo ili tuweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba kushauri; pamoja na kuwa kazi inayofanyika ni kubwa na nzuri lakini bado kuna nafasi kubwa ya kuboresha na hayo ambayo tutayasema ili mjitahidi kuboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ninaomba lile suala la Serikali kurudisha madaraka ya Waziri wa Fedha na Mipango ya kusamehe kodi, tulifuta huko nyuma kwa ajili ya matumizi mabaya ya msamaha huo. Mimi naomba haya madaraka yarudi ili miradi mingi ambayo tunapata msaada katika Serikali Kuu, Halmashauri zetu na taasisi mbalimbali iweze kuisaidia Serikali. Leo hii inashindwa kupata msamaha wa kodi na miradi mingi inakwama kutokana na suala hilo.

Kwa hiyo, mimi naamini kwenye hii Serikali ya Awamu ya Tano hakuna atakayethubutu kutumia hayo madaraka vibaya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba mje na mpango huo tuirudishe ili miradi ambayo inakwama kutokana na suala la kusamehewa kodi, basi na yenyewe tuweze kufaidi misaada hiyo ambayo tunapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninapenda nikupongeze kwa kuondoa kodi ya Motor Vehicle Licence, Sheria ya Traffic Act. Hapa tunajichanganya, zile ni sheria mbili tofauti, Traffic Act umeondoa kwa kulipa kila mwaka, haijaondolewa kwa ujumla, umeondoa utalipa mara moja tu kwa gari inaposajiliwa. Hii nyingine ni excise duty ilikuwepo, shilingi 400 umeongeza hii shilingi 40, hongera sana kwa sababu fedha hizo hizo ndizo zitakazoboresha barabara na huduma nyingine ambazo hawa ambao tunalalamika kwamba mafuta ya taa na nini, kwamba wanafanyaje, kwa sababu hiyo barabara ambayo inaenda huko kijijini ndiyo inalipiwa na fedha hiyo. Mimi nasema ungeongeza zaidi ili huduma hizi nyingine zote ziendelee kuboreshwa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba katika ule wigo ulipotaja vile viwanda ambavyo vitapata msamaha umetaja sekta kama nne; ya mafuta, ya ngozi, lakini ninaomba mtanue wigo zaidi ili sekta nyingine pia kama za kilimo, mifugo, uvuvi pia viwanda vidogo vidogo. Hao wakubwa watakuja watapitia TIC watapata huo msamaha, lakini hivi viwanda vidogo vidogo vya Watanzania wenye mtaji mdogo pia na wenyewe mngewapatia huo msamaha kwenye capital goods na wakati wanataka kuanzisha. Hiyo kodi ikiondoka nina uhakika kwamba huko tunakotaka kuelekea kwenye uchumi wa viwanda tutaweza kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tutakapoelekea kwenye Finance Bill nitaomba maeneo mengi yale niliwapongeza kwamba mmeondoa kodi nyingi kwenye sekta ya kilimo; lakini kwenye sekta ya mbegu bado kuna kodi nyingi ambazo zimeachwa, lakini pia tuangalie mfumo mzima kwamba tunafanyaje. Tumesamehe, kwa mfano kwenye mbolea inayotoka nje ya nchi, pongezi kubwa kwa hilo, lakini je, kiwanda cha ndani, huyu wa nje kama amesamehewa yote na wa ndani anaendelea kulipa je, si kwamba tunaendelea na mfumo ule ule kwamba tutaua viwanda vya ndani kwa kuruhusu vitu kutoka nje kuingia bila kodi? Kwa sababu huyu wa ndani hawezi kutoza VAT, inputs zake hawezi kudai, kwa hiyo bado utaendelea kuumiza viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mimi naona kwenye sera yetu panatakiwa kufanyika mabadiliko makubwa na wigo wa kukusanya kodi bado ni mdogo. Nikupongeze kwamba mmesema kila Mtanzania ambaye anafanya biashara hata kidogo aendelee kulipa kodi, elimu kubwa iendelee kutolewa ili kila Mtanzania aweze kulipa kodi. Muhimu ni kwamba sekta isiyokuwa rasmi bado ni kubwa na inaendelea kukua; mimi ninaomba, sijaona kabisa kwenye bajeti nzima sehemu ambapo mtaweza kufanya sekta isiyokuwa rasmi ihamie kuwa rasmi kwa sababu ile sera haijakaa vizuri na incentives zile hazipo, na muhimu kwenye uwekezaji wa aina yoyote ni zile incentives.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningependa kuona kwamba vyanzo vingine vyote vipya tuendelee kuviangalia na tuweze kupata kodi ambapo badala ya kutegemea hao wenzetu ambao wanatupa misaada kwa sababu ile pia ni kodi ambayo wamelipa kule kwao. Tanzania kwa rasilimali tuliyonayo tunaweza kujitegemea na inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mimi naunga mkono hoja na ningeendelea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, niombe na nichangie kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo. Naomba nichangie Wizara hii muhimu kwanza kwa kuwapongeza Waziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wote pamoja na wasaidizi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri kwanza kuiomba Serikali iondoe kodi kwenye mitambo ya kutengeneza barabara lakini pia utasaidia katika sekta ya maji kwenye mabwawa. Kodi itozwe kwenye kazi na siyo kwenye kuingiza mitambo pia kuondoa kodi kwenye miradi yenye maslahi ya kitaifa na ya kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri pia Wizara kupitia Serikali iangalie namna ya kuhakikisha suala la NEMC - utafiti wa mazingira katika suala la minara ya simu. Miradi mingi hukwama kwa ajili ya Environmental Impact Assessment (ripoti ya masuala ya mazingira). Serikali iangalie namna ya kuboresha mawasiliano hasa data ili twende na teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze, ushauri wangu wa kuendelea kutumia taasisi za kwetu kama TTCL kwa shughuli za Serikali. Kazi yao sasa ni nzuri sana na tuendelee kuboresha kwa kuwekeza.

Naomba pia tuangalie namna ya kuboresha mapato kupitia mitandao hasa utumiaji wa simu za ndani na hasa fedha zinazopitishwa humo. Sim Banking leo hii hatupati mapato ya sekta hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri Wizara iwekeze kwenye viwanja vya ndege na bandari, zaidi huduma za kuhifadhi bidhaa ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwa na cold rooms. Huduma za kuwekeza bidhaa hizo kwa hali ya hewa inayoweza kuratibiwa uwanja wa KIA inahitaji kwa haraka huduma hiyo kwa ajili ya kusafirisha maua na mboga mboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na baraka zake kwetu. Naomba nichukue fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu akiongoza timu yake ya wataalam kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ndiyo Wizara mama ambapo Wizara zote zingine zinategemea ufanisi wa Wizara hii. Naamini Wizara ya Fedha inaweza kufanya vizuri zaidi ili matumaini ya Watanzania yaweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishauri Waziri wa Fedha alete mabadiliko ya sheria Bungeni kumrudishia uwezo wa kutoa msamaha wa kodi katika miradi mbalimbali na pia katika misaada tunayoweza kupata kama Serikali, taasisi zinazotoa huduma na Halmashauri zetu. Naamini tulikosea kufuta uwezo wa Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa kodi. Kelele nyingi za wawakilishi na pia taasisi zetu kupunguza masuala ya kodi siyo katika hii miradi na misaada midogo, walikuwa wanalenga misamaha mikubwa kama ya kwenye migodi, utafutaji wa madini (research) na uchimbaji wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii imekuwa kero tukipata misaada kutoka kwa wafadhili ambao hawako tayari kutoa au kulipia kodi, mfano magari ya wagonjwa, miradi ya maji, madaraja, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, huduma za elimu na zingine. Muhimu ni kuweka wazi misamaha hiyo na tulio wengi tusiadhibiwe kwa ajili ya wachache waliofanya vibaya kwa kutumia vibaya mfumo wa msamaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishauri Wizara iongeze wataalam zaidi katika Idara ya Mipango. Idara hii ndiyo inayoweza kuleta mafanikio makubwa sababu ya kushauri kwenye sera na pia kuboresha mapato ya Serikali hasa kutanua wigo wa kukusanya kodi (tax base).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri waajiriwe wataalam hasa kutoka private sector wenye uzoefu ili kuleta mabadiiko ya fikra (mind set change) ndani ya Wizara. Jukumu la Wizara ni kusimamia kukusanya mapato yote ya kikodi na yasiyo ya kikodi pia matumizi ya mapato hayo pamoja na kuweka mipango ya miradi ya maendeleo. Kwa sasa sera yetu imefanya Tanzania iwe moja ya nchi ambapo sekta isiyo rasmi (informal sector) kuendelea kukua kwa kasi na formal sector kuendelea kushuka. Hatukusanyi kodi katika sekta isiyo rasmi na kuumiza sekta rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara iangalie uwezekano wa kuleta mabadiliko ya sheria ambayo itaweka muda wa ukomo wa kodi, tozo au ushuru ambayo haijakusanywa kwa muda maalum na siku mkusanyaji akizinduka usingizini anataka alipe kutoka siku sheria ilipotungwa. Sio kila mwananchi anajua sheria, ni wajibu wa Serikali ngazi zote kutafsiri sheria na kutoa elimu kwa wakati. Kwa sasa wananchi wanalalamika sana, pamoja na baadhi za Halmashauri kutoza kodi, tozo za miaka mingi iliyopita, uzembe wa kutokusanya wakati huo siyo wao. Mfano ni Motor Vehicle License, SDL, Withholding Tax na je, hao waliosababisha kutokukusanya wamechukuliwa hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Wizara iangalie namna ya kuongeza fedha katika taasisi zilizo chini yake kuna TADB na TIB. Pia kupitia Sheria ya Kodi kuleta mabadiliko ya kupunguza kodi mbalimbali ili compliance iwe kubwa na fine na adhabu kwa watakaodanganya iwe kubwa. Wizara iangalie namna ya kuhakikisha mifuko iliyokuwa chini yake kama Mdhibiti wa Mahesabu ya Serikali na Mkaguzi Mkuu (CAG), Mahakama na Bunge zifanyiwe utafiti zaidi ili kazi zao kama mihimili tofauti na huru zifanikiwe. Pia Msajili wa Hazina, Kitengo cha Utafiti na Uendelezaji (R&D) kiboreshwe ili taasisi zote chini yake ziweze kuleta faida na kuchangia katika uchumi wa Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichangie kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na uzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya hasa katika sekta hii ya elimu, sayansi na teknolojia. Nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi yake ya kutoa elimu ya msingi bure. Watanzania wengi hasa wenye kipato cha chini watapata haki ya elimu.

Mheshimwa Mwenyekiti, naomba nishauri katika maeneo machache; moja, nashauri Serikali iangalie namna ya kurejesha asilimia mbili iliyochukuliwa mwaka 2014 kutoka Skills Development Levy ya asilimia nne kwenda kwenye Bodi ya Mikopo kwa ajili ya dharura. Kwa sasa urejeshwaji wa mikopo hiyo ni nzuri basi asilimia mbili irudi kwenda kwa skills development (VETA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya vyuo vyetu vya ufundi (VETA) ni mbaya sana na tunahitaji mageuzi makubwa. Leo hii kila kitu ni kutumia teknolojia ya computer (IT). Kwa mfumo wetu wa sasa wa VETA tunatumia mfumo wa miaka ya nyuma ambapo hazifundishi kutumia IT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ufundi kwa mfano wa magari (umeme) yote inategemea mfumo wa IT wa kutumia diagnostic equipment. Umeme wa majumbani pia vyombo na vifaa vyenye (sensors) kutumia programu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawahitimu wengi wa vyuo vikuu (shahada)/wenye digrii. Kwa sera ya viwanda tunahitaji kuwa na mafundi (technician). VETA kwa mfumo wa kisasa unaweza kuwa mkombozi wa ajira kwa Watanzania. Mfumo wa elimu wa apprentice utasaidia Watanzania mbalimbali wenye ujuzi wa ufundi kupata elimu rasmi na kujiboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Wizara kutukubalia VETA Manyara kupata mradi wa Wajerumani wa mafunzo ya apprentice. Tunashukuru pia kwa kutuweka katika bajeti ya kukarabati na kuongeza karakana ya Babati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia mnapogawa fedha za miradi ya kukarabati mgawe kwa uwiano kwa kufuata idadi za shule katika Halmashauri na idadi ya watoto na mazingira. Sisi Halmashauri ya Babati tumepata shule moja tu, shilingi 60,000,000; Halmashauri yenye shule mbili kati ya 137. Wilaya zenye shule 30 zimepata shule mbili zaidi ya shilingi 170,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri COSTECH ipatiwe vyanzo vya kudumu ili angalau ipate shilingi bilioni 100 kwa mwaka. Hali ya utafiti nchini ni mbaya na sehemu kubwa inategemea ufadhili wa nje kwa kuendesha tafiti zao; tukumbuke mfadhili hutoa anapokuwa na maslahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kirudishwe chini ya Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji kwa usimamizi, wataweza kukitendea haki kwa kufuatilia kwa karibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe unafuu wa kodi ya mapato kwa mashirika na wadau kwenye michango yao ya kwenye sekta ya elimu au huduma za jamii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue furasa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na uzima. Nichukue fursa hii pia kumpongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu akiongoza wataalam wa Wizara kwa kazi nzuri sana wanayofanya kusimamia sera na wajibu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kama ifuatavyo:-

(i) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iangalie namna ya kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa na hasa fursa za uwekezaji ndani ya nchi yetu lakini pia fursa za Watanzania kuwekeza katika nchi za Afrika Mashariki na nchi zingine.

Leo hii Watanzania wakihitaji msaada wa kupata taarifa mbalimbali za fursa hizo za kibiashara nje za Afrika Mashariki au zingine ni ngumu kupata. Wizara iboreshe Kitengo cha Uchumi Wizarani na kuwezesha Balozi zetu zote katika Kitengo cha Uchumi ili waweze kutusaidia kufanya biashara kirahisi na kujua utaratibu wa sheria na kanuni. Nipongeze Kitengo cha Protocal kwa msaada mkubwa wanaotupa sisi Watanzania tukisafiri.

(ii) Wizara ihamasishe Watanzania kutumia fursa mbalimbali zilizopo kibiashara.

(iii) Wizara ya Mambo ya Nje ishirikiane kwa karibu na Wizara ya Elimu kuboresha mitaala ya elimu na kusaidia kupata vifaa na nyenzo za kufundishia masomo ya mahusiano ya kimataifa katika vyuo vyetu. Hali ni mbaya sana na wanaohitimu hawana viwango vya kufanya kazi waliosomea.

(iv) Wizara iangalie namna ya kuwatambua diasporas wetu hasa kwa wale waliokuwa Watanzania na sasa wamechukua uraia wa nchi nyingine (Persons of Tanzanian Origin) kwani wengi wao wamechukua uraia wa nchi nyingine kutokana na mazingira yao ya kupata huduma za kijamii kama afya, elimu, ajira na fursa zingine ambazo wasingezipata bila uraia wa huko. Nchi yetu haina utaratibu wa kisheria wa kuwa na uraia wa nchi mbili hivyo Watanzania hao walilazimika kuchukua uraia wa huko.

Pia Wizara ingeangalia utaratibu wa kisheria wapate kitambulisho kitakachowapa fursa ya kuwa watu wenye asili ya Kitanzania na waweze kuishi nchini na kuwekeza hapa kama Watanzania wengine ila wakose fursa ya kupata ajira ya Serikali, kuwa afisa au shughuli yoyote katika masuala ya ulinzi na usalama, kuchagua au kuchaguliwa (kupiga kura au kupigiwa kura).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itafanya hao waliokuwa Watanzania kuwa na fursa ya kuwekeza nyumbani (Tanzania) kwa urahisi sana. Nchi nyingi zimefanya hivyo na kuongeza mapato ya nchi kwa kuwapa haki hao waliokuwa Watanzania. Leo hii hawaruhusiwi kumiliki ardhi na wakitaka kuwekeza wanatakiwa kufuata utaratibu sawa na mtu asiye raia (non Tanzanian).

(v) Wizara hii iangalie namna ya kuwapatia Wabunge mafunzo mbalimbali hasa kuhusu itifaki kama walivyokuwa wanafanya miaka ya nyuma. Mafunzo haya yatolewe kwa Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wawakilishi na Wabunge wa EALA.

