Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Julius Kalanga Laizer (30 total)

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jambo hili sasa limechukua muda mrefu tangu 2007 mpaka sasa ni zaidi ya miaka kumi na wananchi wa Enduimet na Ngarenairobi wameendelea kupata matatizo ya ardhi na maeneo ya kujenga.
Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato huo na kuyagawa mashamba hayo kwa wananchi hao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa jambo hili
la ardhi pia limefanana na maeneo mengine ya Monduli na kwa kuwa Serikali iliyafuta mashamba 13 mwaka 2015 na mashamba hayo mpaka sasa pamoja na mapendekezo ya wananchi bado hayajagawanywa.
Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuyagawa mashamba haya, iko katika mazingira gani ili wananchi waweze kunufaika nayo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Waziri, ni wazi Monduli kuna mashamba mengi ambayo wameleta kwa ajili ya kufutwa na yaweze kupata umiliki mwingine, lakini mpaka sasa mashamba mengi bado yapo kwenye mchakato; zile hatua za awali zimeshafanyika lakini mpaka yaweze kugawiwa ni pale ambapo umiliki wake utakuwa umeshafutwa rasmi na kuweza kuwarejeshea ili wao waweze kupanga tena matumizi kwa ajili ya wananchi wao au kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo, hatua hiyo itakapokuwa imekamilika, watapewa na watafanya zoezi la kugawa upya kama ambavyo waliomba toka awali.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali kwamba kwa kuwa ahadi za Rais wakati anaomba kura zimekuwa nyingi na Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kuzitekeleza ikiwepo barabara ya Monduli Juu kule kwa Sokoine. Ni kwa nini Serikali sasa isilete programu maalum inayoonyesha ni lini ahadi hizo zitatekelezwa na fedha zake katika nchi nzima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi zote ambazo Mheshimiwa Rais alizitoa wakati wa kampeni tunazitekeleza awamu kwa awamu, hatuwezi kuzitekeleza zote katika kipindi cha mwaka mmoja. Kuna kipindi cha miaka mitano na tutahakikisha…
… ahadi zote tunazitekeleza.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii pia kuishukuru Serikali kwa kutuongezea matenki mawili ya maji katika Kata ya Nalalami na Moita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa mradi huu kweli umeanza katika Kata ya Sepeko katika Kijiji cha Lendikinya lakini mradi huu umesimama karibu miezi miwili na miradi mingine minne katika Jimbo la Monduli kwa sababu ya upatikanaji wa fedha ambapo wakandarasi wameandika barua ya kusimamisha mradi na hakuna kazi yoyote inayoendelea kwa sababu Serikali imeshindwa kulipa fedha kwa wakati kwa wakandarasi. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu kulipa fedha za wakandarasi ili waweze kurudi site na kuendelea na mradi kwa ajili ya kuwapatia wananchi maji katika kipindi hiki ambacho kiangazi kimeanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo la maji na lenyewe limeendelea kuwa kubwa nchini ni lini Serikali itafanya utafiti wa kutambua ukubwa wa tatizo kwa kila halmashauri katika nchi yetu ili kuleta mipango thabiti ya kuwapatia wananchi maji, kuliko ahadi hizi ambazo zinachua muda kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS - TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nipokee hii concern kwamba certificate zimeenda lakini bado hazijalipwa. Naomba niweke kumbukumbu sawa; juzi nilitoka Malinyi nilikutana na mradi mkubwa wa maji ambapo tulipata concern kama hiyo. Kwa kushirikiana na Wizara ya Maji tutaziangalia zile certificate ambazo wakandarasi wameshapeleka ambazo zinahitaji malipo zifanyike kwa haraka. Lengo kubwa ni kuwa wakandarasi waendelee na miradi ili ikamilike na wananchi waweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kufanya utafiti katika halmashauri zote; nakumbuka, tukifanya rejea katika Bunge la Bajeti, nilizungumza na kuziagiza halmashauri zote zifanye tathmini ya miradi yote inayotengenezwa kwa sababu tunaona kwamba tuna idle project maeneo yote ya nchi na nilitoa deadline siku ile nikiwa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri tumeshapata tathmini ya nchi nzima ya miradi yote nini kimekwamisha. Lengo letu ni kujua changamoto zinazoikabili miradi ya maji na nini tufanye. Kwa hiyo mpango huo Mheshimiwa Julius tumeshaenda mbele zaidi, tumeshafanya hilo. Ofisi yetu pale sasa hivi kupitia team ya ma-engineer wetu wanafanya kazi kubwa ya kufanya uchambuzi na kuweka mikakati ambayo italeta majibu ya kuhakikisha miradi hii tunaiwekea mipango sahihi ya kuweza kuitekeleza ili wananchi waweze kupata huduma ya maji kama tunavyokusudia.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna Kamati Maalum iliyoundwa kwa ajili ya kushughulikia matatizo hayo na wakati huo huo Kamati inavyoendelea na kazi yake, Serikali imeendelea kuwaondoa wafugaji na kutaifisha mifugo yao, je, haioni ni wakati muafaka wa kusubiri Kamati hiyo imalize kazi yake ili waje na suluhu ya kudumu juu ya jambo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema, Kamati iko site, lakini sijajua kwa sababu wakati mwingine kuna case by case.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine haya mambo yanatofautiana mazingira kwa mazingira; na kwa sababu katika maeneo mbalimbali tuna Wakuu wetu wa Mikoa ambao wapo; na ni viongozi Wakuu wa Kamati za Ulinzi na Usalama wa Mikoa hiyo, hali kadhalika na Wakuu wa Wilaya, mambo haya wakati Kamati inafanya kazi wao watapima uzito wa maeneo haya na kuona jinsi gani ya kufanya ili utaratibu uende vizuri. Lengo kubwa ni kumsaidia Mtanzania katika mazingira yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kwa sababu tuna Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Kamati inaendelea kufanya kazi, nawaomba Wakuu wa Wilaya kuratibu mambo haya katika maeneo yetu na mikoa yetu. Jambo kubwa ni kuwalinda wananchi wetu waweze kuishi kwa usalama ili kujenga uchumi wa nchi yetu.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo la REA II katika vijiji vingi umeme umepita bila kugusa maeneo ya wananchi. Je, nini Kauli ya Serikali kwamba, vijiji vyote ambavyo vilipitiwa na REA II na haujafika kwa wananchi vinarekebishwa ili wananchi waendelee kupata umeme kuliko umeme umepita katika vijiji lakini haujawagusa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Julius kwa swali lake zuri na kwa kuwa, swali lake limejielekeza kwamba, utekelezaji wa miradi ya REA II kwamba kuna baadhi ya wananchi hawakufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimtaarifu pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba Serikali baada ya kuliona hilo kwamba, kuna maeneo yanatakiwa yafikiwe na miundombinu ya umeme ilikuja na mradi mpya densification, maana yake ujazilizi. Mradi huu unajielekeza kwenye maeneo ambako miundombinu ya umeme mkubwa imepita, lakini zipo kaya, vipo vitongoji, zipo taasisi za kijamii ambazo hazijafikiwa, kwa hiyo, huu mradi wa densification ambao umeanza kwa majaribio Mikoa Nane ikiwemo Mkoa wa Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Mara, Songwe, Iringa pamoja na Pwani umeonesha mafanikio na katika maeneo hayo kazi zinaendelea na wamefikia hatua sasa ya kufunga transformer.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi huu ambao umelenga vijiji 305 na kuunganisha wananchi elfu 53, kwa kuwa, Serikali imeona mradi huu una mafanikio mradi, nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, hii densification sasa itaendelea na mikoa mingine. Hata sasa Mshauri Mwelekezi yuko katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutathmini na kuona namna ambavyo tutatekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtaarifu tu Bunge lako kwamba, kwa kweli, wananchi wasiwe na wasiwasi, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli itakamilisha miradi hiyo.
