Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Khadija Nassir Ali (10 total)

MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Tanzania tunalima pamba kwa wingi lakini bado tunaagiza Gauze toka Uganda ambao hawana zao la pamba, lakini pia tunaagiza Drip toka nje ya nchi wakati tuna maji ya kutosha ya kuweza kutengeneza Drip hizo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia malighafi hizo ili kuzalisha Gauze na Drip hapa nchini na kuacha kuagiza bidhaa hizo toka nje?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Khadija alivyotoa mfano wa gauze na Intravenous Fluid zinazotundikwa wagonjwa na kujulikana kama drip tumekuwa tukiagiza bidhaa toka nje ya nchi ambazo kimsingi zinaweza kutengenezwa kirahisi hapa nchini. Ukirejea mkakati unganishi wa maendeleo ya viwanda IIDS na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano, lengo lake hasa ni kuondoa upungufu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mashirika ya MSD, TIRDO, NHIF, TIB, TFDA wamepewa jukumu la kuandaa mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika Sekta ya Madawa ya Binadamu na Vifaa Tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa bidhaa inayolengwa ni ya IV Fluids na gauze zitokanazo na pamba. Chini ya uhamasishaji wa Wizara yangu na Kituo cha Uwekezaji (TIC), wawekezaji wamejitokeza kuwekeza katika Sekta ya Madawa ya Binadamu na Vifaa Tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako nitaje baadhi ya makampuni ambayo yamejitokeza. JSN solution watakaojenga kiwanda cha IV Fluid, China Dalian International group watakaojenga kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba, Zinga Pharmaceutical watakaotengeneza madawa mbalimbali ya binadam; Boryung Pharmaceutical kutoka Korea ambao watatengeneza Penicilin na Antibiotics za namna hiyo; Agakhan Foundation Network watakaoanzisha viwanda vya madawa mbalimbali na Hainan Hualon ambao watazalisha madawa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu kuwa katika hiki kipindi kifupi, tutaweza kuwa na sekta ya madawa ya binadamu ambayo pamoja na kuzalisha madawa na vifaa tiba itatoa ajira kwa vijana wetu.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itarekebisha mitaala ya elimu ili elimu
ya ujasiriamali na stadi za maisha ziweze kufundishwa kwa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na kidato cha nne ambao hawatabahatika kuendelea na masomo na hatimaye waweze kuwa na uelewa wa kujiajiri na kujitegemea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuboresha mitaala ili kuendana na mahitaji ya jamii kwa wakati husika. Mwaka 2005 Serikali iliboresha mitaala ya elimu ya msingi na sekondari ambapo masuala ya ujasiriamali yaliingizwa ili kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri. Uboreshaji huu ulihusisha pia kuingiza maudhui ya stadi za maisha kama suala mtambuka. Kwa ujumla mitaala imezingatia kutoa elimu ya ujasiriamali kupitia maudhui na mbinu za kufundishia na kujifunzia ambazo zinawafanya wanafunzi kuwa watendaji wakuu au kitovu cha kujifunza.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
• Ni vifaa gani muhimu vimewekwa kwenye vifungashio vya akinamama wakati wa kujifungua (delivery kit) takribani 500,000 zinavyokusudiwa kusambazwa na Serikali?
• Je, ni kwa nini Serikali inasuasua kwenye usambazaji wa delivery kits kama mkakati ulivyo?
• Je, ni kwa kiasi gani agizo la Mwandoya la Serikali la kuanzisha huduma za upasuaji kwenye vituo vyote vya afya nchini limetekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kuna tofauti ya matumizi ya maneno delivery kits ambayo humaanisha vifaa vyote vinavyopaswa kuwepo kituoni katika chumba cha kujifungulia na delivery Packs ambavyo, ni kifurushi muhimu anachotakiwa kupewa mama mjamzito akija kliniki kitakachomsaidia wakati wa kujifungua, kwa maana ya vifungashio (delivery packs). Vifungashio hivi vina vifaa vifuatavyo; pamba, pedi, kifungia kitovu cha mtoto, kitambaa cha kumfutia mtoto, sindano, mipira ya kuvaa mikononi (surgical gloves), mpira wa kulalia wakati wa kujifungua, uzi (chronic cutgut 2”), vidonge vya kuzuia umwagikaji wa damu na wembe. Na gharama ya vifungashio hivi ni shilingi 25,000 kwa kila kifurushi.
