Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. William Tate Olenasha (11 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kunipa fursa kutumika katika Serikali yake, Serikali ambayo imefufua matumaini ya Watanzania walio wengi. Vile vile nitumie fursa hii kumshukuru sana Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa ushirikiano mkubwa anaonipa katika majukumu yangu ya kila siku. (Makofi)
Nimejifunza mengi sana kutoka kwake, ni mtu ambaye anatoa ushirikiano.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Kwa hiyo, namshukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nitumie fursa hii kuwashukuru Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano wanaonipa katika majukumu yangu ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge na lazima niseme kwamba nimefarijika sana kwa namna Waheshimiwa Wabunge mlivyoonesha hamasa kubwa katika kuchangia Wizara ambayo ndiyo inabeba maslahi ya Watanzania walio wengi. Wote mmetoa michango ambayo itatusaidia katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda haitawezekana kujibu hoja zote, mengine yatajibiwa na Mheshimiwa Waziri, lakini mengine tutayaleta baadaye kwa maandishi kabla ya Bunge hili kwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein kwamba Serikali haina vision ya kilimo. Naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya eneo ambalo nafikiri tuko mbele sana ni kuhusu visioning, sera, mipango na mikakati. Wizara yetu katika sekta zake zote zina sera ambazo zinaainisha kwa kirefu sana kuhusu dira katika maeneo tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Sera ya Mifugo ya mwaka 2006, Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, Sera ya Uvuvi ya Taifa ya mwaka 1997. Zote hizi zinachangia katika kufikia malengo na sera na dira ambayo imeainishwa katika Sera ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025, katika maana ya kwamba development mission 2025. Zote hizi kwa pamoja zinaeleza kwamba dira yetu katika kilimo ni kuwa na kilimo cha kisasa, cha kibiashara na chenye tija na faida ambacho kinatumia rasilimali kwa ufanisi na endelevu na kuwa kiungo muhimu na sekta nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze tu kwa ufupi kwamba kuhusu vision na sera, hili ni eneo ambalo tuko mbali sana. Kuna changamoto katika utekelezaji, lakini siyo kwenye eneo la sera.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa vilevile niangalie eneo ambalo limechangiwa kwa hamasa kubwa na kwa msisimko mkubwa na Waheshimiwa Wabunge walio wengi. Hili ni eneo la migogoro kati ya watumiaji mbalimbali wa ardhi hususan kati ya wafugaji na wakulima. Hili ni eneo ambalo kama Wizara tunatoa kipaumbele kwa sababu ya namna inavyoleta changamoto katika kuendeleza kilimo; ni eneo ambalo linatishia amani ya nchi yetu. Kwa hiyo, Wizara imeweka kipaumbele katika shughuli zake za kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima ina vyanzo vingi, lakini chanzo kikubwa ni ukosefu wa ardhi, lakini vile vile inasababishwa na kukosekana kwa huduma kwenye maeneo ya wafugaji, inasababishwa vilevile na wafugaji mara nyingine kukimbia magonjwa kwenye maeneo yao na kwenda maeneo ambayo magonjwa siyo mengi. Vile vile inatokana na kukosekana kwa baadhi ya huduma kama maji na kama mlivyosema Waheshimiwa Wabunge wanalazimika kufuata maji maeneo ambayo yana maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ni lazima tukubali kwamba kwenye baadhi ya maeneo wafugaji wanahama kwa sababu ya ongezeko la watu, lakini vile vile kwenye baadhi ya maeneo wanahama kwa sababu ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Kimsingi tunasema kwamba kuna tatizo, tunakiri kwamba ni tatizo ambalo ni lazima tulishughulikie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni namna gani Serikali kupitia Wizara yetu imejipanga kutatua tatizo sugu la migogoro ya ardhi? Mkakati wa kwanza ni namna ya kupata ardhi. Tunapanga kutafuta ardhi ambayo itatosheleza mahitaji ya wafugaji kwa kufanya masuala yafuatayo:-
Moja, kulinda ardhi ya wafugaji kwa kuitangaza kwenye Gazeti la Serikali. Vile vile kufanya mkakati wa zoning katika maana ya kwamba kutafuta na kutenga ardhi katika baadhi ya mikoa ambayo ina ardhi kubwa na kuyasajili ili itumike kwa ajili ya wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vile vile kwa muda mfupi uliobakia kuchangia kuhusu uvuvi haramu na hili nasema kwa ujumla wake kwa sababu mmechangia sana. Waheshimiwa Wabunge, tunaomba mtuunge mkono katika jitihada zetu za kupambana na uvuvi haramu. Ukiruhusu uvuvi haramu uendelee, hautakuwa unampenda mvuvi wako kwa sababu rasilimali za uvuvi zitakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari kuna matatizo makubwa kwenye baadhi ya maeneo, samaki wanakwisha. Kama mnavyofahamu Ziwa Victoria, tayari kuna crisis na Ziwa Rukwa; yote ni kwa sababu ya uvuvi haramu. Kwenye baadhi ya maeneo ya maji ya chumvi, baadhi ya species za samaki, mfano kamba mti (prawns) zimekwisha kwa sababu ya uvuvi haramu. Naomba mtuunge mkono! Hatuwezi kumpenda mvuvi kwa kuendelea kumruhusu aendelee na uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tufahamu wazi kwamba uvuvi haramu kwa kutumia njia ambazo haziruhusiwi na sheria ni mbaya na huwezi kuruhusu kwa sababu tu unataka kumlinda mvuvi. Kwa hiyo, tunawaombeni Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono katika hili, Serikali ina nia ya dhati ya kuendelea kutoa elimu. Wavuvi wengi kabla ya kupewa Leseni ya Uvuvi, wanapewa elimu kuhusu uvuvi ambao unaruhusiwa na sheria. Kwa hiyo, mara nyingine inakuwa ni suala la kawaida tu la kutokufuata sheria na wala siyo suala la kutofahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kidogo kuhusiana na suala ambalo limeibuliwa sana na Mheshimiwa Dau kuhusiana na uvuvi kwa kutumia mitungi ya gesi. Uvuvi wa kutumia mitungi ya gesi unaruhusiwa kwenye aina fulani fulani za uvuvi hususan uvuvi wa samaki wa mapambo. Mara nyingine mitungi ile hutumika kufanya uvuvi wa majongoo; atakuwa anafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi ule unaharibu matumbatu; kwa hiyo, unaharibu mazalia ya samaki. Kwa hiyo, tunaendelea kusisitiza kwamba leseni zitolewe, badala ya kusema kwamba turuhusu tu kila mtu atumie uvuvi wa aina ya gesi ambao unaharibu mazingira. Serikali nia yake ni ya dhati katika hili, kwa hiyo, tunaomba mtuunge mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wametoa hoja ya msingi sana kuhusu kodi au leseni zinazotolewa kwa wavuvi katika Ziwa Victoria ambao wanalazimika kupata leseni kwenye Halmashauri mbalimbali ambapo wanakwenda kuvua, suala tunaloliita migratory licences au migratory taxes.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge kwamba nia ya Serikali katika hili ni jema. Tukiruhusu kwamba mvuvi akipata leseni katika Halmashauri moja, basi anaruhusiwa kwenda kote; moja, tutanyima Halmashauri zetu mapato, lakini vile vile ni vigumu kuzuia uvuvi haramu pamoja na uhalifu ambao wengi wenu mmeulalamikia sana. Kwa hiyo, tunatumia utaratibu ule wa leseni kutolewa katika kila Halmashauri kama namna ya sisi kuratibu uvuvi unaofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge kwamba, siyo kwamba maji hayana mipaka. Maji ya Ziwa Victoria; kila Halmashauri inafahamu maji yake yanaishia wapi, kuna alama. Kwa hiyo, nawaombeni mfahamu kwamba ni kwa nia njema na hata hivyo leseni ya uvuvi ni shilingi 15,000/=. Kwa ambao hawafahamu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba umalize.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Kwa ambao hawafahamu, ndiyo bei ya samaki mmoja. Kwa hiyo, naomba mtuunge mkono kwa sababu tunafanya kwa nia njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii na mimi nichangie kwa ufupi kwenye pendekezo la mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tumesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge, na kimsingi mingi imekuwa ikitushauri namna ya kuboresha baadaye mpango wakati tunautayarisha, kwa hiyo kazi waliofanya ni kazi ya kwao kimsingi wanashauri serikali wao kama wawakilishi wa wananchi tumepokea mapendekezo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi nyingi zimejikita katika kuonesha kwamba mapendekezo ya mpango hayajajikita kwa undani kuhusu kilimo. Tunapokea mapendekezo ambayo yametolewa, lakini tufahamu kwamba hata baadaye tukiwa na mpango bado itabakiwa ni frame work haiwezi ikaingia kiundani kila eneo la kilimo, mifugo na uvuvi, baadaye itabidi tujenge mikakati mahususi kuhusiana na eneo moja moja la sekta hizo.