MHE. JULIUS K. LAZIER: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza swali la nyongeza naomba nikiri kwamba kwa kweli naipongeza Wizara hii kwa jitihada kubwa ambazo imefanya katika kusaidia wananchi wa Wilaya ya Monduli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla pia sijauliza swali la nyongeza, naomba nimwambie tu Waziri kwamba waliokuandalia majibu wamekudanganya. Kwanza kwa mujibu wa taarifa tu ekari zilizofutwa Monduli ni ekari 13,000 na si 131,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, mashamba tunayoyazungumzia ni mashamba ambayo Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alivyokuja katika Jimbo la Monduli mwaka 2016 mwezi Machi, alizuiliwa na wananchi njiani na akatoa maelekezo kwamba Halmashauri ifanye mchakato wa mashamba yale ambayo yalikuwa na mashamba pori na wananchi wale walikuwa wanasumbuliwa na wale ambao waliyatelekeza mashamba na kuchukua mikopo kwa hati ya mashamba yale. Waziri akatoa maelekezo ambayo ndiyo ambayo mchakato wake ukafanyika na tarehe 09 Januari, 2018 tuka-submit taarifa ya Wilaya kwa kamishina wa ardhi wa kanda ambae taarifa yake haionekani hapa, kwa hiyo mchakato wa Halmashauri tulishamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, nataka nijue tu kwamba, kwa kuwa jambo hili Waziri wa Ardhi alishatoa maelekezo na kwa kuwa Halmashauri ilishafanya mchakato wa kuyafuta mashamba haya 25, je, ni lini Serikali itamalizia huu mchakato wa ufutaji wa mashamba hayo 25 ambayo tumeanza mchakato upya kama ulivyoeleza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Waziri alitoa pia maelekezo kwamba mapendekezo ya matumizi ya mashamba yale 13 yaletwe na kwa kuwa Halmashauri na wananchi tumeshamaliza mchakato wa kutenga maeneo kwa ajili yauwekezaji, maeneo ya akiba ya ardhi na maeneo mengine ya wananchi na kwa kuwa huu ni msimu wa kilimo na mchakato huo bado haujakamilika japo Halmashauri imeshakamilisha na taarifa yote iko Kanda; ni lini Serikali itaagiza Mkoa na Kanda walete mapendekezo ya wananchi ya matumizi ya mashamba hayo 13? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua ni lini mchakato utakamilika. Mchakato wa kukamilika unategemea na wao wenyewe kwa sababu si kazi ya Wizara kufuatilia na kuweza kujua ni jinsi gani mchakato unakwenda mbele; kwa hiyo wao wameshaona hawajaendelezwa na sheria zipo. Ibara ya 45 mpaka ya 47 kuna maonyo ambayo yanaweza kutolewa kwa muhusika kama hajaendeleza; na Ibara ya 48 unabatilisha kwa maana ya kumpelekea ilani kwa ajili ya ubatilisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wao wenyewe ndiyo wanatakiwa wakamilishe na wakileta kwa Waziri haina tatizo. Kwa hiyo si jukumu la Wizara kuona ni lini itakamilishwa ni mchakato ambao unatakiwa umalizwe na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anauliza kwamba ni lini Wizara itaagiza Mkoa ili waweze kutimiza. Kila Mkoa unataratibu zake katika mipango yake, kwa hiyo kama mlileta maombi mahitaji ambayo mnataka kutumia yale maeneo ni jukumu lenu pia kuona kwamba maeneo hayo yanatakiwa yafanyiwe kazi ile iliyokusudiwa. Kwa sababu unapoleta kubatilisha tayari umeshaona kuna hitaji na tayari una mpango.
