Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Martha Jachi Umbulla (20 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii. Kwanza kabisa na mimi nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema na kuwa mahali hapa leo hii, na kwa moyo wa dhati nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa hotuba nzuri na zaidi kwa mengi ambayo anawatayarishia Watanzania kupitia hotuba yake.
Mheshimwia Naibu Spika, wananchi wa Tanzania wamemuunga mkono sana Mheshimwia Rais kupitia hotuba yake na kwa hakika Tanzania nzima inampongeza, Afrika inampongeza na dunia inampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ameainisha maeneo mengi muhimu kwa maendeleo ya haraka ya nchi yetu. Vilevile ameainisha kero na malalamiko mengi sana ya Watanzania na baada ya kuainisha kupitia hotuba yake akatuletea sisi Wabunge wasaidizi wake ambao anatutarajia tuweze kumsaida katika kutatua kero hizo na malalamiko ya wananchi, alijua mahali pa kupeleka akijua kwamba Wabunge bila kujali kwamba ni wa chama gani wote ndiyo wananchi wanawategemea. Sasa kilichonishangaza mimi na kunisikitisha ni kujiuliza kwamba hivi wananchi wameiopokea na kuipongeza hotuba ya Rais na bila kujali itikadi. Amekwenda kila Jimbo akaainisha kero na malalamiko ya wananchi, sasa hawa wenzetu ambao hawakutaka kusikiliza hizi kero na malalamiko ya wananchi wanamwakilisha nani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningewaona mashujaa kama siku ile wangemsikiliza Mheshimiwa Rais, wakaona hotuba ile inasema nini na basi leo ama jana tulivyoanza kuchangia kwa kuona kwamba haiwafai basi wakatoka. Lakni tukashangaa wanaendelea kunga‟nga‟nia kujaribu kuchangia jambo ambalo hawakuweza kukubaliana naye. Lakini ya Mungu mengi niachie hapo.
Mheshimwia Naibu Spika, naomba nichangie kidogo sekta ya ardhi. Ardhi yetu imekuwa na thamani kubwa sana na inaendelea kuwa na thamani, tena kwa kasi kubwa sana, na hivyo kadri watu tunavyoongezeka na mifugo na mahitaji ya ardhi, kunakuwa na mahitaji makubwa ambayo ardhi inaendelea kuwa finyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mfano, kule kwetu Manyara kuna migogoro kila Wilaya na hasa kufuatia uhaba wa ardhi. Ukienda Wilaya ya Kiteto kuna migogoro, ukienda Wilaya ya Mbulu, ukienda Wilaya ya Hanang, ukienda Wilaya ya Babati, Simanjiro kote kuna migogoro kutokana na uhaba wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mapendekezo mazuri ya Mheshimwia Rais na maainisho yote ya kwenye framework ya mpango wa miaka mitano mimi naomba kutoa mawazo ya ziada. Nchi yetu tumejaliwa kuwa na mapori makubwa sana ambayo mengineyo yana-potential kubwa ya kuweza kuzalisha mazao na hasa kutumika kwa ufungaji. Sasa ninaomba kwa sababu wananchi wenyewe hawawezi kuyawezesha hayo mapori ili yaweze kutumika kwa kilimo na ufugaji, naiomba Serikali itenge bajeti ya maksudi kabisa, ili iweze kusaidia kuwezesha haya mapori makubwa ambayo ni potential yaweze kutumika kwa ajili ya kilimo na kwa ajili ya ufugaji na zaidi sana kwa ajili ya uwekezaji vilevile kwa sababu tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda.
Mheshimwia Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Manyara pia sasa hivi, kuna wimbi kubwa la wizi wa mifugo, wafugaji wanawaibia wakulima mifugo yao ikiwa ni njia mojawapo ya kuwafukuza wale wakulima ili waweze kuwaachia maeneo hayo waweze kuingiza mifugo yao. Sasa hii ni tabia inayopelekea mauaji, naiomba Serikali iweze kubuni ni namna gani wanaweza wakaikomesha hii tabia ya wizi wa mifugo ambayo pia inapelekea mauaji. Itakapotoa tamko ya kuhakisha kwamba Serikali imetoa tamko kuhakikisha kwamba inatoa adhabu kali kama fundisho wimbi hilo la wizi wa mifugo linaweza likapungua na wananchi watafanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya viwanda tunaiona na kwa hakika mimi nakubaliana nayo, viwanda vitajenga uchumi wetu kwa haraka na kuongeza Pato letu la Taifa. Ninakubaliana na mapendekezo yote yaliyopo kwenye Hotuba ya Rais wetu, lakini vilevile niombe kwamba Mkoa wetu sisi wa Manyara ni maarufu sana kwa kilimo cha mazao hasa vitunguu swaumu. Najua vitunguu swaumu siyo zao lililozoeleka, niwahakikishie lina soko hata nje ya nchi. Ninaiomba Serikali wakati ukifika tuweze kufikiria kuweka kiwanda katika Mkoa wetu wa Manyara hususani Wilaya ya Mbulu ambapo tunalima kwa wingi sana zao hili ambalo kwa sasa hivi soko lake halina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu matumizi ya shilingi milioni 50 alizoahidi Rais wetu. Tuna mifano mingi sana ya fedha za aina hiyo ikiwepo mabilioni ya Kikwete ambayo tuliyasikia kipindi kilichopita, lakini vilevile asilimia 10 ya fedha zinazotengwa na Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi kwa bahati mbaya hazikuwekewa mfumo mzuri ambao ungeweza kuwafikia walengwa. Ninaiomba Serikali itakapofikia wakati huo wa kutupa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na hasa kwa kuwawezesha wanawake na vijana na makundi mengine. Tuangalie isije ikaenda kwenye mfumo huo huo wa upotevu bali tuiwekee utaratibu mahsusi, bila haraka yoyote kuhakikisha kwamba kunakuwa na taaluma ya kutosha ili fedha hizi ziweze kuwafikia walengwa waweze kufanya kazi iliyokusudiwa na hivyo kufikisha dhamira ya Rais iliyo njema ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo waweze kufanya kazi yao kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa na haya machache naunga mkono hoja na naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa juhudi kubwa anayoiweka katika kuliongoza Taifa letu, ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uzima na kunipa afya kuweza kusimama hapa ili kuchangia hoja ya Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kwa kweli kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Naibu wake, na jopo zima la wataalam katika Wizara yao kwa kazi nzuri sana wanayoifanyia nchi yetu na kuitendea haki sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kipekee pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa dhamira njema sana ya kuhakikisha kwamba sekta ya afya hapa inakwenda kuboresha afya za wananchi walio wengi wa vijijini na hasa wale watu maskini ambao hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamekwishafanyika na Mheshimiwa Rais wetu, kipekee naomba nilenge sekta ya afya, ametenda mengi lakini kubwa ambalo katika sekta hii naweza kulisema ameondoa tatizo sugu la uhaba wa vitanda katika Hospitali ya Muhimbili; ameweza kutoa amri na kurekebisha vitendea kazi ambavyo vilikuwa havifanyi kazi, na zaidi sana dhamira yake njema ya kuboresha sekta ya afya kwa kuinua hadhi hospitali mbalimbali, vituo vya afya na zahanati katika vijiji katika kuboresha afya ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Mkoa wa Manyara hatuna la kusema, tunatoa pongezi na shukrani nyingi sana kwa kuridhia kupandisha hadhi Hospitali yetu ya Haydom ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja akaitembelea, akaiona na akatoa pendekezo kwamba anakubali iwe Hospitali ya Rufaa ya Kanda, lakini vilevile akatoa jopo la wataalamu kuja kuangalia vigezo na ninaamini kwamba vigezo vinakidhi. Kubwa la kushukuru amemtuma Mheshimiwa Waziri wa Afya hivi karibuni, hana hata siku tatu ametoka Manyara kuangalia Hospitali ya Haydom kama inakidhi vigezo vya kuwa Hospitali ya Rufaa. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu, hongera Mheshimiwa Waziri Mkuu, hongera Mheshimiwa Ummy Mwalimu na timu yako nzima katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ametupandishia hadhi kituo chetu cha afya cha Dongobesh kuwa Hospitali ya Wilaya na hilo nalo ni katika harakati za kuboresha afya katika Mkoa wetu wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatoa shukrani nyingi, kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. Lakini sambamba na kupandisha hadhi ya Hospitali ya Haydom kuwa ya Rufaa ninatoa tahadhari na ombi kwa Serikali kwamba mara nyingi wakipandisha hadhi hospitali, huduma zinazotolewa kwenye hospitali hizo zinakwenda kupanda gharama. Tunaomba kwa dhamira hiyo hiyo ya kuboresha afya katika vijiji tunaomba wasimamie kwamba Hospitali ya Haydom itakapopanda hadhi kuwa ya rufaa, basi na huduma zitakazotolewa ziweze kuwa wananchi wetu wanazimudu kwa maana ya kwamba kutopandisha gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na habari njema hizi nilizotaja bado Mkoa wa Manyara una matatizo lukuki. Kubwa sana ni katika Wilaya za Simanjiro na Kiteto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Kiteto, mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya ya Kiteto kwa miaka mitatu. Wilaya haina gari la wagonjwa. Miaka yote niliyokuwa pale, gari ni moja iko garage kila wakati, miundombinu ya Wilaya ile ni mibaya sana, bila gari wananchi wanafia barabarani na sasa hivi tunasikia habari njema za kugawa magari kwenda katika Wilaya mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa moyo wa dhati Hospitali ya Kiteto iweze kupata gari ya kubeba wagonjwa ili iweze kuondokana na tatizo la usafiri kwa wagonjwa wetu. Tukizingatia Wilaya ile ni kubwa sana, miundombinu ni mibaya barabara ni za rough roads, tunakuomba Mheshimiwa Ummy iangalie Kiteto kwa jicho la ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika Wilaya ya Simanjiro, hapo ndipo fungakazi. Wilaya ya ile ni ya siku nyingi lakini hakuna Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, leo, walivyosikia jina langu nachangia mchana, Mkurugenzi alinipigia simu. Akasema najua kwamba na Mbunge yupo mama tunaomba utoe kilio chetu kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Menyekiti, hakuna kituo cha afya pale au Wilaya yetu ya Simanjiro haina Hospitali ya Wilaya na hili ni tatizo kubwa sana. Wagonjwa wanatoka Orkesment kwenda kupata huduma ya afya Seliani – Arusha, kilometa karibu 200. Wanatoka Orkesment kwenda Mererani kilometa karibu 122, wataoka hapa wanakwenda KCMC kwa kilometa nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba, najua kwamba Wilaya imeshakuandikia barua toka Disemba, 2016 na ninadhani hapo nitashika shilingi pamoja na mambo mazuri na sifa niliyokupa.

Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Simanjiro iweze kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Urban cha Orkesment kuwa Hospitali ya Wilaya ili wananchi wale wapate huduma ya afya kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa hivi ambapo hali ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo niendelee kuchangia kwamba huduma za afya hasa zahanati zetu za vijijini, katika Wilaya hizo nilizotaja ni za duni sana. Hata hivyo tumepata habari njema kwamba, Wizara ya Afya imetenga shilingi bilioni 251, hizo zinakwenda kuboresha huduma za afya. Pamoja na hayo, katika zahanati na vituo vya afya vingi vijijini hakuna madaktari, hakuna wahudumu wataalam wa afya kwa hiyo, hizo fedha zinakwenda kutumika kwa jinsi ambavyo haitaboresha afya za wananchi. Tunaomba sambamba na kutoa fedha kwa ajili ya huduma za afya, Serikali iangalie kupeleka wataalam, madaktari, wauguzi na wahudumu wenye taaluma katika Wizara ya Afya. Kituo kizima kinakuwa na mhudumu ambaye hana hata elimu yoyote na ndiye anayetegemewa kama daktari, kama muuguzi. Haya ninayosema ni ya kweli, tufanye utafiti tusaidie wataalam waende katika wilaya zetu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haraka haraka nije kwenye sekta ya maendeleo ya jamii na mimi nioneshe masikitiko yangu kidogo katika sekta hii. Najua kwamba umefanya mengi na tumesikiliza jinsi ambavyo umetueleza mengi katika sekta ya afya na hata katika sekta ya maendeleo ya jamii, lakini niseme mengi bado yanaonekana kama nadharia. Tutakwenda kuboresha, tutasimamia, bado hatujapata hasa hasa ni nini kimefanyika, hatujaona sheria zinazokandamiza wanawake kuletwa hapa ili tuweze kuzirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuoni mikakati madhubuti ya kuondoa ajira haramu ya watoto wetu katika migodi na kadhalika. Hatujaona ni jinsi gani wazee wetu wanaenda kunufaika na hizi shilingi 251,000,000,000 za sekta ya afya. Kwa hiyo, mimi nitoe rai kwamba pengine ni vizuri Wizara ya Afya ni giant ministry, sekta ya maendeleo ya jamii ni kama imemezwa, nilikuwa nashauri na kwa kuzingatia kubana matumizi, pengine sekta ya maendeleo ya jamii ingeenda kwenye wizara ambayo si kubwa kama Wizara ya Afya ili iweze kutendewa haki na yenyewe iweze kuhudumia wananchi zaidi kwa jinsi ambavyo sasa hivi inahudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni ombi ambalo niliona nilitoe na ni mawazo yangu, lakini ninazingatia suala la kubana matumizi. Ninaomba kwamba Waziri atakapokuwa ana-wind up atueleze sasa sisi wananchi wa Mkoa wa Manyara, kwanza pamoja na shukrani tulizompa, na asituone kwamba hatuna shukrani, lakini atutendee haki katika Wilaya zetu nyingine, hasa hizi za wafugaji za Simanjiro na Kiteto. Waheshimiwa Wabunge wa Wilaya nilizotaja, mimi ni Mbunge wa Viti Maalum, tunajenga nyumba moja, tusaidiane wala mtu asinielewe vibaya, lakini mimi pia nimepata kura zangu kutoka kwa wananchi Wilaya hizo, naomba tusaidiane kuhakikisha kwamba na Wilaya hizi zinapata huduma ambazo wananchi wengine wanapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ni gari la kubeba wagonjwa. Wilaya zetu hizi zina kilometa nyingi sana, hususan Wilaya ya Simanjiro ina square kilometer zaidi ya 20,000; unaweza kuangalia kutoka kituo cha afya hadi makazi ya wananchi ni zaidi ya kilometa 20, 30 hadi 50, nadhani utaona umuhimu wa kupeleka gari katika maeneo haya. Tunakuomba Mheshimiwa Ummy na tunakuamini, wewe unatosha na unatosha kabisa na chenji inabaki, naomba upeleke gari katika Hospitali za Kiteto na Simanjiro ili tuweze kuhudumia wananchi wetu na wenyewe wanufaike na huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, hongera CCM, hongera Serikali yangu ya CCM kwa kufanya haya, hasa Serikali ya Awamu ya Tano, wamefanya kazi kubwa na tunampongeza Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia uzima na kuweza kusimama hapa kuchangia hoja
hii ya Wizara ya Elimu. Naomba na mimi nichukue fursa kama wenzangu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako, na Naibu Wake Mheshimiwa Stella Manyanya, aidha nimpe pole kwa msiba wa mama yetu na Mungu ampe subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ni ufunguo wa maisha na lazima Watanzania wapate elimu itakayowafungua katika maisha yao. Aidha, niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, kwa sababu imekwisha anza kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu wote na wanakuwa na ufunguo wa maisha kwa sababu ya kuanza mfumo wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya msingi pamoja na sekondari hadi kidato cha nne ni kama msingi wa nyumba, na kama msingi wa nyumba ni imara basi elimu yetu ya msingi na sekondari itakapokuwa imara tutakuwa na elimu iliyo bora hadi vyuo vikuu na hatimaye Watanzania wote watakuwa na elimu bora Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini elimu bora pia inatokana na walimu walio bora, na wenye moyo wa kufundisha kwa sababu walimu ndio watakaoweza kuboresha elimu yetu na kwa hivyo ni lazima tuhakikishe kwamba changamoto zote zinazokabili elimu ya msingi na elimu ya sekondari tuweze kuzitatua ili dhamira yetu ya kuboresha elimu kuanzia msingi na sekondari iweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kuzungumzia mazingira wezeshi kwa ajili ya walimu wetu hasa wa sekondari za kata. Walimu wetu wa sekondari za kata wako katika mazingira magumu sana, hasa sisi ambao tunatoka katika mikoa ya pembezoni. Walimu wengi wa sekondari hizi za kata wako katika maeneo ambayo hakuna umeme, maji, huduma mbali mbali za jamii, hospitali ziko mbali na hatimaye hata mitandao hizi ambazo vijana wengi wanazitumia hazipo; na kwa hivyo utaona changamoto nyingi zinazowakabili vijana hawa walimu ili waweze kufanya kazi katika Sekondari hizo ama maeneo hayo, inahitajika ushawishi ili waweze kuendelea kufanya kazi katika shule ama maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naiomba Serikali kwamba iweze kuangalia uwezekano wa kuwapa walimu wa sekondari za kata, na maeneo mengine yenye mazingira ambazo ni mbaya, waweze kupata hardship allowance ili iweze kuwapa motisha. Hili ni muhimu sana, najua walimu wengi wote wana matatizo ya hapa na pale, lakini hawa ambao wako katika sekondari hizi zenye mazingira ambayo sio wezeshi n wanahitaji uangalizi ama huruma ya Serikali kwa kuweza kuwapa motisha waweze kufundisha kwa sababu elimu bora kama ambavyo nilianza ni pamoja na mwalimu ambaye atakuwa na moyo wa kufundisha baada ya kuwezeshwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia mengi yameisha zungumzwa. Lakini ni suala zima la kutenga maeneo ya shule ambayo yatawezesha kilimo ya mashamba na bustani. Tuki-refer elimu za hapo awali, shule zetu nyingi zinakuwa na mashamba ama maeneo ambayo wanafunzi wanalima na kilimo hicho kinaweza kikasaidia pia kuwapatia chakula cha mchana, ama matunda ambayo yatawajenga wanafunzi wetu kiakili, kimwili na kiafya. Kwa hiyo, najua changamoto ya ardhi ambayo inakumba nchi yetu hasa kwa maeneo ya mjini lakini bado kwa maeneo ya mikoani tuna ardhi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uanzishwaji wa shule ziende sambamba na maeneo ambayo wanafunzi watapata kulima na kuweza kujijenga kimwili na kiafya. Lakini vilevile kupata chakula kwa bei nafuu. Tukisema wazazi waendelee kuchanga kwa ajili ya chakula cha mchana cha wanafunzi, bado ni mzigo na kwa hivyo tutafute namna rahisi ya kuweza kuwapatia wanafunzi wetu chakula cha mchana, kupunguza pia utoro shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia upungufu wa walimu wa sayansi. Hili limezungumzwa sana. Lakini mkoa wetu wa Manyara una upungufu mkubwa sana wa walimu wa sayansi, najua pengine na maeneo mengine lakini ya kwetu lazima niisemee, hatuna walimu kabisa wa masomo ya sayansi, kwa hivyo tunaomba Serikali iweze kuangalia inapo-allocate walimu, iweze kufikiria maeneo ambayo tayari kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itafute kila mbinu, jinsi ambavyo ilipata mbinu ya kujenga maabara nchi nzima, tukaweza kujenga kwa kipindi kifupi. Hiyo ni hatua ya kwanza na tumemaliza, na mimi naipongeza Serikali, wanaoibeza wana lao, lakini tayari tuna maabara zetu, nina hakika kwamba walimu wa sayansi watapatikana. Serikali iweke juhudi ya hali ya juu, kuhakikisha kwamba walimu wa sayansi wanapatikana ili waweze kufundisha masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa maabara umefanikiwa, lakini ninajua kwamba suala hili lilikuwa suala kama la zimamoto na imetumia fedha ambazo zilikuwa zimekusudiwa kwa madhumuni mengine. Kwa mfano, huko katika Wilaya yetu ya Mbulu ama Mkoa wetu wa Manyara, maabara tumezijenga katika Wilaya zote, lakini tumetumia fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi kwa hiyo baadhi ya miradi sasa hivi imekwama kwa kukosa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kulikuwa na ujenzi wa madaraja muhimu sana katika maeneo ya vijijini kama Daraja la Gunyoda kule Mbulu, ujenzi wa kituo cha afya kule Endagikoti, Mbulu, tayari miradi hii na miradi mingi ya umwagiliaji imekwama kwa sababu ya kukosa fedha, kwa sababu fedha zile zilikuwa diverted kwenda kujenga maabara. Naiomba Serikali iweze kuangalia hili na ihakikishe kwamba fedha hizi zinarudishwa ili miradi hii ya maendeleo iweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala zima la matatizo ya walimu wastaafu. Hili ni tatizo sugu na wengi wamelizungumzia, lakini ni kilio cha wastaafu walimu wengi ni lazima Serikali iwe sikivu, wananchi wanapolalamika kwa kipindi kirefu na kilio hiki cha wastaafu ambao hawapati stahili zao ni cha muda mrefu sana. Walimu wengi kipindi kile cha kupandisha madaraja kiliposimamishwa, wengi walikuwa wanaendelea kufanya kazi na huko wanastahili na wanapaswa kupandishwa daraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala hili lilikuja kufikia kupandishwa madaraja wakati wengi wameshastaafu vilevile, ninaiomba Wizara iangalie walimu ambao tayari walistahili kupandishwa na wamekaa katika cheo kimoja zaidi ya miaka 15, lakini hadi wanastaafu hawakuweza kupata stahili zao. Na sasa wako wengine ambao wamesimama kwa kipindi kirefu, mishahara yao inatofautiana na walimu ambao walikuwa nao wameajiliwa hata baada yao, lakini wana mishahara ambayo ni midogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nachukua fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Maliasili Utalii Profesa Maghembe, Naibu wake Engineer Ramo Makani kwa kazi nzuri sana wanayofanya kwa Wizara hii, kumbukeni methali ile isemayo mti wenye matunda hauishi kutupiwa mawe. Hata hivyo mmeweza na tunawatakia kazi njema na ya ufanisi kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo hoja zangu kadhaa ambazo naomba mnapo-wind up mnipatie majibu.
(i) Burunge Game Control Area iliyoko Makuyuni na Babati Vijijini ni eneo kubwa sana igawanywe ili ibakie sehemu ndogo tu na nyingine irudishiwe wananchi na hivyo sheria iliyoko ibadilishwe kuruhusu mapendekezo hayo.
(ii) WMA iliyoko eneo la Vilima Vitatu Babati ni mateso makubwa kwa wafugaji walioko eneo lile, kiasilia eneo hilo lilikuwa la wafugaji na hata baada ya kushtakiana na WMA wafugaji walishindwa kesi. Hadi leo wananchi hao hawajapewa haki yao, naiomba Wizara ilishughulikie suala hili kuwapa wananchi wa Vilima Vitatu utulivu wa maisha na usalama wa maisha yao na mifugo yao. Naomba kauli ya Wizara.;
(iii) Vijiji 16 vinavyozunguka hifadhi ya Tarangire na Magugu walipoondolewa waliambiwa watapewa kifuta jasho hadi leo kati ya fedha walizoahidiwa Tanzania zaidi ya shilingi milioni 100 wamepewa shilingi milioni 12 tu. Huu ni unyanyasaji wa wananchi. Naomba msaada wako Professa na naomba kauli ya Serikali.
(iv) Wananchi wanaozunguka Hifadhi za Ayamango, Gedamar na Giijedabonga – Babati wako pale tangu Operesheni Vijiji, leo na kwa muda mrefu ndani ya hifadhi isitoshe wengi wao hawajaonyeshwa maeneo ya kuhamia kila mara ni mapambano na askari na wanyamapori. Mheshimiwa Profesa na Engineer (Wizara) naomba sana mtoe suluhu ya migogoro hii, fidia wanayopewa haijengi hata choo.
(v) Wakati wa Operesheni Tokomeza aliuwawa mwanamke kwa maelezo yaliyotolewa hata hapa Bungeni na kwenye vyombo vya habari, Serikali iliunda Tume ya Kijaji na hadi leo hii hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Serikali. Mheshimiwa Jitu amewaandikia barua bila majibu yoyote, naiomba Wizara itoe kauli juu ya jambo hili linalosubiriwa na wananchi wa Babati na Mkoa wa Manyara.
(vi) Halmashauri ya Wilaya zinazopaswa kupata asilimia 0.3 ya service levy za hoteli za kitalii zinazopaswa kulipa Halmashauri lakini hoteli zimegoma kulipa kiasi hicho mpaka Mahakama ya Rufaa, lakini Wizara imekaa kimya. Tunaomba ufumbuzi wa malipo haya ya asilimia 0.3 service levy kwa Halmashauri husika hapa nchini ni imani yangu Mheshimiwa Waziri utatolea kauli.
(vii) Tanzania Forest Service wanakusanya ushuru mkubwa kutokana na mkaa wa magogo. Naiomba na naishauri Serikali kuwa taasisi hii irudishe kiasi fulani cha mauzo haya ili kuendeleza upandaji wa miti itafika mahali misitu itaisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARTHA J.UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa mchango wangu kwa hoja hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuthamini shughuli ndogo ndogo za wananchi katika kuzalisha mali, lakini naomba kutoa masikitiko yangu kuhusu wajasiriamali wadogo wanaonyweshea mbogamboga kutumia maji machafu yanayotiririka kwenye mifereji, Jijini Dar es Salaam. Mboga hizi huuzwa kwenye mahoteli mbalimbali jijini humo na kusababisha madhara kiafya pia inasababisha kinyaa kwa walaji. Kero hii inajulikana na watu wengi wakiwepo viongozi wanaoweza kufanya uamuzi kupiga marufuku kutumia maji hayo. Vinginevyo Serikali ishughulikie kusafisha mifereji yote michafu ili maji yanayotiririka humo yawe salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Sekta ya Kilimo, kuna athari kubwa sana ya uharibifu wa mazingira kwa mfano robo tatu ya ardhi ya Wilaya ya Kiteto imelimwa, (kuacha mapori yasiyofaa kwa kilimo na ufugaji) kwa sababu hiyo miti yote katika maeneo hayo yamekatwa na ardhi kubakia tupu (bila miti). Nini mikakati ya Serikali katika kunusuru Wilaya hiyo (ardhi yake) kugeuka kuwa jangwa? Tuliambiwa ardhi hiyo imepimwa miaka mitatu iliyopita, lakini hadi leo wakulima wakubwa wanaendelea kulima na ardhi inaendelea kuwa finyu pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Sekta hii; sehemu kubwa asilimia 80 inategemea fedha za nje, hali inayohatarisha kutekelezeka kwa miradi ya mazingira kwa sababu fedha za nje mara kwa mara haziletwi kwa wakati. Naomba kujua Serikali inasemaje kuhusu hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya na kuweza kuchangia hoja hii. Mchango wangu ni kama ifuatavyo:

(i) Fedha zinazotengwa na kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinachukua muda mrefu sana kutolewa na Hazina na pengine itolewe kidogo sana na hivyo kutokidhi ukamilishaji wa barabara zetu. Hali hii imeathiri sana ujenzi wa barabara zinazounganisha Mkoa wetu wa Manyara Makao Makuu Babati na Wilaya zake zote kwa kiwango cha lami. Matokeo yake hali hii ya kutokuwa na barabara za uhakika, hasa wakati wa masika, inarudisha nyuma uchumi wa mkoa na wilaya zote za mkoa wetu ambazo ziko pembezoni, bila barabara hali ya wananchi inabaki kuwa duni sana, hususani Wilaya za Mbulu, Simanjiro, Kiteto na Babati Vijijini. Tunaomba Serikali itoe fedha kwa wakati kwa barabara zote zilizo ndani ya Ilani ya CCM 2015- 2020 mfano barabara ya Kondoa – Kibaya – Kongowa; barabara za Babati – Dareda – Haydom - Mbulu na barabara zote zilizoko kwenye njia kuu za kiuchumi.

(ii) Serikali ibuni utaratibu mzuri wa kuboresha manunuzi ya umma. Uzembe na kukosa uaminifu kunasababisha kujenga miundombinu hafifu ya barabara na sekta nyinginezo zilizo ndani ya Wizara ya Ujenzi.

