Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Mary Michael Nagu (12 total)

MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Afya ni uhai na ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata afya bora katika Wilaya ya Hanang:-
(a) Je, ni lini Serikali itaziba upungufu wa watumishi wa afya katika Wilaya ya Hanang ambao wamefikia watumishi 202 hadi sasa?
(b) Je, ni lini Serikali itafungua duka la MSD na kuboresha vifaa tiba kwenye vituo vya afya katika Wilaya ya Hanang?
(c) Je, ni lini Serikali itajenga wodi zaidi za akina mama na watoto katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini iliyopo Hanang ili kupunguza msongamano katika Wodi hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang ina upungufu wa watumishi wa afya 456. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Halmashauri imeidhinishwa kibali cha kuajiri watumishi 64 ambao wataajiriwa muda wowote katika Halmashauri hiyo. Vilevile katika mwaka wa fedha 2016/2017 wameomba watumishi wengine 59 wa kada mbalimbali za afya.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka kipaumbele kwa kufungua maduka ya dawa kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa kutokana na upungufu na ufinyu wa bajeti. Maduka hayo ya Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) yatafunguliwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Mkoa wa Manyara na Halmashauri zake inaendelea kuhudumiwa na Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) iliyoko Mkoa wa Kilimanjaro.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, wodi moja ya wazazi iliyoko katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang haikidhi mahitaji kutokana na idadi kubwa ya wazazi wanaofika Hospitalini hapo kujifungua. Kwa mwezi wodi hiyo inapokea takribani wazazi 200 wengine kutoka Wilaya jirani. Serikali kwa kushirikiana na Shirika la EngeredHealth inaendelea na ujenzi wa wodi mpya moja ambao utakamilika kwa mwaka huu wa 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kulaza akina mama wajawazito 16 kwa wakati mmoja. Vilevile katika mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri imetenga shilingi milioni 70 kupitia ruzuku ya maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi ambapo fedha hizo bado hazijapokelewa.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 400 za awamu ya kwanza kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Endagaw na mradi huo kwa ujumla unagharimu shilingi milioni 800:-
Je, ni lini Serikali itamalizia kiasi cha fedha kilichobaki ili kukamilisha mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIANI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Endagaw ina jumla ya eneo la hekta 256 linalofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kwa sasa eneo linalomwagiliwa ni hekta 200. Wananchi wa Skimu ya Endagaw kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang waliibua miradi wa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang iliwasilisha maombi ya kupatiwa fedha yenye jumla ya shilingi milioni 800 kutoka Mfuko wa DIDF kwa ajili ya kuboresha mfumo wa umwagiliaji. Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi milioni 410 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa skimu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kujenga mfereji mkuu wa upande wa kushoto wa kijito cha Endagaw kwa kuusakafia ili kudhibiti upotevu wa maji ardhini kwa urefu wa meta 3,000 na maumbo sita ya kudhibiti mwenendo wa maji ya umwagiliaji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imepanga kuendelea na ukamilishaji mfereji mkuu wa upande wa pili wa kijito wenye urefu wa meta 3,000.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Katika Mwaka wa Fedha 2014.15 Serikali iliunganisha umeme kwenye vijiji vinne tu katika Wilaya ya Hanang; hata hivyo, Mwaka 2015/2016, Serikali iliahidi kuunganisha umeme vijiji vingine 19:-
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hiyo, ambayo inasubiriwa kwa hamu na wananchi wa Wilaya ya Hanang?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi kabambe wa REA awamu ya pili katika Jimbo la Hanang umevipatia umeme vijiji saba na shule za sekondari tatu kati ya Kata 19 zilizokuwa zimeombewa umeme katika awamu ya pili. Hata hivyo, vijiji vilivyobaki Hanang, vyote alivyoomba Mheshimiwa Nagu vitapatiwa umeme kwenye REA awamu ya tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji 44 alivyoomba Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu pamoja na shule za sekondari, vituo vya afya pamoja na zahanati vinatarajiwa kupatiwa umeme kwenye REA awamu ya tatu kama alivyoomba. Kazi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo inajumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 262.4, ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 169.8, lakini pia ufungaji wa transformer 54.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hizo, kazi nyingine itakayofanyika ni kuwaunganishia umeme wateja wa awali wapatao 11,449. Kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Hanang itagharimu Shilingi bilioni 15.8.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Wilaya ya Hanang ni moja ya Wilaya ambazo ziko katika Bonde la Ufa na hivyo upatikanaji wa maji ni wa shida sana. Suluhisho la kudumu ni kuchimba visima virefu na kujenga mabwawa.