Mhe shimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimesema kwamba hawajaleta mpango wowote kwa hiyo sisi hatuwezi kuwasukuma mfanye nini pengine hamjahitaji kwa maana hiyo. Kwa hiyo, ni jukumu la Mkoa kuhakikisha taratibu zote zinakamilika na Wizara inaweza ukafanya pale ambapo itakuwa imeletewa ofisini.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mweyekiti, nampongeza sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anasema kazi zote ziko kwenye kanda na watumishi wa kanda ni wa Wizara sisi tutafuatilia kule kwenye kanda tuone yale yaliyokwama yaje haraka Wizarani ili niweze kuyaona. (Makofi)
MHE. ABDALLAH S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Alhamdulilah. Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana, lakini pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima, nina afya njema, akili timamu na utayari wa hali ya juu ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kinondoni na tunasema dua la mwewe halimpati kuku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo letu la Kinondoni na Manispaa ya Kinondoni kwa ujumla TARURA inafanya kazi vizuri, tunawapongeza sana. Hata hivyo, Manispaa yetu ya Kinondoni ina barabara za kiwango cha lami siyo zaidi ya asilimia 10 za barabara zote katika Manispaa ya Kinondoni na tumewaambiwa wananchi tunataka kuleta Kinondoni mpya; je, TARURA ina mpango gani wa kutuongezea barabara zetu katika kiwango cha lami ili angalau kufikia asilimia 50 kama siyo asilimia mia moja?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) - MHE. JOSEPH S. KANDEGE:
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa, welcome again uko katika nafasi iliyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo chombo chetu TARURA kinafanya kazi vizuri ni pamoja na Manispaa ya Kinondoni, nimepata fursa ya kwenda kutembelea, Halmashauri zingine zinatakiwa kwenda kuiga na kutazama kazi nzuri ambayo inafanywa na TARURA Kinondoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la kuongeza ili angalau tufike asilimia 50 ya barabara zote kuwa za lami, kati ya Miji ambayo ina fursa ya kupata maendeleo kwa maana ya miundombinu ya barabara ni pamoja ni Jiji letu la Dar es Salaam. Naamini katika mpango mzima wa kuboresha Jiji la Dar es Salaam na program zinazoendelea hakika, barabara za Kinondoni zitahama kutoka hiyo asilimia kufika asilimia 50 katika kipindi ambacho siyo kirefu sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu niongezee katika majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba katika eneo la Kinondoni ambako Mbunge aliyeapishwa leo Mheshimiwa Mtulia anatoka ni kwamba hiyo coverage tutaifika haraka sana kwa sababu tuna combination mbili; tuna mradi wa DMDP ambao Mheshimiwa Mbunge anaufahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu una kazi kubwa sana ya kuboresha miundombinu ya barabara za lami katika Jiji la Dar es Salaam na eneo la Kinondoni ni eneo moja wapo, lakini kuna upande mwingine upande wa TARURA, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge aondoe hofu zile ahadi alizozisema kwa wananchi wake, naamini ikifika mwaka 2020 zote zitakuwa zimetekelezwa tena kwa zaidi.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa mabwawa yameendelea kupasuka katika nchi hii na kwa kuwa katika Wilaya ya Monduli, Kata ya Esilalei, bwawa la Josho na Oltukai, tulishaleta mpaka kwa Waziri Mkuu kuomba Serikali iweze kukarabati mabwawa yaliyopasuka mwaka 2015. Je, ni lini Serikali itakuja kukarabati mabwawa haya ambayo Serikali ilishahaidi kuyakarabati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ukiangalia kila mtu anazungumza kuhusu bwawa lililopasuka na nimetoa maangalizo, kwamba mabwawa haya yanapasuka huenda kandarasi haikusimamiwa vizuri, ile spillway (utoro wa maji) haukuwa vizuri au ile embarkment haikushindiliwa vizuri au utaalam wenyewe uliotumika huenda haukutumika sawasawa; kwa hiyo hapa inawezekana kila mtu atazungumza bwawa lake limepasuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelekezo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri zote wafanye tathmini ya mabwawa yote yaliyopasuka ili Serikali tuone kwamba tuna tatizo kiasi gani tuweze kulipangia mpango na tulirekebishe na hatimaye mabwawa haya yawasaidie wananchi katika mifugo, maji ya kunywa na matumizi mengine. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili bwawa mwaka 2017 liliharibika spillway. Spillway ilikuwa upande wa mashariki mwaka 2016/2017 ikaharibika ile ambayo ilikuwa upande wa mashariki na mkandarasi akairekebisha akaiweka upande wa magharibi ambayo mwaka huu imeharibika. Sasa Serikali inasemaje kuhusu hilo na kuwahakikishia wananchi wa sehemu hizo kwamba spillway haitaharibika tena baada ya kuikarabati mwaka huu? La kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, bado niko kwenye maji Chunya Vijijini; Mji Mdogo wa Makongorosi una watu zaidi 20,000 na una uhaba sana wa maji. Hata ule mradi wa maji visima kumi kila kijiji Makongorosi walikosa maji. Sasa hivi wananchi wa Makongorosi pamoja na Mbunge wao, wamechimba kisima kwenye kijiji cha Ujerumani. Kisima kina maji mengi sana lakini hakina miundombinu ya kuweza kutoa maji hapo kuyapeleka kijijini.
Je, Serikali iko tayari kusaidia mradi huo ili kumtua mwanamke ndoo kichwani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri inayoifanya katika Jimbo lake. Kama nilivyoeleza kuhusu suala la kuharibika kwa spillway, sisi kama Wizara ya Maji tunatoa fedha katika kuhakikisha wananchi wale wanapata mradi uliokuwa bora ambao utaweza kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sasa ni kipindi cha pili mradi huo unaharibika, labda nitatuma timu ya wataalamu wetu wa Wizara kwenda kuhakikisha mradi ule ili mwisho wa siku ukamilike kwa wakati, lakini mradi utakaokuwa bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la pili kuhusu yeye pamoja na wananchi wake kuchimba kisima, lakini bado kumekuwa na changamoto ya miundombinu ya kuwafikiwa wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie sisi kama Wizara ya Maji hatututakuwa kikwazo katika kumsaidai yeye pamoja na wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. Kubwa nimwombe Mhandisi wa eneo hilo achangamke, asilale. Alete mchanganuo tuangalie namna gani tunaweza tukamsaidia ili wananchi wake waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa mwenyekiti, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba na mimi nimuulize Mheshimiwa Waziri.
Kwa kuwa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli katika Kata ya Makuyuni, Lemowoti na Halaramii wameonesha juhudi kubwa katika ujenzi wa vituo vya afya; na kwa kuwa Waziri wa TAMISEMI alivyokuja Monduli mwaka 2016 akiwa Naibu Waziri aliahidi kutoa michango kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi wale. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya kuwasiadia wananchi wale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri na kwamba na yeye mwenyewe atakiri na kuungana na jitihada za Serikali na hivi karibuni tumepeleka pesa katika vituo 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba safari ni hatua, azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinajengwa katika kila kata. Kama tumefanya katika kata nyingine, naamini kabisa na kwake itakuwa katika safari ijayo.