(iii) Serikali pia iweke fedha ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Arusha ambao sasa hivi hauruhusu ndege kubwa kutua. Uwanja huo utasaidia sana kwa sababu sasa hivi wageni wengi, wakiwepo watalii wengi wanatua KIA wanaelekea Arusha. Hivyo wakitua Arusha moja kwa moja itawawia rahisi kufika Arusha saa 1.30 bila adha ya kuandaa shultle na kuchukua muda mrefu kuliko muda waliotumia toka Dar es Salaam KIA kwa ndege (dakika 45-50).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kupata nafasi hii na mimi nichangie hoja iliyoko mbele yetu. Na mimi nichukue fursa hii kwanza kukupongeza wewe binafsi kwa umahiri wako na ushupavu wako wa kuliongoza vyema Bunge letu, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyoko mbele yetu ni mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti ya 2016/2017 na katika kuliangalia hilo, ni lazima tuangalie utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 ili tuweze kujifunza tulikosea wapi na vipi tujisahihishe ili tuweze kwenda vizuri kwa bajeti yetu ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vipaumbele vilivyowekwa katika bajeti ya 2015/2016 mimi nimevichukua viwili ili niweze kuvichambua tuone ufanikiwaji ulikwenda kwa kiwango gani? La kwanza kabisa, kipaumbele chetu cha kwanza ilikuwa kupunguza umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la kupunguza umaskini, tukiangalia katika jamii zetu, kwa mabilioni na matrilioni ya fedha tulizowasomea wananchi mwaka 2015, ni kwa kiwango gani umaskini umepungua baina ya jamii yetu ya Watanzania. Hali bado ni mbaya sana vijijini, wananchi wetu bado hawana milo mitatu, wananchi hawana nyumba bora za kuishi, wananchi wetu bado hawana vyanzo vya uhakika vya fedha na kwa hiyo, ni vizuri kutafakari, ni kwa namna gani umaskini utapungua katika nchi yetu hasa kwa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujipima hivyo, ni vizuri pia tukaangalia changamoto zilizojitokeza, changamoto kubwa ambayo imejitokeza katika kupunguza umaskini baina ya jamii zetu, kubwa ambalo limeonekana ni upatikanaji wa rasilimali fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali imeweka mfumo thabiti wa ukusanyaji wa fedha katika bajeti ya mwaka huu na zaidi sana ni hili la kutumia electronic machines. Mfumo huu bado una changamoto kubwa sana. Pamoja na kuweka mikakati na adhabu zitakazotolewa kwa ajili ya watakaokiuka kutoza kutumia mashine hizo, bado mimi nina wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vituo vya petroli, kwa mfano, wakikwambia mashine hii ni mbovu ama iko out of order na ni kweli utakavyodhihirika hivyo, bado utakapomchukulia hatua mfanyabiashara ambaye mashine yake hiyo ni mbovu, utakuwa hujamtendea haki. Kwa sababu utakuta ni ukweli na umempa adhabu na kutakuwa na msururu wa watu kutaka huduma na watakapokosa huduma ya kupata petroli na dizeli wataleta lawama tena kwa Serikali. Kwa hiyo, nadhani tuangalie ni namna gani tutaboresha mfumo mzuri wa ukusanyaji kodi ili tuweze kutekeleza miradi yetu ya maendeleo katika Vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nililotaka kuishauri Serikali ni kwamba bajeti iendane na tathmini halisi ambayo tumeiona katika utekelezaji wa kipindi kilichopita. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona kwamba pamoja na jitihada za kupunguza umasikini ametenga shilingi milioni 50 kila kijiji. Dhamira yake ni njema na itakapotekelezwa itakwenda vizuri. Utekelezaji watatengeneza wataalam, lakini bado ametenga fedha hizo ili kuona ni namna gani umasikini utapungua katika jamii zetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kipaumbele cha pili, kilikuwa upatikanaji wa huduma za jamii. Kilio kikubwa cha Waheshimiwa Wabunge tangu waanze michango humu tumeona ni kilio cha maji. Maji bado ni tatizo kubwa katika jamii zetu na kwa hiyo, kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ni vizuri kuendelea kubuni mikakati bora ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. Sasa utaratibu uliopo, naipongeza pia Serikali kwa kutenga hiyo asilimia ndogo ya kuongeza kwenye tozo ya mafuta ya shilingi 100. Nina uhakika shilingi bilioni 250 zitakapopatikana, shilingi bilioni 220 zikienda kwenye usambazaji wa maji vijjijini itasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni mkatakati mzuri na mimi nauamini kwa sababu tozo ya kwenye mafuta na petroli ni tozo yenye uhakika, kwa sababu huduma hiyo ipo kila siku na tumeona kwenye miradi ya REA pia. Tozo zilizowekwa kwenye REA imetusaidia kusambaza umeme vijijini na kwa hiyo, hiki ni chanzo ambacho kinaweza kikatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma nyingine ya jamii ni suala la elimu. Nampongeza tena Mheshimiwa Rais kwa kuleta mfumo wa elimu bure, nina hakika tathmini mwisho wa siku itakwenda vizuri katika kuboresha elimu katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la huduma za afya. Huduma za afya ni kipaumbele kingine cha pili baada ya maji. Suala la afya hasa kwa kabrasha hili ambalo limetolewa na TAMISEMI kwa Mkoa wangu wa Manyara, ni masikitiko makubwa sana. Nimeona katika taarifa hii iliyotolewa na TAMISEMI na hasa ikishirikiana na Wizara ya Afya; Mkoa wa Manyara katika mlolongo wa kuodhoresha zahanati na uboreshaji na ukarabati wa vituo vya afya, nimesikitika kuona Wilaya ya Simanjiro imewekewa zahanati moja tu, wakati Mikoa mingine na Wilaya nyingine zina zahanati mpaka 10 hadi 15. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Wilaya ya Kiteto kubwa kama hiyo, imewekewa zahanati tatu tu. Tena cha kusikitisha fedha ambazo zitakwenda kukarabati majengo hayo ni Capital Development Grants ambazo mara nyingi wala hazipatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha kwa Mkoa wa Manyara, sijui mikoa mingine imetumia mbinu gani kuhakikisha kwamba wamewekewa fedha za kutosha, lakini naiomba Wizara na Serikali na hasa maeneo husika kwamba waangalie hili. Wilaya ya Mbulu ina Majimbo mawili, lakini zahanati na vituo vya afya vilivyoorodheshwa hapa na vya Jimbo la Mbulu Mjini; tunaishukuru Serikali kwa hilo kwa sababu na mimi natokea huko, lakini ni vizuri kuiona Mbulu Vijijini kwani hakuna hata zahanati moja iliyoorodheshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeliona kabrasha hili nikadhani kwamba ni makosa yamefanyika, naamini kwamba wahusika watakwenda kuiangalia vyema na kuhakikisha kwamba kila Wilaya inanufaika na usambazaji ama upatikanaji wa huduma za afya ikiwepo kujenga zahanati na vituo vya afya katika kila kijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo…