(vi) Kwa Wabunge wa EALA, muda huu ambapo bado hawajaanza kazi rasmi, wangepewa mafunzo maalum ya kuijua Afrika Mashariki, mikataba mbalimbali, nchi yetu inatarajia wafanye nini katika uwakilishi wao huko EALA pamoja na mambo mengine ambayo Wizara inaona ni muhimu wapate elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na kupongeza Wizara na timu nzima ya wataalam pamoja na Balozi wetu wote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo. Nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya yeye na Serikali yake. Vile vile naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Kapteni Mkuchika na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, Katibu Mkuu na timu yake nzima kwa kazi nzuri wanayofanya. Naomba kushauri baadhi ya masuala ili kuboresha huduma na hasa katika Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni suala la OPRAS; ni muhimu sana jambo hili lisisitizwe ili uadilifu na uwajibikaji uwe wa hali ya juu. Pia naomba Wizara iboreshe Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, sekretarieti hii hufanya kazi nzuri na kubwa, ingetumika pia kwa ajili ya ajira kwa taasisi za watu binafsi iwe sehemu ya kuwa benki ya wanaotafuta ajira. Wote wanaohitaji ajira waweze kuweka rekodi zao pale na wenye kuhitaji watumishi basi wapate orodha kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri suala la watumishi wanaokaimu kwa muda mrefu utoke mwongozo na pawe na kanuni juu ya nafasi ya kukaimu; Babati Vijijini tunao wakuu wa idara wanaokaimu zaidi ya saba. Pia Serikali iangalie suala la kukaimisha watumishi bila utaratibu na inaleta gharama kwa halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la huduma kwa mteja (customer charter); suala hili likumbushwe kila wakati na itangazwe kwa wananchi, kila idara, taasisi iweke wazi suala la huduma kwa mteja (customer charter). Nashauri pia Sekretarieti ya Maadili ya Umma pia iweze kuweka mfumo wa kielektroniki ili tuweze kujaza fomu hizo kwa njia ya kielektroniki na pia tukihitaji kupata taarifa zingine na kujaza taarifa muhimu tuweze kujaza kwa njia ya kielektroniki (update information). Nashauri pia kuwa na mfumo mpya wa urasimishaji wa uendelezaji wa biashara (One Stop Center) hii itasaidia kupunguza gharama urasimu na muda wa kupata huduma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nichukue furasa hii kwanza kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na kuleta matumaini makubwa. Migogoro mingi imeendelea kupungua na tunaendelea kuomba kwamba waendelee kufanya kazi hiyo kubwa ili migogoro ya ardhi sasa hapa nchini iishe. Tunaomba ile migogoro hasa ile ya Babati ambayo Wabunge wenzangu wote tumekubaliana kila anayepata fursa aisemee, ile ya vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gidejabug wale wananchi wapatiwe maeneo mbadala kuna mapendekezo tumeshaleta, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ifanyie kazi ili Wizara ya Ardhi iweze kutoa vibali, lakini pia ile migogoro ya mashamba ya kule Kiru yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu Mheshimiwa Waziri ninaomba utuletee sheria mpya hapa ndani ya hii Sheria ya Ardhi kipengele cha kuzuia matumizi ya ardhi ya kilimo ilindwe kisheria ili ukitaka kubadilisha matumizi ya ardhi ya kilimo ije hapa Bungeni kwa sababu maeneo mengi yenye rutuba Tanzania yamebadilika matumizi sasa yamekuwa makazi, viwanda na matumizi mengine ambapo hayo matumizi mengine tungeweza kuyapangilia yakawa katika maeneo mbadala na italinda ardhi yetu ya kilimo, kwa sababu hatuna uwezo kama Serikali kuandaa maeneo mapya ya kilimo katika maeneo ya jangwa au maeneo ambayo hayana rutuba kuwa ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba kwamba la Wabunge wote wamelalamikia suala la kupatiwa vifaa, mpango wenu mzuri wa kuweka vifaa vya kupima kwenye Kanda haitoshelezi, tunaomba muwe na mpango, mtukopeshe wala hatuhitaji kwamba Serikali iweke bajeti ituletee bure, kila Halmashauri tukopeshwe vifaa ili sisi tutaendelea kulipa hilo deni la vifaa vya kupimia ardhi zetu, ili tupime viwanja vya watu, mashamba ya watu lakini pia vifaa vya kutolea hati miliki zile za kimila huko katika Halmashauri zetu. Hiyo itatupunguzia sehemu kubwa ya matatizo ili wananchi wote waweze kupata huduma ile muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hapo naomba kwamba kuna ile asilimia ambayo kodi ya ardhi inapolipwa ile Wizara basi iwe badala ya kufika Hazina na huko Halmashauri iweze kukata moja kwa moja ili tuweze kuyapangia matumizi ya ile fedha ambayo tunawasaidia Wizara kukusanya ile kodi ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna migogoro mingi ambayo sasa hivi kwa sababu Serikali haijatoa tamko maalumu kwamba watu kuvamia maeneo ya hifadhi, kuvamia maeneo mbalimbali na katika mali za watu Serikali iweke msimamo kwamba nini maamuzi ya Serikali na mahali ambapo Serikali huko nyuma tayari ilishakosea kwa kuanzisha vijiji ndani ya maeneo ambapo ni hifadhi au ni mashamba mengine ya lease, basi mgogoro huo utatuliwe mapema ili kila mmoja aweze kuishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pia naomba iangaliwe namna kwa wale waliokuwa Watanzania ambao sasa wamebadilisha uraia wao kwenda nchi zingine ili huko wapate haki, pawe na mpango maalum. Najua Wizara ya Ardhi mnao mpango masuala ya derivative rights, lakini waweze kurudi nyumbani angalau kama wanataka kuwekeza kujenga nyumba na kadhalika, waweze kuwa na haki hiyo kwa sababu kuna diaspora kubwa ambao wana uraia wa kule lakini ni Watanzania kiasili na wao waweze kupata haki yao kuja kuwekeza hapa nyumbani bila kuwa kupitia TIC. Labda anataka kuweka nyumba tu ya kuishi na nini na wengine wana ndugu zao ambao wapo hapa, lakini wakirithishwa ile mali ni haki yake kurithi ya mzazi wake au baba yake au babu yake, akija hapa inakuwa ni mgogoro kwa sababu yeye tayari anao uraia wa nchi nyingine. Watanzania wengi wanakosa fursa hiyo naomba muangalie namna kwa wale ambao walikuwa Watanzania wameenda wamebadilika sasa kuwa raia wa nchi nyingine aendelee kuwa na haki maalum, kuna haki zingine wasipewe lakini angalau hii ya kwao ya kuja kuwekeza humu nchini basi pawe na mfumo mzuri waweze kuja na kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu na ninaendelea kusisitiza kwamba hivi vifaa tumeona pale nje mmetuletea aina nyingi, pawe na mpango maalum tuweze kukopa kila Halmashauri kwanza itakuwa fursa ya kumaliza migogoro ya watu kupatiwa hati miliki na hati za kimila, lakini pia maeneo mengi yatakuwa yamepimwa, muhimu ni coordination baina ya Halmashauri zetu na Wizara, namna ya kuelekeza Maafisa Mipango Miji na namna ya kupanga makazi hata huko vijijini tunahitaji kupanga matumizi bora ya ardhi ili huko mbele tunakoelekea migogoro isiendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kwa kunipa afya njema hata kupata fursa ya kuchangia.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anafanya na pia wasaidizi wake wote. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na viongozi wote wa Wizara na Taasisi zake zote kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya katika kuboresha Sekta ya Elimu.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo machache katika kuboresha sekta hii. Kwanza naomba kuishauri Serikali kurejesha upitiaji wa Sheria ya Skills Development Levy (SDL) ya asilimia mbili ya SDL iliyopelekwa Bodi ya Mikopo mwaka 2014 kwa dharura. Muda sasa umefika kurejesha hiyo asilimia mbili iende kuboresha taasisi zetu za ufundi. Kwa hali yetu ya uchumi na tunakoelekea, hasa kwa sera yetu ya viwanda na uhitaji wa wataalam katika viwanda (technicians) na pia ujuzi katika maeneo mbalimbali ambayo yatatoa fursa kubwa za ajira badala ya Watanzania wengi kwenda katika elimu ya ajira ya utawala na usimamizi tu (white collar jobs), tuboreshe shule zetu za ufundi, vyuo vya ufundi na pia kuwa na mfumo kuanzia sekondari ya kufundisha ujuzi mbalimbali ili tuweze kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, pili, katika sayansi na technolojia, naomba Serikali iweke bajeti ya kutosha; na pendekezo lilikuwa kwa asilimia moja ya bajeti yetu. Nchi haiwezi kwenda bila sayansi na teknolojia. Bajeti inayopelekwa katika utafiti ni ndogo sana. Bajeti yote haikidhi hata haja ya kituo kimoja ya utafiti. COSTECH iwezeshwe zaidi, kwani ndiyo chanzo kikubwa na pekee nchini kinachoratibu masuala ya utafiti. Fedha zile shilingi tano kwa unit ya TTMS zirudishwe. COSTECH walikosa baada ya Wizara kuwa na muundo tofauti. Ni chanzo cha uhakika cha mapato kwa ajili ya kuboresha utafiti.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naomba nimshukuru Mwenyekiti Mungu kwa kunipa fursa ya kuchangia leo, lakini pia niipongeze Wizara kwa kuleta Mpango, ni Mpango huu wa miaka mitano ambao tunanyofoa vipande vipande kila mwaka ili kuutekeleza mpango huu. Hakuna cha ajabu na hakuna kitu kipya, ni mambo tuliyoyapitisha mwaka wa kwanza tulipoingia Bungeni. Muhimu ni vipaumbele, mimi naona tumepishana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vipaumbele kuna mambo ambayo tungebadilisha, yale ya kusogea huko mbele na yale ambayo tungeanza nayo. Muhimu kabisa katika mpangio huu, na kitu ambacho sijaona kama kimewekwa katika mpango wa mwaka huu ambao tunataka kuutekeleza, (2018/2019) ni suala la utafiti. Hakuna nchi inayoweza kuendelea bila ya kuwekeza katika utafiti katika Nyanja zote, iwe kilimo, mifugo, uvuvi, elimu, sayansi, afya na masuala mengine yote kwa kweli hata bajeti ambayo huwa tunatenga kwenye utafiti huwa inakuwa ni ndogo sana, haitoshi hata kwa kitengo kimoja. Katika vituo 16 vya utafiti vile vifaa vyote sasa hivi vimekaribia kuwa vimepitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sehemu nyingine ambayo ingeweza kutusaidia sana ni katika masuala ya hali ya hewa, tungewekeza zaidi huko. Kama tunataka wakulima wetu wanufaike tukiwekeza kwenye masuala ya hali ya hewa, kama ilivyo kwenye nchi za wenzetu unaambiwa kesho mvua itanyesha muda wa saa fulani, hata wakulima wetu, mimi ninaweza kwenda kupanda mbegu leo kwenye udongo wakati mkavu lakini nina uhakika wa mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Serikali ikae pamoja na kuangalia suala zima la uratibu. Hapa kila Wizara inajitegemea kama vile ni Serikali yenyewe; mfanye kazi kama timu. Niwapongeze juzi Mawaziri wannne walipozindua ule mpango wa viwanda kila mkoa na viwanda, huo ndio uratibu inatakiwa mkae mfanye kazi kwa pamoja. Tuna mifano mingi, tumechimba visima leo mwaka wa tatu umeme haujafikishwa, lakini ingekuwa mnafanya kazi kwa kuratibu Wizara zote, idara zote zinafanya kazi kwa pamoja miradi ile ingekuwa inatekelezwa na mafanikio yangekuwa yanaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kuwa na sera na mfumo wa kodi ambao ni stable, ambao haubadiliki kila wakati. Mwaka huu tunaweza tukapitisha jambo fulani watu wakaona sera imekaa vizuri na masuala ya kodi, tax regime imekaa vizuri mwakani tumebadilisha tunarudisha, hiyo ndiyo inafanya watu warudi nyuma na kwa mfumo huu hatutoweza kuendelea kwenye masuala ya viwanda tunayotarajia kwamba itashika kasi. Ni muhimu viwanda vile vidogo na vidogo kabisa mngevi-regulate; haya mambo ya Osha, fire, nani mngewaondoa mtu akishalipa leseni yake na muanzishe one stop center kila mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwenye sheria mtu asipojua sheria haikupi kinga mahakamani lakini tungekuwa na center moja; mimi nikienda uniambie ni kiasi fulani nikilipa masuala mengine yote wao ndio watanielekeza. Kila mkoa kuwe na one stop center watu wafanye kazi na viwanda vidogo na nini kama mlivyo-regulate kwenye uzalishaji mdogo vivyo hivyo fanyeni kwenye viwanda, pasiwe na urasimu mkubwa utakuwa na mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu kuliko yote pia ni kuwekeza kwenye Benki ya TADB. Wakulima hawahitaji kupewa sadaka wala ruzuku, wekeni pesa kwenye benki tukakope na si wajanja wajanja. Wakulima wanaweza kukopa, wakafanya shughuli zao wakalipa hizo hela.Hiyo benki leo haina hela. Mkulima wa kati na wa juu kama anashindwa kukopa pale mdogo atapataje? Kwa hiyo, ninaomba tuwekeze pale na tuhakikishe kwamba benki hiyo inakuwa na mtaji wa kutosha.

Mheshimiwa Mawenyekiti, lingine tukirudi kwenye suala la utafiti ni cost of production. Utakuwa na viwanda, lakini kutokana na utitiri wa hizi regulatolly bodies yaani taasisi za udhibiti unakuta tozo zao zinakuwa ni nyingi kiasi ambacho hata tukizalisha gharama ya ile bidhaa yetu siku zote itakuwa juu kuliko bidhaa ambayo unaagiza kutoka nje ya nchi. Leo hii hata mfumo wetu ukiagiza bidhaa kutoka nje nyingi hazina kodi, hasa zinazotoka kwenye nchi za Afrika Mashariki na Kati. Hayo usipoyafanyia kazi hata tukiwa na viwanda hapa bidhaa zetu hazitauzika. Kwa hiyo, ni vizuri ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango mfanyie kazi suala la utafiti ili tuweze kupata…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo na pia kupata fursa kuchangia. Niipongeze Serikali kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya na pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wote wa Wizara hii, tumeona mabadiliko makubwa ya mtazamo na fikra (mind set change). Nipoongeze na kumshukuru Mheshimiwa Rais kuanzisha Wizara ya Uwekezaji na kazi yao kubwa ni kufanya uratibu baina ya Wizara zote kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi na bora katika uwekezaji ambayo ni muhimu kwa suala la biashara na pia viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri katika maeneo machache; kwanza Serikali iharakishe kutekeleza Blue Print. Jambo hili linahitaji uratibu wa Wizara zote na utafanya gharama za uzalishaji zipungue bila kuathiri ubora na viwango. Nashauri Serikali iunganishe Taasisi za Udhibiti kuwa mbili, muundo wa juu na muundo wa chini. (Upper Stream Regulatory Authority na Lower Stream Regulatory Authority) na taasisi hizo zifanye majukumu yao ya udhibiti na zisiwe taasisi za kuwa chanzo cha mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii taasisi hizi ndizo kikwazo kubwa cha kufanya urahisi wa kufanya biashara (Ease of doing business) na pia (cost of doing business) kupunguza gharama za uzalishaji. Pia tunashauri Maafisa Biashara ngazi ya Taifa, ngazi ya Mkoa, ngazi ya Wilaya ndio wawe sehemu ya kutoa leseni na ushauri wote unaohitajika kufanya biashara yoyote (one stop center). Pia pawe na kanuni ya kubana utoaji wa adhabu (fine) ili kwanza mtu apewe fursa ya kurekebisha kabla ya tozo ya adhabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali iwekeze katika kuelimisha kupitia taasisi zetu za elimu ya ufundi, SIDO, TEMDO na pia katika Taasisi ya Utafiti - TIRDO. Bila utafiti hatutaweza kuwa na mafanikio. Tunaomba SDL, fedha zote asilimia nne na nusu 4.5% ziende katika kuboresha taaluma ya ujuzi kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu Serikali tuwekeze katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kukuza ajira, biashara na kupatikana kwa malighafi ya viwanda vyetu. Muhimu kupata utafiti wa bidhaa tunazoagiza kutoka nje ambazo tunaweza kuzalisha ndani ya nchi ili tuweze kuzalisha ndani ya nchi badala ya kuagiza nje. Leo hii Serikali itaona sekta isiyokuwa rasmi inakua kwa kasi kubwa na sekta rasmi kushuka kwa sababu ya kutokuwa na mazingira na usawa wa kufanya biashara. Napongeza na kushukuru jitihada zote za Wizara na wataalam wote. Siku zote changamoto ndogo ndogo zitakuwepo na ni kuangalia namna ya kuboresha na kuondoa hizo changamoto.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nami nichukue fursa hii kuchangia katika Kamati hizi tatu muhimu sana. Moja naomba wakati ujao ikiwezekana kwa baadhi ya hizi Kamati zingepewa umuhimu siku zingeongezwa ili watu wengi zaidi waweze kuchangia. Ni muhimu kwa kuleta tija ili Serikali iweze kupata mafanikio makubwa sana na wapate mawazo ya Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja naomba niishauri Serikali; tumeanza vizuri sana, ndoto ya kuwa na nchi ya viwanda na inawezekana, lakini naomba kabisa Serikali itathmini upya, tuangalie mahali ambapo gharama za uzalishaji. Tusipoweza kuangalia gharama za uzalishaji kwa ajili ya tozo, kodi na ushuru mbalimbali ambao unatozwa na taasisi za udhibiti na taasisi mbalimbali ili mtu aweze kuzalisha hatutaweza kufikia hayo malengo; kwa sababu hatimaye mfanyabiashara anachohitaji ni faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na hasa kwa mfano kwenye Afrika Mashariki au SADC ambazo zinaingia bila kodi, halafu huku ndani ya nchi unakuwa na utitiri wa kodi na tozo mbalimbali, ndoto hiyo hatutaifikia. Tuna hizi taasisi za udhibiti ziko nyingi sana lakini pia ushuru na kodi mbalimbali ambayo inafanya bidhaa zetu za Tanzania zisiweze kushindana kutokana na gharama kubwa ya uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mmoja tu net ambazo zinazalishwa hapa ni kiwanda kikubwa kuliko chochote cha Afrika A to Z. Pia mbolea tunayoizalisha ndani ya nchi unakuta kodi mbalimbali ambayo ile import tax wanatozwa hawaruhusiwi ku-claim back lakini neti ikitoka nje ya nchi au mbolea ikitoka nje ya nchi haina kodi. Sasa viwanda vyetu tunavilinda au ndio tunavimaliza? (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, naomba Serikali iangalie suala hili kwa mapana zaidi na tuwe na one stop center. Kwamba mtu akija akitaka kukata leseni ya biashara yoyote akishakata hapo basi gharama na tozo zote kila kitu viwe hapo hapo ili baadaye pasiwe na kurudi nyuma, kwamba tunadaiwa, leo umekata leseni umeanza biashara, baada ya miaka mitatu anakuja mtu wa OSHA, anakuja NEMC, hizo zote zinakuwa ni kero. Natakiwa nikishalipia hapa; si kila mtu anajua sheria zote na kwenye sheria wansema kutokujua sheria sio kinga, lakini sio wananchi wote watajua hizo sheria, ni vizuri tuwe na one stop center kama TIC iwe ngazi ya mkoa, ngazi ya wilaya mtu akishalipa wagawane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la muhimu ni Serikali kuwa na e-government na malipo yote yaendelee kufanyika kwa kupitia hiyo hiyo TRA lakini wabadilishe mfumo. Kwa mfano kodi hii ambayo tumekubaliana ya majengo na kodi ya mabango hayo yote mtu akishalipia pale basi risiti ikitoka na halmashauri yangu iwe inajua kwamba mtu fulani amelipa kiasi fulani na mgao wa Serikali kuu ni kiasi fulani, mgao wa halmashauri yangu ni kiasi fulani na mgao ambao unatakiwa kwenda mpaka ngazi ya chini ni kiasi gani. Kila mmoja akijua hiyo tutawezakufanikiwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine kubwa ni kuwekeza kwenye utafiti. Sisi tunaimba tu pesa zote za utafiti asilimia kubwa zaidi ya asilimia 99.8 zinatoka nje ya nchi, za kwetu za ndani hakuna. Ilikuwa tumekubaliana 1% ya total budget imeshindikana, tumekuja thirty billion imeshindikana. Bila utafiti hatutaweza kusonga mbele, hivyo ni vizuri tuwekeze kwenye utafiti hasa kwenye sekta ya kilimo, madini kote huko hata kwenye biashara inataka tuwe na fedha za kutosha za utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Tume ya Ushindani (FCC) pia iweze kufanya kazi yake vizuri iangalie mambo haya yote lakini mbali na hilo iharakishe lile suala la CETAWICO ambayo inazalisha mvinyo hapa Dodoma iweze kuchukuliwa na breweries ili wakulima wa zabibu hapa Dodoma waweze kunufaika na Watanzania tunywe mvinyo ambao unatoka Tanzania, si huu wa sasa hivi ambao asilimia kubwa unatoka South Africa na sawa na juices nyingi ambazo tunanunua concentrates kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie kwamba bidhaa zote ambazo tunaweza kuzalisha ndani ya nchi tuwe na muda maalum; kwamba ndani ya miaka miwili au mitatu tutakuwa tunazalisha hapa nchini ikiwa ni pamoja na hizo juice concentrates, mafuta ya kupikia, kwa sababu baada ya bili kubwa ya mafuta ya magari au mafuta ya dizeli ya pili inayofuata kwa gharama kubwa tunayoagiza ni mafuta ya kula ambayo ni vegetable oil tunayoagiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni sukari; na haya mambo yote tunaweza kuzalisha hapa nchini kwa gharama nzuri, wakulima wetu wakanufaika na pesa zote hizo zikabaki ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie suala la budget cycle. Ni muhimu sana sisi tuangalie kubalisha budget cycle kama Bunge kwa sababu kipindi tunakaa Kamati ya Bajeti na Kamati zingine zote kupitia hizi bajeti hakuna mabadiliko tunayoweza kuleta zaidi ya asilimia moja au mbili. Tungekaa sisi kuanzia Agosti, Oktoba ili kama kuna inputs zote, mawazo yote yaingizwe ili halmashauri zetu na taasisi zote zinapokwenda kupanga bajeti zao basi wajue hii itapanda, itashuka au haitakuwepo; hiyo itatusaidia sisi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba tuangalie kwenye sekta ambayo ni rasmi na ambayo isiyo rasmi (formal and informal sector). Hii informal sector yaani sekta isiyo rasmi inazidi kukua kutokana na haya masuala ya kodi, tozo na usumbufu mbalimbali. Ingekuwa tumeweka viwango maalum na mtu anajua akishakuja kulipa sehemu moja hatasumbuliwa tena kila mtu atapenda kuwa formal. Pia kila mtu atapenda kwamba mambo yake yaendelee vizuri, lakini yule ambaye hatakiwi kuwa na rekodi yeyote unakuta ana unafuu sana kuliko yule ambaye anaweka record ndiye anayekamuliwa mpaka dakika ya mwisho. Kwa hiyo naomba na hilo pia lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye masuala ya madini kuna mengi ambayo tumezungumza kwenye Kamati kama tulivyokuwa tunasema kwamba, ni vizuri kodi nyingi ambazo ziko ni vizuri tupate muda wa kutosha ili tuweze kutoa mawazo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine muhimu ni suala la kulinda ardhi yetu. Nina uhakika kwa kazi nzuri sana ambayo anafanya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ambaye ameondoa kero nyingi pia atatusaidia kuhakikisha ardhi za kilimo zinalindwa. Tukiwa hapa Makao Makuu yetu ya Dodoma, nina uhakika atalinda mashamba yote ya zabibu yasibadilishwe kuwa makazi na utakuwa mfano kama nchi zingine unakuwa na mashamba ndani ya mji, inakuwa ni green belt. Mheshimiwa Waziri najua hicho kitu anakiweza na nina uhakika kwamba hiyo kazi tutafanikiwa vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kupanua wigo wa kodi, tusipopanua wigo wetu wa kodi hatuta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kuchangia taarifa nzuri ya Kamati na kushauri kuboresha katika maeneo mbalimbali kwa kila sekta.

