Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Mary Michael Nagu (33 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na ni mara yangu ya kwanza kuongea kutoka back bench. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutoa mchango wangu ndani ya Bunge hili na naahidi kushirikiana na wengi ili tuweze kutoa mchango wa Bunge kama unavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Wilaya na Jimbo la Hanang walionipa kura nyingi kurudi hapa Bungeni. Kulikuwa na changamoto na hujuma nyingi lakini hawakutetereka. Naomba waendelee kusimama na msimamo huu wa kujenga Wilaya yetu. Wale wabinafsi wakae kule wenyewe na sisi tuendelee kuliendeleza Jimbo letu la Hanang. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda sana kuwashukuru wananchi wa Hanang kwa kumpa Rais John Pombe Joseph Magufuli kura nyingi na CCM ikapita. Nashukuru sana na nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amedhihirisha kutoka CCM wananchi wa Tanzania wanaweza wakapata mabadiliko ya kweli na ya uhakika. Kwa sababu wengi walifikiri mabadiliko yanaletwa na vyama vya upinzani lakini Mheshimiwa Rais ameonesha kwamba mabadiliko yaliyo dhahiri na ya uhakika yataanzia kutokana na Mpango huu wa pili na wa kwanza wa miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye Mpango ambao uko mbele yetu. Msingi wa Mpango huu ni ujenzi wa uchumi wa viwanda. Ujenzi wa uchumi wa viwanda utaleta maendeleo ya watu na si maendeleo ya vitu kama utaunganishwa na maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi, shughuli ambazo zinahusu Watanzania walio wengi. Mimi kama Mbunge wa Hanang nashukuru sana kwa sababu Wilaya yangu kwa kiasi kikubwa ni ya mifugo, ni ya ukulima na kutokana na Ziwa Basotu kuna wavuvi vilevile. Kwa hiyo, viwanda vikijielekeza kwenye kuendeleza tija ya kilimo maendeleo ya watu yatapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutambue kwamba kilimo kimekuwa ni shughuli ya watu wengi lakini na inaonesha kwamba maendeleo ya kilimo yanasuasua. Jambo moja ambalo ni dhahiri ni kwamba lazima tuunganishe mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo jambo ambalo liliharibika wakati wa ukoloni lakini hatujawahi kulirudisha mpaka leo. Viwanda hivi vitasaidia kwa sababu kwanza kutokana na viwanda teknolojia inayotakiwa kwenye kilimo itapatikana, zana bora zinazotakiwa kwenye kilimo na mifugo zitapatikana pia. Badala ya kuuza mazao yetu nje bila ya kuongeza thamani viwanda hivi vitasaidia kuunganisha mnyororo ule. Kwa hiyo, naomba sana viwanda ambavyo tutavianzisha viwe na uhusiano wa karibu sana na kilimo, mifugo na uvuvi bila ya kusahau utekelezaji wa Liganga na Mchuchuma ambavyo ni viwanda mama vitakavyojenga viwanda vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai, maji ni maendeleo na maji ni siasa. Ukiangalia katika kampeni ambazo tumezimaliza juzi wananchi wa Tanzania walio wengi walikuwa wanadai maji. Maji ni kazi ya akina mama ambapo wanaacha watoto nyumbani wanaanguka au wanaungua na moto kwa sababu ya kutafuta maji kwa umbali mrefu. Bila maji itakuwa ni vigumu sana viwanda kuendelezwa. Kwa hiyo, naomba sana, kabla sijafika kwenye maji, kuna misingi ambayo tunapaswa kuitekeleza katika Mpango huu. Kwa mujibu wa makubaliano hata ya kimataifa, sekta ya kilimo inapaswa kupewa si chini ya asilimia kumi ya bajeti kila mwaka ndipo ambapo tutaona maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango huu, mkiunganisha na maji, suala la kujenga mabwawa ya kumwagilia ambayo yatatoa maji kwa mifugo na kusaidia maji hata kwa wananchi litakuwa ni suala muhimu. Maji ni muhimu kwa ajili ya uhai lakini yatasaidia vilevile kuongeza tija kwenye kilimo. Kwa hiyo, naomba suala la mabwawa tulitilie mkazo katika Mpango huu na mimi narudia kusema tena kuhusu suala la Wilaya ya Hanang ya kuomba maji ya Mlima Hanang yakusanywe kwenye Bwawa la Gidahababieg ili watu waweze kupata maji ya uhakika, ili watu waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji na ili mifugo mingi ya Hanang nayo iweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka kwenye wilaya ya wafugaji, watu wanaohamahama. Naomba nikazie elimu kwani ndiyo itakayobadilisha mindset ya wafugaji wanaohamahama. Ili tuweze kuhakikisha watoto wa wafugaji wanapata elimu ya uhakika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu na wale wote wanaohusika na TAMISEMI waone suala la mabweni na hosteli kwenye Wilaya za wafugaji linatiliwa mkazo kwa sababu hawataacha kuhama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele ya kwanza imelia, naomba niseme kwamba jamani nzi anakwenda pale ambapo kuna mzoga haendi kwenye marashi. Kwa hiyo, tukitaka mambo ya polisi na FFU kutokuingia humu ndani, naomba Wabunge tuwe waungwana wakati tunatoa michango yetu. Humu ndani sisi ni Wabunge, sisi ndiyo dira ya wananchi, ni wawakilishi wa wananchi, tukileta fujo humu ndani, tunaashiria kwamba kule nje napo wafanye fujo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana tuwe watulivu, tuwe waungwana, tuheshimiane humu ndani na tuliweke Taifa letu mbele ili tuongee mambo yanayohusu maendeleo ya watu wa Tanzania badala ya kuongelea mambo ambayo kila mmoja anataka ajiinue ili aonekane. Tukiwa waungwana, tukitumia muda wetu vizuri, wananchi wa Tanzania watatuona zaidi kuliko tunavyopiga kelele humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ni mdogo, naomba niishie hapa na mimi nitasaidiana na Waziri wa Mipango kwa sababu nilikuwa naye kabla nikiwa Waziri wa Mipango …
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Katika kuleta mambo ambayo yatasaidia Mpango huu. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DKT. MARY M. NAGU – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kufanya majumuisho ya hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili taarifa ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Namshukuru Makamu Mwenyekiti kwa kuwasilisha taarifa vizuri asubuhi na nawashukuru Wajumbe kwa maandalizi mazuri ya taarifa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa kutoa ufafanuzi kwa hoja mbalimbali ambazo zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia kwa maandishi na kwa kuzungumza. Wingi wao umeonesha jinsi sekta hii ilivyo muhimu na nyeti sana kwa wananchi na kwa maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge 60 wamechangia ambapo 25 walichangia kwa maandishi na 35 walichangia kwa kuzungumza. Kwa muda ulionipa, naomba nisipitie orodha hiyo lakini nimeihifadhi na Waheshimiwa wanaweza kuja kuona ili waone kwamba mchango wa kila mmoja umechukuliwa na unafanyiwa kazi kuboresha taarifa ya sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuhitimisha hoja za Kamati kama ifuatavyo. Kwanza, nikiri kwamba hoja zile zilizotolewa kwa kweli zimeboresha taarifa yetu. Kuna Wabunge wawili walioleta ammendments ambazo tutaziongeza na nitapenda kusema ni kwa namna gani tutaziongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zote zilijadiliwa lakini naomba niongelee hoja chache tu kwa sababu ya muda na ninyi wote mnajua muda huu ni mfupi sana. Nitajitahidi kama muda utaniruhusu nitakwenda kwenye hoja kadri ambavyo zitakuja kwenye taarifa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mgogoro wa wakulima na wafugaji. Mimi nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kwamba si jambo dogo, ni kubwa. Wananchi wa Tanzania walio wengi ni wakulima na wafugaji na kama wao hawatakuwa wanapatana, ni migogoro kila wakati mfahamu ya kwamba na wao wenyewe wataathirika lakini maendeleo ya nchi yatakuwa yameathirika kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi inatokana na ardhi. Suala la mgogoro wa ardhi linahusisha wakulima na wafugaji kwa kiasi kikubwa. Nataka niseme kwamba kuna mgogoro wa wakulima au wafugaji na hifadhi, kuna mgogoro wa wakulima na wafugaji na wawekezaji, hakuna namna nyingine ya kumaliza migogoro hii bila ya Serikali kutekeleza kwa vitendo mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kupima na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo, uhifadhi na shughuli nyingine za binadamu kama Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 inavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mchengerwa ameleta hoja hapa, yeye ametaka tuondoe hoja ya Kamati. Mimi naomba hoja ya Kamati ibaki kwamba Bunge liazimie Serikali iongeze kasi ya kutekeleza kwa vitendo mpango wa matumizi bora ya ardhi kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 na Bunge linaazimia kwamba mgogoro wa wakulima na wafugaji sasa ushughulikiwe katika ngazi ya Kitaifa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini kwa kuwashirikisha wadau wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nataka kusema kwamba Watanzania ni vizuri sana wafahamu kwamba ardhi ni mali ya asili na mali ya asili ambayo inatupa sisi maisha. Mifugo ni mali ya mtu mmoja-mmoja, lakini hata hivyo mifugo ni mali ya asili ya Taifa vilevile. Ni kweli kwamba kuna maeneo ambayo hayana utamaduni wa kuwa na mifugo, lakini kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, Watanzania wana uhuru wa kwenda kila mahali lakini kwa utaratibu uliowekwa. Na mimi naona suala hili ambalo linawapa taabu hasa Mikoa ya Kusini na ile ambayo haikuwa na utamaduni wa mifugo, Serikali na wadau wanaohusika tujaribu kuangalia matumizi bora ya ardhi yanatekelezwa na sio kusema kwa mdomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi ndugu zangu kwa sababu Ethiopia ina ng’ombe milioni 55, Sudan ina milioni 38, sisi tuna milioni 25.8, tuna ng’ombe wachache kuliko wenzetu na ukiangalia nchi zile zina jangwa kuliko hata Tanzania. Kwa hiyo, jambo kubwa ni kwamba sisi hatujajipanga na tukijipanga tutaondoa migogoro hii, wakulima walime kwa amani na wafugaji wafuge kwa amani kwa manufaa ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilisemee hapa ni kuhusu ruzuku ya pembejeo. Ndugu zangu kama tunataka tuwe na tija kwenye kilimo suala la pembejeo halina mjadala. Kwa kweli, Wabunge waliochangia hoja hii wameeleza jinsi pembejeo za kilimo zisivyowafikia wakulima kwa wakati na hivyo kukwamisha shughuli za kilimo. Wamependekeza pembejeo za kilimo ziuzwe madukani ili kuwapa wakulima fursa ya kununua pembejeo wakati wowote wanapohitaji na tozo yoyote iondolewe kwenye pembejeo ili waweze kumudu bei ya kununua na hivyo kuhakikisha kwamba tija ya kilimo inakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye pembejeo kuna suala la mawakala, naomba mmalize uhakiki Mheshimiwa Waziri. Hatuwezi kuendelea na uhakiki kwa mwaka mzima. Tukishahakiki tuwalipe mawakala wale ambao wanastahili kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni vyanzo vya mapato kwa Mfuko wa Taifa wa Maji. Waheshimiwa Wabunge wengi wamekubaliana na mapendekezo ya Kamati, lakini hapa Mheshimiwa Zitto alileta mabadiliko kidogo. Sisi tunacholilia ni kwamba Mfuko wa Maji uliopo hautoshelezi mahitaji na hasa ukizingatia kwamba mwaka huu fedha nyingi zilizoenda kwenye Wilaya zetu ni zile zinazotokana na mfuko na hela ya bajeti iliyotolewa ni kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wabunge wengi kwanza wameitaka Serikali itoe fedha hizo kwa sababu suala la maji kama alivyosema Mheshimiwa Waziri ni uhai, ni uchumi na bila maji hakuna viwanda, hakuna uhai na hakuna kuishi kule nyumbani. Kwa kweli wanaoteseka ni akina mama na ambapo wanapotumia muda mrefu kutafuta maji watoto wanaanguka au wanaungua kwa moto na gharama za afya na usalama wa watoto unakuwa hatarini. Kwa hiyo, naiomba Serikali ilione hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndugu zangu naomba Kauli Mbiu hii ya maji tuipokee. Pia kama alivyoleta mapendekezo Mheshimiwa Zitto, niwaombe wataalam waliangalie na wakati wa bajeti tuli-effect. Kwa hiyo, tumepokea mpendekezo yake, lakini inatakiwa kufanyiwa kazi na nina hakika itapita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji katika kukabiliana na ukame na mabadiliko ya tabianchi. Waheshimiwa Wabunge sisi na Watanzania wote ni mashahidi kuhusu ukame wa mwaka huu ulivyoleta frustration, umeleta hofu na ndiyo maana bei ya vyakula mbalimbali imepanda. Najua kuna Wilaya ambazo zina chakula, kuna Wilaya ambazo hazina chakula na zimesemwa kwamba ni 55, lakini hata wale wenye chakula kidogo kutokana na hofu iliyoletwa na ukame huu, bei ya chakula imepanda na kwa kawaida itachangia kwenye mfumuko wa bei.
Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na wengine wote wanaohusika kwa kweli tutafute na tusambaze chakula ili tu-stabilise bei ya chakula na kuondoa hofu ya watu na watu waishi kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili miaka ijayo tuweze kuondokana na hofu hii ya ukame, hatuna njia nyingine, Kamati inasisitiza umuhimu wa Tume ya Umwagiliaji kutegewa fedha za kutosha na kupelekewa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa wakati ili iweze kutekeleza vyema miradi inayohusu kilimo cha umwagiliaji. Tunachoona ni kwamba Tume haijapelekewa fedha yoyote, tunamuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji afuatilie kwa Waziri wa Fedha. Kilimo cha umwagiliaji kitasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa chakula na njaa na itaifanya nchi hii iishi kwa amani zaidi kuliko kama tunakuwa na hofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ambayo ningeweza kusema ila nawaaomba sana Waheshimiwa Wabunge mapendekezo yaliyomo kwenye Maazimio ambayo Kamati imeyaandaa ambayo yamechukua mambo yote muhimu muyaunge mkono. Vilevile kama walivyosema Wenyeviti walionitangulia tutafute namna ya kuona kwamba Serikali inafanyia kazi Maazimio haya. Inaonesha kwamba taarifa za Kamati zimeleta manufaa makubwa sana na utaona kwamba Wabunge wengi wamebakia hapa na Mawaziri wamechukua muda wao kutoa ufafanuzi, lakini haitakuwa na manufaa kama kweli maazimio haya hayatafanyiwa kazi na Serikali na wale wote wanaohusika na tukiyafanyia kazi kila mwaka, ndivyo tutakavyopiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo niliyoyasema, narudia tena kutoa hoja kwamba muunge mkono Maazimio ya Kamati hii ya Kilimo, Mifugo na Maji na ahsanteni sana kwa usikivu wenu.
MWENYEKITI: Toa hoja.
MHE. DKT. MARY M. NAGU – MWENYEKITI WA WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa hoja lakini naomba nirudie. Natoa hoja tupitishe Mapendekezo na Maazimio ya Kamati ya Bunge.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupa shukurani kwa kunipa fursa hii na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge kuwapongeza Mawaziri walioteuliwa na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwateua watu ambao nafikiri wataongeza kasi yake ya kuendesha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi ni siasa na siasa ni uchumi na uchumi ambao unategemewa ni ule ambao una mipango mizuri au mpango mzuri. Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana na mimi kwamba mpango wa miaka mitano ambao unatekelezwa kila mwaka ni mpango mzuri ambao tumeupitisha na kilichobaki sasa ni utekelezaji. Kwa hiyo, mpango ni mzuri na aliyeuandaa ni Mpango huyu Mheshimiwa Waziri, na ninajua alivyohangaika na kuja na mpango huu mzuri kwa kweli kwa hilo nampongeza. Na azma ya Taifa kupitia mpango wa miaka mitano unaotekelezwa klia mwaka kwa vyovyote vile ni kufikia dira ya 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango watu wengi wanakutegemea na nina hakika umefanya hivyo kuona kwamba dira yetu ya 2025 inataka nini na kuona mipango hii kila mwaka kama inatupeleka kule. Na mpango huu unatekelezwa kupitia bajeti ya klia mwaka na azma yetu ni kuwa na uchumi wa kati na wa viwanda, sasa katika mipango hii kuna vipaumbele vilishaonyeshwa na ni kiasi gani cha uchumi kitakuwa ambacho kinatufikisha kule ambako tulitegemea kwenda. Kama tunaenda kwa mpango wetu uchumi wa mwaka huu ungekuwa unakuwa kwa 8% mpaka 10% kufidia kule ambako nyuma tulikuwa hatujafikia kule tunakotakiwa na inawezekana kwa sababu miaka iliyopita tulishafika 8% na zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ilivyobaki sasa ni kuangalia kwanini sasa uchumi unakuwa kwa 6.8% ambayo ametuletea sisi ambayo sio 8%, na kazi yetu Waheshimiwa Wabunge ni kuonyesha mapungufu yako wapi na kuishauri Serikali ifanye nini kusudi tusonge mbele na mimi nitatumia muda wangu zaidi katika kuonyesha tufanye nini ili tupige hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaotekeleza mpango huu sio Serikali peke yake, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla tunapaswa kutekeleza mpango huu. Tutakachouliza kwa Serikali na ninachoomba kwa Serikali ni kuiwezesha sekta binafsi na wananchi kusaidiana na Serikali kutekeleza mpango huu utufikishe mbele na kwa upande wa Serikali unachangia kupitia bajeti ya Serikali, kwa hiyo, tuseme kwa kiingereza tuwe na consistency ya kukusanya mapato bila kuua uchumi. Mimi ndio ushauri wangu kama VAT inapunguza production angalieni! Kama VAT inapunguza ajira angalieni! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwaambie hakuna shamba linalovunwa bila ya kupanda, hakuna uchumi utakaokuwa bila investment au uwekezaji haiwezekani. Kwa hiyo, tuangalie kama uwekezaji unakwenda kwa principal ambayo tunataka uchumi wetu ukue. Kuna jambo ambalo siku zote nimelishauri na hata mimi mwenyewe nimejitahidi ni kuweka One Stop Center kwa ajili ya investors ili wasihangaike hangaike na kupoteza muda. Muda ukishakwenda haurudi ndugu zangu.

La pili ni kwamba, pale sasa hivi huu uchumi unaokuwa kwa 6.8 unatokana na sectors ambazo sio za watu wengi, wamesema wengine. Kwa hiyo, ndugu zangu tuangalie ni sekta zipi na bila mjadala na wengi wamesema kwamba sekta ambayo itaifanya viwanda vifanye kazi nchi hii ili vipate malighafi na chakula kwa wafanyakazi ni sekta ya kilimo, Mheshimiwa Mpango angalia bajeti ya mwaka juzi na mwaka jana kama tunaongeza bajeti ya kilimo bila ya kutafuta visababu sababu. Bila ya kilimo kama walivyosema wengine ndugu zangu hatuwezi kwenda popote kwa sababu malighafi itatokana na kilimo lakini kilimo ndicho kinachoajiri watu wengi nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo, hata wafanyakazi wa viwandani baadaye watapata chakula chao wapi? Ni kutokana na kilimo. Lakini sio hivyo, leo utaona ajabu, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambayo Mheshimiwa alitaja asubuhi kwamba unaona Songea na Kusini kule bei ya mahindi ni shilingi 25,000 kwa gunia lakini Serengeti na Maswa ni shilingi 80,000 mpaka 100,000 na zaidi. Kwa nini kuna tofauti hii? Lazima kuna tatizo na ndilo ambalo tunapaswa kuliangalia. Mimi siamini kama uchumi umerudi kwenye ujamaa, huu ni uchumi wa soko lakini Serikali lazima i-regulate, ione kwamba bei ya Kusini inapanda na ione kwamba bei ya chakula kule Kaskazini inashuka na tulimwambia Mheshimiwa Waziri kwa nguvu zote na nilitegemea ametekeleza kwamba hakikisha NFRA iweze kwenda kununua mahindi kule ili bei kidogo ipande na ipeleke kule ili bei kidogo ishuke kwa chakula. Lakini hatujui kama amefanya hiyo ripoti kama sekretarieti inaleta itakuwa imefika kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipaswa aeleze ame-act namna gani na hapo ndipo ambapo tunaleta matatizo, lakini kwa kilimo lazima kuwe na tija. Tija ya kilimo inatokana na pembejeo na zana, lakini ukiwa umelima sana hamna soko ni sawasawa na kutupa shilingi chooni. Lazima tuwe na masoko, lakini kazi ya masoko ya kilimo haiko kwenye Wizara ya Kilimo, iko kwenye Wizara ya Viwanda na hatujawahi kusikia viwanda ikiongelea masoko ya mazao ya kilimo hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo, namna ambavyo Wizara ya Viwanda inaweza kutengeneza masoko ya mazao ya kilimo ni kuanzisha viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo, hilo ndilo soko la uhakika. Kwa hiyo, tuangalie bajeti kama inafanya hivyo, kama hivyo vipaumbele tunaviweka kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba Mwenyezi Mungu ameijaalia Tanzania. Tuna rasilimali nyingi, tuna madini, tuna vito, tuna ardhi na tutakachoweza kufanya nchi hii iendelee ni kuongeza thamani ya rasilimali hizi. Sasa wamesema kwamba kuna mfumko wa bei, kuna mfumko wa bei nzuri na mfumuko wa bei mbaya. Kama mfumko wa bei unatokana na credit squeeze au kuondoa money kwenye circulation hiyo sio nzuri sana. Mfumko wa bei unapaswa kupungua kwa kuongeza uzalishaji na chakula nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tu-manage hayo mambo, tunataka au hatutaki lazima tuya-manage. Sasa sio mfumko wa bei tu kuwa chini ndiyo sifa, umetokana na nini? Tujue kwa nini hakuna hela kwenye circulation, na kama hakuna hela namna ya kuwekeza ndani ya nchi ni kutokana na mikopo au equity. Hamna namna nyingine, kutokana na hela yako mwenyewe au kutokana na mikopo. Angalieni wenye hela kama wanawekeza, angalieni mabenki kama yanatoa mikopo kwa ajili ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani nilivyokuwa viwandani nilikuwa kwenye bodi ya benki moja. Ilikuwa inatoa hela kidogo sana kwenye kilimo na ilikuwa inatoa hela kwenye biashara nyingi. Kwa hiyo zile hela zikawa zinakwenda kuzungusha vitu ambavyo havitokani na production ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuangalie hayo mambo na mimi mwenyewe na Mheshimiwa Mpango kama unataka tunaweza tukakaa pamoja, tukaangalia hayo mambo tutayafanyaje? Na fahari yangu ni wewe ufanye vizuri na kufanya kwako vizuri ni kufanikisha uchumi wa nchi hii. Serikali imefanya makusudi kuweka uwekezaji na Wizara ya Fedha pamoja, sasa usiuzuie uwekezaji ukawa mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo tunapaswa kuwa na kipaumbele ni miundombinu kwa sababu bila miundombinu soko haliwezi kufikika na pembejeo haziwezi kufika kwenye kilimo. Lingine jamani ni kwamba tuone ajira kama inapungua nchi hii au inaongezeka, vijana ni wengi na nguvu kazi ni nyingi, kama ajira haiongezeki maovu yataongezeka ndani ya nchi yetu na hilo lita-affect uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nisisitize kwamba jamani One Stop Center iko kule Rwanda tukaiangalie, tuilete Tanzania na halafu tuweke ile Logistic Centre pale Kurasini ndipo tutaona demand kubwa ni ya nini halafu tunawekeza na mengine yote ambayo tunaweza kuyafanya ili uchumi wetu uweze kupiga hatua. Serikali ijaribu kuona kwamba private sector jamani inakuwa na confidence, Serikali iweze kuona kwamba private sector iwekeze na wakipata faida watoe kodi, bila kodi na wao hawawezi kuendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tuangalie upya kama sera inatekelezwa vizuri kwa sababu kuwa na sera nzuri si jambo la muhimu sana ni kuwa na sera ambayo inatekelezeka na inatekelezwa. Kwa kweli huu ni uchumi wa soko na private sector kama walivyosema wengine ndiyo engine na hiyo engine isipokuwa inafanyiwa maintenance kila wakati na kuangalia mahitaji yao itabaki Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja nataka nilisahihishe, mahali ambapo private sector haifiki, Serikali lazima iende. Kwa hiyo, kama shipping haiendi vizuri kwa kuwaachia private sector peke yake sioni ajabu kama Serikali inakwenda pale. Kwa hiyo, Serikali haiendi sana kwa ajili ya faida, Serikali inaenda kwa ajili ya mahitaji. Kama wananchi wanahitaji jambo na sekta binafsi haiendi lazima Serikali iende, kwa hiyo makampuni ya Serikali lazima yaendelee kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ndugu zangu tukosoe Serikali lakini tukosoe kwa namna ambayo tunaishauri na tunasaidiana nayo kufanya uchumi wa nchi hii kushamiri na nina hakika ni rahisi kutoka katika ukuaji wa uchumi wa asilimia 6.8 kwenda 8 mpaka 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilifanya thesis yangu ya kuondoa umaskini na kukuza uchumi. Wakati nilipofanya nafikiri ni mwaka 2002 au 2003, niliona kwamba kukua kwa uchumi kwa asilimia 11 ndiyo mahali ambapo tuna uhakika na kuondoa umaskini wa Tanzania. Inaweza kuwa chini, inaweza kuwa juu zaidi lakini asilimia 11 ndiyo ukuaji wa uchumi ambao utatuhakikishia Tanzania kupiga hatua mbele kiuchumi na kupunguza umaskini na kuongeza ajira na kuleta maisha mazuri kama dira yetu inavyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nzuri ya kuweza kuchangia bajeti ya Serikali itakayotekeleza mpango wa mwaka unaokuja, kwa sababu bila bajeti mpango ulioletwa mbele yetu utakuwa ni vigumu sana kutekelezwa. Naomba nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutoa maelekezo kila wakati ya kuimarisha uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mnyimi wa fadhila bila kutambua kazi nzuri ya Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango; Naibu Waziri, Dkt. Kijaji; Katibu Mkuu, wataalam wote wa Wizara ya Fedha kwa kuchukua ushauri na kuufanyia kazi na wote umeoneshwa kwenye bajeti hii ilivyokuwa nzuri. Ahsanteni sana na Mungu awaongezee afya na nguvu ya kuweza kutekeleza hayo yote ambayo mmeyaweka kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa kutekeleza yote ambayo yako kwenye bajeti kwa sababu kutekeleza hayo ndiyo yanayofanya maendeleo yawepo na matumizi ya fedha za Serikali ziende kwenye kuleta ustawi wa jamii. Ukiangalia mwaka uliopita, mwaka 2017/2018, utaona kwamba Wizara ilitengea kila sekta kiasi fulani cha fedha na mwenyewe Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba kwa miradi ya maendeleo ni asilimia 45 tu imetolewa katika fedha zilizotengwa. Kwa hivyo utekelezaji bila shaka utakuwa umeenda kwa asilimia hiyo.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia bajeti vile vile kwa matumizi ni asilimia 80 imetumika. Kwa kiasi hicho matumizi yameenda vizuri kwa sababu ukitaka kuonesha kwamba mpango uliowekwa ni mzuri unaweza tu ukapungua kwa asilima 15 au ukawa zaidi kwa asilimia 15, ikiwa zaidi ya hivyo ni kwamba mipango yetu haitaenda kama tulivyoweka. Kwa hivyo, kwa sababu Mheshimiwa Waziri mwenyewe ametambua hili nina hakika kwa mwaka 2018/2019, mambo yatakuwa tofauti na nategemea kwamba miradi ya maendeleo imetengewa tayari itatolewa hela zaidi na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi utaenda kama ulivyotengemewa na nitashukuru sana kuona hilo linatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, tuangalie fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi zinalipwa kwa nani, kwa sababu kama ma- contractor wanaotoka nje na hela ni za bajeti ya Serikali tukiwalipa kama hatuna masharti ya hela hizo kubakia ndani ya mabenki yetu, ni kwamba hela hizo zitakwenda kujenga uchumi wa watu wengine. Kwa hivyo nategemea ma- contractor watakaopewa kazi watakuwa ni hawa wa ndani ambao wakipata hela, fedha zao zitabakia ndani ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo ambayo pengine hatutapata contractor wa ndani; kwa mfano kwenye reli hii ambayo inatengenezwa watakuwa wametoka nje, lakini Mheshimwa Waziri wa Fedha aweke masharti fedha hizo zikae kwenye mabenki yetu kwa muda ili nazo zichangie katika ujenzi wa uchumi wetu, kwa sababu Serikali mpaka sasa ndiyo businessman mkubwa. Kama kweli mipango yake haitapangiliwa vizuri kufikia uchumi wa viwanda na kipato cha kati itakuwa ngumu sana kama hatutakuwa waangalifu sana. Ndiyo maana nasema tuone nani anapewa miradi mbalimbali ili fedha zinazotolewa za Serikali zizunguke ndani ya nchi.