(a) Je, ni lini Serikali itajenga bwawa la maji katika Kijiji cha Gidahababiegh ambalo lilibomoka kutokana na mvua?
(b) Je, ni lini Serikali itarudia kuchimba visima katika Vijiji vya Hirbadamu, Dajameda, Mwanga, Gidika, Lalaji na Wandela ambavyo awali vilipata ufadhili kupitia Mradi wa Benki ya Dunia lakini maji hayakupatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Jimbo la Hanang, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Bwawa la Gidahababieg ni bwawa kwa ajili ya umwagiliaji na lilibomoka kutokana na athari za mvua za mwaka 2006. Makisio ya gharama ya ujenzi wa bwawa hilo ilikuwa ni shilingi bilioni 1.09 na yaliwasilishwa kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu – TAMISEMI tarehe 18/02/2013 kwa ajili ya kuomba fedha za ujenzi wa bwawa hilo. Ukarabati wa bwawa hilo haukuweza kufanyika kwa wakati huo kwa sababu ya kukosa fedha.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji itatuma wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa bwawa hilo katika robo ya tatu ya mwaka 2016/2017. Aidha, katika bajeti ya 2017/2018, Serikali itatenga fedha ili kuanza ujenzi wa Bwawa la Gidahababeigh ili liweze kutoa huduma kwa wananchi.
(b) Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Mradi wa Maji Vijijini kupitia Mpango wa Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri, Halmashauri ya Hanang ilikamilisha miradi saba na miradi mitatu ya Wandela, Dajameda na Hirbadawa ilikosa vyanzo vya maji. Vilevile miradi ya Mwanga, Gidika na Lalaji iliyofadhiliwa na wadau wengine ilikosa vyanzo vya maji. Vijiji vyote vilivyokosa vyanzo vya maji vimepewa kipaumbele katika Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ili viweze kutafutiwa vyanzo vingine vya maji na hatimaye wananchi waweze kupata huduma ya maji kama ilivyokusudiwa.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Watumishi wa yaliyokuwa mashamba ya NAFCO walishinda kesi yao ya madai dhidi ya Serikali na Mahakama kuiamuru Serikali kuwalipa mafao na madai yote lakini Serikali imeendelea kukaa kimya kwa muda mrefu na hivyo kuwanyima haki yao jambo ambalo linasababisha adha kubwa kwa familia zao.
Je, ni lini Serikali itawalipa haki yao waliokuwa watumishi wa mashamba ya NAFCO ikiwemo shamba la Murjanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba ya kilimo yaliyokuwa chini ya Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO) yaliajiri watumishi 314 kwa nyakati tofauti na kazi tofauti ambapo NAFCO kupitia makampuni hayo iliingia mikataba ya hali bora na watumishi hao kwa lengo la kuboresha maisha yao. Utekelezaji wa mikataba hiyo ulitegemea ufanisi na utendaji wa taasisi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 16 Juni, 1996 NAFCO iliwekwa chini ya uangalizi wa PSRC kwa ajili kubinafsishwa kulingana na Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992. Aidha, baada ya zoezi la ubinafsishaji wa mashamba ya NAFCO, watumishi hao waliachishwa kazi kati ya mwaka 2003 na 2004 ambapo walilipwa malimbikizo ya mishahara yao na mafao mengine, bila kulipwa mafao yanayotokana na mikataba ya hali bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa baada ya kutolipwa madai yatokanayo mikataba ya hali bora, watumishi hao chini ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani Makao Makuu, walifungua kesi ya mdai Mahakama Kuu tarehe 5 Juni, 2004 dhidi ya PSRC na kushinda kesi hiyo ambayo ilichukua miaka minne mpaka mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hao walistahili kulipwa mafao ya mikataba ya hali bora kama ifutavyo:-
Mishahara miwili baada ya notisi, magunia matatu ya ngano kwa kila mwaka waliofanyia kazi au fedha badala yake kwa bei ya wakati huo ilipofungwa mikataba, mwisho walipwe misharaha ya miezi minne kila mmoja kwa kila mwaka waliofanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kwamba madai haya yamepitia vyombo mbalimbali vya usimamizi wa Serikali, hata hivyo, kumekuwepo na madai yasiyo sahihi baada ya uhakiki wa kurudia.
