Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kiteto Zawadi Koshuma (10 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jina naitwa Kiteto Zawadi Koshuma, ni Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Spka, kwanza kabisa, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, japokuwa muda ni mdogo lakini nitachangia kwa kiasi fulani. Kwanza naomba niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Mwanza ambao wameweza kuniamini ili kuwawakilisha katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niongelee kuhusiana na hotuba ya Rais ambayo ilikuwa nzuri sana na imeweza kugusa nyoyo za Watanzania na kuweza kuwaonyesha Watanzania kwamba Tanzania sasa tunaweza tukawa na matumaini na Tanzania yetu na tukaishi kwa amani na mategemeo makubwa sana kutoka katika nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Rais kabla sijaendelea ili muda usije ukaniishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongelea kuhusiana na mama lishe kitu ambacho kilimgusa sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, alipowaongelea mama lishe alisema Serikali sasa imefikia wakati iwatambue pamoja na shughuli zao wanazofanya. Mama lishe wamekuwa wakidharaulika sana, kama ambavyo Wabunge wengine wametangulia kusema.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikazie kwamba Waziri husika wa TAMISEMI atusaidie kwa kuwasiliana na Halmashauri zinazohusika ili ziweze kuwashirikisha kuhusu ni maeneo gani ambayo ni rafiki kwao kuweza kufanya shughuli zao za mama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mchango mkubwa ambao mama lishe wanao katika jamii yetu. Wengi wetu tunakula chakula kwa hawa mama lishe, lakini pia hawa mama lishe ambao wanatupatia chakula, wanajisaidia na wao kupata kipato, ambapo wanaweza wakatatua matatizo mbalimbali. Kama tunavyojua katika familia, mama pekee ndio mtu ambaye anajua kwamba watoto wamekula nini au baba amekula nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, naomba Serikali sasa ifikie hatua ya kuwatambua hawa mama lishe na kufahamu kazi ambazo wanazifanya kwamba zinachangia katika pato la Taifa na kukuza uchumi wa Taifa, hasa ukiangalia katika kauli mbiu ya Rais ambayo inasema Hapa Kazi Tu na sasa hivi ni kazi tu, hivyo tuwatambue hao mama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia aliguswa sana tatizo la bodaboda. Bodaboda ni vijana wetu ambao, badala ya kutangatanga na kuwaibia watu kwenye mifuko yao wameamua kujiajiri kwa kupitia pikipiki ili waweze kujipatia kipato na hatimaye kutatua matatizo yao. Bodaboda hawa wamekuwa wakipata matatizo ya kuhamishwa kwenye vituo vyao ambavyo wanapaki kwa ajili ya kupata abiria.
Naiomba Serikali yangu ambayo ni sikivu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, iwasikilize hawa watu wa bodaboda, wawawekee vituo ambavyo na wao pia kwao ni rafiki ambapo wanaweza kupata abiria. Hii ni kwa sababu, nimegundua katika Halmashauri nyingi wanapangiwa vituo ambavyo siyo rafiki kwao. Boda boda hupangiwa sehemu ambayo hawezi kupata abiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu sikivu, itusaidie, mshuke kwenye Halmashauri ili muweze kuzishauri kwamba wanapotaka kuwapangia vituo hawa watu wa bodaboda, basi waweze kuwashirikisha ili wao pia wawepo katika kuchangia maamuzi kwamba ni wapi tukae ili kuweza kupata abiria na hivyo basi kuweza kusaidia katika shughuli zao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nichangie upande wa viwanda suala ambalo Mheshimiwa Rais amelipa kipaumbele sana. Suala hili kama ambavyo wengi wametangulia kusema kwamba bila viwanda Tanzania haitaweza kuendelea, lakini sasa viwanda hivi vitaendeleaje kama hatutaweza kuwashirikisha watu ambao tayari wanahusika na viwanda?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika Mkoa ninaotoka, Mkoa wa Mwanza ni Mkoa maarufu sana ambao samaki wa aina ya sato wanapatikana, lakini ni viwanda vichache sana ambavyo viko pale, kama vile Vic Fish, TFP na viwanda vingine lakini ni vichache sana.
Naiomba Serikali yangu inapokuwa inaleta mpango kazi wake, basi iangalie huu Mkoa wa Mwanza na kuufanya kuwa mkoa wenye viwanda. Kwa sababu gani nasema hivyo? Mwanza tunapata samaki…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa mzungumzaji)
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie sentensi yangu. Pale Mwanza pia kuna Kiwanda cha Ngozi...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda tafadhali! (Kicheko)
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/2017-2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa suala la Benki ya Wanawake Tanzania (TWB). Benki hii ilipoanzishwa mwaka 2009 lengo kuu ilikuwa kuwakomboa wanawake kiuchumi kupitia mikopo nafuu, kinyume na matarajio ya wanawake wote nchini, benki hii imekuwa ikitoa mikopo kwa riba kubwa sana, ya asilima kumi na tisa, riba hii imewafanya wanawake kushindwa kufanya biashara zao vizuri, kwa kuwa wanafanya biashara kwa kuhudumia mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeupitia vema Mpango huu wa Miaka Mitano, sijaona mwanamke akipewa kipaumbele, ukizingatia mwanamke hata katika jamii amekuwa mtu wa mwisho kuthaminiwa katika kipaumbele. Hivyo basi, naishauri Serikali, imwangalie mwanamke kwa jicho la tatu, hasa katika Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa, ili kumwezesha kukabiliana na changamoto anazokutana nazo kama mwanamke katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali katika kipaumbele cha fedha katika Mpango huu, basi iongeze mtaji katika Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), kwa kiwango cha shilingi bilioni thelathini, ili ifanye jumla ya mtaji wa benki hiyo, kuwa bilioni hamsini, kwani kwa sasa benki hiyo ina mtaji wa karibu bilioni ishirini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, katika Mpango huu, katika suala la afya, Serikali imeweka mkakati wa kujenga blood bank mikoani. Mkoa wa Mwanza unayo blood bank katika hospitali teule ya Bugando, lakini wanawake wengi hupoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kupungukiwa na damu. Hivyo basi, naishauri Serikali badala ya kujenga blood banks bora inunue majokofu ya kutunzia damu, katika kila Kata na kila Wilaya. Ili kusudi kila kituo cha afya na hospitali ya wilaya, iweze kujitunzia damu, kwa kuwa watu wengi Watanzania hupenda kujitolea damu. Hii itasaidia kupunguza vifo vya akinamama.