Nilikuwa nasema tuwaangalie ma-contractor ambao tunawapa miradi yetu wawe ni wale ambao wataendelea kuangalia mzunguko wa fedha unabaki ndani ya nchi yetu na kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, sekta binafsi ina nafasi kubwa sana ya kuchangia uchumi wa nchi yetu na Mheshimiwa Waziri amelisema hilo kwenye hotuba yake; nampongeza na namshukuru kwa kutambua sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hili Serikali imeweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na naomba na ya kitaratibu iwekwe. Daima nimesema kuweni na one stop centre kwa ajili ya sekta binafsi kuwekeza kwa urahisi. Ukitaka kuijua hiyo iko Rwanda. Rwanda kuna Rwanda Development Center ambapo TBS sijui TFDA na kila mtu yuko kwenye ofisi moja anapoenda mwekezaji hachukui siku moja inachukua hata masaa ameshapata leseni na kibali cha kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hizo sheria na utaratibu pamoja na sera iweze kurahisisha uwekezaji wa sekta binafsi ambayo ni muhimu sana. Napongeza Serikali kwa hili lakini naomba ifanyike kwa matendo kuliko ilivyo kwenye hotuba. Jukumu la sekta binafsi ni kutumia mazingira haya ili kuwekeza; naomba mwone bajeti hii ni nzuri na hotuba ya Waziri ni nzuri na sekta binafsi iweze kuwekeza. Naomba sera na sheria ziwe zinatabirika (predictability) wawekezaji wanachotaka wajue wakiweza leo waliyoyaona leo yatakuwepo mwaka ujao na hasa ifikie miaka mitatu au zaidi ili wasiwe na wasiwasi, tuondoe wasiwasi huo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naipongeza Serikali, kwa mfano kuondoa VAT au kuondoa tozo na kodi mbalimbali kwenye pembejeo na kwenye zana za kilimo na Waziri mwenyewe kwenye hotuba yake amesema kilimo kimepewa kipaumbele; isiwe ni kwa kusema tu naomba tufanye kwa matendo, kama walivyoondoa tozo mbalimbali na kodi mbalimbali kwenye pembejeo na kwenye zana za kilimo zitasaidia sana wawekezaji kuwekeza kwenye kilimo. Hakuna investment inayohitaji fedha kama kilimo. Naomba watakapokuwa wamewekeza mazao yatakayopatikana yaweze kushindana na mazao katika nchi nyingine za East Africa au Afrika Mashariki na za SADC.

Mheshimiwa Spika, tulienda Iringa tukakuta wamezalisha chai nzuri na ina hadhi ya juu kweli kweli na ubora wa hali ya juu. Hata hivyo, ukienda sokoni Kenya inauza zaidi kuliko sisi kwa sababu ya vivutio vilivyowekwa. Naomba sana tunavyopeleka nje basi nasi tuangalie mazao yetu ya kilimo yanataka nini ili tuweze kushindana kwenye soko. Kwa hiyo, naomba sana Sera na Sheria ziwe na uhakika na ziwe zinatabirika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kushukuru sana kuona kwamba malighafi zinazokwenda kwenye viwanda hazitozwi kitu chochote, kwa sababu kwenye bidhaa za mwisho tunaweza tukatoza kodi ili tuwe na viwanda ambavyo vitachakata mazao ya kilimo na malighafi nyingine ambazo zinapatikana Tanzania. Siyo hivyo tu, viwanda hivi vitafanya watu walime zaidi kwa uhakika wa soko na kwa hivyo Watanzania wengi watapata ajira kwenye kilimo na viwanda.

Mheshimiwa Spika, naomba niungane na akinamama wenzangu kupongeza kuondoa tozo na kodi mbalimbali kwenye taulo za kike. Huko ni kudhamini uzazi kwa sababu chimbuko la uzazi ni hedhi. Kwa hivyo, taulo hizo zitakavyopunguzwa bei iende moja kwa moja kwa wanaotumia si kwa wale ambao watakuwa hapa katikati. Kwa hivyo, naomba Wizara ya Afya na Wizara ya Viwanda Biashara na Masoko; wataona kwamba taulo hizi zinawapa manufaa wale watakaozitumia na siyo wale watakaotengeneza na wale ambao watauza.

Mheshimiwa Spika, vile vile naomba niungane na wenzangu, tunasema Tanzania inatakiwa kuwa nchi ya viwanda na yenye kipato cha kati. Nami nataka niwaambie katika viwanda kuna viwanda mama au viwanda vya msingi, kuna viwanda vya Kati kwa ukubwa lakini vile vile kuna viwanda ambavyo vitatengeneza bidhaa zitakazotumika kwa kuliwa au kwa matumizi mengine. Naomba tuone viwanda vya msingi vinapewa kipaumbele; na Mheshimiwa Waziri amesema atatoa kipaumbele kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie, hakuna kitu ambacho hakitegemei chuma nchi hii. Huwezi kuwa na tairi bila chuma, huwezi kuwa na baiskeli bila chuma, huwezi kuwa na jembe bila chuma na tukiacha kuona umuhimu huo tutakuwa tunajenga uchumi wa wale wenye chuma kule nje na wa kwetu hauendelei kwa sababu tumeacha makusudi kutekeleza mradi wa Linganga na Mchuchuma.

T A A R I F A . . .

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Spika, Liganga na Mchuchuma iko maeneo ambayo hayajaendelea hata kidogo. Linganga na Mchuchuma zitakapotekelezwa watu watapata miradi na watapata kazi za kufanya. Mama ntilie watapika, vijana wataajiriwa na wakulima watalima kwa sababu watakaokuwa kule watakula. Kwa hiyo naomba sana, Mheshimiwa Waziri Bajeti ijayo au hapo katikati tutakapofanya review aseme Liganga imeanza kutekelezwa, tutamshukuru sana na tutamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mhehimiwa Spika, Kampuni ya General Tire tulifunga kwa sababu ilikuwa inasimamiwa na wawekezaji kutoka nje na walikuwa wanachukua hela zetu hatujui wanapeleka wapi na matairi yalikuwa hayatengenezwi. Serikali ikasimamisha, tukasema tutafute wawekezaji walipatikana, sasa tunajiuliza hiki ni kitu gani kiko hapa katikati? Hakuna tairi zinazotoka Arusha; tungefurahi kuona tairi zinatoka ili na sisi uchumi wetu uwe rahisi.

Mheshimiwa Spika, viwanda si kazi rahisi, viwanda vinataka taknolojia, utaalam, ufanisi na tija, viwanda ni soko la rasilimali ambazo zinatokana na maeneo yetu kama mazao ya kilimo, madini na mengine kama misitu; kwa hivyo tutakavyoanzisha viwanda mjue kwamba rasilimali zinazotoka Tanzania zitakuwa zinapewa thamani kubwa humu nchini badala ya kwenda hivi hivi.

Mheshimiwa Spika, tanzanite ikitengenezwa mikufu, pete, ikitengenezwa mambo mengine ya vito itakuwa na thamani kubwa zaidi Tanzania kuliko kwenda Jaipur au Marekani na South Afraica. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwenda kuweka kipaumbele kule Manyara ambako tanzanite inapatikana na kuweka ukuta ambao utahakikisha kwamba mnada utakapofanyika pale Wakenya watakuja pale badala ya Watanzania kupeleka tanzanite Kenya na badala ya Tanzania kupeleka tanzanite South Africa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini hii bajeti ilivyoandikwa ni nzuri sana. Hata hivyo, naomba sana mazao ya kilimo yasiwe na kodi mbalimbali jamani, yafike kwenye soko ili tuweze kushindana vizuri. Soko zuri na la uhakika ni viwanda vyetu; kama hakuna kodi viwanda hivyo vitatumia malighafi rahisi na bidhaa zitakazotokana na viwanda zitakuwa ni rahisi zitashindana na viwanda vya Kenya vya Malawi na South Africa.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo nakushukuru sana na naomba sana kwamba wananchi wa Hanang ni wakulima wa mbaazi iliyokosa soko; mahindi yakafungiwa mipaka watu wakawa maskini, lakini safari hii imefungua mipaka naomba tusaidiane kuona wakulima wanapata soko wa Kibaigwa, huko wa Hanang, Kiteto na maeneo yote hasa wale wa kusini wanaolima mahindi mengi sana na mahindi yana bei nzuri isipokuwa ni sera tu inakosesha wananchi kupata bei nzuri; naomba sana.

Mheshimiwa Spika, wananchi wengi Watanzania asilimia 80 wanalima, sera zikiwa nzuri na hasa za kodi zitasaidia sana wakulima kuwa na masoko na wataendelea kulima na kwa sababu wakilima bila masoko ni sawasawa na kutupa shilingi chooni na hilo halikubaliki.

Mheshimiwa Spika, nimesahau kusemea Serikali kwa kufunga mipaka na kuona wananchi walivyodidimia, lakini watafurahi sana wakisoma hotuba hii na kuona kwamba inatekelezwa. Mungu awape afya, nakushukuru na nakupongeza Waziri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na Mungu akubariki. Naunga mkono kwa nguvu zote hotuba ya Waziri wetu wa Fedha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
kunipa nafasi hii na ni mara yangu ya kwanza kwenye bajeti hii ukiacha maoni ya Kamati niliyoyatoa hapo mbele kuchangia kwenye bajeti ya mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana na kumpongeza sana Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa hotuba nzuri iliyojaa takwimu ambazo tunazihitaji, na mimi sihitaji kurudia takwimu hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Taifa lililoendelea bila viwanda. Viwanda kwanza vinatumia teknolojia, lakini viwanda vinazalisha teknolojia kwa ajili ya sekta nyingine. Kama viwanda ndiyo vinavyozalisha teknolojia ya kuboresha sekta nyingine, itakuwaje nchi hii iondokane na umaskini bila ya kuwa na msingi wa viwanda? Kwa hiyo, naishukuru Serikali kupitia Mpango wa miaka mitano kufanya msingi wa maendeleo uwe ni viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu wa viwanda, mimi nilisomea uchumi wa viwanda, maisha yangu mengi sana nilifanya kazi viwandani kama Ofisa mdogo mpaka nikawa Meneja Mkuu. Siwezi hata siku moja nikaongelea maendeleo bila viwanda. Napenda kusema kwamba uendelevu wa viwanda unategemea sana sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimondiyo inayotoa chakula kwa wale watakaofanya kazi viwandani. Sekta ya kilimo ikiongeza tija ndiyo itakayoleta ajira kwenda viwandani, ikisaidiana na sekta ya elimu. Kwa hiyo, ndugu zangu, hatuwezi tukaongelea maendeleo ya viwanda na msingi wa uchumi wetu na maendeleo yetu kama hatutatilia nguvu sana sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ili iweze kutekeleza wajibu wake katika kuendeleza viwanda, ni lazima iwe ni kilimo cha kisasa. Tutumie zana bora na kisasa, tutumie mbolea na mbegu za kisasa; tutumie viwatilifu, lakini hatimaye ni viwanda ambavyo vitaongeza maisha ya malighafi na chakula kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri, ninampongeza sana.
Kwa hiyo, sisi wote ili tuweze kui-support Serikali au kuipa msukumo kwa msingi huu wa viwanda ili tufikie uchumi wa kati na wa viwanda, tukubaliane kwamba bila ya kuongeza bajeti kwenye kilimo, tusahau maendeleo ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba wakati wa ukoloni mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ulivunjika nchi hii. Tulikuwa tunakula tusichozalisha na kutumia tusivyozalisha na tunapeleka nje vitu ambavyo tungepaswa vitumike kwenye viwanda vyetu. Sasa ni lazima turudishe mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo. Namna moja ya kurudisha mnyororo huu ni kupitia viwanda, kwasababu baada ya kufanya kazi mashambani, lazima mazao yale yatakayozalishwa na wakulima yasipopata masoko viwandani ni sawa na kutupa shilingi chooni. (Makofi)
Kwa hiyo ndugu zangu, wakati tunakazania sana kilimo, namna moja ni kukazania viwanda ambavyo vitachakata au vitasindika mazao ya kilimo. Na mimi naomba Bunge hili liazimie kwamba viwanda ambavyo tutaanza navyo ni hivi ambavyo vitakuwa na uhusiano wa karibu na kilimo ambavyo vitaipa kilimo malighafi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo waliotangulia kutoa mchango kwa viwanda wamesema miundombinu ni jambo muhimu, na mimi naungana nao kwamba bila miundombinu viwanda haviwezi vikaendelea. Ndiyo maana hapa katikati kutokana na ukosefu wa umeme hatukuweza kuanzisha na kuendeleza viwanda vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Muhongo aangalie sana mgao wa umeme kuelekea kwenye viwanda kama tunataka kuwa na viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niongelee jambo moja; ndugu zangu, kuna viwanda mama, kuna viwanda vya kati na kuna viwanda vya kuchakata. Bila viwanda mama hatuwezi kuwa na viwanda vingine. Kwa hiyo, napenda kwa muda uliobaki niongelee umuhimu wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Liganga na Mchuchuma ni viwanda mama. Mchuchuma itatoa makaa kwenda kwenye mradi wa chuma. Kwa hiyo ndugu zangu, tuna jambo moja ambalo Wabunge wengi hawalifahamu kuhusu chuma cha Liganga. Chuma cha Liganga siyo kama maeneo mengine ya migodi ya chuma ina kitu kinaitwa mchanginyiko wa madini mengine ambayo kama huna teknolojia sahihi huwezi ukapata chuma safi kutoka Liganga. Kwa hiyo, siyo rahisi kupata wawekezaji ambao wana ujuzi huo, naomba mjue hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana tutoe msukumo kuanza utekelezaji wa mradi huo. Ilituchukua muda mrefu kupata mwekezaji wa Liganga; na naomba niseme kwamba nilishawahi kuwa Waziri wa Viwanda ili mjue kwamba ninaposema hivyo, nasema mambo ambayo nafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipotangaza tender ya Mchuchuma, ilituchukua muda mrefu kupata teknolojia sahihi. Teknolojia hiyo watu wengi wanaipiga vita ili sisi tuendelee kutokuwa na chuma tuagize nje. Mjue kwamba kuagiza chuma nje itakuwa ni ghali kwa viwanda vyetu kwa sababu mazao ya chuma ni mazito na kwa hiyo ni lazima zitakuwa na gharama ya kuleta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi yenye bahati kama Tanzania, Liganga na Mchuchuma ni mwendo mfupi tu! Kwa hiyo, tutakapotengeneza chuma, makaa ya mawe tunayoyahitaji yatakuwa pale karibu. Naomba sana tupiganie mradi wa Liganga uanze mapema inavyowezekana kama kweli tunataka kuwa na viwanda Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka tuwe na viwanda na kilimo bora, tukazanie viwanda vya mbolea vile vile. Tuna gesi lakini wale wanaoleta mbolea kutoka nje, hawataki tuwe na viwanda vya mbolea. Ninawaombeni sana hilo mlijue. Mtwara ina gesi na mambo yanayowezekana tuyafanye sasa, tuanzishe viwanda na hivi ndivyo vinaitwa viwanda mama. Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Mbolea na mashamba ya mbegu ndiyo yatakuwa ni msingi wa uchumi wa kati wa viwanda. Tukifanya hivyo, tutafanikiwa na mpango huu wa miaka mitano au utabaki kwenye vitabu kama ilivyokuwa muda uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka mbali, sasa hivi nimetoka Hanang, naomba niwakumbuke watu wa Hanang tena kuendelea kuwashukuru sana kwa ajili ya kunipa kura na nitaendelea kuwajibika kwao. Naomba ushirikiano wa dhati na ninaomba ushirikiano wa Wizara ya Viwanda na Bunge hili ili kweli nchi hii iwe nchi ya viwanda na uchumi wa kati kupitia kilimo cha kisasa na haiwezi kuwa kilimo cha jembe. Ahsanteni sana na Mungu awabariki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anazofanya na mimi nitajikita zaidi kwenye ujenzi wa barabara na pengine kwa ujumla, mambo mengine machache. Napenda kuwapongeza kwa sababu si kazi rahisi kujenga barabara za lami katika miaka michache kwa kilometa 17,000 na ninashukuru sana Mkoa wa Manyara una kilometa 223 za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiomba Wizara, pamoja na kilometa hizi 223 sisi tuna barabara ambayo tumeiomba na Mheshimiwa Rais aliahidi barabara kutoka Mogitu kwenda Haydom – Mbulu mpaka Karatu na Haydom ndio Hospitali ya Rufaa, kuna miezi mingi ya mvua ambapo wananchi hawawezi kwenda kwenye hiyo hospitali, kwa hiyo, tunaomba sana barabara hiyo iwe ya lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zangu naomba Wizara iangalie gharama za kujenga barabara za lami. Nilivyoangalia takwimu kwenye kitabu hiki ni karibu shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja kujenga kilometa moja. Ninaomba sana tuliangalie hilo kwa sababu, badae hii itakuwa reflected kwenye gharama za uchumi ndani ya nchi na ninajua kwamba, mwanzo ni mgumu, lakini tunavyoendelea tunaweza tukafanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naliomba ni barabara za Mkoa wa Manyara, ni chache sana ambazo zina hadhi ya mkoa, tunaomba sana barabara zile zipandishwe hadhi. Na tumeshaandika barua kwenye Wizara, lakini naomba nikumbushe barabara ya Dongobesh - Obesh - Basodesh - Gawal mpaka Singida tunaihitaji kwa sababu itatusaidia sana kwenye uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo ninaliomba ni kwamba tumeweza kujenga barabara nyingi kuu kwa ajili ya kupewa asilimia 70 ya Mfuko wa Barabara. Ninafikiri muda umefika sasa kupeleka nguvu kubwa zaidi kwenye barabara za Wilaya na vijijini na ni wakati muafaka na ninawaomba Wabunge tukubaliane kwamba sasa mgawanyo uwe asilimia 50 kwa 50 ili barabara hizi ziende sambamba na barabara kuu ziwe served na barabara zile za Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwamba nitajielekeza zaidi kwenye mambo ya ujumla; nasema kwamba jamani katika usafirishaji na uchukuzi, gharama ndogo iko kwenye usafiri wa maji, ukifuatiwa na usafiri wa reli. Na uchumi utakuwa na gharama ndogo kama reli itakuwa inatumika zaidi kuliko barabara. Ninaungana mkono na watu wa reli ya kati, reli ya Tanga na ile ya Kaskazini kuelekea Kaskazini Magharibi kwa kufanya uchumi wetu uwe wa ufanisi kulinganisha na nchi zingine ili tuweze kufanya biashara nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana hili tuliangalie ili baadae sasa barabara ziwe zina-feed reli na ninajua kuna watu, na mimi kama ningekuwa na malori ningeogopa kwa binafsi yangu kuzamisha reli kwa ajili ya barabara. Ninaomba sana hili tuliangalie, lina maslahi binafsi, ni ngumu na tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ningependa kusema namna ya kuendesha Bunge hapa. Ninaomba sana jamani habari ya kutukanana, habari ya kukashifiana, haikubaliki na Kanuni za Bunge, lakini hili ni jumba tukufu, hili ni jumba ambalo tunapaswa kuwaheshimu viongozi wetu wa nchi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti ya Waziri, pamoja na…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, bila kupoteza muda, dakika tano ni chache sana, naomba nianze na suala la barabara ya Mogitu – Haydom – Sibiti. Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba itaiwekwa barabara hii lami kwa sababu tuna Hospitali ya Rufaa kule na watu wengi wa maeneo ya Hanang, Mkalama na hata Sibiti yenyewe wanakuja pale Haydom kupata huduma ya afya.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, kuna maeneo ambayo wakati mvua ya El-Nino iliponyesha, makorongo makubwa yalitokea na yakitenganisha shule na watoto au zahanati na wagonjwa. Kwa hiyo, naomba wasiiachie Halmashauri tu, Wizara hii ya Ujezi nayo isaidie na namwambia Waziri kila siku.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, naomba ni-declare interest kwamba aliyesaini mkataba ule kuhusu Bandari ya Bagamoyo ni mimi wakati nikiwa Waziri wa Uwekezaji. Nataka niwaambie tulifanya hivyo kwa sababu ilionekana Afrika nzima Ukanda wa Pwani the best place ya kuweka bandari ni Bagamoyo lakini Bagamoyo si bandari tu, Bagamoyo ni Economic Special Zone ambapo kutakuwa na viwanda na miradi mingine mingi ambayo itainua uchumi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana na mimi nisingesemea, mimi natoka Hanang huko hakuna bandari, lakini naisemea Bagamoyo kwa sababu kwa kweli ni mahali ambapo itasaidia sana na hii SGR itumike vizuri kuleta economic change kwenye Tanzania yetu na kwa kweli naombeni sana muangalie hilo na sisi Wabunge nimeshukuru sana Spika mwenyewe alivyosema na sisi wote tuwe pamoja, lakini sidhani kama hii Serikali wala inakataa, ina sababu labda kuchelewesha, lakini wajuwe ya kwamba kwa kweli hapa ni mahali ambapo tukipapuuza tunapuuza kukuza uchumi wa nchi hii ulingane na tunachotaka baadaye.