yamezungumzwa mengi kuhusu hali ya uchumi katika kipindi ambacho Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano tuliahidi kuleta mabadiliko, tena mabadiliko makubwa, hatutegemei mabadiliko makubwa yatokee lakini tusihisi au tusione mabadiko yenyewe. Kwa hiyo tofauti ambayo tunaiona sasa ndio ushahidi kwamba kuna mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo hii tukasema kwamba tunashughulikia kuhusu ubadhilifu na matumizi mabaya ya fedha za Umma lakini hapo hapo pale wanaposhughulikiwa wanaofanya hivyo tukalalamika kwamba ni kitu kibaya, haiwezekani. Lakini vilevile haiwezekani kwamba tunategemea Serikali ilete mabadiliko makubwa lakini sisi Waheshmiwa Wabunge hatutaki kuwa sehemu ya mabadiliko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahatma Gandhi alishawahi kusema be the change that you wish to see (kuwa sehemu ya mabadiliko ambayo unataka tuone). Naombeni Waheshimiwa Wabunge tuweni sehemu ya mabadiliko, tukubali kuondoka kwenye comfort zone zetu ili tuweze kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano kuleta mabadiliko ambayo tunaka, nashukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami napenda kuchukua fursa hii kuzipongeza sana Kamati za PAC na LAAC kwa kazi waliyofanya kwa sababu kimsingi kupitia kwao Bunge limeendelea kufanya kazi yake ya Kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya PAC ilijadili na kutoa ushauri kuhusu upotevu wa fedha katika Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA kutokana na mahindi yaliyoharibika. Kimsingi walishauri kwamba, namna mojawapo ya kuhakikisha kwamba hilo tatizo halijirudiii tena ni kutoa fursa kwa wakulima kuuza mahindi nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na Wizara imelichukua pendekezo hili na kimsingi kwa sasa hatuzuii wafanyabiashara kupeleka mahindi nje, lakini napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, tunaruhusu chakula kipelekwe nje kulingana na ziada au hali halisi ya chakula ndani ya nchi. Kwa hiyo kuna wakati tunalazimika kupunguza kiwango kinachoenda nje si kwa sababu hatutaki wakulima wetu wanufaike na biashara ya chakula, lakini ni kwa sababu tunatanguliza maslahi mapana ya nchi ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na usalama wa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miezi ya hivi karibuni mnafahamu kwamba, tumekuwa tukichukua hatua kadhaa ili kuhakikisha kwamba, kunakuwa na usalama wa chakula kwa sababu majirani zetu hali yao si nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge pale unapoona kwamba, kuna kidogo kupunguza kasi ya kupeleka nje, mfahamu si kwa sababu hatutaki wakulima wetu wauze chakula nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo na ushauri mwingine ambao Serikali imeupokea ni kwamba, Wakala (NFRA) wajenge maghala kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, katika bajeti ambayo tunaitekeleza Wakala una mpango wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kutoka tani 246,000 hadi kufikia tani 496,000 kwa sababu tuna mpango wa kujenga vihenge vyenye uwezo wa tani 190,000, lakini vilevile maghala yenye uwezo wa tani 60, 000. Vihenge na maghala hayo yatajengwa Babati, Dodoma, Shinyanga, Makambako, Mbozi, Songea, Sumbawanga na Mpanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hoja ya Kamati ya PAC, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa vilevile ya kuzungumza baadhi ya masuala ambayo ningependa kuyatolea ufafanuzi. Mheshimiwa Omary Mgumba pamoja na Mheshimiwa Aeshi Hilaly walizungumzia sana kuhusu wafanyakazi wa NFRA waliosimamishwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kutumia fursa hii kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, ni kweli kuna wafanyakazi wanne wa ngazi ya juu wa NFRA ambao wamesimamishwa kazi. Nisingependa kuzungumzia kwa undani kuhusu suala hilo kwa sababu tayari Wizara imeunda tume ili kuchunguza tuhuma ambazo zinawakabili na kimsingi itakuwa prejudicial, hatutawatendea haki tukianza kulijadili Bungeni na hata wale wanaofanya uchunguzi nao vilevile, si vizuri wakaingiliwa wakati bado wanaendelea na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa maelezo kidogo tu ni kwamba, wafanyakazi waliosimamishwa, tuhuma yao si hiyo tu inayosemekana na Waheshimiwa Wabunge, kuhusu uharibifu wa mahindi. Uharibifu wa mahindi ni moja tu kati ya masuala mengi ambayo tume ya Wizara iliyoundwa inachunguza. Kuna masuala kuhusu uuzaji wa mahindi; kuna malalamiko ambayo yanachunguzwa katika mchakato mzima wa kuuza mahindi, lakini vilevile kuhusu fedha zinazotokana na uuzwaji wa mahindi yenyewe…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachosema tu ni kwamba, tuvute subira, taarifa ikiwa tayari Waheshimiwa Wabunge mtataarifiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Awali ya yote, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa nilipo nikiwa na afya njema. Niwahi mapema kabisa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kujibu na kutoa maelezo ya hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge, naomba kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongoza nchi yetu kwa busara na hekima ambayo imeendelea kuleta amani, utulivu na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile kumshukuru sana Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Eng. Charles John Tizeba, Mbunge wa Buchosa kwa kunishirikisha kwa karibu sana katika majukumu ya kuongoza Wizara hii nyeti ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Vilevile napenda kuwashukuru sana Makatibu Wakuu wa Wizara yetu, Eng. Mathew Mtigumwe, Dkt. Yohana Budeba na Dkt. Mary Mashingo, Wakuu wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara na wafanyakazi wote wa Wizara kwa ushirikiano wa hali ya juu wanaonipa katika kazi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Ngorongoro kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa Jimboni na mara nyingine wamekuwa wavumilivu pale ambapo shughuli za kitaifa zinanifanya nisiwepo Jimboni mara kwa mara. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, namshukuru sana kwa dhati kabisa mke wangu mpendwa Asha Mlekwa na watoto wangu wapendwa. Wao wamekuwa sehemu kubwa sana ya mafanikio yangu kwa kunipa nguvu na faraja katika shughuli zangu za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi, sasa nianze kuchangia moja kwa moja hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Mapema kabisa niseme kwamba zimetolewa hoja nyingi sana na sitaweza kujibu kila hoja lakini vilevile itaniwia vigumu kuwataja Wabunge mmoja mmoja kwa majina. Niseme tu kwamba tunathamini sana michango yao na tutaendelea kuifanyia kazi, hatutaweza kuyajibu yote hapa, lakini niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaleta majibu ya hoja zote ambazo wametoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kwa hoja ambayo imezungumziwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi na hii inahusu umuhimu wa sekta ya mifugo hapa nchini. Michango ya Waheshimiwa Wabunge ilielekea katika sehemu kubwa kuonyesha kwamba Serikali haitoi kipaumbele katika sekta ya mifugo na wala haitambui kwamba ni sekta muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haiwezi kamwe kuitenga na kuiweka nyuma sekta ya mifugo. Sekta ya mifugo ina umuhimu sana katika usalama wa chakula, uchumi na ajira ya watu wetu. Sekta ya mifugo inatoa ajira kwa kaya zipatazo milioni 4.4 ambayo ni karibu asilimia 50 ya kaya milioni tisa zilizopo hapa nchini na vilevile sekta ya mifugo inachangia asilimia 7.7 ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inajulikana kuwa zipo baadhi ya nchi zinazoagiza mazao ya mifugo kwa asilimia 100 endapo nchi yetu ikiingia kwenye kundi hilo, ingetumia jumla ya shilingi trilioni 17.8 kwa mwaka ambayo ni sawasawa na asilimia 60 ya bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kuagiza mazao ya mifugo. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za ulaji yaani consumption data ya mwaka 2016/2017. Kwa maana hiyo, hata pale kunapokuwepo na watu wanaosema sekta ya mifugo haichangii katika pato la Taifa, ni vizuri kuangalia kwamba tungeweza kupata hasara gani kama tusingekuwa na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile bei ya mazao ya mifugo ingekuwa kubwa sana na wananchi wa kawaida wasingemudu kutumia mazao hayo kama tusingekuwa na mifugo. Kwa hiyo, sekta ya mifugo ni muhimu sana na Serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa sekta hii, lakini jitihada mbalimbali lazima ziendelee kufanyika ili kuendelea kuboresha sekta hiyo na iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano inachukua hatua kadhaa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya mifugo ili kuongeza mchango wake kwa Taifa. Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mipango mbalimbali ya kuendeleza sekta hiyo ikiwa ni pamoja na Mpango Kabambe wa Sekta ya Mifugo (Livestock Master Plan) ambao unatekelezwa kupitia ASDP II. Vilevile mradi wa uendelezaji wa uhamilishaji; mradi wa kuendeleza tasnia ya maziwa wa Afrika Mashariki; mradi wa kuendeleza nyanda za malisho; mradi wa kuboresha ambali za kuku; mradi wa kuboresha ambali za ng’ombe na maziwa na mradi wa kuimarisha lishe wa kaya kupitia ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kupitia mkopo wa riba nafuu wa dola za Kimarekani milioni 50 kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Serikali ya Korea umepanga kukamilisha ujenzi wa machinjio ya Ruvu na hii itaendana na ujenzi wa viwanda vingine vya kusindika ngozi, kutengeneza bidhaa za ngozi na viatu. Vilevile itaboresha Ranchi ya Ruvu kuwa ya mfano; kukarabati na kuweka mizani katika minada 164 nchini kote; kuweka mfumo wa kidigitali wa kuunganisha wafugaji, wasindikaji na wafanyabiashara wa ndani na nje na vilevile mradi huu utajenga mtandao wa wasambazaji wa nyama Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo Waheshimiwa Wabunge walitumia muda sana kuijadili, ni suala la migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali. Migogoro ya matumizi ya ardhi inayohusisha wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi imeendelea kuwepo hapa nchini kwa muda mrefu. Juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali inawezekana hazijaweza kumaliza tatizo hili na hii ni kutokana na ukweli kwamba migogoro hii huhusisha sekta zaidi ya moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo, Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kuunda timu ya wataalam kutoka sekta zinazohusika na ardhi ili kuhakikisha kwamba masuala ya kila sekta yanaangaliwa kwa pamoja. Tayari kama tulivyoweza kuonesha wakati wa hotuba ya bajeti yetu, ripoti ile tumeshaipata na inafanyiwa kazi ili iweze sasa kwenda kwenye Baraza la Mawaziri na hatimaye utekelezaji wa mapendekezo uweze kufanyika. Kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge wavute subira kazi iliyofanyika ni kubwa na tunaamini mapendekezo yale yatatusaidia sana kuondokana na tatizo la migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni vizuri kueleza kwamba changamoto tuliyonayo katika sekta ya mifugo ni zaidi tu ya migogoro ya ardhi, mifugo mingi tuliyonayo nchini iko kwenye maeneo yanayopata mvua kidogo kwa mwaka ambayo kwa kiwango kikubwa yameathiriwa na madhara yatokanayo na mabadiliko tabia ya nchi hususani ukame ambao umeacha maeneo haya yakiwa hayana nyasi zinazofaa kwa malisho ikiwemo kuongezeka kwa majani yenye sumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wakaendelea kufahamu kwamba hata maeneo ambayo ardhi ya wafugaji bado inapatikana kwa kiwango kile kile, lakini ubora wa ile ardhi kwa malisho umepungua sana na ndiyo maana lazima tufikirie tu zaidi ya migogoro. Hali hii imesababisha wafugaji kuhitaji maeneo makubwa zaidi ya kawaida na wakati mwingine hulazimika kuhamia maeneo yenye unafuu na upatikanaji wa malisho na maji na hivyo imekuwa chanzo cha migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro pia imesababishwa na ongezeko la watu, mifugo na shughuli za kijamii na kiuchumi ambazo zinafanyika kwenye ardhi hivyo kusababisha mgongano wa matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na hali ya nyanda za malisho kuendelea kupungua na malisho nayo kuwa duni Wizara imeanza mpango wa kuboresha nyanda za malisho kwa kupanda mbegu za nyasi zinazoweza kukabiliana na hali ya ukame hasa katika maeneo yaliyoathirika. Kwa hiyo, Wizara inazihamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo Waheshimiwa Wabunge nyie wote ni Madiwani, kuandaa mipango itakayowashirikisha wafugaji katika kuunga mkono juhudi za Wizara kwa kutenga maeneo ya wafugaji pamoja na kuboresha malisho na kuweka miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwasisitiza wafugaji wetu kubadilisha aina ya ufugaji ili waendane na mabadiliko ya tabia ya nchi. Katika enzi hizi ambapo mvua na nyasi zimepungua ni lazima nazo tabia zetu za ufugaji zibadilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameizungumzia sana ni kuhusiana na suala la upigaji wa chapa. Zoezi la upigaji wa chapa linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo Na.12 ya mwaka 2010. Utekelezaji wa sheria hii unaendelea nchi nzima na tunafahamu kwamba kuna changamoto ambazo zinaendelea kutokea. Wizara ilibidi isitishe kwanza zoezi hilo ili kutoa fursa kwa Wizara na wadau wengine kujipanga upya na hususani kutoa hamasa na elimu ili wadau waweze kushiriki kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto moja ambayo imetokea karibuni ni kuhusu bei na gharama ya kufanya zoezi hilo. Wafugaji wanalalamika nchi nzima kwamba bei imekuwa kubwa lakini niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwamba utaratibu ambao unatakiwa ufuatwe ni kwamba Halmashauri inayotaka kupiga chapa mifugo ni lazima ijadiliane na wafugaji na wadau wengine kuhusu gharama. Kwa hiyo, ni marufuku Halmashauri au Mkurugenzi mwenyewe kujiamulia bei ya kupiga chapa bila kuwashirikisha wafugaji na wadau wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tatizo la elimu limekuwa kubwa na ndiyo maana Wizara ilielekeza kwamba kabla Halmashauri haijafanya zoezi la chapa ya mifugo ni muhimu kutoa elimu kwa wafugaji na wadau wengine. Nalo hili ni sharti ambalo tumeliweka na tunaomba Halmashauri zote zizingatie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunatambua kwamba suala la upigaji wa chapa linahusiana vilevile na ubora ngozi, tumetoa maelekezo ya namna ya kupiga chapa ambapo haitaathiri ubora wa ngozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nalo limevuta hisia ya Waheshimiwa wengi ni suala la maendeleo ya ushirika nchini. Serikali inapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa itaendelea kusimamia maelekezo ya kisera na Sheria ya Vyama vya Ushirika, Na. 6 ya mwaka 2013 ili kupata maendeleo endelevu ya ushirika nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika inaendelea kushirikiana na Wizara ya kisekta kuwahamasisha wananchi kote nchini kujiunga na kuanzisha vyama vya ushirika wa