Hivyo, napenda nichukue nafasi hii kuwataka wawasilishe madai hayo ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo itashirikiana na Wizara ili tuweze kuyachambua na kujiridhisha ipasavyo iwapo wanastahili kulipwa na hivyo kuiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuchukua hatua stahiki.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Mwaka 2014/2015 Serikali kupitia Agizo la Mheshimiwa Rais iliwataka wananchi kuchangia ujenzi wa maabara na wananchi waliitikia kwa kiasi kikubwa sana, hasa katika Wilaya ya Hanang:-
(a) Je, ni lini Serikali italeta vifaa vya maabara katika majengo hayo ya maabara yaliyokamilika katika Wilaya ya Hanang?
(b) Je, Serikali itasaidia vipi kukamilisha maabara ambazo kutokana na njaa wananchi hawakuweza kukamilisha ujenzi wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang ina jumla ya shule za sekondari 33 zenye mahitaji ya vyumba vya maabara 99 kwa ajili ya masomo ya sayansi. Ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule 11 umekamilika kati ya 33 hizi zilizopo.
Mheshimiwa Spika, shule 10 zilizokamilisha ujenzi wa maabara kabla ya Januri 2017 zimepatiwa vifaa vya maabara. Shule moja haikupata vifaa vya maabara kwa kuwa, ilikamilisha ujenzi baada ya Januari 2017. Aidha, Serikali kupitia Mpango wa Elimu Msingi Bila Malipo inatoa fedha ambazo sehemu yake zinatakiwa kutumika kwa ajili ya kununua vifaa na kemikali za maabara. Katika kipindi cha kuanzia Disemba 2015 mpango ulipoanza kutekelezwa, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imepokea na kutumia Sh.253,913,281/= kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara.
(b) Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, zilitengwa shilingi milioni 70 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa maabara katika Shule za Sekondari za Hanang, ikiwepo Msqaroda, Bassodesh, Gidahababieg na Simbay. Vilevile katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, zimetengwa jumla ya shilingi 233,564,900 kwa ajili ya kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa maabara ambazo hazijakamilika. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 80 zinatokana na makusanyo ya ndani ya halmashauri na shilingi 153,564,900 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa maana ya CDG.
MHE. DKT. MARY MICHAEL NAGU aliuliza:-
Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni mia tatu (300,000,000/=) kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Katesh, hata hivyo mradi huo bado haujaweza kuwanufaisha wananchi kwa sababu ya gharama kubwa za umeme zinazosababisha pampu za maji kufanya kazi kwa muda mfupi tu.
