Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jitu Vrajlal Soni (6 total)

MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiuliza Serikali, je, katika maeneo ambapo sisi kama wananchi na viongozi tumejitahidi, kwa mfano, Kituo cha Afya Magugu tumeweza kuwekeza vifaa mbalimbali ambavyo ngazi hiyo haina mpango au kwa mpango wa Serikali haipeleki wataalam wa aina hiyo, kwa mfano, tuna ultra-sound na vifaa vya macho. Je, Serikali itakuwa tayari mahali ambapo sisi wananchi tumewekeza vifaa mbalimbali ituletee wataalam wa ngazi hiyo? Kwa mfano, Kituo cha Afya Magugu watuletee Madaktari wa Upasuaji wa Macho na wa Ultra-sound kwa sababu vifaa vyote tunavyo na havitumiki. Inabidi tuombe wataalam kutoka mkoani wawe wanakuja mara moja kwa wiki kutusaidia. Je, Serikali itakuwa tayari kutusaidia wataalam hawa?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nikiri miongoni mwa Wabunge ambao wanafanya kazi kubwa ni Mheshimiwa Jitu Soni. Mwaka juzi nilikuwa ni shahidi Detros Group ya Arusha imesaidia vifaa vyote kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Magugu. Kwa hiyo, juhudi hii amefanya Mbunge akashirikiana na wadau wenzake kutoka Arusha lakini kusaidia Mkoa wa Manyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri katika mgao wa mwaka huu zoezi kubwa tunalokwenda kufanya, juzi nilijibu swali hapa kwamba mwaka huu mkakati wa Serikali ni kuajiri watumishi wapya wa afya 10,780. Katika watumishi hao wapya ambao tunakwenda kuwaajiri, naomba nikuambie Mheshimiwa Jitu Soni; Kituo cha Afya cha Magugu kitapewa kipaumbele kwa sababu wananchi wa Manyara, Babati Vijijini mmefanya kazi kubwa, lengo letu akinamama wapate huduma bora pale. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nitoe tu majibu ya ziada kwamba Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jami ipo kwenye mchakato wa kutengeneza utaratibu wa kuwasainisha mikataba maalum watumishi wote ambao wataajiriwa kuanzia sasa kwa kipindi maalum, kama miaka mitatu ama miaka mitano ili wasiondoke kwenye maeneo ya pembezoni kama ilivyo kwenye Kituo cha Afya cha Magugu.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuiuliza Serikali, hii miradi yote ya mwaka 2015/2016 ambayo tunaendelea nayo ambayo fedha zake hazijaenda kwa mfano Babati Vijijini na zimebaki siku kumi, je, kipindi hiki cha bajeti cha 2017 mbali na hii pesa iliyotengwa, hii ya nyuma yote tutapatiwa ili ile miradi ambayo haijatekelezwa itekelezwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Jitu Soni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kushukuru Ofisi ya Wizara ya Fedha wamefanya kazi nzuri, wamekusanya fedha na wanatupatia na hata wiki iliyopita walitupatia zaidi ya shilingi bilioni 15. Katika Bunge hili nimekuwa nikiagiza kwamba Waheshimiwa Wabunge wawaambie Wakurugenzi wa Halmashauri yeyote aliye na hati mkononi ailete ili tuweze kulipa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jitu Soni kama kuna certificate, sijui kwa siku hizi zilizobaki itawahi kwa sababu tarehe 26 ni mwisho, inabidi tuwe tumeshamaliza kulipa lakini hata hivyo wala usiwe na wasiwasi hata ukichelewa kama certificate ipo naomba ije ili tuweze kulipa. Nikuhakikishie kwamba miradi yote ambayo ilikuwa haijakamilika Mheshimiwa Jitu Soni tutahakikisha kwamba tunaikamilisha.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naishukuru Serikali kwa kututengea fedha kwenye barabara ya Mbuyu wa Mjerumani Mbulu ambapo ina daraja la Magara ingawa fedha hiyo ni kidogo na imetengwa katika maeneo matatu au manne. Wabunge wa Babati na Mbulu tukishirikiana na Mheshimiwa Issaay na Mheshimiwa Flatei, tumekuwa tunaomba ile fedha yote iliyotengwa mwaka huu shilingi milioni 300 kama inawezekana na tumeshawasilisha kwa uongozi wa Mkoa, iende kujenga daraja la Magara ambapo itaonyesha mafanikio badala ya kuitumia katika maeneo mengine. Tunaomba Wizara itukubalie tupeleke fedha hiyo kwenye daraja na likikamilika basi hayo maeneo mengine yaendelee kufanyiwa kazi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Jitu, ingawa siyo sahihi ni Jitu Soni lakini kule wanasema Mbunge wetu ni Jitu lakini nadhani wana maana ya umakini unaotumia katika kufuatilia mahitaji yao. Nampongeza sana kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu hili halimhusu yeye pake yake, linamhusu Mheshimiwa Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini na Waheshimiwa Wabunge wengine kama watatu hivi. Naomba kuwahakikishia kwamba ombi lenu tumelipokea, tutalitafakari na tutalifanyia kazi.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nilikuwa naomba niulize Serikali na niulize Wizara ya Maliasili na Utalii, je, ni lini sasa italipa fidia au italipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi katika hifadhi zote ambazo zinapakana na wanyamapori, leo ni mwaka wa tano fedha ambazo wananchi wamelipwa ukizingatia vijiji 16 Wilaya ya Babati Vijijini bado hawajalipwa wamelipwa shilingi milioni 12 tu kati ya shilingi milioni 100 na, na nikifuta jasho na wala siyo fidia.