(b) Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, hadi sasa imesambaza vifungashio (delivery packs) 60,000 kwa mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ambayo vifo vingi vya wamama wajawazito na watoto vinatokea huko. Aidha, ni jukumu la kila halmashauri kuweka mahitaji ya vifungashio kwenye mpango kabambe wa afya wa Halmashauri, yaani Comprehensive Council Health Plan (CCHP).
(c) Mheshimiwa Spika, agizo la Mwandoya lilitaka kila Halmashauri nchini kwa kutumia pesa zao za ndani kuhakikisha wamejenga au kukarabati vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya kwa kipindi cha miezi sita, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto na kupeleka huduma karibu zaidi kwa wananchi. Baada ya muda huo kumalizika Wizara imeongeza miezi mitatu kukamilisha agizo hilo. Wataalam wa Wizara kwa sasa wanatembelea vituo katika Halmashauri nchi nzima kufanya tathmini kubaini waliotekeleza na ambao hawajatekeleza, ili hatua za kinidhamu zifuate mkondo wake.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imepata ufadhili wa shilingi bilioni 66 kutoka Benki ya Dunia na imeshirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kubainisha vituo 100 vitakavyoboreshwa, ili kutoa huduma za dharura za upasuaji wa kutoa mtoto tumboni. Taya ri fedha za utekelzaji zimeanza kupelekwa katika Halmashauri mbalimbali husika hapa nchini.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Kila mwaka Tanzania inaagiza tani laki nne za mafuta ya kula wakati tuna malighafi za kutosha kama vile alizeti, ufuta na kadhalika kwa ajili ya kuzalisha mafuta hayo.
Je, Serikali haioni haja ya kuchukua hatua za makusudi za kutumia malighafi hizo ipasavyo na kuokoa fedha za kigeni zinazopotea nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Khadija kuwa nchi yetu imebarikiwa kuwa na mazao ya aina nyingi ambayo ni vyanzo vya mafuta ya kula. Ni kweli kuwa kama Taifa, Tanzania tunaagiza zaidi ya tani laki nne za mafuta hali inayotugharimu fedha nyingi za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua fursa ya kuwa na malighafi pamoja na soko la bidhaa zitokanazo na mazao hayo. Katika uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda, tuna mkakati wa uhamasishaji wa kilimo na ujenzi wa viwanda vinavyosindika alizeti ili kupata mafuta ya kula. Mkakati wa pamba mpaka mavazi utekelezaji wake utatuwezesha kupata mafuta ya kula yatokanayo na mbegu za pamba. Pia kupitia Shirika la NDC, mradi wa mfano unaandaliwa Mkoani Pwani ambako shamba la mchikichi litaanzishwa tukilenga kuzalisha tani 60,000 za mafuta ghafi ya mawese kila mwaka. Ni maoni yetu kuwa sekta binafsi itaazima uzoefu wa Mkoa wa Pwani na kuanzisha mashamba kama hayo katika mikoa ya Mbeya, Kigoma na Kagera kwa kutaja tu baadhi ya maeneo yanayostawisha michikichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuomba Mikoa, Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinapohamasisha suala la ujenzi wa viwanda sekta ya mafuta ya kula pia ipewe kipaumbele. Vilevile wananchi wahimizwe kuongeza uzalishaji wa malighafi kama alizeti, mawese na pamba kadri zinavyopatikana kwenye maeneo yao.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Tanzania ina idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Je, Serikali inajua idadi kamili ya watu wenye ulemavu na aina ya ulemavu waliokuwa nao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa viti maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2012 inaeleza kuwa, ulemavu ni hali inayotokana na dosari ya kimwili au ya kiakili ambayo inampunguzia mtu uwezo na fursa sawa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii. Upungufu huo unaweza kuchochewa na mazingira na mtazamo wa jamii kuhusu ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aina mbalimbali za ulemavu ambao umegawanyika katika makundi yafuatayo:-