Mheshimiwa Spika, ya mwisho Rufiji si mahali padogo ni mahali pa kubwa, babu yangu mimi alikuwa akipingana sana na wakoloni wakampeleka Rufiji wakamzika huko alipokufa, sasa na mimi nashindwa kwenda kuona lile kaburi la babu yangu, kwa hiyo tumsaidie Mchengerwa na yeye tuone umuhimu wa kuona eneo ambalo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaunga bajeti hii mkono na nina imani na Serikali hii kwamba wala haina shida na Bagamoyo, lakini wataona umuhimu wake na kutoa kipaumbele, ahsante sana, sana na Mungu akubariki. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa kuongea kwenye sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi na kwa maslahi ya watu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya kuangaza Tanzania na kuleta maendeleo kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kwa sababu muda ni mfupi ningependa kushukuru watu wengi lakini niende moja kwa moja kwenye mambo ambayo ni pressing kwa Wilaya yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Mkoa wa Manyara ni Mkoa wa kilimo na Wilaya ya Hanang ni Wilaya ya kilimo na ufugaji. Umeme wa REA namba moja ulitpelekwa kwa vijiji vinne tu Wilaya ya Hanang na mpaka leo vijiji vile vinne bado havijapata umeme, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze vijiji hivyo vitapata umeme lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tulipata vijiji vichache wakati Wilaya za jirani zinapata zaidi ya 20, zaidi ya kumi nikamwomba vijiji 19 na yeye akaniahidi, naomba uwahakikishie watu wa Hanang kwamba Hanang nayo inathaminiwa kwa hivyo vijiji 19 kuweza kupata umeme na orodha nimekupa. Kwa ajili ya muda mfupi nisingependa kupoteza muda. Ninaomba uone umuhimu wa Wilaya moja kwa REA zote tatu sasa tunaenda kwenye REA tatu imepata vijiji vinne na nafikiri utaona umuhimu wa kuona kwamba Mbunge akilia hapa ana sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Tanzania ni nchi iliyojaaliwa kuwa na vyanzo vingi vya nishati, siwezi kuvitaja kwa kuwa mnavijua, lakini ninafikiri gharama ya kupata nishati kwenye chanzo kimoja vinatofautiana na vingine. Na miaka ya awali ya Tanzania tulikuwa tunapata umeme kutokana na maji. Tabianchi ilipoanza kubadilika tukakumbwa na ukame tukapatwa sasa na dharura za kukimbilia kuweka umeme wa dharura. Mimi nafikiri sasa wakati umefika wa kuwa na mkakati mzuri. Ninajua kuna power master plan, lakini ninaomba sana tuangalie mix ya hiyo power master plan kusudi gharama iwe baadaye si kubwa kwa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba tusifikirie vidogo vidogo, mmefanya kazi kubwa, kuna Kinyerezi I, Kinyerezi II, Kinyerezi III mnafanya kazi nzuri na kuna vyanzo vingine ambavyo mnashughulikia. Mimi bado naamini tufikirie vikubwa na mimi nafikiria hakuna umeme ambao utaokoa Tanzania kama siyo ule wa Stigler’s Gorge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Stigler’s Gorge unaweza ukatoa umeme wa kilowatts 2100, tukijielekeza huko wakati wa master plan nimeona Stigler’s Gorge iko kwenye master plan lakini iko mbali. Naomba muilete karibu kusudi tuwe Taifa la kufikiria vitu vikubwa. Nitakushukuru sana, najua una uwezo na ukiamua hilo unaweza ukalifanya vizuri na mimi sina wasiwasi, ninajua wakati wa dharura dharura ile ndipo tulipoingia kwenye IPTL, kwenye DOWANS na mambo ambayo yalileta madhara makubwa kwa Taifa letu.
Kwa hiyo, sasa ni wakati mzuri wa kufikiria kwamba katika ile master plan tuwe na mkakati ambao utajielekeza kwenye kuona kwamba tumeamua kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati. Bila kuwa na umeme wa hakika huko hatutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiria kwamba Mkoa wa Manyara ndipo ambapo Mererani ipo. Kutokana na Tanzanite ya Mererani Wilaya ya Simanjiro ikatoa eneo la EPZA bure na wengine wote wanadai fidia.
Ninaomba sana tuangalie Mererani na tuone jinsi ambavyo tutaweza kuongeza thamani ya Tanzanite kwa kuweka viwanda ili tuweze kuwa na faida ya Tanzanite kuliko inavyoonekana sasa Tanzania ni nchi ya tatu. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeleta manufaa makubwa ya vito ambavyo vimeletwa na Mwenyezi Mungu nchini kwetu na Mkoa wa Manyara ambao hauna resources nyingi isipokuwa ardhi yenye rutuba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana nirudie tena kwamba naomba Wilaya ya Hanang iletewe umeme kwenye vijiji nilivyosema ili tuongeze thamani ya mazao ya kilimo, thamani ya mazao ya mifugo na watu ambao zamani ndiyo walikuwa nyuma kuliko wengine wamekubali kukimbia muwawezeshe kukimbia kuwakuta watu wa Kilimanjaro na Arusha. Mkoa wa Manyara umejigawa kwa sababu tulikuwa nyuma sana na kwa ajili ya Arusha tukawa tunaonekana tumeendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa tuingie kwenye huo mkakati wa kuendelea wa kutuletea umeme na wewe ndiye utakuwa savior, ninakushukuru, ninakupongeza na Mwenyezi Mungu atakupa nguvu zaidi na kuendelea kuwa kwenye hii Wizara, maneno yapo, Upinzani wanasema wao wanaisimamia Serikali naomba tukumbushane hapa kwamba ni jukumu la Wabunge wote pamoja na wale wa CCM kuishauri na kuisimamia Serikali, siyo kazi ya Wapinzani tu. Na sisi ndiyo tuna wajibu mkubwa wa kuishauri na kuisimamia Serikali yetu kuliko ninyi, Ilani ya Uchaguzi ni yetu na kwa hivyo lazima tuisimamie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kama dakika zangu hazikuisha wengine nao wanufaike. Ahsanteni wote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nyingine tena. Na mimi kutoka mwanzo niseme kwamba naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niungane na wenzangu kukubali kwamba viongozi wa Wizara hii, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wengine wote wamejitahidi sana hasa katika eneo la kuondoa migogoro. Tunawapongeza na tunaomba muongeze bidii. Mimi namfahamu Waziri, Mheshimiwa Lukuvi tulikuwa naye Ofisi ya Waziri Mkuu na najua jinsi anavyochapa kazi, endelea kuchapa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ndiyo rasilimali kuu ya Tanzania na pengine nchi hii ya Tanzania imejaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba lakini ardhi inakuwa na thamani pale tu ambapo imepangwa, imepimwa na kumilikishwa. Bila ya kuwa na vipimo, bila kuwa na hati miliki, ardhi kwa kawaida pamoja na kwamba ni rasilimali muhimu lakini inakuwa haina thamani. Mpaka sasa hivi ni asilimia 15 tu ya ardhi ya Tanzania imepimwa na imemilikishwa. Kwa hiyo, asilimia ile yote 85 maana yake haina thamani. Kama Tanzania tunataka kuondokana na umaskini inabidi kwa kweli tuipe rasilimali hii muhimu thamani inayotakiwa kwa kupangwa, kupimwa na kumilikishwa. Wananchi wanapokuwa na hati miliki au haki miliki wanaweza wakaitumia ile ardhi kwa shughuli za uchumi lakini ikatumika vilevile kama dhamana kukopa kuweza kutumia ile ardhi vizuri zaidi. Kwa hiyo, ndugu zangu nawaombeni kipaumbele kipelekwe kwenye kupima ardhi hii ya Tanzania na kumilikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wananchi zaidi ya dhamana wanaweza wakatumia ardhi hii ikiwa na hati miliki kama hisa na kuungana na wenye mtaji wa fedha ili ardhi hii itumike katika uwekezaji. Watanzania wanashindwa kuwekeza kwa sababu ardhi waliyonayo haina thamani na kwa hivyo hawawezi kuwa na hisa kwenye uwekezaji. Kwa kiingereza inaitwa land for equity ambapo alipokuwa Waziri Mheshimiwa Anna Tibaijuka na mimi tuliibuni ili Watanzania wawe na uwezo wa kushiriki kwenye uwekezaji bila ya kutafuta fedha, wanaweza wakatumia hiyo ardhi kwa kukopa au wanaweza kuwa na hisa kwenye uwekezaji kupitia ardhi hiyo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende kwa wawekezaji na nataka nijielekeze Hanang. Hanang ni eneo la kilimo na mifugo na ardhi ipatayo heka 70,000 iko mikononi mwa wawekezaji. Wawekezaji wenyewe wale hawaitumii ardhi ile kama inavyopaswa. Kwanza wametumia sehemu tu ya ardhi ile waliyopewa wakati watu hawana ardhi ya kutosha wanaingalia ile ardhi na kuitamani, napenda tuwasimamie wale ili waitumie hiyo ardhi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, sioni sababu ya mwekezaji kutoka nje achukue ardhi ya Tanzania, kwa mfano pale Hanang watu wa Hanang wanazalisha ngano nyingi zaidi kwa heka moja kuliko wawekezaji waliokuja na ina-defeat the whole purpose inakuwa haina maana. Kwa hiyo, naomba tuangalie na tija katika uwekezaji ili tupate faida ya kutosha kwenye uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi ya hivyo kutokana na uwekezaji kwenye ile ardhi, wawekezaji walituahidi kufanya mambo mbalimbali. Siwezi kuorodhesha, lakini moja ambalo nalijua ni kujenga mabwawa makubwa kwa ajili ya umwagiliaji na wananchi kuweza kunufaika lakini mpaka sasa limechimbwa bwawa moja na halijakamilka. Nataka na ahadi zile zote nazo ziweze kutekelezwa ili watu wa Hanang wanufaike na uwekezaji ule na kama hawalimi vya kutosha, kuna wengine wana mashamba zaidi ya moja, mashamba yale ambayo hawawezi kuyalima yarudi mikononi mwa wananchi. Mimi najua wananchi wa Hanang wanaweza kulima ardhi ile na kuweza kuleta manufaa ambayo wawekezaji hawaleti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndugu zangu migogoro ya ardhi iko mingi Wilayani Hanang. Kuna migogoro ya mipaka kati ya kata na kata, vijiji na vijiji na hata wilaya na wilaya zingine zinazopakana na Hanang hata Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Singida, Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine tunakuwa na migogoro. Namuomba Waziri Mheshimiwa Lukuvi aje Hanang na Mkoa wa Manyara ili migogoro ile itatuliwe maana kila wakati kumekuwa na vifo kupitia migogoro hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wale wawekezaji watimize ahadi yao moja ambayo wameahidi ya kujenga branch ya university ya Sokoine kwenye yale mashamba, mpaka sasa imebakia ahadi tupu hakuna utekelezaji wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo nataka kuongelea kuhusu ardhi ni kwamba jamani bila ya kupima hii ardhi na kuiweka kwenye shughuli mbalimbali, mifugo, kilimo, biashara, huduma za jamii, migogoro itaendelea kuwepo. Migogoro itaendelea kuwepo kati ya wafugaji na wakulima, migogoro itaendelea kuwepo kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi mbalimbali, migogoro itaendelea kuwepo kati ya wawekezaji na wananchi wa Tanzania. Kwa sababu bila ya kujua wafugaji wawe wapi, wakulima wawe wapi, wawekezaji wawe wapi, jamani hatuwezi kuondokana na mambo haya hata tukiwa na operation ngapi haitasaidia. Ukiwatoa wananchi kutoka kwenye hifadhi na haijulikani wapi wanakwenda kwa ajili ya kuhakikisha ng‟ombe wao zinabakia kuwa hai watavizia kurudi kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nathamini hifadhi za Tanzania na ni mmoja wa watu ambao nitakuwa wa mwisho kabisa kuondoa hifadhi lakini lazima tuone kwamba wakulima na wafugaji wana maeneo ya uhakika la kufanya shughuli zao. Wakijua eneo lao ni hekta ngapi watahakikisha ng‟ombe wanaoweza kubaki kule watabaki na wengine watauzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna nyingine ya kuwasaidia ni kuwa na masoko mbalimbali tushirikiane pamoja kushughulikia suala hili. Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza Wizara zile zikae mara moja ili kuona kwamba wananchi wavyotolewa kutoka kwenye hifadhi, wananchi wanavyogombania ardhi kunakuwa na mahali mahsusi pa wale wananchi kwenda kama ni wafugaji au wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shirika la Nyumba, mambo ya msingi kwa binadamu ni chakula, mavazi na makazi. Shirika la Nyumba linafanya kazi nzuri lakini kama lilivyoundwa zamani baada ya uhuru ilikuwa ni kuwapatia maakazi watu wanyonge zaidi kuliko wale wanaojiweza.
Kwa hiyo, naombeni sana Shirika la Nyumba lifanye kazi hiyo ya kuona watu wa Manzese, Keko wamepata nyumba, watu wa maeneo ya chini wamepata nyumba. Maeneo yale ya matajiri wajenge wenyewe kwa sababu wana mali ya kuweza kuweka dhamana kwenye benki na kujenga nyumba zao, sisi tujielekeze kwa Watanzania wanyonge, wana haki ya kukaa kwenye nyumba na hakuna mtu ambaye ana fedha yake mwenyewe asijenge, lakini ni kwa sababu ya kukosa mali ya kuweka dhamana hawawezi kujenga nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie pongezi zangu na shukrani zangu za dhati kwa Wizara na viongozi wa Wizara, watendaji na taasisi ambazo zipo kwenye Wizara hii. Na mimi nashukuru sana migogoro inapungua, tuendelee kupunguza migogoro hii hadi inapokwisha. Sisi wengine tumekaa kwenye migogoro tukiona watu wanakufa na hatutaki kuendelea kuona watu wetu wanakufa. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hisani yako ya dakika tano. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge katika ku-support lile suala la kuongeza fedha kutoka petroli na dizeli na tukaomba kwenye simu vile vile ili Mfuko wa Maji uwe na fedha zaidi. Tatizo la maji ni kubwa na wote tunakubaliana kwamba Maji ni Uhai na ili fedha hizo zitumike vizuri ni vyema tukawa na wakala ambao utakuwa na wataalam na utasimamia kazi ya kuleta maji kwenye vijiji mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hilo nililoongelea, naomba niongelee kidogo juu ya Jimbo langu la Hanang. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri amekubali kuja kutembelea Hanang. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi shilingi milioni 300, kwa ajili ya maji ya Mji Mkuu wa Hanang, Kateshi na zile fedha zikatolewa na kazi nzuri ikafanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naamini kuna tatizo la utaalam ambao kama litakuja kuangaliwa na Ma-engineer itasaidia na naomba Mheshimiwa Waziri anitumie watu kutoka Makao Makuu waje waone tatizo ni nini. Tunaamini kwamba gharama ni kubwa, lakini tunaweza tukafanya linalowezekana ili maji ya Kateshi yapatikane kwa uhakika na kwa gharama inayohimilika.
Mhesheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang iko kwenye Rift Valley na sehemu kubwa iko kwenye mwinuko na ni mpakani na Singida. Hatuna maziwa isipokuwa ziwa la Basotu ambalo chanzo chake ni maji ya mvua, hatuna mto wa kudumu. Kule kwingine chini kwa ajili ya Rift valley kunakuwa na joto chini ya ardhi, kwa hiyo maji yako mbali, sisi hatuna maji. Maji yetu yanapatikana kwa visima au kwa mabwawa, hatuna mto, naomba sana kwa yale yaliyofanyika, nawashukuru lakini bado sehemu kubwa ya Hanang haina maji. Naomba awatume watu na yeye kuja Hanang ili basi maeneo yale ambayo hayana maji yaweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji Hanang ni kubwa kweli na jana tu jioni kulikuwa na watu wanalalamika kwamba wanapata maji kutokana na chanzo kimoja na ng‟ombe na hata wanyamapori. Kwa hiyo, naomba sana tuwatume watu na Wakala wa Maji Vijijini utasaidia kufanya surveys kwenye vijiji vyetu kwa sababu kila wakati hatuwezi kwenda kufanya kazi mara moja, kuchimba kisima kimoja. Ni vizuri kwa mfano Wilaya ya Hanang iliyo na tatizo la maji kwa ujumla Serikali ikaenda pale na kujua vyanzo mbalimbali na namna ya kuondoa matatizo ambayo yanawasibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge kwamba akinamama wanapata tabu sana na kutokana na akinamama kutumia muda mrefu kutafuta maji watoto wamekuwa wakiungua, watoto wamekuwa wakifanya utundu na kuumia na vile vile kazi zingine za nyumbani zimelala ukiacha sababu ya kwamba wanaume wanawa-accuse kwamba labda wanatumia muda kwenye mambo mengine kumbe wako misituni wanatafuta maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaombeni sana hili la wakala tulitilie mkazo kwa sababu watafanya kazi ambayo itajulikana na kutakuwa na mtu ambaye tunaweza kumnyooshea kidole kwa sababu Halmashauri hazina watu wenye uwezo na Halmashauri hazina capacity ya kuweza kuletea Wilaya mbalimbali au Majimbo yetu maji. Kwa hiyo, naombeni sana tuwe pamoja na na-declare interest kwamba ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maji, Kilimo na Mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa pamoja, tukiamua tuongeze fedha za kuchangia kutoka kwenye mafuta na vile vile kutoka kwenye simu na tukiwa na wakala tutakuwa tumeondokana na tatizo la msingi na tutakuwa na uwezekano mkubwa wa kuondoa tatizo la maji katika nchi yetu ikiwemo Wilaya yangu ya Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutaja vijiji ambavyo havina maji na ningependa kutaja miradi ambayo ina matatizo lakini muda hauko na sisi, na mimi na…
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mtolea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana na vilevile niseme kwamba hii ni sekta ambayo inatoa chakula kwa asilimia mia moja kwa Watanzania na inatoa ajira kwa asilimia 65. Inatoa malighafi kwa Viwanda kwa asilimia 65, jamani sio Sekta ya kupuuza, lakini leo napenda sana kujielekeza kwenye suala moja tu kama ulivyotuelekeza ni suala la umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, suala la tabianchi kubadilika linajulikana kwa kila mmoja na nafikiri ni muhimu sana kwa Waziri wa Kilimo kulifahamu hilo, bila kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hili suala la chakula, suala la kupata malighafi kwa viwanda, suala la ajira ya watu wengi na mambo mengine ambayo sitayasema sasa hivi litakuwa halina maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina hakika, labda mimi mwenyewe sijaiona, suala la umwagiliaji halijapewa umuhimu unaotakiwa kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, naomba atueleze kwa nini ni kwa sababu tu ndiyo imehamia kwake. Pamoja na hilo sisi watu wa Hanang, tuna miaka kumi tuliomba kuchimbiwa Bwawa la Gidahababieg ambalo linakusanya maji ya Mlima Hanang yote kwenye eneo ambalo ni kavu na hawana uhakika wa chakula, kwa nini Mheshimiwa Waziri hajaorodhesha miradi ambayo katika bajeti hii itapewa hela ningeweza kujua kama Gidahababieg ipo au haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana na Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Hanang ni moja ya Wilaya ambayo ina udongo mzuri sana, ndiyo Wilaya ambayo inalima sana, lakini mvua siyo za uhakika. Kwa hiyo masuala ya Mabwawa ni muhimu sana, pamoja tunajua kwamba kuna upungufu kwenye maeneo mengine ya kilimo, lakini naomba leo niseme kwamba, kama tunataka tutumie udongo huo mzuri wa Hanang na Mkoa wa Manyara kwa ujumla, hatuna jambo lingine isipokuwa kukazania mabwawa ili watu wapate maji lakini vilevile kilimo kipate maji na mifugo vilevile ipate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ya Hanang ukiangalia tukichimba hata mita 200 ya visima hatupati maji. Kwa kweli ni mabwawa yanayotakiwa ni makubwa, wananchi wetu wanajitahidi hata wanachimba wenyewe mabwawa lakini wanahitaji kwa kweli msaada wa Serikali kwa mabwawa makubwa kwanza kwa kufanya survey, lakini kwa kuchimba mabwawa kwa namna ambayo inatakiwa kwa ufundi. Kwa hiyo naomba sana, naunga mkono hotuba hii na naunga mkono bajeti hii na ukiangalia Waziri katengeneza kitabu kizuri sana, lakini kitabu hiki basi kiweze kuwasilisha manufaa kwa wananchi. Kwa mwaka huu kwa Wilaya ya Hanang ni kujua kwamba Bwawa la Gidahababieg litachimbwa na sisi tuweze kunufaika na Mwenyezi Mungu ambariki sana Mheshimiwa Waziri katika kazi yake hiyo mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono bajeti hii na yote ambayo anayafanya Waziri. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami niungane na wenzangu wote ambao wametangulia kusema kwamba tukitaka Bunge hili liweze kutekeleza wajibu wake na kwamba kila mtu awe na nafasi, lazima kanuni zisimamiwe humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia toka ulipoanza umekuwa ukilikazania hilo, naomba uendelee hivyo, kusitokee mtu anakukatisha tamaa kwa sababu ukikata tamaa maana yake ni kwamba uendeshaji wa Bunge hili hautakuwa na utaratibu ambao unategemewa kisheria. Nakupongeza sana, nakutia moyo na nina uhakika wale waliotaka kukutikisa au kulitikisa Bunge hili watarudi bila wewe kutikisika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wake na watendaji wote kwa kazi nzuri ambayo tayari wameshaionesha kwa hotuba hii ambayo ni nzuri. Baada ya pongezi hizo nipende kumshukuru na kumpongeza Rais kwa kumchagua Waziri anayeongoza Wizara hii. Waziri nimefanya naye kazi, na-declare interest kwamba nilikuwa Waziri wa Uwekezaji, na nilipohamia Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilikuwa chini yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo naomba niseme machache kuhusu PPP au ubia kati ya Public Sector na Private Sector. Hii ndiyo namna ya kuweza kuhimiza uwekezaji mkubwa ndani ya nchi hii. Huwezi ukaiachia sekta binafsi peke yake wala huwezi kuiachia Serikali peke yake. Tukitaka kujenga uchumi wa soko lazima Serikali na sekta binafsi washirikiane na hakuna namna ambavyo wanaweza kushirikiana ila katika ubia. Sera ipo, sheria ipo, ilifanyiwa marekebisho, kilichobaki ni utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ubia kitu ambacho kinatakiwa ni kuona risk ambayo kila mbia anabeba. Kuna athari (risks) nyingine ambazo sekta binafsi haziwezi kubeba, pale ambapo Serikali inahitajika iingie, lakini inapotokea mtaji unapotakiwa na upo kwenye sekta binafsi, Serikali ina uwezo mkubwa wa kuzuia mambo ambayo sekta binafsi wenyewe hawawezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo lilikuwa limeisibu PPP ni urasimu ambao haukuwa na maana, au kutokuelewa vizuri sera na sheria ile. Wizara ya Fedha na Uwekezaji ndizo zilikuwa zina sera na sheria lakini utekelezaji uko kwenye sector Ministries. Kwa mfano, Wizara ya Ujenzi inaweza ikajenga barabara nyingi sana na katika muda mfupi kama ikipata sekta binafsi ambayo inaweza ikaingia nayo ubia na kuna namna nyingi ya kuweza kuingia kwenye ubia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kuliongelea ni nafasi ya mabenki katika kujenga uchumi wa soko. Katika mambo ambayo yaliathiri sekta binafsi ni pale ambapo walipokuwa crowded out na Serikali yenyewe kupitia treasury bills au wakati mwingine hata bonds. Kwa sababu Serikali inapokopa kwenye mabenki, mabenki yatapendelea Serikali kwa sababu risk ya kukopesha Serikali ni ndogo sana au hakuna, kwa hiyo sekta binafsi haiwezi kupata nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Wizara ya Fedha kuamua kutoa fedha zake ambazo zinakopa, ambazo ni zake zenyewe na kuzirudisha Benki Kuu, sasa mabenki yameanza kuwahimiza watu wapeleke fedha benki. Kabla ilikuwa ni uchaguzi wao kupata fedha kutoka kwa watu binafsi, walikuwa wanategemea zile fedha za Serikali ambazo hatimaye Serikali inakopa. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo benki sasa zimeanza kuchacharika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, najua kwamba Serikali haiwezi kuacha kukopa, lakini mjaribu ku-balance ili sekta binafsi isikose nafasi. Huwezi kuwa na uchumi wa soko kama sekta binafsi haiko active. Kwa hiyo, naomba mliangalie suala la treasury bills.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni riba. Katika uchumi wa soko huru faida haiwezi ikawa juu ya asilimia 10. Sasa kama riba ya benki inayotoza ni zaidi ya asilimia 10 maana yake yule ambaye yuko kwenye soko huru hawezi kwenda kukopa halafu apate faida ya chini. Hili ndilo limelikumba Taifa hili. Naomba muangalie suala hili la riba zinazotozwa na benki zetu. Kwa sababu mkitaka sekta binafsi ambayo ni rational ikakope benki lazima riba iwe chini ya faida ambayo inapatikana kwa sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia hilo, naomba niongelee VICOBA. Kuna fedha nyingi sana ndani ya VICOBA, na fedha zile haziendi benki, tujiulize kwa nini? Ni kwa sababu hakuna sera na sheria. Kuna watu ambao wamesemea hapa, naomba Benki Kuu iangalie sera ambayo itafaa VICOBA viwe rasmi na vinufaishe watu kama inavyohitajika. Vijijini kuna VICOBA vingi sana na sioni namna ambayo soko huru linaweza kwenda vijijini bila VICOBA hivi kutumika. Naomba sana tuone watu walio wengi ambao hawatataka kukopa hela nyingi lakini kwa wingi wao wakikopa kidogo kidogo italeta impact kubwa ndani ya uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kuliongea kwa ufupi ni Benki ya Kilimo. Nimesikia na Ushirika unataka kuanzisha benki na Serikali ndiyo itakayochangia benki hizo mbili. Tukianza tena kuzindua Benki ya Ushirika maana yake Benki ya Kilimo itasimama kwa sababu hatuna hela za kuchangia benki hizo zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Wizara na Benki Kuu kwamba tukazanie Benki ya Kilimo, hatimaye kama Benki ya Ushirika inaanza tuondokane na Benki ya Kilimo lakini hatuwezi kuwa na benki zote mbili na zianze kwa wakati mmoja. Tukiruhusu benki zote mbili zianze kwa pamoja tutatawanya nguvu zetu na hakutakuwa na impact kwenye kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima ndio watakaoikomboa nchi hii, mazao ya kilimo ndiyo yatakayokuwa malighafi ya kiwanda. Mazao ya kiwanda ndicho kitakachokuwa chakula cha wale wanaofanyakazi viwandani na kilimo ndio uti wa mgongo ambao watu wangu wanategemea. Kwa hiyo, tusipokazania benki hii, najua kwamba suala hili liko kwenye bajeti tutakayojadili, lakini kwa leo nataka nisisitize kwamba hatutakuwa tumetenda haki kwenye Benki ya Kilimo kama tutaanzisha Benki ya Ushirika wakati hii ya kilimo bado haijapewa mtaji wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Najua kuwa suala la sovereign ratings ni muhimu sana ili nchi hii ionekane kwamba inaweza kukopa kwenye masoko ya nje, lakini hilo tuliangalie kwa sababu kuna nchi ambazo zimefanya hivyo zikaingia kwenye matatizo. Tusiiachie nchi yetu ikaingia kwenye matatizo. Nchi hii tunapata fedha kidogo sana kwenye investment kutoka nje. Kiasi cha investment inayokuja Tanzania ni 0.03 percent, ni hela kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana Waziri wa Mambo ya Nje alivyokuwa anaongelea issue ya Economic Diplomacy; tunachopigania ni kwamba investments zaidi zije na share yetu ya international markets iwe kubwa; hilo ndilo matokeo mazuri ya Economic Diplomacy ambayo ni nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiisimamia Benki Kuu na Benki nyingine na sekta binafsi nina hakika tutapiga hatua kubwa kwenye kujenga uchumi wetu na sioni pengine ambapo kazi hii inafanyika isipokuwa kwenye Wizara yetu ya Fedha na Mipango. Nawaombea Mwenyezi Mungu awape afya njema muweze kusimamia. Waziri Mpango ana uwezo, Naibu Waziri ana uwezo, Watendaji wana uwezo, nina hakika Wizara hii itasimamia uchumi wetu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba usikate tamaa. Wewe ni mtoto wetu, sisi tuko hapa kuona kwamba kazi ambazo zinanufaisha Bunge hili unaendelea kuzifanya na usitetereke sisi tuko na wewe. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na wenzangu kukupongeza, kwa kutumia sheria, kanuni na taratibu za kuendeshea Bunge, na unaona amani ilovyorudi humu ndani. Ni mategemeo yangu kwamba wenzetu waliotoka humu ndani watakuja kukuona na mfikie muafaka warudi huku Bungeni turudishe heshima ya Bunge letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vilevile kuungana na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote kwa kuja na mpango mzuri wa kutekeleza Mpango wa Awamu ya Pili wa Miaka Mitano, na bajeti ya kutekeleza mpango huo. Ninawapongeza kwa sababu, kwa kweli wameonesha kwamba kuna maendeleo ambayo tutayapata, lakini nina yafuatayo ambayo ningependa kusema.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa mpango wa miaka mitano wa pili ni viwanda na tuna bahati sana Mheshimiwa Rais mwenyewe amelisimamia hili, na amelielekeza Taifa hili kwamba hakuna sekta nyingine ambayo itapeleka nchi hii kuondoa umaskini na kutupeleka kwenye kipato cha uchumi wa kati. Ninampongeza, ninamshukuru na nina uhakika Bunge hili litamuunga mkono kuona kwamba viwanda vinasimamiwa na tutahamasisha uanzishaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa Waziri aone kwamba hamna namna ambavyo uchumi wa viwanda utanufaisha wananchi walio wengi Watanzania bila ya kupitia sekta ya kilimo. Ninaomba tusiiseme kisiasa, tuongee kwa vitendo. Pia ningeomba kwamba namna moja ya kuhakikisha kwamba viwanda vinakuwa ni kufanya kwamba kilimo kinakuwa cha kisasa. Azimio la Maputo tumeliridhia hapa lililosema kwamba tuitengee sekta ya kilimo asilimia kumi ya bajeti. Mwaka huu tumetenga asilimia 4.6; ninaomba kadri tunavyokwenda Mheshimiwa Waziri aone hili linafanyika ili tujielekeze kwenye vitendo zaidi ya kusema tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni kwamba kilimo hakitakuwa cha kisasa kama zana, kama mbegu, kama viuatilifu havitatiliwa mkazo. Watu wangu wa Hanang na Wilaya ingine wangependa kuona matrekta yanamwagwa kama namna ya kuboresha tija katika kilimo. Wangependa kuona mbegu zinapatikana kwa wakati na vilevile mbegu bora zinapatikana na mbolea nayo inapatikana. Ningependa kusema kwamba viwanda ambavyo vitapeleka nchi hii mbele na vitasambaza mapato kwa wananchi ni viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, viwanda vya kusaidia tija kwenye kilimo kama viwanda vya mbolea na vilevile kuona kwamba masoko yanapatikana kwa kuhakikisha kwamba (a),(b), (c), (d) zinazotakiwa kwenye soko zinatiliwa mkazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la kusisitiza ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo, bila Benki ya Maendeleo ya Kilimo wananchi hawawezi kupata fedha za kuweza kuboresha kilimo. Ninaomba sana kila mwaka kama Serikali ilivyoahidi iweze kutoa zile fedha ambazo zitaimarisha benki hiyo. Kubwa zaidi ambalo lazima tulikumbuke ni kwamba bila ushirika imara, bila ushirika usioibia watu, kilimo hakitaendelea. Kwa hiyo, naomba sana tuone kwamba hayo mambo yametekelezwa ili kilimo kiwe cha kisasa kiwe bora kiweze kutoa malighafi na soko kwa viwanda ambavyo tunataka kuvianzisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo, kama unataka maendeleo ya watu kama Waziri alivyoandika kwenye mpango wa maendeleo, hamna namna ya kuleta mapinduzi ya viwanda kama kilimo hakitapewa uzito unaosaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuliongolea ni kuhusu maji, ningependa kuungana na Wabunge wote kwamba tumeahidi kutua ndoo ya maji kutoka kwa wanawake wa Tanzania wakiwemo wale wa Hanang na hatuwezi kufanya hivyo bila ya kuwa na mpango madhubuti. Ninampongeza Waziri kwa sababu mwaka jana fedha zilizotengewa Wizara ya Maji ilikuwa shilingi bilioni mia nne na kitu, lakini mwaka huu tumefika bilioni 900 hata hivyo hazitoshi. Kwa hiyo ninaomba suala la kukata shilingi 50 kwa kila lita ya dizeli na petroli tuitilie mkazo jamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua bei ya petroli ilivyokuwa juu mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 6.2 leo mfumuko wa bei ni asilimia 5 .9 tofauti ni nini? na sidhani kama ni mafuta yameleta. Kwa hiyo, naomba hili tulitilie mkazo na Waheshimiwa Wabunge tunaishauri Serikali yetu kwa jambo jema, wakati huu ambako bei ya mafuta iko chini ndiyo wakati wa kuchukua fursa baadaye yakipanda hatuwezi kulifanya hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niongelee suala la logistic center ya Dar es Salaam. Naomba ni-declare interest logistic center ilianza wakati mimi nikiwa Waziri wa Viwanda na baadaye Waziri wa Uwekezaji. Tumetaka logistic center ili Dar es Salaam iwe Hongkong ya Afrika. Nawaambieni kwamba Dar es Salaam ina hinterland kubwa na hiyo hinterland ikitumika vizuri italeta manufaa makubwa. Naomba niwaondolee hofu, kufikiria kwamba bidhaa kutoka nje itafanya viwanda visianze, nataka niwaambie kwamba hilo siyo kweli. Kwa sababu bidhaa zitakazoletwa Dar es Salaam zikionekana zinanunuliwa Congo, Rwanda na kwingineko wawekezaji watakuja kuwekeza kwenye viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo logistic center ni mahali pa ku-test demand au mahitaji ya bidhaa ili kuwavutia wawekezaji wa viwandani. Kwa hivyo, tukitaka tujue bidhaa ambazo zitauzika haraka, na vipi viwanda ambavyo vitatengeneza bidhaa hizo ni lazima tuhakikishe kwamba logistic center ya Dar es Salaam inaanza. Ninataka niongelee vilevile kuhusu jamani mwaka jana Bunge lilitengewa hela nyingi shilingi bilioni zaidi ya 100 mwaka huu tumetengewa shilingi bilioni 99. Ninaomba sana kuona kwamba bajeti ya Bunge, ndiyo inayotuwezesha kutembelea miradi na oversight inayotakiwa. Kwa hivyo, kama zinatosha lakini tuhakikishe kwamba wajibu wetu wa kuwa Wabunge, unatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningetaka kulizungumzia ni kwamba ningependa kusema kwamba takwimu za umaskini vina vigezo vyake, mkiwa mnabadilisha vigezo kila wakati, tutakuwa tunabadili mikoa ambayo ni ya umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Mkoa wa Manyara ulitoka Arusha kwa sababu ulikuwa unaonekana kama umeendelea kutokana na Arusha na tukataka tugawanyike ili umaskini wetu uonekane. Mkoa wa Manyara ndiyo una Wahadzabe, Mkoa wa Manyara ndiyo una Wabarbaig wanaotembea nchi nzima. Mkoa wa Manyara ni moja ya Mikoa ambayo ni maskini na haina vyanzo vingi vya kuondoa umaskini. Ninaomba tuangalie vigezo hivyo, kama Pwani ilivyolalamika tuone kama kweli vigezo hivyo vinatufikisha kujua Mikoa ipi kweli ambayo ni maskini na tuchukue hatua ambazo zinatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nirudie tena, naomba sana Bunge hili na Mheshimiwa Waziri tunamsihi aone umuhimu wa kuongeza shilingi 50 kwa kila lita ya petroli na dizeli kwa ajili ya maji na Wabunge tunalisema hili kwa ajili ya ushirikiano na Serikali siyo tunataka tupingane na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, naomba uvute uzi, uendelee kusimamia Sheria, uendelee kusimamia Kanuni za Bunge hili, uendelee kuona utaratibu unaleta heshima ndani ya Bunge hili na tunawasihi wale wenzetu ambao hawaoni umuhimu huo, hatimaye waone hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na ninampongeza tena Mheshimiwa Waziri.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuongea na .kutoa mapendekezo kuhusu mpango huu ambao ameuleta Mheshimiwa Dkt. Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kwenda hapo, naomba niwakumbushe Wabunge kwamba jukumu letu humu ndani kama wengi wanavyosema ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Siyo jukumu letu kuonyesha Serikali haifai na kupinga pale ambapo hata haistahili kupingwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna ya kushauri na kusimamia Serikali kati ya vyama vya upinzani na chama tawala lazima ni tofauti. Nasema hivyo kwa nini?
Nimewasikiliza hamkusikia mama Nagu akisema naomba na wengine wanapoongea msikilize. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mama ukiwa na watoto nyumbani wengine wa kwako na mwingine wa kambo, yule wa kwako anapoangusha glass unasema bahati mbaya, wa kambo anapoangusha glass unasema makusudi, huo ndiyo ukweli wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utamaduni wa vyama vingi unless mnakataa jukumu la vyama vyenu, utamaduni wa vyama vingi ni upinzani kuonyesha Serikali…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Nagu hebu kaa kwanza...
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mama yao hata wakinitukana nitaosha mkono sitaukata. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba jukumu la wapinzani ni kupinga Serikali iliyo madarakani hilo linajulikana, lakini basi pingeni kwa lugha ya staha. Sisi ambao ni chama wa tawala kazi yetu ni kuisimamia, kuishauri kwa lugha ya staha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naenda kwenye Mpango wa Maendeleo, huu ni mpango wa miaka mitano wa pili ili kufikia dira ya Taifa letu. Dira ya Taifa letu inatutaka mwaka 2025 tuwe ni Taifa ambalo lina uchumi wa kati na tunatumia mipango hii na utekelezaji wake kutusogeza pale. Kwa hivyo, tulifanya tathmini ya miaka mitano ya kwanza tuliyoitekeleza na tukaona kwamba tumepiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ilikaa bila mipango kwa miaka mingi. Mimi nakumbuka kabla ya mipango hii uchumi wa nchi hii ulikuwa ni hasi mbili leo tuko asilimia sita na zaidi maana yake uchumi umepanda kwa asilimia nane. Kwa hiyo, miaka mitano ya mpango huu, mwaka wa kwanza ulitufanya tukapiga hatua na huu ninaamini utatufanya tupige hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie kwamba hakuna kazi nzuri ambayo haifanywi kwa bidii. Sisi akina mama na nitatumia mfano ambao unanihusu mimi, tunabeba mimba miezi tisa tunatapika tunaenda labor ward tukitegemea kufa na kupona. Katika mpango huu vilevile tufikirie hivyo kwamba baada ya kutekeleza tutapiga hatua. (Makofi)
Sasa nataka niseme tulivyotathmini mpango wa kwanza wa miaka hii mitano ya mpango tumepiga hatua uchumi unapanda. Hata hivyo, tunajua maeneo yanayopandisha uchumi siyo yale ambayo yanahusika na watu directly. Kwa hivyo, sasa tuangalie yale ambayo yanahusika na watu directly. Tunakubaliana kwamba azma yetu ya miaka hii mitano ni kujenga uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimkumbushe Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango kwamba hatutakuwa na viwanda bila kuwa na kilimo kinachotegemewa. Huo ndiyo ukweli wenyewe kwenye maelezo yake ya hakuongea hata kidogo juu ya kilimo. Kwanza kuongea juu ya kilimo ni kuwapa moyo Watanzania asilimia 80 wanaotegemea kilimo. Kilimo ndiyo kitatoa chakula kwa wale watakaofanya kazi viwandani, kilimo ndiyo kitakachotoa malighafi ya viwanda, tija ya kilimo ndiyo itafanya watu waondoke kwenye kilimo waende kwenye viwanda. Kwa hiyo, naomba katika mpango huu na tunapotekeleza mpango huu kupitia bajeti tuone kwamba kilimo kinapewa kipaumbele ili tufikie viwanda tunavyovitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumeamua uchumi wa viwanda lazima tuangalie ni viwanda gani ambavyo vitatusaidia. Kiwanda cha kwanza narudia tena kama walivyosema Wabunge kiwanda cha chuma ni kiwanda mama, kiwanda cha kemia ni kiwanda mama. Viwanda vile mama lazima tuvipe kipaumbele ili vituwezeshe twende kwenye viwanda vingine na tuwe na sustainable industrial development. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ndugu yangu Mheshimiwa Mpango hakikisha utekelezaji wa kiwanda cha chuma cha Liganga na mkaa wa Mchuchuma umepewa kipaumbele. Vilevile katika kuchochea kilimo hakikisha viwanda vya mbolea vinapewa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tujue kwamba siyo bajeti ya Serikali tu ndiyo itakayotekeleza mpango wetu. Kwanza naomba katika kukusanya kodi huwezi ukamkamua ng‟ombe bila ya kumlisha, lazima tutambue sekta binafsi inataka kulishwa, muone ni namna gani tutaipa nguvu na iweze kutoa kodi ya kuaminika. Kuna wale wanaokimbia kodi wale ni wachache lakini kwa ujumla sekta binafsi lazima tuiimarishe. Sekta binafsi itatusaidia kutekeleza mpango huu kupitia kilimo, kupitia viwanda na vingine vyote tulivyovipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna rahisi ni utekelezaji wa sera na Sheria ya PPP, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Naomba sana tusipuuze hili kwa sababu huu ni uchumi wa soko tumeshakubali na uchumi wa soko unategemea sekta binafsi. Nasema kwamba pengine kuna mahali ambapo tumeenda kando, naomba tuache kule tulikoenda kando mimi napendekeza kwamba tukae na sekta binafsi ijue kwamba kodi yao ndiyo itawatengenezea mazingira mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta binafsi naomba tuwe na One Stop Center effective ile ambayo ipo ni ya maneno tu. Naomba mfanyabiashara anapotaka kuandikisha biashara yake aweze kutoka na leseni na ajue aende kukopa au equity itatoka wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulisema ndugu zangu mliongea juu ya Logistic Center ya Kurasini. Logistic Center ya Kurasini tulikuwa tumepanga kwa ajili ya ku-feed Kariakoo siyo kuua Kariakoo. Bidhaa zinazouzwa Kariakoo zinatoka China, Thailand na Indonesia, Kurasini ndiyo italeta bidhaa hizo in bulk na wale wa Kariakoo watachukulia pale, hiyo ni namba moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ya pili Logistic Center itaonyesha viwanda gani ambavyo vitakuwa na faida Tanzania kwa sababu pale ndipo demand itajulikana kama ni nguo watu wanataka tukijenga kiwanda cha nguo tutapata faida, kama ni viatu tukijenga kiwanda cha viatu tutapata faida. Kwa hiyo, Logistic Center hiyo tumeshaanza kuitekeleza naomba iharakishwe kusudi tunapojenga viwanda vyetu tujue ni viwanda vipi ambavyo vinatakiwa na tusikisie viwanda vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo nataka kulisema ndugu zangu ni kwamba hii ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi lakini uongozi mpya. Uongozi mpya unapokuja kwa vyovyote watu hawatakuwa na uhakika; na mfanyabiashara anataka awe na uhakika; kabla hajawa na uhakika yanayotokea ndiyo yanatokea. Pale ambapo tutawahakikishia uchumi wao wafanyabiashara watarudi na mimi nina hakika nchi hii baada ya hapo itakuwa steady hatuna sababu ya kuogopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudia tena uchumi huu ambao tunaujenga lazima uwe na uhusiano wa watu na ndiyo maana kama Mheshimiwa Mpango atakumbuka nilimwambia tuandike maendeleo ya watu ili isiwe maendeleo ya vitu tu. Tunavyopiga hatua tunataka maisha ya watu yawe bora zaidi, tunataka uchumi wa nchi uwe bora lakini ubora wake utokane na watu kusema kwamba tuna nyumba bora, tuna dawa za kutosha, tuna nguo za kutosha hii ndiyo itakayofanya mpango huu uwe mpango wa maendeleo ya watu na si maendeleo ya vitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ili wengi wapate nafasi na ninaombeni pingeni, tusimamie na tushauri lakini wote wawili tutumie lugha iliyo na staha na tutajenga heshima ya Bunge hili kwa upande wa upinzani na upande wa chama tawala mimi sina wasiwasi, ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi niseme kutoka awali kwamba naunga mkono taarifa za Kamati zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda halina mjadala, Bunge lako Tukufu hili limekubali kama Serikali inavyotaka kwamba ili tufike nchi yenye kipato cha kati ni lazima tupitie kwenye viwanda. Lakini nataka niwambie kwamba kama tunataka tufaulu kwenye viwanda lazima tuwe na uwezo wa ushindani kwa sababu bidhaa za viwanda zitashindana na bidhaa za nchi nyingine.
Kwa hiyo, nataka niwaeleze wale waliokuwa wanataka viwanda vya miaka ya 1960 na 1970 vifufuliwe, inaweza ikawa hasara kwetu kwa sababu uwezo wa ushindani utakuwa mdogo, ila tutake viwanda vipya vya korosho na sehemu zingine vianzishwe. Tusipoangalia hilo tutajiingiza na mimi nafurahi sana Serikali hii ya Awamu ya Tano inalijua hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka niseme jambo moja ambalo lilishaanzishwa na sisi tusipolipeleka mbele tunaweza tukajirudisha nyuma. Kupitia SIDO na Wizara ya Viwanda kulikuwa na mradi wa MUVI ambao unajua kila Wilaya inaweza ikawa na viwanda vipi ili tuwe na uwezo wa kubadilishana ndani ya nchi ambamo viwanda vingi ni vya kuchakata mazao ya kilimo katika kuongezea thamani.
Kwa hiyo, naomba mradi huu wa MUVI muuangalie upya kusudi kusiwe na Wilaya ambayo haina viwanda, ama sivyo tutaifanya nchi iwe na sehemu nyingine ina viwanda, sehemu nyingine haina viwanda halafu wengine wakawa nyuma na wengine wakawa wamepiga hatua. Kwa hiyo, naomba sana, hili liangaliwe, tuwe na nchi ambayo ina uwezo wa kuwa na viwanda nchi nzima na kwa kuangalia kwamba kila Wilaya ina-specialize kwanza issue ya division of labour na specialization lazima iangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, mimi nataka kusema habari ya mikataba. Mikataba ya nchi hii imetayarishwa na wataalam na wataalam ni binadamu. Inawezekana kwamba kuna maeneo yamekosewa, lakini sidhani kama mikataba yote ni mibaya kiasi hicho. Kwa hiyo tuwe watu wa kuangalia mikataba ipi inaupungufu na mikataba ipi ambayo ni mizuri iendelezwe na ile ambayo ina upungufu iweze kuangaliwa na kuboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema kwamba tuhakikishe kweli viwanda vinafanikiwa. Ili viwanda vifanikiwe kuna kitu kinaitwa basic industries au viwanda mama. Viwanda vya chuma, viwanda vya chemicals, viwanda ambavyo vinaweza vikafanya vingine vikazaliwa na vikaendelea kuzaliwa. Tusipofanya hivi tunaweza tukaanzisha viwanda ambavyo havitasonga mbele. Kwa hiyo haya yote tuyaangalie na suala la uwekezaji lazima tulitilie mkazo. Watu wasipowekeza ndani ya nchi, nchi itatawaliwa na watu wengine wa nje. Tulianzisha forum ya uchumi katika kila mkoa, naomba Waziri uendeleze zile forums ili kila mkoa ujue kwamba wanaweza kuwekeza sehemu gani ili nchi yetu iwe na maendeleo sawia kwa kila mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, mchango wa Sekta ya Kilimo ni mkubwa na muhimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, 30% ya Pato la Taifa; 30% ya bidhaa zinazouzwa nje; 65% ya malighafi za viwanda; 65.5% ya ajira; na 100% ya chakula kudhibiti mfumuko wa bei. Hivyo kilimo ni muhimu katika kuifikisha Tanzania yetu kwenye Dira ya Tanzania ya 2025 kuwa na uchumi wa kati, Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, ikiwa hivyo ndivyo ilivyo, inabidi kuimarisha kilimo na upatikanaji wa chakula uwe na uhakika. Namna ya kuimarisha kilimo kwa kufanya utafiti wa kweli wa udongo, mazao na teknolojia sahihi ili kuwa na masoko ya uhakika na kuwa na bei ambayo inafanya wakulima wapate faida ya kukuza kilimo.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kilimo kinakuwa kwa 3.1%; Malaba ilitaka kilimo kikue kwa 6% na uwekezaji wenye kilimo ufikie 10% ya Pato la Taifa. Sasa uwekezaji kwenye kilimo ni chini ya 5%, Serikali isaidie. Tatu, wakulima wanahitaji Wagani kwa kila kijiji watosheleze mahitaji yao. Sasa hivi kuna vijiji vingine havina Wagani, naomba Serikali Wagani wote waliofuzu waajiriwe kuongeza nguvu ya wakulima ya kuzalisha mazao.