Je, ni lini na ni lini sasa Serikali itakuja tulipendekeza hapa kwamba hifadhi husika ndiyo ziwe zinalipa hizo fidia badala ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili iwe rahisi sasa hifadhi ambazo ziko jirani na hivyo vijiji waweze kulipa mara moja ili wananchi hao sasa wapate unafuu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na naomba nijibu swali la nyongeza moja au mawili pengine inaweza kuwa moja kwa mawili kadri alivyouliza Mheshimiwa Mbunge.
NAIBU SPIKA: Ujibu moja tafadhali kwa sababu ndiyo kanuni zinavyosema kwa hiyo, chagua moja.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Ahsante, suala la ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi, yapo mambo mawili jambo la kwanza ni utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa kanuni kwamba ule ni lazima utimie ukamilike na ambao unaanzia kwenye ngazi ya kitongoji au kijiji kwenda wilaya kwenda mkoa halafu kwenda hifadhi inayohusika na mpaka kwenye Wizara. Yale maombi au madai yanayopata sifa za kuweza kulipwa sasa yataingia kwenye kikwazo kingine cha pili ambacho si kikwazo lakini ni utaratibu kwamba kuna suala pia la bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna suala la kutimiza vigezo halafu kuna suala la uwepo wa fedha. Sasa yale yanayohusiana na utaratibu kwa sababu unahusisha pia Wizara kama kuna madai ambayo yamekidhi vigezo lakini pengine yanachelewa kwa sababu tu ya procedure za kiofisi hayo tunakwenda kuongeza kasi kuharakisha ili yakae pending kusubiri uwepo wa fedha na fedha zitakapokuwa zimepatikana madai yote yanayohusiana na kifuta jasho, na kifuta machozi yatalipwa mara moja.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliouliza swali hilo hilo la 0.3 percent service levy. Naomba kuuliza, je, Serikali itakuwa tayari pamoja na hiyo bodi mpya kuundwa, tunashukuru imeundwa kuwanyima leseni hoteli zote za kitalii ambazo zinafanya biashara ndani ya maeneo yetu ya halmashauri zote nchini ambao hawajalipa arrears za nyuma na kila mwaka kabla hawajapatiwa leseni mpya kama ilivyokuwa kwenye kodi nyingine, wasipewe leseni kabla ya kuhakikisha kwamba kodi zote za halmashauri zetu zimelipwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na kila jambo ambalo ni kubwa linagusa maslahi ya wananchi, linagusa maslahi ya Taifa ni vizuri tukaliacha likaenda kwa kufuata taratibu za kisheria. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa tumesema kwamba madamu bodi imeshaundwa, tunakwenda kupitia hukumu lakini pia kwa kuzingatia Sheria zilizopo tunaenda kuangalia namna ambavyo maslahi ya Taifa yanazingatiwa. Ikiwa kutakuwa kuna mapungufu kwenye Sheria basi tunaweza kulazimika kufanya maerekebisho ya Sheria lakini kama Sheria iko vizuri basi tutatekeleza Sheria jinsi inavyosema ili mradi tu mwisho wa siku maslahi na maslahi ya jamii yaweze kulindwa.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niiulize Serikali badala ya kutumia fedha nyingi kujenga mabwawa makubwa au yale ya kati kwa nini isiweze kununua mitambo yenye thamani hiyo hiyo ya bwawa ikaipa halmashauri husika ili baada ya kumaliza kuchimba hilo bwawa moja waweze kuendelea kuchimba mabwawa mengine mengi na thamani ya ile kazi itakuwa ni kubwa? Hii itakuwa ni njia moja ya kutumia force account vizuri sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali zuri sana la Mheshimiwa Mbunge Soni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo hayo ni mazuri lakini mara nyingi mabwawa Mheshimiwa Mbunge hatuchimbi, tunakinga ili tuweze ku-retain maji yaweze kufanya kazi. Mawazo yako naomba tukutane baada ya kikao hiki ili uweze kunieleza vizuri tuweze kuyafanyia kazi. Sisi kazi yetu kama Wizara tunasikiliza mawazo ya Waheshimiwa Wabunge, tunayapeleka kwa wataalam ili wakiyafanyia kazi vizuri basi tuweze kuyaingiza katika mfumo wa Serikali.