NAIBU SPIKA: Kengele ni ya pili hiyo Mheshimiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara ya hii ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamezungumzwa na wazungumzaji wamenifilisi kidogo lakini niendelee kusisitiza kwamba kwanza naishukuru Serikali yangu kwa kuhakikisha kwamba bajeti ya mwaka asilimia 40 zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo. Hii ni hatua ambayo imekuwepo kwa mara ya kwanza na kabla kabisa ya utekelezaji, kadri wenzangu walivyosisitiza tunaomba na kwa muda mrefu tumesisitiza kwamba Sheria ya Manunuzi iletwe haraka sana Bungeni tuweze kuifanyia marekebisho ili asilimia hiyo 40 iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo iweze kuwa na impact kwa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupanga matumizi ni jambo moja lakini kutekeleza yale yaliyokusudiwa ni jambo la pili na la muhimu zaidi. Nishauri Wizara kuhakikisha kuwa yale yote yaliyokusudiwa, yaliyopangiwa matumizi yaweze kutekelezwa jinsi ambavyo Bunge litapitisha na kuidhinisha matumizi hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hadi kufikia Machi 2016 fedha zile zilizokuwa zimepangwa kwa bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa mfano mafungu 62 yale yaliyoko chini ya Serikali Kuu ni mafungu 33 yaliweza kupewa fedha kwa asilimia 50. Kwa hiyo, ni wazi kwamba bajeti hiyo haitakidhi matarajio yale ama matumizi yale ambayo yamepangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria ya bajeti ambayo ni ya 2015 mwaka jana tu, tunatarajia kwamba sheria hiyo italeta impact kwa bajeti ya mwaka huu. Kwa kuwa kuna sheria, tuna imani kwamba matumizi ya fedha ambazo zimepangwa kufikishwa katika miradi yetu yatasimamiwa na sheria hiyo. Zaidi sana kwa kuwa tuna mid term review ya bajeti yetu, tunaamini kwamba Sheria ya Bajeti itaisimamia kikamilifu kuhakikisha kwamba jinsi Bunge litakavyoidhinisha fedha hizo zitaweza kufikishwa jinsi zilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu spika, nizungumzie na mimi mradi wa Village Empowerment maarufu kama shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Kwanza ni-declare interest kwamba mimi nina utaalamu kiasi fulani wa micro-finance na kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu kwa kubuni mradi huu wa shilingi milioni 50 kila kijiji. Pia nieleze hofu yangu, sijajua vizuri kwamba hiyo shilingi milioni 50 ambazo zitatolewa kama mikopo kwa wajasiriamali ni pamoja na fedha zitakazotumika katika kuhamasisha wananchi ama zitakazotumika katika kuweka wataalamu watakaosimamia miradi hiyo ama ni fedha zitatengwa na bajeti nyingine ili kuweza kuhakikisha kwamba shilingi milioni 50 kwa kila kijiji inamfikia kila mwananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze wasiwasi wangu pia kwamba je, shilingi milioni 50 zinavyokwenda kwenye kijiji ni kwa jinsi gani kila mwanakijiji atafikiwa na fedha hizo? Kama hivyo ndivyo ilivyo na nadhani ndiyo matarajio ya Rais wetu kwamba kila mtu atapaswa kupata mkopo hasa wale waliolengwa wanawake na vijana. Kwa hiyo, ni lazima kuwe na mkakati madhubuti kuhakikisha kwamba hizi fedha zinawafikia walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, fedha hizo zinawafikiaje? Mimi siamini utaratibu huu wa SACCOS, naamini zaidi utaratibu wa revolving loan fund ili fedha hizi zitakapotolewa kwa awamu ziweze kuzunguka zimfikie kila mwananchi. Kwa sababu tuna uzoefu tumeona kwamba katika mifuko mingine ambayo tumeahidiwa na viongozi wetu, kwa mfano mabilioni ya JK, bahati nzuri mimi nilikuwa mmoja wa walioteuliwa kati ya Wabunge saba kushauri katika ile National Executive Empowerment Council lakini tukaishia kupata barua na hatukuweza kuitwa hata siku moja na hatukujua hata yalikwendaje na yaliishia wapi. Kwa hiyo, tuna hofu kutokana na uzoefu wa kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba fedha hizi za sasa zikiwekewa utaratibu madhubuti, zikawekewa na riba kwa sababu riba ni suala muhimu sana katika kukopesha wananchi, unapoweka riba inazalisha zaidi na kupunguza uzito kwa Serikali kwa sababu ile riba inaweza ikatumika katika kuhakikisha kwamba kunakuwepo na wataalamu watakaolipwa ili wasimamie kwa kikamilifu utoaji wa mikopo na urejeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilishikwa na wasiwasi kama Wajumbe wengine wa Kamati yangu, ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, kwa shilingi milioni 50 zinapaswa ziende shilingi bilioni 980 na zitafikia jumla ya vijiji 19,600. Hata hivyo, tunaona kwamba zimetengwa tu shilingi bilioni 59.5 ambazo hazitoshi kabisa. Kwa hiyo, naishauri Serikali yangu iongeze bajeti hiyo ili azma ya kufikia kila kijiji kwa shilingi milioni 50 iweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile fedha hizi ziwekewe utaratibu ili zisiweze kupotea kama ambavyo tunaona utaratibu wa mikopo ya Halmashauri inavyopotoea kwa sababu haina ufuatiliaji, haina riba, haina hata namna yoyote ili ya kufuatilia nani kapewa, nani karejesha na kwa muda gani urejeshaji ufanyike. Mkopo ni fedha unayompa mtu kwa matarajio ya kurejesha kwa hivyo ni lazima uwe na utaratibu madhubuti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamekwishasemwa lakini nashauri kwamba utaratibu huu wa revolving loan fund ni sawa unapompa mtu mwenye njaa samaki ukitarajia kwamba kesho atakuomba tena, lakini kumbe ni vizuri basi ukampa mtu vifaa vya kuvulia samaki ili aendelee kupata chakula badala ya kumpa samaki ambaye atakula leo tu na kesho atakuwa hana kitu. Kwa hivyo, mimi nashauri, revolving loan fund ndiyo utaratibu ambao utawezesha kila mwananchi kufikiwa ndani ya kijiji na hatimaye mradi utakuwa endelevu, hata Rais atakapokuwa amemaliza muda wake wa miaka kumi, atakuwa ameacha legacy ya mikopo hii inaendelea ndani ya nchi yetu, wananchi wanaendelea kukopeshana na hatimaye tunapunguza umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na haya machache mengine yamezungumziwa sina sababu ya kurudia, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa nami nitoe mchango wangu kwenye sekta hii ya maji. Nami nachukua nafasi hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Engineer Lwenge na Naibu wake, kwa kweli wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni; wametembelea sana Mkoa wetu wa Manyara, wameona changamoto mbalimbali; pale palipowezekana, walitatua na kule ambako hapawezekani tunaendelea kuwaomba watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna asiyekubali kwamba changamoto kubwa katika nchi yetu ni uhaba wa maji. Kilio cha Waheshimiwa Wabunge hakijaanza leo, ni miaka mingi huko nyuma na hadi sasa tumewasikia Waheshimiwa Wabunge. Kama kungekuwa na mahali pana nafuu, tungeelezwa humu ndani. Bado changamoto inayokabili Taifa letu ni uhaba wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha ni kuona kwamba kila mtu anaeleza kwa ufasaha, anajua changamoto ni uhaba wa maji. Penginepo wanaeleza pia ni namna gani tuondokane na tatizo hili, lakini bado hatuna majawabu. Tuna program nyingi za maji, tuna mikakati, tuna mipango kadhaa, lakini hakuna ambacho tunaweza kutamba nacho leo kusema kwamba mipango hii na program hizi na mikakati hii imeweza kuleta unafuu wa uhaba wa maji kwa kaya pengine hata laki mbili kwa mahali fulani. Hiyo hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuendelee kuweka mikakati madhubuti ambayo ni halisia. Tufanye nini ili kuondokana na uhaba wa maji? Tuache kulia sana hapa, wapanga bajeti ni sisi wenyewe, mipango yote tunatengeneza wenyewe; kwa hiyo, tukiendelea kulia hapa kwa miaka mingi, nadhani hatuna majawabu. Ni muda muafaka sasa tuweze kupata majawabu, nini kifanyike ili tuweze kuondokana na tatizo hili la uhaba wa maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuona sura ya umaskini, tembelea kijiji ambacho hakuna hata tone la maji, halafu ukitoka pale tembelea na kijiji ambacho kina maji. Ukitoka hapo utakubaliana nami kwamba kusema kweli maji ni uhai, maji huondoa umaskini, maji huondoa maradhi na maji ni kila kitu; maji ni viwanda na uchumi wa kati katika nchi yetu. Kama hivyo ndivyo kwamba maji ni kila kitu, iweje sasa bajeti ya maji ya mwaka 2016 ambayo ilipangwa shilingi bilioni 900 ikatolewa shilingi bilioni 180 tu kwa ajili ya Sekta ya Maji, hapo ndiyo unakuja mchanganyiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza nikawa nimesahau kidogo takwimu naomba radhi, lakini ukweli ni kwamba fedha zinayotolewa kwa ajili ya miradi ya maji ni kidogo sana kulingana na bajeti inayowekwa. Kwa ajili hiyo, naomba tupange bajeti yenye uhalisia, tusiwadanganye wananchi kusoma matrilioni ya pesa hapa, lakini fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi muhimu sana kama ya maji ni kidogo kama ambavyo tunaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza sana kuhusu mikakati ya kuondokana na uhaba wa maji, lakini tunajua kwamba nchi yetu ni tajiri sana, tumejaaliwa na Mwenyezi Mungu, tuna mito, tuna maziwa tuna wataalam waliobobea, nadhani tunakosa ubunifu. Tuanze kubuni ni namna gani tunaondokana na tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri ambao nilishautoa hata kwenye michango yangu ya huko nyuma, kwamba, tuangalie sekta ambazo tumeshafanya vizuri kiasi fulani kama Sekta ya Barabara, tu pull resources za sekta hiyo pamoja na nyingine ili tuelekeze kwenye miradi ya maji. Tukimaliza kuondokana na tatizo hilo, tunaweza tukarudi kuendelea na sekta zetu za barabara na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni jambo muhimu ambalo naona pengine litakuwa ni suluhisho pamoja na mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuzungumzia. Ni lazima tuwe wabunifu ili tuweze kufikia mahali tuseme sasa basi tumechoka na kulia kilio hiki cha uhaba wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukikosa chakula unaweza ukaagiza hata kwa jirani yako ukaomba msaada, ama ukaagiza hata nje ama nchi jirani, lakini kwa vyovyote vile huwezi kuomba msaada wa kupewa maji kutoka nje ama kwa nchi jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni sisi wenyewe, majawabu tunayo wenyewe tuone ni namna gani tuweze sasa kukaa chini na kuona tunasaidiaje katika kuondoa changamoto hii ya maji inayotukabili. Kama hivyo ndivyo, iweje bajeti ya mwaka 2016 sasa iwe imeshuka mwaka huu wakati bado tunasema kwamba changamoto yetu kubwa ni uhaba wa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na wenzangu wote kusema kwamba, tozo ambayo tunaweka kwenye petrol na diesel iweze kuongezwa hadi sh.100/= ili na yenyewe isukume. Siyo hiyo tu, nilikuwa nashauri kwamba tuangalie hata maeneo mengine kama EWURA, TANESCO na kwingineko tujaribu kuona ni namna gani tunajizatiti, tufanye maamuzi magumu kuweza kuondokana na tatizo la uhaba wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza sana kuhusu changamoto hii, hebu sasa Wizara iweze kukosa usingizi kuhakikisha kwamba inafanya ubunifu kuondokana na tatizo hili la uhaba wa maji. Tukiacha bajeti ya kushuka, Hazina inathubutuje kuchelewesha fedha zinazokwenda kwenye miradi ya maji? Kuchelewesha fedha za miradi ni tatizo sugu la Hazina. Tunataka pia wakati Wizara inafanya majumuisho, ituambie kuna tatizo gani Hazina kuchelewesha fedha za miradi, ikiwepo na miradi ya maji kama ambavyo tunaiona? Tunaomba hili tatizo sugu nalo liweze kuondoka, tusiwachanganye wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mipango yetu na programs za maji, nashauri tuweke benchmarks ili tuweze kupima mipango yetu tunayotengeneza, tuweze kujua kwamba mwaka 2016 tulipanga mipango hii na sasa hii ndiyo benchmark, tumefikia hatua hii, lakini kusema kwamba tunajizatiti ama tunaendelea kupanga mipango ambayo haitekelezeki, ama inatekelezwa lakini haina majawabu, nadhani hatutafikia muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nioanishe uhaba wa maji na maisha ya wanawake wa Tanzania hasa wa vijijini. Kwa bahati mbaya teknolojia ya kisasa haijaweza kumsaidia mwanamke aondokane na tatizo la kubeba maji kichwani huko vijijini. Siyo hilo tu, usafiri wa mwanamke wa kijijini kwa bahati mbaya, teknolojia haijamsadia, bado anatembea kwa miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuweze kuwasaidia wanawake hawa wa vijijini hasa wanawake wa jamii ya kifugaji. Wanawake hawa wanaotafuta maji, siyo maji tu kwa ajili ya binadamu, ni pamoja na mifugo.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kupata fursa hii niweze kuchangia hoja ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanyia nchi yetu katika sekta ya viwanda. Kama kweli kila mtu amesoma vizuri kitabu hiki, na mimi ni mara chache sana nasoma vitabu vya Wizara, lakini katika wizara hii nadhani kwa sababu nilikuwa najua kwamba nitachangia nimesoma vizuri sana; kusema kweli nia njema ya Serikali yetu baada ya kusoma kitabu hiki ya kuhakikisha kwamba inatuvusha kwenda uchumi wa kati na uchumi wa viwanda, nina hakika tutafikiwa hasa kwa takwimu ambazo zimesheheni katika kitabu hiki cha Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu nikianza na sekta ya viwanda, katika nchi yetu. Sekta ya Viwanda ni ya kimkakati, kwa nini nasema ni ya kimkakati? Si tu inaenda kupeleka nchi yetu katika uchumi wa kati lakini inakwenda kutatua changamoto nyingi ambazo nchi yetu na wananchi wetu wamekuwa wakipigia kelele sana, nikianza na migogoro ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na wafugaji. Kama tutazingatia maelekezo ya nia ya Serikali yetu katika kutupeleka kwenye viwanda, nina hakika wafugaji wetu wanakwenda kuachana na matatizo ya kuhangaika kugombania ardhi, kunyanganyana ardhi na wakulima kwa sababu azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaenda kujenga viwanda vya nyama, ngozi, pamoja na maziwa.