Kwanza, nishauri suala la mbolea, bado tozo ya USD 10,000 kwa mbolea mpya ingeondolewa na Serikali, hii imefanya aina nyingi za mbolea hasa za maji kwa ajili ya (horticulture) kilimo cha mbogamboga na matunda kukosekana sokoni. Pia Serikali iangalie jinsi ya makampuni za mbolea zitoe huduma za ugani (soil testing) kupima udongo badala ya kuiachia Serikali kama Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri tuwekeze kwenye utafiti, zaidi kwenye mbegu ambapo asilimia 75 za mbegu za mahindi zinatoka nje ya nchi, mbegu za mazao ya kahawa mafuta kama alizeti, soya na mbogamboga asilimia 95 zinatoka nje ya nchi. Tuna uwezo wa kuzalisha mbegu zetu nchini, pia hulinda viwanda vyetu vya mbolea na mbegu zinatozwa kodi, tozo, ushuru na ada mbalimbali tofauti zinazoingizwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Serikali iweke bajeti ya kutosha kuboresha vituo vyetu 16 vya kilimo kwa kuongeza vifaa vya kazi na nyenzo mbalimbali. Makutupora wamalizie kuwekeza katika vifaa vya tissue culture, tuwekeze kusindika mazao yetu nchini badala ya kusafirisha mazao ghafi kama korosho, kahawa, pamba mbaazi mikunde na kadhalika. Serikali kupitia ASA na vituo vya utafiti, wapewe bajeti ya kuagiza miche ya matunda ambayo tunaweza kuzalisha nchini kama (apple, peas, plums, citrus, grapes) hata jamii ya michungwa, embe, nanasi, zabibu zikiletwa chache, tutazalisha nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iondoe au kupunguza kodi, tozo, ushuru na ada nyingine katika sekta ya kilimo ikiwemo kodi ya ardhi, malimbikizo makubwa mfano; ni VAT, Income Tax, Withholding Tax, Land Rent, OSHA, Fire Rescue, TBS, TFDA, Weights and Measurements, WCF na nyingine nyingi, uzalishaji nchini inakuwa gharama kuliko kuagiza kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishauri Serikali kuondoa kodi kwenye kuagiza (Importation) kwa mitambo ya kuchimba maji (Borehole drilling equipment) pamoja na mitambo ya kuchimba mabwawa ya kuvunia maji (Excavators, Bulldozers, Shovels Rollers) itasaidia kupunguza gharama za uchimbaji visima na mabwawa kama ushindani utakuwepo kutokana na mitambo kuwa mingi. Tutoze kodi kwenye kazi na siyo Importation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nasisitiza iongezwa Sh.50 kwa maji vijijini na kuundwa kwa Wakala wa Maji Vijijini. Nashauri tuondoe kodi ya pampu za sola za maji (Solar water pump) ili kuondoa adha ya akinamama kuchota maji mbali na makazi yao pamoja na kupunguza gharama za kusukuma maji kwa kutumia mafuta ya diesel na umeme kwa miradi midogo ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugani wa madawa ya mimea na mifugo pia zitolewe na makampuni yanayouza hayo madawa. Serikali iondoe kodi kwenye madawa, chanjo vifaa tiba vya mifugo na chakula cha mifugo (Supplements) na kurudisha VAT kwenye chanzo cha mifugo ili waweze kupata unafuu wa kupata taxes.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubali turidhie hizi itifaki zote tatu na ninapongeza Serikali kwa kuja nazo ili iweze kurahisisha katika utekelezaji wa majukumu yetu yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika eneo lile la kwanza la Montreal, ni vizuri sana, nashukuru kwamba turidhie hiyo itifaki, lakini muhimu ni Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha kwamba tunaendelea kuzuia na tunaendelea kuzingatia sheria zilizowekwa kwa manufaa yetu sisi Watanzania. Tusije tukawa dumping ground, yaani eneo la kutupa taka ambazo baadaye itakuwa ni sumu kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hilo pia kuna Mjumbe mmoja alichangia kwamba sheria za kodi ndiyo zinafanya sisi tununue vitu chakavu; hiyo sio sahihi. Sahihi ni kwamba tumeweka kodi kubwa kwenye bidhaa ambazo ni used, yaani bidhaa chakavu ina kodi 20% extra ili tusinunue bidhaa chakavu, kwa hiyo hiyo record ikae vizuri; Serikali imefanya vizuri sana, bidhaa zilizotumika zina kodi ya 20% ili kulinda mazingira yetu, kwa hiyo hiyo record ikae vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa upande wa WTO, naomba pia itifaki hii Wabunge wote turidhie ili iweze kufanya kazi. Lakini muhimu kuliko yote, tutakaporidhia hizi itifaki za kimataifa ni vizuri sisi kama ndani ya nchi pia tuhakikishe kwamba tunatenda yale ambayo tumekubaliana huko kimataifa. Kwa mfano kwenye hii ya ufanyaji biashara, ease of doing business, ni vizuri yale yote ambayo tumekubali tutafanya kimataifa huku ndani ndiyo tuwe na dirisha na tuwe tunafanya vizuri zaidi ili huko nje tuwe wa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwenye hizo bring business naomba Serikali ije na hiyo Sheria ya Blueprint itekelezwe kwa asilimia 100, bidhaa zetu ziwe na gharama ndogo ya uzalishaji kutokana na regulatory bodies nyingi. Na pia kuingia kwenye mfumo mzima wa kufanya kazi kwa kupitia internet na urahisi wa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa Itifaki ile ya SADC, naunga mkono sana kwa sababu changamoto hizi zote ambazo zinahusiana na masuala ya mazingira hakuna namna tunaweza kujitenga kama kisiwa. Kwa hiyo, tufanye kazi kwa pamoja. Sheria zote za nchi za SADC zikiwa zinafanana na itifaki tukikubaliana nayo naamini kabisa tutaweza kusaidia nchi yetu kufanya kazi kwa pamoja kwa sababu tunashirikiana katika mambo mengi. Kwa hiyo, itifaki hizi zote naomba Wabunge wote tuunge mkono ili ziweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ombi langu pia; zile itifaki zingine ambazo tuliwekewa kwenye orodha ya ratiba kwamba zitakuja, basi ziletwe, kwa mfano International Solar Alliance na itifaki nyingine. Basi na hizo zenyewe zije zote turidhie ile tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja itifaki zote. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napongeza Kamati zote mbili kwa kazi nzuri na taarifa nzuri waliyotuletea. Nawaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kurudia kwamba Bunge lingeangalia mfumo wa namna ya kuboresha ili hizi Kamati tuweze kufanya kazi kwa pamoja, Kamati mbalimbali na Waheshimiwa Wabunge hawako kwenye Kamati hiyo wakitaka kuchangia pawe na namna ya kuweza kuchangia kwa sababu kwa hii siku moja Waheshimiwa Wabunge wachache, haya mawazo yetu bado hayatoshi kuboresha hizo taarifa za hizo Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la afya, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaendelea kufanywa hasa hii ya kujenga vituo vya Afya. Ombi langu ni kwamba kama kuna maeneo kwenye Kata, Wilaya au Vijiji wana ramani tofauti ambazo zinakidhi vigezo vyote na ubora wa majengo, basi hizo ramani waruhusiwe kama gharama za ujenzi zitapungua, tusiwe na mfumo ambao lazima zote zifanane nchi nzima. Watu wanaweza kuwa na design nzuri na wakaweza kujenga vituo vyao ambavyo vinapendeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye sekta ya afya suala la non-communicable disease (magonjwa yasiyoambukizwa) tulichukulie kwa uzito mkubwa sana. Juzi tulipofanya high camp kule Magugu kwenye watu 600 tumekuta watu zaidi 160 wana kisukari hawajijui, kuna watu zaidi ya 200 na kitu wana pressure hawajijui. Kumi kati yao ilibidi walazwe siku hiyo hiyo kwa sababu hawajui. Sasa ni jambo ambalo ni vizuri tulifanyie kazi kwa haraka na watu wapewe taarifa na wapewe elimu namna ya kujikinga na haya magonjwa na nini wafanye kama tayari wameshapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la lishe bora. Mimi naomba Serikali iangalie upya suala la lishe bora, tutilie mkazo elimu itolewe, lakini pia tukifika kwenye Finance Bill, mwaka 2017 tuliweka kodi kwenye virutubisho vya kuongeza kwenye unga, mafuta, vitamini A. Vile virutubisho baada ya kuweka kodi, wale wote ambao walipewa misaada na USAID na wengine ambao wana viwanda vya kuongeza hivyo virutubisho, wamepunguza au wameacha kabisa kuweka. Kwa sababu huwezi kuuza unga au hayo mafuta kwa bei ya juu zaidi kuliko bei ya unga ya soko. Ina maana wenye hasara ni sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina kiwanda hata kimoja, kwa hiyo, tunaposema isipokuwa kwa Serikali; Serikali haina viwanda. Kwa hiyo, wangerudisha tu ile na waangalie namna ya kuratibu kwamba hivyo virutubisho watu waendelee kupewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuomba kwamba tuangalie namna ya kuboresha na kuongeza bajeti ya COSTECH ili suala la tafiti mbalimbali liendelee kupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara safari hii ikija ituwekee bajeti kwenye Kitengo cha Ngozi pale KCMC ambacho ndiyo kitengo pekee Tanzania kinachotengeneza madawa, sunscreen yaani lotion kwa ajili ya albino (watu wenye ulemavu wa ngozi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka yote kuna taasisi ambayo inafadhili, inatoa huduma pale, inatengeneza, wameweza kufikia maalbino 4,000 lakini ingependeza kama Serikali ingeweka bajeti kidogo ili badala ya 4,000 wafikie hata zaidi kwani wako zaidi ya 64,000. Kwa hiyo, bado tuna hatua ndefu na Serikali ingeunga mkono pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwenye suala la elimu, Serikali iangalie namna ya kurudisha ile 2% kati ya nne ambazo zinazotakiwa kwenda VETA kwa ajili ya Skills Development Levy (SDL). Leo hii 2% inaenda kwenye Bodi ya Mikopo. Tuangalie chanzo kingine cha kupata fedha kwa ajili ya Bodi ya Mikopo ili zile 4% zote ziende kwenye skills development kwa sababu nchi ambayo tunatarajia kuwa na viwanda, VETA ina kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunatakiwa kubadilisha mitaala kwa sababu leo hii mitaala mingi bado ni ile ya tindo na nyundo na sasa hivi tunatakiwa kubadilika kwenda kwenye IT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hata mashine ya kushona lazima ujue namna ya ku-program. Sasa ni vizuri hata hao mafundi umeme, mafundi gari wote hao wanafundishwa VETA kwa ule mfumo wa zamani, watakuja kukosa ajira na wazazi wao wamechangia fedha nyingi. Ni vizuri tubadilishe mfumo, vitu vyote sasa vinaenda na mfumo wa IT yaani wa computer. Kwa hiyo, tuhakikishe kwamba kuanzia Juni safari hii suala la hiyo VETA na namna ya kubadilisha hiyo mitaala tuwe tumeshakamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni muhimu ni suala la vyuo vyetu. Mimi ningependekeza, Chuo kwa mfano cha Sokoine ambacho ni cha Kilimo na Mifugo kingerudishwa Wizara ya Kilimo badala ya kubaki Wizara ya Elimu. Kwa sababu kwa Wizara ya Elimu inafanya kazi nzuri lakini inaona watoto wote wale ni sawa tu, bajeti inapelekewa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Wizara inayohusika ikisimamia chuo chake, kama Chuo cha Madini, kiko chini ya Wizara ya Madini, kile chuo kingekuwa kinapata msukumo mkubwa na Wizara ingeweza kukiangalia kwa ukaribu zaidi. Kwa hiyo, naomba suala hilo tuliangalie kwa umuhimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala la michezo, ningeomba pia Mheshimiwa Waziri angetoa tamko kwamba huko tunapokuwa na michezo katika ngazi ya Kata na ngazi ya Wilaya, hivi vyama vya mipira au vyama vya michezo vinadai sasa walipwe asilimia fulani ya fedha ambazo watu wamechangishana ili gharama za uendeshaji wakati hawajawahi kuchangia hata shilingi moja, wala kutoa elimu wala jambo lolote. Ukianzisha tu ligi, wao wanataka waingilie kati na wanataka walipwe hizo fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashauri Mheshimiwa Waziri kwa hilo angetoa tamko ili kama wamewekeza, wana haki ya kudai, kama hawajawekeza, waachane kabisa na kudai watu wakichangishana kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine pia ningependa tuliangalie ni kwenye suala la elimu. Ni vizuri sasa tuangalie huko tunakoelekea tunahitaji kuwa na mafundi wengi kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo.

Pia tuondoe dhana nzima kwamba tukiwa na viwanda tutaajiri watu 4,000 au 5,000. Viwanda vya kisasa vyote vinaajiri watu wachache, skilled labour na ni vizuri sasa katika hizi taasisi zetu za kufundisha tubadilike na sisi tuwe tunaenda na mitaala hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba TFDA kwa suala hilo hilo la afya sasa, wawe na mashine za kupima. Leo hii mboga mboga nyingi ambazo zinaletwa sokoni, unakuta zimepigwa dawa leo, jana, ndani ya siku mbili, tatu zinapelekwa sokoni. Ndiyo maana magonjwa mengi haya ya cancer na nini yanatokea. Hizo mashine zingekuwa zimewekwa katika maeneo mbalimbali hasa katika masoko makubwa ya mboga mboga inaweza kusaidia...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeza kwa kazi nzuri Kamati iliyofanya. Naomba nichangie kwanza kwa kuliomba Bunge liangalie namna ya kuratibu kazi za Kamati ili Wabunge wapate fursa ya kuchangia wanaotoka Kamati zingine ili taarifa na maazimio ya Kamati kuzishauri Serikali namna ya kutatua changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika shughuli za Kamati nichangie suala la afya. Niipongeze Serikali kwa kuboresha na kufanya vituo vya afya ambavyo vitakidhi haja ya huduma za afya katika ngazi ya kata. Nashauri Wilaya zisizo na hospitali kwa sasa wasikimbilie kwenye hospitali bali waboreshe huduma za afya ya msingi katika kata mbalimbali itaharakisha huduma kuwa karibu na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali ikubali sehemu ambapo Kata, Wilaya au Kijiji wana ramani zao za majengo ambayo yanakidhi mahitaji bila kuondoa ubora wa majengo waruhusiwe kuwa na ramani zao (different design in architecture).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie gharama za vifaa tiba na madawa yanayosambazwa na MSD kama tunafanya bulk procurement mbona bado kwa watu binafsi bei ni karibu sawa au wakati mwingine ni bei ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba suala la non communicable diseases (magonjwa yasiyoambukizwa) litiliwe mkazo na kupewa umuhimu kama Kamati ilivyoshauri. Elimu juu ya magonjwa hayo itolewe kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la lishe bora, Serikali iondoe kodi kwenye virutubisho vya kuchanganya kwenye unga na mafuta vya kupitia. Leo hii ni kwa taasisi za Serikali tunazopata huo msamaha na Serikali haina hata kiwanda kimoja, suala la lishe bora hatutafikia kwa tamaa za kupata kodi. Wenye viwanda wameacha kuweka hivyo virutubisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri Serikali iangalie namna ya kuongeza bajeti ya COSTECH; bajeti ya utafiti na maendeleo. Tupange asilimia moja ya bajeti au bilioni 120.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie kwa bajeti hii kuchangia kituo cha kutengeneza mafuta ya wenye ulemavu wa albino pale KCMC. Kitengo cha ngozi tuwekeze katika dawa za asili (homeopathy).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu nashauri tuangalie namna ya kurudisha asilimia mbili ya SDL inayoenda Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwenda VETA. Bodi itafutiwe chanzo kingine. VETA ipate haki yake ya asilimia nne. Pia tubadilishe mitaala ya kuwa ya mfumo wa IT, kutumia kompyuta. Leo hii hawa vijana tunaowafundisha kwa teknolojia ya zamani watakosa ajira, leo mfano haya magari ya kisasa lazima ujue kutumia kompyuta, huwezi kurekebisha bila teknolojia, hata fundi umeme wa nyumba, taa na vifaa vingi vinatumia sensors, kama hawajui IT (masuala ya kompyuta) namna ya ku-programme elimu yao haitahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwekeze kwenye utafiti na maendeleo, COSTECH tupange angalau bilioni 120 kwa mwaka; asilimia moja ya bajeti nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Vyuo Vikuu Maalum kama SUA, virudishwe chini ya Wizara husika ili vipate huduma za karibu zaidi. Chini ya Wizara ya Elimu haviwezi kupata kipaumbele na Wizara kwa haki inatenga bajeti sawa kwa wote. Chuo cha Nelson Mandela kingeenda Wizara ya TAMISEMI pamoja na VETA zote, vyuo vya afya viende Wizara ya Afya. Aidha, vyuo vikuu viwe specialized na hata suala la field katika masomo yao lingepata unafuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo. Lakini pia niwapongeze Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yao nzima kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya, ningependa kushauri katika baadhi ya maeneo ambapo ushauri huu ukizingatiwa naamini kwamba tunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta hii ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tunahitaji kuwekeza zaidi katika vocation training yaani katika masuala ya ufundi wa hasa katika shule zetu za VETA. Mwaka 2014 Serikali ilileta hoja Bungeni kwa dharura kwamba ilikuwa inahitaji kutumia zile fedha za Skills Development Levy (SDL) ile four percent; asilimia mbili iende kwa ajili ya kusaidia kutoa mikopo kwa wanafunzi kipindi hicho hali ilikuwa ni mbaya na kweli ilisaidia Watanzania wengi. Sasa kwa ajili ya urejeshwaji wa ile mikopo ni mzuri sana na unakusanya fedha nyingi, naomba ile two percent ambayo inaenda kwenye Bodi ya Mikopo ya Skills Development Levy irudi sasa na ile asilimia zote nne ziweze kutumika kwenye VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA yetu bado tunaenda na mfumo ule wa zamani teknolojia ya zamani, leo hii kwa sera yetu ya viwanda tunahitaji kuwa na mafundi mchundo (technicians) ambapo leo hii wengi wenye degree tunao, lakini hao ngazi ya technicians hatuna kabisa yaani ni wachache mno. Sasa ni vizuri VETA zote zikaboreshwa kwanza kwa vifaa na vifaa vingi vinatakiwa tubadilishe pia mfumo uendane na masuala ya IT, leo hii hata fundi wa umeme wa nyumbani, fundi wa magari suala la kupima na ile teknolojia ya zamani imepitwa, leo hii ni lazima wajue namna ya kufanya programming, kwenye magari yote ya kisasa lazima unaenda pale unatumia diagnostic equipment ambapo VETA zetu hazifundishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa majumbani kote siku hizi unaona kuna sensors, watu kama hawajui ku-program hata akipata ufundi pale VETA akitoka mtaani hatapata kazi kwa sababu ni masuala ya kutumia IT. Kwa hiyo, ni vizuri tuwe na transformation kubwa, mabadaliko makubwa kwenye VETA kwenda na wakati na njia pekee ya kwenda na wakati na kuwekeza zaidi na kuwekeza zaidi kunahitaji fedha kwa hiyo, ile asilimia mbili ambayo inakwenda Bodi ya Mikopo tuirudishe ije huku na VETA ikifanya vizuri Watanzania wengi watakuwa wanaweza kujiajiri kwa sababu Serikali haina uwezo wa kuajiri watu wote ambao wanahitimu vyuo. Sasa ni vizuri tukahakikisha kwamba VETA zetu zote zinapata, ile fedha na irudishwe na ziboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ile programu ya entrepreneurship iweze kurudishwa, mafundi wetu ambao wamejifunza wenyewe kwa kufanya practicals, yaani kujiunga na maeneo mbalimbali na mafundi wenye uzoefu sasa waweze kufanya programu ndogo ndogo za muda mfupi ili na wao sasa wahitimu na wawe na vyeti na wanaweza kujiendeleza kusoma. Kwa hiyo, suala la VETA ni muhimu sana.

Mheshimiwa, lakini lingine lilikuwa ni suala la kuhakikisha kwamba tunakuwa na mfumo wa kuhakikisha masuala ya utafiti yanapata fedha, kwa sababu masuala ya sayansi na tekonolojia yako katika Wizara hii, mimi nilikuwa napendekeza ule mfumo, kwa mfano, ile pesa ya TTMS ambayo ilikuwa COSTECH, leo hii ile fedha imeondolewa kwa sababu COSTECH imehama Wizara sasa haipo kule kwenye wizara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba tuangalie na vyanzo vingine kwasababu ahadi huko ilikuwa tupate one percent ya bajeti nzima kwenda kwenye utafiti lakini ikashindikana, tukaahidiwa kwamba itakuwa bilioni thelathini; lakini hata hiyo kwenye bilioni thelathini fedha iliyokwenda kwa maximum ni bilioni kumi na mbili. Na kwenye utafiti mbali na tuseme upande kilimo tu ambao unahitaji zaidi ya bilioni thelathini kwa haraka lakini utafiti wa mambo mengine yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo suala la kupatiwa fedha kwenye mfuko wa utafiti yaani COSTECH ni muhimu sasa Serikali wakati tunakuja kwenye finance bill tuwe na vyanzo mbadala na vyanzo vingine ili tuhakikishe kwamba tunafanyaje ili angalau kwa mwaka waweze kupata si chini ya bilioni mia moja ili tuweze kusaidiana katika masuala mbalimbai ya utafiti; na bila utafiti hakuana kitu ambacho kitaweza kuendelea ndani ya nchi hii. Kwa hiyo ninaomba wakati Waziri anapokuja basi watueleze kwamba wamepanga vipi, kwamba suala la COSTECH kupatiwa fedha za kutosha ili tuweze kwenda kwenye utafiti mbalimbali tunaweza kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lilikuwa binafsi naipongeza Serikali kwa kuanzisha mfumo huu wa kuboresha zile shule za zamani; na nilikuwa pia naomba muanze kuifikiria Shule ya Sekondari Gidas. Ni shule ambayo ilikuwa ni middle school enzi hizo, imejengwa 1947 nayo muifikirie. Lakini pia Wizara mnapopanga fedha kwenda kwenye shule mbalimbali za kuboresha muangalie Wilaya zenye shule nyingi na idai kubwa ya shule, isifanane na Wilaya ambazo zina shule chache yaani uwiano kati ya Wilaya ambazo zina shule nyingi na zile ambazo zina shule chache pia fedha ziende kwa uwiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa napenda Serikali iliangalie, niipongeze Serikali kwa kukubali kuwa na PPP kwenye mambo ya vyuo. Chuo cha kwanza cha PPP kiko Babati, Mamire pale. Ni mpango mzuri ambapo kwa kushirikiana na wadau mbaimbali wa private sector ambapo Mheshimiwa Jenista aliweza kuja kuzindua kile chuo mwaka juzi, nampongeza kwa hilo, alichukua mammuzi magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mngeweza kujifunza kutokana na Mamire, nina uhakika kabisa hivi vyuo vingine vyote ambavyo Serikali hamuwezi kufanya pekeenu, hebu mjifunze kutokana na hii PPP mnaweza kupata partners kwenye vyuo vyote, kama tunavyofanya kwenye afya, kwa kushirikiana na taasisi za dini. Kama mnaona hiyo moja ni nzuri, hiyo ya Mamire basi inaweza kuwa ya mfano. Vyuo vingine vyote vya ualimu na vyuo vikuu vikaingia kwenye partnership ili vizweze kusaidiwa na Serikali kwa namna ya kuboresha vyuo hivyo na namna ya kuboresha elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo ni muhimu sana; nilikuwa naomba Serikali ifikirie, Chuo Kikuu cha Sokoine, Chuo pekee cha Kilimo hapa Tanzania, nilikuwa naomba kiondoke kweye Wizara ya Elimu kirudi Wizara ya Kilimo kwa sababu Wizara ya Elimu wanafanyakazi nzuri. Wao vyuo vyote ni sawa kwao, watoto kwao ni sawa lakini ikipelekwa Kilimo kwa sababu ndio wenye uhitaji na wahitimu wa pale wote ndiyo wanakwenda kwenye sekta hiyo ya kilimo, mifugo, uvuvi na masuala ya misitu, wao wataionea umuhimu na watakuwa wanaisimamia kwa ukaribu zaidi.

