Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khadija Nassir Ali (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa naomba kuchangia mawazo yangu baada ya kupitia kitabu cha hotuba ya Wizara ya Maliasili na utalii. Nimesikitishwa sana kuona hotuba yenye kurasa zisizopungua 120 kutoelezea vizuri mipango na mikakati ya sekta ya utalii Zanzibar. Sote tunajua contribution ya Zanzibar kwenye sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Wizara yako inajitihada za makusudi katika kuhakikisha utalii wa Zanzibar unainuka na unatambulika zaidi duniani, ila kiukweli wazawa hawafaidiki ipasavyo. Inasikitisha kuona hata mpishi wa hoteli ni foreigner, sitaki kuamini kwamba wazawa hawana elimu ya kutosha ku-operate hoteli na sehemu nyingi za kitalii. Ni kwa nini Wizara isichukue juhudi za kuboresha mitaala katika vyuo vyetu vya utalii vilivyo ndani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sitapata maelezo mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wakati wa ku-wind-up nakusudia kushika mshahara wa Mheshimiwa Waziri.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa nikiwa mwenye afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kasi iliyoanza nayo, imani yangu, Tanzania yetu iko kwenye mikono salama chini ya Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, sasa naomba kujikita moja kwa moja kwenye michango yangu, ambapo nitaanza kuongelea suala la ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi inazochukuwa kuhakikisha vijana wanapatiwa ajira. Pamoja na jitihada hizi bado tunauhitaji mkubwa wa ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali hizi milioni 50 ambazo zinatakiwa kwenda kwenye kila Kijiji zingetumika kuanzisha Community Bank katika kila Wilaya, ambayo vijana na makundi mengine yangeweza kukopa kwa masharti nafuu na kuweza kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee issue ya elimu. Naipongeza Serikali kwa kuanzisha elimu bure hadi kidato cha nne. Huu ni mwanzo mzuri wa kuweza kuwajengea fursa sawa watoto wote nchini kwa kuwajengea uwezo. Naiomba Serikali iweze kwenda mbele zaidi hadi kidato cha sita kufanya kuwa elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, napenda kuishauri Serikali ione namna ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wanasoma Kada za Afya na nyingine ambazo tunahitaji sana kama Taifa mfano wa Kada hizo ni kama Kada ya Utabibu, Ukunga na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee suala la kodi katika Sekta ya Utalii. Sekta ya Utalii inachangia asilimia 12 ya Pato la Serikali kwa Tanzania Bara na asilimia 27 kwa Tanzania Visiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, average ya Watalii kwa mwaka ni milioni moja na hii average imekuwa stagnant kwa zaidi ya miaka mitatu. Hii inatokana na Imposition ya kodi ambazo hazina tija katika Sekta hii. Ushauri wangu kwa Serikali iangalie upya hizi kodi na kuzifuta ili tuweze kuinua Utalii wetu kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijajitendea haki nisipoongelea issue ya CAG. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, naelewa umuhimu wa CAG naelewa kazi zake na naelewa umahiri wake. Wenzangu waliopita wameongelea sana kwa kirefu na kwa kina zaidi. Namwomba Waziri atakaposimama kwa ajili ya majumuisho atueleze ni jinsi gani atakavyoweza kupata fedha za kumwongeza CAG ili aweze kufanya kazi zake kwa umahiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo sina michango mingi, naunga mkono hoja, ahsante!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. KHADIJA N. ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Fedha na Mipango. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama hapa leo lakini pia napenda kuwapa heri ya mfungo wa Ramadhani Waislam wote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile dakika zangu ni chache, naomba sasa nijikite moja kwa moja kwenye mchango wangu na nitaanza kuongelea mtiririko mzima wa fedha za miradi ya maendeleo. Mwaka wa fedha 2015/2016, fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya miradi ya maendeleo ilikuwa ni bilioni 1,031.7 na kwa mwaka wa fedha 2016/2017, fedha zilizotengwa ilikuwa ni bilioni 791.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa Serikali imepunguza budget ceiling ya hizi fedha za maendeleo lakini bado tatizo la kupeleka fedha hizi kwenye miradi imekuwa ni changamoto kubwa. Mfano, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Wizara iliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 791.9 lakini mpaka kufikia Machi, 2017 Serikali ilikuwa imepeleka jumla ya shilingi bilioni 18.8 ambayo ni sawa na asilimia mbili tu ya bajeti ambayo imeidhinishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali juu ya hili ni kwanza, Serikali kupitia Bunge iidhinishe bajeti ambayo itaweza kwenda ipasavyo na siyo kuidhinisha bajeti kubwa ambayo haitaweza kwenda. Bajeti za Wizara ziendane na kasi ya makusanyo ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili; muda muafaka sasa kwa Serikali kuhakikisha fedha zote zinazoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo zipatikane kwa wakati ili kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga Tanzania ya viwanda. Ushauri wangu wa tatu; Serikali isitegemee sana fedha za wafadhili kwa sababu fedha hizi hazina uhakika wa kutosha, zinaweza kuja au zisije au zikaja kwa kuchelewa na hili linaweza kuathiri maendeleo ya miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza kuongea kwenye hili suala naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha anipe majibu ya maswali haya yafuatayo:-

