Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Martha Moses Mlata (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
shukrani kwa utaratibu huu mzuri ambao unatuwezesha kutoa mchango wetu kwa wale ambao hatujapata nafasi ya kuongea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kubwa na ambayo ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo na ukuzaji uchumi kwa Taifa letu hasa kwa wananchi walio wengi. Wizara hii ndiyo pekee itakayomwondolea umaskini mkulima, mvuvi na mfugaji pamoja na wote wanaotegemea mazao yatokanayo na sekta hizi. Naomba nitoe maoni yangu kama ifuatavyo:-
(i) Ukitaka mali utaipata shambani:-
(a) Endapo Waziri utawapatia nyenzo za kisasa wakulima wako kama trekta, power tiller, jembe la ng‟ombe na kadhalika;
(b) Mbolea, pembejeo za aina zote ambazo zitamfikia mkulima kwa wakati na za kutosheleza; na
(c) Maafisa Kilimo wapelekwe vijijini kuliko na wakulima ili watoe ushauri wa kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ushauri huo, naomba Mkoa wa Singida uingizwe kwenye orodha ya mikoa inayolima mahindi kama zao la biashara ili kuweza kuwapatia pembejeo (mbegu) ya zao hili. Zao la vitunguu katika Mkoa wa Singida lipewe kiapumbele kama ni zao la biashara, pia na kupewa pembejeo. Zao la alizeti, bado wakulima wengi wanalima kwa mkono, hivyo, tunaomba trekta angalau kila Kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu matrekta ya SUMA JKT ambayo yalisaidia sana na ndiyo yaliyoinua ongezeko la kilimo kwa mazao yote, kwani yalikuwa yanatolewa kwa mkopo wa Halmashauri zilikuwa zinawadhamini wakulima na utaratibu huo uliwasaidia sana. Je, ni kwa nini SUMA JKT hawana tena utaratibu huo ambapo walishirikiana na TIB au Benki ya Kilimo?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo. Ombi langu ni:-
(i) Pembejeo ya zao la mahindi Singida;
(ii) Zana za kisasa za kilimo;
(iii) SUMA JKT warejeshe utaratibu wao wa kukopesha matrekta kwa kushirikiana na TIB kupitia Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nitoe mchango kidogo kwenye hotuba hii ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kwanza kabisa nianze kwa ku-declare kwamba na mimi ni moja kati ya wale wasanii ambao tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba sasa tunatambulika rasmi kwenye Wizara. Lakini nimesimama kwa ajili ya mambo mawili tu au matatu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kumpongeza Mheshimiwa Rais na kumshukuru kwamba nilipoingia mwaka 2005 ndani ya Bunge hili, kwa kweli kulikuwa hakuna namna yoyote au neno lolote kuanzia kwa Waziri au Mbunge aliyezungumzia suala la sanaa. Lakini tulilianzisha na hatimaye Serikali ya Awamu ya Nne ikaweza kulitambua na kuanza kulifanyia kazi. Nitoe pole sana kwa wasanii wengi ambao wamekuwa kwanza ni maarufu kwa kujitahidi wao wenyewe, wamekuwa ni maarufu kwa kufanya kazi katika mazingira magumu, lakini na wengine ambao wana vipaji wameshindwa kuendelea kutokana na taratibu ambazo hazikuwa zinatambuliwa rasmi katika mfumo ambao sasa hivi umewekwa na Rais huyu wa Awamu ya Tano kwa kweli nampongeza na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kasi kubwa ambayo wameianza sasa inayoonekana. Ninapongeza kwamba ameweza kuzindua tamasha la filamu la Kimataifa pale Arusha ambalo naamini tamasha lile ni mwanzo mzuri utakaowapa fursa wasanii wetu kutangaza kazi zao ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo, ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niseme jambo moja, Mheshimiwa Waziri kwamba sanaa haikuwa na Wizara ambayo tumeililia pamoja na wasanii wenzangu ambao tuko ndani ya Bunge hili. Kwa umoja wetu tuliweza kushirikiana kulilia ili sanaa hii sasa iweze kupewa nafasi katika Wizara. Umepewa nafasi sasa, hebu ninaomba kwa sababu inaonekana kuna wasanii ambao wanaonekana labda ni wakubwa sana, wengine ni wadogo sana au kuna ubaguzi. Mimi nataka niwashukuru sana wale watu, vyombo mbalimbali na taasisi mbalimbali ambazo ziliwasaidia wasanii wetu hadi kufikia hapa walipo kwa sababu Serikali ilikuwa haijatia mkono wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vyombo mbalimbali ambavyo vimekuza vipaji vya wasanii hata tukizungumza Diamond, Diamond amepitia kwa ndugu Ruge kwa kweli tunawapongeza, mimi binafsi kuna wasanii wengi wamesaidiwa hata tulikuwa na kina Saida Kalori walisaidiwa, wakakuza vipaji vyao. Ninapongeza vyombo hivyo kwa sababu walihangaika, ndugu Msama alijitolea kuanza kukamata kazi za wasanii ambazo zilikuwa zinaibwa, kwa sababu Serikali ilikuwa haijatia mkono wake pale, kwa hiyo mimi napongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mzee King Kiki ambaye leo tunae hapa, wazee hawa wamepata taabu kubwa, wamehangaika, Serikali haikutia mkono kule kuwasaidia lakini wameweza kufika hapa na wametangaza pia kazi za sanaa na Taifa letu, mimi ninawapongeza wote.
Lakini Mheshimiwa Waziri, tunayo mashirikisho ambayo mashirikisho haya yako manne, kuna Shirikisho la Filamu lina vitengo vyake, kuna Shirikisho la Muziki lina vitengo vyake, kuna shirikisho la Sanaa za Ufundi na Shirikisho la Sanaa za Maonyesho. Ukienda kwa mfumo huu ukapitia mashirikisho haya, hii kuonekana kwamba wasanii sasa wanatengwa, nafikiri haitakuwa na mashiko maana yake hata sasa hivi sina hakika kama umealika viongozi wa mashirikisho haya, sana sana utakuwa umeita watu wachache kuja kuwawakilisha wasanii.