MHE. JULIUS K. LAIZER. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo hili la tembo katika nchi yetu limekuwa likiwasababishia Watanzania umaskini mkubwa sana na mkakati wa Wizara hauoneshi kama kuna jitihada nzuri ya kushughulikia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nauliza swali hili jana usiku tembo wamevamia mashamba ya wananchi zaidi ya ekari 20 na kumaliza kabisa na ni kilomita zaidi ya 20 kutoka eneo la hifadhi. Je, Serikali ina makakati gani wa haraka katika kipindi hiki cha mvua na cha mazao yetu ili kusaidia wananchi kuwaondoa tembo hao waache kuharibu mazao yetu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na matukio ya tembo katika maeneo mengi hapa nchini na hii imetokana na kuimarika kwa uhifadhi katika maeneo mengi na hivyo tembo wameongezeka. Pale ambapo pametokea tatizo la namna hiyo tunaomba tuwasiliane haraka ili kusudi askari wetu wa doria waweze kwenda na kuchukua hatua na kuwafukuza tembo hao ili warudi katika hifadhi pale ambapo wanastahili.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, kwanza mradi wa Sepeko Lendikinya mwisho wake kwa mujibu wa mkataba ni Juni 2018. Kwa hiyo, ni muhimu Wizara ikachukua hatua ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize sasa maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, tatizo la maji katika Shule hii ya Nanja Sekondari limekuwa la muda mrefu na kusababisha adha ya wanafunzi kuacha masomo na kwenda kutafuta maji katika malambo upande wa pili wa barabara ambao ni hatari kwa usalama wao. Je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba fedha hizi ambazo Wizara imetenga mwaka huu na mpaka sasa haujaanza zinapelekwa ili mradi huu uweze kukamilika kwa haraka na wanafunzi wale waweze kupata maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mradi huu wa mabwawa ni wa muda mrefu na utagharimu fedha nyingi shilingi bilioni 1.4, ni kwa nini sasa Serikali kupitia DDCA isichimbe visima vifupi katika Kata ya Makuyuni Esilalei ambako ni gharama nafuu na kwa haraka zaidi ili wananchi hao waondokane na adha ya maji ambayo imechukua muda mrefu sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto kubwa ya maji baadhi ya maeneo mbalimbali, Serikali imekuwa ikitenga fedha katika kuhakikisha inatatua tatizo la maji. Nimwombe Mhandisi wa Maji wa Monduli asilale, Serikali imeshatenga fedha, ahakikishe ana-raise certificate ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza pamoja na wanafunzi wa shule hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa ni kuhusu suala la uchimbaji visima DDCA. Nimuombe tu Mhandisi wa Maji aingie mkataba na watu wa DDCA na ile fedha aliyopangiwa ili watu wa DDCA waanze kazi ile mara moja. Ahsante sana.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Kwandikwa, ni mchapa kazi na msikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, barabara hii ya Nyakahanga – Nyabionza – Chamchuzi kwenda Nyakakika imekuwa korofi miaka yote na ndiyo maana wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliona ipo haja ya kuweka lami kilometa 5 kipande cha Kajura - Nkeito. Mvua iliyonyesha imefanya mawasiliano ya hii barabara yawe magumu sana na maeneo mengine ya Karagwe, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini wananchi wa Karagwe kuhusu kukatika kwa mawasiliano ya barabara hii na maeneo mengine ya Wilaya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wanaoishi katika barabara za Bugene, Kasulo na Mgakorongo Mlongo wamesubiri kwa miaka mingi sana kupata fidia ili kuweza kujengwa lami barabara hizi. Je, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia zao? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bashungwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pongezi nazipokea lakini kwa ruhusa yako nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Bashungwa kwa sababu anazifuatilia sana barabara hizi za Jimbo lake. Nimwambie tu eneo lake hili ni kati ya maeneo ambayo yanaunganika na nchi za jirani, ndiyo maana kuna vipaumbele vingi tunavifanya kuhakikisha kwamba tunatekeleza sera ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya kuungana na wenzetu, kwa maana ya Intergration ya East Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, ninawaambia nini wananchi, upande wa Serikali tunao mkakati ule wa kuhakikisha kwamba barabara hizi zote zinapitika wakati wote. Kwa hiyo, kama ilivyo kawaida tumetenga fedha mwaka 2017/2018, lakini mwaka 2018/2019 pia tunazo fedha za kuhakikisha kwamba tunaboresha. Kwa sababu, tumekuwa na mvua nyingi kama tulivyoshuhudia, labda niweke msisitizo tu, tumeelekeza TANROADS Mikoa yote na TARURA kwenye maeneo yote kuhakikisha wanayatambua maeneo ambayo yameharibiwa na mvua na kuleta gharama zake. Upo utaratibu wa kupata gharama za pamoja ili tuweze kurejesha hiyo miundombinu iliyoharibika. Kwa hiyo, niwatoe tu hofu wananchi wa Karagwe na Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kurejesha maeneo haya ambayo yameharibiwa na mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia ya muda mrefu, niseme tu kwamba kama ilivyo utaratibu suala la fidia ni la kisheria, sisi Serikali tutaendelea kulipa fidia kulingana na taratibu na sheria zilizopo, kwa hiyo, wananchi hawa wa Karagwe watalipwa fidia. Hata hivyo, Mheshimiwa Bashungwa azingitie kwamba katika bajeti tuliyopitisha, barabara aliyoitaja ya Bugene – Kasulo – Mlongo tunategemea kuipandisha hadhi kwenda kwenye kiwango cha lami (double surface dressing), kwa maana hiyo, uko umuhimu wa kuzingatia tunalipa fidia haraka ili wakati wa kuipandisha hadhi tuweze kwenda bila mkwamo wowote.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tumekuwa na tatizo la kuungua kwa majengo mbalimbali ya Serikali ikiwemo vyuo na shule za sekondari hata katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli. Je, nini mkakati wa kuhakikisha kwamba angalau kila halmashauri inapata gari moja la Zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, swali lake linafanana sana na swali ambalo limeulizwa kwenye swali la msingi ambalo nimeshalijibu. Kwa hivyo jibu lake linakuwa vile vile, kwamba, mikakati ni ile ile ambayo nimeizungumza kuhakikisha kwamba tuna dhamira hiyo hiyo ya kuona kwamba magari yanafika katika maeneo takribani yote. Ndiyo maana tumeanza jitihada sasa hivi za kutanua wigo wa kuweza kupeleka huduma ya Zimamoto katika Wilaya nyingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, kila mwaka tumefanya jitihada hizo kwa kufungua Ofisi, kupeleka Maaskari wetu kuanza kutoa huduma za kutoa elimu ili pale ambapo magari yatakapokuwa yamepatikana na vifaa vingine tuweze kuvifikisha huko viweze kusaidia jitihada hizi ambazo tumeanza nazo kwa mafanikio makubwa.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika ziara ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI mwezi Machi, 2017 katika Halmashauri ya Monduli aliahidi kusaidia juhudi za wananchi katika Kituo cha Afya cha Makuyuni. Pamoja na hayo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 fedha zote za ruzuku tulielekeza katika ujenzi wa Vituo vya Afya.