Mheshimiwa Spika, nne, kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna. Sasa upotevu wa mazao unafikia kati ya 30% - 40%. Hii inawaletea wakulima hasara na hata Taifa. Najua Serikali inajitahidi kupunguza upotevu lakini bado jitihada inatakiwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, tano, suala muhimu ni kuimarisha na kuongeza miundombinu ya umwagiliaji kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Hanang iliomba kujengewa bwawa la Gidahababieg. Tumeomba bwawa hili ili kusaidia eneo la Gidahababieg kupata fursa ya kulima kwani ni eneo lenye uhaba wa mvua. Vilevile, bwawa hili linajengwa katika eneo ambalo maji yote ya mvua kutoka Mlima Hanang yangekusanywa. Huu ni mwaka wa kumi toka watu wa Hanang kupitia kwa Mbunge wameomba kujengewa bwawa. Nataka kujua kwa nini tumecheleweshewa bila kupata maelezo ya kuchelewesha ujenzi wa bwawa hili, itabidi nitoe shilingi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii ya awali kabisa kukushukuru kwa dhati kabisa kwa kunipa nafasi ya mwanzo jioni ya leo ili kujadili hoja ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijafika huko, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia na wewe Mheshimiwa Naibu Spika, kuwapa pole wale wote waliofiwa na wanafunzi wa shule ya St. Vincent na wengine wote waliopata ajali kwenye maafa mbalimbali na kufariki. Mwenyezi Mungu alaze roho zao mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naupongeza sana uongozi wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania kwa kutambua umuhimu na unyeti wa Sekta ya Maji na kuipangia Sekta hii siku tatu za majadiliano. Naomba Waheshimiwa Wabunge wasirudi nyuma kutumia siku hizi tatu kuijengea hoja ili Mheshimiwa Rais wetu mwema aweze kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vile vile kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali kusikiliza ushauri wa Wabunge wetu. Vile vile kwa kututeulia Waziri Lwenge na Naibu Waziri Kamwelwe ambao ni mahiri sana katika kuongoza Wizara hii pamoja na watendaji wote; na Mungu awape afya njema waweze kusikiliza wanayosema Wabunge na watekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwamini sana Mheshimiwa Rais na nampongeza sana. Naisihi Serikali yake kuona kwamba inapokea kilio cha Wabunge kuhusu Bajeti ya Maji kwa sababu maji ni uhai na usafi wa mazingira ni utu wa binadamu. Hivyo sina shaka changamoto nitakazozitoa hapa zitachukuliwa na kufanyiwa kazi kwa kuzitolea uamuzi kwa manufaa ya Taifa letu na wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya 2016/2017 iliyotengwa ilikuwa sh. 939,631,302,771 na kati ya hizo fedha zilizotengwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ni sh. 915,193,937,771. Hata hivyo, fedha zilizotolewa kwa Miradi ya Maendeleo mpaka Machi mwaka 2017 ni sh. 181,209,313,609 sawa na asilimia 19 peke yake. Mbaya zaidi Bajeti ya Mwaka huu wa 2017/2018, iliyotengwa ni sh. 623,606,748,052 ambayo ni ndogo ukilinganisha na mwaka uliopita lakini mahitaji ya maji yameongezeka, population nayo imeongezeka, mahitaji ya viwanda yameongezeka na mahitaji ya jumla ya maendeleo yameongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, kwa sababu mwenendo huu unasikitisha na utawasikitisha Watanzania, naomba Serikali bajeti yetu irudi kama ilivyokuwa mwaka jana ili kuona kwamba ndoo hii ambayo mwanamke ameteseka nayo kwa muda mrefu inatua kutoka kwenye kichwa chake. Naomba bajeti hii iongezeke kama ilivyokuwa bajeti ya mwaka jana. Maji ni uhai narudia tena na usafi wa mazingira ni utu. Bila maji hakuna maendeleo, bila maji hakuna uhai, bila maji jamani viwanda hivyo tunavyovisema haviwezi kuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ili tuwe na uhakika wa kutekeleza miradi ya maji na maendeleo ya maji ambayo matokeo yake ni maji kupatikana, naomba sana kama tulivyoomba mwaka jana na Kamati yangu imerudia mwaka huu kwamba Mfuko ule wa Maji unaochangiwa sh. 50 kwa kila lita ya diesel na petrol uongezewe sh. 50 ili iwe sh100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Serikali yenyewe iliahidi kuifanyia kazi. Nina hakika kwa mwaka mmoja hiyo kazi itakuwa imefanyika na naomba mwaka huu tufanye hivyo hasa tukizingatia bajeti yenyewe inayotengwa huwa haitolewi na fedha hizi zitasaidia sana miradi ya maji iende kwa kasi zaidi. Ukiangalia mpaka mwisho wa mwezi Machi, 2017 utaona kwamba hela iliyotolewa ni kidogo sana. Nchi hii inakabiliwa na njaa na inakabiliwa na ukame, hakuna kitu ambacho kitai-rescue au itasaidia nchi hii kama miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuone kwamba fedha zinazotengwa kwenye umwagiliaji zitasaidia kuongezeka kwa uhakika wa chakula, uhakika wa kupata mazao ya biashara unaongezeka. Kwa hiyo, naomba Tume ya Umwagiliaji nayo iangaliwe kwa jicho la huruma na kuongezewa fedha ili nchi hii iwe na uhakika wa chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeshukuru sana kuona kwamba katika bajeti hii, bwawa ambalo nimeliomba kwa miaka saba lingelijitokeza lakini sikuona na nimekuwa nikiomba kila mwaka hata pale ambapo nipo kwenye Sekta hiyo ya Maji, bwawa la Gidahababiel halikuonekana na nasema naipenda sana Serikali, naiamini sana lakini kwa bwawa hili la Gidahababiel nitatoa shilingi kwa sababu watu wa Hanang hawawezi kuelewa hili, wataniona naimba tu halafu Serikali haichukui hatua yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mjue kwamba bwawa hili lilikuwepo toka wakati wa ukoloni lakini likapasuka wakati wa el-nino. Mpaka leo hakuna ambaye amelihangaikia bwawa hili. Namuomba Waziri na Watendaji wake waone umuhimu wa bwawa hili. Sisi tuko kwenye bonde la ufa na wilaya ambazo ziko kwenye bonde la ufa zina matatizo makubwa sana ya maji. Hanang ikiwa moja ya Wilaya ya Bonde la Ufa haina maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile zaidi ya bwawa la Gidahababiel naomba visima vile ambavyo tumeviomba viweze kuchimbwa ili wananchi wa Hanang waweze kupata maji. Mpaka hapa tulipo wananchi wanaopata maji kwenye Wilaya ya Hanang nafikiri ni asilimia 46, na sisi ni wilaya ya mifugo. Wananchi wa Hanang wamehama wilaya ile kutokana na ukame na kwenda wilaya zingine na kutoa adha kwa watu wengine. Naomba sana, wale waliobaki na mifugo, wasihame, wabakie Wilaya ya Hanang kwa kuhakikisha kwamba mabwawa na visima vinachimbwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo naomba vile vile katika kuimarisha Sekta ya Maji, tunaomba kuwe na maafisa wa kutosha wa maji, wahandisi wenye uwezo wa kukabiliana na tatizo la ukame. Sasa hivi tuna wahandisi wachache, Wilaya ya Hanang ilikuwa na wahandisi wazuri, wamehamishwa, basi na mimi ningeomba TAMISEMI ione umuhimu wa kuwaleta wahandisi imara ambao watakabiliana na tatizo hilo ambalo ni kubwa katika wilaya yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge waone umuhimu wa kuongeza bajeti ya maji iwe angalau kama ile ya mwaka jana. Naomba Waheshimiwa Wabunge waunge mkono hoja ya kuongeza sh. 50 kwa kila lita ya diesel na petrol ili mfuko wa maji uwe na fedha za kutosha kutekeleza miradi mbalimbali. Tukifanya hivyo, Mheshimiwa Rais wetu atakuwa na uwezo, na ana upendo mkubwa sana na wananchi wake wa kutua ndoo kwenye kichwa cha akinamama ambao ndio wanapata adha kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nishukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono Bajeti hii ya Sekta ya Maji au ya Wizara ya Maji kwa moyo wangu wote, lakini yale niliyoyasema myazingatie na wakati wa kutoa majibu myatolee majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kwa mara ya pili kujadili bajeti hii ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishatoa pole kwa wale ambao walifiwa kwenye maafa mbalimbali hivyo naomba niende moja kwa moja kwenye hoja hii ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda ni lazima kwa ustawi wa wananchi wa nchi yoyote. Ninasema hivi kwa sababu viwanda na kilimo kwa pamoja ndivyo vinavyosaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo yake, huo ndio ukweli. Kwa hiyo, kama nchi haisisitizi viwanda na kilimo hakitaendelea kwa sababu kilimo kwa kiasi kikubwa kinasaidiana sana na viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuipongeza Serikali na siipongezi tu kwa maneno na kwa vitendo kwa sababu sekta hii imekuwa kwa asilimia 7.8 ukilinganisha na ukuaji wake mwaka uliopita wa asilimia 6.5, na imekuwa ikikuwa hivi wakati zamani ukuaji wa viwanda ulikuwa chini. Ukuaji huu umetokana na sera nzuri ambayo kuna wengine walisema imekaa muda mrefu, Sera ya Maendeleo (Sustainable Industrial Development) ya mwaka 1996 mpaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri wa sera ni kukaa muda wa kutosha ili muda wa utekelezaji uwe unatosheleza. Kwa hivyo, ninaomba niipongeze wizara hii kwa kuendelea kutekeleza sera hii ambayo kwa kiasi kikubwa inataka viwanda visambae nchi nzima na vifike hata kule pembezoni ili maendeleo ya nchi yawe na uwiano mzuri. Kwa hivyo, ni sera nzuri ninaomba tuendelee kuitekeleza, na mwaka 2020 utakapofika tutaifanyia kazi changamoto ili tuboreshe sera nyingine itakayofuata.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kutokana na sera hii SIDO imekuwa na program inayoitwa MUVI ambapo imetaka kila mkoa uwe na viwanda ambavyo una malighafi yake na ili uwiano wa maendeleo kwenye mikoa yetu iweze kufanana. Hii programu karibu itakwisha. Ninaomba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ijiandae baada ya MUVI kutakuwa na nini? Kwa sababu mwenendo na mwelekeo wa MUVI ni mzuri sana. Unapokuwa na specialization kwa kila mkoa unawezesha kuwe na biashara kutoka mkoa hadi mkoa, na ndiyo baishara ya ndani itakavyokuwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nitoe mfano kwa Wilaya yangu ya Hanang ambapo ilipangiwa kutengeneza kuwa na viwanda vidogo vya ngozi kwa sababu sisi ni wafugaji na mazao mengine yanayotokana na mifugo na Singida imepewa specialization ya mafuta ya alizeti kwa sababu inalima alizeti. Kwa hiyo, watu wa Singida watakuja kununua bidhaa za ngozi kwetu na sisi tunanunua mafuta kule. Tukiwa na utaratibu wa namna hii nchi nzima tutaendelea na maendeleo yatakuwa na uwiano mzuri, hakutakuwa na mahali ambapo patabaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba MUVI ifuatiliwe ili muda wake utakapokwisha tuwe na programu nyingine nzuri, na tumeifanya program; mimi nasema hivyo kwa sababu nilikuwa Wizara ya Viwanda; ili muda wake usiishe, huu si mradi ni programu na programu haina mwisho wake. Kwa hivyo ndugu zangu ninaomba sana tufanye hivyo ili tuongeze ajira kwa watu wetu, ili tuongeze mauzo ya nje. Nilipokuwa Wizara ya Viwanda tulikazana, kuna miaka miwili tulipita mauzo ya kwenda Kenya kuliko ununuzi wa bidhaa kutoka Kenya, inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mtajitahidi kutekeleza sera hii ya sustainable Industrial Development tutafika pazuri na hata tutaipita hii Kenya kwa sababu sisi tuna resources au maliasili nyingi kuliko hiyo Kenya ambayo inatupita kwa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili viwanda vilete manufaa nchini lazima tuwe na uwiano mzuri. Kwa sasa hivi kwa mujibu wa hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri viwanda vidogo sana ni asilimi 85, viwanda vidogo asilimia 14, viwanda vya kati asilimia 0.35, viwanda vikubwa asilimia 0.5 uwiano huuu si mzuri. Tunataka tuwe na uwiano mzuri wa viwanda vidogo kuwa vingi kama asilimi 65; vya kati vifuate na vikubwa hata vikiwa asilimia 5 haitakuwa mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwiano huu utatusaidia sana kuona kwamba malighafi zinatumika vya kutosha, itatufanya tuone kwamba mazao ya kilimo yanapata masoko kwa sababu viwanda ndio soko la uhakika la mazao ya kilimo. Vilevile itaajiri wananchi wengi. Hata hivyo ajira imeongezeka. Mwaka 2016 viwanda viliajiri watu 146,892 ukilinganisha na mwaka jana ambapo 139,000 waliajiriwa, kwa hivyo, trend ni kukua lakini ajira hii haitoshi na ndio maana nasisitiza umuhimu wa uwiano wa viwanda.