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naishauri Serikali katika Mpango huu wa Maendelo ya Taifa, kwa kushirikiana na Wizara ya afya itenge fedha za kununulia CT scan katika kila hospitali ya Mkoa, ikiwemo hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwani wananchi hufa kwa magonjwa mbalimbali, ambayo kama kipimo cha CT scan kingekuwepo, mgonjwa angeweza kubainika ugonjwa unaomsumbua ili apatiwe matibabu sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja baada ya kuwasilisha ushauri wangu kwa njia hii ya maandishi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Pili, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia fursa hii ili niweze pia kuendelea kuchangia katika Hotuba hii ya Wizara ya Katiba na Sheria. Ninawashukuru pia wanawake wa Mkoa wa Mwanza ambao waliniamini na kunipa kura nyingi na kuweza kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba kuchangia kwa upande wa Sheria ya Ndoa. Katika Sheria ya Ndoa nimeangalia na kuona kwamba kuna upungufu ambao unafanya sheria hii kukandamiza haki za wanawake katika Sheria ya Ndoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kuna contradictions ambazo zinatokea katika Sheria ya Ndoa. Mtoto wa kike katika sheria hii anaweza akaolewa akiwa na umri wa miaka 16 lakini ukija katika Sheria ya Watoto (Children Act Law) mtoto anajulikana ni mtoto mwenye umri wa kuanzia sifuri hadi miaka 18, lakini kuna sheria ya Sexual Offensive Act, sheria hii pia na yenyewe inakuambia kwamba mtu ambaye anafanya mapenzi na mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 amefanya kosa la jinai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapata wakati mgumu sana kwamba hizi sheria tatu ambazo nimeziangalia zinaleta contradictions na zinamgusa mtoto wa kike, kwa sababu mimi ni mwakilishi wa wanawake siyo tu wa Mkoa wa Mwanza bali ni mwakilishi wa wanawake Tanzania nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, inaniuma sana kuona kwamba mtoto mdogo, tayari umemuita ni mtoto katika Children Act Law, mtoto ni wa umri chini ya miaka 18 lakini kwenye Sheria ya Ndoa unampa mwanaume mamlaka ya kumchukua huyu mtoto asiyekuwa na hatia, ambaye psychologically akili yake bado haijaweza kufikiria lolote kuhusiana na suala zima la ndoa. Lakini umempa mamlaka mwanaume aweze kumchukua mtoto huyu na kumweka unyumba kitu ambacho naona ni unyanyasaji kwa mtoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, ninaitaka Serikali itakapokuja kujibu hoja za hotuba yake basi ije na kauli moja, kwamba inasema nini kuhusiana na hizi contradictions ambazo zinatokea katika hizo sheria tatu ambazo nimeziainisha hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusiana na kesi kurundikana katika mahakama zetu. Kesi zimekuwa ni nyingi sana zinarudikana kwenye mahakama na kufanya mahabusu kuwa wengi kwenye mahakama zetu. Lakini ukiangalia katika kesi hizo siyo wote wanaoenda kushtakiwa mahakamani wana makosa, wengi wao wamekuwa wakibambikwa kesi. Mfano mtu kaiba kuku lakini kwa sababu kuna fisadi mmoja ambaye amejificha somewhere anataka kumtumia huyu mtu ambaye ameiba kuku tu basi ahukumiwe kwa kesi ya kuiba kuku, lakini mtu huyu anapewa kesi ya mauaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha sana unajiuliza Taifa letu la Tanzania tunaelekea wapi. Kwa uchungu mkubwa sana ninaiomba Serikali ianze kuangalia kesi hizi, japokuwa kwa juhudi za Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli amelikemea sana suala hili la kesi kurundikana mahakamani hadi akaweza kuwaongezea Majaji fedha kwa ajili ya kuweza kuendesha kesi, lakini bado kesi zinaendelea kurundikana mahakamani na kesi nyingi kwa kweli ni zile za kusakiziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naiomba Serikali itoe tamko kwa vyombo hivi vya kisheria ambavyo vinasimamia reinforcement ya sheria kwamba ni nini kinatakiwa kifanyike kwenye kesi ambazo ziko mahakamani ili kuweza kupunguza watuhumiwa hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni kuhusiana na utoaji wa haki na utawala wa sheria. Kwa masikitiko makubwa sana na hata kama ni kulia ningeweza kulia mbele ya Bunge lako Tukufu, wanawake wamekuwa wakinyanyasika sana, mwanamke utakuta amepigwa na mume wake, anakwenda kushtaki polisi mwanaume anapelekwa mahakamani, lakini bado mwanamke huyu anaoneka kwamba ilikuwa ni halali kwa mwanaume kumpiga huyu mwanamke kana kwamba ni ngoma yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ijaribu kuangalia suala zima la wanawake kunyanyasika katika utoaji wa haki zao. Unakuta kwa mfano, hapa sijui ni sheria gani inahusika lakini unakuta mwanamke ameolewa na mume wake kwa ridhaa yake na wanaishi vizuri, baada ya muda mfupi mwanamke huyu na mwanaume wanaamua kutengana kwa sababu labda wametofautiana baadhi ya vitu. Katika utofauti huo basi unakuta mwanaume anapofika Mahakamani kwa ajili ya kutoa talaka, mwanamke huyo anapopewa talaka anaambiwa nenda halafu mali zote anaachiwa mwanaume.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha sana kwa sababu ni wanawake wengi sana afadhali hata wale ambao wamejaliwa basi hata kusoma wamepata elimu wanajua ni jinsi gani wataweza kujikwamua kuondokana na unyanyasaji huu ambao tunaupata kutoka kwa wanaume. Lakini vipi wale kundi kubwa la wanawake ambao hawajakwenda shule? Hawajui ni nini wafanye?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kwa kushirikiana na Wizara husika waweze kuangalia dawati la kijinsia ambalo lipo lakini kiuhalisia halina kazi linayofanya. Ninaitaka Serikali sasa ianze kuangalia masuala ya kusaidia utoaji wa haki kwa wanawake na kuhakikisha kwamba wanawake wote wanapatiwa haki zao. Kwa sababu wanawake wengi wamekuwa wakinyimwa haki zao hata pale wanapofiwa na waume zao. Wajane wameteseka, wamenyang‘anywa mali na kuondoka bila chochote, wanabaki wanahagaika mtaani wakati ndugu wamebeba mali zote wameondoka wanajisifia mtaani kwamba wanazo mali halafu mwanamke huyu anaanza kukanda maandazi, anauza karanga, anafunga ufuta ili mradi maisha yake yaweze kusogea. Inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuongelea kuhusiana na kesi za Serikali. Inasikitisha kwamba Serikali inakuwa na kesi nyingi sana, inashitaki watu kwa kufanya makosa, lakini kesi zote almost 99 percent ya kesi za Serikali inapoteza ama Serikali inashindwa. Ninaitaka Wizara ije iseme, itoe tamko lake kwamba kwa nini Serikali inapoteza kesi nyingi? Ni kwa sababu gani kesi ziwe nyingi Serikali inashindwa? Kesi 1000 Serikali inashinda kesi mbili tu, inasikitisha sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia kwa kuongelea kuhusiana na suala zima la majengo ya mahakama ambayo yamechakaa sana. Naomba Serikali katika bajeti yake iangalie ni namna gani itaweza kusaidia kufanya renovation ya majengo ya mahakama Tanzania nzima kwa sababu ya kuweza kuwasaidia wananchi kupata haki zao lakini pia kuongeza watumishi katika Mahakama zetu. Kwa sababu upungufu wa watumishi ume-deprive haki za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nimalizie kwa kukushukuru