aina mbalimbali kulingana na mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameonesha wasiwasi mkubwa sana wa baadhi ya tozo ambazo tunapendekeza kufutwa kwamba zitaua ushirika nchini na hususani vyama vya msingi. Tunafahamu kwamba ni kweli kabisa ushuru ni chanzo kikuu cha mapato ya vyama vya ushirika katika kusaidia uendeshaji wake lakini nataka nitumie fursa hii niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara imebadilisha mfumo wa upatikanaji wa fedha hizo ambazo awali zilikuwa zikichukuliwa moja kwa moja kulingana na mjengeko wa bei wa mazao husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu tunaopendekeza sasa ni kwamba bodi za vyama zinatakiwa kuomba fedha hizo za uendeshaji kupitia mikutano mikuu ya wanachama ambao wataidhinisha kutokana na hali halisi ya uzalishaji katika makisio yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kimsingi ushuru ule wa kuendesha vyama vya ushirika utakuwepo lakini siyo kwa mpango wa sasa ambapo tunaweka kiwango kimoja katika nchi nzima, ni lazima mahitaji ya chama kimoja kimoja yajadiliwe na kuombewa ruhusa ili hizo fedha ziweze kupatikana. Kwa hiyo, kimsingi Waheshimiwa Wabunge ninachosema tunajali suala hili kwa sababu vyama vya ushirika ndiyo hasa vinaendesha maendeleo ya mazao kwa hiyo siyo kwamba vyama vya ushirika vitakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walitoa hoja kuhusu kupatiwa ruhusa ya baadhi ya vyama vikuu ambavyo vimeonekana vikubwa viweze kugawanywa. Mfano uliotolewa ulikuwa ni chama cha TANEKU. Tunachosema kulingana na sheria lakini vilevile kulingana na Katiba, uhuru wa kujumuika ni pamoja na uhuru wa kutotaka kujumuika kwa mtu au taasisi ambayo inapenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama chochote cha ushirika ambacho kinataka kuchukua hatua za kujigawanya ni sharti wazo hilo na maamuzi yafanyike katika mikutano ya kisheria hasa mikutano mikuu lakini baadaye wakishafanya kwa sababu Wizara na hasa Tume ndiyo inayosimamia Sheria ya Ushirika, ni lazima vitu vingine viangaliwe ikiwa ni pamoja na kuangalia kwamba ushirika unaendelea kuwa imara lakini vilevile kuangalia economic viability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wananchi na wanachama wa TANEKU wanakusudia kugawa chama cha TANEKU wao wakae kwenye mikutano yao halafu baada ya hapo walete mapendekezo Wizarani na sisi tutaangalia kama kweli masharti mengine wameweza kukidhi ikiwa ni pamoja na kuangalia isije ikasababisha migogoro zaidi kwa sababu kuna maeneo ambayo tumegawanya vyama lakini migogoro ikatokea hususani wakati wa kugawanya mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosisitiza tu ni kwamba tunachoangalia sana siyo utitiri wa vyama, sio uwingi, lakini ni ubora na uwezo wa kujiendesha kama taasisi ambazo zina demokrasia lakini ambazo zinaweza kujimudu kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ningependa kuzungumzia suala la uwekezaji katika maeneo tengefu ya Shungimbili, Mbarakuni na Nyororo kwa sababu ya muda nitazungumzia kuhusu kisiwa cha Shungimbili. Hoja ilitolewa kwamba kisiwa cha Shungimbili kimeuzwa, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba hakuna ukiukwaji wowote wa utaratibu uliofanyika katika uwekezaji katika kisiwa cha Shungimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hifadhi ya bahari na maeneo tengefu haijawahi kupora maeneo na kuyauza, shughuli zinazofanyika katika maeneo tengefu ni zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria ambazo ni mafunzo, utafiti na utalii ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya utalii ambayo ni rafiki kwa mazingira, hicho ndio kilichotokea Shungimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo wasiwasi wa wananchi wa Mafia kwamba kisiwa kimeuzwa ni kwa sababu mwenye hoteli amegeuza jina akaita Thanda Island na hivyo akaona kwamba imeuzwa mpaka imebatizwa jina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari kuna maelekezo kutoka Wizara ni kwamba mwekezaji abadilishe jina kutoka Thanda Island lirudi kuwa Shungimbili. Haiwezekana kisiwa ambacho cha watu wa Pemba kwa miaka yote wanafahamu kwa jina la Shungimbili halafu leo hii Mwekezaji anakuja anabadilisha jina analotaka yeye, tumetoa amri kwamba ni lazima jina lirudi kama ilivyokuwa mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa tu kumhakikishia Mbunge wa Mafia kwamba taratibu zinaendelea, lakini vilevile Halmashauri ya Mafia imekuwa ikinufaika na uwekezaji uliofanyika hapo, changamoto zingine ambazo zipo tutaendelea kujadiliana na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi na Halmashauri ya Mafia ili kuendelea kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, machache, nashukuru sana na niombe kuunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, wa Mwaka 2016
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kwa muda mfupi kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge ikiwa ni pamoja na yale yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia napenda kuongezea kidogo kwa lile alilozungumzia kwa ufasaha sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusiana na kifungu cha 3(5) cha Muswada wa Taasisi ya Kilimo unaopendekezwa. Iliibuliwa hoja na Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba lengo la kifungu hicho ni kuzuia mtu, shirika, taasisi au kampuni binafsi kupata haki endapo TARI itashitakiwa Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema lengo la kufanya hivi kwa vyovyote vile haiwezekani ikawa ni kwa ajili ya kutaka kumuathiri mtu binafsi au taasisi. Lengo lake kubwa ni kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya umma lakini vilevile ni kwa sababu ndiyo sheria na Katiba yetu inavyotutaka. Kama alivyosema Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ibara ya 59 inaweka wazi ndiyo maana ofisi hiyo imeanzishwa. Kimsingi Mwanasheria Mkuu wa Serikali ana nguvu na anapaswa kuwepo pale taasisi ya umma au Serikali inaposhtakiwa Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo lake ni pamoja na kulinda maslahi ya umma kwa sababu kwenye mashtaka yale mara nyingine yasiposhughulikiwa kwa ufasaha na kwa weledi, inawezekana Serikali ikapoteza kesi au taasisi ya Serikali ikapoteza kesi na hivyo Serikali ikapata hasara kubwa na umma wa Watanzania ukabeba mzigo mkubwa ambapo pengine kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali angeshiriki labda isingetokea hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba ukitaka kufahamu kwamba hakuna nia mbaya katika kuleta hayo matakwa ya Kikatiba, hata kwenye kesi za uchaguzi anaingia. Jana kulikuwa na Mheshimiwa alikuwa anashangilia kwamba ametoka kushinda kesi, kwenye kesi dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mwanasheria Mkuu naye vilevile anakuwepo. Kama Tume ndiyo imeshtakiwa haijalishi kama Mbunge anayeshtakiwa ni wa Upinzani au ni wa Chama Tawala, Mwanasheria wa Serikali anakuwepo upande wa Tume na mara nyingine sasa unakuta hata ushindi wanaopata Wabunge wa Upinzani ni kwa sababu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametia mkono wake. Kwa hiyo, kama mnavyoona hakuna lengo baya, haimbagui mtu yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitoa vilevile mapendekezo kuhusiana na viwango vya posho za Wajumbe wa Bodi, wao wakipendekeza kwamba zipangwe na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Ofisi inayohusika na Utumishi wa Umma. Mapendekezo ya viwango vya posho huandaliwa na Bodi kwa kuzingatia Waraka wa Msajili wa Hazina.