Ninaomba niongelee kidogo Kurasini Logistic Center, sijui mtakuwa mmefika wapi jamani. Tulianzisha Logistic Center ya Kurasini ili tuweze kuagiza vitu kwa bulk purchases na wafanyabiashara wa Kongo, Rwanda waje pale ili Kariakoo iwe Hong Kong ya Afrika, hilo ni moja. Hata hivyo kuna watu wanaogopa kwamba tutakuwa tunaagiza vitu kutoka China. Kutokana na Logistic Center tutajua mahitaji ya watu na nchi ambazo zinazunguka Tanzania na viwanda vitaanzishwa kwa haraka sana.

Kwa hiyo naomba sana Logistic Center ianze. Vilevile nataka tuongeze mauzo kwenda nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini ninaomba Liganga ni kiwanda mama tukisisitize kianzishwe. Ninaunga mkono na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu anafanya kazi nzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru, kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watendaji wao wote kwa kazi nzuri waliyoifanya. Naomba niende moja kwa moja kwenye kuchangia Wizara hii ambayo ni muhimu kwa watu wote; siyo hata kwa asilimia kiasi gani, ni kwa watu wote. Asilimia 75 inatoa ajira, asilimia 100 yote inatoa chakula, inatoa malighafi kwenye viwanda na inachangia pato la Taifa kwa 28%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wote kwa pamoja kama tulivyoonesha toka juzi kwamba sekta hii ni sekta muhimu na tuombe Serikali ione umuhimu wake kwa kujali kuiongezea bajeti, hata kama siyo mwaka huu, basi miaka inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia utaona kilimo kinashuka, hakipandi. Ndiyo maana umaskini wa watu unaongezeka ndugu zangu. Mwaka 2011 kilimo kilikua kwa 3.5%, mwaka 2016 kilimo kilikua kwa 1.7%. Angalieni kutoka 3.5% mpaka 1.7% na bado tunategemea kuondoa umaskini wa Tanzania itakuwa ni kazi ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kilimo kimechangia 28% katika pato la Taifa. Bajeti ya kilimo kwa mwaka 2011 ilikuwa 7.8% ya bajeti ya Serikali. Mwaka 2016 bajeti ya kilimo imepangiwa 4.9%. Kwa hiyo, muone uhusiano kati ya ukuaji wa kilimo na jinsi bajeti inavyotolewa. Kwa hiyo, naomba Waziri aone na Serikali nzima ione kwamba namna pekee ya kukuza sekta hii ni kuiongezea bajeti yake na kujielekeza kwenye changamoto ambazo zinakabili sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kuona kwamba, namna moja ya kukabiliana na changamoto ni kuwa na ununuzi wa pamoja wa pembejeo na hususan mbolea. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumeisaidia sana, lakini naomba sana mbolea hii ifike kwa wakulima na wapate manufaa ya ununuzi wa pamoja, isiishie hapa katikati kwa sababu kuna hatari ya manufaa haya kwenda kwa wafanyabiashara badala ya wakulima na hivyo isiwe na impact kwenye kilimo chenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee kwa muda uliobaki juu ya mifugo. Mimi ni mtoto wa wafugaji, lakini vilevile wafugaji ambao wanalima. Kwa hiyo, sina sababu ya kupendelea upande mmoja, ila ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Serikali tuone kwamba mifugo ni mali ya watu mmoja mmoja, lakini ni rasilimali ya Taifa. Mifugo kweli ni mali ya mtu mmoja mmoja lakini ni rasilimali ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi zimepangiwa maeneo na yanajulikana. Kilimo kinajulikana kwa sababu mazao yako shambani, lakini mpaka leo maeneo ya wafugaji hayajulikani, wao wanahangaika nchi nzima. Ninaomba sana, mipango na matumizi ya ardhi ndiyo namna pekee ya kuondoa migogoro na hifadhi na wakulima na watumiaji wengine na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba kwa maisha yao wafugaji wanategemea mifugo hiyo, kunapokuwa hakuna majani wanatafuta. Mipaka ya hifadhi wakati mwingine haijulikani, kwa hiyo, ng’ombe wanaingizwa kwenye hifadhi labda kwa bahati mbaya, siyo kwa sababu watu wanataka kuvunja sheria. Kwa hiyo, wanapokutwa ng’ombe kule, wanapokamatwa na wanapoadhibiwa wafugaji, wakiamua kwamba ng’ombe warudi, ni lazima warudi wamepungua. Hii ni sawa na ni haki jamani? Naomba tuwasaidie wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba, kunapokuwa na ukame, kwanza bei ya mifugo inashuka, lakini na ng’ombe wanahitaji maji na mito itakuwa kwenye hifadhi. Tunafanya nini? Badala ya kungojea kuwaadhibu wafugaji, naomba tujielekeze katika namna ya kuweza kutatua matatizo yao kwa kuwa na mabwawa na miundombinu ambayo itasaidia wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili kwamba vilevile kunapokuwa na migogoro, wafugaji wanapoenda Mahakamani, pamoja na kwamba watu watalia kwamba kuna rushwa, lakini wanaposhinda basi, ama wale wanaoshindwa, wakate rufaa, lakini wasiamue kuwatesa wafugaji kwa kuwanyima ng’ombe wao au kuwauza. Hata sasa hivi, najua hifadhi zina sheria kali, lakini tuone hali yenyewe ya nchi ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tuone kilio cha wafugaji; wafugaji ni Watanzania, wana rasilimali ya Taifa, wanalinda mali ya Taifa kwa sababu Tanzania ni ya tatu katika ufugaji Afrika. Manufaa ya wafugaji hayaonekani, siyo kwa sababu tu ndugu zangu wanahamahama au wanachunga badala ya kufuga, ni kwa sababu, wanahitaji elimu, wanahitaji miundombinu na kuzijua sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye alama au chapa ya ng’ombe. Naelewa kwamba ufuatiliaji wa mifugo (traceability) ni muhimu sana, lakini naomba tuwaelimishe wafugaji. Vilevile unapoandikisha ng’ombe wako Gairo, kama hakuna maji, hivi watabakije pale? Lazima wahame, kwa hiyo, wafugaji wanaona mkiwachapa ng’ombe, ni kwamba sasa mnawa-condemn wale ng’ombe kufa yatakapotokea matatizo ya ufugaji, kama ukame au magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana, wakati tunachapa ng’ombe, ili traceability iwe rahisi, tuhakikishe na miundombinu ipo; ili wananchi waone manufaa. Wafugaji nao waelewe kwamba ng’ombe wanavyoweza kufuatiliwa, soko la dunia inakuwa rahisi kulipata. Kama hakuna namna ya kufuatilia, Soko la Dunia linakuwa na wasiwasi. Kwa hali ilivyo sasa hivi, tunakazania kuchapa ng’ombe, lakini hatukazanii kuunda miondombinu kuweza kuwasaidia wafugaji na changamoto ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo juu ya uvuvi na Mheshimiwa Waziri anatoka kule kwenye uvuvi. Jamani ni Tanzania tu ambapo uvuvi haramu umeenea. Ninaomba tuchukue hatua ambazo zinatakiwa ili huu uvuvi haramu uweze kwisha. Wavuvi vilevile waelimishwe waone umuhimu wa kutumia nyenzo zile ambazo zinatakiwa katika uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaiangalia sekta hii vizuri, Tanzania itaondokana na umaskini na itafika kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda. Bila kilimo kutengemaa, viwanda havitawezekana nawaambia. Wafanyakazi wa viwandani watakuwa wanakula nini kama hakuna kilimo nchi hii? Tutakuwa tunaagiza nje. Malighafi zitatoka kule, kama hakuna kilimo, viwanda vitakuwaje imara? Kama viwanda vya Tanzania havitahusishwa na kilimo, maana yake tutakuwa hatuna utengamavu kwa sababu, tunachotaka tuwe na uchumi ambao unapanda kupitia kuongeza thamani ya mazao ambayo Watanzania wengi ndio wanayategemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nilikuwa nafikiri nitachelewa kutoka Dar es Salaam, nimewahi. Naomba Wabunge wote tuone umuhimu wa kilimo, ufugaji na uvuvi kusudi nchi yetu iendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wafugaji waangaliwe kwa macho ya huruma badala ya kuwafunga au kuchukua ng’ombe zao na bila kuona kwamba pengine siyo makusudi. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi hii ili nami nipate kuchangia bajeti hii ya Serikali. Nianze kabisa kwa sababu muda ukiisha unaweza hata ukasahau kuunga mkono bajeti hii au hoja ya Waziri wa Fedha, kwa hiyo, nasema kutoka mwanzo naiunga kwa nguvu zote hoja hii ya Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuungana na Wabunge wenzangu kumpongeza na kumshukuru sana na kumuombea Mwenyezi Mungu Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa ujasiri wake huo aliouonyesha kuhusu suala la makinikia na kuibua ukweli wa uwekezaji wa kinyonyaji na uovu unaotudidimiza badala ya kutuondolea umaskini na udhalili. Rais amefanya jambo kubwa na kwa kweli hajajifanyia mwenyewe amewafanyia Watanzania. Kwa hiyo, sisi wote tumuunge mkono, tumsaidie na tuone kwamba hii economic order ya dunia inapokuja kwenye nchi yetu lazima kuwe na watu ambao wanajitolea na lazima iingie kwenye vitabu vya historia kwamba Mheshimiwa Magufuli amesaidia sana katika kuondoa economic order ya kinyonyaji. Tukifaulu hapa tujue nchi hii itakuwa imechangia mchango mkubwa sana katika uchumi wa dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima kama alivyoelekeza litakuwa kwenye sera na kwenye sheria tutakavyoziangalia hapa Bungeni. Wote ambao ni wataalamu tuziangalie kwa uzuri ili kazi hii aliyoifanya ilete manufaa kama yeye alivyokuwa anategemea. Mwenyezi Mungu atampa yeye na sisi nguvu tuwe pamoja kuona kwamba madini ambayo Mwenyezi Mungu ametupa yanaleta manufaa katika nchi yetu na kuendeleza nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu wake Mkuu na watendaji wote kwa kuikalia bajeti hii. Bajeti hii imefanyiwa kazi, ina ubunifu mkubwa, imesikiliza kilio chetu ambacho kimetokana na wananchi, nawapongeza sana. Haitoshi kuwa na bajeti bali utekelezaji ndiyo utakaoleta maana kubwa. Naomba tutekeleze bajeti hii na kule kwenye Halmashauri kama ushuru hautatozwa hovyo hovyo, nawaambia kilimo, ufugaji, uvuvi utaendelea na huduma mbalimbali zitapatikana bila shida. Kwa hivyo, suala la usimamizi lazima lipewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ione umuhimu wa kilimo, ufugaji na uvuvi. Wenyewe ndiyo waliotuambia kwamba kilimo kinachangia asilimia 29.1 na viwanda vinachangia asilimia 25 na uchangiaji wake unapanda, lakini kilimo ukuaji wake unashuka na ni wao wenyewe ndiyo wameandika. Naomba tu reverse hii trend ya ukuaji wa kilimo kwenda chini kwa sababu mchango hautaongezeka kwenye Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, ili kilimo kiendelee tuhakikishe kwamba bajeti ya kilimo inayotengwa basi itolewe kwa wakati. Ukienda ukasaidia wakulima kupata mbegu wakati msimu wa kupanda umepita hujasaidia wakulima. Wakulima wakitaka pembejeo wakati ukifika lakini hawapati hawatafaidika. Naomba sana tuangalie ni wakati gani tunafanya mambo yote haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia madini yanakua kwa asilimia 13, uchukuzi na mawasiliano unakuwa kwa asilimia kubwa sana, lakini ukiangalia mchango wao kwenye pato la Serikali ni mdogo sana. Hicho ndiyo kielelezo kwa nini umaskini wa Tanzania haupungui kwa sababu kule kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo kwa kiasi kikubwa ndipo walipo wananchi wote wa Tanzania hakujapewa uzito. Kwa hiyo, Watanzania hawataondokana na umaskini kama hatutawakazania. Naomba sana hili mlitambue, mmetuonyesha wenyewe kwenye takwimu. Kwa hiyo, naomba sana muone kwamba ili kuondokana na matatizo ya wakulima, kwanza tuhakikishe kwamba wanapata pembejeo, huduma za ugani, masoko na wanapata viatilifu kwa wakati ili mazao yao yasiliwe na wadudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kitu kimoja, kilimo na ufugaji hautaendelea kama migogoro ya wakulima na wafugaji itaendelea. Nataka niwaambie kwamba hifadhi zinajulikana narudia, kilimo mahali wanapolima panajulikana kwa sababu mazao yanaonekana, wafugaji hawaoni maeneo yao kwa sababu ng’ombe akirudi nyumbani, hamtajua kwamba hilo ndiyo eneo la wafugaji. Naomba mtenge bajeti ya kwenda kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima nao hawatapata hasara kwa sababu kama wafugaji wanajua maeneo yao katika kila Wilaya, hawatakuwa na sababu ya kupeleka ng’ombe kwenye mashamba ya watu, hawatakuwa na sababu ya kupeleka mifugo kwenye hifadhi, naombeni sana mfanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niongelee habari ya maji, akina mama ndiyo wanaolima mashambani, wakitumia masaa mengi kutafuta maji maana yake muda wa kuwa shambani unapungua. Naomba ile tozo ya shilingi 50 iende kwenye suala la maji. Nampongeza Mheshimiwa Waziri ameonyesha maeneo ambayo yanaongeza bajeti ya maji lakini sehemu hiyo sio ya uhakika. Kama Mfuko wa Maji ukipata tozo hizi kutoka kwenye mafuta au mahala pengine mtakapoamua, tutakuwa na uhakika wa bajeti ya maji na maji ndiyo uhai kama alivyokuwa amesema Mbunge aliyetangulia kuongea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile kuongelea ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini. Ndugu zangu wananchi wamejitolea kujenga madarasa, zahanati mpaka kwenye lenta na vituo vya afya. Serikali ione basi pale ambapo wananchi wamechangia na yenyewe ichangie. Mahitaji ni mengi, vipaumbele mkiviweka sawasawa, nina hakika bajeti hii itakuwa mkombozi wa Mtanzania na tutaendelea kuona manufaa na umasikini utaendelea kutoweka. Mheshimiwa Waziri utaweka historia kama bajeti hii itatekelezwa. Mheshimiwa Waziri tutaona ulivyotumia nguvu yako kama bajeti itakwenda ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyopita ilitoka kwa sehemu ndogo sana, umeeleza na tumeelewa hatuna ugomvi na wewe lakini sasa hivi kazana na ukusanyaji wa kodi. Hakuna mtu ambaye atakuwa na hiari ya kulipa kodi. Kuna maeneo ambayo tukiyasahihisha kodi itaongezeka na mapato ya Serikali yataongezeka. Kule ambako mmeondoa hizi tozo za ushuru mpeleke nguvu zenu kama kwenye madini, utalii na maeneo ambayo kuna fedha. Tukifanya hivyo ndugu zangu tutakuwa tumejielekeza na tutakuwa na mkakati mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tuwe wamoja wakati huu wa vita, vita inataka umoja na mshikamono, vita inataka umakini mkubwa. Msifikiri hao watu watakuwa tayari kurudisha hayo ambayo wametaka kuyachukua, watatudanganya danganya na sisi tuone wapi tunadanganywa. Naomba suala hili la makinikia tulishughulikie wote, Rais ameshaonyesha njia, wataalam na wananchi kwa pamoja na ikiwezekana nchi nzima irindime kuwa na maandamano ili dunia nzima ione kwamba Tanzania ina watu wajasiri wakiongozwa na Rais wao anayepita kwa ujasiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana kunipa nafasi hii na Mwenyezi Mungu ambariki Rais wetu, Mwenyezi Mungu ambariki Waziri wetu wa Fedha na Naibu wake na Naibu wake na Watendaji wao na Mwenyezi Mungu abariki Bunge hili na naomba bajeti hii iweze kutekelezeka. Narudia tena, naunga mkono kwa nguvu zote bajeti hii na kwa moyo mmoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. DKT. MARY M. NAGU - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kutoa majumuisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri naanza ili dakika zangu zisipotee.