sana na kumshukuru Mungu kwa sababu ya kutoa speech hii ahsante sana. Naunga hoja mkono ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwa maandishi katika Wizara hii. Kwanza nianze na suala la wabunifu wa teknolojia katika nchi hii. Nchi hii wapo watu ambao wana ubunifu wa kutumia teknolojia, lakini hawajulikani wala kutambulika na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa Kampuni ya Young Scientist Tanzania ambayo huwasaidia kuwaendeleza vijana chipukizi wa ubunifu na teknolojia, Kampuni hii mwaka huu imewapa tuzo vijana wawili wa Shule ya Sekondari Morogoro ambao ni Edmund na John Method. Pia vijana hao Kampuni imewapelekea kusoma Dublin University huko Ireland kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao vya ubunifu na ufumbuzi wa teknolojia. Nashauri Serikali iwe inafuatilia vijana wabunifu kama hawa ili wanapomaliza masomo yao, Serikali iwashawishi kurudi nchini ili kutumia ujuzi wao kusaidia maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuboresha mishahara ya Walimu pamoja na mazingira ya kufanyia kazi kama vile nyumba, umeme na maji. Hii itaondoa upungufu wa Walimu mashuleni hususan shule za pembezoni mwa Miji. Walimu wengi wanapopelekwa au kupangiwa na Serikali shule za vijijini huwa hawaendi kutokana na mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahitaji kuongeza juhudi katika kutoa elimu bora ili kushindana na nchi nyingine duniani. Nasema hivi kwani wanafunzi wengi humaliza Kidato cha Nne ambayo ni elimu ya awali bila kujua kusoma na kuandika vizuri, lakini pia hata kutokuwa na uwezo na kujieleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na namshukuru Mungu kwa kuendelea kunipa uwezo wa kushiriki katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu, mama ambaye ameufahamu wajibu wake kwa nafasi aliyopewa kwa kuwaangalia wanawake wa Tanzania kwamba wana upungufu wa damu na hivyo kuweza kuhamasisha katika Mkoa wa Dodoma na watu wamekwenda kujitolea damu. Tunaamini kwamba mama yetu Mama Samia Suluhu ataendelea kutambua na mikoa mingine kwamba wanawake wengi wanakufa kila siku kwa ajili ya upungufu wa damu pale wanapokwenda kujifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pongezi hizo, sasa naomba nijikite katika kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Afya. Natokea Mkoa wa Mwanza ambapo tuna Wilaya ya Ilemela ambayo bado ni changa ilianzishwa mwaka 2012. Kwa masikitiko makubwa sana Wilaya ya Ilemela hakuna Hospitali ya Wilaya. Kwa bahati mbaya sana Halmashauri ya Ilemela wakati imekatwa kutoka kwenye Halmashauri ya Jiji la Nyamagana iliomba shilingi milioni 300. Baada ya kupatiwa fedha hizo Halmashauri hii imeweza kutumia shilingi milioni 193 kuanzisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana kwa kuanza na jengo la emergence. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilipokuwa nikitazama kwenye vitabu mbalimbali vya bajeti ya Wizara ya Afya sijaona ni wapi ambapo Serikali imetenga pesa kwa ajili ya kuweza kutusaidia Wilaya ya Ilemela kujenga majengo yetu ya Hospitali ya Wilaya ya Ilemela. Hivyo basi, namuomba Waziri wa Afya, dada yangu pale, aweze kutusaidia kiasi ambacho kimeombwa na Halmashauri ya Ilemela shilingi bilioni mbili na milioni mia tatu kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ilemela. Nitamuomba Waziri wetu wa Afya anaporudi kujibu hoja basi atusaidie kutueleza ametenga kiasi gani au Serikali imetenga kiasi gani kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea suala la upungufu wa dawa. Tumeona katika Mkoa wa Mwanza limefunguliwa duka la MSD, lakini kwa masikitiko makubwa sana dawa katika lile duka hakuna. Namuomba Waziri aweze kufanya uchunguzi kwamba katika hilo duka ni dawa gani zimepelekwa au hizi dawa zimeishia wapi. Yawezekana dawa zimepelekwa lakini zimebaki zina-hang somewhere na hazijaweza kufika katika hili duka la MSD ambalo limefunguliwa pale katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, Mkoa wa Mwanza hakuna mashine za CT-Scan. Watu wengi wamekuwa wakifa kutokana na matatizo ya ubongo. Tunafahamu kabisa CT-Scan ina uwezo wa kutambua mgonjwa ana matatizo gani kwenye kichwa ili kuweza kuepuka mgonjwa kupata stroke. Tumeweza kuwa na wagonjwa wengi sana ambao wanapata stroke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri atakapokuja aje na majibu sahihi tena ya uhakika kwamba katika Mkoa wa Mwanza hususani Hospitali ya Bugando ambayo imesemekana kwamba kuna CT-Scan lakini ninao uhakika wa asilimia mia moja, hata sasa hivi Waziri akisema tupande ndege twende Mwanza au twende kwa basi au kwa gari gani lakini twende Mwanza sasa hivi tukakague Hospitali ya Bugando CT-Scan hakuna. Naomba sana Wizara yetu iweze kuwa makini katika kuangalia vifaa ambavyo vinakuwa vinapelekwa je vimefika au havijafika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukazia kuomba CT-Scan katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Sekou-Toure. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy aliahidi na kusema kwamba CT-Scan itapelekwa mara moja iwezekanavyo. Hivyo basi, nakuomba Waziri wakati ukiangalia bajeti yako utusaidie pale Mwanza utupelekee CT-Scan katika Hospitali yetu ya Rufaa pale Mwanza ya Sekou- Toure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza inazo kata 19. Mheshimiwa Rais alitoa ari kwamba kuwepo na vituo vya afya katika kila kata, lakini pawepo na zahanati katika kila kijiji. Kwa masikitiko makubwa sana Wilaya ya Ilemela tunazo kata kumi na tisa lakini tuna vituo vya afya vitatu kikiwepo Kituo cha Sangabuye, Bugogwa pamoja na Karume. Kwa bahati mbaya hivi vituo vyote vitatu havina hadhi ya kuitwa vituo vya afya. Ukiangalia katika Kituo cha Karume hakina huduma nzuri, vitanda hakuna, kuna vitanda viwili tu, hakuna kitanda cha akina mama kujifungulia, huduma ya kufanyiwa upasuaji akina mama pia hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Ummy kwa kuwa na wewe ni mwanamama na unafahamu kabisa kina mama tunapopata matatizo wakati wa kujifungua, utusaidie. Kwa kuwa umesema akina mama wengi wanapoteza maisha wakati wakipata haki yao ya msingi ya kutuletea watoto hapa duniani, naomba utusaidie basi kutuboreshea vituo vya afya hivi vichache tu ambavyo vipo katika Wilaya ya Ilemela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namuomba pia Waziri aweze kuisaidia Halmashauri ya Ilemela kwani ni change, kila inapotenga pesa kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma bora za afya haiwezi kufanikiwa kwa sababu inakuwa ina majukumu mengi na hivyo kuielemea halmashauri. Hivyo, namuomba Waziri aweze kutusaidia basi Wilaya ya Ilemela tuondokane na hivi vituo vitatu basi walau atuongezee vituo viwili ili tuweze kusogeza huduma karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia leo nilikuwa sina mengi sana lakini naongelea pia kuhusiana na suala zima la Benki ya Wanawake. Naomba Serikali iweze kuiangalia hii Benki ya Wanawake. Mheshimiwa Mbunge ambaye amechangia katika hili suala la huduma ya Benki ya Wanawake amesema kwamba Serikali imetenga shilingi milioni 900, ninasita mimi katika kusoma bajeti ya Serikali, nimeona Serikali imetenga shilingi milioni 500 tu na siyo shilingi milioni 900. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri Ummy aliwahi kusema kwamba atatoa shilingi bilioni mbili kila mwaka. Kwa mwaka huu wa fedha kama Serikali imetenga shilingi milioni 500 tu sioni kama tutafikia malengo ya kuweza kuiendeleza Benki hii ya Wanawake hapa Tanzania. Ukiangalia benki hii sasa hivi ina mtaji wa shilingi bilioni 20 tu peke yake. Kwa hiyo, kama katika mwaka huu watafanikiwa kuongeza hizo shilingi milioni 500 ambazo zimetengwa bado benki hii haiwezi kuwasaidia wanawake. Hakuna matawi mengi hapa nchini, kuna matawi machache sana ambayo yako kwenye mikoa michache nadhani ni mitano au nane...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini pia, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuipongeza Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na hasahasa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Lukuvi pamoja na Mheshimiwa Mama yangu Mama Angelina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea suala zima la National Housing, kama walivyochangia Wabunge wengi kuhusiana na suala la National Housing kujenga nyumba ambazo zinaonekana ni nyumba za bei nafuu kwa kinadharia tu, lakini nyumba hizi si kwa ajili ya wale wananchi wasiojiweza kwa sababu, nyumba hizi za National Housing ni nyumba ambazo ni za gharama sana. Kwa mfano, katika Hotuba yake Mheshimiwa Waziri page number 58 mpaka page number 61 ameonesha kwamba nyumba za National Housing zinajengwa ili kuweza kuwasaidia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia hapa mfano Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ilemela tunazo nyumba za National Housing ambazo zimejengwa Buswelu. Nyumba hizi zilikuwa ni nyumba nzuri, lakini sasa zinauzwa bei ya juu, zinauzwa kwa gharama ya shilingi milioni 80, sasa najiuliza je, mwananchi wa hali ya kawaida, hali ya chini, anao uwezo wa kununua nyumba ya shilingi milioni 80?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomwambia kwamba, aende kuchukua mkopo benki, tunafahamu wote kwamba, unapoenda kuchukua mkopo benki unaulipa kwa riba. Hivi kweli, je, tunaposema hii nyumba inauzwa milioni 80 mwananchi huyu aende kuchukua mkopo benki unakuwa umemsaidia mwananchi wa hali ya chini au unakuwa sasa umezidi kumgandamiza. Hii ni kwa sababu, anapokwenda kuchukua mkopo benki riba itakuwa ni kubwa; akikopa milioni 80 anaweza akarudisha milioni 120 kwa hesabu za harakaharaka kwa sababu, mimi pia ni mtaalam wa masuala ya benki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naishauri Serikali iweze kusaidia shirika hili. Kwa mfano, shirika hili ukiangalia mara nyingi wanasema kwamba, nyumba hizi zinakuwa ni za gharama kwa sababu ya kupitisha miundombinu kwa sababu halmashauri zinakuwa zimewapa eneo lakini miundombinu kama vile maji, umeme, barabara, inakuwa haipo. Kwa hiyo, nashauri kwamba, basi Serikali au Wizara husika isaidie kupitisha miundombinu ya barabara, maji pamoja na umeme, ili pale shirika hili linapoanza kujenga hizo nyumba basi ziwe za bei rahisi, ili kuweza kuwakwamua wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, niweze kuishauri Serikali kwamba, Shirika la National Housing liweze kujenga nyumba za bei nafuu kwenye makazi ya vijijini kwa sababu, vijijini ndiko sehemu ambako tuseme asilimia kubwa ya wananchi hapa nchini Tanzania wanaishi, lakini makazi yao bado ni duni sana. Kwa hiyo, naishauri Serikali kupitia Shirika lake hili la National Housing kujenga makazi ya bei nafuu huko vijijini.
Mheshimiwa Mweyekiti, lakini pia, ukiangalia sehemu nyingi za vijijini tayari kunakuwa kuna makazi yamekwishajengwa pale, kulikoni Serikali iende kujenga sehemu nyingine, naishauri Serikali kwamba, itumie lile eneo la kijiji husika kubomoa zile nyumba zilizopo kwa kuwapa elimu wananchi kwamba, ni kwa nini nyumba zinabomolewa, lakini kuweza kunyanyua majengo aidha ya magorofa au majengo ya kawaida, ili wananchi wa eneo hilo waweze kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia maeneo mengi ya watu wanaoishi vijijini ni wakulima. Kwa hiyo, watakapokuwa wamejenga nyumba zile wananchi wanaweza wakapangishwa au wakauziwa kwa bei nafuu na wakulima hawa wakaweza kulipa kidogo kidogo hatimaye kumaliza deni na nyumba kuwa za kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la squatters, squatter imekuwa ni suala ambalo ni sugu sana hapa nchini Tanzania. Naishauri Serikali kwamba, izisaidie fedha Halmashauri, ili ziweze kusaidia kurasimisha makazi na hii inaweza ikasaidia Serikali pia kupata mapato kwa sababu, katika hizi squatter hawa wananchi wanalipa tu mapato kwa Halmashauri lakini Serikali inakosa mapato kwa kupitia property tax. Kwa hiyo, nashauri Serikali iweze kuzisaidia halmashauri hususan Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ilemela, watusaidie fedha kwa ajili ya kurasimisha makazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia wakazi wa Mkoa wa Mwanza wanaishi sana kwenye milima, matokeo yake tunaona disaster zinatokea, wananchi wanaangukiwa na mawe. Kwa hiyo, utaona kama maeneo yale yakiweza kupimwa na Serikali na kuweza kurasimishwa kwa wananchi kihalali, basi tutakuwa tumeondokana na hizo disaster za wananchi kuangukiwa na mawe pia hata kuondoa hili suala zima la bomoabomoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikijiuliza, kuna tatizo moja limetokea hapo Mkoani Mwanza, Wilaya ya Ilemela, kuna rada imejengwa katika Mlima wa Kiseke, rada ile imesababisha makazi 500 sasa yatakwenda kubomolewa ili kupisha rada hiyo ya Mlima huo wa Kiseke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza, hivi wakati hawa wananchi wanaanza kujenga kuanzia nyumba ya kwanza mpaka zimefika nyumba 500 na sasa zinahitajika kubomolewa, Serikali ilikuwa wapi? Haikuwaona hawa wananchi toka wanaanza kujenga nyumba moja mpaka zinafika nyumba 500? Leo hii waseme kwamba, wanataka kuzibomoa nyumba hizo, ili wananchi hawa wapishe eneo hilo la rada, kwa sababu, kwa kweli ni eneo ambalo limekuwa ni hatarishi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri sana Serikali, wananchi wanapovamia sehemu moja kwenda kujenga, basi mwananchi wa kwanza anapoanza kujenga ile nyumba moja, Serikali iweze kutoa elimu kwa wale wananchi, ili wasiendelee kuathirika pale nyumba zinapokuwa