Je, ni lini Serikali italeta fedha za CDG katika Halmashauri ya Monduli kwa ajili ya kumalizia Vituo vya Afya Lemuoti, Nalarani, Makuyuni pamoja na Duka Bovu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Mheshimiwa Julius Kalanga awe na mawasiliano ya karibu na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa sababu wakati wowote fedha za ruzuku zinaweza zikaingia. Sasa zikiingia waweke kipaumbele kwenye hayo maeneo.
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika madaraja yaliyopo nchini kwetu Tanzania yote huvuka bure isipokuwa daraja la Kigamboni na NSSF ilikusudia daraja hilo kutumika bure mara baada ya marejesho. Je, ni lini Serikali sasa itasitisha tozo la kupita daraja la Kigamboni ili liweze kutumika kama yalivyo madaraja mengine ya Mkapa, Kilombero, Ruvu, Wami na mengineyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kuna adha kubwa ya usafiri kwa wananchi wa Kigamboni hususan mabasi ya daladala na daladala ili ivuke inalipa Sh.7,000 ikivuka mara 10 ni Sh.70,000. Kwa hiyo, wamiliki wa daladala huona hakuna haja ya kupeleka route ya Kigamboni, Machinga Complex na wananchi wanapata adha sana ya Usafiri. Je, Serikali haioni haja sasa kutafuta vyanzo vingine ili kuweza kulipa deni la NSSF watu wapite bure kuliko kufanya biashara maana imekaa kibiashara zaidi kuliko huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA : Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niyajibu maswali yake kwa pamoja. Nikianza na swali la kwanza la kuhusiana na uwekezaji uliofanyika hapo, naomba tu ieleweke kwamba daraja hili ni sehemu pia ya uwekezaji wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii na fedha iliyotumika kwa ajili ya uwekezaji huo ni fedha ya wanachama ambao mwishoni pia ndiyo fedha hii hii huwa inatumika kwa ajili ya kwenda kulipia mafao kwa sababu ni sehemu ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kukisema tu ni kwamba, Shirika linategemea sana daraja hilo kwa ajili ya kupata kipato na hatuwezi katika hali ya kawaida kufuta kabisa tozo na watu wakapita bure katika eneo hilo kwa sababu ni eneo la investment. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba huu ni uwekezaji ambao unafanywa na shirika na hii ni michango ya wanachama ambayo baadaye inarudi pia kwa ajili ya kulipia katika mafao mbalimbali.
Mheshimiwa wenyekiti, ukienda duniani kote utaratibu ndiyo uko hivi kwa sababu hii fedha ya uwekezaji, fedha lazima ipatikane kuja kulipia katika shughuli mbalimbali za shirika.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli REA III ni vijiji 10 tu kati ya 42 ndivyo vimewekwa kwenye mpango. Je, ni lini Serikali itaongeza vijiji vingine katika REA III katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Monduli?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeze Mheshimiwa Mbunge. Tumekaa na Mheshimiwa Mbunge wiki iliyopita. Ni kweli kabisa tulipopitia katika Jimbo la Monduli tulikuta ni vijiji 10 tu ambavyo tumevipangia umeme. Baada ya kufanya mapitio kwa nchi nzima, tumeongeza vijiji 1,442 na vijiji 12 vya Mheshimiwa Mbunge wa Monduli vimo. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa wazo lake zuri lakini tumefanya mapitio na tumeongeza vijiji zaidi ya 1,542 kwa nchi mzima. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge maeneo yote ambayo tulikuwa tumeyaruka hivi sasa kwa kiasi kikubwa tumeyaingiza ili nao wapelekewe umeme kwa pamoja.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na upungufu wa watumishi katika sekta ya afya lakini maslahi ya watumishi katika sekta ya afya yamekuwa duni hasa on call allowance ambayo Serikali kwa muda mrefu sasa haijapeleka fedha hizo katika OC. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizo ili kusaidia Madaktari kufanya kazi zao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo ninavyoongea katika maeneo yote ambayo kumekuwa na hamasa kubwa wananchi wakajiunga na CHF, hakuna tatizo la Madaktari kulipwa on call allowance. Akitaka kuchukua mfano, nimeenda Tanga pale sasa hivi katika hizi pesa ambazo wananchi wanachangia kwa kujiunga na Bima ya Afya, kulipana on call allowance si tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Naomba Mheshimiwa Mbunge ahamasishe maeneo ya kwake wananchi wajiunge na Bima ya Afya na michango ile ambayo inatolewa ya ‘Papo kwa Papo, Tele kwa Tele’ hakika katika maeneo yote ambayo nimepita tangu utaratibu huu umeanza, kulipana on call allowance siyo tatizo tena.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Madini ya rubi yanayopatikana katika Wilaya ya Longido kule Mundarara, biashara yake imedorora kwa sababu mpaka sasa Serikali haikutoa utaratibu wa kuendesha biashara ya madini hayo. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuleta mchakato mzima wa kusimamia na kuendesha biashara ya madini yale?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli madini ya rubi yanapatikana kule Mundarara, Mkoani Arusha. Madini yale ni pamoja na madini mengine. Baada ya mabadiliko ya Sheria 2010, tulizuia kutoa madini ghafi nchini. Tunataka madini yote yapitie kwenye uongezwaji wa thamani ili yaongezwe thamani kwa ajili ya kutengeneza ajira kwa wananchi lakini na vile vile kuisaidia nchi kupata kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi ni kwamba madini yale, baada ya zuio hilo, imeonekana kwamba imeshindikana kwa wale waliokuwa wanatoa madini ghafi. Sasa hivi sisi kama Serikali tunaangalia utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunawakaribisha wawekezaji, na wako wawekezaji ambao wameonesha nia, ya kuja kuyaongezea thamani madini ya rubi ili kusudi sasa yawe yanauzwa katika hali ambayo yameshaongezwa thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itawasaidia watu wa Mundarara na wachimbaji wote wengine kwa maana kwamba watakuwa sasa wanapata soko la uhakika kuuza ndani lakini vile vile madini hayo tutayatoa nje, yakiwa tayari yameshaongezewa thamani. Hii itasaidia kwa wawekezaji wa ndani wenyewe, lakini vile vile kama Serikali, itazidi kupata kipato kwa maana kwamba tutapata kodi na mrabaha katika madini ambayo yameongezewa thamani. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge kuwa tayari tu kwamba tunaendelea …
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali kwamba kwa kuwa tatizo kubwa la nchi yetu katika wafugaji ni suala la upatikanaji wa maeneo ya malisho na sheria ya mwaka 2010 ya Nyanda za Malisho Serikali ilishayaridhia.