Kama tutapata viwanda hivi na mazao yote yanayotokana na mifugo nina hakika kwamba wakulima wetu wanakwenda kupunguza mifugo yao maradufu na matatizo ya kuhamahama na mifugo kuhakikisha kwamba nchi yetu sasa inafuga kwa namna ambayo wana uwezo wa kupata kunufaika kwa mifugo yao na nina hakika migogoro hiyo itapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwa wakulima. Wakulima wetu wamekuwa na matatizo makubwa ya kukosa masoko. Hamasa kubwa ya mkulima ni kumuhakikishia soko. Kama viwanda vyetu vitakwenda kuchukua malighafi ya kilimo nina hakika kwamba wakulima wetu watahamasika vilivyo, watalima kwa bidii, tena kwa ubora unaotakiwa ili malighafi ambazo zitatumika katika viwanda vyetu hivi vitokane na mazao ya kilimo. Kwa hiyo, nina hakika kwamba hata umasikini wa kipato ambao bado umekidhiri baina ya watanzania, umasikini pamoja na MKUKUTA I, II, III uliokuwepo bado umebaki palepale. Tutakapogusa sekta inayowaajiri watu wengi ambayo ni kilimo na ufugaji nina hakika umaskini utapungua maradufu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nirudi kwenye point yangu ya kusema kwamba viwanda ni mkakati maalum wa kuvusha nchi yetu kuondokana na matatizo mbalimbali. Tutakuwa na biashara ya uhakika, tutakuwa tumepunguza umasikini kwa jinsi nilivyoeleza, kwa sababu sekta inayogusa watu wengi ni ya kilimo na ufugaji. Tutakuwa tumehamasisha pia vijana kujiunga na kilimo kwa hivyo tutakuwa tumeongeza ajira kwa wananchi wetu, lakini pia tutakuwa tumepunguza migogoro ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu biashara ya utalii. Katika biashara ya utalii nchi yetu bado haijanufaika kadri ambavyo inalingana na maliasili tuliyonayo, rasilimali tulizonazo katika sekta hii. Tunayo mapori mazuri sana katika nchi yetu ambayo hayapo kule duniani, tunao wanyamapori wazuri ambao hawapo katika nchi mbalimbali, lakini nchi yetu bado haijanufaika kwa jinsi ambavyo tuna maliasili hiyo niliyotaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo amekuwa mbunifu ameona kama tutakuwa na maliasili ya aina hii, tuwe na mapori mazuri, wanyama wazuri, lakini kama watalii hawaji kwetu kuja kuangalia maeneo haya, bado hatutakuwa tumenufaika. Kwa hiyo, amekuwa mbunifu, na biashara ni ubunifu na viwanda ni mbunifu. Amenunua ndege ambazo atahakikisha watalii wetu watakuja Tanzania, watakuja kutembelea mapori niliyoyataja kwa ajili ya kuona wanyama wetu na hivyo uchumi wetu utakwenda kasi na kuhakikisha kwamba tunanufaika na sekta hiyo ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kambi ya Upinzani Bungeni ukurasa wa 23 imebeza ununuzi wa ndege. Kubeza sikatai kwa sababu ni kazi yao, lakini wabeze kwa takwimu. Mimi nimeeleza kwamba huo ni mkakati kwa sababu hata Biblia inasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Hayo ni maarifa ya kuhakikisha kwamba tunawaleta watalii nchini mwetu ili tunufaike na sekta yetu ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niweze kutoa ushauri kwa Serikali. Tozo katika sekta hii bado ni tatizo. Watalii wakisikia kwamba Tanzania wanatoza VAT kwenye huduma za utalii, bado kuna hatari ya kupunguza manufaa tutakayopata kwa sababu atakwenda katika nchi nyingine na sisi tutabaki kulalamika. Ninaomba Serikali yangu kama si tatizo kubwa iondoe tozo la VAT kwenye huduma za utalii ili tuweze kunufaika maradufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu Benki ya Rasilimali (TIB). Benki hii iko Dar es Salaam, biashara ni mikopo, tunaomba Benki ya Biashara ifungue matawi yake katika mikoa mbalimbali ili wananchi wetu waweze kukopa, wakulima waweze kukopa ili waweze kupata mitaji ya kutosha kuweza kuendesha biashara zao. Ninaiomba Serikali yangu iweze kufikiria jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sasa Mkoa wangu wa Manyara. Mkoa wetu wa Manyara uko pembezoni na mkoa huu uchumi wake uko chini, lakini cha kushangaza ni kwamba tunayo mazao mengi ambayo mengine pia hayapo popote pale Tanzania. Kwa mfano zao la pareto, linalimwa kwa uchache sana kule kusini lakini mazao mengi ya pareto yanaozeana kwenye godown kwa sababu hakuna soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali iweze kuangalia uwezekano wa kuanzisha kiwanda kule Bashnet ambako tunalima sana zao la pareto. Pareto ni zao zuri sana, dawa ya mbu ambayo ni very effective kuliko dawa zote, inaitwa expel inatengenezwa kutokana na pareto. Kwa hivyo, tunaiomba Serikali iweze kutujengea kiwanda katika Mkoa wetu wa Manyara hususan Bashnet. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunalima vitunguu saumu. Vitunguu saumu ni zao ambalo kwa kweli ubora wake sina haja ya kueleza, lakini wakulima wanalima kwa kutumia zana duni, wakulima hawanufaiki kwa sababu, masoko bado yako chini. Ninaiomba Serikali yangu katika harakati hii ya kuanzisha viwanda hasa kujenga mkoa wetu wa Manyara ambao upo pembezoni na uchumi wake uko chini lakini una rasilimali nyingi iweze kutujengea kiwanda kule Mbulu ambako tunalima zao la vitunguu saumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza kidogo, maeneo ambayo yana mifugo mingi kanda ya kaskazini mkoa wangu wa Manyara, Wilaya ya Mbulu inaongoza kuwa na mifugo mingi, Wilaya ya Kiteto, Simanjiro na Hanang, lakini cha kushangaza kiwanda cha nyama kipo Arusha. Tunaiomba Serikali na sisi Manyara iweze kutujengea kiwanda cha nyama Mkoa wa Arusha ili wananchi wetu wafugaji waweze kunufaika kutokana na mazao yao ya mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwa msisitizo kabisa mikoa ya pembezoni kama Manyara ni mikoa ambayo inalimwa mazao mengi kama mahindi, maharage na mazao mengine ndiyo maana bodi nyingi za mazao yameanzishwa, bodi ya korosho, bodi ya katani, lakini sisi hatuna bodi huko. Lakini tunaomba recognition ya Serikali kuona kwamba mkoa wetu unazalisha mazao mengi ya biashara, tunaomba viwanda vielekezwe kule ili na sisi tuweze kunufaika na sekta hii ya viwanda na biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza haya naomba kuunga mkono hoja, na nashukuru kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia hoja iiyopo mbele yetu. Nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa ofisi yake kwa kazi nzuri wanayoifanya nchi yetu. Kipekee Mheshimiwa Waziri amekuja Mkoani kwetu Manyara, ametusaidia migogoro mingi na kwa kweli Mungu aendelee kumwongoza na kumpa afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye sekta ya ardhi, rasilimali ardhi hakuna asiyejua umuhimu wake na uhitaji wake sasa hivi katika nchi yetu. Uhitaji wa ardhi miaka 30 iliyopita na leo, mwaka huu tuliopo na miaka 30 ijayo ni tofauti kabisa kuashiria kwamba nchi yetu inanyemelewa na ufinyu wa ardhi. Hili ni jambo la hatari kama hatutaweka mipango madhubuti katika kuiweka ardhi yetu iweze kutusaidia katika mipango yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana jioni tulikuwa na mjadala mzito baina ya Wabunge wanaotetea wakulima na wengine wanaolaumu wafugaji, lakini hakuna mshindi hata wangetumia lugha namna gani kusema kwamba wafugaji ni wabaya, wakulima ni wabaya wanafanya hivi na vile kwa sababu wakulima ni Watanzania wale wale na wataishia kuwa Watanzania na wataendelea kulima na wafugaji hali kadhalika ni Watanzania wataendelea kufuga na wataendelea kuwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la maana ni kuhakikisha kwamba tunabuni mipango madhubuti ili kuhakikisha kwamba jamii zote mbili hizi na hata watumiaji wengine wa ardhi wanaishi vizuri katika nchi yao bila kuwa na migogoro ya hapa na pale na bila ya kuwa na migogoro ya kuvamia ardhi na kusababisha maafa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ninaloona ni kubadilisha mindset, ni lazima tubadilishe mindset yetu. Huwa natumia mfano wa mkoa mdogo wa Kilimanjaro kulinganisha na Mkoa wetu wa Manyara, ukiangalia Mkoa wa Kilimanjaro mnisamehe wananchi wa Kilimanjaro na Wabunge wa huko. Mkoa wa Kilimanjaro una eneo dogo sana lakini una watu wengi, Mkoa wa Manyara una eneo kubwa sana watu ni wachache, lakini utakuta katika eneo dogo hilo hakuna migogoro inayolingana na migogoro iliyoko Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu wananchi wa Kilimanjaro toka mwanzo waliona kwamba ardhi yao ni finyu kwa hiyo lazima waweke mikakati madhubuti, wameweka mindset yao kwamba ni lazima ardhi yao finyu wanaitumia kwa busara ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi wao. Kwa hivyo eneo kubwa linaleta udanganyifu kwamba bado ardhi yetu ni kubwa kwa hiyo tunaweza tukavamia hapa tukaitumia kwa ajili ya matumizi ya mashamba au kufuga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima tubuni kama nilivyoeleza, kwamba ardhi inanyemelewa na ufinyu wa ardhi na ongezeko kubwa la watu, kwa hivyo lazima kuwe na ubunifu. Jana nilikuwa nasoma mipango ya miaka mitano yaani 2015/2016 na 2016/2017. Tuna mipango mizuri sana, tuna mipango madhubuti kuhusu sekta ya ardhi, lakini cha kushangaza bado hatuwezi kutamba leo kusema mipango tuliojiwekea imeweza kuleta impact hii hasa katika sekta ya ardhi, hivyo bado tuna safari ndefu kuhakikisha mipango yetu tunayopanga lazima iwe real, iende sambamba na hali halisi, kama kuna ongezeko kubwa la watu ni lazima ardhi yetu iende sambamba na ongezeko kubwa la watu na kuhakikisha kwamba inatumika madhubuti na inatutosha kwa matumizi yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tujizatiti na matumizi bora ya ardhi. Naishauri Serikali kwamba to pull resources zote sasa hivi kwa sababu kilio hiki ni kikubwa. Tangu niingie Bungeni hapa kilio cha wakulima na wafugaji kiko pale pale, sijaona tofauti, kilio kinazidi kila siku na kwa kilio hicho, tukiangalie sasa mipango yetu iweze kutupa ahueni. Tuhakikishe resources tulizonazo tuweze kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi yetu ili tuondoe kilio cha wakulima wetu na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali pia kutoa elimu hasa kwa jamii ya wafugaji. Jamii yetu ya wafugaji bado hawajawa na upeo wa uelewa katika matumizi ya ardhi. Sheria ni jambo ambalo lazima tujizatiti nalo liweze kusaidia katika kuhakikisha ardhi yetu tunaiwekea mikakati
madhubuti ili liweze kwenda kusaidia wananchi wake na hatimaye tuweze kuwa na maisha bora na harmony baina ya jamii zetu za watumiaji wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna migogoro ya wakulima na wafugaji lakini na watumiaji wengine wa ardhi kama wawindaji, warina asali, waokota matunda, nao itafika mahali watahitaji ardhi ya kuitumia. Tumeweka mipango madhubuti ya kupanua kilimo chetu bila kuzingatia kwamba kilimo hicho hicho kinahitaji ardhi madhubuti ambayo tutakwenda kuitumia kupanua kilimo ili tuweze kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu na kadhalika ili tuweze kuinua uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sheria ni suala muhimu sana katika kudhibiti matumizi bora ya ardhi, naomba kutoa mfano wa Wilaya ya Kiteto katika Mkoa wa Manyara. Wilaya ya Kiteto ilivamiwa na wakulima toka nje ya Wilaya na hii ni kwa sababu ilionekana kwamba Wilaya ile ilikuwa na ardhi prime, haina mwenyewe sana, kwa hiyo walikuja wakulima kutoka nje wakapasua pori wakalima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu mmoja ambaye amekuja kama kibarua, msimu unaofuata hawi tena kibarua anafyeka pori anakuwa yeye ndiye mmiliki wa shamba. Kwa hiyo, anafika mahali anawaita watu wengine 200 zaidi, analima msimu mmoja kama kibarua msimu unaofuata anawaleta 200, kwa hiyo ni 200 x 200x 200 ardhi inakuwa imekwisha kulimwa kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze kwamba, sheria huwa inafanya kazi kwa sababu wavamizi wote waliovamia mbuga mbalimbali katika Wilaya yetu tuliweza kuwaondoa kwa kutumia sheria. Kwa hiyo, sheria inafanya kazi kuhakikisha kwamba tunadhibiti matumizi bora ya ardhi kama ambavyo tumefanya kule Kiteto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, bado Kiteto kuna matatizo kadhaa. Kwa bahati mbaya Tume mbalimbali ambazo zimeundwa ili zituletee majawabu tuweze kufanyia kazi, bado hatujapata majawabu yake, naomba basi tuweze kupata maelekezo ili wananchi nao wapate utulivu katika Wilaya yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano, kwa nini naipongeza hasa Mawaziri wake? Wakati nikiwa Kiteto kama kiongozi miaka yangu mitatu ambayo nimekuwa nikipambana kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, hakuna ambaye hajasikia Kiteto kulikuwa na mauaji ya wakulima na wafugaji lakini bahati mbaya wala simteti mtu, hakuna Waziri aliyekanyaga kusaidia kutatua migogoro ile ama kuona ni namna gani tunaisaidia Serikali kuhakikisha kwamba migogoro inakwisha na watu wanaacha kupigana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi. Hapa Mvomero wamekatwakatwa ng’ombe usiku, asubuhi Mheshimiwa Mwigulu yupo pale, alipokuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo, nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia migogoro ya ardhi, Awamu hii Mheshimiwa Lukuvi ametembelea pale mara nyingi, sikumwona Waziri wa Ardhi wala wa Kilimo na Mifugo wakati ule kwa miaka yote mitatu na ndiyo maana naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano wakiongozwa na Jemedari wao Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kutatua migogoro ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti nimeona nichangie haya machache katika sekta ya ardhi, naunga mkono hoja na ahsante kwa kunipa nafasi.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi nami nichangie hoja hii iliyoko mbele yetu.

Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama mahali hapa kuchangia hii hoja, aidha niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango, Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa kutuletea bajeti ya kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni nzuri, ni ya matumaini makubwa kwa wananchi na wananchi wameipokea pamoja na kebehi zote zinazotolewa na Wapinzani Wabunge wenzetu, lakini bado wananchi wameisifia na wanakwenda kuitekeleza kwa sababu ni bajeti shirikishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mawasilisho ya Kambi Rasmi ya Upinzani, wenzetu wameibeza bajeti hii katika misingi ya takwimu. Kutofautiana kwa vitabu Volume One, Two, Three, Four ni suala la takwimu tu ndugu zangu, haiwezi kuwa suala la kihistoria kwamba bajeti hii haifai. Kuna wachangiaji wachache wametuhumu sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kujenga kiwanja cha ndege kule Chato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais wa Tanzania lakini ni Rais anayetambulika kimataifa, ni Rais anayetambulika na dunia nzima, ajenge kiwanja cha ndege mashuhuri, tena kikubwa sana kule Chato, watu wengi watapenda kwenda kuona amezaliwa wapi Rais Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu ni wa kimataifa na watu wengi wanampenda, kujenga kiwanja cha ndege ni kitu kidogo sana na binadamu hana jema…

TAARIFA.....