Kwa hiyo, ningeomba ninyi mbaki kwenye sera lakini Chuo Kikuu hiki cha Sokoine mkirudishe Wizara ya Kilimo ili Wizara iweze kusimamia vizuri na mtaona kwamba ubora wa elimu pale na namna ya kusimamia na namna ya kufanikisha matokeo yatakuwa ni bora zaidi kwa sababu wao ndiyo walengwa na wao watakuwa na moyo zaidi wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo. Mimi naomba nitoe ushauri kwa Serikali, kuna maeneo mengi tu lakini naomba nianze kwa kusema Mheshimiwa Spika kama alivyounda Kamati mbalimbali za kuangalia kwa mfano Tanzanite, makinikia na masuala ya uvuvi wa baharini, angeunda Kamati ya kukaa pamoja Wabunge ili tuweze kuona maoni mbalimbali na tuweze kuishauri Serikali nini cha kufanya kwenye sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ningeomba Serikali kwa kupitia Waziri wa Kilimo waangalie Hansard za miaka ya nyuma ushauri mbalimbali ambao ulikuwa unatolewa miaka nenda rudi, je, upi umefanyiwa kazi? Kwa sababu haya mambo Wabunge tunayasema kila mwaka lakini kwa sehemu kubwa unakuta ushauri huo hautiliwi maanani. Haya mawili yakifanyika, nina uhakika kuna mengi tutakuja kufaidi huko mbele ya safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kusikitika kwamba bajeti ya sekta hii ya kilimo kila mwaka huwa inaendelea kushuka lakini bajeti kuu inaendelea kupanda na lengo lilikuwa bajeti iongezeke. Wizara ya Kilimo inafanya kazi yake vizuri sana ikiongozwa na Waziri, Naibu Waziri na wataalam wao, lakini hakuna uratibu au coordination baina ya Wizara ya Kilimo na Wizara zingine zote na ndiyo maana tunakwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu tuangalie tunataka kuelekea wapi. Moja, naomba tuwe na mkakati kwamba bidhaa zile kuu ambazo tunaagiza kutoka nje kwa mfano mchele, sukari, mafuta, mbegu hata hizi juice zote za matunda hakuna tone la juice ambayo tunakunywa inazalishwa hapa nchini, yote ni concentrates zinazotoka nje ya nchi wakati bidhaa zote hizi tunaweza kuzalisha hapa nchini.

Ni vizuri tuje na mkakati kwamba ndani ya hii miaka miatatu au minne mchele, sukari, mafuta, mbegu na vitu hivi tutazalisha ndani ya nchi, uwezo tunao na namna ya kufanikiwa hivyo ni kuwekeza kwenye utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuweki fedha kwenye utafiti na hata hii leo tukisema tunataka kujitosheleza kwa mafuta hatuna mbegu. Hatuna mbegu nzuri ambayo tunaweza kujitosheleza lakini hivyohivyo kwenye maeneo yote inatakiwa tuwekeze zaidi kwenye utafiti. Tuna vituo 17 vizuri na bajeti yake sijaona kwamba kila kituo kitapatiwa shilingi bilioni ngapi ili vituo hivyo viweze kuboreshwa kwa kuwekewa vifaa vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo narudia kusema kwamba hakuna coordination ndani ya Serikali. Leo hii vituo vya utafiti vinaomba msaada kutoka nje, vifaa vikija vinatozwa kodi, vifaa vinasaidia Mikocheni, Makutupora hapa kwenye umwagiliaji, vifaa vya umwagiliaji ambavyo havina kodi lakini wametozwa zaidi ya shilingi milioni 42. Sasa kama Serikali kwa Serikali inatozwa kodi, je, mwananchi na mkulima wa kawaida itakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima kitu anachohitaji ni uwezeshaji na mazingira mzuri ya kufanya kazi. Moja, Benki ya Kilimo ingepewa mtaji wa kutosha ile itoe mikopo wakulima waweze kununua vifaa vya kisasa kufanyia kazi na Mfuko wa Pembejeo uwezeshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hilo tufanye utafiti, ndiyo maana nasema hiyo tume au Kamati ya Bunge ikikaa iangalie masuala haya. Leo hii kodi na tozo tulizoainishiwa hapa nyingi tumeshangilia, lakini ipi yenye athari hata moja ambayo imemsaidia mkulima moja kwa moja, hakuna. Ukiangalia ushuru wa mazao iko palepale, ni ile tu kwamba waliokuwa wanakusanya 3% tumeshusha kwenye maandishi tu kutoka 5% kuja 3%, lakini mkulima wa kawaida hakuna mahali amefaidika na hilo. Zile kodi kumi na zaidi hakuna mahali mkulima zimemnufaisha moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwekeza zaidi kwenye ushirika na kutoa elimu vizuri hatutafika popote. Tumeanzisha commodity exchange leo mwaka wa tano hakuna maendeleo yoyote yanayofanyika pale. Stakabadhi ghalani pamoja na commodity exchange inaweza kuwa mkombozi
wa mkulima. Kwa hiyo, kwenye suala hilo pia, tuweke nguvu zadi, elimu itolewe, lakini Serikali iwe na nia njema, iwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba haya yote tunaweza kufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Wabunge wengi wamechangia masuala ya mbolea. Kwenye mbolea kuna upotoshaji mkubwa unatokea kwa sababu hatuelewi. Ni vizuri tukajua kwamba sawa na binadamu huendi hospitali ukapewa tu dawa, ukimueleza unaumwa kichwa, basi daktari anakupa dawa; hivyohivyo kwenye udongo unatakiwa ukapimwe. Pima udongo kujua mbolea inayotakiwa wataalam watakwambia tumia mbolea A, B, C, ndiyo utumie mbolea hiyo badala ya hii ya kwa ujumla tu. Watu wanapiga kelele kwamba Minjingu haifai, nini haifai, mkakati wa Minjingu ni kuzalisha mbolea ifikapo mwaka 2021 kiwanda kile kinachojengwa kule…

T A A R I F A . . .

MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wangekuwa kwanza wanaelewa kinachosemwa badala ya kurukia tu. Nimesema fanya utafiti kwenye udongo wako, ukifanya utafiti upate ushauri. Je, nyanda hizo zilifanya utafiti wa udongo wao wakaambiwa watumie aina gani ya mbolea? Kama utafiti huo upo ulete mimi niko tayari hapa kukulipa fidia wewe. Mimi niko tayari kulipa fidia kama ana utafiti wa udongo uliofanywa, nina uhakika hamjafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masuala yote lazima twende kwa utafiti na ndiyo maana nasema tuwekeze kwenye utafiti badala ya kila siku hapa kupiga tu kelele kwamba tufanye A, B, C. Twende kisayansi, kilimo ni sayansi, kilimo ni biashara, kilimo tukiwekeza vizuri ndiyo kitakomboa watu wote. Watanzania 100% wanategemea kilimo cha humu ndani kwa sababu tunategemea chakula kinachozalishwa humu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine muhimu sana inabidi Serikali ijipange kuhusu hili suala la regulatory bodies. Uzalishaji wa ndani ya nchi gharama inakuwa kubwa na ndiyo maana bidhaa hizi zinatoka nje ya nchi kutokana na hizi tozo, ushuru, ada na leseni mbalimbali ambazo tunatozwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tungekuwa tumeyafanya vizuri nina uhakika kwamba gharama za uzalishaji zitapungua na viwanda vingi huku ndani vitapata malighafi kutokana na sekta hii ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye yale mazao ambayo Wabunge wengi wameyazungumzia, leo hii Dodoma inaweza kuzalisha zabibu, lakini bado tunaagiza zabibu kutoka nje ya nchi wakati mvinyo na zabibu zingeweza kuzalishwa kwa wingi tukapata fedha hapa ndani lakini pia tukawa tuna-export. Tukiangalia upande wa migomba, Serikali ilikuwa na mpango mzuri wa kuzalisha miche ya tissue culture ipelekwe Kanda ya Ziwa. Suala lile lingefanyiwa kazi ungekuta ugonjwa ule ungepungua sana na wananchi wa kule wangekuwa wamepata chakula cha uhakika na ndizi za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nishukuru kwamba mpango wa kuanzisha LAPCOT mmeusema. Naendelea kushauri kwamba mpango huu uanzishwe mapema ili kanda ile pia ambayo inaweza kuzalisha mambo mengi sana katika hii sekta ya kilimo kwa ujumla wake na wenyewe waweze wapate mafanikio kama SAGCOT …

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake nzima ya wataalam kwa kazi wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ulikuwa ni mmoja, kama inawezekana, Serikali ikae tuangalie mfumo wa kubadilisha. Leo hii tunapanga matumizi kwanza halafu ndiyo tunaenda kuyatafutia mapato. Nashauri kwamba tuangalie namna kwamba tukusanye kwanza halafu ndiyo tuyapangie matumizi. Haya yote tungeondokana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tubadilishe budget circle, kwa mfano, badala ya sisi huu muda Wizara zote, taasisi zote, kila mmoja ameshapanga bajeti yake, kuleta mabadiliko hapa ni ngumu, yaani utafanya mabadiliko labda kwa asilimia moja au mbili. Tungekuwa tunakaa mwezi wa nane mpaka wa kumi na mbili ili mambo yote ambayo tunataka kushauri tuweze kushauri ili yaweze kuingia kwenye circle kama kodi za kupanda, kuna vitu vya kuondoa, nini kiongezwe ili wanaopanga bajeti zao wajue kabisa hii nikipanga inakubalika na kutokana na mapato ya uhakika ambayo tunatarajia, tutaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, la pili naomba Wizara ya Fedha, kwa sababu mapato na matumizi yote nyie ndio mnaya- control. Ni vizuri mngejitahidi kuangalia mifumo hii yote ya kulipa iliyopo, muangalie namna yaku-integrate yaani hizi mifumo yote iwe imeunganishwa ili kama Wizara ya Fedha, kwa mfano kuna dai lolote linaanza ngazi ya Halmashauri au kwenye Taasisi yoyote, nyie mnaiona moja kwa moja. Mpaka ifike hatua ya kuwafikia ninyi, kama kuna maswali mnakuwa tayari mmeshauliza.

Mheshimiwa Spika, vile vile iunganishwe na Ofisi ya CAG ili muda wa uhakiki uondoke na mambo yaende kwa haraka zaidi. Tukiwa vizuri na mifumo hiyo, nina uhakika kwamba masuala haya ya uhakiki na nini hayatakuwepo. Pia ni vizuri sasa tuendelee kuangalia namna ya kuboresha Chuo chetu cha Kodi ili iweze kufanya shughuli yake vizuri zaidi na elimu itolewe kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye suala la utafiti na maendeleo, ni vizuri tuwekeze zaidi kwenye utafiti ili kujua mifumo mbalimbali wapi tunaweza tukawekeza Serikali ikafanya vizuri na tukapata kodi nyingi zaidi na tuweze kuangalia mifumo mbalimbali. Kwa nini sekta isiyokuwa rasmi inazidi kukua na sekta rasmi inazidi kupungua. Ni vizuri tukiwekeza zaidi kwenye masuala ya utafiti. Haya yote yanawezwa kufanywa tukiwa na Tume nzuri na Tume ya Mipango ambayo itaweza kuratibu mambo yote hayo ili tuweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la kuangalia, kwa sababu yote hii iko chini ya Wizara ya Fedha, taasisi zote ambazo zinatoa elimu kwenye masuala ya kodi, masuala ya uhasibu, masuala ya clearing and forwarding, mara nyingi ukikuta wataalam wa uhasibu wakifanya makosa au wale wa clearing and forwarding anayeumia ni yule mteja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wakifanya makosa kwenye ethics, unakuta anayeumia ni mteja. Sasa hiyo inaleta changamoto kwa wateja kwani gharama zinapanda, zinakuwa juu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu ni suala lile la kuleta blueprint, kwa sababu Wizara ya Fedha ime-base zaidi kwenye makusanyo na tusipopata ile blueprint mapema bado tutakuja kuambiwa huko mbele kwamba tumeweka chini ya mwamvuli mmoja, lakini bado tozo na ada ambazo ni kero kwa biashara zetu zitaendelea kuwepo. Kwa hiyo, uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwanda hapa nchini gharama yake itakuwa ni kubwa na tutashindwa kushindana na bidhaa ambazo zinatoka nje ya nchi.

Kwa hiyo, kabla ya kufikia huko kwenye bajeti kuu ni vizuri jukumu hilo, Wizara ya Fedha iunganishe Wizara nyingine zote na Taasisi ambazo ziko chini yake, kama Serikali basi ije ituletee mapema ili tuweze kuifanyia kazi mapema.

Mheshimiwa Spika, mwisho pia kwenye suala zima hili la procurement, ni vizuri kwamba Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha muweze kuangalia kwamba hizi Taasisi zetu je zinafanya vizuri? Kwa mfano, PPRA na GIPSA ili tuweze kuleta mafanikio.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na uwezo wa kuchangia leo.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nashukuru na kupongeza jinsi Wizara inavyojipanga kwa kuleta mabadiliko katika mfumo wa kukusanya mapato na kusimamia matumizi. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watalaam wa Wizara hii kwa kazi nzuri sana wanayofanya.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya maeneo naomba nishauri ili kuboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika Wizara ya Fedha na taasisi zilizoko chini yake. Pakiwa na ufanisi katika Wizara hii ya Fedha, basi ufanisi katika Wizara zote utapatikana.

Mheshimiwa Spika, kwanza naishauri Serikali ikae pamoja na kufanya pendekezo la kubadilisha mfumo wetu wa bajeti pamoja na budget cycle. Nashauri tungepanga bajeti yetu ya matumizi baada ya kufanya makusanyo. Leo hii tunapanga matumizi ndipo tunatafuta hayo mapato. Tusipofikia malengo ya kukusanya kwa ajili ya matumizi tuliyopanga inaonekana tumefanya vibaya.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali iangalie namna ya kuibadilisha budget cycle. Leo hii baada ya bajeti mbalimbali kuandaliwa na kuletwa Bungeni, muda wa kufanya mabadiliko makubwa hayapo, kama kuna upungufu hakuna namna ya kuboresha.

Mheshimiwa Spika, hata Bungeni, Kamati ya Bajeti ingekaa kuanzia mwezi wa tisa hadi kumi na mbili (Septemba hadi Desemba) ili kuishauri Serikali pamoja na kupata maoni ya Serikali kabla ya kufanya maamuzi. Hii italeta utulivu (harmony) kwa sekta binafsi na wawekezaji wataweza kujua sera ya kikodi, tozo na ada mbalimbali na kujipanga kabla badala ya kapata taarifa za kushtukiza.

Mheshimiwa Spika, pia nashauri kutokana na malalamiko mengi yanayotokea kutokana na urasimu unaojitokeza katika suala la uhakiki, ningependa Serikali iangalie namna ya kuunganisha mifumo ya utoaji wa taarifa baina ya Wizara ya Fedha na Wizara zote hasa katika maeneo ya mapato na matumizi ili madai yanapokuwa yanatolewa (lodged) katika hatua ya kwanza kupitia Wizara yoyote au taasisi, Wizara ya Fedha iweze kuiona na waanze kuifanyia kazi mapema. Ikifika hatua ya Wizara ya Fedha kupitia Hazina kufanya maamuzi, watakuwa wana taarifa zote na pia watakuwa wameomba ufafanuzi mapema. Mifumo iwe integrated, hii ni pamoja na Ofisi ya AG.

Mheshimiwa Spika, pia nashauri mifumo hii iwe na design mapema ili ziendane na wakati na pia ziweze kuwa na uwezo wa kuingiliana (design, integrated systems). Naomba pia nishauri tuwekeze zaidi kwenye utafiti na maendeleo (research and development). Utafiti utasaidia kujua mwenendo wa biashara na uzalishaji, kujua gharama za uzalishaji ili kuweza kupanga mipango na sera bora ya fedha na kodi.

Mheshimiwa Spika, nashauri tuwekeze zaidi kwenye elimu ya kodi na mifumo yake. Tuboreshe Chuo chetu cha Kodi na kuwekeza zaidi kwenye elimu ya uhasibu, haki za walipa kodi, haki ya kujua nini ni sahihi na nini siyo sahihi. Leo hii wahasibu, mawakala wa kutoa mizigo katika bandari na mipakani (accountants and clearing agents) wakifanya makosa, adhabu inakuwa ya mteja na mara nyingi maafisa wachache wa TRA wanashirikiana na hawa wahasibu na wakala wa kutoa mizigo kwa maslahi binafsi kuwaumiza wateja wao.

Mheshimiwa Spika, pia nishauri task force ya kodi ifanye kazi yake mwaka mzima, wawe na ofisi ya kudumu na wakutane na wadau wa Kamati ya Bajeti. Hii itafanya waweze kujua kila sekta kwa undani. Pia muda wa kutosha kufanya utafiti iwe full- fledged office. Pia task force hii iwe na wajumbe zaidi wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, muhimu kuliko yote ni elimu kuanzia ngazi ya msingi juu ya ulipaji wa kodi, faida zake na elimu juu ya matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nashukuru. Kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo, lakini pia niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika Wizara hii, Ofisi ya Rais, (Utumishi) lakini pia Ofisi ya Rais, (TAMISEMI). Kwanza nawapongeza Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Mkuchika kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na wasaidizi wao, Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Kakunda, lakini pia Katibu Mkuu Ndugu Iyombe, Mzee Ndumbaro pamoja na watumishi wote kwa kazi nzuri na ngumu ambayo wanaifanya, lakini kwa kuhakikisha kwamba huduma hii ambayo Watanzania wengi wanahitaji na ambapo ndiyo engine nzima ya Serikali, wanafanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza niishukuru TAMISEMI kwa niaba ya wananchi wote wa Halmashauri ya Babati kwa fedha tulizopewa kwa ajili ya Kituo cha Afya Ngaiti. Tunashukuru sana, ni kituo ambacho kiko pembezoni na huduma ile itawasaidia watu wengi sana. Tumepata shilingi milioni 400 na kituo kinakaribia kukamilika, pamoja na ahadi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya vifaa, lakini pia fedha za P4R pamoja na ambulance kwa ajili ya Kituo cha Afya Magogo. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Jafo pamoja na timu yako nzima.

Pia tulikuwa na ombi kwamba Kituo cha Afya Magugu pale kinahudumia siyo tu Kata ya Magugu ya watu 30,000, lakini pia Tarafa nzima pamoja na baadhi ya nje ya Tarafa na pale ni highway, ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu wa Babati Mjini. Tunaomba iongezewe bajeti kwani kile siyo Kituo cha Afya, kile kimekaribia kufanana na hospitali na idadi ya watu wanaotibiwa pale bajeti ikiongezwa itaweza kutoa huduma bora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaiombea Hospitali ya Mrara pale Babati Mji kwa sababu na yenyewe pia inaendelea kuhudumia watu wengi wa Babati Vijijini, lakini pia sasa hivi Mji wa Babati unakua kwa kasi sana na ni highway baada ya kufungua hii barabara kutoka Dodoma kwenda Babati na ile ya Singida. Sasa hivi magari mengi yanapita pale na pindi ajali inapotokea, hospitali ile huwa inazidiwa.

Pia nilikuwa naomba wakati tunapopanga bajeti na baadhi ya miradi, pawe na uwiano kutokana na idadi ya kata na vijiji, kwa sababu kama tunagawa sawa kwa Wilaya zote, unakuta Wilaya kama yangu, Halmashauri yangu ina kata 25, vijiji 102 lakini kilometa za barabara kule ni zaidi ya 1,000 zinazohudumiwa na TARURA lakini mgao wa fedha tunaopata unakuta ni sawa na yule ambaye ana robo ya watu wetu, halafu robo ya kata na vijiji. Kwa hiyo, huo uwiano ninaamini kabisa mkijipanga, mtaenda vizuri. Pia nilikuwa naomba kwamba fedha zile za CDG tulizoahidiwa za maendeleo kwa mwaka 2017/2018 zije mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa naomba kwenye suala la TARURA naipongeza Serikali kwa kuanzisha chombo hiki baada ya Wabunge wengi kukisemea, lakini kama wenzangu wote walivyounga mkono kwamba tunaomba fedha zile asilimia za mfuko wa barabara badala ya kwenda asilimia 30 kwa 70 kama ilivyo sasa, basi iwe 50 kwa 50 ili TARURA iweze kufanya kazi yake vizuri. Pamoja na hiyo, tuendelee kuipatia TARURA rasilimali watu pamoja na nyenzo nyingine ili kazi yao iende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala la maji, nilikuwa naomba kwamba Wakala wa Maji Vijijini uanzishwe mapema. Mmeahidi kwamba mpaka mwezi wa Saba itakuwa tayari lakini bado naendelea kusisitiza kwamba ile shilingi 50 tuliyoomba kwa kila lita ya mafuta iendelee kuongezewa ili mfuko ule utune ili suala la maji liende vizuri. Vile vile pamoja na hayo yote, Serikali iendelee kufikiria kwamba bado kwenye suala la maji kuna vifaa kwa mfano vya kuchimba visima vya maji. Ile mitambo inapokuja inakuwa na kodi kubwa. Serikali ingeangalia namna ya kufuta kodi kwenye mitambo wakati inaingia, lakini wakati inapofanya kazi iendelee kutozwa kodi ili mitambo iwe mingi na watu wengi, huduma zisogee katika Wilaya zote na Mikoa yote ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye suala la maji, nilikuwa naomba Serikali iendelee kuangalia suala la e-water, mita za maji ambayo inatumia mfumo huu wa kielektroniki.

Babati Vijijini ni eneo la mfano, tayari tuna vijiji vitatu ambapo inaenda vizuri sana na wananchi wote wamezoea kutumia njia hiyo. Tukifanya vizuri naamini kabisa tatizo na changamoto hii ya maji inaweza ikaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni muhimu sana, naomba kwa sababu Ofisi ya Rais ndiyo ina Wizara zote hizi mbili ya Utumishi pamoja na TAMISEMI, mwangalie suala la watendaji, yaani kada ya chini, ngazi ya kijiji na kata, watumishi wote wanaohitajika huko, mhakikishe mnatoa vibali vya kutosha ili watendaji kwa mfano wa vijiji, kada ya afya, wale wa sekta ya kilimo wale wote ambao wanatakiwa ngazi ya kata na vijiji wawe wametosheleza badala ya kujaza huku juu. Kwa sababu tukiwa na Watumishi huku juu, ngazi ya Wilaya na Mkoa na huku Taifa na huko chini hakuna na maendeleo yote yanaenda kufanyika kule, unakuta fedha nyingi tunapoteza kwa sababu OC zinatolewa za kutosha, lakini kule chini hakuna mtu wa ku- monitor.