Kwa hiyo, tayari kuna Waraka unaoelezea na kuainisha ni namna gani posho hiyo ilipwe na viwango vinatakiwa viwe vipi. Mara nyingi viwango hivyo huwasilishwa kwenye Wizara Mama kwa ajili ya kuvipitia na hatimaye huwasilishwa kwa Msajili wa Hazina na Idara Kuu ya Utumishi kwa ajili ya kupata idhini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwafahamishe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna utaratibu tayari wa kikanuni wa namna masuala ya posho yanavyofanyiwa kazi kwa hiyo, haitakaa itokee kwamba Wizara au Bodi au Waziri wakavuka mipaka ile ambayo haitakiwi kwa sababu tayari Msajili wa Hazina atakuwa na mkono wake pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitolewa vilevile hoja na Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba muundo wa Taasisi ya TARI utaidhinishwa na chombo kipi kama Bodi ya Wakurugenzi imepewa nguvu ya kuanzisha Idara na Vitengo kwa kadri inavyoona inafaa? Muundo wa taasisi hutegemea majukumu ya taasisi moja moja na yalivyoainishwa katika sheria ambayo inaanzisha taasisi hiyo. Kwa msingi huo, taasisi husika huandaa mapendekezo ya muundo na kuwasilisha kwa Wizara Mama, Msajili wa Hazina na hatimaye Idara Kuu ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kuidhinishwa. Kwa hiyo, tayari kuna taratibu ambazo zinatumika ili kuondoa nafasi au uwezekano wa Bodi kuweza kuunda vyombo vingine au idara kinyume na taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iliibuliwa vilevile hoja kwamba muda wa watendaji kuhudumu ungekuwa wazi ili kuondoa tabia ya watendaji kukaa muda mrefu katika nafasi zao. Watendaji wa taasisi ni watumishi wa umma ambao wanatekeleza majukumu yao katika taasisi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji katika taasisi watahudumu katika nafasi zao kwa kuzingatia masharti ya ajira zao. Muda wa kustaafu na masharti mengine vinafanya kazi kwao kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma. Kwa hiyo, hamna kitu kipya kinachoanzishwa, wale watendaji wakuu siyo kwamba wao watakuwa na masharti tofauti ya utumishi tofauti na wengine. Kwa hiyo, taratibu za kawaida kuhusu muda, marupurupu zitaendelea kutumika bila ubaguzi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitolewa vilevile hoja kwamba Waziri mwenye dhamana ya kilimo ndiyo mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu rufaa. Utaratibu wa Waziri mwenye dhamana katika jambo fulani kuwa na uamuzi wa mwisho katika maamuzi ni wa kawaida kwa sababu Waziri ndiyo ngazi ya juu kabisa ya maamuzi katika Wizara. Kwa hiyo, anapotoa ule uamuzi inamaanisha tu kwamba katika ngazi ya Wizara yeye ndiyo mwenye maamuzi ya mwisho, lakini haimaanishi kwamba hakuna fursa zozote nyingine za mtu anayefikiri kwamba hakubaliani na maamuzi ya Waziri kwamba hawezi kupata nafuu ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wetu kama mtu haridhiki na uamuzi wa Waziri anaweza akaenda Mahakama Kuu kufanya mapitio na kama itaonekana kwamba Waziri alikiuka taratibu au hajatenda haki, mara nyingi Mahakama zetu hubadilisha na kuyafutilia mbali maamuzi ya Waziri. Kwa hiyo, finality clauses kwenye sheria hizi zisiwape tabu kwa sababu haimanishi kwamba mtu hawezi kwenda Mahakamani, inawezekana lakini kwenye ngazi ile ukitoka kwa Waziri hamna sehemu nyingine ya kwenda katika Wizara lakini anaweza akaenda Mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wameleta hoja na hoja ziko nyingi, nitaziangalia baadhi, Mheshimiwa Waziri baadaye atapata naye fursa ya kuangalia hoja za Wabunge. Imetolewa hoja kwamba sheria inayotungwa iainishe ni vipi matokeo ya tafiti zitakazofanyika yatawafikia walengwa. Ili kuongeza ufanisi wa kufikisha matokeo ya utafiti kwa wadau, taasisi inayopendekezwa inatarajiwa kuweka Kurugenzi ya Usambazaji Teknolojia na Mahusiano. Kwa njia hii tunafikiri tafiti zile zitaweza kuwafikia walengwa kirahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetolewa vilevile hoja kwamba muda wa miaka kumi ya uzoefu unaotakiwa kwa Mkurugenzi Mkuu ni mrefu na imetolewa hoja kwamba upunguzwe. Nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ni nyeti sana katika kusimamia na kuhakikisha kuwa Taasisi ya Utafiti inayokusudiwa kuanzishwa inaendeshwa kwa umahiri na kuweza kufikia malengo ya uanzishwaji wake. Ili kumpata mtu kushika nafasi hii kunahitajika weledi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaamini kuwa na sifa au uwezo wa kuiongoza taasisi nyeti kama hii inahitaji mtu aliyebobea kwenye utafiti, mtu ambaye tayari ana uzoefu wa kimenejimenti na mtu ambaye ukimleta ni rahisi kuongoza taasisi kama hiyo. Kwa hiyo, ni kawaida hamna kitu kipya, tunafikiri miaka kumi siyo mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetolewa hoja vilevile kwamba taasisi inayopendekezwa ya TARI ingekuwa vema kama ingeunganisha tafiti za kilimo pamoja na mifugo. Tungependa kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari kuna taasisi inayohusika na utafiti wa mifugo na hii inaitwa TALIRI (Tanzania Livestock Research Institute). Hata hivyo, tungependa kuendelea kutenganisha mifugo na kilimo kwa sababu kwa muda mrefu imekuwa ni rahisi mifugo kumezwa ndani ya kilimo. Kwa hiyo, tunapokuwa na taasisi mbili inasaidia utafiti kufanyika kwa umakini zaidi katika maeneo yote hayo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetolewa vilevile hoja kwamba taasisi ione jinsi itakavyoshirikisha vyuo vikuu vinavyofanya utafiti. Napenda kusema kwamba taasisi inayopendekezwa imeweka muundo wa uendeshaji ambapo kwenye Bodi na kwenye Jukwaa la Ushauri, viongozi wakuu wa vyuo vya elimu ya juu ni mojawapo ya wajumbe ili kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika shughuli za utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetolewa hoja kwamba inabidi mfumo wa uteuzi wa kutumia ushindani utumike katika kumpata Mkurugenzi Mkuu. Utaratibu uliowekwa na Muswada unaleta ushindani. Kwa sababu kabla ya uteuzi kufanyika lazima usaili ufanyike ili kuwapata watu wale ambao ndiyo wanapendekezwa waweze kuteuliwa na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, tayari kuna ushindani katika nafasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile imetolewa hoja kwamba Taasisi ya Utafiti ya Kilimo imeonesha kuwa itakuwa Tanzania Bara lakini kwenye Katiba utafiti ni jambo la Muungano, inabidi maelezo yatolewe. Suala la kilimo siyo suala la Muungano, kwa hiyo, taasisi inayoanzishwa ni kwa ajili ya Tanzania Bara tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru ningeomba kuchangia kuhusu hoja ya Kamati na kwanza niseme kabisa kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia sana kuhusiana na masuala ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo ni kielelezo tosha kabisa kuhusu namna suala la Kilimo, Mifugo na Uvuvi lilivyo na kipaumbele kwa Watanzania wengi ndiyo maana Wawakilishi wa wananchi wameweka mkazo katika kulizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja za Wabunge ziko nyingi kwa vyovyote vile kwa dakika tano sitaweza kuzipitia zote lakini kwa ujumla wake, Waheshimiwa Wabunge wameonesha moja; kwamba kuna haja ya kuongeza bajeti ya kilimo kuliko vile ilivyo sasa ili iweze kuakisi umuhimu wa sekta hii katika jamii. Kimsingi Serikali inakubaliana na hili na nafikiri Waheshimiwa Wabunge tutashirikiana nao tunavyoelekea katika bajeti inayokuja ili kuona kwamba bajeti ya Kilimo inaongezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia sana kuhusu suala la pembejeo katika maana ya ubora, kufika kwa wakati kwa wakulima lakini vilevile kuhusu bei ambayo inaweza ikahimilika kwa wakulima wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imejipanga kukabiliana na changamoto hii ya pembejeo na tunafikiria tuko mbioni kuanzisha utaratibu ambao mbolea inapatikana kwa utaratibu wa bulk procurement kama utaratibu ulivyo wa sasa wa mafuta unaofanywa na EWURA. Kimsingi tunaamini kwamba kama tunaweza kuta-subsidies kutoka kwenye source inakuwa ni rahisi Watanzania wote kupata mbolea kwa bei moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaamini kwamba, gharama ya sasa ya juu iliyopo katika mbolea na baadhi ya pembejeo ni suala vilevile linalosababishwa na tozo na kodi ambazo zimewekwa katika bidhaa hizi. Kwa hiyo, vilevile tutaomba Bunge lako, tutakuja na mapendekezo ya namna ya kuondoa kodi, tozo na ada mbalimbali ambazo zinaendelea kuchangia pembejeo iwe bei ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Serikali bado ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha kwamba mbolea inazalishwa ndani. Tunaamini kwamba bei kubwa iliyopo ya sasa ya mbolea ni suala vilevile la kwamba ni gharama kwa sababu tunaagiza kutoka nje kwa hiyo tukiwa na viwanda vya kuzalisha mbolea ndani tunaamini kwamba itatusaidia kupunguza bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa vilevile suala la ukame na uhaba wa chakula. Hili tulishalitolea ufafanuzi katika Bunge hili lakini niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba kutokana na tathmini ya kina ambayo Serikali imefanya, Serikali inaamini kwamba tumejizatiti vya kutosha vya kuhakikisha kwamba hamna Mtanzania atakayekufa na njaa na nimhakikishe tu Mheshimiwa Lwakatare ambaye yeye keshasema watu watakufa njaa mwezi wa tatu, kwamba, Serikali itahakikisha hili halitokei, tumeweka mikakati ya kufuatilia kuhakikisha Watanzania wanakuwa na usalama wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la migogoro kati ya wafugaji na wakulima; Hili nalo limevuta hisia ya Waheshimiwa wengi. Kimsingi kama Serikali tunakubali kwamba hili ni eneo ambalo matokeo chanya na ya haraka yanahitajika kutokea kwa sababu migogoro hii imeongezeka. Tunavyozungumza tayari Serikali ina Tume ambayo inazunguka nchi nzima kupitia migogoro yote ili kuweza kutoa mapendekezo ambayo tunaamini kwamba yakifanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa tunaweza tukaondoa migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia vilevile kuhusiana na suala zima la haja ya kuongeza jitihada katika kufanya kilimo cha uwekezaji. Wizara imelipokea hili tunaamini kwamba ni kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache nashukuru sana na naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO A UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja ya Kamati.