Kwa hiyo, ninaomba ufanye kazi na mashirikisho haya, wao watakueleza ni nini adha na wanahitaji kufanya mambo yapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashirikisho haya yatakusaidia katika mambo mengi, kwa mfano, msanii aliyepo Kigoma, Singida au Mtwara kuwe na branches kule ambazo wao watatambulika kule. Kwa sasa hivi msanii hawezi kukopesheka pamoja na kipaji alichonacho, pamoja na kazi nzuri aliyonayo hatambuliki, lakini anapokuwa ni mmoja kati ya wanachama ambao ni wanachama katika mashirikisho haya, ninaongea kwa kifupi kwa sababu yana mapana na marefu yake lakini yatasaidia sana. Kwa hiyo msanii huyu anaweza akakopesheka kupitia haya mashirikisho, lakini unaweza ukamtambua kupitia pia kwenye haya mashirikisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la COSOTA. Ni kweli nilikusikia kwamba unasema COSOTA ihamie kwenye Wizara yako na sisi tutakuwa na furaha ikihamia kule. Sasa hivi inakusanya mrahaba kwenye vyombo mbalimbali redio, tv, magazeti na kila kitu, lakini nani anasimamia kujua msanii fulani, kuna chombo gani ambacho kinaonesha kwamba wimbo wa mtu fulani umepigwa mara ngapi, gharama yake ni kiasi gani na anatakiwa alipwe nini? Kwa hiyo, tunaomba sana kama COSOTA itahamia kwako tunaamini kabisa utaweza kusimamamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna suala la mikataba la uuzwaji wa kazi za wasanii. Nadhani kwenye mashirikisho haya uweke wanasheria watakaosimamia kazi hizi na mikataba ya wasanii. Wasanii wengi anapewa shilingi milioni 10 anaenda anagawana na wenzake inatoka lakini anaendelea kutajirika yule msambazaji. Simamia haya mashirikisho yatakusaidia kusaidia wasanii hawa waweze kupata kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kuna mmoja amesema kazi za nje. Hebu pigeni kazi za ndani lakini bado na zile zinazouzwa mitaani, sisi tunalipa sticker, tunalipa TRA lakini kuna kazi hazina sticker, zinaharibu soko la wasanii hapa nchini. Tunaomba jamani mipaka, akitaka kuuza basi waende TRA na wao wakalipe zile sticker na utoaji wa sticker uende mpaka mikoani. TRA wapunguze ule mlolongo, waende mikoani ili wasanii wote waweze kupata huduma kule walipo. Hakuna haja ya mtu kutoka Mtwara, Kigoma au Bukoba, aende Dar es salaam kwa ajili ya ku-register kazi yake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninaamini kabisa suala hili utalisimamia barabara.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala jingine nakuomba ujenge Kituo cha Sanaa. Kituo kikubwa ambacho wasanii wote watapatikana pale, watafanya kazi pale, hata kama mtu anataka kufanya nendeni kwenye nchi za wengine mkaone ni namna gani ili hata kama watu wanataka kwenda kumuona msanii fulani, wanajua tukienda kwenye kituo fulani leo kuna maonesho haya, kesho kuna maonesho haya. Lakini na wale wanaotaka kufanya filamu zao kunakuwa na eneo kubwa ambalo linakuwa limetengwa, ardhi tunayo, lakini siyo vibaya hata tukajenga kukawa na kijiji cha wasanii kule, maana sasa hivi ukweli ni kwamba wasanii bado ni maskini sana, tunalo Shirika letu la National Housing, tupeni ardhi, tujenge, dhamana ni kazi zetu, tutalipa! Ili wasanii wapate maeneo mazuri ya kuishi, tupeni ardhi. Mimi ninakutakia kheri, ninaamini na ninakuamini, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niaze kwa kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa zawadi kubwa ambayo ameitoa kwa wanasanaa wote kwa kitendo chake cha kutambua sekta hii na pia Wizara hakika tunampogenza kwa hili. Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuitambua sekta ya sanaa na kuipa Wizara Mheshimiwa Rais ameweza kupatia katika uteuzi wake kwa kumteua Mheshimiwa Nape Moses Nnauye kuwa Waziri katika Wizara hii, kwani tuna imani kubwa na Mheshimiwa Nape pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Anastazia Wambura. Tunaamini ataifikisha mbali sekta hii, suala la msingi ni kwamba Wizara hii ipewe support hasa kwenye suala la bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo tayari wameshaanza kuifanya. Pia naomba nimpongeze Waziri kwa kuzindua Tamasha la Filamu la Kimataifa la Tanzanite tarehe 23 Aprili, pale Mount Meru Hotel, Arusha. Tamasha hili lina tija sana kwa Serikali na wadau wa sanaa, kutangaza kazi zao, kimataifa. Pia litatoa ajira kubwa kwa Watanzania, litaongeza idadi kubwa ya watalii kuja Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba Mashirikisho ya Sanaa yaimarishwe ili yaweze kusaidia Wizara namna ya kuisaidia sekta hii. Mashirikisho hayo ni:-
(a) Filamu; waigizaji, waandishi wa miswada, uigizaji, wazalishaji na wasambazaji.
(b) Muziki; Muziki wa Dansi – CHAMUDATA, Muziki wa Injili - CHAMVITA, bongo flava, taarabu na rumba.
(c) Sanaa za Ufundi; tingatiga, uchoraji, ususi na ufinyanzi.