Je, ni mkakati gani ya Serikali kuhakikisha kwamba kwa kutekeleza sheria hiyo inatenga maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nashukuru kwa kunipongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Na. 13 ya mwaka 2010 inatekeleza sheria mama za ardhi Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5 ya mwaka 1999, lakini inatekeleza pia Sheria Na. 6 ya Matumizi ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizi zote zinataja kwamba umuhimu wa Serikali za vijiji kutambua wadau wanaokwenda kutumia ardhi zile na kuwatengea na kuwapimia na kuwamilikisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado inabaki kuwa ni kazi ya Halmashauri yenyewe, kisha kazi ya kutambua na kuwapa idhini ya kwamba hili ni eneo la malisho ni yetu sisi kwa kulingana na sheria yetu Na. 13 ya mwaka 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote….Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nakushuku, kwanza niishukuru Serikali kwa majibu yao katika swali hilo la msingi, lakini nasikitika kwamba maeneo mengi ya Serikali katika majibu haya hayakidhi swali ambalo nimeuliza.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amesema kwenye jibu la msingi eneo la Mswakini na Makuyuni wanapata maji, lakini tumekuwa tumeleta malalamiko Serikali ya muda mrefu kwamba visima hivyo havitoi maji kwa sababu hakuna nishati ya umeme na Serikali imekuwa ikiahidi kila siku kwamba wanatuletea nishati ya umeme katika visima hivyo. Je, ni lini Serikali itatuwekea umeme katika visima vya Makuyuni na Mswakini ili wananchi wetu waweze kupata maji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nataka commitment ya Serikali kwa kuwa wamesema watatupa fedha kwa ajili ya miradi hii ya maji katika vijiji alivyotaja nini commitment ya Serikali kwamba kwa mwaka wa fedha 2019/2020 tutapata fedha ya kutosha kwenye Bajeti kwa ajili ya miradi hii ambayo usanifu wake umekamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Kalanga kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika Jimbo lake la Monduli na nimeshakwishafika Monduli tumeona kazi kubwa anayoifanya na sisi kama Wizara ya Maji tutahakikisha tunamuungisha mkono katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Lakini kuhusu suala zima la nishati ya umeme nataka nimuhakikishie tutafanya mawasiliano ya haraka na watu wa Wizara ya Nishati katika kuhakikisha eneo la Makuyuni wanapatiwa umeme ili uendeshaji wake uwe wa nafuu na wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, lakini suala zima la bajeti la mwaka 2019/2020 tunakumbuka Mheshimiwa Kalanga mbele ya Mheshimiwa Rais katika wakati anaweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Arusha ulitoa malalamiko yako na ukaomba atakapotembea na kudhulu wengine asikupite. Sisi kama Wizara ya Maji hatutokupita wala hatutokuacha wala hatutokutosa katika kuhakikisha tunakuongezea bajeti na wananchi wako waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kumekuwepo na operesheni inayofanywa na Wizara ya Mifugo katika mipaka yetu ya Tanzania hasa eneo la Namanga na ambapo wafugaji wetu wamekuwa wakipata matatizo makubwa ya kunyang’anywa mifugo na wakati huo huo sheria hairuhusu mifugo kutaifishwa lakini ipigwe faini; na operesheni hii haishirikishi wananchi wanaohusika wala viongozi wa maeneo husika na imesababisha madhara makubwa sana kwa wafuaji wetu. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba wafugaji wanaoenda kutafuta masoko nje ya nchi kwa sababu hakuna viwanda huku ndani, hawapati madhara na madhila wanayopata katika mipaka yetu ya Tanzania, hasa Namanga?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Laizer, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wetu wanapofanya shughuli zao za biashara wanashauriwa kuzingatia sheria za nchi zilizowekwa ili wasiweze kupata usumbufu wowote ambao unaweza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Mbunge anazungumzia kama mifugo imekamatwa halafu ikakosa mwenyewe, sheria inawaelekeza wale waliokamata mifugo kuitafisha na baadaye kuipiga mnada hadi pale yule mwenyewe atakapokuwa amepatikana. Nimhakikishie kwamba operesheni hizi haziendi hivyo. Kwa hiyo, wananchi wanachotakiwa ni kutoa ushirikiano tu wa kuhakikisha kwamba wanafuata sheria na taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado sasa hivi soko la nje ni kubwa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge mwenyewe kwamba tuna tatizo la viwanda hapa nchini, lakini Waheshimiwa Wabunge kwa sababu baadaye taarifa ya Kamati itawasilishwa, niwahakikishie kwamba mipango tuliyoipanga ni mizuri, viwanda vyetu vingi vitakamilika hivi karibuni na suala la wananchi wetu kuhangaika kutafuta masoko nje litakuwa limekoma kwa sababu karibia kila kona tutakuwa na viwanda vikubwa vyenye uwezo wa kuzalisha na tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuuza mpaka nje ya nchi.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika ziara ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI mwaka 2018 katika Jimbo la Monduli aliahidi kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya vya Nararami na Lemooti.