Kwanza, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa kazi nzuri ambayo wameifanya na hatimaye kutuletea ripoti ambayo imesheheni ushauri ambao ni mzuri. Kimsingi Kamati imekuwa karibu sana na sisi kama Wizara na tumeendelea kunufaika na ushauri wao, kwa kweli tunawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao kwa wingi wao wamechangia sana kuhusu masuala mbalimbali ya Wizara, masuala ya kilimo, mifugo na uvuvi. Inaendelea kuonesha namna gani Waheshimiwa Wabunge wanavyowajali wapiga kura wao ambao wengi wao ni wakulima, wafugaji na wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, napenda kuchangia baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, kwa vyovyote vile na kwa sababu ya muda sitaweza kumaliza yote. Ya kwanza kabisa ni kuhusiana na suala la migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima na watumiaji wengine wa ardhi. Wizara inatambua fika kwamba hili ni tatizo kwa muda mrefu na imefika wakati kama wanavyoshauri Waheshimiwa Wabunge tatizo hili tukaondokana nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la migogoro ya ardhi ni suala mtambuka, linahusu Wizara zaidi ya moja. Ndiyo maana Serikali katika kuhakikisha kwamba tunalishughulikia tatizo hili imeunda Tume ambayo inashirikisha Wizara tano ikiwa inaratibiwa na Wizara ya Ardhi ili kwa pamoja tujaribu kuangalia migogoro hii ili hatimaye tuweze tukatafuta suluhu ya kudumu. Hivi tunavyozungumza, Tume hii ipo field na tayari imeshatembelea baadhi ya mikoa inawahoji wadau, inapitia ripoti mbalimbali za Kamati zingine za siku za nyuma kuangalia nini kilichosemwa na mwisho wake wataleta mapendekezo Serikalini ambapo na sisi tukishapata tutaleta mapendekezo kwa wadau mbalimbali mkiwepo ninyi Waheshimiwa Wabunge ili kwa pamoja tuangalie na tujadili namna gani ya kuweza kutokomeza hili tatizo ambalo kwa kweli limekuwa sugu kwa miaka mingi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge muwe na subira, ripoti itakuja, inawezekana ikaonekana kwamba imechelewa lakini tatizo la migogoro siyo tatizo dogo limekuwepo kwa miaka mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuzungumzia kuhusiana na hoja iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu madeni na ubadhirifu kwenye Vyama vya Ushirika hususan kwenye vyama vya korosho. Wizara yangu inatambua kwamba ubadhirifu katika Vyama vya Ushirika inachangia sana katika kudidimiza kilimo na ndiyo maana tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba tunakabiliana na wote wale wanaofanya ubadhirifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni COASCO imekamilisha kupitia mahesabu ya vyama 200 Mtwara na Lindi na imebaini kwamba kuna upungufu mkubwa na kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha za wananchi. Napenda kuwataarifu Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mikoa ya Lindi na Mtwara kwamba tupo njiani kwenda kuhakikisha kwamba tatizo hili linashughulikiwa na wale wote ambao wamehusika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuvunja Bodi za Vyama vya Ushirika hivyo 200. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa vilevile suala la Hifadhi ya Ngorongoro na Loliondo. Napenda kusema machache, Hifadhi ya Ngorongoro kama alivyosema Mheshimiwa Sakaya ni hifadhi ya kipekee sana duniani. Upekee huu pamoja na mambo mengine ni kwa sababu ni hifadhi ya pekee duniani ambayo binadamu anaishi kwa amani na wanyamapori. Hiyo ndiyo imeipatia Ngorongoro kuwa na sifa hiyo ya kipekee na Serikali inatambua hilo na inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zilizopo ili tabia hii ya wananchi kukaa vizuri na wanyamapori iendelee kutokea.
Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mapema kabisa kuanza kuiunga mkono hoja iliyopo mezani ili nisije nikasahau. Vilevile nitumie nafasi hii kutoa pongezi sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa hotuba nzuri, lakini vile vile kwa jitihada kubwa ambayo ameonesha katika kutupeleka katika nchi ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, yeyote yule anayebeza jitihada za Mheshimiwa Waziri na Timu yake, najua atafanya hadharani lakini nina hakika kimoyo moyo anampongeza. Kwa sababu haiwezekani kwamba ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu tu tayari tunashuhudia uanzishwaji wa viwanda zaidi ya 300. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakati wanachangia, wameibua masuala yanayogusa kilimo ambayo ningependa kuyatolea ufafanuzi kwa muda mfupi nilionao. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusiana na biashara ya chakula na bidhaa zinazotokana na kilimo katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki, wakiashiria kwamba wangetaka na sisi tufuate kinachofanyika kwenye nchi nyingine kuagiza chakula kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na changamoto ya chakula tuliyopata katika mwaka uliopita, lakini ukifananisha na picha tuliyonayo katika ukanda wetu wa Afrika Mashiriki, nchi yetu imeendelea kuwa na hali nzuri ya chakula kuliko nchi yoyote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua baadhi tu ya bidhaa za chakula tutaona picha kuhusiana na hali halisi ya bei kwa sasa. Tukichukua zao la mahindi, bei ya wastani Uganda tunavyozungumza leo ni Sh. 96,000/=, wakati Kenya ni Sh.114,000/=; Rwanda ni Sh.88,000/=, Juba au Sudani ya Kusini ni Sh.135,000/=, Burundi ni Sh.152,000/= wakati kwetu bei ya wastani kwa leo ni Sh.95,000/=. Kwa hiyo, unaweza ukaona tumekaaje katika mizania ya kikanda ikija suala la bei ya mahindi. Hata zile nchi nyingine ambazo zinaelekea zina bei nzuri kama Rwanda ni kwa sababu wao wameagiza kutoka Brazil. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tukiangalia zao la mchele au basi chakula cha mchele, tunaona kwamba bei ya wastani Uganda kwa leo ni Sh.203,000/=, Kenya ni Sh.267,000/=, Rwanda ni Sh. 204,000/= lakini Burundi ni Sh.236,000/= na kwetu bei ya wastani wa mchele kwa leo ni Sh.174,000/=. Unaweza ukaona kwamba bado sisi tukiangalia kikanda tuko katika hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile imezungumzwa sana kuhusu sukari. Ukiangalia bei ya sukari katika Nchi za Afrika Mashariki, utagundua kwamba nchi yetu bado tuko katika hali nzuri ukifananisha na nchi za jirani. Bei ya wastani Burundi kwa leo ni kati ya Sh.3,700/= mpaka Sh.4,000/=; Uganda kati ya Sh.3,500 mpaka Sh.4,000/=; Kenya ni kati ya Sh.3,500/= mpaka Sh.5,000/=. Kwa hiyo, ukiangalia sisi Tanzania tuko katika hali nzuri bei ya sukari ni kati ya Sh.2,500/