(d) Maonesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Wizara yako inayo orodha ya vyama vyote ambavyo ni wanachama katika mashirikisho yote kupitia BASATA. Hakika Mheshimiwa Waziri utakapotumia mashirikisho haya kuyawekea mkazo na utaratibu mzuri ni wazi utakuwa umeleta mafanikio makubwa sana. Kuna vyama ambavyo vimeshapiga hatua kubwa sana mfano, Chama cha Muziki wa Injili, kina matawi hadi mikoani japo si yote lakini chama kwa kupitia viongozi wake wamehamasisha na watu wengi (wasanii wa nyimbo/muziki wa injili) wamejiunga rasmi na kuna vitambulisho maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni wameweza kujiunga na bima ya afya na wanachama wengi wameweza kupatiwa kadi za bima ya afya na hivyo kunaondoa adha kubwa ya wasanii wanapougua kuanza kuomba misaada wa kuchangiwa kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu. Ninaamini utaratibu huu utaendelezwa kwa vyama vingine vilivyo wanachama wa mashirikisho husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usambazaji wa kazi za sanaa bado ni tatizo kubwa, Waziri tunaomba uingilie kati jambo hili na hasa kwenye mikataba, kwani ndipo penye uonevu na wizi mkubwa wa haki ya msanii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya adhabu ya mtu anayekamatwa na uharamia wa kazi za sanaa bado inamlinda mhalifu kwa kupewa adhabu ndogo, nayo iangaliwe upya ili kukomesha wizi wa kazi za wasanii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, COSOTA itoe maelezo ya malipo ya mirahaba kwani ni muda mrefu sasa hawalipwi. Je, ni chombo gani sasa kitapewa kazi ya kusimamia takwimu na ukusanyaji wa fedha hizi na kujiridhisa kuwa ni kiasi gani zimekusanywa na zimeenda kwa nani na je, ndicho anachostahili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, CD na DVD (mazagazaga) zinazouzwa mitaani kwa bei ya shilingi 1000, kwanza Serikali inapoteza mapato kwa sababu hazina stamp za TRA hazijalipiwa kodi. Pia zinawaumiza wasanii wetu wa ndani ambao wamepitia mlolongo mrefu sana hadi kupata stamp za TRA. Pia naomba stamp hizi ziwekwe utaratibu wa kupatikana mikoa yote. Naomba niishie hapa na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwateua Mheshimiwa Profesa Muhongo na Naibu wake Dkt. Kalemani, tuna imani nao na tunawaombea pia tutawapa ushirikiano. Pamoja na pongezi hizo pia tunawapongeza sana Viongozi Wakuu wa Wizara hii, Katibu Mkuu na Watendaji wote wanayoyafanya katika kutekeleza majukumu yao vizuri sana, hongereni sana na naunga mkono hotuba.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi nina mambo mawili ya kuomba:-
(i) Mradi wa umeme wa upepo Singida tafadhali tunaomba sana mradi huo uanze, tuna makampuni mengi yanayotaka kuwekeza huko na mengine yalishafanya tathmini ya fidia kwa wananchi na wananchi wanasubiri kulipwa fidia. Hii itasaidia sana kutuliza maswali.
(ii) Wachimbaji wadogo wa Sekerike, Hondo na Samsaru wanaomba wapatiwe umeme, pia kuna wawekezaji ambao ni ASHANTA wamezuia maeneo ambayo hawayafanyii kazi yoyote, hivyo inaleta mtafaruku sana kwa wachimbaji wadogo. Naomba Wizara iliangalie ili itende haki ya kuwapa wananchi walio tayari.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii lakini naomba tu kwanza nikupongeze kwa kazi kubwa unayoifanya na nataka nikuhakikishie kwamba Mungu yupo upande wako, upo hapo kwa makusudi ya Mungu na ataendelea kukulinda, sisi tupo pamoja na wewe. Kupitia Mwezi huu Mtukufu naamini wengi wanakuombea kwa hiyo tunaomba Mungu aendelee kukubariki, songa mbele mwanamke mwenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amerejesha imani kubwa sana kwa Watanzania. Ninasema haya kwa sababu nidhamu makazini imerejea, watu wanatulia maofisini, watu wanawahi maofisini na wanafanya kazi wanayostahili kulipwa mshahara huo, kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote tunawaamini, tunaomba muendelee kuchapa kazi lakini naomba sana mtembee kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura na wakati analihutubia Bunge, nataka nimpongeze kwa sababu anatembea kwenye yale maneno yake aliyokuwa anayasema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri sijaona kipengele kimojawapo ambacho Mheshimiwa Rais alikuwa anazungumza wakati akiomba kura na wakati anahutubia Bunge. Alizungumza sana kuhusu watu wa kima cha chini, wafanyabiashara ndogo ndogo, kina mama lishe, wauza nyanya, viazi, vitunguu, boda boda na wengine wote, nashangaa ametoka kwenye mstari hata hao boda boda sasa naona amewapandishia tozo badala ya kutembea kwenye maneno ambayo Mheshimiwa Rais aliongea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisema mgambo watatafuta kazi nyingine ya kufanya lakini hotuba ya Waziri haionyeshi kama mgambo watatafuta kazi nyingine ya kufanya kwa sababu wale mama lishe au wafanyabiashara ndogo ndogo kwenye ushuru mdogo mdogo ambao Mheshimiwa Rais alisema usio na maana utaondolewa hatujasikia, nilidhani TAMISEMI wangeleta lakini halikuonekana hili na bajeti hii iko kimya. Naomba Waziri atamke jambo kwa ajili ya wafanyabiashara hawa wadogo wadogo hasa akina mama lishe, wauza nyanya, vitumbua, wanaofukuzwafukuzwa na mgambo. Ukienda Singida pale utakuta kuna miwa, nyanya, vitunguu, karanga, tunaomba utulivu wa hawa watu ambao walisubiri sana kauli ya Mheshimiwa Rais itekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli wafanyabiashara hawa wanategemewa na watu wengi sana. Kuna watu ambao ni wafanyabiashara wanategemewa na watoto wao, wazazi wao lakini wale wanaofanya kazi kwenye viwanda wenye vipato vya chini wanategemea kupata huduma kutoka kwa hawa mama lishe ambao wanatoa huduma kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie suala la Mkoa wangu wa Singida. Waziri amesema kwamba Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo uchumi wake bado upo chini sana lakini nashangaa sana kwamba mtoto ambaye amekonda ndiye ambaye bado unaminywa. Sasa sielewi Mkoa wa Singida tumekosa nini? Ametaja reli ya kati ambayo inaenda kujengwa, akataja michepuo ya reli zote lakini akaacha kuitaja reli inayotoka Dodoma - Manyoni - Singida na reli ile ndiyo iliyokuwa inawasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Singida. Mkoa huo unategemea uchumi wake kupitia reli ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni wakulima wazuri sana wa zao la alizeti, tunategemea uchumi wa viwanda, lakini tuna mifugo, tuna