Naomba nichukue nafasi hii ya awali kabisa kukushukuru wewe kwa kuendesha majadiliano hapa Bungeni kwa umahiri mkubwa. Nawashukuru sana Wabunge kwa kujadili na kushauri na kuonesha maeneo ambayo yalikuwa na sababu ya kuyaonesha ili Serikali iweze kuyachukulia hatua na kutekeleza ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Wabunge wa Kamati yetu kwa ajili ya kufanya kazi nzuri na ninyi wote mmeshuhudia kwamba hakuna jambo jipya ila mlisisitiza zaidi yale yote yaliyokuwa kwenye taarifa ya Kamati yetu, ninawashukuru na kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge waunge mkono mambo mengi ambayo tumeyaongelea kwa sababu kwa kweli ni muhimu sana, na Wabunge wengi wamejadili kwa kuongea na maandishi, jumla yao imefika 51 katika muda mfupi huu, ninawapongeza sana na kuwashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru vilevile Mawaziri wanaoongoza sekta hii kwa kujitahidi sana kutoa na wao majibu au kuelezea mambo ambayo wameyatekeleza ninaomba wazingatie yale yote ambayo yametiliwa mkazo na Waheshimiwa Wabunge wote. Ninawashukuru kwa kuchangia hoja na kusisitiza zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana kuona matatizo yaliyoonekana Lake Victoria au Ziwa Victoria katika kuona kwamba Waziri kuhangaika na wenzake kuona kwamba wanajaribu kudhibiti uvuvi haramu, lakini ninaomba wachukue jitihada ambazo zitaondoa uvuvi haramu bila kukandamiza wavuvi. Vilevile jitihada zinazochukuliwa ziondoe uvuvi haramu ili tusiendelee na hayo mambo ambayo yanaumiza watu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo sikuweza kuliongelea pale kwenye taarifa lakini ipo ni kwamba Ziwa Victoria siyo la Tanzania tu ingawa sehemu kubwa ipo kwetu ni ziwa ambalo kuna nchi tatu ambazo zinazunguka, tusichukue hatua ya kunufaisha nchi zingine na kuinyima manufaa Tanzania. Vilevile nafikiri kwa sababu kuna malalamiko mengi kama walivyoomba Waheshimiwa Wabunge tuunde tume ili tuondoe malalamiko hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni migogoro ya watumiaji wa ardhi. Mheshimiwa Lukuvi alisema kwamba tume iliundwa ya Mheshimwa Sendeka, ilikuwa zaidi kati ya wafugaji na wakulima. Lakini malalamiko ya safari hii ni zaidi ya wafugaji na Hfadhi za Taifa, ninaomba kama tulivyoomba awali kwamba tuunde Tume ili migogoro hii vilevile iweze kuondoka na malalamiko yaondoke. Ninaomba Bunge liweze kuunga mkono hayo ili migogoro hii isiendelee na malalamiko ya wananchi yawe yametumika kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la pembejeo, Waheshimiwa Wabunge bila pembejeo hakuna kilimo na hakuna tija, kwa hivyo Mheshimwa Waziri na Serikali tunaomba sana hatua mliochukua Wajumbe wa Kamati waliwaungeni mkono na Wabunge waliwaunga mkono, lakini mmeona changamoto zilizojitokeza, naomba mzitathmini, msimamie na mratibu ili kudhibiti usambazaji na upatikaji wa wakati wa pembejeo. Serikali isipofanya hivyo kilimo kitazidi kudidimia.

Lakini vilevile kuna issue ya wadudu waharibifu, tusipochukua hatua haraka mazao yatakuwa hayapo na umaskini utazidi kuingia Tanzania. Kwa hiyo, naomba sana hatua ya haraka kwa upande wa Serikali na wale wote wanaohusika kuona kwamba dawa zinapatikana au viatilifu vinapatikana ili kunusuru kuingia kwenye janga la Taifa la mazao ya kilimo. (Makofi)

Kuhusu masoko ya mazao, soko la uhakika na bei ya mazao lenye faida ni kichocheo cha uzalishaji wa mazao ya kilimo. Serikali iwe na utashi wa kusimamia kwa makini, kuratibu na kufanya utafiti wa soko la mazao. Ukosefu wa soko la mazao ya kilimo ni moja ya sababu inayofifisha kilimo nchini. Hivyo, Serikali iangalie bei ya mazao hasa katika kilimo cha mkataba, lakini vilevile Wabunge walilalamikia sana bei ya mahindi na masoko ya mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli lazima tuchukue hatua wakati unaotakiwa kuchukua. Kama ukiangalia Tanzania inazalisha mahindi kabla ya Zambia na Malawi, na kwa hivyo tusipotumia masoko ambayo yapo wakati tumevuna, tutakutwa na nchi za jirani na hivyo itakuwa ni sababu ya kukosa masoko kwa ajili ya mahindi yetu. Kwa hiyo. Mheshimiwa Waziri tunaomba sana pamoja na Wizara yako muwe makini sana katika kutoa uamuzi ambao unaleta hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya mwisho kuhusu kilimo, ninaomba Serikali ione umuhimu wa kutoa kodi, tozo, ushuru na ada mbalimbali kwenye pembejeo na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na zana za sekta hiyo. Tukifanya hivyo tutahamasisha kilimo na kodi zitalipwa kwenye kununua bati, kwenye kununua cement na maeneo mengine yote na uchumi wa nchi utachanganya kwa urahisi zaidi kwa sababu kilimo ndiyo chimbuko la uchumi wa Watanzania. (Makofi)

Kwa upande wa maji; maji ni uhai, maji ni uchumi, maji ni usafi na afya. Umuhimu wa maji hauna mjadala, tunaomba wakala uanzishwe mara moja na tunaomba sana ile shilingi 50 Waheshimiwa Wabunge tuazimie tena, tulishaazimia tumuombe Waziri wa Fedha aone umuhimu wa maji ndani ya nchi hii kwa sababu utaondoa gharama za sekta zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mifugo, tunaomba Tume ya kuangalia malalamiko kama nilivyosema, lakini mifugo ni rasilimali ya Taifa na ni mali ya wafugaji mmoja mmoja, naomba tuone kwamba wafugaji wanapaswa kuhamasiswa, wafugaji wanapaswa kusaidiwa, wafugaji wanapaswa kuangaliwa ili mifugo iwe sehemu ya rasilimali ya Taifa, tusigombane na wafugaji, haitusaidii lolote na ninaomba sana mgogoro huu wa wafugaji na hifadhi uangaliwe kwa kuunda Tume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusu uvuvi, naomba tuunde bandari ya uvuvi na tununue meli za uvuvi na ili tuwe na samaki wengi ambao ni rasilimali kubwa kuliko hata hayo madini tunayoyapigania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunaomba tuongeze thamani, kwa hiyo suala la viwanda vya kuongeza thamani na kuongeza muda wa maisha ya mazao ni jambo muhimu ambalo litawahakikishia wakulima wanaozalisha mazao ya kilimo na yanayoongeza maisha ili mazao ya kilimo yasiharibike sana kwa sababu mazao ambayo hayajaongezewa thamani, hayajachakatwa yanaharibika upesi na viwanda vinapaswa kuwa masoko.

Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, namshukuru sana kwa yeye mwenyewe kusema kwamba viwanda ndivyo vitakavyookoa uchumi wa nchi hii na kutufikisha kwenye uchumi wa kati na mapato ya kati na tukifanya hivyo tutatuwa tumeiokoa nchi hii na mambo yataenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili nami niokoe muda niishie hapa niwaombe Waheshimiwa Wabunge waunge mkono Maazimio ambayo yako kwenye taarifa ya Wabunge ili tuweze kuimarisha sekta hizi ambazo ni muhimu na wala haina mjadala kwamba kilimo, ufugaji, uvuvi na maji ni eneo muhimu ambalo tukiliangalia vizuri nchi hii itaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa kutoa hoja ili Bunge liweze kupokea na kuweza kuunga mkono masuala ya Kamati hii, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja na naomba muunge mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii ya awali kabisa kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ambayo naitafuta kwa udi na uvumba ahsante sana. Vilevile nimshukuru Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu na Waziri mwenyewe kwa dhamira yao ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani na kama itatokea hivyo kwa kweli Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mnyimi wa fadhili kama sitampongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote chini ya Wizara hii kwa sababu kwa kweli kama siyo ufinyu wa fedha utaona kwamba wanajihadi kubwa sana. Kwa hivyo, naomba muendelee kukazana ili nchi ipate maji kwa malengo ambayo mmeyaweka na kwamba watu wasiende zaidi ya mita 400 kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai, maji ni usafi wa mazingira, maji ni afya na kwa ujumla maji ni maendeleo lakini ilivyo maji ni siasa vilevile. Kwa hivyo, ninaomba tutekeleze haya maji kwa kuondoa kiu ya maji, vilevile kusambaza miradi hii nchi nzima ili kusudi kila mwananchi wa Tanzania aweze kunufaika na miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga mambo mengi na imetekeleza mengi, Serikali ilipitisha sera hii nzuri kwamba maji yasiwe mbali zaidi ya mita 400 kutoka kaya mbalimbali na Serikali imetaka by 2020 wananchi asilimia 85 wamefikiwa na maji, lakini hadi sasa utaona na kama Waziri alivyoeleza ni asilimia 58.7 ambao wamepata maji na hasa vijijini. Ninaomba tufanye yafuatayo ili hayo mambo yatekelezeke kwa kasi kubwa zaidi. Niko kwenye Kamati hii na ni lazima ni-declare interest, nimeona changamoto nyingi ambazo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba Serikali kama imetenga shilingi fulani itoe zote basi kwa sababu bajeti ndiyo instrument kuu ya kutekeleza mambo ya maendeleo bila bajeti hatuwezi kufika mbali. Pili kwa sababu bajeti inaonekana kwamba haifikii malengo basi tuendelee na kuhakikisha kwamba katika bajeti hii shilingi 50 zimeongezeka kwenye mfuko wa maji kutokana na mafuta, dizeli na petroli na mafuta ya taa. Kwa sababu mimi ninavyoona ndivyo namna pekee na kila moja ni shahidi kwamba miradi ya mwaka huu au mambo yaliyopangwa mwaka huu yametekelezwa kwa asilimia 66 na mfuko wa maji na bajeti iliyopangwa imetekeleza kwa asilimia 22 tu. Kwa hivyo, Wabunge wanapokazania hii tozo ya shilingi ya 50 ni kuitaka Serikali iweze kufikia azma yake na wanachi waweze kupata maji kama tunavyotegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna vifaa au ya kujenga miundombinu ya maji mingi inatozwa kodi, maana yake ni kwamba mnapunguza bajeti ya kutumia vifaa kwenye miundombinu, naomba tuangalie na hilo. Jambo la nne ni uundaji wa wakala wa maji, hakuna labour force ya kutosha au wataalam wa kutosha kwenye Halmashauri zetu ambao watatekeleza miradi ya maji na ndiyo maana contractors wengi kwanza hawana uwezo kwa hivyo tukiwa na wakala miradi mingi itatekelezeka upesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye Wilaya yangu ya Hanang ambako Mbunge ni mimi. Niliomba kwa miaka minane lambo ya Gidahababieg na Waziri anaijua, ninaomba wakati akitujibu aweze kuniridhisha na awaridhishe watu wa Hanang kwamba miaka hii minne hatudanganywi bali lambo litapatikana. Ninajua anataka sana kufanya hivyo lakini aendelee kutupa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni maji katika Mji wetu Mkuu wa Katesh, ninaishukuru sana Serikali imeipa kazi hii Mamlaka ya Maji Babati lakini kwa muda mrefu Katesh haina maji, shilingi milioni 100 haitatosha, naomba Waziri uangalie na hata kwenye mfuko huo mdogo ambao tunao ili Katesh ipate maji. Huwezi kuwa na Makao Makuu ya Wilaya ambayo hayana maji, kwa kweli siyo jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna miradi mingi kwa mfano, tulitengewa shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya mradi wa Endasaki, Endagau, Endasiwold, lakini mpaka sasa tumepokea shilingi milioni 700 naomba hizi shilingi milioni 600 zitoke kusudi maeneo yaliyobaki kama Endasiwold Endagau waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna mradi mwingine wa Malama, Maskararoda, Masakta na Lambo ambao tulitengewa shilingi bilioni 1.2 hatukupata hata senti moja na kule kuna matatizo makubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang ipo kwenye Rift Valley ukichimba kisima unaenda zaidi ya mita mia moja huoni maji, kwa hiyo gharama ni kubwa. Ninaomba sana watu wetu wasibaki bila maji wakati malengo ya Serikali ni mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba fedha hizi za Malama, Endagau, Endasaki na Endasiwold zimepangwa kwa miaka mitatu mpaka leo maji hayajapatikana. Naishukuru sana Serikali kutokana na mradi huu Endasaki imepata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna visima zaidi ya tisa ambavyo vimeshachimbwa watu wanaona na wanataka kututoa macho kwa sababu miundombinu haipo, hakuna pump hakuna nini, watu hawachoti maji wanaangalia maji yako pale, ninaomba sana ninaomba sana miradi hii ikamilike na ninaomba Waziri kama walivyosema wengine kwa kweli tuunde Tume wakaangalie miradi ya maji nchi nzima ikiwepo Hanang yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie kwamba Endamdaiga haina maji, Gawidu haina maji, Gisambalang haina maji na vijiji vingi ambavyo havina maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba kwa vile Hanang haina maji ya chini ya kutosha bonde la ufa ninaombeeni mtupangie fedha za kuweza kuchimba mabwawa au malambo. Sisi tuna wafugaji, wanaotumia maji watu wengi takribani laki nne, tunao wakulima vilevile.

Jambo lingine ambalo nilitaka niongelee ni kuhusu umwagiliaji. Tuna mradi wa Endagau ambao ulipokea shilingi milioni 900, kama utatekelezwa vizuri Hanang watakuwa na manufaa makubwa kwa sababu hatuna uhakika wa mvua. Naomba sana kama Serikali ilivyoanza iendelee kuufuatilia mradi ule ili uende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linalosikitisha ni kwamba design zinakuwa si sawa na hasa ukienda kwenye miradi yote ya umwagiliaji ndani ya nchi utakuta kwamba zina faults au zina matatizo. Endagau ni moja ya maeneo yenye matatizo lakini naomba sana Serikali nayo iweze kuuangalia mradi huu ili Hanang nayo iweze kunufaika na miradi ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba, kama tunavyojua maji yalivyo na umuhimu barabara hazijengeki bila ya maji, hakuna mradi wowote utakuwepo bila ya maji, hata viwanda havitajengeka bila ya maji. Ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wote hapa wanataka hiyo tozo ya shilingi 50 iongezwe kusudi maji yatakapokuwa na uhakika ndani ya nchi hii, mengine yote yatawezekana na watoto watakuwa na malezi mazuri kwa sababu mama zao hawatachukua muda mwingi na hawataenda masafa marefu ya kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na kwangu mimi kipaumbele cha kwanza ni maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri, naomba Waheshimiwa Wabunge tuipitishe ili Watanzania wapate maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye sekta hii ambayo ni kipaumbele cha Taifa na vilevile ni Dira ya Taifa kupitia Mpango wa II wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile niipongeze sana Wizara kupita kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa sababu kwa kweli utaona wanafanya kazi na kama walivyoeleza kwamba viwanda vinaongezeka, niwapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kuonyesha dhamira yake ya dhati ya kujenga Sekta ya Viwanda katika Taifa letu. Ukikuta Rais ameonyesha dhamira yake nina hakika Watanzania wote watajielekeza huko na naomba tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ndani ya Bunge hili, alisisitiza kuwa sekta ya viwanda ina jukumu kubwa la kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025. Toka alipozindua Bunge hili, dhamira ya Rais inatupa uhakika wa kufikia azma hiyo.

Mheshimiwa Spika, vilevile nilimuona Mhesimiwa Waziri wa Fedha, akizindua kitabu kilichoandikwa na Watendaji Wakuu wa Serikali kilichoelezea changamoto ambazo zinaikabili azma yetu hii, kama ifuatavyo:-

(i) Ukosefu wa vipaumbele madhubuti;

(ii) Sera thabiti;

(iii) Ukosefu wa umeme wa uhakika;

(iv) Ukosefu wa mitaji;

(v) Ukosefu wa uzalendo wa kiuchumi; na

(vi) Ukosefu wa mfumo mzuri wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na viwanda hayo yote ni muhimu. Nimefurahi sana katika ukurasa wa 140, Waziri wa Viwanda mwenyewe amesema kwamba watajaribu kuangalia Sera ya Viwanda endelevu na ndiyo ilikuwa changamoto ya pili kwamba sera zikipitwa na wakati azma yetu inaweza isifikiwe. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri fanyeni haraka ili tusishindwe kufika kwenye azma yetu ifikapo 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda nizungumzie mradi wa Liganga na Mchuchuma wa chuma na mkaa. Kama Waheshimiwa Wabunge wengine walivyosema, kwanza niipongeze sanasana Serikali kwa kuuweka mradi huu kuwa mradi wa kielelezo. Wamefanya hivyo, umeanzia Awamu ya Nne na awamu hii imeweka umuhimu mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwa uhakika uchimbaji wa chuma ni nguzo muhimu na ni sekta mama kwa kweli, ni viwanda mama au ni viwanda vya msingi. Liangalieni jengo hili thamani yake robo tatu ni chuma uone chuma inavyohitajika nchi hii. Kwa hiyo, tutakavyoharakisha utekelezaji wa mradi huu utasaidia sana nchi hii. Angalieni hata maendeleo ya nchi za Ulaya yametokana na chuma wakati wa Oliver Twist. Angalieni maendeleo ya India, Mahalanaumis alifungwa lakini chimbuko la uchumi wa India leo ni mradi wa chuma kule India. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuone hilo, fikirieni kama reli hii ya kati inayojengwa sasa hivi chuma chake kingekuwa kinatoka Liganga ni kiasi gani cha ajira kingebaki Tanzania? Ni kiasi gani cha manufaa makubwa ya uchumi yangebaki Tanzania? Kwa hiyo, naomba sana tuangalie mradi huu ambao unaelezwa toka nikiwa shuleni hata kabla, naomba utekelezaji wake uende kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana miradi kama hiyo incentive zinazoombwa mziangalie, tunaweza tusipate faida lakini baadaye maendeleo ya kiuchumi na ya viwanda yatakuwa ni ya upesi zaidi, iron and steel industry ni chimbuko la maendeleo yote duniani. Angalieni chuma tutakachoagiza nje na kitakavyojenga ajira na uchumi wa nchi ambazo zinatuletea, hayo tunawanyima Watanzania. Nikimwangalia Waziri na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano, sina wasiwasi na nina hakika tunataka bati na misumari itoke hapa, kila kitu ambacho kinataka chuma kitoke hapa, tuna uwezo. Chuma kina multiplier effect, sina neno la Kiswahili, kinanufaisha sana sekta zingine kwa haraka. Naomba Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile kuongelea masuala ya biashara, naomba Serikali ijitahidi sana kuweka mazingira bora ya kufanya biashara nchini. Tumejitahidi toka miaka iliyopita lakini sasa tuendelee na jitihada hizo. Jambo kubwa ambalo linafanya sasa biashara iwe ya shida, Waziri wa Fedha yupo hapa ni mzunguko mdogo wa fedha. Mzunguko wa fedha uongezeke lakini ziwe fedha ambazo zinakubalika zisiwe ni fedha chafu. Kama cash haipo biashara haitakuwepo. Kwa hiyo, Serikali iangalie ni namna gani mzunguko wa fedha utaongezeka ili biashara iende na nchi yetu iendelee kupata faida kutokana na biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mazingira ya uwekezaji, nami ni-declare interest hapa nilikuwa Waziri wa Uwekezaji. Mazingira ya uwekezaji yakiwekwa sawa ujenzi wa viwanda hivi utaenda kwa kasi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nitalishauri hapa na ambalo limeanza na najua Wizara nayo na Serikali kwa ujumla inafanyia kazi, ni kuwa na One Stop Center. Hatuwezi kuwa na taasisi mbalimbali zinazohusika na ambazo zimetawanyika tukafikiri kwamba mwekezaji atakuwa na uvumilivu awaze kuona kwamba atabaki hapo na hela zake zinabaki benki halafu hazimletei faida hatakubali . Kwa hivyo, naomba tuharakishe hii One Stop Center ianze kufanya kazi. Ukimkamua ng‘ombe kama humlishi hutapata maziwa. Kwa hiyo, wawekezaji tuwawezeshe ili waweze kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee juu ya viwanda Hanang. Hanang ni eneo la kilimo, kwa hiyo, viwanda ambavyo vinatakiwa pale ni vya kilimo. Sisi tuna limestone nyingi sana kwenye ukuta wa bonde la ufa na hakuna mahali patakuwa na bei na gharama nafuu kutengeneza cement kama Hanang. Kuna mwekezaji amekuwa anaomba kuwekeza pale mpaka anakata tamaa kwenda Singida lakini hatapata mazingira mazuri kama ya Hanang, ukuta ule wote una limestone. Itigi kuna gypsum ambayo inatakiwa umbali wake ni chini ya kilomita 100. Fikiria Dar es Salaam na Mtwara wanapata gypsum wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kiwanda hiki kiweze kuanzishwa na tumfanye yule mwekezaji awe na matumaini na kwa hivyo tusimzungushe. Napenda kusema kwamba bureaucracy au urasimu unapaswa utumike kuwezesha viwanda vianzishwe na kurahisha uwekezaji. Naomba tusitumie urasimu kuzuia wawekezaji kuwekeza vinginevyo nchi yetu haitapiga hatua. Nataka niseme kwamba Tanzania ni ya pili Afrika katika ukuaji wa uchumi na naipongeza Serikali kwa hili. Ili maendeleo ya nchi yawe sustainable lazima yapitie kwenye uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Wizara, naunga mkono hotuba ya Waziri na tukizingatia ushauri huu, kazi yangu ni ushauri siyo kupinga. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Waziri na Serikali kwa bidii. Naomba leo nianze kwa kuongea suala la masoko ya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima ndio wanaopinda migongo yao kulima mashambani na wanabeba gharama zote za kilimo. Hawakubaliani na wasingependa kukutana na pingamizi lolote la kuuza mazao yao ambapo wamepata masoko hata kama ni nje ya nchi, badala yake wanataka wasaidiwe ipasavyo. Jukumu la kuona Taifa lina uhakika na usalama wa chakula siyo la mkulima mmoja mmoja zaidi ya wao kulima kwa tija. Uamuzi wa Serikali wa kuwafungia mipaka wananchi kuuza mazao yao, matokeo yake ni Zambia kunyang’anya masoko ya asili nje ya mipaka (nchi jirani). Wakulima wa Hanang wamepata hasara kubwa na kukosa mitaji ya kulima msimu huu kwa kushindwa kuuza mazao yao. Walishindwa kununua pembejeo zao kutokana na bei ya juu pamoja na bei elekezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuamua kujenga maghala makubwa yenye uwezo wa kuhifadhi angalau tani 500,000. Jitihada hizo zikutane na NFRA kuongezwa fedha za kununulia nafaka ya akiba kuhakikisha usalama wa chakula na matumizi bora ya maghala. Napenda kuomba Serikali ipunguze kodi na tozo katika mifuko maalum ya kuhifadhi mazao ili bei ya kununua iwe nafuu. Hatua hii itapunguza upotevu wa mazao ndani ya maghala yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuuliza utekelezaji wa commodity exchange umepotelea wapi toka sheria kupitishwa? Utekelezaji wa commodity exchange unategemewa kuwa ufumbuzi wa kudumu wa kuwapatia wakulima soko la mazao lililo muhimu. Tungependa kuona Serikali ikiweka mazingira mazuri katika kushiriki sekta binafsi katika sekta hii kikamilifu. Hii ni kwa sababu sekta binafsi ina uwezo mkubwa wa kuwekeza katika sekta hii ikiwa sekta binafsi itawekewa mazingira mazuri hasa yanayohusiana na sera za kikodi na udhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ninalotaka kuongea ni ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka 6% mwaka 2004/2005 hadi 2.1% mwaka 2016/2017. Ukichunguza sababu kubwa ni kupungua kwa bajeti iliyotengwa na kutolewa kila mwaka katika miaka iliyofuata. Naiomba Serikali iwe inaongezea sekta ya kilimo bajeti hadi kufikia 10% ya bajeti yote kwa mujibu wa Azimio la Malaba na Maputo. Ikiwa azimio hili likitekelezwa, litavutia sekta binafsi kuwekeza zaidi katika kilimo. Uwekezaji wa ziada utaongeza uzalishaji wa mazao na tija ambao utanufaisha Taifa kwa usalama na uhakika wa chakula, upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda, ongezeko la mauzo ya nje ya mazao ya kilimo na ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi na ushuru. Matokeo ya manufaa niliyotaja hapo juu ni kuongeza kasi ya azma ya Taifa kufikia uchumi wa viwanda na mapato ya kati ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni vigumu kufikisha bajeti ya kulima 10% ya bajeti ya Taifa tuondoe tozo zote kwenye pembejeo zote, zana zote za kilimo na uchakataji wa mazao ya kilimo. Hii itasaidia kupunguza gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kuongeza bajeti iliyotengwa kutoka shilingi 162,224,814,000 mwaka 2017/2018 mpaka shilingi 214,815,759,000 katika bajeti hii tunayoijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhakiki wa mawakala ni jambo muhimu, lakini tunataka matokeo ya uhakiki ili wale wanaostahili wapate kulipwa na wasiostahili wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika ni muhimu kwa wakulima lakini uliingiliwa na mchwa na kuingiza hofu kubwa kwa wakulima. Tuwauwe mchwa na kuupanga ushirika vizuri kabla ya kupitisha fedha za wakulima katika ushirika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niungane na wenzangu wote kwamba nami natambua kazi inayofanywa na Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Nishati.