= mpaka Sh.3,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo asubuhi nilipata wasaa wa kuongea na Ma-DC wa Wilaya za mpakani za Kakongo, Misenyi, Ngorongoro, Rombo na Tarime, kujaribu kuangalia hali ya chakula na kimsingi wote wanasema kwamba sisi kama nchi bado tuna hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge waliokuwa wanataka na sisi tuagize chakula kutoka nje, wangeshauriwa vizuri zaidi kuhusiana na athari ambazo nchi yetu ingeweza kupata kwa kufanya kama hivyo. Kimsingi Kenya na Rwanda wao wameagiza chakula kutoka nje kwa sababu wao wana changamoto kubwa ya chakula, hali yao ya chakula siyo nzuri; wakati sisi mwaka uliopita tulikuwa na ziada ya tani milioni tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tathmini ambayo tumeifanya karibu mikoa yote inatuonesha kwamba mwaka huu inaelekea kwamba tutapata chakula kingi zaidi. Sisi hatuna haja ya kuagiza. Kenya wameagiza chakula kutoka Mexico kwa sababu hali yao ni mbaya, lakini kawaida wao wanategemea Tanzania na Uganda katika kupata chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nami kupata fursa ya kuchangia mjadala unaoendelea. Napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole sana kwa Mheshimiwa Tundu Lissu kwa yaliyompata na kuungana nao vilevile kumwomba Mwenyezi Mungu amjalie apate afya njema na arudi katika shughuli zake za kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita katika hoja moja iliyotolewa kuhusiana na Azimio la Kuridhia Mkataba Kuanza Kamisheni ya Pamoja Bonde la Mto Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Azimio hili ni muhimu sana kwa nchi yetu na katika hali ya kawaida, limechelewa sana. Kumekuwepo na majadiliano ya kuanzisha Kamisheni ya kusimamia bonde hili kati ya Tanzania na Malawi tokea mwaka 1976. Kwa kweli imechelewa sana kwa sababu rasilimali ambayo inatumika na nchi zaidi ya moja katika hali ya kawaida ingetakiwa iwe na utaratibu wa pamoja wa kusimamia; na katika hali ya kimazingira ambayo bonde lile lipo kwa sasa, kwa kweli Kamisheni hii ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ilitolewa kwamba kifungu cha convention hii inayozungumzia kuhusu usuluhishi wa migogoro inapingana na sheria ambayo tulipitisha ya Natural Wealth and Resource Permanent Sovereignty Act ya 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa hoja kwamba kwa sababu itifaki ambayo tunaizungumzia inaanzisha utaratibu ambao kama kutakuwa na mgogoro kati ya Malawi na Tanzania kuhusu usimamizi wa Bonge la Mto Songwe, basi itapelekwa kwenye Tribunal la SADC. Yeye aliona inaingiliana na inavunja sheria ambayo tumepitisha hivi karibuni ya kusimamia rasilimali zetu, sheria ambayo nimeitaja ya Natural Wealth and Resource Permanent Sovereignty Act of 2017, hasa katika Kifungu cha 11(1) mpaka (3).

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba hii au sheria hizi ni tofauti. Wakati Mkataba wa Kuanzisha Kamisheni ya Pamoja ya Usimamizi wa Bonde la Mto Songwe inashughulika na uhusiano wa nchi na nchi, yaani katika maana ya bilateral agreement, sheria yetu ile ambayo nimeitaja ya Permanent Sovereignty, yenyewe inahusika na uhusiano wa nchi yetu na wawekezaji au makampuni ambayo yanawekeza katika rasilimali zilizoko katika nchi yetu.

Kwa hiyo, katika hali ya kawaida ni mikataba tofauti; mwingine ni mkataba wa Kimataifa ambao unaongoza ushirikiano kati ya nchi mbili lakini nyingine ni sheria ya ndani inayohusiana tu na mikataba ya kutumia rasilimali zilizopo ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, ni vitu tofauti na wala hakuna hatari yoyote katika sisi kuridhia itifaki hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ni lazima tufahamu kwamba katika hali ya kawaida kama rasilimali ambayo inalindwa na sheria inatumika na zaidi ya nchi moja, haiwezekani sheria ya nchi moja ikawa ndiyo inayotawala rasilimali ile. Kwa hiyo, kwa sababu rasilimali ya Bonde la Mto Songwe ni shared resource, ni rasilimali ya nchi zaidi ya moja, katika hali ya kawaida ni lazima isimamiwe kwa pamoja na kwa sheria ambayo ni ya pamoja. Itifaki hiyo ambayo ndiyo tunasema sasa tunataka ianze kufanya kazi, imetengenezwa kwa utaratibu wa itifaki za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika SADC ambayo sisi ni wanachama na Malawi vilevile ni mwanachama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa pamoja tulishakubali huko nyuma tulipojiunga kwamba masuala yote ambayo yanahusiana na maji au rasilimali ambazo zinamilikiwa kwa pamoja, kama kuna migogoro, migogoro ile itaamuliwa kwa kutumia Tribunal au Mahakama ya SADC. Kwa hiyo, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba hakuna sheria yoyote iliyovunjwa, tuko sahihi kabisa. Sisi tukiridhia Azimio hili wala hatutakuwa tumevunja sheria yetu ambayo sisi wenyewe tumeipitisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile hoja ile iliekea kutaka kujenga hoja kwamba sisi hatuheshimu sheria za Kimataifa tunapotunga sheria kama ile ya kwetu The Natural Wealth and Resources Permanent Sovereignty Act, 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunaheshimu sheria za Kimataifa na ndiyo maana hata leo hii tupo hapa tunazungumzia kuhusu Bilateral Convention, ni sheria ambayo kwa mwonekano wake, kwa hali yake ya kawaida ni Sheria ya Kimataifa, bado tunaendelea kuheshimu, lakini kuheshimu kule haitunyimi sisi kuendelea kulinda rasilimali zetu ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kusuluhisha migogoro ambapo tunafikiri italinda zaidi rasilimali zetu, itatupa nafasi kubwa zaidi ya kuweza kusimamia rasilimali zetu bila kuingiliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, napenda kuunga mkono hoja ya Azimio lililopo mbele yetu. Nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. WILLIAM T. OLENASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumpongeza Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri pamoja na watumishi wa Wizara ya Ardhi kwa kutayarisha hotuba nzuri iliyosheheni mikakati mizuri ya kuondoa changamoto ya sekta ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutumia fursa kutoa changamoto kadhaa za ardhi kwenye Jimbo la Ngorongoro ambayo ningeomba Wizara ya Ardhi iangazie mwanga ili kutafuta suluhu ya kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya vijiji na vijiji. Ngorongoro kuna migogoro mingi ya ardhi inayohusu mipaka. Kutokana na kukosekana mipaka ya kisheria kati ya kijiji kimoja na kingine migogoro hii mara nyingine imesababisha mauaji na uharibifu wa mali. Mifano ya migogoro ni kama ile kati ya vijiji vya Naar na Kisangiro Maaloni na Yasi Ndito, Sale na Malambo, Ngarwa na Oloipiri na Kirtalo Oldoinyosamba na Pinyin na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuwasihi wenzetu wa Wizara ya Ardhi washirikiane na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ili kupima mipaka ya vijiji. Ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima na kuokoa maisha na mali za wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya hifadhi na vijiji. Wilaya ya Ngorongoro ina mgogoro mkubwa kati ya vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Serengeti National Park). Vijiji hivyo ni pamoja na Ololosokwari, Kiitalo, Oloipiri, Oloiriori, Lopulun, Loosoitik, Arrash, Piyaya na kadhalika. Kukosekana kwa mpaka unaoeleweka kwa alama kunaleta mgogoro mkubwa sana kwani mara nyingi wananchi wanakamatwa na kutozwa fine kwenye eneo ambalo wao wanafahamu kuwa ni eneo la vijiji toka siku nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutoa rai kwa Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana Wizara ya Maliasili na TAMISEMI kupima na kuweka bayana mipaka ya hifadhi ili kuondoa migogoro isiyokuwa na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya vijiji na wawekezaji. Migogoro mingine ambayo ningependa Wizara ya Ardhi iitazame na kutatua kwa kushirikiana na wadau wengine ili ipatikane suluhu ya kudumu ni migogoro kati ya kampuni ya uwindaji ya Orthelo Business Cooperation (OBC) na vijiji vilivyopo ndani ya Pori Tengefu la Loliondo (Loliondo Game Controlled Area). Migogoro hiyo ni dhahiri kuwa inasababishwa na mgongano wa Sheria za Ardhi (Na. 4 na 5 za mwaka 1999) na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009, ambazo zinatoa ardhi kwa vijiji na hapo hapo kuweka mamlaka ya rasilimali za wanyamapori chini ya mamlaka nyingine na hivyo kuleta mgongano wa matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Wizara ya Ardhi ishirikiane na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutengua na kufuta mapori tengefu yaliyopo ndani ya ardhi ya vijiji vya Loliondo ili wananchi waweze kupata mamlaka kamili ya kusimamia ardhi zao kama vijiji vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mwingine kati ya vijiji na wawekezaji ni kati ya vijiji na wawekezaji, ni ule kati ya kampuni ya kitalii ya Thompson Safaris na vijiji vya Sukenya, Mundorosi, mgogoro ambao umezuka baada ya TBL Ltd. kuuza ardhi ya shamba la Sukenya ambalo kwa miaka mingi lilitelekezwa na wananchi kulitumia zaidi ya miaka 20. Aidha, wananchi wamefungua kesi mahakamani ya kupinga shamba hilo kuuzwa kwa kile wanachosema kuwa wameporwa na TBL bila kufuata taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya Wilaya/Mkoa. Ningependa vilevile kati ya mipaka ya Wilaya/Mkoa. Kuna migogoro ya mipaka kati ya Wilaya ya Meatu (Simiyu) na Ngorongoro (Arusha), Longido (Arusha) na Ngorongoro (Arusha) na Karatu (Arusha) na Ngorongoro (Arusha). Mgogoro kati ya Meatu na Ngorongoro umechochewa zaidi na wawekezaji wa Mwiba Holdings ambao wanasemekana kusogeza mpaka wa Meatu na Ngorongoro na kumega ardhi ya kijiji cha Kakessio ili kunufaika na rasilimali ya wanyamapori waliopo ndani ya hifadhi. Mwiba Holdings Ltd. inasadikika kuwa wanamiliki ardhi ya kijiji cha Makao kinyume na sheria kwani kampuni ya nje ya kijiji mwekezaji hawezi kumiliki ardhi ya kijiji bila ardhi hiyo kuhuishwa na kuwa ardhi ya jumla na hati kutolewa na kamishina wa ardhi. Aidha, kampuni hiyo inafanya ufugaji wanyama pori pembezoni mwa Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Maswa kinyume cha Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai kwamba Wizara ifute miliki ya Mwiba Holdings kwenye ardhi ya kijiji cha Makao, lakini vilevile Wizara ishirikiane na TAMISEMI kupima mipaka ya Wilaya zenye mgogoro. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. WILLIAM T. OLENASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Naibu wake kwa kuwasilisha hotuba nzuri. Hotuba hii imetoa dira ya sekta katika mwaka ujao kwa ufasaha mkubwa. Kama Mbunge wa Ngorongoro, Jimbo ambalo zaidi ya asilimia 80 ni hifadhi za wanyama pori, naomba kuchangia hotuba ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kubadilisha Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Act), Sheria ya Ngorongoro imepitwa na wakati na ni sheria ya siku nyingi sana, ni sheria ya kikoloni. Sheria hii haiendani na mazingira ya sasa ya uhifadhi na inapingana na sheria za sekta nyingine kama ardhi, barabara, Serikali za Mitaa na kadhalika. Aidha, Sheria hii ya Ngorongoro haiendani na Sheria Kuu ya Uhifadhi (Framework Legislation), yaani Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009.
Vilevile sheria hii haitambui dhana ya kushirikisha wananchi katika uhifadhi (community conservation), dhana ambayo ni muhimu sana kwenye eno la matumizi mseto ya ardhi (multiple land use). Ni rai yangu kwa Wizara ichukue haraka hatua za kurekebisha sheria hii kwa kushirikiana na wadau muhimu hususan wenyeji wanaoishi ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vijiji kunufaika na uwekezaji Ngorongoro, vijiji vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro havinufaiki moja kwa moja (direct benefits) kutokana na uwekezaji wa kitalii unaofanywa kwenye ardhi zao. Aidha, kwa utaratibu wa sasa wawekezaji hawalazimiki kuingia mkataba na vijiji badala yake wanaingia mkataba na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Kwa utaratibu huu ni vigumu wenyeji kupata ajira na fursa zingine zinazopatikana kwa kuingia mikataba na wawekezaji kama ilivyo kwa vijiji vingine Ngorongoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Wizara iainishe utaratibu wa kuviwezesha vijiji vya Hifadhi ya Ngorongoro kuweza kushirikishwa katika uwekezaji unaofanywa katika ardhi yao. Wizara iwalazimishe wawekezaji wanaotaka kujenga hoteli na kambi ya kitalii kupata ridhaa ya kimkataba kabla ya kuingia lease na mamlaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mgogoro wa Pori tengefu la Loliondo, ningependa vilevile kuchangia kuhusu mgogoro wa muda mrefu uliopo ndani ya pori tengefu la Loliondo (Loliondo Game Controlled Area). Mgogoro huu kwa sehemu kubwa umechangiwa na muingiliano wa mamlaka ya usimamizi wa eneo husika kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Serikali za Vijiji. Wizara ina mamlaka kuhusu rasilimali za wanyamapori lakini vijiji vina mamlaka kuhusu ardhi. Wizara ya Maliasili imetoa kibali cha uwindaji kwa kampuni ya OBC tangu mwaka 1992 bila ridhaa ya vijiji. Mgogoro huu umedumu kwa zaidi ya miaka 20 na hauelekei kuisha bila hatua maalum za kisheria kuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai yangu kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii itatekeleza matakwa ya Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 inayomtaka Waziri kutenganisha mapori tengefu (Game Controlled Areas) na ardhi ya vijiji ili kuondoa migogoro isiyokuwa na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la manyanyaso ya wananchi ndani ya pori tengefu la Loliondo, ningependa kuwasilisha kero inayowakumba wananchi wa Jimbo langu wanaoishi ndani ya pori tengefu la Loliondo. Askari na watendaji wa KDU wamekuwa na tabia ya kuwakamata na kuwanyanyasa wananchi pale wananchi wakikata miti kwa ajili ya ujenzi kwa kisingizio cha kuharibu mazingira. Wananchi wa kabila la kimaasai hawana tabia ya kukata miti hovyo au kuua wanyama na ndiyo maana eneo hilo lina wanyama na mazingira mazuri mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ardhi hii iko chini ya mamlaka za vijiji ambazo hazijakataza utumiaji wa ardhi kwa matumizi ya kujenga nyumba na maboma. Aidha, watendaji hao wamekuwa wakiwasumbua wananchi wasilime kwenye baadhi ya maeneo kwa kisingizio kuwa wanaharibu mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Wizara iwaonye watendaji wake waache tabia ya kuingilia mamlaka ya Serikali za Vijiji ambazo ndizo zinazohusika na mipango ya matumizi ya ardhi. Serikali za Vijiji kwenye pori tengefu la Loliondo ndilo zenye mamlaka ya matumizi ya ardhi. Ni vizuri Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Serikali za Mitaa (vijiji) pale inapohitaji kuchukua maamuzi kuhusu matumizi ya ardhi kwani ndizo zenye mamlaka kisheria.
Mheshimiwa Mmwenyekiti, baada ya kusema hayo machache naomba kuunga mkono hoja.