Huu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma; Je, Serikali imetumia kiasi gani cha fedha katika mpango huu? Pili; Je, mpango huu umeathiri vipi fedha za umma ambazo zingeweza kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niingie kwenye suala la misamaha ya kodi. Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kila mwaka lakini bado misamaha hii haitolewi kwa uwazi kwa maana ya kwamba mimi na wewe na wananchi wengine hatujui misamaha hii inatolewa kwa vigezo gani. Wabunge na wananchi tunahitaji kujua projection ya misamaha hii lakini pia tunahitaji kujua uhalisia wa misamaha hii, pia ushauri wangu kwa Serikali ni kwanini isiwe ina-publish misamaha hii ili tuweze kujua kiwango na watu ambao wanasamehewa hizi kodi ni akina nani na wanatolewa kwa vigezo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nigusie kidogo issue ya deni la Taifa. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 malipo ya deni la Taifa ilikuwa ni bilioni 8,000 matumizi ya kawaida kwa mwaka huu yalikuwa ni bilioni 8,009.3 na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 malipo ya deni la Taifa yanatarajiwa kuwa bilioni 9,461.4 na matumizi ya kawaida yanatarajiwa kuwa bilioni 9,472.7. Naipongeza Serikali kwa hili, kwa kuwa wameweza kuongeza bajeti ya malipo ya deni la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali ihakikishe kuwa fedha hizi zinatolewa kwa wakati ili nchi iondokane na madeni yanayosababisha nchi kulipa fedha nyingi yaani ile fedha inayotoka kama riba ingawa Serikali inasema kwamba deni la Taifa ni himilivu lakini lazima Serikali iendane……………..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa vile dakika nilizonazo ni chache naomba sasa niende moja kwa moja kwenye kuelezea hali halisi ya kibishara inayoendelea Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zilizoungana na visiwa kama Tanganyika ilivyoungana na Visiwa vya Zanzibar hutumia visiwa hivyo kama strategic center za kibiashara kutokana na geographical position za visiwa. Kwa bahati mbaya sana mpaka sasa Serikali yetu haijaona umuhimu wa kutumia Zanzibar kama center ya kibiashara kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miezi michache iliyopita Tanzania Bara ilipatwa na shortage ya sukari ambayo kwa taratibu za Serikali ilizozichukua sina mashaka nazo, hatua ambazo Serikali imechukua ku-solve tatizo hili pia sina mashaka nazo. Mashaka na malalamiko yangu makubwa kwenye hili ni baadhi ya Watendaji wa Serikali kulichukua hili jambo na kulitekeleza kinyume na maagizo ambayo yametokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ambayo inaendelea sasa kwenye bandari yetu, Wazanzibar au wananchi wetu hawana ruhusa hata ya kuingiza sukari kilo mbili kwa ajili ya matumizi yao binafsi. Tatizo hili limekuwa kubwa mpaka sasa wananchi wetu hawawezi kuingiza hata kilo mbili za matumizi yao ya kawaida. Kisa tu tamko lilitoka, kibali hakijatoka na utekelezaji huo umekuwa namna hiyo ambayo naielezea. Kwa masikitiko makubwa sana nathubutu kusema kwamba bado sijaona faida ya kibiashara ndani ya Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuelezea malalamiko yangu, naomba sasa nielezee juu ya Wabunge ambao wamebeba agenda ya kuibeza Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla. Kuna baadhi ya Wabunge humu wamebeba agenda ya kuibeza Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla na wamekwenda mbali mpaka kujiita kwamba wao ndiyo wababe wa Wazanzibari. Niwaambie tu, mbabe wa Wazanzibari ni Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye ndiye Rais wetu na hakuna mbabe zaidi ya huyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza hayo, naomba sasa nijikite kwenye mchango wangu moja kwa moja na nitaanza kuelezea hali ya kiuchumi nchini. Ukurasa wa nane umeelezea viashiria vya kiuchumi vinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba, 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8. Sina mashaka na maelezo haya na kwa vile hotuba hii haijaonesha ni viashiria gani ambavyo vimepima ukuaji uchumi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie ripoti ya REPOA na takwimu ambazo imeonesha. Ripoti ya REPOA inaonesha kwamba mwaka 2014 asilimia 22 ya Watanzania walikuwa wanashinda na njaa wakati mwaka 2018 asilimia 27 ya Watanzania wanashinda au kulala na njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti hii pia imeonesha hali ya ajira nchini. Ripoti hii inaonesha kwamba vijana wa Kitanzania asilimia 43 walikuwa na imani kuwa Serikali itatengeneza ajira wakati mwaka 2018 ni vijana asilimia 31 tu ndiyo wenye imani kuwa Serikali itatengeneza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti hii pia inaonesha hali ya ufukara nchini. Kwa mwaka 2014 asilimia 64 ya Watanzania hawakuweza kumudu maisha yao wakati kwa mwaka 2018 ni asilimia 76 ya Watanzania hawakuweza kumudu maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia tuangalie ripoti ya Serikali kupitia Taasisi ya NBS ambayo inaonesha hali ya udumavu kwa mwaka 2014 ni asilimia 34.4 ya watoto nchini walikuwa wamedumaa, wakati kwa mwaka 2018 asilimia 34.7 ya watoto nchini wamedumaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti hiihii pia imeonesha vifo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)