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Monduli?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama ambavyo katika swali lake ameuliza kwamba Mheshimiwa Waziri wa Nchi TAMISEMI aliahidi juu ya ujenzi kumalizia vituo vya afya viwili katika Jimbo lake, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hakuna hata siku moja ambayo Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI alishawahi kuahidi akakosa kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuvute subira. Kwa muungwana ahadi ni deni, nami nitamkumbusha kwamba kwa Mheshimiwa Kalanga uliahidi kumalizia vituo vya afya hivyo viwili. Kwa kadri fedha itakavyopatikana, hakika naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hivyo vituo viwili vya afya vitaweza kumaliziwa.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Moja ya tatizo kubwa linalowakabili wafugaji wa nchi hii hata wakianzisha ufugaji wa kisasa ni upatikanaji wa mbegu bora, lakini mpaka sasa ukifuatulia katika maeneo ambayo kuna artificial insemination ng’ombe waliopo no Borana pamoja na ZEBU wale wa Mpwapwa. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inaingiza mbegu bora nchini kwa ajili ya kusaidia wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mfugaji, Mbunge wa Monduli, Mheshimiwa Julius Kalanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango kabambe mzuri sana wa kuhakikisha tunaboresha mbali kwa maana ya kwa safu zetu mifugo katika nchi kwa kusimamia mikakati mikubwa mitatu:-

(i) Wa kwanza ni ule wa artificial insemination ambao umeenea nchi nzima katika vituo vyetu.

(ii) Wa pili ni ule wa kutumia njia ya asili kwa kutumia madume bora ambayo yanapatikana pia katika mashamba yetu. Ukienda katika shamba kama vile la Mabuki-Mwanza, Sao Hill - Iringa na kwingineko tunao Bulls wa kutosha ambao wanaweza kwenda kuboresha mifugo hiyo.

(iii) Ya tatu tunao mpango tunaita “multiple ovulation” ambapo mpango huu unakwenda kukamilika mwaka huu kupitia shamba letu la Mpwapwa ambao huu utakwenda kumaliza kesi hi ya kupatikana kwa mifugo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kalanga na…

MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, sekta hii ya mifugo bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwepo utitiri wa tozo mbalimbali kwa wafugaji ambao karibu ng’ombe moja tozo zake zinazidi shilingi elfu hamsini. Swali la kwanza, je, nini mkakati wa Serikali kuwapunguzia wafugaji tozo hizo ili waweze kuzalisha kwa tija?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tatizo linalowakabili wafugaji wengi nchini ni pamoja na ugonjwa wa Ndigana Kali ambapo wafugaji tunapoteza zaidi ya asilimia 60 ya ndama wakati wanapozaliwa na chanjo hii bei yake ni shilingi 12,000 kwa ndama. Je, nini mkakati wa Serikali wa kuweka ruzuku au kuondoa kodi katika chanjo hii ili wafugaji waweze kumudu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya mawili ya Mheshimiwa Laizer, Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utitiri wa tozo, Wizara imeendelea na utaratibu wa kupitia tozo zote zinazotozwa katika sekta hii ya mifugo na zile zinazoonekana kuwa ni kero kwa wafugaji wetu na wafanyabiashara wa mifugo tumeendelea kuzipunguza. Vilevile zile ambazo zimeonekana kuwa ziko chini tumeendelea kuziongeza kwa manufaa mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili anataka kujua kuhusiana na chanjo. Taasisi yetu ya TVLA na TVI mpaka sasa Tanzania sisi wenyewe tumefanikiwa kutengeneza chanjo tano na chanjo ya Ndigana Kali ni miongoni mwa chanjo tunayoifikiria kuiongezea. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili lipo katika mkakati wa Wizara na yenyewe itatengenezwa hapa Tanzania na tutakapofanikiwa itapunguza bei na kuwasaidia wafugaji wetu.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu na mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwepo Mbeya kwenye ziara na Mheshimiwa Rais Mkoani Mbeya na aliona mwenyewe msongamano ulivyo kwa barabara hiyo ya TANZAM, ambayo kwa kweli inahudumia sio Mikoa ya Mbeya na Songwe tu, ni nchi nzima pamoja na nchi ya DRC, Zambia, Malawi pamoja na nchi zingine.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa fedha yake yenyewe ikisubiri fedha za Benki ya Dunia?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwambalaswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuanza kabla ya kukamilisha usanifu, lakini suala la msongamano wa magari lina solution nyingi pia ukisimamia taratibu za kiusalama na ndio maana tuna Jeshi la Polisi bado wanameneji vizuri ili msongamano ule usiwe mkubwa na ndio maana msongamano upo kwa muda fulani fulani tu, lakini muda mwingine panakuwa pamekaa vizuri.

Mheshimiwa Mwambalaswa, hili tunalifanyia kazi, Serikali inatambua hiyo changamoto, kwa hiyo asiwe na wasiwasi, baada ya muda mambo yote yatakwenda vizuri.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza; na unipe ruhusa niwape pole wananchi wa Monduli, hasa wa Mto wa Mbu ambao wamekubwa na mafuriko kwa muda wa wiki moja sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Serikali imesema imetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa kilometa tisa; lakini bilioni saba hizo inawezekana zisipatikane kwa wakati. Nataka kujua commitment ya Serikali ya kuhakikisha kwamba walao barabara hii inawekwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Barabara hii ya Monduli Juu ambayo Waziri anasema ipo katika hali ya upembuzi yakinifu, upembuzi yakinifu umekamilika na document zote zipo tayari. Je, ni lini hasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Julius Kalanga yenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa Mto wa Mbu unaufahamu vizuri. Na Mheshimiwa Mbunge amekuwa akipigania kwa sababu adha ambayo imekuwa ikipatikana kila wakati mvua zinaponyesha mafuriko yanakuwepo eneo lile. Kwanza kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akilipigania eneo hili kwa muda mrefu. Naomba nimhakikishie, katika bajeti ya mwaka 2020/2021 tutaanza na mifereji na ujenzi wa kilometa moja utaanza ili tupunguze adha kwa wananchi wa Mto wa Mbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ameongelea barabara ya kwenda kwa Marehemu Sokoine. Kama anavyokiri hata yeye mwenyewe, kwamba usanifu ulishakamilika. Naomba nimhakikishie, kufanyika kwa usanifu tafsiri yake ni kwamba, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi kwamba fedha ikipatikana nako ujenzi utaanza. Aendelee kuiamini Serikali kama ambavyo tukiahidi daima tumekuwa tukitekeleza.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana mwezi Septemba Naibu Waziri alifika Monduli na mwaka huu mapema Mheshimiwa Rais alivyokuja Arusha ilizungumzwa habari ya tatizo la maji Monduli na baadae nikaenda Wizara tukakutana na Waziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa maji. Tukapata kibali cha miradi miwili, Mradi wa Meserani na Mradi wa Nanja na wakaniahidi kwamba mwezi wa nne mradi ule ungesainiwa, mpaka leo mradi ule bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua commitment ya Serikali. Ni lini mkataba huu utasainiwa ambavyo Serikali imeshaahidi kwa wananchi wa Monduli?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, anafanya kazi nzuri pale Monduli na mimi nikiri kabisa nilifika pale na moja ya maeneo ambayo alikuwa ameyazungumza na akasema Tenzi za Rohoni, tusimpite, sisi hatukumpita ndiyo maana tukatoa kibali kama Wizara katika kuhakikisha kwamba mradi ule unaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama viongozi wa Wizara tulishasema hatutakuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa miradi ya maji na ndiyo maana tumetoa kibali. Nimuombe tu sana Mhandisi wa Maji wa Monduli ajitathmini kama sisi Wizara tumekwishatoa kibali yeye anakwamishaje katika utekelezaji wa miradi ya maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya hapa nitafanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha mradi ule unaanza na wananchi wake wanaanza kupata huduma ile ya maji.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na kwa kweli nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri kwa sababu katika Wilaya ya Monduli vijiji vilivyokuwa vimepatiwa umeme peke yake vilikuwa 16 na sasa karibu vijiji vyote 64 vitaingizwa kwenye awamu ya tatu. Lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tatizo kubwa la REA katika maeneo mengi ni kwamba umeme unafika kwenye kijiji lakini vitongoji na maeneo mengi ya wananchi umeme ule haufiki.