nyingi na hatimaye kubomolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, mtakapokuja kuhitimisha hoja hii mnisaidie tu kunipa majibu kwamba, je Wananchi wale wa Kiseke wategemee nini? Je, watalipwa fidia? Kama watalipwa fidia, ni vigezo gani vitatumika kuangalia katika kulipa fidia hizo? Hilo naomba sana mnisaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuongelea suala zima la hizi mashine ambazo zilitolewa na Shirika la National Housing, mashine za kufyatulia matofali kwa vijana wetu. Ukiangalia mashine hizi za kufyatulia matofali kwa kweli zina malengo mazuri tu; kwanza ni kupata ajira kwa vijana, lakini pili, kujenga nyumba ambazo ni za bei nafuu na pia ni imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vijana hawa wameshindwa kupata soko la kuuza haya matofali ambayo wamepatiwa hizo mashine na hatimaye hata kuna mikoa ambayo iliathirika na wakanyanganywa hizo mashine kwa mfano Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini je, Serikali kwa nini inashindwa kuwasaidia hawa vijana ili wanapokuwa wanafatua yale matofali basi wapate tenda hususani kwenye halmashauri zetu, wapate tenda za kujenga. Lakini unakuta kwamba kwenye halmashauri wanatoa tenda kwa watu wengine na wanatumia matofali haya ya kufyatua ya kawaida. Hivi hawa vijana ambao mmewapa hizi mashine kwa nini Serikali isiwasaidie ili na wao waweze kujiendeleza? Pia na hizi Halmashauri nazisihi kwamba ziendelee kutoa mitaji kwa hawa vijana ambao wamegawiwa hizo mashine za kufyatua matofali ili waweze kusaidia kufyatua matofali mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo sikuwa na mengi, ni hayo tu, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na pia namshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye anaendelea kunijaalia afya njema ili na mimi niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu hasa katika Wizara hii ya Fedha na Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niipongeze Wizara ya Fedha kwa sababu imekuja na mpango ambao wananchi sasa wanaanza kuwa na imani kwamba kama mpango huu utatekelezwa basi wananchi wote wataenda kufaidika na nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika michango yangu. Kwanza kabisa naomba kuchangia suala zima la Deni la Taifa. Ukiangalia Deni la Taifa, faida zake kubwa sana ni katika kusaidia kuchangia katika maendeleo ya Taifa hususan katika kuendeleza miundombinu kama vile barabara, viwanja vya ndege, reli na hata kwenye afya pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kusikitisha sana ni kwamba Deni la Taifa limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, ninazo data kidogo hapa; mwaka 2005 hadi mwaka 2010 Deni la Taifa lilikuwa yapata trilioni 10; mwaka 2010 hadi mwaka 2012 Deni la Taifa liliongezeka hadi kufikia trilioni 14, lakini mwaka 2015 hadi sasa Deni la Taifa sasa limefikia trilioni 41; hii inasikitisha sana. Kwa sababu gani nasema inasikitisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Deni la Taifa linaongezeka lakini wananchi bado hali inazidi kuwa ni ngumu. Swali langu sasa kwa Waziri, na naomba Waziri atakapokuja anisaidie walau kunipa majibu lakini si mimi peke yangu wala Bunge lako hili Tukufu bali hata wananchi wote wanaonisikiliza sasa hivi, kwamba; ni kwa sababu gani deni hili lime-shoot kutoka trilioni 14 mwaka 2012 hadi kufikia trilioni 41 kwa mwaka 2015. Ninaomba Waziri atakapokuja basi aje na ufafanuzi utakaoweza kuwasaidia wananchi wa Tanzania kuelewa ni kwa nini deni hili linazidi kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia na Wabunge wenzangu deni hili linapokuwa linazidi kuongezeka ni kwamba kila Mtanzania katika nchi yetu anazidi kuwa na ongezeko la kulipa deni hili. Kwa mahesabu, bahati mbaya hesabu nilipata “F” kwa hiyo, sijui namna ya kupiga deni hili kwa kila Mtanzania lakini mtanisaidia pamoja na Waziri, kwamba hivi deni hili ni lini basi litaweza kuwafaidisha wananchi wa Tanzania. Deni linaongezeka, barabara bado ni mbovu, kila Mbunge akisimama hapa wakati wa kipindi cha maswali na majibu hata wakati wa maswali ya nyongeza utasikia kila mtu analalamika kuhusiana na suala zima la barabara lakini hata hivyo, masuala ya maji, kila Mbunge anasimama hapa akiwakilisha wananchi wake kwa kulalamikia suala la maji. Hivi kwa nini Deni la Taifa linazidi kuongezeka? Ninaomba na ninamtaka Waziri atakapokuja anieleze tu ni kwa nini Deni la Tafa linazidi kuongezeka na wakati wananchi bado wana maisha ya chini au la sivyo naomba nitoe taarifa kabisa kwamba nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri itakapofika muda wake, kama hatakuja na majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Nampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu amesaidia. Tunaona kabisa ongezeko la mapato hapa nchini sasa limeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna changamoto ambazo zipo. Kwa mfano, baada ya kuongezeka kwa mapato haya, Halmashauri zetu hazifaidiki na ongezeko la Pato la Taifa. Nasema hivyo kwa sababu kwenye Halmashauri zetu kuna kero mbalimbali ambazo zimefutwa ambazo zimekuwa zikiwakera wananchi, na hata Mheshimiwa Rais nae pia amekuwa akiziongelea kero hizi. Baada ya kero hizi kufutwa hakuna mbadala wa mapato ambao umekuwepo katika Halmashauri zetu na ndiyo maana unakuta kwamba hata Halmashauri inapotenga fedha kwa ajili ya kuondoa changamoto za barabara, maji hata afya, hawawezi kufikia malengo yao kwa sababu ongezeko la pato katika Halmashauri zetu – mapato yanapokuwa yanakusanywa malengo ya Halmashauri yanakuwa ni makubwa kiasi cha kwamba Halmashauri zinashindwa hata ku-prioritize kwamba tuanze na lipi na tumalizie na lipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi ninaishauri Serikali walau katika Wizara hii kwa sababu Wizara hii ndiyo Wizara ambayo inakusanya mapato ya Taifa kwa ukubwa kabisa. Wizara hii naweza nikaisema kama ni Wizara nono, Wizara ambayo imeshiba, basi tunaomba kwamba Wizara ya Fedha iweze kupeleka fedha ziwafikie wananchi hasa katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mdogo tu; katika Halmashuri zetu tuna mpango mzuri sana ambao tumeuweka wakuzitenga asilimia10 ambayo asilimia tano inatakiwa kwenda kwa wanawake na asilimia tano iende kwa vijana. Lakini ukiangalia Halmashauri nyingi kwa tathmini ya haraka haraka zimekuwa hazitengi fedha hizi na si kwa sababu wanafanya makusudi kutokutenga fedha hizi iliziweze kuwafikia wananchi, lakini ni kwa sababu ya kulemewa na mzigo wa mipango ambayo wanakuwa nayo kiasi cha kwamba ile fedha hata kama inakuwa imetengwa matokeo yake inakuja kufanya dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; nikiongelea katika Jimbo la Ilemela ambalo ni Jimbo la Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi Mama Angelina Mabula, kule tumekuwa na mipango mizuri sana, kila mwaka wamekuwa wakitenga fedha hizi lakini inapofika wakati kwamba sasa fedha hizi ziweze kugawiwa kwa wananchi hasa wanawake na vijana unakuta fedha hizi zinatumika katika kutengeneza barabara. Ukiangalia katika Wilaya ya Ilemela, ni Wilaya ambayo bado Halmashauri yetu ni changa. Ninaitaka na ninaiomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa sana kwamba iweze kuangalia Halmashauri zetu ili basi waweze kuongezewa fedha walau ziweze kuwasaidia wanawake hususan akina mama kama vile mama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mzunguko wa fedha umekuwa ukionekana kama unaishia huku juu tu, yaani unaishia kwenye sehemu za juu, yaani wananchi wa hali ya juu ndiyo ambao wanafaidika na pesa. Sasa unapoongelea Pato la Taifa limeongezeka wakati mwananchi wa chini bado fedha haijamfikia ni masikitiko makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninamuomba Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake anisaidie tu kuja na mikakati kwamba Serikali imejiwekea mikakati gani ya kuziba mianya ya fedha ambazo imekuwa ikipoteza, kwa sababu inawezekana tukakusanya pesa nyingi lakini wako watu ambao kazi yao wamekaa kuchungulia hizi pesa na kuweza kujinufaisha wao wenyewe matokeo yake wananchi hawafaidiki na fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee suala la shilingi milioni 50 kila kijiji. Tulipokuwa tukizunguka katika kampeni zetu za mwaka huu. Kila mwananchi anakuuliza kuhusiana na suala la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Swali kwa Waziri ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kila mwananchi ananufaika na pesa. Ukiangalia kwa mfano katika ukurasa wa 24 Maoni ya Kamati au Uchambuzi wa Kamati, unaonesha kwamba Tanzania tunavyo vijiji 19,600, tunahitaji shilingi bilioni 980. Serikali imetenga asilimia sita tu ambayo ni shilingi bilioni 59 na milioni 500. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata nisipoendeea kusoma taarifa hii ya Kamati lakini utaona kabisa kwamba tunayo changamoto ambayo bado ni kubwa sana kwa sababu inaonesha wazi sasa ni vijiji vichache sana, yapata vijiji 1,000 ndiyo ambavyo vitafaidika na hii shilingi milioni 50. Ni masikitiko makubwa sana. Hivi tunaenda kurudi vipi kule kwa wananchi? Tutawaeleza nini wananchi wetu kuhusiana na suala la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji? Naiomba Serikali ifuate ushauri ambao umetolewa na Kamati ya Bajeti kwamba waongeze pesa walau ifikie asilimia 20 japokuwa na fedha hii bado ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba Sheria ya Manunuzi iletwe…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili pia niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu. Pia naendelea kumshukuru Mungu kwa sababu ameendelea kunipigania na kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoanza kuchangia Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2017/2018 nitapenda sana niwapitishe katika kitabu hiki kwa kutumia pages. Kwanza kabisa, naomba tuangalie ukurasa wa pili wa Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa, kifungu cha 1.4 kinazungumzia utaratibu wa kuandaa Mapendekezo ya Mpango. Katika utaratibu wa kuandaa Mapendekezo ya Mpango umeangalia mambo mbalimbali ikiwemo hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati anafungua Bunge la Kumi na Moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anafungua Bunge hili la Kumi na Moja wote tulimsikiliza kwa makini. Mheshimiwa Rais aliongea vizuri sana na hotuba yake ilikuwa inalenga katika kuwakomboa wananchi wa Tanzania. Mheshimiwa Rais aliongea mambo mengi sana na moja ya jambo ambalo alisisitiza ni viwanda. Mheshimiwa Rais alisisitiza kwamba anataka Tanzania iwe ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimepitia mpango huu vizuri sana, ukiangalia viwanda vimeongelewa kwa kuguswaguswa, nasikitika sana kusema hilo. Kwa maana kwamba mpango haujajikita katika kusema waziwazi kwamba ni viwanda gani ambavyo sasa vinaenda kuangaliwa na mpango huu. Hivyo basi, napata wasiwasi kama kweli sisi tuko tayari kufuata ushauri ambao Mheshimiwa Rais alikuwa akiuongea? Aliongea katika kampeni zake, aliongea katika kulifungua Bunge hili na mpaka sasa bado Mheshimiwa Rais anaendelea kuongea na kusisitiza kuhusiana na suala zima la viwanda, napata wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kwamba anapotuletea mpango mwezi Mei nadhani baada ya kuchukua mapendekezo yetu Waheshimiwa Wabunge, namsihi sana katika mpango wake atuelezee ni viwanda gani hasa ambavyo anaenda kuviweka katika mpango wake. Vivyo hivyo atakapokuja kutenga bajeti atenge bajeti ambayo kweli ita-reflect kwamba sasa Tanzania inaenda kuwa Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la maji. Hatutaweza kuwa na viwanda nchini Tanzania na hatutaweza kamwe kufikia malengo ya Mheshimiwa Rais ambayo ni malengo mazuri sana kama haitakuwa Tanzania ambayo wananchi wa kawaida, mwananchi aliyeko kijijini anaweza akapata maji wakati wowote atakapoyahitaji. Nasema hivi kwa sababu gani? Maji ni kiungo kikubwa sana kwani yanaweza yakasaidia katika kilimo. Ukiangalia sasa hivi naweza nikasema nchi hii inaelekea kwenye jangwa kwa sababu hakuna maji kabisa. Nchi imekuwa na ukame na hata watu wa Idara ya Hali ya Hewa pia wametabiri kwamba sasa hivi hakutakuwa na mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Mwanza kuna kilimo cha pamba na mazao mengine mbalimbali lakini wananchi wanashindwa kulima kwa sababu ya ukosefu wa maji. Hata hivyo, ukiangalia katika mpango huu, kama ninavyosema na nitarudia kusema maji yanatajwa tu kwamba maji, maji yanafanya nini? Tuna mikakati gani kwamba maji sasa yanaenda kupatikana Tanzania? Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mipango atakapoleta mpango atuletee mpango mkakati kwamba anaenda kufanya nini ili kuhakikisha kwamba Tanzania inaenda kuwa na maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kuna suala pia la irrigation scheme, nimeliona limetajwa humu katika mpango lakini halioneshi dhamira kwamba kweli tunataka kufanya irrigation scheme hapa nchini Tanzania ili kuwezesha kilimo ambacho ndicho kitakachotupeleka kwenye viwanda. Kwa sababu tutakapoanzisha viwanda tunatarajia kuwa na raw materials, tunaenda kupata wapi hizi raw materials kama hatutaweza kuimarisha kilimo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena niongelee suala kubwa sana ambalo Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, ameliongelea wakati wa kampeni zake. Wakati wa kampeni zake akifanya ufunguzi pale Jangwani aliongea kwa ari kubwa sana na alikuwa anamaanisha. Najua anamaanisha kwa sababu niliona jinsi alivyoongea. Hakuna mtu aliyemtuma kuongea, alijituma mwenyewe kwa sababu anao uchungu na anayo nia ya kuwasaidia Watanzania ili waondokane na umaskini. Mheshimiwa Rais alisema kwamba atahakikisha Serikali yake inatoa milioni 50 katika kila kijiji, hii ni katika kuwawezesha Watanzania kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitisha bajeti hapa niliongea kwa uchungu sana kuhusiana na suala la milioni 50. Nashukuru kwamba Serikali ilisikiliza na ikaongeza pesa kidogo hadi kufikia kutenga bajeti ya shilingi bilioni 49. Hata hivyo wakati nikichangia katika bajeti iliyopita nilisema kwamba shilingi bilioni 49 ambazo zimetengwa bado hazitoshi. Tuna vijiji 13,000 hizi hela ambazo zimetengwa bado ni ndogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, natambua juhudi za Serikali, natambua juhudi ambazo Mheshimiwa Waziri wa Fedha anazifanya kuhusiana na suala la kutimiza ahadi ya Rais ya milioni 50, ili kuweza kuwakomboa Watanzania kutokana na umaskini, namwomba na ninamsihi sana katika mpango wake ajaribu kuelezea ni vijiji vingapi ambavyo vitaweza kupata hii shilingi milioni 50. Atuoneshe na atuelezee wazi kwa sababu tunapata kigugumizi tunapozunguka kwenye Majimbo yetu, wananchi wameandaa vikundi mbalimbali wamevi-register, wako kamili wanasubiri milioni 50 ya Mheshimiwa Rais, lakini sasa kama hatutataja kwenye mpango wananchi tutawaambia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapoleta mpango uwe umejumuisha ni vijiji vingapi, vitapata shilingi ngapi, ni mkoa gani kwa Tanzania nzima? Hivyo vijiji avitaje ili tuweze kufahamu kwamba sasa mimi Mkoa wangu wa Mwanza vijiji kadhaa vitapata na Mkoa wa Tanga vijiji kadhaa vitapata. Naomba sana kuishauri Serikali kuhusu hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea suala la afya. Juzi nilisimama hapa kwa uchungu mkubwa sana na nikasema kuhusiana na suala la dawa. Kumekuwa na upungufu wa dawa na hata Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu alikiri kuwepo kwa upungufu wa dawa. Tumekuwa tukiilaumu Wizara ya Afya ambapo sasa hivi naomba kabisa niombe radhi kwa Wizara ya Afya kwa sababu naamini kabisa nimewakosea kuwaonea nilitakiwa nimlaumu Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa sababu yeye ndiye ambaye anahusika na suala zima la kutenga fedha kwa ajili ya dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wa Mipango atakapoleta Mpango katika Bunge hili, atuoneshe wazi kwamba sasa ni fedha kiasi gani au ni mikakati gani aliyonayo ya kuhakikisha dawa zinapatikana Tanzania nzima ili akinamama wasiteseke. Akinamama ambao wanateseka ni wajawazito wanakwenda kwenye hospitali wanaishia kupimwa ujauzito tu basi, kuangalia vipimo kwamba mimba imefikia katika hatua gani lakini dawa hakuna! Inapotokea anapata tatizo lolote mama huyu anaandikiwa dawa anaambiwa nenda kanunue kwenye pharmacy, pesa hana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunayo nia ya kuwasaidia Watanzania namsihi sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu nadhani bado upo, dakika 15?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Pia naomba
nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye
ameweza kunijalia afya njema ili niweze kuendelea kutoa
michango yangu katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze
kuongelea suala zima la uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 15
ameongelea suala la uwezeshaji wanawake kiuchumi na
ukisoma pale ndani ameandika kuhusiana na maendeleo
ya wanawake kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake
wa mwaka 2007 ambao unalenga kuwawezesha wanawake
kiuchumi ili waweze kukopesheka. Lakini kwenye bajeti ya
mwaka 2016/2017 Mfuko huu wa Maendeleo ya Wanawake
haukutengewa fedha zozote. Naomba niiombe Serikali
itusaidie kutenga fedha kwa ajili ya kuuwezesha huu Mfuko
wa Maendeleo ya Wanawake ili wanawake waweze
kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa nina kikao na
wanawake wa Mkoa wa Mwanza, kwa kweli swali zito
ambalo nilikumbana nalo ni huu Mfuko wa Maendeleo ya
Wanawake. Wanauliza Mfuko huu wa Maendeleo ya
Wanawake unawasaidiaje wanawake ili waweze
kujishughulisha na masuala mazima ya uchumi? Ukiangalia
wanawake wengi wa Mkoa wa Mwanza wanajishughulisha
na shughuli mbalimbali kama vile mama lishe hata
wamachinga pia wapo ambao ni wanawake lakini kama
Mfuko huu wa Wanawake usipotengewa fedha, ni jinsi gani
wanawake wataweza kujikwamua kiuchumi? Hivyo, naomba
sana katika bajeti ya Waziri Mkuu basi suala hili la wanawake
liweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika mataifa
makubwa duniani na hata yale ya nchi jirani kama vile
Zimbabwe, Malawi na Msumbiji na nchi nyingine hata Kenya
tu hapo jirani, wamekuwa wakiliangalia suala zima la
wanawake katika kutenga bajeti. Ukiangalia hapa Tanzania
katika bajeti zote ambazo zimekuwa zikitengwa suala la
mwanamke limekuwa liki-lag behind. Unakuta mwanamke
anatajwa katika maeneo machache sana. Sisi wanawake
tumeamua sasa kuiambia Serikali, lakini kuiomba kwa
unyenyekevu mkubwa sana kwamba sasa ianze kuangalia
suala zima linalowahusu wanawake. Kwa sababu wanawake
ndiyo ambao wanachangia katika pato la Taifa na hivyo
basi naomba wasiachwe nyuma. Hivyo basi, naendelea kuisihi
Serikali yangu kuuangalia mfuko huu na kuweza kutenga
fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wizara hii ya Afya
inayoshughulika na wanawake, huyu mama ambaye ndiyo
ameshikilia hii Wizara, dada yangu Mheshimiwa Ummy
Mwalimu, tunapomuweka kuwa yeye ndiyo mshika dhamana
ya wanawake hapa Tanzania halafu mfuko ule
haujatengewa fedha, ina maana tunamdhoofisha huyu dada
katika kuisimamia hii Wizara ya wanawake. Kwa hiyo,
naendelea kusisitiza na kuiomba Serikali, kwa mwaka huu
wa fedha iweze kutoa fedha na kuweka kwenye mfuko ule
ili kuweza kuwasaidia wanawake kwenye VICOBA ambavyo wamevianzisha waweze kujikopesha na kuweza kujikwamua
kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee
suala la afya. Katika hotuba ya Waziri Mkuu ukiangalia
ameongelea suala zima la afya na amesisitiza kwa kusema
kwamba Serikali inaendelea kujenga vituo vya afya ili
kuhakikisha wanawake nchini wanapata huduma za kiafya
vizuri. Ukiangalia katika afya kuna pillars tatu, yaani zahanati,
vituo vya afya pamoja na hospitali za Wilaya. Kule ndiko
ambako zile basic needs za afya zinaanzia. Katika Mkoa wa
Mwanza tunavyo vituo vya afya vya Serikali 46 tu ukiunganisha
na vituo vingine vya binafsi jumla ni vituo 388.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hivi vituo 46 va Serikali
ni vituo vinne tu katika mkoa wa Mwanza ndivyo ambavyo
vinatoa huduma ya upasuaji. Wanawake wengi wamekuwa
wakipoteza maisha wakati wa kuleta watoto hapa duniani.