kuku, tunalima viazi vitamu ambavyo hakuna mkoa mwingine unaolima viazi vitamu kama Mkoa ule wa Singida. Tuna vitu vingi ambavyo tunategemea kuvisafirisha kwa kutumia reli ile. Kwa hiyo, naomba sana aiingize kwenye hiyo michepuo ya reli nyingine alizozitaja, vinginevyo anawavunja moyo wananchi wa Mkoa wa Singida ambao wao wameinuka kwa kasi kubwa sana katika kujiletea maendeleo na wamejitahidi sana mpaka sasa hivi na nawapongeza. Kwa hiyo, naomba asiwavunje moyo, vitunguu vilivyo bora Afrika Mashariki vinatoka Singida. Kwa hiyo, namuomba sana reli hii aiweke katika list yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nizungumzie pia miradi ya zamani. Kuna miradi ambayo imekuwa ikitengewa fedha, inaanzishwa lakini matokeo yake inaachwa, fedha zile zinakuwa zimepotea. Tunafika hapa tunatenga tena fedha tunapeleka kwenye miradi mingine, hivi hatuwezi tukaanza na kitu kimoja tukakimaliza ili twende kwenye kitu kingine? Kwa mfano, ukienda Mkalama utakuta kuna mabwawa ambayo yalishaanza kuchimbwa, miradi ile haikukamilika imeachwa takribani miaka kumi sasa ipo tu na fedha zilitumika. Kuna bwawa la Mwanga, Mwangeza, Msingi, ukienda Iramba kule Urugu na maeneo mengine miradi mingine imekuwa kama magofu. Naomba fedha hizi ziende kukamilisha miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la wakulima kuna ruzuku lakini wavuvi mbona wametengwa hakuna ruzuku yoyote? Hebu ondoeni kodi kwenye vifaa vya uvuvi. Mheshimiwa Rais alisema anatamani kuona meli ya uvuvi ambayo ni kiwanda kuanzia mwambao Tanga, Dar es Salaam, Lindi mpaka Mtwara. Hebu ondoeni ushuru kwenye mafuta yanayoendeshea vyombo vya uvuvi ili muwasaidie na wenyewe maana hawana ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuzungumzia tozo kwenye utalii, wengi wamezungumza. Hivi mnataka Kenya waendelee kutupiga bao kwamba ukifika Kenya utauona Mlima Kilimajaro! Mkishaongeza na hiyo tozo ambayo mnaiweka watafika Kenya wataona Mlima Kilimanjaro wataondoka zao. Halafu tunasema tunaongeza ajira kwa vijana, hapa tunawaminya wale ambao wapo kwenye sekta ya utalii. Kwa hiyo, naomba sana kwenye eneo hili na lenyewe Mheshimiwa Waziri mliangalie.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu na suala la mikopo upande wa wajasiriamali wanawake. Amezungumza mwenzangu, akina mama wanazalilishwa sana, wengine wamevunja ndoa zao kwa sababu asubuhi anakuja kunyang‟anywa TV na mume wake anashuhudia, anaambiwa TV ikiondoka, friji ikiondoka ongozana navyo, hakuna kurejea hapa nyumbani. Kwa hiyo, naomba sana suala hili liangaliwe na hizi benki zinazohudumia akina mama ni lazima ziende kwenye mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naomba nipongeze Kamati
zote kwa taarifa walizowasilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina machache, kwanza ninapongeza kwa maendeleo
yote ambayo yamepatikana tangu uhuru mpaka sasa, maana kwa kweli tumepiga hatua
kubwa sana kwenye upande wa miundombinu ya barabara, lakini bado hata kwenye matumizi
ya simu za mikononi. Sasa hivi watu wanapata redio, mawasiliano na taarifa kwenye simu za
mkononi, yote ni maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mambo yafuatayo:-
Kwanza, nilikuwa naomba sana Wizara ihimize taasisi zinazohusika, kwamba kwenye kasi
ya maendeleo na wenyewe wakimbie. Kwa mfano, mji unapokua, miundombinu ya umeme
ambayo inakuwa imewekwa, TANESCO hawaendani na ile kasi. Utakuta maeneo watu
wameshajenga, hakuna transfoma hakuna nini, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana waendane na
kasi ya maendeleo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna suala la hawa wakandarasi wa REA. Pale Mkalama,
kuna vijana 40 ambao wanadai hela zao kwa muda mrefu, miezi mitatu sasa hawapewi.
Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba tusaidie kuhusu mkandarasi yule, wale vijana walipwe
maana anawakimbia mpaka sasa hivi hataki kuwaona.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nimepata taarifa kutoka kwa wananchi wanaolima
vitunguu kule Mkalama, kwamba kuna mtafiti mmoja amepewa leseni ili akatafiti madini
yanayopatikana pale na awaondoe wale wakulima wanaolima vile vitunguu. Ninaomba suala
hili lisitishwe mara moja, wananchi waachwe, waendelee kulima zao la vitunguu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine, Mheshimiwa Waziri nakushukuru
ulifika Singida ukaenda Tumuli ukakuta kuna wachimbaji wadogo wananyanyaswa na
wanadhulumiwa, ukaagiza tatizo lile litatuliwe, lakini mpaka sasa hivi bado wale wachimbaji
wadogo hawaelewi hatma yao. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba sana ufike pale ili uweze
kuwasaidia wale vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo tu. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii. Na mimi niungane na wengine kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Singida kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo aliamua kwa vitendo kuleta Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma. Kwa kweli ni uamuzi wa kishujaa na busara, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu yeye ndiye aliyeongoza jahazi la Mawaziri kwa maana ya Wizara zote kuja hapa. Nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista na Ofisi yake maana yeye ndiye aliyetangulia kufungua mlango kumpokea Waziri Mkuu. Kwa kweli pongezi sana Mheshimiwa Jenista kwa kuratibu zoezi hili na kuhakikisha Wizara zote zinakuja hapa
Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza haya kwa sababu Dodoma ni pacha na Mkoa wa Singida. Kwa hiyo, pacha wetu akipata neema na Singida tunapata neema kwa maana ya kwamba Wizara zote na watu wengi watakaoishi hapa Dodoma watatumia bidhaa kutoka Singida. Kwa hiyo, sisi wana Singida tumejiandaa kuleta mazao mbalimbali kwa maana ya kuku, karanga, viazi, vitunguu na mazao mengine mengi pamoja na mafuta mazuri sana ya alizeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kidogo kwamba mara nyingi Makao Makuu ya Serikali jengeni Mji uwe Makao Makuu ya Serikali. Naomba ile miradi mikubwa ya uwekezaji leteni kwenye Mikoa yenu iliyo jirani ukianzia Singida ili Mji huu ujengeke kama Mji wa Kiserikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niwapongeze Mawaziri wote. Mawaziri safari hii mmekuwa wanamgambo kweli kweli. Mmeweza kuchapa kazi hamjakaa maofisini. Sisi wenzenu tunataka tuwaambie, mnapofika mikoani hata wale watendaji wenu waliopo kule hakika wanapata hamasa ya kufanya kazi. Pia wananchi wanapoona Mawaziri mnatembelea miradi na kuangalia changamoto mbalimbali hiyo tunajijengea imani kwa wananchi kwamba Serikali yao inawajali. Pongezi sana Mawaziri wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini alikuja Singida kufungua Mradi wa REA III. Kwa kweli napongeza sana na tunawaomba wale wakandarasi wakatimize sawasawa na mkataba unavyosema ili wananchi waendelee kunufaika na mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoileta hapa nataka kusema iko sahihi kabisa, lakini nataka kushauri katika eneo moja tu. Eneo hilo ni kutokana na diplomasia ya kiuchumi inayofanywa na Mheshimiwa Rais wetu. Marais waliopita wamefanya lakini