Je, Serikali haioni haja ya kupunguza au kuondoa kabisa tariff zilizopo ili gharama ya umeme iwe chini kidogo na kusaidia kusambaza maji kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu inasambaza umeme vijijini kwa kuweka kipaumbele kwenye huduma za jamiii ikiwemo Mradi wa Maji wa Katesh. Lengo la Mradi huu ni kuwezesha huduma hiyo kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za kuendesha mtambo wa kusukuma maji kwa kutumia umeme ziko chini ukilinganisha na gharama ya kutumia mafuta ya dizeli. Gharama ya kuzalisha unit moja ya umeme ni shilingi 292 wakati gharama za kufua umeme kwa kutumia mafuta shilingi 450 hadi shilingi 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, gharama ya kuunganisha umeme kupitia Mradi wa REA ni shilingi 27,000 tu ambayo ni VAT kwa ajili ya Serikali kwa sababu Serikali imegharamia kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa gharama za umeme ni nafuu kuliko gharama za mafuta, tunashauri Halmashauri husika itenge pesa kwa ajili ya kuunganisha umeme katika mitambo ya maji.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y. MHE. DKT. MARY M. NAGU) aliuliza:-
Katika msimu wa mwaka 2015/2016, Wilaya ya Hanang ilikumbwa na mvua kubwa sana iliyosababisha kuharibika kwa miundombinu ikiwemo ya barabara.
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kilitengwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga na kukamilisha barabara iliyofunguliwa na Wachina inayopita katika Vijiji vya Mig’enyi, Milongoli, Gawidu hadi Ngamu na barabara inayounganisha Sechet, Wilaya ya Babati Vijijini kupitia Vijiji vya Basodesh, Basotu mpaka Mulbadaw?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zilizoharibika ziliandaliwa maombi ya fedha za dharura ambapo barabara ya Getasam – Mto Bubu ilikarabatiwa kwa shilingi milioni
438.259 katika mwaka wa fedha 2015/2016. Barabara ya Basotu – Basodesh katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilitengewa shilingi milioni 455 zilizotumika kujenga daraja moja lenye urefu wa mita 20 na kukarabati barabara hiyo urefu wa kilometa sita kwa kiwango cha changarawe.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Februari, 2018 Mfuko wa Barabara ulitoa fedha za dharura shilingi milioni 500 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Ming’enyi – Milongori. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, barabara za Endasak – Gitting – Dawar – Gawal – Gawidu zimeombewa shilingi milioni 209 za kuzifanyia matengenezo. Aidha, barabara ya Basotu – Basodesh imeombewa shilingi milioni 90 za kuwezesha ujenzi wa daraja linalounganisha Wilaya ya Hanang na Babati Vijijini.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Wilaya ya Hanang ni miongoni mwa Wilaya zinazozalisha kwa wingi nafaka za mahindi, ngano na shayiri lakini inashangaza kuona kuwa ruzuku ya pembejeo imepungua kutoka vocha 20,000 kwa mwaka 2012/2013 hadi vocha 10,000 mwaka 2014/2015:-
• Je, ni kwa nini vocha zimepungua na lini Serikali itaanzisha mfumo mpya wa pembejeo?
• Je, Serikali inatumia utaratibu gani kuhakikisha kwamba Mawakala wa pembejeo hawawauzii wananchi kwa bei kubwa kuliko bei ya soko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2012/2013, bajeti ya ruzuku ya pembejeo kwa utaratibu wa vocha ilitokana na mchango wa fedha za Serikali na Benki ya Dunia hivyo kupelekea kuwa na vocha nyingi ambapo Wilaya ya Hanang kaya 20,000 zilinufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mwaka 2015/2016 bajeti ya ruzuku ya pembejeo kwa kutumia vocha ilitokana na mchango wa Serikali pekee na hivyo kupungua kwa idadi ya vocha zilizotolewa, ambapo idadi ya kaya katika Wilaya ya Hanang ilipungua na kufikia kaya 10,000 ikilinganishwa na mwaka ule wa 2012/2013.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha mfumo wa usambazaji wa pembejeo kwa wakulima, kuanzia msimu wa 2017/2018, Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja kwa maana ya Bulk Procurement System, ambao umeongeza upatikanaji wa mbolea kwa wingi, bei nafuu na kwa wakati. Aidha, kwa kutumia utaratibu huo, bei za mbolea aina ya DAP na Urea zimepungua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja hutoa bei elekezi kwa kuzingatia umbali kutoka makao makuu ya wilaya kwenda kwenye kata na vijiji. Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na pindi ukiukwaji wa bei elekezi unapobainika hatua stahiki zinachukuliwa kwa wahusika.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-