Ulemavu wa viungo, wasioona, viziwi, wasioona, ulemavu wa akili, wenye ualbino, ulemavu wa vichwa vikubwa na mgongo wazi, ulemavu wa matatizo ya afya ya akili, yaani walioupata ukubwani bada ya kuugua kwa muda mrefu pamoja na ulemavu wa ngozi yaani walioathirika na mabaka mabaka ya ngozi mwilini. Sababu za kiujumla ni pamoja na ukosefu wa chakula bora au lishe duni, magonjwa kama malaria, uti wa mgono na surua, ajali mbalimbali, urithi na hali ya mama yaani umri na hali ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maelezo hayo, naomba kujibu sasa swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na wingi huo wa aina za ulemavu, Sense ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 imejumuisha vipengele mahususi kwa ajili ya kupata taarifa zinazohusu watu wenye ulemavu hivyo Tanzania inakadiriwa kuwa na takribani watu 44,928,923 ambao sasa kwa hapo mgawanyo wake uko kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye ualbino ni 16,477,000 ambayo ni sawa na asilimia 0.04, wasiiona ni 848,530 sawa na asilimia 1.19, ulemavu wa uziwi ni 425,322 sawa na asilimia 0.97, viungo ni 525,019 sawa na asilimia 1.9, ulemavu wa kumbukumbu ni 401,931 ambayo ni sawa na asilimia 0.9, ulemavu wa kushindwa kujihudumia ni 324,725 sawa na asilimia 0.74, na ulemavu mwingine yaani kwa ujumla wake ni 99,798 ambao ni sawa na asilimia 0.23.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Miongoni mwa matakwa ya Serikali ni kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi. Je, Serikali inatekelezaje suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na kutungwa kwa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 pamoja na sheria mbalimbali zinazohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi, Serikali inatekeleza Mpango wa Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi kama ifuatavyo:-
Moja, ni kutambua umuhimu wa mafunzo ili kuwawezesha wanawake na vijana kukuza shughuli zao za kiuchumi na kujikwamua kimaisha.
Pili, ni kuhamasisha vijana na wanawake kujiunga na vikundi vya kiuchumi vya Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ili kujipatia kwa urahisi mitaji ya kuanzisha na kuendelez amiradi ya kibiashara.
Tatu, ni kuwekeza katika Sekta ya Ufundi stadi ili vijana wanaohitimu waweze kuwa na ujuzi wa kuweza kujiajiri.
Nne, kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ni chanzo cha ajira kwa wanawake na vijana.
Tano, ni kuanzisha Benki ya Wanawake kwa lengo la kutoa mikopo kwa wajasiriamali wanawake na pia uwepo wa mifuko maalum ya uwezeshaji wa akina mama (WDF) na vijana (YDF).
MHE. ASHA ABDALLAH JUMA (K.n.y. MHE. KHADIJA NASSIR ALI) aliuliza:-
Sera yetu ya Elimu inatueleza kuwa elimu ya msingi ni hadi kidato cha nne.
Je, ni lini Serikali itaboresha kiwango hiki cha elimu ya msingi hadi kufika ngazi ya Ufundi Stadi yaani VETA?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa elimu wa Tanzania unasimamiwa na Sheria ya Elimu Na.25 ya mwaka 1978. Sheria hii inabainisha wazi kuwa elimu ya msingi ni miaka saba kuanzia Darasa la Kwanza hadi Darasa la Saba. Hivyo, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, elimu ya msingi inatolewa kwa muda wa miaka saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa elimu ya msingi kwa miaka saba bila kuunganisha na mafunzo ya ufundi stadi. Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kwamba maudhui yaliyopo kwenye mtaala wa elimu ya msingi bado yanakidhi mahitaji ya sasa ya wahitimu wa ngazi hiyo ya elimu ya msingi lakini pia muda ambao wanafunzi wa elimu ya msingi wanakaa shuleni hauwezi kutosha kuunganisha na mafunzo ya ufundi stadi. Hivyo, mafunzo ya ufundi stadi yataendelea kutolewa na Mamlaka ya Ufundi Stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza nafasi za udahili katika Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi. Juhudi hizi ni pamoja na kujenga Vyuo vipya vya Ufundi Stadi na vilevile kufanya ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ili viwe na mazingira fanisi ya kujifunzia na viweze kutoa mafunzo katika fani mablimbali.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-