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, binadamu hafananishwi na mwenzake, kila mtu na mazaliwa yake, mapendo yake, juhudi zake na mambo yake tofauti, kwa hiyo siipokei hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la ukusanyaji wa fedha TRA. Mwaka jana wakati tunapitisha Sheria ya Fedha (Finance Bill) tulikubaliana TRA inaenda kukusanya kodi ya mapato kwa ajili ya mapango na kadhalika. Sheria hiyo ya Fedha, tuliipitisha hapa Bungeni wakiwemo Wapinzani ambao leo wanaikebehi. Sababu za TRA kukusanya kodi iko katika ukurasa wa 28 waende kusoma, kipengele cha 38. TRA imefanya ufanisi mkubwa sana katika ukusanyaji wa kodi na TRA ina mtandao mpana sana hapa nchini kulingana na Halmashauri zetu.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba nijielekeze kwenye kuchangia bajeti. Bajeti hii siyo tu imeanisha namna ya kukusanya mapato kwa ufanisi, bali pia imefafanua namna ya kupata, kutumia na kwa uwazi zaidi, ndio maana tunampongeza sana Dkt. Mpango pamoja na Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji. Kubwa zaidi ambalo limewapendeza wananchi ni kwamba bajeti hii imejielekeza kuwanufaisha wakulima wadogo na walalahoi wa vijijini kwa sababu inaenda kuboresha kilimo kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta pekee inayogusa wananchi walio wengi ili waweze kuendelea na kuondoa umaskini ni sekta ya kilimo. Kwa hiyo, bajeti hii inakwenda kuboresha kilimo na kuondoa umaskini katika nchi yetu na ndio maana wananchi wameipokea kwamba ni bajeti ya kihistoria na inaenda kuwanufaisha wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya 2016/2017. Bajeti hii imeainisha ufanisi, pia imeainisha changamoto, bado kuna changamoto chache. Katika miradi ya maendeleo tumeona kwamba fedha zetu za miradi zilichelewa, tuna imani kwamba Waziri wetu anaenda kuangalia kwa umakini sana changamoto ya kuchelewesha fedha za miradi, vilevile kuhakikisha kwamba zinafika kwa wakati na zinakwenda jinsi bajeti hiyo ilivyokuwa imeidhinishwa na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna mikakati ya mipango tuliyojiwekea kwamba haijakaa vizuri na hiyo nayo ni eneo la kuliangalia kwa sababu haina maana mipango yetu tuiweke mizuri lakini haiendi kutekelezwa jinsi ambavyo tumeainisha kwenye kitabu cha mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwamba ili bajeti hii iwe shirikishi tuweze kuteua kamati itakayosaidiana na Baraza la Madiwani kuhakikisha kwamba Wenyeviti wa vijiji, Maafisa Watendaji, wazee wawili, viongozi wa dini, timu kamili iweze kuundwa kuhahakikisha kama watchdogs, kuhakikisha kwamba fedha zinazokwenda kwenye miradi na fedha zinazotoka kwenye tozo mbalimbali zinazokwenda kwenye maji ziweze kuangaliwa, ziweze kunufaisha wananchi jinsi ambavyo Bunge limepitisha na kuhakikisha kwamba zimewanufaisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye kukuza uchumi. Tanzania tumebarikiwa, tunazo rasilimali nyingi, tuna rasilimali watu, Rais wetu alisema kwamba kwenye maeneo mbalimbali imesheheni maprofesa, madaktari, mainjinia lakini bado tuna tatizo la rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwajibikaji na utekelezaji wa masuala mbalimbali bado uko nyuma kwa ajili ya utendaji usio wa uaminifu, wezi na mambo kama hayo. Naamini kwamba Waziri wetu Mheshimiwa Angellah Kairuki katika eneo hilo anahusika. Yeye ni Waziri makini, aende kuangalia ni namna gani atajengea uwezo watumishi wa umma ili waweze kuwa waaminifu kuhakikisha kwamba miradi yote ya maendeleo, mipango yote inayoelekezwa katika kuleta maendeleo, suala la rasilimali watu linapewa kipaumbele kuacha hata rasilimali fedha. Kwa sababu Baba wa Taifa aliwahi kusema kwamba fedha siyo msingi bali watu ndio maendeleo zaidi na juhudi inaletwa na rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye suala zima la vipaumbele katika nchi yetu. Katika utekelezaji wa bajeti ninashauri Serikali iangalie maeneo ya pembezoni. Naomba kutoa mfano mdogo, leo hii ukamchukua mwanamke wa Kihadzabe, ukamweka pale ukampa milo mitatu, ukampa mavazi, ukampa na mafuta ya kujipaka. Upande huu ukampa mwanamke wa Kiswahili, ukampa chakula milo mitatu, ukampa mavazi, ukampa na mafuta, yupi atakayeonesha impact haraka? Ni yule ambaye hana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wetu wa Manyara tuko pembezoni sana, tuna makabila ambayo bado wako nyuma sana, tunaomba utekelezaji wa bajeti hii ilenge maeneo ya pembezoni, iweze kuwanufaisha wananchi wale wa chini sana ili na wao waweze kuona maana ya kuwa Tanzania, maana ya kuishi katika hali nzuri kuondokana na umaskini na kuondokana hali duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara tuligawanyika kutoka Mkoa wa Arusha mwaka 2002, lakini hadi leo resources nyingi bado ziko Arusha. Mkoa wetu unazalisha mazao mengi sana, mazao haya yanafaa kwa ajili ya kuanzishwa viwanda vidogovidogo. Tazama ng’ombe wengi wanatoka Mkoa wa Manyara, wanatoka Simanjiro, Kiteto, Hanang na Mbulu lakini kiwanda cha nyama kiko Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iangalie kwa umakini sana ni wapi inaenda kuanzia kwa kuweka kitu gani? Ni wapi inaenda kuanzia viwanda kwa ajili ya rasilimali zipi? Tunaomba Kiwanda cha Nyama kijengwe Babati ili tuweze kutengeneza ajira ya wananchi wetu na kuweza kunufaisha wananchi wa Manyara na wanufaike na rasilimali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie potential ya kila mahali, Mkoa wa Manyara una potential katika michezo ya riadha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze na kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uzima na kuniwezesha kusimama hapa kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu yake yote ya Watendaji kwa kazi kubwa ya kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Ukusanyaji wa fedha ni jambo moja, lakini kutumia vizuri na kwa wakati ni jambo lingine ambalo ni muhimu zaidi katika maendeleo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo yanayotumia fedha nyingi tukiacha mishahara ya Watumishi wa Serikali, lakini asilimia zaidi ya 60 hadi 70 zinatumika katika manunuzi ya umma. Eneo hili limekuwa na changamoto kubwa sana tena kwa muda mrefu na kwa miaka mingi. Manunuzi ya umma hayaendani na thamani ya fedha ambazo zinatumika katika kununua bidhaa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni wakati sasa nilitarajia kuona katika taarifa ya Waziri pia, kwamba, tatizo hili ama changamoto hii ya muda mrefu imeweza kuangaliwa kwa kiwango gani na utatuzi wake ukoje kwa sababu ni eneo muhimu sana katika rasilimali fedha ambazo hatunazo katika nchi yetu ambazo zinatosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Tunaiomba Serikali wakati inaainisha iweze kutupa ni namna gani sasa inaenda kuhakikisha kwamba, fedha zinazotolewa katika manunuzi zinakwenda sambamba na ubora wa bidhaa zinazotumika hasa katika maeneo ya ujenzi katika nyumba za Serikali zinazojengwa, na katika barabara, eneo ambalo limekuwa changamoto kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wizara ya Fedha. Tunaambiwa kwamba, takwimu zinasema hadi kufikia Februari, 2017 Wizara ilipokea shilingi trilioni 27.4 ambayo ni sawa na asilimia 3.5 tu ya fedha zote za maendeleo ambazo zimeidhinishwa na Bunge. Tena isitoshe katika hizo fedha trilioni 27 tuliona kwamba, trilioni 1.9 ni fedha za ndani na fedha trilioni 25.4 na zaidi kidogo ni fedha za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaona kwamba, hata Wizara ya Fedha yenyewe sehemu kubwa ya fedha inazotumia kwa miradi yake ni fedha za kutoka nje, hili ni suala ambalo kidogo ambalo halipendezi katika taratibu zetu za Serikali. Tunajua uncertainity za fedha za nje, fedha za wafadhili ambazo zinaweza zikakwama hapa na pale. Tunaiomba Serikali na kuishauri Serikali iweze kubuni mikakati mbalimbali ya kuweza ku-raise fedha za ndani, ili ziweze kutekeleza miradi yake ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la mafungu ya Wizara ya Fedha. Katika Mafungu nane yaliyo chini ya Wizara ya Fedha, ukisoma taarifa ya Waziri ni Mafungu matatu tu yaliletewa fedha ambazo ziko zaidi ya asilimia 60, lakini asilimia 50 na kwenda chini ndio mafungu yaliyobakia, sasa hii ni hatari. Tunataka kujua pengine ni vizuri Waziri atuambie ni nini tatizo la Hazina kuchelewesha utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi iliyo chini ya Wizara ya Fedha na hata miradi mingine ya miradi ya maendeleo katika nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imekuwa changamoto, wananchi wengi wanalalamika kwamba, kwa nini Serikali na Bunge inaidhinisha fedha za kutosha, lakini hazifiki kwa wakati na zinafika chini ya kiwangi kilichoidhinishwa na Bunge. Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 ipo sasa hivi, inaeleza kwamba ni vema fedha zilizoidhinishwa na Bunge ziweze kutolewa kwa wakati, ili miradi ya maendeleo iweze kutekelezwa kwa wakati. Hili limekuwa tatizo sugu, tunaiomba Wizara ya Fedha wakati inahitimisha ituambie ni changamoto gani ya Hazina kutotoa fedha kwa wakati, ikiwepo hata zile za kufadhili miradi ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kupata ufumbuzi wa kuchelewesha fedha za miradi, nashauri kwamba Wizara haijafanya kazi kubwa zaidi katika ukusanyaji wa maduhuli. Ukusanyaji wa maduhuli ni jambo jema, ni jambo la muhimu sana, lakini pamoja na hilo la pili ni kuhakikisha kwamba, Deni la Taifa halipandi. Vilevile kuhakikisha kwamba, thamani ya shilingi yetu haishuki. Mambo haya matatu ambayo ni jukumu la Wizara ya Fedha ihakikishe kwamba, uchumi wa Taifa unapanda, sambamba na kuhakikisha kwamba, inasimamia maeneo haya matatu ambayo nimeyaeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia isimamie kikamilifu kushuka kwa thamani ya shilingi, hili nimelizungumzia na ninadhani hilo likisimamiwa vizuri tunaweza kuwa na maendeleo ya uhakika katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, ukurasa wa 76, imeandikwa utaratibu wa mikakati ya kupunguza umaskini, inaeleza kufanya uchambuzi na tathmini ya miradi ya kuondoa umaskini ngazi ya Wilaya na vijiji. Sina hakika anamaanisha nini, lakini najua kulikuwa na MKUKUTA namba I,II na III ambazo hazikufanya vizuri sana katika nchi yetu. Pamoja na nia njema ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inaondoa umaskini baina ya watu wake, lakini bado maeneo mengi, harakati nyingi ambazo zimeainishwa na Serikali katika kuondoa umaskini hayajafanya vizuri. Nitoe mfano mdogo tu wa asilimia 10 ambayo inatolewa na Halmashauri katika kuwapa mitaji wanawake na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Halmashauri nyingi zinatoa hizi fedha kama kuondoa lawama, lakini ukiangalia kwa undani kabisa, ukienda kuulizia, hizi fedha hazijaonesha impact hata kidogo, haijulikani kapewa nani? Haijulikani riba ilikuwa shilingi ngapi? Haijulikani wamenufaika watu gani? Hata hivyo, Halmashauri zinaenda kutenga na kuzitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali katika harakati mbalimbali za kuondoa umaskini, iweze kuangalia kwa undani, iweke utaratibu mzuri na hasa tunakoelekea kupata zile milioni 50 za kila kijiji, Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila mtu ananufaika na hizi fedha ili tuone umaskini unapungua katika nchi yetu kwa nia njema ya Serikali ya kuwezesha wananchi kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie njia ambayo mimi naiamini kwamba, kwa sababu suala la utoaji mikopo, naomba labda ku-declare interest, mimi nimetoa mikopo kwa takribani zaidi ya miaka 20 kwa watu maskini na kwa ufanisi. Hivyo, naomba pamoja na nia hiyo, lakini njia ambayo ina uhakika na endelevu ni kuwawezesha wakulima, kwa sababu mkulima anaweza akalima kwa kupata fedha kuliko mtu maskini ambaye anapata mlo mmoja kwa siku, ukamwambia chukua mtaji huu kafanye biashara, hataweza kufanya biashara, atazila hizo fedha na matokeo yake hayataonekana, lakini mkulima atachanganya shughuli yake ya kila siku, atalima na ukimhakikishia soko la uhakika kwa bidhaa zake anaweza akaondoa tatizo la kipato chake, akapata mapato kwa ajili ya familia yake na hatimaye kuondoa umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo na ufugaji ndio sekta ambayo inagusa maisha ya watu wengi. Kwa hivyo, naona kwamba, Serikali ikielekeza uwezeshaji wa wakulima na wafugaji kuwapa mitaji ili waboreshe kilimo chao, si kwa namna ya mikopo yenye riba ambazo tunaziona, pale ndio mahali ambapo tunaona Serikali itaweza kuondoa umaskini kwa uhakika baina ya wananchi wake, kuliko sasa hivi kuwapa mitaji ya mikopo ambayo hatuna hakika inamlenga nani hasa, ikimlenga mtu ambaye ni maskini anayepata mlo mmoja kwa siku hatafanya kazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanyia nchi yetu. Naomba nichangie kwa kifupi kama ifuatavyo:-

(i) Mabalozi wote wa Tanzania wawe chachu ya maendeleo ya nchi yetu hasa kwenye sekta ya viwanda na biashara ili tutimize azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda. Waweze ku-connect fursa za kiuchumi ili tupate malighafi ya viwanda vyetu kwa urahisi, lakini zaidi tupate soko la uhakika la nje la bidhaa za viwanda.