Kwa hiyo, tungejaza huko chini ambapo huduma ndiyo inakotolewa na mishahara yao ni midogo. Mtu mmoja huku juu ukimwajiri, anaweza kuajiri watu wanne kule chini. Kwa hiyo, mwajiri huko chini wa kutosha halafu huku juu watu wafanye kazi kwa ufanisi zaidi. Lingine ambalo nilikuwa naomba ni suala la kukaimu. Suala hili tungejitahidi pawe na kiwango maalum, kama ni miezi mitatu, isizidi hapo. Baada ya hapo mtu awe amethibitishwa ili ajiamini afanye kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuangalia performance. Siku hizi suala la mtu anavyo-perform na utendaji wake, haiendani na shughuli ambazo tunazifanya. Kwa hiyo, naomba tuendelee kuangalia katika sekta nzima ya utumishi katika performance ya watumishi ili kutokana na hiyo basi, wawe wanapandishwa madaraja, lakini pia wawe wanalipwa kutokana na performance ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la posho za Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Mtaa. Najua Serikali haina uwezo wa kuwalipa, kwa nini tusiwe na mfumo
ambapo Madiwani wakikaa huko kwenye vijiji, wakifanya kazi nzuri wakaongeza mapato zaidi kutokana na mapato ya ndani, basi waweze kupatiwa posho zao, posho ziongezeke. Utaona mtu kwa sababu ya incentive atakuwa anafanya kazi kubwa zaidi na wataongeza mapato ya Halmashauri zetu. Kwa hiyo, nilikuwa naomba suala hilo pia tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ilikuwa ni suala la Sheria hii ya Manunuzi. Tumefanya vizuri sana, niwapongeze hasa TAMISEMI, mmesimamia vizuri suala la force account kwenye sekta ya afya na elimu, imeenda vizuri. Ninaomba hiyo pia mwendele kutumia kwenye maji na pia kwenye TARURA.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na kunipa fursa ya kuchangia siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wetu ambaye ameamua kuleta mapinduzi kwenye sekta hii ya madini. Tunampongeza kuanzisha Wizara kamili ya Madini na Wizara ya Nishati. Kote sasa tunapata ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze wote, Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Doto pamoja na wataalam wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayofanya. Pia pongezi kubwa kwa Prof. Kikula kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini pamoja na team nzima ya Tume hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia kwanza kwa kushauri Kituo cha Mafunzo cha Arusha (TGC), kiwezeshwe sana kwa vifaa vya kufundishia. Wanahitaji mashine 100 za kufundishia na sasa wanazo 45 tu. Pia nipongeze kwa kuwa na mitaala ya kufundishia kozi ya Diploma itakayoanza Agosti, 2018. Nashauri kuwe na short course (Certificate in Lapidary) ya kuchonga vito. Ni kozi ya miezi sita kote duniani, wala haihitaji msomi, hata mtu asiyejua kusoma, anaweza kuwa mchongaji mzuri. Tukiwa na mashine 100 za mafunzo, tunaweza kuzalisha wataalam mia 400 kwa miaka miwili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nashauri pia kwenye leseni za utafiti (Prospecting License) au leseni kubwa, paruhusiwe kuwa na leseni za madini ya ujenzi kama mchanga, mawe, moramu na marumaru. Kwa sasa pamoja na kuwa tulirekebisha sheria kuruhusu kuwepo leseni hizo haifuatwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nashauri katika madini ya chumvi, Serikali iangalie namna ya kupunguza kama siyo kuondoa kodi, tozo na ada kubwa wanatozwa tofauti na thamani ya madini hayo. Leo hii wanatozwa sawa na madini yenye thamani kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, nashauri Wizara itupe tafsiri ya neno “raw mineral” leo hii kila mtaalam ana tafsiri yake ili wakati wa ku-export madini suala la kisheria ya kodi lisilete tatizo. Pia naomba nishauri Serikali ikae kama Serikali moja na siyo Wizara ya Madini tu, kufanya juhudi za pamoja ya kuboresha mazingira ya kufanya Tanzania hususan Arusha kuwa kitovu cha ubora katika biashara ya vito Afrika. Tayari tulianza vizuri na tulianza kuwa maarufu lakini sera za kikodi na usumbufu mwingine ulifanya tupoteze sifa na kudorora kwa biashara hiyo Arusha na Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zilizotuzunguka pamoja na zingine nje ya hapo wenye madini mengi walishaanza kuzoea kuja Tanzania kuuza madini yao katika mnada wetu. Walikuwa wanakumbana na usumbufu wa TRA kwenye ushuru wa import duty, VAT na pia madini ambayo hayakuuzwa ilikuwa ni usumbufu kurudisha kwao. Tofauti na nchi zingine kama Thailand, Belgium, India na kadhalika ambazo hawatozi kodi ya import na VAT. Pia wananufaika kutokana na biashara hizo katika sekta zingine kama katika service industry, hoteli, chakula, usafiri na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie namna ya kuondoa VAT kwenye madini yanayouzwa ndani ya nchi kama dhahabu, fedha, vito ili biashara hii ikue na magendo katika madini yaishe. Sisi kama Tanzania hatupangi bei ya madini kama dhahabu na fedha pamoja na vito (VAT on local sales of gemstone and jewellery), leo hii Dubai inatoza 5% ya mrabaha kwenye dhahabu, Tanzania ni asilimia 18 VAT pamoja na ada na tozo zingine. Nashauri tuweke mrabaha wa hata 7% ili biashara ihalalishwe na Serikali ipate mapato na madini yetu yasitoroshwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyenzi Mungu kunipa fursa kuchangia siku ya leo. Nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuendeleza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nichukue fusa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara pamoja na viongozi wetu wakuu wa majeshi chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Pamoja na changamoto kubwa ya uhaba wa vifaa na nyenzo za kufanyia kazi, hongereni kwa kazi kubwa na nzuri.

Mheshimiwa Spika, naomba nishauri katika baadhi ya maeneo ili kuboresha huduma katika majeshi yetu. Nianze na Jeshi la Magereza, wanafanya kazi kubwa na nzuri. Wana majukumu makubwa sana ya kuwahifadhi wahalifu walioshtakiwa kwa makosa mbalimbali na zaidi ya hapo kutoa elimu ya kuwarekebisha wahalifu (re-habilitation). Jambo hili la kuwarekebisha wahalifu wakiwa katika kutumikia adhabu zao huwa gumu kwa sababu ya kukosa nyenzo, vifaa na mazingira ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ingeweza kulisaidia Jeshi letu la Magereza kupata mkopo wa kupata vifaa vya kufundishia, vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kujenga karakana na madarasa. Jeshi letu hili lina wataalam wa kutosha, mfano mainjinia wa majengo (civil engineers), wachora ramani, mafundi umeme, mafundi bomba na wengine.

Mheshimiwa Spika, tukitumia force account wanaweza kujenga na kupanua magereza mbalimbali. Tukifanya hivyo tutakuwa tumesaidia Watanzania wengi sana watakaopata adhabu na wakitoka baada ya kifungo wawe na utalaam. Gereza liwe ni chuo cha ufundi, wafungwa wapewe vyeti vya kuhitimu mafunzo. Baadhi ya mafunzo yanayoweza kutolewa ni ufundi uashi, umeme, seremala, bomba, gesi, kuchomelea (welding), IT (computer), ushonaji, lugha mbalimbali na uchoraji.

Mheshimiwa Spika, pia kwa wale wanaosubiri kesi (mahabusu) wapate huduma bora zaidi kwa upande wa chakula, makazi, kupata taarifa mbalimbali kupitia redio au TV sababu inawezekana mwisho wa siku anatoka bila kuwa na kesi au adhabu kupitia mahakama.

Mheshimiwa Spika, Jeshi letu la Magereza lina uzoefu na wataalam wa kutosha katika fani mbalimbali, mfano, ujenzi wana usajili wa daraja la kwanza, kilimo, ufugaji, useremara na hata katika kuzalisha mali kupitia miradi mbalimbali na viwanda vidogo. Mfano Babati Magereza imeshirikiana na VETA kujenga jengo lenye thamani ya shilingi milioni 495 ambapo likiisha itafikia shilingi milioni mia tatu wameweza kuokoa shilingi milioni 195 kupita force account. Vilevile jengo la Uhamiaji Arusha lilijengwa na Magereza. Naomba jeshi letu lipewe vifaa vya kisasa vya ujenzi ili kitengo chao cha ujenzi kiweze kufanya kazi ya ukandarasi na washindane katika soko.

Mheshimiwa Spika, pia katika kilimo, ufugaji na uzalishaji mali (kusindika), Jeshi letu likopeshwa zana za kufanyia kazi kama matrekta, vifaa vyake (implements) ili waweze kuzalisha chakula chao na cha biashara na iwe sehemu ya shamba darasa. Kila mwaka katika Maonesho ya Nane Nane hupata kikombe cha ushindi ya kwanza. Wanafuga kuku, bata, ngombe, samaki, mbuzi na sungura kwa ufanisi mkubwa. Siyo lazima baadhi ya hivi vitu viwe kupitia bajeti, wanaweza kukopeshwa mfano matrekta na zana zake kupitia mfumo wetu unaokopesha raia wengine na pia kupitia TADB, Mfuko wa Pembejeo na taasisi zingine za fedha. Pia Serikali kupitia ruzuku na Magereza ipewe mashamba darasa ya kilimo, mifungo na usindikaji.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine muhimu ni suala la mazingira na matumizi ya nishati. Tunashauri Magereza zetu ziwe mfano ya matumizi bora ya nishati (kuni, mkaa na umeme). Leo hii magereza mengi hutumia kuni nyingi sana kwa ajili ya kupikia. Nashauri kwa kupitia CAMARTEC, magereza yote yajenge mifumo ya nishati ya kutumia gesi inayotokana na vyoo na mifungo (biogas na bio-latrine). Hii inaweza kupunguza matumizi ya kuni, pia kuweka mifumo ya solar, upepo na hiyo gesi utakayozalishwa kwa wingi (bio- latrine) wanaweza kupata nishati ya umeme na kupunguza gharama za umeme.

Mheshimiwa Spika, nashauri magereza yetu yote yawekewe mifumo ya kuvuna maji ya mvua. Hii itasaidia kupata maji ya matumizi ya kawaida na pia kupunguza gharama za malipo ya ankara za maji.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nashauri taasisi chini ya magereza zinazozalisha mali ziimarishwe. Pia tuangalie namna ya kuwakopesha Askari wetu wa Magereza usafiri wa pikipiki au magari kutokana na nyadhifa zao na wawe wanalipa kwa mwezi. Vilevile kuwe na bulk procurement kwa vifaa vya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi na naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na walio chini yao ikiwa na Viongozi Wakuu wa Majeshi yaliyoko chini ya Wizara hii. Naomba nishauri katika maeneo machache.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji; naomba nishauri kwanza Jeshi hili lipatiwe zana za kutosha za kufanyia kazi yao vizuri. Leo hii kwa jina la Zimamoto tunatoza kila biashara, viwanda, mgodi na hata kilimo kwa ekari, gharama za fire inspection fee, ni fedha nyingi sana zinazokusaywa. Nashauri badala ya kuweka bajeti ya kununua vifaa vya kuzima moto na fedha huwa haitoki kwa wakati, makusanyo ya tozo tunayokusanya aslimia 20 ziende katika Mfuko Maalum wa Zimamoto ili waweze kununua vifaa vyao vyote.

Mheshimiwa Spika, hapo pia watapata bajeti ndogo ya kutoa elimu juu ya uokoaji wakati wa dharura kwa raia. Pia Wizara ifanye kazi karibu na mipango miji na taasisi za maji kuweka fire hydrants mabomba ya kutolea maji katika kila eneo ili wakati wa dharura zitumike. Huko miaka ya nyuma ilikuwa ni lazima kila eneo liwe na bomba la kutolea maji (fire hydrants).

Mheshimiwa Spika, pia nishauri Idara ya Uhamiaji ambao wanafanya kazi nzuri sana mifumo yao iunganishwe na NIDA, Polisi na Idara ya Kuandikisha Vifo na Vizazi. Itasaidia kupata taarifa mapema na ya uhakika. Nashauri Wizara kupitia Uhamiaji pia iangalie suala la uraia wa Watanzania ambao wamezaliwa Tanzania, wamekulia Tanzania, wazazi wao walizaliwa Tanzania ila hawakujua sheria na utaratibu wa kukaa na uraia wa awali na kupata cheti cha uraia wakati wa uhuru.

Mheshimiwa Spika, nipongeze jitihada za Wizara kupunguza ada ya kupata vyeti vya uraia kwa Watanzania ambao hawakufanya hivyo awali kutoka Dola za Kimarekani 5,000 hadi milioni mbili dependant pass kutoka Dola za Kimarekani 500 hadi 100,000 kwa depandant wa Kitanzania. Nashauri hawa Watanzania waliokuwa na vyeti hivyo tuweke muda maalum, mfano mwaka mmoja wapatiwe kipaumbele na viwango vya milioni mbili vipunguzwe na iwe angalau laki tano kwa kipindi hiki maalum na tuwaondoe hofu Watanzania hawa. Wengi hawana uwezo wa milioni mbili baada ya hapo tubaki na wanaoomba uraia wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, pia haki ya kuomba uraia wa mwanaume aliyeoa mwanamke Mtanzania na mwenye watoto ambao Watanzania iwe na fursa ya usawa kwa uraia wa wanawake raia wa nje walioolewa na mwanaume Mtanzania, Fast Track.

Mheshimiwa Spika, pia Somo la Uraia litolewe kuanzia ngazi ya shule ya msingi na sekondari, itasaidia kuongeza uzalendo.

Mheshimiwa Spika, nayapongeza Majeshi yetu ya Zimamoto na Idara ya Uhamiaji kwa kazi nzuri inayofanywa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo. Nimpongeze Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa kazi nzuri na kubwa anayofanya katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakurugenzi wote na wataalam mbalimbali waliopo Wizarani na katika taasisi zetu chini ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana na anapokea ushauri kutoka kwa kila mdau. Naibu Waziri pia amekuwa mstari wa mbele kutoa ushauri wa kitaalam na kuweka mfumo bora katika utekelezaji wa shughuli za Wizara. Wataalam wote hutupa ushirikiano wa karibu na pia elimu tunapohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri katika maeneo machache ili kuboresha huduma. Kwanza, nishauri kuendelea kupunguza gharama zisizo za lazima ili kuongeza ufanisi kama mlivyopokea ushauri wangu wa ujenzi wa vituo vya afya na hospitali kutoka shilingi bilioni 4.5 kituo cha afya hadi milioni 500 au milioni 400 na Hospitali za Wilaya kutoka shilingi bilioni 705 hadi shilingi bilioni 1.5, hali ambayo ilifanya tujenge vituo vingi zaidi na pia hospitali nyingi za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Kitengo cha Manunuzi (procurement) cha MSD kiboreshwe na tuwe na team ndogo nyingine ambayo itafanya kazi ya kuhakiki manunuzi. Naamini bado tunaweza kupunguza gharama za manunuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze kwa kuendelea kutumia force account. Muhimu pia ni kutumia mfumo wa PPP katika kuboresha huduma za afya. Mfano eneo la huduma za maabara, nchi nyingi huwa na wataalam na vifaa vya maabara ambazo wanashirikiana na hospitali, vituo vya afya na zahanati kutoa huduma. Siyo lazima tuwekeze sisi katika kila hospitali au kituo cha afya. Pia huduma za Radiology za X-Ray, Utrasound, CT-Scan, MRI, tushirikiane na watoa huduma private. Naamini kwa kufanya hivyo bei za huduma hizo zitateremka.

Mheshimiwa Naibu, nishauri pia suala la telemedicine lipewe kipaumbele. Hii itasaidia kusogeza huduma ya mabingwa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kitengo cha kutengeneza viungo bandia kiboreshwe. Watanzania wengi wenye uhitaji wa viungo bandia hushindwa kuvinunua kutokana na kuwa na gharama kubwa. Tuangalie namna ya kuboresha na kutoa huduma hii katika maeneo mbalimbali nchini badala ya maeneo machache kwa bei kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali iangalie namna ya kuwa na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote itakayokuwa ni lazima (universal health care insurance). Leteni sheria mapema Bungeni ili Watanzania wengi wapate bima ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishauri tuendeleze sera yetu ya kinga bora kuliko tiba. Katika magonjwa mengi tunaweza kutoa elimu ya kinga badala ya kuingia gharama ya tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la usalama wa chakula na lishe, nashauri Serikali tujikite katika kinga kupunguza tatizo la lishe bora ili kuepuka tatizo la kudumaa na utapiamlo. Nashauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto ishirikiane na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii na Viwanda na Biashara ili kwa pamoja tuweke mpango na mkakati wa kutokomeza utapiamlo na suala la kudumaa (malnutrition stunting). Pia elimu zaidi juu ya namna ya kupata lishe na mazoezi kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza (non-communicable diseases) itolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri TFDA iweke vifaa vya kupima mazao hasa ya mboga mboga na matunda katika masoko yetu yote makubwa. Leo hii tunakula vyakula hasa mbogamboga na matunda vilivyopigwa dawa (sumu) kabla ya kumaliza muda maalum wa tahadhari kumalizika (chemical residuals from insecticides). Pia katika mifugo tunalishwa nyama na maziwa ya mifugo kutoka kwa mifugo iliyopigwa chanjo na dawa za matibabu kabla ya muda maalum kuisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri pia Serikali iangalie uwezekano wa kuondoa kodi katika vifaa tiba na vifaa wanaotumia wenye matatizo mbalimbali ya afya. Mfano baiskeli za walemavu na viti maalaum vya wagonjwa (wheel chairs) pamoja na magongo na vifaa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia Serikali isaidie kuboresha huduma katika Kituo cha Wazee Sarame-Magugu. Pia kutupatia X-Ray katika Kituo cha Afya Magugu. Niwashukuru kwa kupata vituo viwili Jimbo la Babati Vijijini, Magugu na Haiti. Naomba sana kupata vifaa vyote katika vituo hivyo ili kuboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iangalie namna ya kuboresha na kuweka utaratibu wa kuboresha sekta ya dawa za asili. Katika nchi mbalimbali hasa Bara la Asia na Mashariki ya Mbali (South East Asia), wameweza kuratibu, kuweka rekodi na kufanya utafiti wa mimea na dawa za asili kwa manufaa ya raia wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Tanzania katika kila eneo kuna dawa za asili na zote hazina rekodi wala kufanyiwa utafiti katika maabara ili kuwa na uhakika wa hizo dawa na nini kipo ndani yake (herbal medicine). Nashauri tungeanzisha mafunzo ya dawa za asili katika vyuo vyetu. Tuna rasilimali nyingi sana ambazo zinaweza kutumika kuleta tiba mbadala (homeopathy na allopathy).

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nashauri wataalam wa jadi au wa asili wapatiwe mafunzo ya kitaalam. Mfano tunao wataalam wa asili wenye uwezo wa kufunga mifupa, kurudisha mifupa iliyosogea katika sehemu zake (dislocation), wakipatiwa mafunzo zaidi wanaweza kutoa huduma vizuri zaidi. Hospitali ya Daseda Haydom wanawashirikisha na kuwasaidia kusoma X-ray ili wafunge mifupa vizuri. Nashauri Serikali iweke maabara maalum kwa ajili ya kupima mimea mbalimbali na dawa hapa nchini pamoja na kuweka rekodi za dawa hizo ili kupata dawa za uhakika na bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiboresha sekta hii na pia katika vipodozi (cosmetics) tunaweza kukuza ajira na kuongeza mapato na ikawa ni kivutio cha utalii. Mfano Morocco, Jordan, India, Indonesia, Thailand na nchi zingine zinapata mapato makubwa kutokana na dawa za asili na vipodozi (cosmetics). Ni sekta kubwa sana, nashauri vyuo vyetu vya tiba na maendeleo ya jamii viboreshwe sana. Mitaala yake iboreshwe na vifaa vya kufundishia na kujifunza ili wanaohitimu wawe na viwango vya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nirudie, tuboreshe vyuo vyetu vya uuguzi pamoja na vya afya (nursing and medicine) nchini ili Watanzania wengi wasome na hata kama hakuna ajira nchini waweze kwenda nchi za nje. Tukiwa na wataalam wetu nje ya nchi, watatangaza nchi yetu na kuleta mapato ya fedha za nje. Nchi nyingi za Asia hufanya hivyo. Huduma pia ya mazoezi ya viungo ni muhimu na wataalam ni wachache (physiotherapists).