Maeneo mengi katika Wilaya ya Hanang’ yana matatizo ya maji ingawa Kata za Dirma, Lalaji, Wandela, Gawidu, Bassodesh na Mwanga zina visima vilivyochimbwa licha ya maji kutopatikana:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kutatua matatizo ya maji katika wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang’, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika juhudi za kutatua matatizo ya maji katika Wilaya ya Hanang’, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo katika Vijiji vya Hirbadaw, Kata ya Hirbadaw na Murumba, Kata ya Lalaji utekelezaji wa miradi upo katika hatua za mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Vijiji vya Bassodeshi, Nyabati, Gijetamuhog, Murumba, Gorimba, Diloda na Qalosendo katika Kitongoji cha Merekwa wananchi wanapata huduma ya maji kupitia visima vilivyochimbwa. Sehemu ya Kijiji cha Dirma iliyopo Kata ya Dirma inapata maji kutoka kwenye Mradi wa Maji ya Mtiririko wa Nangwa. Kijiji cha Gawidu ni miongoni mwa vijiji vitakavyojumuishwa katika miradi ya Bassotu ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 90. Aidha, utekelezaji wa mradi huo utaendelea katika vijiji vingine kwa awamu kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kuendelea kutekeleza miradi mipya, kukamilisha inayoendelea na kukarabati ya zamani kwa kadri fedha zitakapopatikana ili kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Hanang’ wanapata huduma ya maji na yenye kutosheleza.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-

Je, ni lini miradi ya visima vya Waranga, Dumbeta, Endamudagya, Gidika, Murumba na Hirbadaw itakamilika na kuanza kusambaza maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Michael Nagu Mbunge wa Hanang kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto ya maji katika vijiji vya Waranga, Dumbeta, Endamudagya, Gidika, Murumba na Hirbadaw, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilichimba visima vitano (5) vyenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha mita za ujazo 45 kwa saa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha visima hivyo vinatoa huduma ya maji kwa wananchi, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia Programu ya Usambazaji Maji Endelevu Vijjini na Usafi wa Mazingira imetenga Kiasi cha Shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji katika vijiji vya Dumbeta, Waraga na Hirbadaw. Aidha, jumla ya vituo 30 vya kuchotea maji vitajengwa katika vijiji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji katika visima vingine vilivyobakia vya Gidika, Endamudagya na Murumba utafanyika katika mwaka ujao wa fedha 2020/2021.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-

Serikali iliondoa kodi kwenye mbegu za mahindi mwaka 2017 – 2018:-

Je, ni lini Serikali itasimamia upunguzwaji wa bei kubwa ya mbegu za mahindi na pembejeo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua ambazo zinzsaidia kupunguza bei za pembejeo ikiwa ni pamoja na kufuta ada na tozo zilizokuwa zinatozwa na taasisi za udhibiti wa pembejeo za kilimo. Katika kipindi cha mwaka 2017 na 2018 Serikali imefuta ada na tozo 12 katika tasnia ya mbegu kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na bei ya mbegu.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Februari, 2019 Serikali imekutana na wadau wa pembejeo za kilimo kwa lengo la kujadili maendeleo ya pembejeo za kilimo, ikiwemo kujadili suala la bei ya mbegu. Katika kikao hicho wadau walikubaliana kufanya utafiti wa kuhusisha taasisi ya udhibiti wa mbegu Tanzania (TOSCI) na Chama cha Wafanyabiashara wa Mbegu (TASTA) ili kutathmini gharama za uzalishaji na usambazaji. Jitihada zinazoendelea ni kutafuta vyanzo vya fedha ili kumuwezesha mshauri elekezi kufanya tathmini hiyo. Matokeo ya tathmini hiyo yatawezesha upangaji wa bei ya mbegu ambayo itamnufaisha mkulima na mzalishaji. Ahsante.