(ii) Mabalozi wetu waiuze Tanzania katika sekta ya utalii. Tanzania haifananishwi na nchi yoyote ya Kiafrika, tukiacha South Africa, kwa kuwa na mbuga nzuri za Ngorongoro, Serengeti, Mlima Kilimanjaro na kadhalika. Wanyama wazuri wawe kivutio cha watalii wengi kuja Tanzania ili tuinue uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi. Kwanza mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu anayetupa zawadi ya uhai kwa wote humu ndani na kuendelea na shughuli zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sitatenda haki bila kuishukuru Serikali yetu kwa kuweka kipaumbele katika Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba inaboresha maisha ya Watanzania walio wengi. Kipekee pia na mimi nimpongeze sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwa kweli mdogo wangu na mwanangu umeweka alama katika nchi yetu, hongera sana. Pia nimpongeze Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mengi mazuri ambayo yamefanywa na Serikali yetu, ninaomba kushauri kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tatizo la vifo vya akina mama wajawazito na watoto ni tatizo sugu katika nchi yetu, miaka nenda rudi tumekuwa tukipewa takwimu za kupanda na kushuka kuhusu tatizo hili ambalo limeshindikana kabisa kuisha. Namuomba Mheshimiwa Waziri kama ambavyo tunaona anaweka alama, tunamuomba ahakikishe kwamba suala hili la vifo ambavyo siyo vya lazima vya akina mama wajawazito naomba alitafutie ufumbuzi. Kwa kuwa sekta ya afya ni sekta mtambuka, naishauri Serikali itenge bajeti kwa kila wizara kuhakikisha kwamba suala hili la vifo vya wanawake wajawazito kila mwaka tunaloambiwa na kwa kuwa changamoto zake zinafahamika zinaweza kutatuliwa, ziweze kufutwa kama ambavyo nchi yetu imeondoa tatizo la ndui katika nchi hii na hili tatizo liwe historia. Naiomba kila Wizara itenge bajeti ili kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna tatizo sugu la malaria, malaria inaua Watanzania walio wengi kuliko ugonjwa wowote hapa nchini. Ninaiomba Serikali kwa kusaidiana na fedha na wafadhili wengi ambao wanatoa fedha katika eneo hili nalo hilo eneo liweze kuangaliwa kwa sababu changamoto zake zinajulikana, zinatatulika na lenyewe liweze kufutwa ili nchi yetu iwe salama kwa ugonjwa wa malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie haraka haraka usambazaji wa dawa kwa asilimia zaidi ya 80 katika maeneo ya vijijini. Naipongeza Serikali kwa hilo, lakini inasikitisha pia kuona juhudi ya Serikali kubwa kwa kiasi hicho maeneo ya pembezoni hususan Mkoa wa Manyara, Hospitali ya Mkoa ya Mrara, Hospitali za Wilaya na vituo vya afya havina dawa za kutosha wananchi bado wanaambiwa wakanunue madawa pembeni. Tunaoimba hili nalo ulivalie njuga uhakikishe kwamba kama kuna hujuma ya aina yoyote, wahusika wote waweze kuchukuliwa hatua hadharani ili iwe fundisho kwa sababu tatizo hili Serikali imekwishalimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia huduma za Madaktari Bingwa kwa sababu nimeona kwenye kitabu cha Waziri ameizungumzia, kwanza nimshukuru kwa hilo. Huduma za Madaktari Bingwa inahitajika kwa sababu magonjwa sugu yapo vijijini, nitoe mfano wa ndugu yangu ambaye alipata mild stroke huko Kambi ya Simba - Karatu na badala ya kupewa huduma ya Udaktari Bingwa pale alipo akasafirishwa umbali wote huo zaidi ya kilometa 200 kwenda KCMC kumbe angeweza kushauriwa kwamba na hatujui kwamba aweze kupumzishwa, apewe huduma ya kwanza na baada ya hapo aweze kusafirishwa kwenda kupata huduma. Sasa hilo lilipoteza maisha na ninaomba kwamba Serikali iweze kuliona hili, imekwishaliona lakini iweze kuweka msisitizo kupeleka huduma bingwa katika maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuzungumzia pia suala zima la Wizara ya Afya kuweza kutenganishwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Michango mingi humu ndani ambayo tumeisikia, katika watu kumi pengine ni mtu mmoja amezungumzia masuala ya wanawake. Mimi nilikuwa natoa ushauri Wizara ya Afya ni Wizara kubwa sana na inameza kabisa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto. Ninaiomba Serikali ione ni namna gani inaweza kutenganisha Wizara hizi mbili ili huduma hizi za masuala ya wanawake yaweze kusambaa na ipate upana mrefu wa kuweza kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru na ninaomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia 100, nitachangia kwa maandishi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya na kuweza kusimama mahali hapa leo kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla sijaanza kuchangia na kutoa mchango wangu katika Wizara hii na mimi niungane na wenzangu Wabunge wa Mkoa wa Manyara ambao wameshachangia kusema kweli, kutoa shukrani za dhati kwa mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais wetu mpendwa katika ziara zake za hivi karibuni ametutendea katika mkoa wetu. Mheshimiwa Rais amesimamia kauli yake, yeye amesema hatabagua mpinzani kwa basis ya itikadi wala ya chama wala ya dini wala ya kabila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mfano Jimbo la Simanjiro liko upinzani na ninategemea mdogo wangu Mheshimiwa James Ole-Miliya hapa atakaposimama amshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa maendeleo makubwa ambayo ameyafanya katika Jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais tunamshukuru kwa mambo makubwa mengi lakini makubwa matatu naomba nichukue nafasi hii kumpongeza nayo; la kwanza; madini ya Tanzanite ambayo yalikuwa yananufaisha watu wengine na pengine hata nchi nyingine Mheshimiwa Rais ametuletea mfumo thabiti, mfumo rasmi kuhakikisha kwamba wanufaika wa kwanza wa madini haya watakuwa Watanzania na zaidi sana hata akina mama yeyoo wa Wilaya ya Simanjiro, hususan Mererani watanufaika na madini haya. Amesema atahakikisha kwamba ukuta uliojengwa hauwaathiri wale wanawake wanaochenjua madini haya, waliokuwa wanananufaika kidogo kidogo, bali atawatengenezea mfumo rasmi waendelee kunufaika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Rais alipokuja Mererani tulimwambia tunakuomba baba yetu tenda miujiza kwa sababu shida ya maji katika Mji wa Mererani imedumu miaka nenda rudi. Aliwaangalia wale wanawake wa Mererani wanaoswaga punda toka asubuhi mpaka jioni wakisaka maji, akasema nimelichukua hilo. Baada ya muda mfupi ametuletea mradi mkubwa wa maji wa thamani ya shilingi milioni 780, sasa hivi baada ya muda mfupi shida ya maji itakuwa historia Mererani, tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu, tulimlilia, wanawake wa Mererani walimlilia, baba tunaomba msaada sisi tukipata complication ya kujifungua tunakimbizwa kwenda Kilimanjaro KCMC ama Selian kwa kutumia magari ya polisi, tunakuomba utusaidie gari la wagonjwa. Mheshimiwa Rais bila kigugumizi, bila kumung’unya maneno aliwajibu palepale nitawaletea ambulance. Juzi amekuja kufungua ukuta amekuja na ambulance yetu mkononi, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mungu ambariki. Ni dhahiri kwamba huyu ni Rais wa wanyonge. Tunamshukuru kwa moyo wa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na haya yote si kwamba, Mkoa wetu wa Manyara uko salama kwa masuala mengi. Wilaya ya Kiteto inasikitisha kwa suala la ambulance haina. Tunaomba Wizara iliangalie hili kwa sababu, tangu nikiwa Kiteto gari la wagonjwa linakwenda kumchukua mgonjwa linaharibikia huko huko linatafutwa gari lingine. Tangu wakati huo hadi leo hakuna gari la ambulance Kiteto. Naomba hili Mheshimiwa Waziri alibebe na atusaidie katika nyanja hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nizungumzie suala la uwezeshwaji wananchi kiuchumi. Kwanza kabisa naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mtaalam wa microfinance. Nimefanya suala la kutoa mikopo kwa wanawake na vijana kwa takribani miaka 20; kwa hiyo, ninaelewa ninachosema, lakini niipongeze Serikali kwa kututengea shilingi bilioni 61.6 kama asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zetu kwa ajili ya wanawake na vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa naomba na nia yangu ya kuzungumzia eneo hili ni kuliboresha na kuhakikisha kwamba bilioni 61.6 zinaweka impact, si kwamba zitolewe tu kwa sababu sisi kama Wabunge kazi yetu kubwa ni kuhakikisha kusema kwamba hizi fedha zitoke, hizi fedha zitoke na bado ni kidogo, lakini hatuliangalii sana suala la kusema inaweka impact kiasi gani na wanufaika wanakuja kunufaika kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi 18,000 vilivyotajwa katika kitabu cha Waziri je, ni vikundi vya watu wawili wawili, watu 10, watu 30, kwa sababu, hatuna uhakika wanufaika ni wananchi wangapi. Maana vikundi hivyo ni vikundi tu vya wanawake na hatujui kama ni vikundi vya wanawake pamoja na vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iwekwe wazi, ili tuhakikishe kwamba, fedha hizi zinazotoka kwenye Halmashauri zetu zinaweka impact sahihi na zitanufaisha wanawake na vijana, na pia nadhani tuweze kujua kwamba katika wanawake na vijana, je, hawa vijana ni pamoja na vijana wa kike ama ni vijana wa kiume? Na umri wa hawa wanawake sasa unaishia wapi, ili wao wawe wanawake wanaonufaika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina wanawake wengi wakulima na wafugaji. Sasa hawa ni wale waliowekwa pembeni na mfumo rasmi wa ukopeshaji. Je, hii asilimia 10 fedha hizi shilingi bilioni 61 zinawanufaishaje wanawake wakulima na wafugaji, ili nao waweze kunufaika na asilimia hizi zinazotoka kwenye halmashauri yetu? Nadhani Mheshimiwa Waziri atakapo wind up atatueleza. Vilevile pengine si vibaya tukajua ni criteria gani inayotumika kuwapata hawa wanawake na vijana, kila mtu anaweza akakopa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hizi fedha kama ni mikopo ni lazima zifuatiliwe, katika bajeti ya ufuatiliaji, bajeti ya kuunda vikundi, bajeti ya kuweka criteria wanawake gani wakope, inajumuishwa katika hiyo bilioni 61 ama kuna bajeti ya pembeni ya kuhakikisha kwamba fedha hizi zinafuatiliwa vizuri? Na nani wanaofuatilia, ni maendeleo ya jamii ndani ya Halmashauri ama kuna kundi la watu ambao wanaweza wakafanya kazi hii kwa ufanisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tungeweza kuweka wazi suala la urejeshaji. Kama hizi fedha zinarejeshwa kwenye halmashauri sijui ni kwa nini basi tuendelee kutenga asilimia 10 kila mwaka? Fedha zinazorejeshwa naamini kwamba, kama ni mfuko wa kuzunguka ina maana kwamba ni fedha zinarudi ili ziweze kukopeshwa. Kwa hiyo, nina hakika kwamba zinaweza zikapunguza hii asilimia inayotolewa kwa kila mwaka kwa Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwa kifupi sana pia suala la Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Mbulu Vijijini; Wilaya ambayo ni halmashauri mpya ambayo tunaishukuru Serikali yetu kututengea na kutupa wilaya mpya. Hata hivyo tunaelewa kwamba suala la Makao Makuu ya Wilaya ni suala la kisheria, lakini kumekuwa na kigugumizi cha kuhakikisha wananchi wanagongana vichwa kwa sababu kila mtu anatamani Makao Makuu ya Wilaya yawe mahali fulani. Sisi wananchi hatujali wa Manyara, mimi binafsi ninayechangia, ili mradi TAMISEMI ituambie, kwamba Makao Makuu ya Wilaya ya Mbulu Vijijini yawe Dongobesh kwa sababu, kwa sensa ya mwaka 2012 ina idadi ya watu 239,637 wakati Haydom iko pembezoni sana na ina idadi ya watu 80,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa masuala haya ni ya kisheria, kama Serikali ina sababu ya kuridhisha, inataka kuweka Makao Makuu Haydom, ruksa. Ilimradi wananchi sasa wawe watulivu, taarifa hii itolewe rasmi na TAMISEMI ili wananchi wetu watulie na waendeleze shughuli zao za maendeleo badala ya kuwaza usiku kucha Makao Makuu yanaweza kuwa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nimepanga kuzungumzia kwa nguvu haya. Naendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa juhudi kubwa aliyotupa maendeleo katika Mkoa wetu wa Manyara, naomba Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu na tunamuombea Mungu azidi kumbariki, asante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii awali ya yote kabisa naomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uzima na kuweza kusimama kuchangia hoja iliyopo mbele yetu siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze ni join wenzangu kumpongeza sana Waziri wa Fedha na Naibu wake Dkt. Mpango na Dkt. Ashatu kwa kazi kubwa nzito na nzuri wanayoifanyia wizara hii ya fedha ambayo kusema ukweli ndiyo uti mgongo wa mpango ambao tunautengeneza kuweza kuinua uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichangie maeneo matatu eneo la kwanza ni katika pato la Taifa katika uchambuzi ambao tuliufanya kama Kamati ya Bajeti, niko kwenye kamati hiyo tuliona kwamba takwimu hizi tulizochambua za mwaka 2016, 2017/2018 pato letu la Taifa lilikuwa kwa asilimia saba hadi 7.2 na katika miaka yote hii tofauti ni asilimia 0.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukitizama matarajio ambayo tunayaweka mwaka 2020/2021 tunatarajia kwamba tutakuza pato letu la Taifa kwa asilimia 10 sasa tunajiuliza hizi takwimu za ukuwaji wa pato la taifa katika jinsi ilivyoainishwa imeweza kukuwa kwa ajili ya nini, kwa ajili ya uwekezaji upi ambao umewekwa na Serikali hadi pato letu limekuwa kwa kiasi hicho na tutakuza sekta hipi ama tutawekeza sekta zipi ili tuweze kufika asilimia 10 mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchambua takwimu hizo tumeona kwamba sekta ambayo haikuwezeshwa vizuri ni sekta ya kilimo, lakini tukiendelea kuchambua tunaona kwamba pamoja na uwezeshwaji duni wa sekta ya kilimo imechangia pato la Taifa kwa asilimia 28.2. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza hivi ukuwaji wa sekta ya kilimo ya asilimia 3 kwa mwaka na inachangia pato kwa asilimia 28.2 je, Serikali ikawekeza kwa hali ya juu katika sekta ya kilimo tutaweza kufikisha asilimia ngapi ya pato la Taifa, ni wazi kama itakuwa kwa asilimia zaidi ya zaidi ya tatu sasa kwa mfano sita au saba itachangia pato letu kwa asilimia zaidi ya 70. Kwa hiyo, hii ina justified ni kwanini Wabunge wengi na sisi na mimi mmoja wapo kwamba tunataka Serikali iwekeze kwa nguvu sana kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivyo kwa sababu sekta ya kilimo ndiyo inaajiri watu wengi na tunaposema pato la Taifa ni asilimia 10 basi haieleweke vizuri kama bado kwenye mifuko ya watanzania hakutakuwa na chochote watu watakuwa bado maskini, lakini tukikuza sekta hii ni wazi itafungamanisha pato la Taifa ukuwaji wake pamoja na maendeleo ya watu na kuondoa umasikini, lakini vile vile, kwa sababu ina ajiri watu wengi inaweza pia kupunguza mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naungana na wenzangu wengi ambao wanaunga mkono kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo kwa manufaa ambayo tumeitaja hapa kwamba kusema kweli tunataka kufungamanisha pato la Taifa na maendeleo ya watu wetu, watu watakuwa na hela mfukoni na umasikini wa kipato utapungua mara dufu na hivyo kujiza uchumi na wananchi wetu watasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuzaji wa sekta ya kilimo ambapo tunaambiwa kwamba sekta hii inajumuisha sekta ya mifugo na uvuvi ni wazi basi tutakapokuza sekta hii ama tutakapo wekeza kwenye kilimo sitaki kuingia details kwa sababu Waheshimiwa wengi wameizungumzia na kueleza kwamba tukuze hasa tulenge mazao gani na hapa na pale. Lakini kusema kweli naungana na wenzangu na ninaomba Waziri aweze kutuwainishia katika mwongozo wa mpango tunaoelekea kuutengeneza wa 2020/21 ni mikakati ipi mizuri ya kuwezesha sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni sekta ya Benki ambayo nataka kuchangia kwa kifupi sana vilevile, uchambuzi wa kamati unaonyesha kwamba Ma benki yetu sasa hivi yanaukwasi mkubwa sana sasa tunajiuliza kama benki zinaukwasi na hatuna tatizo ni suala la kuelekwamba ni kwanini sasa bank zinakuwa na ukwasi wakati tunatarajia kwamba pengine ukuaji wa sekta ya benki ni pale ambapo benki zinatoa mikopo unaweza kukuza wigo na kupanuka na kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kidogo halijaeleweka kwahiyo tutaomba Mheshimiwa Waziri atueleze ni kwanini kuna ukwasi mkubwa liquidity ya fedha katika benki zetu kiasi ya ziada kiasi ambacho kinatarajiwa kwa sababu tunajuwa kwamba ukuwaji wa sekta ya benki ni kule ambapo inatoa mikopo tumeelezwa katika taarifa kwamba pengine sababu ni sekta za benki kuogopa kukopesha kwa kukwepa mikopo chechefu, lakini bado si sababu za kutosheleza. Nadhani ni vizuri kuangaza macho zaidi Mheshimiwa Waziri katika sekta hiyo ili iweze kukaribisha sekta binafsi waweze kukopa na hata watanzania wenye uwezo kuweza kuwekeza na kuweza kuendeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika eneo hili nilitaka kuzungumzia riba benki, kwa miaka mingi tumekuwa tukilalamika kwamba riba inayowekwa na benki kwenye amana za wateja tunapoenda kukopa ni kiwango kikubwa sana asilimia 16 na kuendelea lakini unapowekeza fedha zako benki unawekewa riba ndogo sana ya asilimia 3 sasa najiuliza, kwa sababu nafanya kidogo ukobeshaji kwa wanawake maskini kwa hiyo, najuwa kidogo suala la ukopeshaji siendi kwenye kiwango cha benki lakini najuwa riba unapoweka katika amana za mteja unaziweka kama cost borrowing kwa mfano gharama ile ambayo una incur wakati unakopesha.