Mheshimiwa Spika, napenda nijielekeze sasa kwenye Wilaya yangu halafu baadaye nitaongea habari ya Stiegler’s Gorge pamoja na fidia kuhusu gridi ya Taifa. Wilaya Hanang ina vijiji 96 na ni moja ya Wilaya mbili, Mbulu na Hanang ndio tulipewa vijiji vichache sana mwanzoni, baadaye nikaongea na Waziri akaongezea vijiji, lakini kuna vijiji 30 ndio vipo kwenye mpango wa kuletewa umeme, lakini spidi ni ndogo na bado 40 hawajui ni lini kwa sababu kuna ahadi ya Serikali lini vijiji vyote vitapata, nafikiri atafanya kila linalowezekana na bado ahadi yake ya tarehe 2 kwenda kwenda Hanang pamoja name ipo pale ili tukaangalie matatizo ya Vijiji vya Hanang. Naomba sana spidi ya contractor iangaliwe.

Mheshimiwa Spika, la pili ni kuhusu Gridi ya Taifa, kuna maeneo ambayo gridi ya Taifa imepita na wameahidiwa wapate fidia na wanalia kila siku hasa vijiji, hivyo naomba sana fidia ile iweze kupatikana.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye Stiegler’s Gorge mimi ni moja kati ya watu mbao tunafurahi sana mradi wa huu unatekelezwa katika nchi hii. Na sisi wote humu ndani tunajua chanzo cha maji kwa umeme ndio chanzo ambacho kina gharama ndogo na hatimaye bei ya umeme itakuwa ndogo na ndio itakayochochea viwanda nchi hii. Kwa hiyo namshukuru sana Rais na ninashukuru Serikali nzima kujielekeza kwenye Stiegler’s Gorge jambo ambalo kwa kweli litawafanya wananchi wa Tanzania wapate umeme ambao sio ghali.

Mheshimiwa Spika, nataka niwambie wale ambao hawaelewi vyanzo vyote ni vyetu vya gesi vya jua vya maji na hata ile nuclear bado ni chanzo chetu tunacho, ni lazima tuchague vyanzo vile ambavyo tukianza navyo vitatuletea manufaa makubwa na Stiegler’s Gorge ni mahali ambapo tutapata kweli gharama ndogo.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka wakati NGO’s zikipiga kelele kwa ajili ya Stiegler’s Gorge isitumiwe kama chanzo cha umeme walikuwa wanaongelea chura, jamani utalinganisha chura na wananchi? Haiwezekani! Namshukuru sana Rais huyu kwa kuwa imara na kuwa na ujasiri wa kukataa mambo ambayo hayana sababu na wengine wote humu ambao wanawaunga mkono wale watu kwa sababu zingine mbalimbali, naomba tuwe pamoja kwa hili kwa sababu ni manufaa ya Taifa hili la Tanzania, tumpe moyo Rais wetu na Waziri wetu ili waweze kukazania na hata kama hela itachukuliwa mahali pengine kwa manufaa ya sekta zote tusiwe na malalamiko ili tuwe tunapitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, watu wa Hanang wanaomba Mradi wa REA, wanufaike nao kama wilaya zingine zinavyonufaika na wale ambao hawapata fidia waweze kupata fidia.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono kwa moyo wangu wote bajeti hii ya Waziri Kalemani na Serikali hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika sekta yangu hii iliyo muhimu sana lakini haijulikani kama ni muhimu. Napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Makatibu Wakuu Wataalamu na Watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hotuba hii ya Waziri kutoka mwanzo ili muda ukiniishia, nisionekane kwamba siungi mkono jitihada za Serikali. Hata hivyo, napenda kusema yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mifugo na samaki inaangaliwa kama ni mali ya mtu mmoja mmoja, lakini kwa ukweli ni rasilimali muhimu ya Taifa. Siyo mali ya mtu mmoja mmoja ila ni rasilimali ya Taifa. Ningependa kusema kwamba, Tanzania ni nchi ya pili kwa wingi wa mifugo. Tanzania ni nchi yenye maziwa mengi na kwa hiyo, ni nchi yenye samaki wengi. Kwa hiyo, tuna bahati kubwa ya kuwa na rasilimali hii ambayo ikisimamiwa na wote na wanaohusika, nchi itanufaika na hii hali ya umaskini ni rahisi kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hivyo kwa sababu tuna ng’ombe milioni 30, tuna mbuzi milioni 18 na kondoo zaidi ya milioni tano. Utaona jinsi nchi ilivyokuwa na rasilimali kubwa kutokana na mifugo hii. Mwaka 2017 tumezalisha nyama tani laki sita na zaidi; tumekamua maziwa lita bilioni 2.4. Sekta hii imekua kwa asilimia 2.8, ingepaswa ikue kwa asilimia zaidi na kuchangia pato la Taifa kwa asilimia 6.9. Uchangiaji huu ni mkubwa kuliko hata Sekta ya Madini. Hata hivyo utaona kwamba macho mengi yanaangalia madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini kwa mwaka 2017 imechangia pato la Taifa kwa asilimia 3.5. Inasikitisha kuona kwamba fedha za maendeleo zilizotengwa ni shilingi bilioni nne lakini pamoja na kutenga fedha hizo senti hata moja haikutolewa kwenye sekta hii ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna namna ya kuikimbia sekta hii, nani ambaye haitaji protini? Nani ambaye hahitaji maziwa? Mtoto gani anayekua bila ya maziwa? Wafugaji ni wachache lakini mahitaji kutoka kwa wafugaji ni makubwa na ni ya watu wote. Naomba tuone hii. Hatua hii ya kutokutoa fedha ya maendeleo, inaonesha kwamba hatuipi sekta hii umuhimu unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sekta hii Serikali imekusanya shilingi bilioni 16 na zaidi. Utaeleza vipi? Kwa nini fedha ya maendeleo haijatolewa jamani kama siyo wa kutotoa umuhimu kwenye sekta hii? Inaonesha kwamba hatuipi umuhimu stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ina migogoro mingi; wakulima na wafugaji, hifadhi na wafugaji, hata wale wenye maeneo ya madini wana migogoro na wafugaji. Migogoro hii inatatuliwa kwa kusimamia sheria bila kuwa na moyo wa ubinadamu. Nasema hivyo kwa nini? Kwa sababu naamini wale wanaotekeleza, pengine azma ya Serikali ni nzuri, lakini wale wanaotekeleza hawana nia nzuri, wana nia mbaya au ovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalia ilivyofilisi watu. Ng’ombe waliochukuliwa kwenye hifadhi, ama wamekufa, ama wameuzwa bila kushirikisha wafugaji. Wamewafilisi wafugaji. Angalia jinsi inavyogombanisha wakulima na wafugaji katika kusimamia sheria hii. Angalia jinsi ambavyo tunapunguza amani kati ya Serikali na watu wake. Kwa hiyo, naomba sana nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba jamani operation hizi ziendeshwe; nami siko against au sipingi lakini lazima kuwe na moyo wa ubinadamu kuona kwamba ng’ombe ni rasilimali ya Taifa na wale wanaochukuliwa ng’ombe wanaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, badala ya kufilisi au badala ya watu kufa, tutumie sheria hii ili tuwasaidie wafugaji. Tuone kwamba fedha hizi zinazotumika kwenye operation zinapelekwa kwenye malambo, madawa ya tiba na chanjo. Ionekane kwamba hata wanapopigwa chapa siyo kuharibu ngozi au alama isionekane. Tukichukua hatua zinazostahili, tutakuwa tumewasaidia wafugaji. Ilivyo hapa sasa hivi wafugaji wanaona hawapo kwenye nchi yao, wanaona kwamba wapo porini kama wanyama wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine muhimu ambalo nataka niliseme, kwa nini kila Wizara isitenge eneo la wakulima na wafugaji? Hizi fedha za kwenda kwenye operation zingetumika kuwa na matumizi bora ya ardhi ili wafugaji wajue kwetu ni hapa na wakulima wajue kwetu ni hapa, lakini katika kufanya shughuli zao watakuwa wanashirikiana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tukifanya hivyo na sisi tuko nyuma ya Mheshimiwa Waziri. Nayasema hayo siyo kuonesha weakness yake, nataka nimshauri ili tushirikiane tuweze kutunza rasilimali hii iongezeke, iweze kunufaisha watu mmoja mmoja na inufaishe Taifa letu

Mheshimiwa Naibu Spika, ningekuwa na muda mrefu, ningesema na watu wa Hanang ambao ni watu wafugaji, wameonewa swagaswaga na kwenye mapori mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hizi Wizara mbili ambazo ziko chini ya Ofisi ya Rais. Kwa kuanza kabisa, naomba niwaombe Waheshimiwa Wabunge pamoja na kusimamia na kushauri Serikali ni muhimu sana kuchangia kwa busara na bila ugomvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa agizo na Mheshimiwa Waziri Mkuu kufuatilia kwa karibu sana na kikamilifu nia ya Mheshimiwa DC wangu kutaka kuniweka ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuwashukuru sana Wabunge wa Mkoa wa Manyara, Wabunge wote ambao wamefuatilia suala langu hususani Mheshimiwa Abuu kuona kuna nini kumbe nataka kuwekwa ndani kwa sababu niko karibu sana na wananchi wa Wilaya ya Hanang. Nawashukuru sana kwa uvumilivu wao nilivyowaomba wasiandamane kuja kule hawakufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba waendelee kushirikiana na mimi, ushirikiano ambao unawapa hofu watu ambao wanataka kuvamia wilaya yangu, napenda niendelee kushirikiana nao na Mungu awabariki sana. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa kwa sababu ni kweli sijawekwa ndani na nimemshukuru Rais kwa agizo lake. Kama walikuwa wanataka niwekwe ndani sijawekwa ndani na ni wao ndiyo chimbuko la matatizo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza sana na kumshukuru Waziri Jafo, wakati nia hiyo ikitaka kutekelezwa yeye vilevile alisaidia sana kuisimamia vizuri TAMISEMI ili wanaofanya kazi chini yake wafanye kazi vizuri. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa sababu kwa kweli wanajaribu sana kusimamia utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mambo ya wilaya yangu. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba agizo lake la elimu msingi bure linatekelezwa vizuri ambalo limezaa uandikishaji wa watoto mara mbili ya uandikishaji wa awali kabla ya agizo hilo. Pamoja na agizo hili zuri nataka niwaambie kwamba sasa watoto walioandikishwa wameongezeka, madarasa yanatakiwa zaidi na vilevile nyumba za Walimu zinatakiwa zaidi na zaidi ya yote tunahitaji walimu wengi zaidi kwa sababu watoto wameongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano tu wa Wilaya yangu ya Hanang kwamba kabla ya agizo lake tulikuwa tunaandikisha watoto laki moja na elfu kumi lakini mwaka huu wa 2018 waliandikishwa elfu kumi na mbili na mia nne themanini na sita. Utaona jinsi watoto walivyoongezeka, kwa hivyo, madarasa mengi yatahitajika, Walimu wengi watahitajika na nyumba nyingi za Walimu zitahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri wananchi wa Hanang wameliona hilo na wanamuunga mkono Rais wao kwa kujenga madarasa mengine lakini naomba tushirikiane nao. Kwa mfano, mahitaji ya madarasa kwa shule za msingi ni mia saba sabini na mbili na sekondari ni sitini na nne, kwa hiyo, wao wako tayari kushirikiana na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwe na utaratibu mzuri, nyumba zinazohitajika sasa hivi ni mia nane ishirini na tano kwa shule za msingi, mia tatu sabini na saba kwa shule za sekondari na madawati mia tisa kumi na mbili kwa shule za msingi na mia tano tisini na tisa kwa shule za sekondari. Haya yote yametokana na kuandikisha watoto wengi zaidi. Wananchi wako tayari kusaidiana na kuunga mkono Serikali yao, wanachoomba utaratibu mzuri wanapoona kwamba wananchi wamejenga mpaka kwenye lenta basi mimi Mbunge wao nipo lakini Serikali za Mitaa pamoja na Serikali Kuu tuone ni namna gani tunawaunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya, Serikali ina utaratibu mzuri kama kusaidia wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya. Hanang wanajitahidi sana, wana vituo kama saba walijitolea wao wenyewe kuvijenga na napenda kuishukuru TAMISEMI kupangia na kutoa shilingi milioni mia tano kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Simbai ambacho kipo kwenye kata ambayo iko pembezoni na kitasaidia watu wengi sana hata wale wa Kondoa watakuja kwenye kile kituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuendelee kuungana na wananchi kwa sababu afya ni muhimu sana. Watu wanaokwenda kwenye kilimo, wanaokwenda katika ufugaji, wanaofanya biashara ni wale wenye afya. Kama hatuna misingi mizuri ya afya itakuwa ngumu sana kutekeleza hata ilani yetu na kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara za vijijini, naishukuru na kuipongeza Serikali kuunda TARURA kwani itasaidia barabara za vijijini. Tujue kwamba barabara kuu na za mikoa hazitafanya kazi kubwa kama vijijini hakuna barabara. Naomba sana ugawaji wa fedha za Mfuko wa Barabara uwe hamsini kwa hamsini na ikiwezekana tutilie mkazo vyanzo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia REA, Serikali imefanya kazi kubwa kwani wananchi wa vijijini walikuwa hawategemei umeme lakini sasa umeme umefika vijijini, naipongeza sana Wizara. Hata hivyo, kuna upungufu mwingi ambao na kwa hakika usipofanya jambo upungufu hautaonekana, naomba Waziri aweze kufanya tathmini kila wakati ili aondoe upungufu ule kama kuruka taasisi au vijiji njiani wanapopeleka kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda nichukue nafasi hii kwa sababu mwaka 2004 nikiwa Waziri wa Utumishi ndiyo tuliotoa ule Waraka kwamba wale watendaji waliomaliza darasa la saba kabla ya muda huo waendelee. Nimeishukuru sana Serikali kuchukua hatua hiyo, nampongeza sana Waziri Mkuchika kuweza kuelewa Waraka ule na kuwaelekeza watendaji waone kwamba ule Waraka unasimamiwa vizuri na watu wasionewe ila pale ambapo wamegushi hatuwezi kusema neno lolote. Napenda kuwashauri watendaji wa Serikali wasipende kughushi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie hakuna mahali ambapo panatakiwa job security kama Serikalini kwa sababu ndiyo uamuzi ambao unahusu maisha ya watu unapotoka. Watumishi wa Serikali wanapaswa wajisikie salama, wanapaswa wajisikie kwamba wanaaminika ili waweze kutenda haki ambayo inaweza ikasaidia maendeleo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana Wizara ya Utumishi iweze kusimamia sana usalama wa kazi kazini kwa sababu kwa kweli wasipokuwa salama hawatakuwa na uhakika katika kufanya uamuzi na mambo mengi yatasimama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hotuba ya Mawaziri wote wawili, naiunga mkono Ofisi ya Rais kwa kazi nzuri inayofanyika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adimu ya kuweza kuchangia sekta hii ambayo inaonekana ina manufaa makubwa kama tutachukua hatua zinazotakiwa. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kama Waheshimiwa Wabunge waliotangulia walivyosema, amesimamia na kama hatua anazozitaka zikichukuliwa madini yataliletea Taifa hili manufaa makubwa kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri ninayemfahamu sana, pengine namfahamu kuliko watu wengi, alikuwa Msaidizi wangu na nafurahi kuona kwamba anapaa juu na Mungu ampe kila analolihitaji ili afanye kazi yake vizuri. Napenda kuwapongeza Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kumshukuru Rais kwa sababu kama hatutachukua hatua madhubuti, kwa kweli hatutaenda mbali. Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia statistics zinaonesha kwamba mifugo, kilimo na sekta nyingine zinachangia Pato la Taifa zaidi kuliko madini. Ilivyo sasa hivi, sekta ya madini inachangia kiasi cha asilimia 4 kwenye Pato la Taifa, ni ndogo sana. Projection inaonesha mwaka 2025 itachangia asilimia 10, naamini hatua hizi ambazo anazitaka Rais zikichukuliwa tutachangia zaidi hata kuliko asilimia 10 hii ambayo iko projected.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuongelea suala la wachimbaji wadogo. Wachimbaji hawa ndiyo kwa kweli wanao-discover au ndiyo wanaogundua madini ambayo yapo nchi hii, tunapaswa kuwathamini na kuwatambua. Ilivyo sasa wapo kwenye vikundi lakini bureaucracy inawacheleweshea hata kupata leseni. Naomba sana wapate leseni ili waweze kujiendeleza na wawe wenye fedha nyingi kuliko wengine, kuliko hao wanaotoka nje kwa sababu wanaotoka nje watapeleka mali nje bila manufaa kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile Serikali, Mheshimiwa Angellah, angalia sera, kwa nini watu wanakimbiza tanzanite Nairobi, kwa nini wasitake kuuzia Manyara na Arusha, kwa nini? Lazima kwa upande wetu tukiangalia, kama Kenya inataka kuchukua tanzanite yetu hawataweka VAT na sisi tunaweka VAT. Sasa tunafanya nini, tuna mkakati gani wa kuona kwamba madini ya Tanzania hayakimbizwi nje na ni athari kubwa sana yakikimbizwa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimepita kule kwenye maonesho na naomba Waheshimiwa Wabunge wote mkaangalie, inaonyesha kwamba ukipeleka dhahabu bila ya kuchenjua unaweza ukawa unapeleka madini mengine yenye thamani kubwa kuliko dhahabu yenyewe. Kwa sababu nilipopita kwenye stall moja kule nje wanaochimba dhahabu walionesha kwamba katika machimbo yao wamepata dhahabu, wamepata vanadium. Vanadium ni madini yenye thamani kubwa kuliko dhahabu lakini yanakwenda kuuzwa kama dhahabu. Kwa hiyo, naomba sana tukazanie hili la kuongeza thamani na kuchenjua madini ndani ya nchi ili yale yenye thamani kubwa yatakapoonekana na watu wa madini au wale wataalam waweze kutusaidia kuona kwamba kwenye migodi ile kama ni dhahabu tu au kuna madini mengine ili Tanzania isipoteze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu mwingine wa madini haya kuchenjuliwa hapa ni nini? Ajira ya vijana inakwenda nje. Ukienda India ajira nyingi za Wahindi kama Jaipur inatokana na tanzanite. Ingekuwa imebaki pale Mererani wananchi wa Manyara, Arusha na Watanzania kwa ujumla wengi wangeajiriwa pale badala yake tunawapa ajira Wahindi. Naomba tuangalie sana hizi sera ambazo zinaweza zikawa zinachangia madini yakimbizwe nje badala ya wawekezaji kuja kuchenjua madini haya na kuongezea thamani na kupata vitu mbalimbali kama pete, mikufu na mengine ambayo tunayafahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hanang au Manyara, sehemu kubwa iko chini ya Rift Valley na wanasema kwamba kule kwenye Rift Valley hakuna madini lakini tuna maeneo machache ambayo yako juu na kule kuna madini. Ukienda Hanang eneo linaloitwa Basotu kumekuwa na madini ambayo yana thamani kubwa na wako watafiti wanaoendelea kufanya kazi kule. Naomba watafiti wasisumbuliwe badala yake wapewe incentive waweze kufanya utafiti unaotakiwa na baadaye tujue Hanang ina nini nasi tuungane na Lake Victoria ambako wanatoa dhahabu kwa sababu inawezekana mwamba ule umetoka kule ukafikia mpaka kwetu au ulitoka kwetu kwenda kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kutoa shukrani zangu za dhati, naomba wawekezaji kutoka nje waone kwamba Tanzania siyo shamba la bibi, Tanzania ni nchi ambayo inastahili kupata manufaa ya rasilimali zake na tuna bahati Watanzania tuna rasilimali nyingi za madini, ardhi, mifugo au mambo mengine Mwenyezi Mungu ametupendelea lakini sisi wenyewe hatujipendi. Naomba tujipende ili tulinde rasilimali hizi kama Mheshimiwa Rais wetu anavyotuonesha na Mungu ampe maisha marefu na afya njema ili haya ambayo Mwenyezi Mungu ametupa Watanzania wanufaike nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ambayo sijaitegemea, nawe Mungu akupe afya njema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii, maana yake nilishaanza kukata tamaa, maana yake muda unazidi kwenda. Naomba kwa kuanza kabisa niunge mkono hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya Bajeti yake na vilevile naunga kwa dhati kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa umahiri wake, kwa uongozi wake na umakini wake wa kusimamia shughuli za Serikali na unaiona katika hotuba aliyoleta mbele ya Bunge hili. Vilevile nitakuwa mnyimi wa fadhila kwa sababu najua kazi wanayofanya Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Angella Kairuki kwa kuweza kumsaidia na kuonyesha mambo mazuri yanayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kutumia nafasi hii vizuri, nitajielekeza kwenye uwekezaji na nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kuona mambo kwa upesi kuitoa Wizara hii, Sekta hii kwenye Viwanda na Biashara na kuileta chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa sababu uwekezaji ni suala mtambuka, uwekezaji uko kwenye viwanda, uwekezaji uko kwenye kilimo, uwekezaji uko kwenye elimu na uwekezaji uko kwenye sehemu nyingi. Kwa hiyo, mahali panapofaa ni kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kuona hili, kwa sababu kwa kweli, katika uwekezaji ndiyo tutaongeza mapata ya Taifa hili, bila uwekezaji hatutaweza kuongeza mapato ya Taifa hili. Vilevile, ajira hii inayoliliwa na vijana ambao wako vijijini na ambao wanatoka vyuo vikuu na vyuo vingine itatokana na uwekezaji ambao tutawekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi ya hapo, vilevile uwekezaji ndiyo unatumia teknolojia mbalimbali na kuongeza maendeleo ya nchi yetu. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, lakini vilevile kwa ajili ya yeye kusimamia uwekezaji huu kupitia ofisi mbalimbali, Tanzania imekuwa ya saba katika bara la Afrika kuvutia uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, mtaji umeongezeka, uwekezaji umeongezeka kutoka dola 640 mwaka 2005 hapo tulipo mwaka 2016 ilifikia mwaka dola 1,365, ingawa umeteremka kidogo mwaka 2017 kuwa dola milioni 1,180 kwa sababu huu ndiyo mwelekeo wa dunia, siyo wa Tanzania, lakini Tanzania ndiyo iko mahali pazuri na wanaotaka kuja kuwekeza Afrika watataka Tanzania kwanza, kwa ajili ya amani yetu. Vile vile uwekezaji kwenye miundombinu, uwekezaji kwenye maji, uwekezaji kwenye maeneo ambayo yanahitaji kufanya uwekezaji uwe rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, ningependa kuona kwamba, mwelekeo wa uwekezaji kwa Tanzania pamoja na mazingira mazuri ambayo Serikali imeweka, Tanzania katika nafasi nzuri iendelee kuona kwamba inasahihisha maeneo ambayo yataifanya Tanzania iwe bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, napenda kuona kwamba mwelekeo wa uwekezaji kwa Tanzania pamoja na mazingira mazuri ambayo Serikali imeweka iendelee kuona kwamba inasahisha maeneo ambayo yataifanya Tanzania iwe bora zaidi. Naomba tuimarishe One Stop Center, kwa sababu bila ya hivyo, kwa mwekezaji kutoka nje au kutoka ndani kwenda BRELA, TRA na sehemu nyingine itamchukua muda na wakati mwingine anakwamishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba tufuate mfano ambao uko Rwanda wa Rwanda Development Company au Center ambapo mambo yote ya uwekezaji yako mahali pamoja na wale ambao wako pale wana uwezo wa kupitisha na wawekezaji wanaweza wakapitishwa sehemu zote hata kwa siku moja. Kwa hiyo, naomba sana sisi Watanzania tuone umuhimu huu badala ya kuwa na TIC peke yake halafu hawana uwezo wa kupitisha kitu cha BRELA ambayo iko viwanda, hawana uwezo wa kupitisha mambo ya TRA ambayo yuko Wizara ya Fedha, tungepaswa kuwa siyo TIC tungekuwa na shirika au taasisi ya uwekezaji ambayo ina watu ambao wanaweza kupitisha kodi kiasi gani na mengine yote yanayohusika kwenye mambo ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali imeimarisha sera, sharia na taasisi. Serikali kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuna Roadmap ambayo imewekwa ambayo kama tutaisimamia vizuri Mheshimiwa Waziri Mkuu uwekezaji utakuja kwa nguvu zaidi. Ni muhimu sana Wizara na taasisi za Serikali zinazohusika katika kutekeleza mpango huu ziwe na mikakati madhubuti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kusema ni kwamba Ofisi ya Waziri kama mratibu wa uwekezaji ni muhimu pia kuratibu na kusimamia mpango ambao unapitia Blueprint ya viwanda kwa sababu wakati huu ni wa kuimarisha viwanda, tuiangalie na mahali ambapo kuna upungufu tuweze kuyaboresha. Ukiunganisha hii Blueprint na Roadmap nina hakika nchi hii itajielekeza vizuri kwenye uwekezaji, mapato ya Serikali na uwekezaji unaotoka nje tukiimarisha hatutakuwa tunarudi nyuma bali tunaenda mbele na tutapata mapato zaidi kwenda kwenye elimu, afya na sehemu zingine. Ndugu zangu kama nchi haitatilia mkazo kwenye uwekezaji hatutafanya mambo makubwa tutakuwa tunatumia au tunakula bila kuangalia kesho tutapata faida gani. Tusipowekeza hatuwezi kujiendeleza kwenye mahitaji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Angellah mwanangu huyu ambaye alikuwa na mimi wakati nikiwa Waziri wa Katiba na Sheria na nimefurahi sana kwa sababu ni mchapakazi na atamsaidia Mheshimiwa Waziri kuona uwekezaji unaenda vizuri na uchumi wa nchi hii utapanda na uchumi ukipanda huduma za jamii na mambo mengine yatakuwa mazuri zaidi. (Makofi)

Nakushukuru sana, nilitaka nijielekeze kwenye uwekezaji kwa sababu najua umuhimu wa uwekezaji ambao sasa hivi unatiliwa mkazo kwa kuwekwa chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naunga mkono hotuba na bajeti hii na hii hotuba itafanya hotuba zingine ziende vizuri. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mwenyekiti wetu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu kwenye sekta hii muhimu. Pia naomba niungane na wewe kuipa pole familia na watoto wa Mzee Mengi kwa kuondokewa na baba yao. Nilivyokuwa Waziri wa Uwekezaji, Uwezeshaji na Sekta Binafsi ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Sekta Binafsi.