Serikali imekuwa ikijitahidi kuvisimamia na kuviwezesha viwanda vyetu vya ndani lakini cha kusikitisha ni kwamba Serikali imeshindwa kusimamia bidhaa zetu ndani ya soko hili huria. Mathalani, bidhaa za viuadudu zinazozalishwa na kiwanda kilichopo Kibaha hazipo sokoni na wananchi hawana uelewa nazo:-

Je, Serikali haioni kwamba kuendelea kuweka fedha kwenye viwanda vyetu bila ya kuwa na mikakati mizuri ya kibiashara ni kuendelea kutumia vibaya fedha za walipa kodi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya uwekezaji wowote kufanywa na Serikali, mara zote utafiti na upembuzi yakinifu hufanyika ili kujiridhisha na manufaa ya uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu waenezao ugonjwa wa malaria kilichopo TAMCO-Kibaha kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia Shirika la Taifa la Maendeleeo (NDC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi mbalimbali zimefanyika katika kutoa elimu kwa wananchi na makampuni ya ndani na nje ya nchi juu ya matumizi ya viuadudu vinavyozalishwa. Uhamasishaji umekuwa ukifanyika kupitia miongozo na jinsi ya kutokomeza viluwiluwi wa mbu waenezao malaria, mikutano, makongamano na hata vipindi vya runinga. Uhamasihaji ulianza mwaka 2015 na kufikia 2018 mwishoni, Halmashauri za Mikoa yote 26 za Tanzania Bara zilikuwa zimenunua viuadudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamasishaji umefanyika pia katika nchi za jirani na Jumuiya za Nchi za SADC ambapo katika kikao cha SADC cha Agosti, 2018 nchi hizo ziliazimia kiwanda cha viuadudu kitakuwa msambazaji pekee wa viaududu kwa nchi hizo. Aidha, ili kuwezesha kaya moja moja kutumia viuadudu, kiwanda kimetengeneza vifungashio vidogo vya ujazo wa milimita 30 ambazo bei yake ni Sh.1,000 na vinapatikana kwenye maduka mengi ya dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya uhamasishaji huo ni kuwa jumla ya lita 466,278 za viuadudu zimeshauzwa ambapo lita 269,900 ziliuzwa katika soko la ndani na lita 196,378 ziliuzwa nje ya nchi katika nchi za Niger na Angola. Nchi ya Angola imeonesha nia ya kununua viuadudu vingine lita 85,192 ifikapo mwezi Februali, 2019. Aidha, nchi za Siri Lanka, Serbia, Msumbiji, Rwanda, Kenya na Burundi zimeonesha nia ya kununua viuadudu hivyo na mazungumzo na ufuatiliaji yanaendelea.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. KHADIJA NASSIR ALI) aliuliza:-

Kwa kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na zoezi la kununua ndege:-