na yeye amefanya diplomasia kubwa sana maana tumeshuhudia viongozi wakuu mbalimbali wa nchi wakitembelea nchi yetu, kwa kweli ninampongeza lakini tumeshuhudia mikataba kwa maana ya makubaliano (MoU) zikisainiwa pale Ikulu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuuliza ni nani anayefuatilia makubaliano haya kwa sababu tunahitaji kupata mrejesho kwamba ilisainiwa 20, 60 au mingapi na imetekelezeka mingapi? Pamoja na kwamba tumeona kuna mingine imeshaanza, lakini kwa ushauri wangu kwa sababu nina mfano halisi, tangu Rais wetu ameingia naomba nisitaje Marais au wakuu wa nchi ambao wameshakuja hapa kwetu na kusaini mikataba mbalimbali ni tisa, ni mingi. Kwa hiyo, nashauri kuwe na chombo maalum cha kitaifa ambacho kitaundwa kiwe chini ya Kamishna ambaye ni mbobezi katika masuala ya uchumi na diplomasia. Chombo hiki kiwe na wanasheria, wanadiplomasia, wachumi na kadhalika ili waweze kukaa kuainisha MoU hizi na kuhakikisha zinapelekea kwenda kwenye mkataba unaotekelezeka. Kamishna huyu awe anaweza kucommunicate na taasisi zote zinazohusika kutokana na MoU hizo au makubaliano hayo ili kuleta matokeo chanya ambayo yamekusudiwa na viongozi wetu husasan Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hayo kwa sababu kabla ya awamu hii alikuja Rais kutoka China na viongozi wengi pamoja na wafanyabiashara na Rais wetu akaenda. Alipofika hapa wakaingia MoUs nyingi lakini utekelezaji wake mmoja tulifika pale Beijing China wakatuambia kwamba kulikuwa na makubaliano ya ndege ya China kuja Tanzania kuleta watalii, lakini hakuna aliyeweza kujibu suala lile hatimaye ndege ile ilihamia Kenya. Hii inatia uchungu na ndiyo maana nimeshauri kuwe na chombo maalum kitakachosimamia makubaliano hayo kupelekea kwenye utekelezaji unaoleta matunda chanya katika taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, isije tukaishia tu watu kupiga picha na kumwaga wino, ni lazima tuwe na mkakati huo. Pia kuwe na library ya kutunza mikataba au makubaliano hayo. Ni nani anaweza akatuambia, je, kuna maktaba inayotunza, iko mingapi? Napenda nijue kwa miaka mitatu au minne awamu iliyopita na hii, je, ni mikataba au makubaliano gani ambayo yamefikia kwenye utekelezaji? Naomba sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kumalizia, tulipotoka ni mbali Taifa hili na Mungu wetu amekuwa akitupenda Watanzania, amependa sana Taifa letu. Naomba kusema anayefikiri na kudhani amesimama na aangalie asianguke. Kwa sababu ufalme ukifitinishwa hakuna atakayebaki salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba anayedhani amesimama na aangalie asianguke. Tusije tukawa kama wale wajenga mnara wa Babeli kila mtu akazungumza lugha yake kwa sababu walitaka kumpandia Mungu kichwani ndio maana Mungu akawasambaratisha. Naogopa Taifa hili tusije tukasambaratishwa kwa kunena na kutaka kupanda kwenye maeneo ambayo hakika sio nafasi yako. Anayedhani amesimama na aangalie asianguke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namtia moyo Rais wangu, endelea kufanya kazi, haukuja kimakosa maana kila utawala ni maridhio ya Mwenyezi Mungu. Fanya kazi tupo pamoja, kuwa mnyenyekevu mbele za Mungu na Mungu atakuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani niliwahi kusema kuna watu humu ndani wako kama hali ya hewa ya Dar es Salaam. Dar es Salaam jua litawaka leo, kesho ni mafuriko, leo ni mafuriko kesho ni kipupwe. Kwa hiyo, kuna watu ni vigeugeu, leo watasifia jambo, kesho watalibeza, leo watalalamikia jambo, kesho watalibeza. Rais wetu kama nyumba inavuja tia gundi, tia nta, endelea kuchapa kazi kwa maana mvua haiwezi kuacha kunyesha. Naomba nimtie moyo Rais wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kusema kwamba naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na sisi Wanasingida tumejiandaa sawasawa, michango mingine nitachangia kwenye Wizara zinazofuata. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia. Wakati naongea, naomba ni-declare kwamba mimi pia ni msanii wa nyimbo za injili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu mwaka 2005 nilichaguliwa kuingia ndani ya Bunge hili na nilipoingia ndani ya Bunge hili, hapakuwa panazungumzwa habari za sanaa ndani ya nyumba hii, lakini mpaka sasa hivi ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati huo kabla sijawa Mbunge tulikuwa tumeanzisha uanaharakati kwa ajili ya kutetea haki za wasanii. Kwa hiyo, nilipoingia kwa kweli niliendeleza na ndiyo maana mpaka leo hii tunamshukuru Mheshimiwa Rais ambaye ameweza kugundua umuhimu na kuingiza sanaa kwamba ni mojawapo ya Wizara maalum kabisa. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe pamoja na dada yangu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya na Katibu Mkuu. Tumeiona kwa sababu sisi tunaelewa tulipotoka mpaka hapa tulipo. Kwa hiyo, nawatia moyo muendelee kufanya kazi pamoja na kwamba bajeti yenu kwa kweli hairidhishi, lakini ninaamini kwa utendaji wenu mzuri hakika mta-perform vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Singida. Naomba nichukue nafasi hii kupongeza sana timu yangu ya Singida United ambayo imeweza ku-perform vizuri na kuweza kuingia ligi kuu. Nampongeza sana Rais wa Singida United, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Singida United, Ndugu yetu Yusuph Mwandami na viongozi wote wa Singida United walioisaidia ikafikia hapa ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe tahadhari na tangazo moja kubwa sana kwamba Dar es Salaam tunaomba mjiandae, nyang’anyaneni kombe hili, yoyote atakayepata tutunzieni. Singida sisi tunaenda kubaki na kombe hili, hamtaliona tena huko. Natoa salamu hizo.