Ukiangalia idadi ya vifo vya akina mama Mkoa wa Mwanza
ni 21% na hiyo inatokana na kukosa huduma za upasuaji
katika vituo vyetu vya afya. Hivyo basi, naiomba Serikali iweze
kutusaidia katika Mkoa wa Mwanza kuwezesha kutupa vituo
vya afya ambavyo vinaweza vikatoa huduma za afya ili
viweze kuongezeka kutoka vituo vinne tufikie hata vituo 15
kwa kuanzia ili wanawake wasiweze kuendelea kupoteza
maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika
Sustainable Development Goals, goal mojawapo ni
kuhakikisha huduma za mama na mtoto na za wajawazito
zinapatikana kwa urahisi na kuendelea kuondoa vile vifo vya
mama na mtoto. Kwa hiyo, kama tumeingia mkataba huu
wa kwenye Sustaibale Development Goals, naiomba Serikali
iweze kutusaidia katika Mkoa wa Mwanza kutuboreshea vituo
vyetu vya afya ili viweze kutoa huduma ya upasuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka siku moja hapa
nilipokuwa nikiuliza swali langu la nyongeza niliuliza suala la
wanawake wanavyopata huduma za upasuaji lakini
hawapati huduma za upasuaji kwa kupangiwa. Nilipokuwa naongea kile kitu nafahamu kwa sababu mama anapopata
ujauzito kuna matatizo ambayo huwa yanaonekana kwenye
scan kabla hata muda wake wa kujifungua haujafika. Kwa
hiyo, kama tatizo limeshaonekana na kwenye kituo cha afya
kuna huduma ya upasuaji, mama huyu anatakiwa apangiwe
ni lini na siku gani atakayofanyiwa upasuaji ili kuweza kuokoa
maisha yake yeye kama mama lakini pia na maisha ya mtoto
yule ambaye anamleta duniani. Kina mama wengi sana
wamekuwa wakipoteza maisha yao lakini mtoto anabaki kwa
sababu ya kutoa damu nyingi na matatizo mengine
mbalimbali ambayo yanawakumba akina mama wakati wa
kujifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika hotuba ya
Waziri Mkuu wameeleza ni namna gani bajeti ya vifaa tiba
pamoja na dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 hadi
shilingi bilioni 251. Katika kuongezeka kule sisi Mkoa wa
Mwanza naiomba tu Serikali katika bajeti hii ya mwaka huu
iweze kutusaidia CT Scan, Mkoa wa Mwanza hatuna CT Scan.
Ukiangalia CT Scan inasaidia katika mambo mengi sana si tu
wanawake. Kuna watoto wanazaliwa kule na vichwa
vikubwa Mkoa wa Mwanza lakini na Kanda ya Ziwa kwa
ujumla…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naunga mkono hoja.
The Finance Bill, 2016
kunipa nafasi hii ili niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu. Katika kuchangia Muswada huu wa Fedha (Finance Bill) naomba kutoa tu ushauri kidogo kwa Serikali kama itaweza kuzingatia. Kuna haya mapendekezo ambayo yametolewa ya kurekebisha hii kodi ya usajili wa namba binafsi kutoka milioni tano hadi milioni kumi. Naamini kabisa kwamba lengo la Serikali lilikuwa ni zuri, kwamba ina lengo la kukusanya mapato na kuyaongeza zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napata wasiwasi kidogo, kwa sababu gani napata wasiwasi. Ukiangalia wakati kodi hii ilikuwa ni milioni tano watu ambao waliweza kusajili namba zao binafsi ni wachache sana, japokuwa sina data kamili, lakini naamini kwamba watu walikuwa ni wachache na wanahesabika na wanafahamika. Kwa hiyo basi, utaona kwamba, sasa hivi tunaposema kwamba, tuongeze kodi hadi kufikia milioni 10 napata shida kwamba inawezekana tukapoteza hata hawa ambao tayari walikuwa wanachangia katika kupata mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi ni ombi langu tu kwa Serikali kwamba, waiache hiyo milioni tano. Nasema hivi kwa sababu gani? Milioni tano hii itakapobaki kwa muda wa miaka mitatu kila Mtanzania ambaye anaona kwamba kwa sababu hii ni luxury kwamba gari lako unaweza ukalisajili kwa bei ile ambayo imependekezwa kwa sasa hivi ya laki mbili na elfu hamsini, , lakini kama umeamua kusajili kwa kutumia jina lako mimi kama Kiteto, unaponiambia nilipe milioni tano kwa miaka mitatu, naona ni nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia inawezekana watu wengi sana watakapopatiwa elimu au matangazo yatakapokuwa yakipelekwa kwenye vyombo vya habari kwa kutumia chombo chetu cha TRA, basi unaweza kukuta watu wengi wataendelea kuhamasika ili kuweza kusajili hizo plate number za binafsi, lakini tunapopeleka kuwa milioni 10, nina wasiwasi kwamba mapato haya yatapungua kwani hawa ambao tayari walikuwa wamekwisha kujiandikisha, baada ya miaka mitatu kwisha wataamua kuachana na hilo suala na hapo Serikali itapoteza mapato yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchangia suala la kodi ya usajili wa pikipiki. Tunafahamu kabisa kwamba suala la pikipiki limesaidia vijana wengi kujipatia ajira. Wako watu wengi ambao wanajiweza wananunua pikipiki nyingi na kuwapatia vijana wetu kwa njia ya mikopo, hawa vijana wanakuwa wanalipa kidogo kidogo na hatimaye kuweza kuzimiliki hizo pikipiki. Kwa maana hiyo kodi ambayo sasa inapendekezwa kuongezwa kodi ya usajili kutoka 45,000 hadi 95,000, napata wasiwasi kwamba hawa bodaboda tutakuwa tumewaondolea hizo ajira. Kwa sababu atakapotokea mfanyabiashara mkubwa ananunua pikipiki anataka kuwapatia hawa vijana ili waweze kufanyia biashara na kulipa kidogo kidogo, wanatakiwa kwenda kuisajili, kwa hiyo bei ya kodi ya sh. 95,000, ina maana hawa vijana watakaposhindwa, Serikali itapoteza mapato katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba niishauri Serikali iweze pia kuendelea kulitazama suala hili, kama nia yetu ni kuendelea kukusanya mapato lakini bila kuwaathiri hawa vijana kwa kuwanyima ajira, basi naishauri Serikali ifuate ushauri ambao umetolewa na Kamati ya Bajeti kwamba kuiacha kodi ile kuwa hiyo hiyo sh. 45,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo kwa sababu ya swaumu, naomba niishie hapo na naunga mkono hoja.