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kunipa fursa ya kuchangia leo lakini pia nipongeze kwa jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali kuboresha sekta nzima hii ya ufanyaji biashara lakini pia kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote hapa huwa nasema pasipokuwa na coordination, namna ya kuhakikisha kwamba Wizara mbalimbali zinafanya kazi kwa pamoja, suala la viwanda na biashara itakuwa ni ndoto. Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikae kama timu mojo, Wizara na Wizara ziwasiliane na kama kuna jambo lolote washirikiane kuhakikisha jambo hilo wanalitatua kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi hapa tutakuwa tunalaumu labda Wizara ya Fedha kwamba kodi ni kubwa, lakini kodi zao ni tatu tu, ukiangalia tatizo kubwa ni regulatory authorities kuhusiana na tozo, ada na ushuru mbalimbali zinazoenda kwenye Wizara zote. Ukiona mmoja sasa hivi anasemwa kwenye Wizara yake atanyamaza lakini wengine wote wanabaki kusubiri yale mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kumekuwa na mtindo ili Wizara fulani ionekane imekusanya mahuhuli makubwa na mengi wanapiga fine za ajabuajabu. Mimi nashauri zile za fine mngeziweka pembeni, isiisabiwe, ikipigwa fine iende kwenye Mfuko Mkuu isiingie kwenye hesabu ya Wizara hiyo, kwenye Wizara ibaki ile ambayo ni jukumu lake, ndiyo tutaona Wizara na hizo taasisi zinafanya vizuri siyo kwenye fine, kwa sababu fine ndiyo inawabeba kwa sehemu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nimeshauri kwamba hizi regulatory authorities tuziunganishe pawe na upper stream na lower stream, zifanye kazi under umbrella ya Tanzania Regulatory Authority kwa sababu ndiyo zote zimebeba hizo tozo, ada, ushuru mbalimbali. Pia nashauri kwamba pawe na ukomo wa kukusanya tozo za miaka ya nyuma. Leo anakuja mtu wa NEMC anakudai ya miaka kumi nyuma, anakuja mtu wa TFDA anakudai ya miaka kumi nyuma, hivi siku zote walikuwa wapi? Kama hii ya TRA miaka mitatu mwisho, siku za nyuma wasiwe na mamlaka ya kudai kwa sababu kama walilala ni makosa yao siyo makosa ya huyo mfanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nilikuwa nimeshauri kwamba tuwe na One Stop Center, Afisa Biashara iwe ya Mkoa, Wilaya au Wizarani, mimi siwezi kujua sheria zote za regulatory authority, leseni na tozo mbalimbali ambazo zinafika mpaka 40. Ni vizuri tukienda Afisa Biashara anielekeze kwamba nikikata leseni natakiwa niwe na vibali vyote hivi na mlipa huyo mtu mmoja One Stop Center kama mwingine amesahaulika hajajulikana, Serikali ndiyo itajua namna ya kufidia huko siyo mimi mfanyabiashara. Ease of Doing Business, tukiweza urahisi wa kufanya biashara ndiyo njia pekee tutaweza kuwa na mafanikio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namna ya kulinda viwanda vya ndani, ni lazima tuwe na mifumo ya kulinda viwanda vya ndani dhidi ya bidhaa zinazotoka nje au zinazozalisha nje. Mkumbuke hawa ndiyo wanaozalisha ajira, ndiyo wanalipa kodi isije ikafika mahali sisi ikawa ni sehemu ya kuleta bidhaa kutoka nje kama Dubai, wanachukua bidhaa kutoka dunia nzima wanachukua tozo ndogo wanafanya biashara, je, sisi tunataka tuwe hivyo? Sisi tunataka tuwe na viwanda na vifanye kazi na lazima tuwe na mifumo ya kulinda viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wenye viwanda na wenye biashara wanalalamika wanalipa SDL lakini fedha hizo hazirudi kwenda kuwasaidia kuboresha kwa mfano SIDO, TIRDO, CAMARTEC. Mimi nasema ile asilimia 4.5 yote ingeenda huko zikaboresha VETA zetu na hizi taasisi zote ili wawe na fedha za kufanya utafiti na kuandaa wataalam ambao wataweza kuja kukusaidia katika masuala ya viwanda vyetu na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima tuunganishe uzalishaji, sehemu kubwa ya nchi yetu ni kilimo, mifugo na uvuvi. Tusipoangalia namna ya kuunganisha bidhaa zao hatutafanikiwa. Leo hii Serikali ifanye tathmini yake, miaka mitano nyuma na leo, sekta rasmi na sekta isiyokuwa rasmi ipi inakua, asilimia kubwa ya watu wameondoka kwenye sekta rasmi wanarudi kwenye sekta isiyokuwa rasmi kutokana na tozo, ada, kodi na ushuru mbalimbali ambapo Serikali itafika mahali haitakuwa inapata ushuru wala kodi ambayo inastahili kupata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vyuo vyetu vya elimu viangalie namna ya kutoa elimu ambayo inalingana na uhitaji wetu ndani ya nchi. Pia bidhaa nyingi zinazokuja nchini ni substandard lakini tunalipa kwa bei ileile ya standard. Kwa hiyo, ni vizuri taasisi hizo ziweze kufanya kazi vizuri na tuangalie namna ya kuondoa huu rasimu uliopo ili tuweze kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tuweze kuangalia namna ya kuwekeza kwenye sekta ambazo zinazalisha kama kilimo, mifugo na uvuvi ili ziweze kuzalisha bidhaa za kutosha na kwa viwango ili tuweze kuwa na viwanda. Serikali ingefanya tathmini kwamba bidhaa tunazoagiza kutoka nje ya nchi nini ambacho tunaweza kuzalisha hapa nchini, moja ikiwa ni mchele, mafuta ya kula, sukari, mbegu bidhaa hizo zote tunaweza kuzalisha humu nchini kwa nini tusiwekeze huko ili watu wetu wapate ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijue kwamba siyo kila mahali lazima upate direct tax kwamba lazima upate kodi au ushuru. Inawezekana katika kiwanda kimoja Serikali haipati chochote pale lakini kinaajiri watu zaidi ya 10,000 au 20,000, tayari watu wakiwa na spending power yaani uwezo wa kununua bidhaa Serikali itakusanya kodi kubwa kupitia indirect taxes.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wangeangalia kwenye tozo, kodi na ada wazipunguze ziweze kulipika na compliance itakuwa kubwa. Badala ya watu kuwa na tamaa ya kukwepa wakizipunguza gharama hizo watu wengi zaidi wataweza kulipa na Serikali itakusanya mapato makubwa lakini uzalishaji ndani ya nchi utakuwa mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunajitahidi kuondoa baadhi ya kodi kwa kupitia Sheria ya Finance lakini baadaye inarudishwa kupitia Kanuni. Mimi naomba suala hili la Kanuni kama Bunge hili litaridhia badala ya Waziri kuwa na mamlaka kupeleka moja kwa moja kutangaza kwenye Gazeti la Serikali haswa popote panapohusiana na kuongeza au kupunguza tozo mbalimbali iwe ni lazima iletwe Bungeni ama kwa kupitia Kamati husika ili zisiruhusiwe kwenda kupandishwa kiholela kwa sababu tunaweza kuondoa kodi fulani hapa baada ya muda mfupi unakuta Waziri kule kwenye Kanuni anapandisha tozo hizo na kufanya wafanyabiashara kuendelea kupata tatizo na urahisi wa kufanya biashara unakuwa mgumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tungekuwa na mfumo wa kuangalia namna ya kufanya uratibu. Mimi nashukuru sasa tuna Waziri wa Uwekezaji na yeye kazi yake kubwa ni kuangalia urahisi wa uwekezaji wa ndani, wa nje, mkubwa au mdogo, yeye ndiye atakuwa sasa ndiyo mratibu wa shughuli zote kwenye biashara akisaidiana na Waziri wa Viwanda na Biashara lakini na Mawaziri wengine wote ili kuangalia wapi kuna changamoto na waweze kuleta mara moja kama ni sheria ibadilishwe lakini kama kwenye Kanuni wawaagize wale Mawaziri waziondoe ili urahisi wa kufanya uweze kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingewezekana kwa miaka yote michango ya Wabunge ingeangaliwa kwenye Hansard walichangia nini na tukaletewa hapa, naamini kila mwaka tutaendelea kusema lakini yanayotekeleza ni machache. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunapata mafanikio, nchi yetu iende mbele na fursa zote tunazo isipokuwa utaratibu wa kuhakikisha hizo fursa zinatumika vizuri ndiyo haufanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ndiyo kubwa kuliko zote ambapo ndiyo inasimamia biashara na masoko yote lakini pia kuendelea kukuza viwanda vikubwa na vidogo, ni jukumu lenu kushauriana na Wizara zingine zote kuweka mazingira wezeshi ili Watanzania waweze kuwekeza. Siyo kwamba Watanzania wanashindwa kuwekeza, mitaji na uwezo wanao, jukumu lenu kukaa na kuhakikisha tunaweza kufanya shughuli hizo kwa unafuu zaidi. Badala ya kuangalia maslahi ya watu wachache tuangalie maslahi ya wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nashukuru na naunga mkono hojo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kupata fursa ya kuchagia na kunipa afya njema.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu pia kutupa Baraka zake nchini na kutupa amani.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Rais wetu wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Mawaziri wake hasa katika Wizara ya Kilimo, Katibu Mkuu, Wakurugenzi wa taasisi mbalimbali chini ya Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, napenda kushauri katika maeneo mbalimbali ili kuboresha sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nashauri suala la bajeti, kwa maoni yangu kila mwaka bajeti ya Wizara hii hushuka kidogo kidogo. Maelezo tunayopewa ni kupanda kwa bajeti ya Wizara nyingine zinazopeleka pia bajeti zao kwa maendeleo ya wakulima. Mimi binafsi nikipiga hesabu kutokana na Bajeti kuu ya Shs. trillion 33, hiyo mikataba tuliyoingia kama nchi, ya Malabo na Maputo kufanya asilimia 10 ya bajeti tatu kwa sekta ya kilimo, bado hatujafikia asilimia 10 ya trillion 33, ni trillion 3.3. Hata ukijumlisha fedha zote za Wizara mtambuka kama TAMISEMI, Ardhi, Mifugo na Uvuvi, (Barabara za vijiji) uchukuzi, Maliasili na Utalii, Maji, Mawasiliano, Elimu, Afya, Fedha zinazokwenda vijijini tulipo wakulima haziendi trillion 3.3 (chukua, Bajeti za REA, TARURA, RUWASA, Afya, Elimu, TAMISEMI)

Mheshimiwa Spika, pia ukilinganisha Bajeti za Kilimo kwa miaka mitatu au mitano, badilisha kwa bei hiyo ya Dollar ya Marekani ($USD) utanona bajeti inashuka.

Mheshimiwa Spika, pili nashauri Serikali itekeleze “Blueprint” ili kuondoa tatizo la urahisi wa kufanya biashara (Fair Competition in Trade). Leo hii tumeona sekta isiyokuwa rasmi inakua kutokana na sekta rasmi kutozwa kodi, Ada, Tozo na ushuru mkubwa na kwa idadi kubwa kutoka kila taasisi ya udhibiti (Regulatory Bodies).

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iangalie namna ya kuboresha sekta ya umwagiliaji. Nipongeze Serikali kurudisha sekta ya umwgiliaji. Niipongeze Serikali kurudisha Tume ya Umwagiliaji kutoka Wizara ya maji kurudi Wizara ya Kilimo. Naamini Wizara hii itaitendelea haki sekta ya umwagiliaji tangu Tume kuanzishwa hadi leo haikupangiwa au kupewa fedha za maendeleo katika umwagiliaji. Nashauri Serikali isibaki kujaribu kufanya peke yake bali iweke mazingira wezeshi na rafiki ili sekta binafsi pia ichangie. Nashauri Serikali iondoe kodi katika mitambo ya kuchimba maji na mitambo ya kutengenezea mabwawa, pamoja na kodi ya Pump za Sola za umwagiliaji na vipuri vya zana za umwagiliaji. Pia Benki ya TADB na Mfuko wa Pembejeo watenge asilimia 20.

Mheshimiwa Spika, nashauri kila Mkoa upewe angalau mitambo ya kuchimba mfereji na mabwawa badala ya kutoa tenda ya kuchimba maji na kutengeneza mabwawa.

Mheshimiwa Spika, napongeza juhudi ya kuwa na Sera na Sheria ya Kilimo, ndiyo njia pekee ya kusonga mbele. Hapa nashauri ardhi ya kilimo italindwa na mijini mashamba ya kilimo yataendelea.

Mheshimiwa Spika, nashauri TARI ipewe kipaumbele kwa kupewa bajeti ya kutosha ya ndani ili wenye kufanya utafiti vizuri wa mbegu, viuatilifu vizuri vya mbegu, viuatilifu vya magonjwa na pia ugani katika kilimo. Bila kuwekeza katika taaisi yetu ya TARI kilimo chetu itabidi kuwa cha kubabaisha na duni bila tija. Tuna vituo 17 na vyote vinahitaji kuboresha miundombinu, vifaa vya kisasa kufanya kazi zao vizuri na zana nyingine kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Nashauri Chuo Kikuu cha SUA kiwe chini ya Wizara ya Kilimo ili kuboresha tija katika chuo hicho.

Mheshimiwa Spika, nashauri ASA iongezewe mtaji ili kuzalisha mbegu bora na zenye viwango kwa kutosheleza mahitaji ya nchi. Nje ya bajeti wao wakopeshwe zana za Kilimo, matrekta na zana nyingine, vifaa vya umwagiliaji vya aina mbalimbali kutokana na shamba husika, vifaa vya kuchakata na kusafisha mbegu na kuweka dawa ya kuhifadhi na kutunza mbegu na hapo hapo TASTA pia ipewe watumishi wa kutosha na wapate mfumo wa TEHAMA kwa ajili ya kusafirisha mbegu za ndani na nje ili kuwa na udhibiti wa uhakika.

Mheshimiwa Spika, pia na shauri TFS wafanye uhakiki wa aina mbalimbali za mbolea na kuishauri Serikali kuondoa vikwazo katika baadhi ya vipengele kwenye Sheria ya Mbolea.

Msheshimiwa Spika, nashauri Serikali na Wizara ishirikiane na taasisi nyingine kuboresha TPRI iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo na kuiboresha pia Miundombinu, vifaa vya kisasa kuifanya kazi yao. Wafanye utafiti wa mabaki ya sumu tunayotumia sisi walaji wa mazao (Nop pesticide Residuals) na kushauri nini kifanyike.

Mheshimiwa Spika, mwisho, Benki ya Kilimo na Mfuko wa Pembejeo ziongezewe mtaji ili Serikali ifanye yale yake na sekta binafsi zifanye juhudi kuendeleza kilimo na umwagiliaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia siku ya leo. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nimshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa nia njema na jitihada kubwa anayofanya kuhakikisha kwamba jambo hili, Sekta ya Mifugo na Uvuvi iweze kuchangia katika pato la Taifa lakini pia kulinda maslahi ya wafugaji na wavuvi kwa ujumla. Pia niwashukuru na niwapongeze Waziri, Naibu Waziri na Katibu Wakuu wote kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri katika maeneo machache:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; naomba tuendelee kujikita na kuboresha huduma mbalimbali kwa mfano ya veterinary, fedha iliyotengwa ni ndogo lakini tuangalie namna ya kuwapatia mikopo na nini ili huduma ya veterinary iendelee kufika katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeendelea kuomba Wizara hii ndiyo ina jukumu la kulinda ardhi zote za wafugaji, leo ardhi za wafugaji zinaendelea kuporwa na kubadilishwa matumizi na yanabadilishwa matumizi kutoka kwenye general land na kuingia kuwa maeneo ya hifadhi, lakini pia vijiji vinabadilisha matumizi ya ardhi ya wafugaji ambayo tayari yalishatengwa kabisa na yalipewa na hati, wanakaa kwenye mkutano kwa sababu wafugaji ni wachache, wanabadilisha hayo maeneo yanakuwa ni maeneo ya kilimo. Sasa ndiyo maana inaleta mgongano mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ningeomba nichangie ni blueprint. Ni vizuri Serikali ikasimamia kweye Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi blueprint hasa tukiangalia kwenye suala la viwanda vya maziwa. Viwanda vya maziwa vinapata tatizo kubwa na vinashinda kushindana na maziwa kutoka nje kutokana na ada, tozo, kodi na ushuru mbalimbali. Jambo hili tusipoliangalia vizuri, viwanda hivi na hii ndoto yetu kubwa tutakuwa hatufikii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na maziwa ya kutosha tushindane na wenzetu majirani, ningeomba kwenye kituo kile cha Nike tuwekeze fedha za kutosha, tuwapatie fedha ili waende kuhimilisha ng’ombe katika maeneo mbalimbali, tupate ng’ombe wazuri, bora na pia ule mpango wa kuzalisha mitamba 5,000 kwa mwaka, ningeomba Serikali iangalie kwa juhudi yoyote ile nje ya mfumo wa bajeti namna ya kuzalisha mitamba ya kutosha. Tukitaka kuwa na maziwa ya kutosha na ng’ombe wazuri, lazima tuwe na mifugo ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mbali na hiyo lazima Serikali wakae kwa pamoja kuangalia ule mnyororo wa thamani wa namna ya kuhifadhi bidhaa za uvuvi lakini pia mifugo, cold storage na chillers nayo waangalie namna ya kuboresha, kuwekeza humo na kuondoa kodi mbalimbali. Tatizo kubwa la wafugaji ni upatikanaji wa maji, majani ya uhakika (malisho), lakini hivyo hivyo njia pekee ya kufanya hivyo ni Serikali kuondoa kodi kwenye mitambo ya kuchimba maji, kutengeneza mabwawa na majosho. Hili siyo lazima Serikali ifanye, Sekta Binafsi wafugaji wakiwawekea mazingira wezeshi na niwapongeze kwamba wana leongo la kuunda ushirika wa wafugaji ili na wao wakakope kwenye Benki ya Kilimo, waweze kukopa kwenye Mfuko wa Pembejeo, wao wenyewe kutokana na mifugo tuliyokuwa nayo tutaweza kuwekeza. Tatizo kubwa linakuja Sekta isiyokuwa rasmi inaendelea kukua kutokana na hiyo blueprint, ada, kodi, tozo na ushuru mbalimbali. Hatutafanikiwa kama wasipokaa na kuangalia namna ya kuboresha jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze kwenye suala la aqua culture, wanafanya vizuri. Ningeomba elimu hiyo iendelee kutolewa na watusaidie katika maeneo mbalimbali ili tukuze pato la Watanzania kwa wingi, lakini pia wapate chakula na bidhaa za kufanyia kazi kwenye viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, naunga mkono hoja, mengi nitaandika kwa maandishi. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa siku ya leo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uwezo wa kuchangia leo. Naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri ya kuleta maendeleo anayofanya na hasa katika masuala ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Pia kwa nia yake ya dhati ya kuleta mabadiliko na pia kuleta ndege za shirika letu la ndani ya usafiri wa anga (ATCL) kuboresha na kutangaza utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wataalam wote Wizarani na pia taasisi zilizo chini ya Wizara hii. Pia Wakurugenzi wa TANAPA na NCCA kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri katika maeneo machache ili kuboresha Sekta hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza naomba Wizara hii ifuatilie kwa karibu kutatua migogoro baina ya hifadhi, jamii na watumiaji mbalimbali wa ardhi. Babati tuna hifadhi mbili ambazo tuna tatizo la mipaka, Tarangire ikiwa na Vijiji vya Ayawayo, Gedamar na Gidejabung. Wananchi walipewa fidia ya majengo yao (au maendelezo) kabla ya miaka zaidi ya kumi na waliahidiwa ardhi mbadala sababu hao wananchi walipelekwa hapo na operation vijijini ekari 17,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni la miaka mingi sana, tunashauri eneo hilo wapewe wananchi kwa ajili ya ufugaji jambo ambalo litaendana na uhifadhi. Pia tuna eneo la Ziwa Manyara (hifadhi) ambapo pia kuna mgogoro na Vijiji vya Mayoka, Moya na Manyara.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni eneo kubwa la Babati, Monduli, Kondoa, lipo kwenye eneo la hifadhi ya wanyamapori (game controlled area) ambapo zamani shughuli za kibinadamu zilikuwa zinawezekana. Kwa marekebisho ya Sheria ya 2009, shughuli zote za kibinadamu ilikuwa makazi, kilimo, uvuvi, ufugaji haziruhusiwi kufanyika tena ila sheria ilitaka Waziri ndani ya miezi 12 atangaze maeneo ya game controlled area na nyingine zitolewe kwa wananchi. Tuna mkinzano wa Sheria ya Ardhi, ya Wanyamapori, WMA, Madini na nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye game controlled area ya eneo la Babati na wilaya za jirani pia tuna WMA ya Burunge. Sheria ya Madini inamruhusu Waziri wa madini kutoa leseni ya kuchimba madini ndani ya hifadhi ambayo ni tatizo.

Tunaomba Wizara itusaidie kutatua mgogoro wa WMA Burunge na jamii ya kifugaji wameondolewa kwa nguvu katika maeneo yao na kupewa maeneo ya makazi tu ya ekari tatu kila mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nishauri Serikali itekeleze suala la Blueprint. Utalii wetu haukui sababu kubwa ikiwa ni ada, tozo, kodi na ushuru mkubwa ambao unafanya utalii wetu kuwa ghali (expensive destination) na pia uongozi wa masuala ya utalii. Binafsi TATO wameomba pawe na one stop centre kulipia leseni, tozo, ada na ushuru pamoja wakati mmoja kupunguza gharama. Nashauri Serikali iwekeze kupeleka nishati katika geti la Tarangire, Sangaiwe na Mamire pamoja na barabara ya lami ili kupunguza gharama za ukarabati wa kila wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri kila hifadhi ilipe fidia au kifuta machozi na kifuta jasho badala ya Wizara ambayo inachelewesha kutokana na bajeti ndogo na hizo hifadhi zikilipa hiyo fidia watafanya kazi ya kuhakikisha wanyama hawatoki nje ya hifadhi kila wakati. Naomba Wizara iharakishe kulipa deni hilo kuanzia 2011 hadi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iwekeze zaidi katika TFS, Kitengo cha Nyuki na pia Wakala wa Miti Taifa. Tukiwekeza hapo zaidi kwa rasilimali watu, fedha na elimu kwa uma, sekta hii inaweza kuchangia zaidi katika pato la Taifa na pia uchumi wa wananchi. Naomba pia nishauri Serikali ibaki na msimamo wake wa kutoruhusu biashara ya wanyama hai. Nashauri tuwe na marufuku ya kudumu (total ban).

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri pawe na uratibu ndani ya Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji kuangalia namna ya kila Wizara kuwekeza kuboresha maeneo muhimu ya miundombinu, nishati, maji, mawasiliano, uwekezaji ili kukuza utalii katika maeneo mbalimbali nchini, utalii wa ndani na nje. Pia Wizara ya Fedha na Wizara nyingine kupunguza kodi, tozo, ada na ushuru kulingana na kukuza biashara ya utalii (coordinate efforts).