Yah, lazima libaki Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nishukuru sana TFF. Namshukuru Rais wa TFF, Ndugu Malinzi, Katibu Ndugu Mwesiga na Ndugu Salum Madadi ambao wamekuwa karibu sana na sisi kutusaidia na kutuelekeza ni namna gani tunajenga uwanja wetu uweze ku-qualify ili mechi iweze kucheza Singida. Na sisi Chama cha Mapinduzi tumejipanga, naipongeza Kamati yangu ya Siasa ya Mkoa ya Chama ambayo wamesimama kidete kuhakikisha uwanja ule unakamilika. Nawapongeza sana, big up sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wadau tushirikiane kwa sababu Kanda ya Kati hakuna timu nyingine ya Ligi kuu zaidi ya Singida United, tuisaidie ili kombe liendelee kubaki Makao Makuu ambayo ni Kanda ya Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, pia nisisahau kumpongeza Alphonce Simbu, kijana ambaye anatoka Singida, ametupa heshima kubwa sana kwa kazi nzuri aliyoifanya na kupata medali ya dhahabu na alipoenda London Marathon ameshika nafasi ya tano, tunamtia moyo, ame-improve, tunaamini mwakani atashika nafasi nzuri na tumtakie heri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze, nimesha-declare interest, nataka niseme kuhusu jambo moja ambalo lipo mitaani sasa hivi, hasa kwenye tasnia ya filamu. Vijana wapo mitaani hawana kazi, filamu zao ambazo wamezicheza zimebaki kwenye makabati, siyo kwamba hazina ubora, lakini kuna tatizo kubwa sana ambalo nashukuru sana Wizara ilishaanza kushughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana muelewe wazi kwamba taratibu zinazotumika siyo sahihi kwa sababu ushindani umekuwa ni mkubwa. Kazi za nje zinazoingia ndani, tena zinatafsiriwa kiswahili na kazi hizi za nje zikija zikitafsiriwa kiswahili, watu wa nchi za Magharibi wanakuja kununua kwa sababu wanazungumza kiswahili. Kwa hiyo, kazi zetu sisi hazipati soko kwa sababu ya bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za ndani kutengeneza filamu moja inatumia zaidi ya shilingi milioni 18. Kuanza tu kuandika andiko kwenda kwenye Bodi ya Filamu ni shilingi 500,000, urudi COSOTA, sijui ikaguliwe, ukiigiza, maudhui, maadili, yote ni hela mpaka COSOTA, uende TRA ni hela. Process hii ni ndefu na ni hela nyingi, kwa hiyo, msanii huyu auze shilingi ngapi? Ndiyo maana unakuta soko za filamu hizi zinakuwa hazinunuliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, hizi kazi za nje wala hakuna haja ya kuwafungia watu. Wekeni utaratibu na wafuate taratibu wanazofuata hawa wa kazi za ndani. Wakishafuata, hakuna tatizo kwa sababu bei itakuwa ni moja na kazi zitanunuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie, Tanzania ni nchi ya pili kwa ubora wa kazi za filamu ikitanguliwa na Ghana, lakini kwa sababu ya gharama za uzalishaji, ndiyo maana unakuta kazi hizi hazipati wateja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumze suala la Sera ya Filamu. Sera ya Filamu kama tutaipitisha hapa itakwenda kurekebisha sheria na taratibu ambazo zitaweza kuwabana hata wale maharamia. Kwa sababu Sheria ya COSOTA sasa hivi ilivyo, mtu akikutwa na kazi haramu za shilingi bilioni moja, akipelekwa Mahakamani ni shilingi milioni tano, lakini kazi ni shilingi bilioni moja au jela miaka mitano. Obviously yule mtu yupo tayari kulipa gharama hizo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe namwamini sana kaka yangu, atakwenda kushughulikia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nashauri, kwa sababu tuna chuo chetu cha Bagamoyo lakini hatuna Chuo cha Filamu, hebu naomba hilo, bado vijana hawa hawawezi kukopesheka. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, wasanii hawa wapo takriban milioni tisa Tanzania. Afanye research ataona, ni ajira na ni kiwanda kikubwa sana kama tutawawekea mazingira mazuri ambayo Mheshimiwa Rais wetu amekusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Sera ya Filamu, Mheshimiwa Waziri aende BASATA akashirikiane nao wampeleke kwenye yale mashirikisho manne ambapo kuna Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Kazi za Ufundi, Shirikisho la Muziki na Shirikisho la Sanaa za Jukwaani. Akienda kule kuna vyama, ndiko wasanii walipo ili wawawezeshe BASATA waweze kufanya kazi na mashirikisho haya kuwasaidia Watanzania wote. Maana tukisema kazi za ufundi; wapo vinyago, wapo akina tingatinga, wapo wachoraji, kuna waandishi na watu wengine, ni kiwanda kikubwa sana! Naomba sana Mheshimiwa Waziri aende BASATA akashirikiane nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba tu nimalizie kwa kusema kwamba, hebu niwapongeze wale wadau wote ambao wamekuwa wakiwasaidia wasanii. Nianze na Ruge Clouds, Msama; wote hawa ndio wamehangaika na wasanii kufika hapa. Nakumbuka wakati tunaanza sanaa, Ruge alianza na Clouds FM kwenye chumba kimoja; lakini wasanii tulikuwa tunaenda kujibanza pale. Ameendelea kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Serikali iwe inawaangalia watu hawa ili muwasaidie waendelee kuwasaidia wasanii. Mwangalie Msama anavyohangaika kukamata kazi za wasanii, anaishia tu kuwapeleka Polisi, hakuna sheria, hakuna nini. Kwa hiyo, naomba washirikiane na wadau hawa ili waweze kuwasaidia wasanii. Kwa mfano,...