Je, nini mkakati madhubuti wa Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo umeme haujafikia japo inaonekana kijiji kimefikiwa umeme unaweza kupelekwa kwa wananchi kuliko kuwa na umeme ambao umefika kijijini lakini wananchi hawajapata umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili katika Kata ya Engaruka katika Shule ya Oldonyolengai tayari laini kubwa imefika ni kazi ya kuunganisha tu katika shule ya msingi Engaruka Juu na katika zahanati ya Oldonyolengai. Je, nini kauli ya Serikali kwa mkandarasi aliyoko site ili aweze kuunganisha umeme katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Julius na kwa niaba yake napokea pongezi zake kwa kazi nzuri aliyoifanya katika Mkoa wa Arusha na maeneo mbalimbali na pia nimpongeze Mheshimiwa Julius kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika jimbo lake la Monduli.

Mheshimiwa Spika, kama alivyouliza na nakiri ndani ya Bunge lako kweli miradi hii ya umeme inayoendelea REA awamu ya tatu au na REA awamu mbalimbali kazi yake ya msingi ya kwanza ni kufikisha miundombinu ya umeme mkubwa katika baadhi ya maeneo kwenye vijiji.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hilo na ndio maana Serikali yetu ya Awamu ya Tano imebuni mradi wa ujazilizi awamu ya kwanza ambao ulifanyika katika mikoa 8 na tumepata mafanikio makubwa wateja takribani 30 wamepatiwa umeme katika vijiji 305. Mpango unaoendelea sasa hivi ni Ujazilizi Awamu ya Pili A kwenye mikoa tisa ikiwemo Mkoa wa Arusha pia Mkoa wa Mwanza, manispaa za Ilemela na Nyamagana na maeneo mbalimbali. Sambamba na hilo katika mradi huu wa REA wa Ujazilizi Awamu ya Pili takribani Bunge lako tukufu limetupitishia pesa shilingi bilioni 169 ambayo inaenda kuwezesha wateja wa awali 60,000 kuunganishiwa umeme.

Kwa hiyo, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa bajeti imeshapita tunawaahidi kwamba tutaendelea kuisimamia ili vitongoji vyote viendelee kuunganishwa lakini kwa kweli kazi kubwa kwanza ni kufikisha umeme katika maeneo ya makao makuu ya vijiji kasha usambazaji ni jambo endelevu. Pia naomba niseme taarifa ya ziada tumeielekeza TANESCO wamebaini maeneo 754 ambayo yamepitiwa na miundombinu ya umeme mkubwa na pale kazi kubwa itakuwa ni kuweka transfoma na kushusha huo umeme na kwa kuwa tumeamua TANESCO, REA yote ishambulie na ndio maana Serikali imefanya maamuzi ya makusudi ya kisera kufanya kwamba bei ya kuunganishia umeme 27,000.

Mheshimiwa Spika, naomba nikutaarifu na Bunge lako juzi tulikuwa na mkutano mkubwa na tutaanza kuzindua wateja wanaounganishwa kwa bei shilingi 27,000 na tunaanza Wilaya ya Kondoa wameshaunganishwa wananchi 500 baada ya uamuzi wa Serikali. Kwa hiyo, niwatoe hofu wananchi wote na vitongoji ambavyo hawajaguswa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameelezea masuala ya kwa kuwa laini kubwa imefika katika Kata ya Engaruka, ameuliza; Serikali inatoa maelekezo gani kwa mkandarasi ambaye ni NIPO Group aliyeko katika Mkoa wa Arusha. Juzi mkutano wetu baina ya REA na TANESCO tumeendelea kutoa msisitizo umuhimu wa kuunganisha taasisi za umma katika miradi inayoendelea.

Kwa kuwa TANESCO tumeipa mamlaka sasa na wao kuendelea kusambaza umeme vijijini kwa bei ya shilingi 27,000 na kwa kuwa imetenga shilingi bilioni 40 na Bunge mmeidhinisha ni wazi maeneo haya ya taasisi za umma yatafikiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, REA na TANESCO wataendelea kushambulia maeneo mbalimbali ili kukamilisha na watanzania wapate fursa ya kutumia umeme kwa bei nafuu ikiwa ni azma ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Ahsante sana.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Kwanza kabisa niwapongeze Serikali kwa kutujengea Mahakama Kuu nzuri na ya kisasa katika Jimbo la Shinyanga Mjini. Swali langu Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Hakimu Mkazi imechakaa sana, actually ilijengwa tangu kipindi cha ukoloni. Nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Mahakama hizo zinakarabatiwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Makamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika mpango wetu kwamba tumetenga fedha za kukarabati majengo yote chakavu nchini na kujenga mapya katika maeneo yale ambayo yana uhitaji huo. Ninakuahidi tu Mheshimiwa Mbunge uvute subira kidogo utaona kazi inaendelea kule kwa ajili ya ukarabati.