Mheshimiwa Naibu Spika, utalii pekee unaweza kufanya Serikali yetu ipate kipato kikubwa bila kugusa rasilimali zetu nyingine kama madini. Bidhaa za misitu kama mbao na magogo hadi tutakapokuwa tayari kama nchi kuvuna wenyewe. Hongereni kwa kazi nzuri na tunawatakia kila la kheri.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana awali ya yote naomba nichukue fursa hii kuanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kuniwezesha kuchangia. Lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yao nzima kwa kazi kubwa na nzuri sana wanayofanya na niwapongeze kwamba bajeti ya awamu hii imeleta matumaini makubwa ni bajeti moja katika bajeti ya hii miaka minne ambayo ni ya mfano kabisa, imelenga kila sekta, lakini imelenga hasa kwa kuwezesha viwanda vya ndani na ukuaji wa uchumi wa ndani kukua kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nishukuru kwa kuanza kutekeleza suala lile la blueprint kwa kuondoa tozo angalau 54, ni mwanzo tu lakini ninaamini kwamba sasa mtakuja na ile sheria Bungeni ya kuweza kuifanya blueprint yote iweze kutekelezwa ili viwanda/biashara ya ndani iweze kukua na tuweze kuzalisha bidhaa na tuweze kushindana kwa bidhaa zinazotoka nje lakini pia bidhaa zetu ziweze kwenda nje kushindana katika masoko mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nishukuru kwamba mmeweza kuendeleza msamaha wa kodi kwa muda wa miezi sita mingine kwa wale ambao ilikuwa bado hawajalipa. Niwapongeze mmeweza pia kupandisha ile threshold ya VAT kutoka milioni 40 kwenda mpaka milioni 100 lakini pia wale ambao walikuwa chini ya/waliotakiwa kupeleka mahesabu baada ya milioni 20, sasa ni milioni 100.

Mheshimiwa Spika, ningeomba kwenye orodha hiyo kama inawezekana makampuni ambayo ni limited, ambayo hayapo kwenye mfumo huu, ambayo yapo chini ya milioni 100 ni watu wamependa formalize biashara zao lakini bado biashara zao zipo chini ya milioni 100 na wao pia waendelee kupata msamaha huo ili pawe na usawa. Mtu anaye- formalize asiadhibiwe na lengo kubwa ni kutoa sekta isiyo rasmi kuwa rasmi. Kwa hiyo, pangekuwa na vivutio zaidi kwa sekta ambayo watu wamejirasimisha basi wao wapate vivutio zaidi ili wengi waondoke huko kwenye sekta isiyo rasmi na kurudi kwenye sekta ambayo ni rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze kwa kushusha kodi ambayo haijasemwa na watu wengi, mmeshusha vile viwango vya kodi kwenye presumptive tax kutoka 150,000 kwenda laki tatu na kitu, kwa hiyo kodi zimeshuka. Kwa hiyo, wafanyabiashara wengi sasa wataweza kulipa zile kodi na hawatafungiwa biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu lingine kwamba tunaomba mkija sasa wakati wa Finance Bill tuweke utaratibu wa kuwa na one stop center badala mtu kutafuta leseni na vibali maeneo mbalimbali kama ilivyo kwenye TIC kwa wale wanaojisajili TIC wale wa nje, sasa na sisi wa ndani kupitia Afisa Biashara wa Mkoa na Wilaya, tukienda tukilipa sehemu moja, tozo na ada zote ulipie sehemu moja unaachana nao mpaka mwakani, sasa huko Serikali ijue kwa sababu yote inaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, wajue namna ya kugawanya hizo tozo na ada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado nasisitiza blueprint usipoitekeleza bado hatutakuwa tunaweza kushindana kwa bidhaa zetu kwenda nje wala humu ndani, lakini ni hatua moja nzuri mmeanza nayo, niwapongeze lakini naomba hiyo sheria ije mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ni muhimu, mnakusanya fedha vizuri lakini bado matumizi mabaya yapo kwa mfano GPSA, TEMESA lakini pia TBA, hayo ni maeneo ambayo haya mabilioni mnayokusanya wanaenda kuyatumia vibaya, ni kichaka ambacho kimejificha ambapo kwa mfano TEMESA ukipeleka magari ya Halmashauri kutengeneza pale ni kero kubwa, unaweza kutengeneza kwa nusu ya bei na kwa viwango vilevile tukiwa tunatengeneza nje hivyohivyo katika majengo ya Serikali na nini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo muichunguze TEMESA na GPSA hiyo Sheria ya Manunuzi wanapanga watu wakuwa- supply 10 kwa mfano kwa mwaka mzima. Iwe ni wazi GPSA ibaki ku-regulate kwamba kama BOT wanaangalia bei za foreign exchange na nini ni ngapi, GPSA ibaki ku-regulate bei, lakini iwe wazi kwa mtu yeyote, saa yoyote tenda ikitolewa waweze kujaza ndiyo mtaona manufaa, value for money itapatikana. Kwa hiyo, GPSA, TEMESA, TBA muwaondoe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ombi langu lingine, undeni Tanzania Regulatory Authority, upper stream, lower stream ili wote wawe chini ya taasisi moja na wao wote waweze kufanya ndiyo mtaweza kuondoa kodi, tozo, ada na ushuru mbalimbali nyingi, lakini pia wafanyabiashara wengi wanaomba kwamba hizi regulatory bodies badala ya kwenda kupiga faini za ajabu ya kwanza watoe onyo na kuwaambia rekebisha, ya pili iwe ni onyo kali zaidi na ya tatu ndiyo iwe faini, siyo mara ya kwanza anakuja anakufungia biashara anakutoza faini za ajabu, hapo ndiyo tutaona lengo lao kuu ni kufanikisha watu wafuate sheria na utaratibu.

Mheshimiwa Spika, lakini ombi langu lingine ni kama Kamati ya Bajeti ilivyopendekeza na siku zote tunapendekeza suala la kuondoa kodi kwenye mitambo ya maji na mitambo ya kuvuna maji ya mabwawa na malambo. Hii itasaidia watu wengi zaidi kuwekeza kwenye sekta binafsi badala ya kutegemea Serikali ifanye mambo yote haya kwenye umwagiliaji, maji ya kunywa, maji ya mifugo na mabwawa ya samaki na bado tukitengeneza hayo mabwawa, athari tunayopata ni uharibifu wa yale maji ya mafuriko kuharibu miundombinu itakuwa haipo, kwa hiyo mkiondoa.

Mheshimiwa Spika, leo hii kwa wale ambao wanapata msamaha ni makampuni makubwa na miradi ya Serikali, lakini mtu binafsi hapati hiyo. Hasa upande wa kilimo hatuwezi kupata kwa sababu bidhaa zetu hazipo vitable, kwa hiyo vital on deferment kwenye capital goods sisi hatupati. Kwa hiyo, nivizuri mkatuondolea ili watu wengi binafsi pia waweze kuleta mitambo ya maji na tuweze kusaidiana na Serikali kuboresha huduma ya maji kwa pande zote.

Mheshimiwa Spika, ombi lingine tunawashukuru na tunawapongeza mmeweza kuondoa kodi kwenye vifaa au mashine za kuchonga vito, lapidary na za kutengenezea jewellery. Tunaomba sasa mfike hatua ya pili kwa sababu hatua ya kwanza mmeondoa duties, mngeondoa na VAT kabisa ili sasa zile mashine ziwe za bei nafuu na Watanzania wengi watakaopata mafunzo pale Gem Center pale Arusha basi waweze kupata hizi mashine kwa bei nafuu zaidi. Kwa hiyo, mngeweza kutuondolea kodi kwenye hilo.

Mheshimiwa Spika, tunawashukuru kwamba mmeondoa kodi kwenye refrigerated trucks kwa ajili ya horticulture, lakini tunaomba mngetanua wigo zaidi ili uweze kuhusisha pia sekta ya maziwa, nyama na samaki kwa sababu bidhaa hizo mkiweza kuondoa kodi, wale wavuvi hawatahitaji kuuza samaki wao wanapovua, wanaweza kuzi- refrigerate kwa bei nafuu kwenye containers ambazo zitakuwa refrigerated za ushirika na hata wale wa kuku badala ya kuuza kuku kwa haraka kwa bei ya chini, wanaweza kuwa-process na kuwaweka kwenye fridge wauze taratibu ili mkulima aweze kufaidi moja kwa moja. Kwa hiyo, pamoja na kuwa mmesaidia Sekta ya horticulture mngetanua wigo kwenda kwenye maziwa, samaki na lakini pia kwa upande wa nyama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni ombi la kuondoa kodi kwenye solar waterpumps itasaidia sekta ya maji kwa upande wote lakini pia ukileta kama umwagiliaji, kodi hizo hazilipiwi lakini ukileta hivihivi bila kutaja umwagiliaji ina kodi. Kwa hiyo, inaleta usumbufu mkubwa, mngeziondoa ili sekta nzima ya maji iweze kupata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Jitu Soni.

MHE. JITU V. SONI: Ahsante, nashukuru na naunga mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kunipa afya na kupata uwezo wa kuchangia. Pia nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na timu yake nzima kwa kazi nzuri na ambayo inaonekana. Ndoto za Watanzania sasa zinaendelea kukaribia kutimia na kila sekta imefanya juhudi kubwa. Lengo letu sisi kama Wabunge ni kuendelea kuishauri Serikali na pia kutoa maoni ili yaweze kufanyiwa kazi na tuendelee kuboresha maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Mawaziri wenzake wote kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya kwa kuratibu shughuli zote za uendeshaji mzima wa Serikali, lakini pia shughuli za sera na masuala ya Bungeni.

Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe kwa kutimiza ile ndoto ya kuwa na Bunge mtandao ambayo sasa wote tumeona mafanikio yake. Ingekuwa hiki kipindi ambapo ugonjwa wa Corona umekuja na hatuko katika masuala ya Bunge mtandao naamini Bunge hili lingekuwa limeahirishwa. Hongera sana na pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu moja, tunaomba sasa na Serikali ijitahidi kuweka katika mtandao huu sheria zote ambazo tayari tumezipitishaili tukihitaji kupitia sheria mbalimbali basi tukiingia kwenye tablet zetu tuweze ku- downlod zile sheria tuweze kufanya reference mbalimbali kama kuna kuleta mabadiliko au kuangalia reference mahali ambapo tunahitaji kufanya hivyo. Hiyo itatusaidia sana na itarahisisha mambo mengi ya uendeshaji wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niipongeze timu nzima ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa suala zima hili la Corona na namna wanavyolisimamia. Kuna mengi ambayo yanafanyika, wengi wanaendelea kulaumu lakini mimi najua. Mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Taifa na tayari sekta ya kilimo inaandaa athari mbalimbali ambazo zinatokana na jambo zima hili kiuchumi kwenye sekta ya kilimo, lakini hivyohivyo kila sekta, ya viwanda na wengine wote wamepewa hayo maagizo. Sekta zote zikishaleta hizo taarifa zao naamini Serikali sasa ndiyo itapata tathmini kamili kutoka kwa wadau wenyewe ndiyo waweze kupanga nini kifanyike ili tuweze kuona hii athari ya kiuchumi na namna ya kusonga mbele, kwa hiyo, hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, ombi langu lingine moja kutokana na suala hili la Corona, kama inawezekana Serikali iangalie namna ya kupata vifaa tiba vile ambavyo vinahitajika basi Serikali ingeweza kuondoa kodi ili vifaa hivyo viweze kuingizwa nchini kwa gharama nafuu bila kodi yoyote. Tunajua kabisa Serikali peke yake haitaweza lakini sekta binafsi na wadau mbalimbali wako tayari kusaidia. Kwa hiyo, bidhaa hizi zikiwa zimeondolewa kodi zitakuja kutusaidia hata baada ya janga hili kupita tuna uhakika vifaa hivyo vitaendelea kutumika kwenye shughuli mbalimbali katika sekta nzima ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niipongeze Serikali kwa ujenzi wa vituo vya afya na zahanati mbalimbali pamoja na hospitali. Nishukuru kwamba sasa hivi tumeona matangazo na madaktari wengi wameomba nafasi zile 1,000; 700 zitakuwa katika ngazi hii ya TAMISEMI lakini 300 zitakuwa ngazi ya Taifa. Tunawapongeza sana, tunaomba hizo ajira mzi-fast track, tunajua wameshaomba ili waende kwa sababu zahanati na vituo vya afya viko tayari ili tuweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, pia nilikuwa naomba kwa upande wa TARURA hali ni mbaya, barabara nyingi zimeharibika nchi nzima na siyo jambo la kawaida bali ni kutokana na mvua kubwa zilizojitokeza. Tunaomba mruhusu kwa mwaka huu kwenye fedha zote zitakazoenda TARURA itumike force account ili tuweze kukodisha mitambo kwa gharama nafuu ili angalau tuweze kurekebisha barabara zetu ziweze kupitika wakati wote lakini pia kutengeneza makalvati na madaraja ambayo hayahitaji utaalamu wa hali ya juu ili mawasiliano yaweze kurudi. Pia tuangalie namna ya kuongeza bajeti kwa upande wa TARURA.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba amezungumzia suala la kilimo na hilo nitalizungumza wakati wa bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mapana yake lakini niongelee suala la lishe. Siku zote naamini kwamba kinga ni bora kuliko tiba. Tungewekeza zaidi kwenye upande wa sekta hii ya kilimo kwa mapana yake na watu wakaendelea kupata elimu juu ya lishe hata hili gonjwa la Corona tusingekuwa tunaliogopa sana kwa sababu miili yetu ingekuwa na kinga na hata yale magonjwa mengine, miili ikiwa na kinga nzuri hii gharama tutayotumia kwenye dawa za kutibu itapungua. Kwa hiyo, tuwekeze zaidi huko kwenye sekta ya kilimo kwa mapana yake ili tuweze kujenga afya zetu wenyewe.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo kwenye Sekta ya Ajira na Vijana, naomba kwenye Sekta ya Kukuza Ujuzi tungeendelea kuwekeza. Ile asilimia mbili tuliyopitisha kwenye sheria wakati wa dharura ambayo inakwenda Bodi ya Mikopo, nashauri irudi kwenye VETA (Skills Development) ili vijana wote sasa waweze kuboreshwa kwenye ujuzi kwa kupitia VETA.

Mheshimiwa Spika, kwenye VETA nashauri twende na mfumo wa Builder Apprenticeship Painting System (BAPS) ambapo Mkoa wa Manyarara pale Babati ndiyo ya kwanza Tanzania tumeanza kufanya majaribio. Ni mfumo ambao mwanafunzi anasoma miezi miwili au mitatu, anaenda kutekeleza yale ambayo amefundishwa katika viwanda au katika karakana mbalimbali. Akitoka pale baada ya miaka miwili ni fundi kamili ambaye ni hands on.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi sasa hivi wanahitaji blue collar jobs, siyo white collar jobs ambapo ana degree yake haimsaidii, hapati ajira. Ingewezekana tungebadilisha sheria kama nchi nyingine, badala ya kwenda JKT ukimaliza Form Four, kila mtu apitie kwenye mfumo huu wa VETA wa kupata skills za aina fulani ili katika maisha kama huna ajira, angalau unajua kitu kingine cha kufanya ambacho kitakupa ajira kwa wakati huo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nashauri, nashukuru kwamba Ofisi ya Uwekezaji sasa iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wanaendelea kuratibu vizuri sana. Tunaomba suala zima kwa kupitia ile road map tumepata hii blue print, tunaomba sasa sheria ile ya blue print ije kwa haraka zaidi ili itekelezwe kusudi gharama za uzalishaji hapa nchini ziteremke, bidhaa zetu ziweze kushindana kwenye soko la ndani na la nje kwa gharama. Hiyo inawezekana kwa kupitia hiyo sheria ya blue print kutekeleza yale yote ambayo yako kwenye blue print.

Mheshimiwa Spika, pia ombi lingine ambalo ni muhimu sana lifanyiwe kazi kwa kupitia uwekezaji, ni suala hili la BRELA, kampuni nyingi zinadaiwa penalty na interest kutokana na kutokuwasilisha returns kwa miaka mingi. Naomba kama mlivyofanya kwenye Kodi ya Mapato, mngewapa msamaha ili tuanze moja. Kwa sababu zile penalty kwa tozo za shilingi 14,000/=, yaani hakuwasilisha kipindi kile, leo ni shilingi milioni 10. Sasa mtu anaona kuanzisha kampuni ni shilingi 300,000/= kwa nini nifufue ile kampuni inadaiwa shilingi milioni 10? Ni vizuri tukafuta yale madeni tuanze fresh…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jitu Soni. Malizia.

MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
The Finance Bill, 2016
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nitoe pongezi kwa Serikali kwa kuja na bajeti nzuri, lakini pia nitoe pongezi kwa mfumo mpya huu wa kutaka TRA ndiyo iwe inakusanya mapato yote ya kodi na yasiyo ya kodi. Muhimu pale nitaomba kile Kitengo cha Elimu na Utafiti kiboreshwe kule TRA pamoja na Wizarani. Hili liwe endelevu, lisiwe jambo la zimamoto na la muda mfupi, yale mambo ambayo tunataka yafanyike basi, iwe ni kazi ambayo itafanyika mwaka mzima, iwe ni idara kamili ambayo itafanya kazi mwaka mzima. Kuna mengi ambayo wanaweza wakafanya, Kitengo cha Elimu kiendelee kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu faida za kulipa kodi na hizo kodi zinafanya kazi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kitengo cha Utafiti kiangalie biashara mbalimbali kama ni Sekta ya Kilimo, Sekta ya Viwanda na kadhalika ili wakifanya utafiti, wakijua gharama za uzalishaji, kodi na tozo mbalimbali, wanaweza kuishauri Serikali. Hii ni kwa sababu kila mmoja anayetoza anaona ya kwake ni hiyo moja tu, lakini ukizikusanya kwa ujumla zile kodi, tozo na gharama za uzalishaji, ndiyo maana tunakuwa hatuwezi kushindana katika soko. Kwa hiyo, kitengo hicho kikiboreshwa Wizara ya Fedha, lakini pia na TRA, nina uhakika kwamba huko tunakoelekea tutapata mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kuzungumzia ni kwamba tuwe na one stop center, urahisi wa kufanya biashara, moja hii ni ya kodi lakini nyingine basi iwe katika kila wilaya au katika mkoa, ukitaka leseni, ukitaka kufanya jambo lolote, ukifika kwenye center moja huduma zote muhimu unaweza kupata hapo. Ifike mahali huko tunakoelekea hata kwa wananchi wa kawaida, akitaka cheti cha kuzaliwa, leseni ya kuendesha gari, akifika kwenye center moja anapata huduma zake zote. Ukimrahisishia mwananchi huduma zote, nina uhakika hatajali kulipa hiyo kodi yake ili tuwe na maendeleo katika nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naipongeza Wizara na naomba kuna mengi ambayo bado tunapenda yafanyiwe marekebisho, lakini basi pawe na mfumo endelevu ambapo tutatoa maoni yetu na Wizara ifanyie utafiti. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Serikali inapata kodi yake na hizo kodi tuhakikishe kwamba huko panapolengwa, basi hizo fedha ziweze kwenda na kazi yote ambayo inategemewa kufanywa iweze kufanywa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sekta ambazo tunazitegemea kwa mfano Sekta ya Kilimo, ningeomba basi na yenyewe pale Wizara ya Fedha pangekuwa na kitengo kabisa chenye wataalam waliobobea katika sekta hiyo ili wawe wanafanya utafiti, wawepo na wataalam katika viwanda na iwe ni process endelevu. Haya yote yakifanyika, nina uhakika mwakani tutafanikiwa. Vile vile wakati tunapoandaa bajeti isiwe kwamba, wafanyabiashara na wale wote ambao wanataka kuwekeza washtukie kwamba kila mwaka sera inabadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili likiwa ni endelevu na maoni yanachukuliwa huko tunakoelekea patakuwa tunajua kabisa kwamba, mwaka huu tunategemea kodi itapanda kwenye jambo moja, mbili, tatu na kwenye jambo moja, mbili, tatu kodi itateremka, wala hatutakuwa tunashtukia au hiyo siku ya Bajeti ya Waziri inakuwa ni jambo la siri. Tuwe kama nchi zingine unajua kabisa kabla ya miezi kadhaa jambo hili litapanda, hili litashuka, kwa hiyo mtu anajipanga vizuri. Tukiweza kufika huko, nina uhakika hatutakuwa wategemezi, ile mikopo ambayo tunahitaji tutaendelea kupata kutoka nje, lakini sehemu kubwa ya bajeti yetu itakuwa tunapata kutoka ndani ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu lingine katika hili la kutumia EFD machines tunaomba Waziri wa Fedha aelekeze TRA wakati wanapoanza katika maeneo waliyotoa zile mashine na wafanyabiashara wanaotaka kununua wenyewe maelekezo kamili yatolewe, wasije wakaaanza baadaye ikawa ni manyanyaso kwa wananchi. Maeneo ambako elimu imetolewa, hakuna Mtanzania anakataa kutozwa lakini isije ikawa ile ya kuviziana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine zikitolewa mashine basi zitolewe kwa usawa, kama kuna mtaa mmoja wote wanafanya biashara moja, wote wawe na mashine, pakiwa na fair play nina uhakika hakuna mfanyabiashara atakataa kuwa nayo, kwani lengo ni kukusanya. Hata hivyo, haiwezi kuwa sehemu moja mtu ana mashine, wengine hawana. Lengo ni kupata kodi, lakini la muhimu Watanzania wengi wakilipa, wajue kwamba Serikali itaweza kuteremsha kodi ili kila mmoja awe compliant.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na timu yake nzima kwa bajeti nzuri pia kwa Sheria hii ya Finance Bill ambayo imekaa vizuri sana, tunawapongeza. Kwa niaba ya wakulima wote wa nchi hii, lakini pia kwa niaba ya huduma zingine zote za jamii, tunawapongeza. Najua hatukupata yote na huwezi kupata yote siku zote. Tunaomba mwendelee na moyo huo na naamini kwamba huko tunakotarajia tutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutoa ushauri. Kuna maeneo ambapo tungependa Wizara iendelee kuangalia. Pamoja na kuwa wametoa msamaha mwingi sana kwenye sekta hii ya mbegu kwa Wizara mbalimbali ambapo haipo Wizara ya Fedha. Kwa mfano (skills development levy) kwenye sekta ya kilimo, masuala ya OSHA, masuala ya fire, weights and measurements na ushuru wa mazao. Ingawa sheria kupitia kilimo inasema ushuru wa mazao hautatozwa kwenye mbegu bado unaendelea kutozwa. Kwa hiyo ni mambo ya kiutawala. Naomba muiweke sawa ili watu wasiendelee kusumbuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tulileta mabadiliko ya sheria kwenye Gaming Act ambapo tulipendekeza na tunaendelea kuomba kwamba badala ya six percent iwe 12 percent na zile three percent kuwa six percent na ile 18 percent kwenda 21 percent. Zile fedha za nyongeza zote tulikuwa tunaomba ziende kwenye Mfuko wa Mazingira ambao hauna chanzo chochote cha mapato. Itaweza kusaidia Mfuko wa Mazingira kufanya kazi yake vizuri na mazingira ndiyo afya ya nchi yetu kwa sababu hali iliyoko huko ni mbaya na hii ni moja katika vyanzo ambavyo vingeweza kusaidia mfuko huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuondoa motor vehicle licence kulipa kila mwaka, badala yake tutalipa mara moja wakati tunasajili, naona watu wengi bado tunaendelea kujichanganya. Hii ni Sheria ya Traffics, Traffic Act – motor vehicle licence. Tunachanganya Sheria ya excise duty ambapo ni sh. 40/= imeongezwa kwenye mafuta yoyote siyo kwa kufidia hii Sheria ya Motor Vehicle Act, hii ya leseni. Ile sh.40/= inaenda kwenye Mfuko wa Barabara, hao ambao tunawatetea kwamba mafuta ya taa yakipanda maisha yao yatakuwa magumu hivi hamhitaji wapate barabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hiyo pesa ije Babati Vijijini na maeneo yote ya vijijini tunaomba hiyo pesa ije barabara zipone. Tungeomba Wakala wa Barabara Vijijini ingeanzishwa haraka ili iwe kama TANROADS sasa iwe ya vijijini ili suala hilo lifanyiwe kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kushukuru kwamba kwenye suala la nyumba property tax imekaa vizuri kabisa. Pia tuendelee kukumbusha kwamba suala la wazee mlishaliondoa kuanzia mwaka jana, naona watu wengi wanachangia, suala la wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 60 kama ilivyokuwa kwenye afya na maeneo mengine wameshasamehewa. Kwa hiyo, mzee kama ana nyumba tatu au nne, achague moja asamehewe zile zingine za biashara aendelee kulipa. Kila Mtanzania alipe kodi kwa kiwango chake.

Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu tunaomba Wizara iangalie kwamba mtu asije akaonewa, yule mdogo ukamtoza kubwa zaidi na yule mkubwa ukamsamehe. Tunachotaka ni pawe na uwiano wa kodi, kila Mtanzania mwenye uwezo alipe kodi, kidogo kidogo na njia hiyo ni kuondoka kwenye ile sekta isiyokuwa rasmi tuje kwenye sekta ambayo ni rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iendelee kufanyia kazi namna ya kurasimisha sekta isiyo rasmi, kwa sababu vivutio vya kuondoka kwenye sekta isiyokuwa rasmi kuja kwenye rasmi bado havijawa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko tunakoelekea kwenye uchumi wa viwanda, naendelea kuomba kwamba Serikali iangalie, ije na mfumo wa kodi ambao unaweza kukaa miaka mitano bila kugusa, ili watu wote ambao wanataka kuwekeza wawe na uhakika kwamba siyo kila mwaka patakuwa na mabadiliko, kama mabadiliko basi yawe ni kupunguza siyo ya kuongeza. Kila Mtanzania akilipa kodi naamini mengi zaidi yanaweza kufanyika kutokana na mapato ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naendelea kuomba kwamba kwenye mfumo wetu Wizara iangalie, Serikali kwa ujumla iangalie pamoja na Bunge. Leo hii tunaanza kukimbizana kipindi hiki cha dakika ya mwisho, naomba bajeti hii ikishapita, tukishaanza Julai Mosi, basi ndiyo iwe mwanzo wa bajeti ijayo. Tuanze kukutana mapema, mipango yote, yale ambayo tunatarajia yapande, yashuke, tuwe tumepanga kabla ya Oktoba ili Halmashauri zote, Serikali, na Idara zote wakati wanaenda kupanga bajeti zao tujue kabisa hii haitaruhusiwa kupangwa kwenye bajeti yao kwamba ni chanzo cha mapato na yale ambayo tumesema yaongezwe, wajue kabisa huku ndiyo watapata nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwapongeza TRA kwa kukusanya mapato yote. Naomba hata yale mengine ambayo bado hayako kwenye orodha ongezeni, mapato yote yawe centralized. Muhimu tujue, mimi kwenye Halmashauri yangu kama nilikuwa nimeweka wakala wa kukusanya mabango labda ilikuwa ya kwangu ndiyo maana nanung’unika, lakini kama hayo mabango utanirudishia hiyo pesa, nanung’unika nini? Kwa sababu TRA itakusanya badala ya huyo wakala ambaye ni private na hiyo pesa itakuwa inaratibiwa vizuri. Pesa zote hata hiyo ya property tax, mabango, kila Halmashauri ipeleke bill yake vizuri na nina uhakika Serikali italeta hizo pesa, muhimu ni kuangalia pesa zitumike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza kwa hilo na nina uhakika hizi pesa zitakuwa na matumizi mazuri. Wengi wamelalamika kwamba kwenye bajeti hii inaumiza wadogo, hakuna kuumiza mdogo. Hii bajeti itasaidia uchumi wa nchi hii na patakuwa na maendeleo, nina uhakika miradi ya maji, miradi ya umeme yote itafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu zaidi tunakushukuru kwamba kulikuwa na wengine wanasema suala la kuondoa pasiwe na tani moja, mtu ambae analima chakula apeleke kiasi chochote kutoka Wilaya moja kwenda nyingine. Naomba sisi kama viongozi ndiyo tuwe wa kwanza kulipa kodi, kwa sababu kama ni gunia kumi, hakuna familia inayokula zaidi ya gunia kumi kwa mwaka, hakuna!

Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza Waziri na Mheshimiwa Rais kwa agizo hilo, nina uhakika, hiyo inatosha. Kwenye hayo mazao mengine, kila mmoja alipe kodi kwa sababu, kama unafanya kazi kwenye Wilaya ya mtu
mwingine hiyo Wilaya pia inataka i-survive, wewe kwako unapoona kwamba huhitaji, ile Wilaya nyingine inahitaji kodi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru lakini naendelea kuomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nichukue fursa hii kwanza kabisa nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa siku ya leo. Pia nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kupitia Wizara ya Maji kwa kuleta muswada huu ambao Wabunge tumeuomba kwa muda mrefu sana. Haya mabadiliko yanatarajia na tunaamini kabisa yataleta mabadiliko makubwa katika kutoa huduma ya maji na hasa maji vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mjumbe wa Kamati ambayo tulipitia muswada huu na tunashukuru kwamba asilimia kubwa ya maoni ambapo Kamati iliyotoa tayari yamefanyiwa marekebisho, tayari Serikali imekubali na tunaamini kabisa sasa kwenye utekelezaji tutapata manufaa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni moja kwenye National Water Fund ni mfuko ambao tunatarajia utakusanya fedha kutoka maeneo na vyanzo mbalimbali ili kuboresha huduma ya maji. Lakini pia tutakuwa na chombo hiki kipya RUWASA hapa imependekezwa kuwa Rural Water Authority sisi tulikuwa tumependekeza iwe RUWASA yaani Rural Water and Sanitation Authority.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaomba ile shilingi 50 ambayo tulitenga huko nyuma ambayo inaenda kwenye Mfuko wa Maji sasa moja kwa moja iwe ni chanzo cha kudumu katika maji vijijini. Lengo huko nyuma ilikuwa ni kwa ajili ya kusaidia huduma ya maji vijiji ile shilingi 50 kwa lita nilikuwa napendekeza kwamba hiyo iandikwe moja kwa moja kwenye sheria kwamba mbali na huu Mfuko wa Maji ambao utatafuta vyanzo mbalimbali lakini ile shilling 50 iende moja kwa moja katika huduma za maji vijiji ili wananchi huko vijiji waweze kupata huduma za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunashukuru kwamba suala la sanitation pia limewekwa wazi na bayana ipo sasa kwenye jina kabisa na hiyo italeta dhana tofauti kwamba hata huko vijijini sasa ambapo tutakuwa na huduma ya maji sio tu kupata maji safi tu na salama lakini pia namna ya kuifanyia kazi mazingira yaani maji yale ambayo ni waste water.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ulewa tofauti na hata katika uchangiaji hapa tumeona kuwa na wengi wanachangia kuwa ile sheria inaposema mtu atakapokuwa anatumia maji vibaya yaani labda mtu ameoga kwenye chanzo cha maji au kwenye eneo ambalo kuna huduma ya maji. Hiyo kwenye eneo ambapo kuna tank au kuna miundombinu iliyojengwa sasa hatutarajii kwa kweli kwamba mtu yeyote ataenda kwenye miundo mbinu ya maji ambayo ina-supply maji hapa Dodoma au kwenye mji wowote au hata kwenye kijiji aende akafanye uchafuzi wa mazingira pale yaani kwa kutumia maji yale vibaya kwa sababu yale maji yanaenda kutumika na binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo ni ombi lingine ambapo Serikali ifanyie kazi na tukielekea kwenye bajeti kwa sasa hivi vifaa vingi tunatafajia huko mbele RUWASA itakuwa ina shughulika na uchimbaji wa maji visima, lakini pia na kutengeneza mabwawa, njia ya pekee ya kuhakikisha kwamba tuweze kupata maji safi na maji salama lakini pia maji kwa matumizi yote ni kuhakiksha kuwa tunavuna maji ya mvua katika maeneo mbalimbali na hasa huko vijiji ni kujenga mabwawa na maeneo ambapo inaleta athari kubwa ambao tunapata maafa yale maji yote tungekuwa tunayavuna tunayaweka kwenye mabwawa,imi nina uhakika kabisa ingekuwa hiyo athari ya mafuriko isingekuwa inapatikana, lakini yale maji tungekuwa tunavuna tungekukwa tunapata maji ya mifugo, maji ya matumizi ya nyumbani, maji kwa ajili ya uwamwagiliaji lakini pia ufugaji wa samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini njia ya pekee ya kuhakikisha hilo linaweza kufanyika ni kuwa na vifaa vya kutosha vya kufanya kazi hiyo Serikali peke yake kwa vijiji tulivyokuwa navyo na maeneo tuliyokuwa nayo haitaweza. Tulikuwa tunaomba Serikali ingalie kwenye bajeti ijayo kwamba kodi zote katika earth moving equipment yaani mitambo ambayo ni ya kuchimba maji, lakini pia mitambo ambayo inaweza kutengeneza mabwawa excavator na bulldozer yaondolewe kodi, ikishaondolewa kodi watu wengi wataingiza hasa zingine ambazo ni used bei yake ukipigana damping charges na nini inakaribia sawa na bei mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo kodi ikiondolewa patakuwa na usindani watu wengi watakuwa na hiyo mitambo ikiwa mingi, tukiangalia nchi mbalimbali hata wenzetu hapa Kongo tu na Kenya bei yao ya uchimbaji maji tofauti na kwetu na hata ukiangalia kule mahali ambapo hiyo mitambo inatengenezwa bei yao ni chini ya shilingi 10,000 kwa mita kwetu ni shilingi 150,000 mpaka 200,000 kwa mita. Kwa hiyo, ukiondoa kodi nina uhakika jambo hilo litaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulishawahi sheria kwamba kwenye makazi yote vibali vikitolewa vya ujenzi basi lazima huyo mtu aonyeshe michoro na miuondo mbinu ya uvunaji wa maji ya mvua. Kwa sababu yale maji yote tukiweza kuvuna katika nyumba zote ambazo zinazojengwa itaweza kusaidia kwa sehemu kubwa kuhakisha kwamba tunapata maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ombi lingine Serikali ikae na pamoja na Wizara nyingi zote kwa pamoja kuangalia kwamba sasa tumeelekea kutumua maji ya ardhini ground water kwa sehemu kubwa. Ni vyema sasa tuhakikishe kwamba recharge ya ile ground water sasa elimu iendelee kutolewa namna bora ya kuhakikisha kwamba yale maji tunavuna toka ardhini tunafanya teknolojia gani itatumika na mbinu gani itatumika ili sasa yale maji yaweze kuwa recharged.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini muhimu ambalo ni kwa uelewa kwa watu wote hii sheria ni kwa ajili ya maji na maji taka au usafi wa mazingira ambayo inahusu miundombinu na upatikaji wa maji. Hii sio ile sheria ya maji ambapo ina vitu viwili tofauti vyanzo vya maji na zile mabonde yote yale yako kwenye ile sheria nyingine tulikuwa tunaomba mahali ambapo inakinzana na mahali ambapo hizi sheria haziende pamoja kuna mabadiliko mengi yanatakiwa yafanywe kwenye ili sheria nyingine ili iweze kuendana na sheria hii. Tunashukuru Wizara imesema itaifanyia kazi na hiyo sheria nyingine wamesema wataileta ili wafanyie mabadiliko hayo yote mawili yakifanyiwa mabadiliko nina uhakika kwamba huko tunakoelekea sasa tunakuwa tunapata mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limekuwa muhimu ni kuhakikisha kwamba matumizi ya maji kwamba maeneo mbalimbali na humu mahali ambapo huko nyuma ilitajwa kwamba kuna gharama za matumizi ya maji. Ni vizuri wadau wote sasa wahakikishe kabisa wale wanakaa pamoja na huduma ya maji iweze kupatikana kwa bei naafuu ili wananchi haswa huko vijiji waweze kupata maji safi na salama na pia tukiweza kufanya hivyo gharama nyingi ambao tunatumia kwenye matibabu kwa Wizara ya Afya pia hizo gharama zitapungua kwa sababu magonjwa mengi yanatokana kutokuwa na maji safi na maji salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu kubwa sisi tulivyopitia muswada huu tunaamini kabisa itakuwa na manufaa makubwa ombi letu ni kwamba Waziri sasa ajitahidi kwamba sheria hii itakapopitishwa kanuni zile ziandaliwe mara moja ili sheria na kanuni ziende kwa pamoja na manufaa kwa wananchi iweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo ni vizuri sasa Wabunge tutakapofika kwenye kipindi cha bajeti tuangalie vyanzo vingine vya mapato ili sasa tuweze kupendekeza hasa RUWASA ambayo ni maji vijijini iweze kuwa na fedha kutosha kutekeleza miradi. Mbali na hiyo pia kuangalia namna bora na baadhi na miradi ambapo inawezakana kwa kutumia force account Wizara izingatie ili iweze kutumia force account.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 6) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia jioni hii. Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kuishukuru sana Serikali na kuipongeza kwa kuleta mabadiliko haya ya sheria mbalimbali na kwa kweli kwa kuleta hizi sheria kutakuwa na mabadiliko makubwa katika hizi sheria tisa walizoleta sekta hizo zitapata unafuu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite katika maeneo mawili; kwanza kabisa niipongeze Kamati ya Sheria Ndogo ikishirikiana na Serikali kwa uchambuzi wa ndani kwa sababu wameweza kutuletea na wakatafsiri ndiyo maana hakuna Mbunge hata mmoja aliyesimama hapa anahoji, kila mmoja anaunga mkono kwa ajili ya kazi nzuri na kubwa ambayo mmeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuleta mabadiliko ya sheria sura 148 katika Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Niipongeze Serikali kwa sababu ile misaada ambayo ilikuwa tupate au zile benki au taasisi ambazo zilikuwa zitukopeshe kwa riba nafuu sasa zitaweza kutukopesha na miradi mingi itaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu; kwenye ambayo imewekwa kwa miradi ambayo inatekelezwa na Serikali, naomba kwenye hiyo tafsiri msije mkasahau Serikali za Mitaa, kwa sababu zote, Serikali na Serikali za Mitaa kwenye sheria isipokaa vizuri misaada ambayo itaelekezwa Serikali za Mitaa tunaweza kuja kukwama. Kwa hiyo, naomba mjitahidi katika tafsiri wakati inapowekwa basi suala hilo la tafsiri ya Serikali ya Mitaa muiweke ili iweze kutusaidia katika misaada mbalimbali ambayo inakuja katika ngazi hiyo ya halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipongeze kwa kuondoa kodi katika malighafi kwa kupitia hii sheria katika kiwanda kile ambacho kitazalisha neti za muda mrefu ile cha A to Z Arusha, itaweza kuwasaidia ili waweze kushindana katika soko la kimataifa ambapo soko kubwa ndiyo liko huko. Lakini ombi langu ni kwamba pamoja na hii sheria mtaweza kuwaondolea Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye hiyo bidhaa ambayo wanaingiza ya kutengenezea hizo neti, bado hawataweza kuwa kwenye ushindani sawa na wengine kwa sababu tatizo halipo Wizara ya Fedha, tatizo halipo kwenye hizi kodi zetu ambazo zinasimamiwa na TRA, tatizo lipo katika hizi regulatory authorities.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba mjitahidi kuleta ile sheria ya marekebisho ya blueprint regulatory reform. Hizo ndiyo zitasaidia kuondoa na kupunguza gharama ya uzalishaji kwa sababu hapa mlipoondoa itaondoa kasehemu kadogo sana kwa hiyo bado kwenye ushindani wa bei bado hamtaona mafanikio makubwa. Lakini mkija na zile reforms za regulatory authority zile tukizifanyia kazi ile blueprint nina uhakika gharama ya uzalishaji itapungua na siyo kiwanda hiki kimoja tu, kuna viwanda vingi vitaweza kushindana katika soko la ndani lakini pia katika masoko ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tozo ambazo zinatozwa na hizi taasisi zetu za udhibiti (regulatory authorities) ni nyingi sana na ni kubwa. Kwa hiyo, tatizo kubwa halipo Wizara ya Fedha kwa kupitia zile kodi zake ambazo huwa tunapitisha za TRA lakini sehemu kubwa ya uzalishaji, gharama kubwa iko huku kwenye hizi regulatory authorities. Kwa hiyo, tunaomba mwezi Novemba kama inawezekana muilete mapema ili tuifanyie marekebisho inayostahili yale ya kisheria ili gharama za uzalishaji zipungue na watu waweze kuzalisha kwa unafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishukuru Serikali kwa kuleta katika Sura 41 kifungu 33 hii michezo ya kubahatisha. Nashukuru kwa sababu tatizo hili, pamoja na kuwa ni faida kubwa kwetu, inaingiza mapato makubwa, lakini tayari imeanza kuwa na athari kubwa katika jamii kwa sababu watoto wengi, vijana wengi wameingia huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Babati limeweza kutokea tatizo wiki iliyopita tu mpaka imefika mahali mtoto wa miaka 12 amevunjwa mikono na amepelekwa hospitali. Sasa hiyo yote ni kwa sababu hizi mashine zimejazwa mpaka vijijini mashine zimejaa, watu sasa hivi wanaona ni bora kuliko kwenda kulima kufanya kazi ajaribu bahati yake. Mmoja kwenye kijiji akiweza kufanikiwa kupata shilingi laki mbili basi wote wanaona kila mmoja ataweza kufanikiwa lakini kwa upande mwingine inatuumiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishukuru kwamba kwa Ibara ya 66 Sura 16 katika matumizi ya kutuma picha mbalimbali, picha ambazo ni za kutisha. Nashukuru kwamba hii sheria sasa imeletwa na imepitishwa. Ombi moja kubwa kwamba tuendelee kutoa elimu kwa wingi, yaani muhimu sana elimu iendelee kutolewa ili watu waweze kuelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata tukiangalia katika mitandao mbalimbali kwa mfano hata TVs za nje hawaoneshi picha hizi mbaya na za kutisha na wakitaka kuonesha wanatoa tahadhari kwamba kinachofuata kama huwezi kuangalia usiangalie kina content ambayo siyo nzuri. Kwa hiyo, niwashukuru kwamba jambo hili litaweza kuweka privacy, pia itaongeza haki za watu badala ya picha mbalimbali wakiwa katika msiba au maeneo ambapo hawataki picha zao zipigwe na zitumwe katika mitandao na kutumika vibaya, itasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishukuru kwamba suala zima lile la kwamba bodi ambazo zitakuwa zimeisha muda wake bado patakuwa na fursa ndani ya mwaka mmoja bodi zitakuwa zimeundwa ili kurahisisha na kuhakikisha kwamba shughuli zote za taasisi hiyo ziweze kuendelea kama kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kama walivyosema Wabunge wenzangu wengi, suala la kuweka interest kwenye adhabu. Ninaomba Serikali ifikirie suala hili la interest wakati inapotunga ile kanuni yake basi iwe fair na iangalie kwa undani. Kwa sababu inawezekana kwamba mtu hakukusudia kufanya kosa hilo, amejikuta kosa limefanyika anatakiwa kulipa adhabu na ile adhabu kwa wafanyabiashara wengine inaweza kuchukua muda kulipa kwa hiyo, bado hujamuondolea adhabu, itakuwa adhabu inaongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia upande wa pili, kwamba je, kama ingekuwa ni kosa hilohilo limetendwa na kwa upande wa pili, upande wa Serikali wao walitakiwa kulipa; je, ingekuwa na wao wanalipa na interest? Sasa tungekuwa tunaiangalia kwa sura zote mbili kwamba ingekuwa tunaangalia kwa upande mmoja tu, kama ni criminal offense huko nakubaliana lakini kama ni hizi offenses za kawaida katika biashara za kawaida basi Serikali iendelee kuwa na ule msamaha na iendelee kuangalia watu wasije wakaitumia sura hii kwa ajili ya kutoza watu ili adhabu iwe kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sehemu kubwa jambo kubwa ambalo nimefurahia ni suala la VAT na niipongeze Serikali, muendelee kutuletea hizo regulatory reforms ili tuweze kuzifanyia kazi mwezi Novemba ili uchumi wetu uendelee kukua na tuingie katika uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)