Mhesimiwa Mwenyekiti, sasa gharama ya kukopesha kwa sekta ya benki kwa mfano sisi Wabunge tukikopa benki hivi wanapata gharama hipi wanangoja tu wamekaa mezani wanachukuwa installment zile ambazo zinakatwa kwenye mishahara yetu ama hata wakopaji kutoka nje ya Bunge wanaokopa benki incur gharama yoyote kulinganisha na mteja gharama anayo incur katika kutafuta mkopo wa benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba kwa kweli suala la riba ya benki kuwa kubwa kwenye amana za wateja ni suala limepigiwa kelele kwa miaka mingi kwa hivyo tulikuwa tunaomba hili nalo liangaliwe sasa kama Serikali tunaweza tukapiga kelele miaka nenda rudi lakini hakuna kinachofanyika asilimia 16 na zaidi kulinganisha na asilimia tatu ni kiwango cha tofauti ya asilimia 13 huo ni kama unyonyaji kwenye fedha za wateja. Kwa hiyo, eneo hilo nalo liweze kuangalia kuboreshwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imelia.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi, kwanza naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia zawadi ya uzima na kuweza kuendelea na shughuli zetu hapa za kuwakilisha wananchi wetu. Kwanza kabisa naomba pia nichukue nafasi hii kuishukuru sana na kuipongeza Serikali ya Awamu Tano kwa kuwa taarifa zote tulizosomewa hapa zote zinaonesha ufanisi na hali chanya ya kuweza kuinua uchumi wa nchi yetu na hivyo tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali kwa sababu mikakati yote ambayo tumeelezwa na kamati zote ni mikakati chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, nitachangia maeneo mawili tu. Naomba nianze kwa kuchangia kwenye suala zima la mfumuko wa bei. Kunapokuwepo na mfumuko wa bei hali hii inaondoa utulivu baina ya wananchi wetu na kwa hivyo hii hasa inatokana na upungufu wa chakula nchini. Kama kuna upungufu wa chakula ni wazi kwamba kutakuwa na mfumuko wa bei. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kipindi kilichopita cha 2017/2018 na 2018/2019 kwamba mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia 5.3 hadi asilimia 3.5, kwa hivyo, ni hali nzuri. Kwa dalili tunazoziona tunamshukuru Mungu ni kudra zake pale ambapo mvua zinakuwa nyingi na hazileti madhara, lakini tunavyoangalia hali tunavyokwenda pamoja na mvua nyingi zinazonyesha lakini huenda ikaweza kuleta athari na kupunguza chakula hapa nchini. Hivyo Serikali isibweteke iweze kuona ni namna gani itajizatiti kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mfumuko wa bei na hali ya chakula itakuwa nzuri nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali pia kwa kuunda chombo cha NFRA, NFRA ni chombo ambacho ni muhimu sana katika kuweka akiba ya chakula ili kuweza kuweza kutumia wakati wa uhitaji na hata pengine kuuza nje. Hivyo tunaiomba Serikali iweze kukijengea uwezo chombo hiki ili kutekeleza majukumu yake ya kununua chakula cha kutosha na hali hii ya kuwa mazao ya kutosha inaweza ikatusaidia katika masuala matatu. Kwanza, italeta utulivu kwa wananchi watakuwa na chakula cha kutosha; lakini vilevile inaweza ikasaidia kuhamisha wananchi kuwa na soko la uhakika mahali ambapo watauza mazao yao. Chombo hiki kitakaponunua mazao ya kutosha na huko tunakoelekea kwenye Serikali yetu ya viwanda tunaweza tukatumia mazao haya haya reserve ambayo itakuwa ziada ili kutumia katika kusindika mazao ya kilimo katika kuanzisha viwanda vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii si ya kubweteka kama ambavyo nilisema lakini Serikali itenge bajeti ya kutosha kuweza kuimarisha chombo hiki cha NFRA lakini vilevile na bodi ya mazao ya mchanganyiko. Naamini kwamba connection ya NFRA na mazao haya ni kuonesha ni jinsi gani kilimo ni muhimu katika kuinua uchumi wa nchi yetu. Kwa hivyo ni vizuri Serikali nayo ikatupia jicho suala zima la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilitaka kuchangia ni deni la Taifa. Tofauti na mfumuko wa bei ambapo umepungua kwa kipindi kilichopita, lakini deni la Taifa limepanda kidogo kwa asilimia 2.1. Hili tunaambiwa imesababishwa na masuala mbalimbali moja ikiwa mahitaji ya kugharamia miradi ya maendeleo na hasa pale ambapo inatumia mikopo vilevile ahadi ya misaada kutoka nje. Tunavyojua tunazo sheria mbalimbali zinazoenda sambamba na kutumia fedha za Serikali na hivyo nilikuwa naishauri Serikali pale ambapo tunahitaji kutumia fedha hizi kwa ajili kugharamia miradi mbalimbali sheria za fedha na kanuni na taratibu mbalimbali zitakapozingatiwa na Serikali nina imani kwamba suala hili la deni la Taifa litakwenda likipungua na hasa pale ambapo Serikali itazingatia matumizi haya ya fedha za Serikali ambapo hakutakuwa na ubadhilifu na itazingatia hata mikataba ya kimataifa pale ambapo tunaona kwamba tunakiuka taratibu zile za kutumia fedha za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kuchangia mwisho mwisho ni pale ambapo unarudia michango mingine ambayo wenzangu wamesemea. Niliandaa kuchangia maeneo haya mawili na naomba sana Serikali izingatie yale ambayo nimeshauri na ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa kukupongeza sana wewe na Naibu wako kwa kazi kubwa na nzuri. Baada ya pongezi nijikite kwenye maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kilimo; hakuna Mtanzania mzalendo atakayeacha kuchangia sekta hii kwa ustawi wa Taifa letu na ustawi wa mtu mmoja mmoja. Umuhimu wa kilimo usipokuwa reflected na bajeti hii kutakuwa na tatizo kwa kuwa, ni sekta inayotegemewa na watu wengi na tegemeo kwa malighafi ya viwanda vyetu. Tunaambiwa sasa hivi Pato la Taifa limepandishwa na sekta ya madini na utalii, ombi langu kwa Serikali, tusibweteke na hali hii tuhakikishe sekta ya kilimo inaboreshwa. Kwa sasa uzalishaji unashuka. Serikali ifanye utafiti wa mazao ya wakulima wadogo, wa kati na wakubwa ili kutatua changamoto zao ambazo kwa kweli hazifanani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba pia, kwa kuwa wakulima wetu hamasa kubwa ni soko la uhakika la mazao yao, naomba wakulima waruhusiwe kuuza mazao yao nje au popote wanapopata soko. Viwanda vyetu vikiimarika tutazuia uuzaji nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wangu wa Manyara hauhitaji hata mafunzo kwa wakulima kwa sababu kilimo ni sehemu ya maisha yao. Wakipata soko la mahindi, mbaazi, maharage, vitunguu, basi kilimo kitapanuliwa na kuboreshwa maradufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifugo. Nikiri kabisa kuwa sekta hii ya mifugo haijapewa kipaumbele kinachostahili na wafugaji pia wapewe fursa ya kuuza mazao yatokanayo na mifugo. Nchi yetu imebarikiwa kuwa na mifugo mingi, lakini hatuna viwanda vya kusindika ngozi, hatuna soko la kuuza ngozi ndani ya nchi. Naiomba Serikali iruhusu uuzwaji wa ngozi ghafi nje ya nchi na pia ipunguze tozo mbalimbali zinazotozwa katika suala la uuzaji wa ngozi, hasa export levy iondolewe au ipunguzwe sana. Ufike wakati sasa Serikali nayo ione namna ya kuwaboreshea maisha wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa fursa na mimi niweze kuchangia muswada huu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.

Kwanza nami naomba niipongeze sana Serikali kwa kuleta marekebisho haya kwa nia ya kuboresha, kuimarisha na kuharakisha utekelezaji wa miradi hii muhimu ambayo kwa kiwango kikubwa katika kutekeleza sheria hii naamini itaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi ilianza kitambo siyo kwamba imeanza sasa hivi, sheria hizi pia zilikuwepo lakini kama ambavyo imeanishwa kwenye muswada sheria hizo zilifanyiwa marekebisho, lakini bado hali haikwenda kwa kasi ambayo ilitarajiwa na hivyo muswada huu sasa hivi umerekebisha yale mapungufu yote ambayo yalikuwa kwenye sheria za awali ambazo zilifanyiwa marekebisho na hivyo tunaamini kwamba sheria hii sasa inakwenda kutekelezwa kwa namna ambavyo imekwishaboreshwa, kuharakisha na kuimarisha hatua zote zitakazotumika katika kuidhinisha miradi hii ya PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi inayotekeklezwa kwa njia ya ubia inahitaji uwiano wa kiutendaji na hivyo kuhitaji sheria, kanuni na taratibu zilizo wazi na zile ambazo zitanufaisha pande zote za ubia, kwa maana ya sekta ya umma na sekta binafsi. Mlolongo wa maamuzi ya kufikia utekelezaji unapaswa kuwa na muafaka usiokatisha tamaa. Mlolongo wa kufanya maamuzi unakatisha tamaa na hasa kwa upande wa sekta binafsi, kwa hivyo naamini Muswada huu umepunguza kwa kiwango kikubwa huo mlolongo wa kufanya maamuzi ama hatua za uidhinishwaji hivyo naamini kwamba hali itakwenda kuboreka na kwa sababu hatua zile za uidhinishwaji zimepunguzwa kutoka sita hadi tatu, na mradi unapaswa kuidhinishwa ndani ya siku 21.

Mimi nimeshangaa kidogo upande wa wenzetu wa Upinzani kulalamikia kwamba siku 21 ni nyingi sana, lakini hapo hapo wanashauri Serikali iwe makini sana katika kufanya maamuzi ama kuchagua miradi ile ya unsolicited kwa umakini zaidi. Siku hizo 21 kama hatua hizo za kuidhinisha miradi hiyo unsolicited wanaona kama ni siku nyingi umakini huo utafanyika kwa jinsi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutumbuke kuidhinisha unsolicited projects nilivyoelewa muswada huu haina maana ya kwamba Waziri anakwenda kuchukua miradi yote ile ya unsolicited na kuiingiza kwenye PPP, hapana. Nilichoelewa ni kwamba Waziri mwenye dhamana atahakikisha anakwepa ile hatua ya ushindanishi ambayo itachukua muda mrefu kushindanisha hizo projects za unsolicited na kwa hivyo kutakuwa na mlolongo wa muda mrefu kuhakikisha kwamba miradi hiyo inachelewa. Kwa hiyo, hatua hiyo imefupishwa kwa sababu hakutakuwa na ushindani, hakutakuwa na kushindanishwa ile unsolicited projects, lakini umakini unabaki palepale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Wizara sasa ya Fedha, Waziri wa Fedha ambaye ndiye Waziri mwenye dhamana atakuwa makini zaidi kuhakikisha kwamba miradi itakayoingizwa kwenye PPP ni ile itakayokuwa na manufaa kwa Taifa letu na ambayo italeta tija katika maendeleo ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Waziri mwenye dhamana ahakikishe kwamba asiwatumie wataalam wale ambao waliokuwa kwenye ofisi yake na naamini kwamba kuna kitengo mahsusi cha PPP ambacho kitakuwa na Wataalam waliobobea watakaoweza kuchagua hiyo miradi ambayo itakuwa na tija, naamini hatua hiyo itakuwa imeshafikiriwa na jinsi ambavyo wenzangu walishashauri kuwe na mafunzo mahsusi, mkakati mahsusi wa mafunzo ambayo utawafanya wale ambao wanafanya shughuli hii wawe na uzoefu na ujuzi wa hali ya juu katika kuhakikisha kwamba suala hili linakwenda kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la transparency na commitment ni suala muhimu sana katika miradi ya ubia. Muswada umeweka sharti la Serikali kutoa compliance report kila baada ya robo mwaka. Naamini hii itajenga nidhamu ya bajeti ya Serikali na itahakikisha kwamba fedha zitakazotolewa kwa ajili ya mradi ya ubia zitakwenda kutolewa kwa wakati. Tunalo tatizo sugu la kutotoa fedha za miradi katika hali ya kawaida ya miradi ya Serikali, lakini basi katika hali hii ya miradi ya ubia na kwa hali hii ya kutoa compliance report ndani ya robo mwaka, naamini kutakuwa na transparency na commitment na kuhakikisha kwamba fedha zitatolewa kwa wakati ili miradi hii ianze kwa wakati, iidhinishwe kwa wakati na iweze kwenda kufanya kazi iliyotarajiwa kunufaisha maendeleo ya nchi yetu.

Mheshiiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni msisitizo wa matumizi ya mwongozo ambao Serikali imejiwekea. Muswada umeeleza bayana kwamba kuna blueprint ambayo itakuwa ndio mwongozo mahsusi utakaoweza kuongoza katika kutekeleza miradi hii. Mimi naamini hii itasaidia kurudisha nidhamu ya utekelezaji wa miradi na hivyo naipongeza Serikali kwa mwongozo huu na endelea kusisitiza kuboresha mazingira ya uwezeshaji kwa kutumia blueprint ama mwongozo uliojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona muswada pia unaruhusu uidhinishwaji wa miradi midogo ya thamani ya chini kidogo ya bilioni 46 na zaidi kidogo kutoka sekta binafsi. Naamini kwamba Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe mwisho wa siku ingawa pia tunahitaji kuwashawishi wawekezaji wakubwa kutoka nje ya nchi kwa sababu miradi mikubwa itakayotekelezwa katika nchi yetu mwisho wa siku itabaki hapa na itakuwa na manufaa kwa mfano miradi ya barabara, wawekezaji hawataondoka nayo wala miradi ya afya naamini kwamba itakuwa na manufaa zaidi. Bado wazawa wa ndani ya nchi wanahitajika pia kushiriki katika suala zima la miradi ya PPP ili na wenyewe wawe na uzoefu na hali hii ya uwekezaji wandani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima kuvutia wawekezaji kutoka nje na naamini kwamba elimu itakayotolewa itawahamasisha sana wawekezaji kutoka ndani ya nchi na kutoka nje ya nchi pia, lakini kwa hali ya kumudu kwa gharama ambayo imeshushwa ambayo imeainishwa katika muswada huu, ndiyo maana tumeona kwamba huu Muswada unakwenda ukiboresha suala zima la PPP katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali halisi tumeona pia Serikali inakwenda kusisitiza uanzishwaji wa benki hizi za uwekezaji na rasilimali. Uwepo wa Benki hizi ni sehemu mojawapo pia ya kuvutia wawekezaji wa ndani, kwa sababu TIB yenyewe haitoshelezi, kwa hivyo, naamini uazishwaji wa benki hizi zisisitizwe na ziwekwe imara ili ziweze kutumika kwa ajili ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono waliosema kuwa mkakati kabambe wa kuanzisha mafunzo ya PPP ni eneo nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ahsante kwa kunisikiliza.