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, Tasnia ya Sanaa za Ufundi ndio yenye ushiriki mkubwa wa Wasanii kuliko sanaa nyingine nchini Tanzania. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na BASATA 2006, idadi ya wasanii nchini ni milioni sita; zaidi ya milioni nne kati ya hao ni wale wanaojishughulisha na sanaa za ufundi wakiwemo, wachongaji, wachoraji, wachoraji katuni, tingatinga, wasusi, wabunifu wa mitindo, walimbwende na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali ikiwemo ya (WIPO) Word Intellectual Property Organization 2012), pia zinaonesha ni kiasi gani tasnia hii inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ajira na pato la Taifa kuliko hata madini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango huo kwa Taifa, sanaa hii haipewi kipaumbele na Serikali, hivyo kudumaza maendeleo yake. Changamoto zifuatazo ni baadhi ya vikwazo vya maendeleo katika tasnia hasa sanaa ya uchoraji. Sheria kandamizi hasa kuporwa kwa maeneo mfano, kama ilivyokuwa katika maeneo mengine ikiwemo Nyumba ya Sanaa, sasa kumetokea watu wanaotaka kupora eneo la wachongaji Mwenge, eneo ambalo lilikabidhiwa Chama cha Wasanii Wachongaji Tanzania (CHAWASATA) na Serikali ya Awamu ya Kwanza mwaka 1984. Kufuatia kuhamishwa kutoka barabara ya Ali Hassan Mwinyi Road (Zamani Bagamoyo Road) ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa mshangao mkubwa wamejitokeza waporaji wenye nguvu za kifedha wanaoshirikiana na Kamishna wa Ardhi ili eneo lile lipewe watu wengine. Jitihada mbalimbali zimefanywa na chama cha CHAWATA ili kunusuru eneo hili lisiingie mikononi mwa wanyang’anyi ikiwemo kuomba msaada kwa vyombo vya umma ikiwemo BASATA ambao kwa barua yao ya hivi karibuni walisema jambo hilo haliwahusu.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara ituambie, nani anayehusika kufuatia hali hii tete ya sintofahamu. Hali ya amani katika Kijiji cha Mwenge Vinyago ni tete na wachongaji wasingependa kulazimishwa kuingia katika uvunjifu wa amani. Jamani, naomba suala hili lipatiwe majibu ili hali ya utulivu iendelee. Naomba sana Wizara hii ambayo iko chini ya Mwanasheria Dkt. Mwakyembe aliyebobea alisimamie hili kwa nguvu zote ili haki ya wachongaji hawa isipotee na wanamtegemea sana na wana imani na Waziri na watendaji wote.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine kubwa inayokabili fani ya uchongaji ni watu wa Maliasili na Utalii ambao wamekuwa wakizuia vinyago visipite Airport hata kama vina stakabadhi halali za TRA. Hali hii imedumaza soko la vinyago toka asilimia 59 hadi asilimia 15 kitu ambacho ni hatari na hii ni fursa kwa majirani zetu hususan Kenya. Kupitia Idara ya Sanaa, watu wa maliasili wameambiwa wakae nao ili kwa pamoja wajue na kufikia muafaka, lakini bila mafanikio. Inasikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, pia kama ukifuatilia utendaji wa Mamlaka zingine hususan Tume ya Ushindani, bidhaa zote feki huwa zinachomwa zile zinazokamatwa tena hadharani, je vinyago vinavyokamatwa vinapelekwa wapi? Hatujawahi kuona vinateketezwa au kupigwa mnada ili kusaidia wenye mahitaji mbalimbali na kadhalika. Kuna tetesi kuwa, vinyago hivyo vinavyokamatwa pale airport hurudishwa Mwenge kwa mlango wa uwani. Naomba ukweli wa jambo hili na maelezo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi kwa kazi nzuri sana inayofanywa na Waziri pamoja na Naibu Waziri, bila kuwasahau Katibu Mkuu na watendaji wote, naomba nitoe ushauri kidogo kuhusu suala ambalo ninaona; kuna utata na linatesa sana wazazi wa watoto wanaohitimu kidato cha nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha nne hufanyika kila mwezi Oktoba ya mwaka, matokeo ya kidato cha nne hutoka kati ya Januari na Februari, lakini wanaopaswa kuendelea na masomo ya kidato cha tano wanasubiri hadi mwezi Julai. Hivyo, mtoto huyu ana miezi takribani nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika hii ni mateso sana kwa watoto kusubiri na wazazi kuwalinda watoto hawa ili wasije wakaingia kwenye kujifunza mambo yasiyofaa na kudumaza ari na moyo wa kusoma na uwezo unapungua. Hali hiyo, huwapelekea wale wenye uwezo kuwapeleka watoto wao pre-form five kitu ambacho kwa wasio na uwezo kinawanyanyapaa.