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuhakikisha kuwa ndege hizo zinakwenda kila mkoa wenye kiwanja cha ndege pamoja na nchi jirani ili kusaidia kushusha gharama za usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania (Air Tanzania Company Limited) inakuwa na ndege za kutosha ili kuweza kutoa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi kwa ufanisi na tija. Uwepo wa ndege mpya na za kutosha kutaiwezesha ATCL kuweza kuhimili ushindani katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upanuzi wa mtandao wa huduma za usafiri wa anga katika kila mkoa wenye kiwanja cha ndege na nchi jirani, unatekelezwa kwa kufuata Mpango Mkakati (Corporate Strategic Plan) wa ATCL wa miaka mitano unaoishia mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na Mpango wa Biashara unaoandaliwa kila mwaka. Hadi sasa, ATCL inasafirisha abiria katika mikoa tisa (9) na katika nchi tano (5) kama ifuatayo: Kwa Tanzania tunasafirisha Mkoa wa Dodoma, Mwanza, Bukoba, Kigoma, Mbeya, Kilimanjaro, Zanzibar, Tabora na Mtwara. Pia ATCL inatoa huduma za usafiri wa anga kwa safari za Kikanda kama ifuatavyo: Hahaya (Comoro), Harare (Zimbabwe), Bujumbura (Burundi), Entebe (Uganda) na Lusaka (Zambia). Hivyo, huduma za usafiri wa anga katika kila mkoa wenye kiwanja cha ndege na nchi jirani unatekelezwa kwa kufuata mpango wa upanuzi wa mtandao wa safari za ATCL pamoja na uwepo wa abiria wa kutosha ili kuifanya kampuni yetu ijiendeshe kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ATCL inatarajia kupokea ndege mbili mpya, Bombadier moja na Boeing moja mwishoni mwa mwaka huu, matarajio yetu ni kuwa ATCL itakuwa na uwezo wa kuongeza mtandao wa safari katika mikoa mingine pamoja na safari za kikanda na kimataifa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. KHADIJA NASSIR ALI) aliuliza:-

Uzito mkubwa wa mwili ni dalili za mwanzo za magonjwa yasiyoambukiza:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na magonjwa haya?

(b) Je, mbali na mazoezi ni mbinu gani nyingine za kitaalamu za kupambana na vitambi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mnamo mwaka 2011 ilianzisha rasmi kitengo cha kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa lengo maalum la kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha tumetengeneza mpango mkakati wa kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza wa mwaka 2016-2020, ambao umewekwa malengo bayana, mikakati na utekelezaji wake ili kupambana na ongezeko la magonjwa haya. Mikakati inayotekelezwa katika mkakati huu ni pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu magonjwa haya na kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo vipeperushi, redio, runinga, mitandao ya kijamii, na nyinginezo ili kuongeza uelewa kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupunguza viashiria vya hatari ambavyo vinaweza kurekebishika kwa kuhamasisha juu ya ufanyaji wa mazoezi, ulaji unaofaa, kuhamasisha kuacha matumizi ya tumbaku na pia kupunguza unywaji wa pombe kupita kiasi. Kuhakikisha huduma za uchunguzi wa awali, yaani screening for early detection, kwa magonjwa haya zinapatikana katika vituo vya afya pamoja na fanya kambi za wazi za kupima na kutibu magonjwa haya. Kutoa chanjo kwa magonjwa yanayoweza kukingwa kwa njia hii mfano, chanjo ya HPV kwa ajili ya kujikinga na saratani ya shingo ya uzazi.

Mheshimiwa Spika, ikitokea kwa bahati mbaya, ugonjwa umegundulika katika hatua za mwisho, pia eneo hili halijasahaulika. Wizara ina mkakati ambao unashughulikia uimarishaji wa huduma za tiba shufaa yaani palliative care na pia huduma ya tiba ya utengamao yaani rehabilitation services. Upo pia mkakati unaoangalia maeneo ya tafiti ili kuimarisha suala zima la upatikanaji wa takwimu sahihi za magonjwa haya.

Mheshimiwa Spika, kitambi ni dalili mojawapo ya uzito uliopita kiasi, hii si dalili njema na hupelekea magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Njia bora ya kupambana na kitambi ni kujikinga kwa kutokukipata kwa kuhakikisha unazingatia ulaji wa vyakula unaofaa na kufanya mazoezi. Iwapo mtu akiwa ameshakipata kitambi, basi njia mojawapo ya kuondokana nacho ni kuzingatia ulaji unaofaa kwa kupunguza kiwango cha vyakula vya wanga, kupunguza kiwango cha sukari, chumvi na mafuta kwenye chakula. Kunywa maji yasiyopungua lita moja na nusu kwa siku kwa mtu mzima na kupunguza unjwaji wa pombe uliopitiliza. (Makofi)