Mheshimiwa Spika, baada ya pole hiyo, sasa naomba nichangie kwenye sekta hii muhimu na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa sababu kila anapoongea na anapokuwa kwenye mikutano ya hadhara, jambo kuu analoliongelea ni kumtua mama ndoo kichwani, jambo ambalo kila mmoja wetu hapa nina hakika analipenda kwa sababu bila maji hakuna uhai, uchumi na maendeleo. Kwa hivyo, analolifanya Rais ni jambo muhimu na nawapongeza sana Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote ili waweze kuona kwamba azma hii ya Mheshimiwa Rais na wananchi wa Tanzania inafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo; Wilaya yetu ya Hanang ni Wilaya ambayo ni kavu, kwanza ipo kwenye lift valley na kwenye lift valley kule chini maji yanapatikana kwa shida sana. Ningependa kuanza na kuwapongeza sana Serikali kwa sababu walitoa shilingi bilioni
2.5 ili kuiletea Makao Makuu ya Wilaya maji na tulitegemea mwaka jana mwezi wa Tisa maji ya Katesh yawe yamefika lakini mpaka hivi nasimama hapa, mradi umetekelezwa kwa asilimia 66 tu. Naomba sana yafuatayo yafanywe; kwamba kuna wakandarasi ambao wanadai hela zao na certificates zimefika, naomba jamani tuweze kulipia certificate hizo ili maji ya Katesh yapatikane, siyo jambo zuri kwa Makao Makuu ya Wilaya kutokuwa na maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,vilevile, nafurahi sana na kuipongeza Serikali kuchimba visima ambavyo vinatumia solar katika Kijiji cha Gehandu, Kijiji Garbapi, Kijiji cha Gidika, Kijiji cha Hirbadaw, Kijiji cha Gawlolo, Kijiji Murumba, Kijiji cha Dawar, Kijiji cha Ginirish na Kijiji cha Laghanga. Naishukuru Serikali kwa nini si rahisi kuwa na visima vingi kwa wakati mmoja, lakini naomba mradi huu uwe wa maana kwa wananchi kwa sababu kutokana na kuwa kwenye Kamati hii ya Maji nimetembelea sehemu nyingi, visima vingi vina solar ambazo zina betri lakini visima visima vyote nilivyovitaja na najiuliza kwa nini. Naomba Mheshimiwa Waziri ajue kwa nini visima vile vinaendeshwa na solar ambazo hazina betri na wanajua Hanang ni eneo moja ambalo lina baridi kwa hiyo maji hayatapatikana kwa ufanisi kama tunavyotaka.

Mheshimiwa Spika, lingine ni lile aliloongelea Mheshimiwa Musukuma kwamba tunatoa mradi na hela zinatolewa, tuna mradi wa Kijiji cha Gehandu ambao tayari ulishapokea shilingi milioni 183 lakini mpaka leo kisima hakijatoa maji na ni muda mrefu sio mwaka mmoja ni miaka zaidi ya miwili. Naomba Waziri aweze kuona ni kwa nini jamani inachukua muda mrefu kupita kiasi kwa miradi kuwa tayari na wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba vilevile niongelee suala la Mfuko wa Maji; Mfuko huu ndiyo utakuwa ni namna ya kuondokana na tatizo hili kubwa la huduma nyeti ya maji. Naomba Waheshimiwa Wabunge tuheshimu azimio letu, nami nasema kwamba Mfuko huu wa Maji ndiyo uliofanya tutekeleze miradi mingi jamani. Kwa hiyo, sasa tukirudi nyuma tutarudisha bidii iliyokuwepo nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ile Sh.50 ya kutokana na mafuta iongezwe lakini na vyanzo vingine navyo viongezeke kwa sababu hata hiyo Sh.50 haitaondoa tatizo linalotukabili kutokana na ukosefu wa maji. Naomba sana ndugu zangu vyanzo vingine kama simu Vodacom, Airtel na vyanzo vingine vingi vije tu kwenye maji, tukiondokana na tatizo la maji, matatizo mengine kwenye sekta zingine yataondoka vilevile. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Musukuma asikubali kwamba wale wenye petroli wamtumetume humu ndani waseme kwamba hii isitokane na petroli. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Kwa hiyo naomba sana kama ata…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa..

MHE. DKT. MARY M. NAGU: ataona kwamba hilo…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mama nakuheshimu sana, eeeeh aisee.

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma hujaruhusiwa kusema tafadhali, Mheshimiwa Mary Nagu endelea.

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Anisamehe kwa jambo lolote kwa sababu na yeye namheshimu, lakini naomba kwa kweli suala la Mfuko wa Maji kama alivyosema Mheshimiwa Chenge na walivyosema wengine, wote tulisimamie kidete. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba jambo moja ninamshukuru Mwenyezi Mungu na nawashukuru na Marais walioniteua kuwa Waziri, Waziri wetu naye akajenge hoja kule Serikalini ili Serikali ione umuhimu wa kuongezea Mfuko huu ambao tayari kama si Wizara hii kujenga hoja, haitoshi kuongea hapa Bungeni peke yake bali kwenye Cabinet na Waziri na wenzake wengine wasaidiane kuona na Serikali inaona umuhimu huo, nina hakika ukosefu wa maji… (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Kuhusu utaratibu

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Inaongeza…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Kuhusu utaratibu

KUHUSU UTARATIBU

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, mahitaji ya maji ya wanawake na wananchi wa Tanzania ni makubwa. Kutokana na kuona umuhimu huo, kama nilisema jambo ambalo halimpendezi yeye basi avumilie na anisamehe. Naomba sana ndugu zangu suala la maji ni muhimu, ni kweli kwamba kuna watu ambao siyo waaminifu kwenye sekta hii, lakini kuna watu ambao wanafanya kazi kwa nguvu. Naomba Mheshimiwa Waziri kama Wabunge walivyosema, aunde hata tume kuona ma-engineer ambao siyo waaminifu waondolewe ili suala la maji lionekane kama linapewa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na sitaki hata kupitisha muda wangu, kama umebaki wengine waongee kuona kwamba hoja ya kuongezea fedha Mfuko wa Maji inaendelezwa vizuri na Mheshimiwa Musukuma akiondoka ananiheshimu, namheshimu, tutaongea naye hapo nje. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kunipa nafasi hii. Mimi natoka kwa wafugaji, baba yangu alikuwa daktari wa mifugo kwa hiyo, ninaelewa mambo mengi sana ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kujiweka kabisa kwamba anapenda wafugaji na anapenda mifugo. Nina hakika kuwepo kwake kutasaidia sana kwa wafugaji kuweza kunufaika na kutoa mchango mkubwa kwenye mapato ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, mifugo imeongezeka na mazao ya mifugo yameongezeka. Pamoja na hivyo mifugo mazao yake ni protein kwa binadamu. Mazao ya chakula na mazao ni malighafi, mazao ya mifugo ni malighafi ya viwanda vyetu. Wakati huohuo nataka niwaambie, kwamba mifugo inaweza ikatoa mapato makubwa kuliko sekta nyingine yoyote kama tutaiangalia vizuri. Hata sasahivi mchango wa mifugo, mazao yake na bidhaa ni kubwa sana kwa Serikali hii. Vilevile nilipokua nikifanya kazi NDC kiwanda cha viatu bora cha kilikuwa namba mbili ya kutoa mapato Serikalini; kwa hivyo hii inaonesha kwamba kama tutaisimamia hii sekta vizuri kwa kweli wafugaji watanufaika na taifa nalo na Serikali itanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na michango hii mikubwa, na sitaki kurudia takwimu kwa sababu Waziri ameweka takwimu vizuri na waliotangulia wameongea juu ya takwimu vizuri. Nikirudia haitasaidia lakini ni wazi kwamba mchango wa mifugo na mazao yake ni mkubwa sana kwa taifa letu. Hata hivyo, pamoja na mchango wa mifugo katika maeneo mbalimbali sekta hii inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kama tutaziondoa wafugaji watanufaika, Taifa hili litanufaika.

Mheshimiwa Spika, ya kwanza, ni kutokutekeleza matumizi ya ardhi na wanajua kabisa kwamba hakuna mfugaji mmoja mmoja mwenye eneo isipokuwa Serikali yenye ranchi. Wafugaji wanakuwa na ardhi ambayo ni ya pamoja (communal) na haiwezekani kuwa ya mmoja mmoja jamani. Kwa hivyo Serikali yetu ikiweza ku-protect au kulinda maeneo hayo ambayo ni communal ya wafugaji wa jadi na wafugaji wa kisasa, nina hakika wafugaji hawatapata migogoro wanayoipata sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, migogoro hii iko kati ya hifadhi na wafugaji, kati ya wafugaji na wakulima na wengine. Kama maeneo ya wafugaji kwanza yatajulikana na yatalindwa, migogoro hii itapotea bila ya nguvu kubwa jamani na naomba hili lifanyike na tutaondoa migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ya pili ni rushwa; kama kuna watu wanaumizwa na rushwa nchi hii ni wafugaji na hasa kwenye hifadhi. Nina mfano mzuri kule kwa Mheshimiwa Millya aliyemaliza kuongea, ng’ombe wa mfugaji wamekwenda kuchukuliwa nyumbani kwa sababu hawapati watu wanaopeleka mifugo kwenye hifadhi. Wamewapeleka kwa kuwadanganya kwamba wanawapeleka mahali pazuri, lakini kumbe wanawapeleka kwenye hifadhi na siyo rahisi kwa mfugaji wa kawaida kujua kwamba mipaka ya hifadhi ni wapi, naomba na hili lionyeshwe. Walipofika kule, wameambiwa mpo kwenye hifadhi, lipeni milioni 10 na wale wakakataa na sasa wapo mahakamani na inawezekana wakashindwa na hii ni laana kwa kila mmoja; kwa yule aliyehusika na hata Serikali yetu itahusika kwa namna fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, suala hili la rushwa liangaliwe na sekta hii iwalinde wafugaji wasiungane kwa sababu nakubali kwamba kuna wachache ambao wanaingiza mifugo kwenye hifadhi, lakini wengi wanaonewa kwa sababu uelewa wao kule porini si mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu, nataka niwaambie kwamba bila kuangalia mifugo, wafugaji watapotea na nchi hii itapata hasara kwa sababu nimewaambia kwamba bila kuwatetea hawa wafugaji, hakuna namna. Nataka niwaambie kwamba jamani kuna suala la dawa feki na kuna watu ambao wanataka washikilie wafugaji wawaone kwamba ni wazuri kumbe wanawashikilia wafugaji kwa sababu wanataka kupeleka dawa feki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali na Wizara hii, Waziri naomba wasimdanganye, ataniuliza kwa nini nasema hivyo, wanakuwa karibu na yeye halafu wafugaji wanapelekewa dawa feki na ng’ombe na wafugaji wanaumia. Namwomba sana Waziri namwamini lakini si rahisi kuwajua watu ambao wanataka kunufaika kwa kuonekana ni wazuri lakini kumbe ni ubinafsi wao wenyewe. Naomba dawa hizi feki ziangaliwe, chanjo za ng’ombe ziwe na uhakika na dawa za tiba ziwe na uhakika, nina hakika Sekta hii itakuwa na mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi hii, itawanufaisha wafugaji, umaskini utapungua; tuwasaidie wafugaji na Mungu atawabariki nyie wote. Ahsanteni. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu.

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Kila siku nasahau kutoa hoja, lakini naunga masuala yote ya Serikali. Naunga kwa mikono yote miwili bajeti hii na mimi nipo pamoja na wao. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya mwanzi kabisa Mungu akubariki na naomba upeleke salamu zangu na shukurani kwa Mheshimiwa Spika kwa kusimamia Bunge letu vizuri na kwa fursa sawa kwetu wote. Ningependa vilevile kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa miaka hii na hii ni Bunge la mwisho kushirikiana kwa pamoja na kila mmoja akafika wakati huu Mungu atubariki wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vilevile kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais mwenye Wizara hii. Mheshimiwa Rais amesimamia Wizara hii na akisaidiwa na Waziri wetu na kwa kweli wengine wamesema na mimi nitakuwa nimekosa fadhila kama sitatambua miradi ile ya mkakati ambayo ametuwekea kwa manufaa ya nchi yetu na mikakati hiyo ndio itasaidia maendeleo ya wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kutaja miradi hiyo kama standard Gauge ya railway ambayo itasaidia sana kubeba mizigo na kuongeza uchumi wetu, ufufuaji wa Shirika la Ndege ambayo itachochea sana maendeleo ya Utalii na usafiri wetu sisi wenyewe vilevile. Ya tatu ni ujenzi wa Bwawa la umeme la Mwalimu Julius Nyerere na ninyi mnajua kuwa na umeme wa uhakika maana yake ni kuwa na maendeleo ya hakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile afya ameichochea sana mpaka leo zahanati 1,198 jamani sio kazi ndogo katika miaka hii minne na miezi, vituo vya afya 487, hospitali 69, hospitali za rufaa 10 na Waziri leo ameelezea vituo vingapi, zahanati ngapi zitaongezeka ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais nina hakika hayo yote yanafanywa kwa ajili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme vijijini na kuanzisha uwakala jamani kuwa na umeme vijijini maana yake na Miji ni kuletewa maendeleo vilevile, hili ni jambo kubwa kutoka vijiji 2118 leo 9000 na zaidi wana umeme jamani hili si jambo dogo na yote haya ni miradi ya mikakati ambayo ameanzisha Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi ndugu zangu ni wakala wa maji, wakala wa umeme na wakala wa barabara vijijini, wakala hizi zitasaidia sana barabara, maji ambayo ni jambo muhimu sana zitasaidia sana vilevile na umeme na kuleta maendeleo ya uhakika na ya haraka. Pamoja na hayo bila Mheshimiwa Jafo na Manaibu Waziri pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wizara hiyo na watalaam wote nina hakika mengi yasingefanyika kwa hiyo nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Jafo na kila wakati tukiwa na jambo Mheshimiwa Waziri Jafo ukimuendea hajawahi kurudi nyuma ahsante sana wakisaidia na Manaibu Waziri pamoja na wataalam wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niseme kwamba jamani ningependa kusema machache ambayo yatasaidia sana vijiji vyetu na wilaya yangu. Kwanza ni sera ya barabara vijijini. Sera inasema kukarabati barabara ijijini haiongei kufungua barabara, ninaomba hii sera tuiangalie ili tuwe na kufungua na kukarabati barabara ambazo zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa sababu tuna wakala wa TARURA ingawa wanapata fedha kidogo lakini tusibakie tu kukarabati kuna Wilaya ambazo hazina barabara nyingi, kuna Wilaya ambazo zina barabara nyingi lakini tukifungua tutawapa kipaumbele wale ambao hawana barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba mimi kwa wakala wa barabara, barabara ya kutoka Gisambarang kupitia Masusu, Milongori, Biroda mpaka Lalaji jamani ni mpakani halafu kuna msitu na kuna watu wengi sana, vilevile barabara nyingine ya kufungua ingekuwa barabara kutoka Mascaroda kwenda Ng’arda, Lambo na kwenda Dareda ambako kuna hospitali kubwa pamoja na kwamba iko Babati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile ningependa kujiekeleza kwenye elimu ni muhimu sana na sasa elimu ya sayansi ndio muhimu nimefurahi, ninashukuru na ninampongeza Waziri kusema kwamba kila Wilaya zitajengwa barabara kwenye shule za sekondari, maabara zimeshajengwa zimefika mbali ninaomba sana tukamilishe ili watoto wetu wasome sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuongea juu ya Watendaji wa vijiji na Kata. Kule kuna kata na vijiji ambavyo havina watendaji. Maana yake ni kwamba maendeleo na hata huduma za wananchi zinaomba muangalie umuhimu wa kuazisha ya kupeleka na kuajiri watendaji ili vijiji vyetu na kata zetu ziweze kuongozwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningependa kuongea kuongea habari ya TASAF ninajua itakuwa kwingine lakini ndio iko vijijini. Ninaishukuru Serikali namshukuru sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Jafo na wengine wote kwamba sasa TASAF inaenda kwenye vijiji vyote TASAF ilikuwa inaenda kwenye vijiji vichache ikienda kwenye vijiji vyote wale masikini watapata namna ya kuweza kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninapenda niseme kwamba kuhusu vituo vya afya niliomba kituo kwa ajili ya Basotu na Endasack lakini mmenipa vituo vya pembezoni ya Hilbadau au pamoja na Simbay sasa mmeniletea fedha kwa ajili ya Mogitu. Ninaomba usisahau kata hizo pamoja na kata zingine nakushukuru umesema kila kata, kila wilaya itapata vituo vitatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na vilevile nisipoongea juu ya mkopo ule wa asilimia 10 nitakuwa sijatenda haki. Jamani mikopo hii inainua wanawake, vijana na walemavu. Naishukuru na wilaya yangu kwamba wanatoa ingawa kuna deni ambalo huko nyuma hawakutoa ninaomba kupitia msukumo wako madeni yale yaliyobaki wapewa wananchi lakini vilevile wanawake waendelee sasa hivi naona msukumo umeongezeka tutaondoa umasikini wakisadiana na TASAF nina hakika tutakwenda mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Wizara hii ni Wizara muhimu sana ni cross cutting ni ya TAMISEMI ina maji na maji ni kitu muhimu sana. Wilaya kama ya Hanang iko kwenye lift valley hamna maji ninaomba jamani mshirikiane na Wizara ya Maji najua Wizara sasa hivi huu ni wakala hauko chini ya TAMISEMI lakini tuweze kuomba vijiji na kata zipate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana naomba niongee juu ya Corona, ni ugonjwa mbaya kuliko magonjwa mengine yote…(Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika muswada huu muhimu wa uwekezaji hasa marekebisho ya Sheria ya PPP. Napenda ku-declare kwamba kwa miaka minne nilikuwa Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji ambapo nilikuwa nasimamia hii sera na Sheria ya PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba tulikuwa wote kwenye hii Wizara, amesaidia sana kuleta marekebisho haya, lakini vilevile napenda kukumbuka jinsi Dkt. John Mboya alivyoifanyia kazi sana sheria hii na leo amekuja na marekebisho alivyomshauri Waziri wake, bila kumsahau Naibu Waziri na Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nasimamia sheria hii, ilionesha changamoto kubwa ambazo kwa maoni yangu kwa kiasi kikubwa zitakuwa zimeondolewa na haya marekebisho ambayo ameyaleta Mheshimiwa Waziri. Madhumuni ya marekebisho haya yameainishwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri kwamba lengo la muswada huu ni kufanya marekebisho ya sheria ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuimarisha mfumo wa kitaasisi na kisheria katika usimamizi wa miradi ya ubia na pia kutatua changamoto zilizopo katika utekelezaji wa miradi ya PPP ili kurahisisha uibuaji, uidhinishaji na utekelezaji wa miradi ya PPP. Vilevile muswada unakusudia kumpa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha mamlaka ya usimamizi ya utekelezaji wa sera na sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nilipokuwa Waziri, Waziri wa Fedha alikuwa na mamlaka na Waziri wa sekta ile ambayo inaibua mradi alikuwa na mamlaka. Sasa kinachohitajika hapa ni uratibu au coordination kwa sababu watu sasa wamepunguza majukumu ya Waziri wa Uwekezaji. Kwa hiyo, watakuwa wamebaki Waziri wa Fedha na wa sekta ile ambayo inaleta mradi wa ubia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeondoa urasimu ambao upo. Na mimi nashukuru sana kuona kwamba tumepunguza urasimu kwa kiasi kikubwa, hivyo muda utakaotumika na tofauti zitakazokuwepo zitakuwa ni chache sana. Vilevile marekebisho haya yataimarisha usimamizi wa sera na wa sharia na nakumbuka kuna miradi iliyoanzishwa kabla hata ya Sheria ya PPP kuanzishwa. Kwa mfano, mradi wa kufua umeme wa Kampuni ya IPTL, mradi wa huduma ya maji wa City Water Dar es Salaam na mikataba ya huduma ya usafiri wa reli ya kati. Hiyo ilikuwa ni miradi ya PPP lakini hapakuwa na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyoonekana yote haikufanikiwa, ndiyo Serikali ikaamua kuanzisha sera na sheria.

Hii ni sheria ya kusimamia miradi ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi iweze kuwa na maandalizi mazuri na usimamizi mzuri. Kuwepo kwa sheria na sera imeonesha kuwa ikisimamiwa vizuri, kutakuwa na urahisi wa kutekeleza miradi ya PPP. Kwa hiyo, nataka nikumbushe alichosema Balozi Kamala kwamba kuna models tano za kuweza kutekeleza PPP. Kuna ile ya design, financial, operate na ku-transfer, kuna ya ku-design, finance operate bila ku-transfer, kuna design, build, operate and transfer, kuna equity partnership na kuna facilities za ku-manage projects. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu katika marekebisho haya tuone kwamba ni model ipi ambayo inafaa kwa kila mradi. Kwa hiyo, suala la kusimamia ni muhimu sana. Vilevile PPP pamoja na maboresho au marekebisho haya itaongeze kasi ya uwekezaji kupitia ubunifu wa pande zote mbili, sekta binafsi na sekta ya umma kutumia ubunifu, teknolojia na matumizi ya mitaji katika sekta binafsi. Utaratibu wa PPP utaharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hudumu za umma kwa sababu bajeti ya Serikali ni wazi haitoshi na mahitaji ya maendeleo kwa nchi yetu ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia uwekezaji huu wa PPP, wananchi watapata ajira. Vilevile zaidi ya ajira, mapato ya Serikali yataongezeka kupitia kampuni hizo ambazo zitatokana na PPP. Hata hivyo ufanisi wa kutoa huduma bora na gharama nafuu itakuwepo. Serikali itaokoa fedha za bajeti kupitia miradi ya PPP. Siyo fedha tu ambazo tunazipata kwa sekta binafsi kuna utaalam ambao Serikali hauna, lakini sekta binafsi unao. Tukitumia utaalam huu vizuri, miradi itaendeshwa vizuri na kwa hiyo, nina hakika kwamba tutapata manufaa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri kuwa miradi inayoandaliwa ikiwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa viwanda vya madawa kwa utaratibu wa PPP, mradi wa ujenzi wa hosteli ya CBE na mengineyo hasa mimi nafikiria miradi ya miundombinu inaweza ikasaidiwa kwenda kwa kasi kubwa kama PPP nayo itatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hatua nzuri sana hapa tumeona kuwa Serikali imedhamiria kwa kuleta marekebisho hayo, naomba marekebisho hayo tuyapitishe ndugu zangu. Kwa sababu tukipitisha, maendeleo yetu yataenda kwa haraka na tutakuwa tumempa Rais wetu ambaye anataka maendeleo kwa haraka yaweze kwenda kwa haraka zaidi. Sioni kwa nini mtu asite kukubali marekebisho ambayo yanaleta maboresho. Ili utaratibu uwe na manufaa kwa Taifa letu, lazima tukabiliane na changamoto kuu za utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 nilipokuwa Waziri wakati nasimamia PPP, nilileta marekebisho ambayo yalianzisha center ya PPP na center hiyo bado ipo. Kwa hiyo, sasa tumeongeza marekebisho, nina hakika mambo hayo yataenda vizuri. Pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kufanya marekebisho hayo na sasa Serikali inaleta maboresho zaidi kuna umuhimu na taasisi kuwa na uzalendo mkubwa na watalam kuwa na uzalendo mkubwa. Kuna watu wanaogopa miradi ya PPP kwa sababu wanafikiri wanagawanya mamlaka, manufaa waliyokuwa wanapata binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nitashirikiana na Serikali kufanya yote yafanikiwe. Ahsante sana.