Ushauri wangu matokeo ya kidato cha nne yanatoka Januari ili kubaini waliofaulu, watoto wanaofaulu kuanzia alama “D” one to three, wapelekwe JKT kwa muda wanaosubiria kuanza kidato cha tano mwezi wa saba. Hivyo, kuanzia Februari hadi Juni. Wakishahitimu watapata muda mdogo tu wa kukaa nyumbani na hivyo kuendelea na masomo vizuri. Hivyo itaondoa JKT ya kidato cha sita haitakuwa na haja ya kuwepo. Utaratibu wa kuwapata vijana kwenda kwenye Majeshi yetu unaotumika utabadilika na badala yake watapata walioenda JKT moja kwa moja. Mfano Jeshi la Polisi, Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama utaratibu wa kuwapeleka Jeshi la Kujenga Taifa litaonekana halifai, basi itafutwe namna yoyote kuhakikisha muda wa kuanza kidato cha tano unasogezwa ili waanze Mei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua umuhimu wa Wizara hii na kazi kubwa sana na nzuri inayofanyika. Aidha, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoongoza Wizara hii kwa hekima na utulivu mkubwa . Pamoja na pongezi hizi naomba nimpongeze pia Jenerali Venance Salvatory Mabeyo kwa heshima kubwa aliyopewa na Mheshimiwa Rais, kwa kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, hongera sana. Kwa imani kubwa aliyonayo Rais wetu kwake ndivyo na sisi Watanzania tuna imani sana na yeye. Tunaamini ataendelea kushirikiana na viongozi wote walio chini yake na walio juu yake ili kuendelea kuwa na utulivu na amani tuliyo nayo nchini pamoja na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi pia niwapongeze wanajeshi wote kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya nchi yetu, hakika tunawapongeza kwani tunatambua kazi kubwa waliyonayo. Wakati wengine tunaendelea na shughuli zetu wao wakiwa katika shughuli nzito ya kutulinda wakati wengine tukiwa tumelala, wao wakiwa macho kutulinda. Hakika tunawashukuru sana. Tuna imani na Jeshi letu, Mungu awabariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi naomba nitoe maoni yangu kwa ufupi kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa hapa Tanzania vijana walioko sekondari na hasa wanaohitimu kidato cha nne, mitihani yao huwa inafanyika mwishoni mwa mwezi wa kumi kila mwaka. Hivyo watoto hawa wanaotajarajia kuendelea na masomo ya kidato cha tano husubiri kwa takribani miezi minane na zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hali hiyo huwa ni kipindi cha mpito mgumu sana kwa wazazi na hata watoto pia kwani mazingira yanaweza kumuathiri mtoto na kujikuta anabadili nia yake ya kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano ama wengine kuangukia kwenye tabia za ama kupata mimba au dawa za kulevya au ulevi na tabia nyingine zitakazokwamisha ndoto yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kutokana na hali hiyo, naomba nishauri kuwa watoto hawa wanaomaliza kidato cha nne, mara baada ya matokeo yao ya mitihani Wizara iandae namna ya kuwachukua watoto hawa kujiunga na JKT kwa miezi kati ya sita na mitatu ili wasipoteze muda bure na pia kutunza uadilifu na nia yao njema ya kuendelea na shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa ya mwaka 1964 (na marekebisho yake) kifungu cha 5(2) kinatoa nafasi kwa kijana mwenye umri wa miaka 16 kujiunga na Jeshi hilo; hivyo haitakuwa tatizo kuwachukua wanafunzi hawa. Kwa sheria hiyo Wizara iongee/ishirikiane na Wizara ya Elimu ili kubadili mfumo wa kuwapeleka JKT vijana wanaomaliza kidato cha sita badala yake tunaanza na wanaosubiri kwenda kidato cha tano kwani hawa wana muda wa kutosha sana kuliko wa kidato cha sita wanaosubiri kwenda vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, vijana watakaofaulu kuanzia division one hadi division three ndio waweze kupata nafasi ya kujiunga na JKT. Pia itaweza kurahisisha kuwapata wanaotaka kujiunga na Majeshi yetu kama Polisi, Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Wananchi na kadhalika kuliko utaratibu wa sasa unaotumika kuwasaka mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho najua jambo hili linaweza kuonekana ni gumu sana, lakini ninaona manufaa yake ni makubwa zaidi, kwani tunaokoa Taifa letu na nguvu kazi pamoja na wasomi na tunapata waadilifu zaidi kwani watoto hawasahau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naunga mkono hoja asilimia mia moja.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami pia naomba niungane na wasemaji waliotangulia, lakini nampongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kututeulia ma-DC ambao tunaamini watakuja kuungana na kaulimbiu ya Hapa ni Kazi Tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana jirani yangu hapa kwenye kijiji chetu cha Maisha Plus, kwa sababu katika kiti hiki alipoteuliwa Mheshimiwa Lucy Mahenga kuwa DC, nilimpongeza na katika kiti hiki pia naomba nimpongeze kwa kustaafu na nimshukuru sana kwamba alikuwa ni DC mzuri katika Wilaya yetu ya Iramba. Hakika tutamkumbuka na tutakumbuka yale mazuri yote aliyotufanyia. Nawapongeza ma-DC wengine kutoka Mkoa wa Singida, waliostaafu na wengine ambao wamepangiwa vituo vingine, basi nawatakia kheri huko kwenye majukumu yao mengine mapya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nami pia naungana na wenzangu kumpongeza Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria kwa kutuletea marekebisho haya. Niende moja kwa moja kwenye sheria ya elimu. Kifungu cha 60 (a) ambacho kinatamka wahusika wa adhabu husika kwamba anayesaidia, anayeshawishi na anayeacha mwanafunzi wa Shule ya Msingi au Sekondari kuoa au kuolewa watapata adhabu hiyo ambayo imeainishwa hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado napata mashaka kidogo kwenye kipengele hicho labda Mwanasheria Mkuu tusaidie ili uongezee. Je, anayesaidia ambaye anashindwa kutoa ushirikiano wa kumpata hasa ninamtaja huyu mtoto wa kike; mtoto wa kike anaweza akapewa mimba halafu asimtaje aliyempa mimba ama kwa sababu ametishiwa ama kwa sababu amedanganywa kwamba mwenzako akifungwa utakosa mtu wa kukutunza. Kwa hiyo, mtoto yule anakaa kimya, hataki kutoa ushirikiano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba sheria itamke, ni nini hasa ili huyu mtu aweze kutoa ushirikiano huyo. Pamoja na hayo, sheria ituambie wazi, kwa sababu huyu mtu anapoenda kufungwa miaka 30, nilikuwa nashauri kabla hajaenda jela hebu tunaomba mtusaidie kabla hajaenda jela aache ametoa fidia kwa huyu mtoto ambaye amempa mimba ili fidia ile iendelee kumsaidia huyu mtoto. Kuwe na alternative kwamba atakayeweza kutoa fidia ile, basi angalau kuwe na unafuu wa ile miaka ya kutumikia jela. Hata kama ana mali, basi zile mali zitaifishwe ili apewe huyu mtoto ambaye amepata ujauzito kwa ajili ya kulea mimba na kwa ajili ya kulea mtoto ambaye anatarajiwa kuzaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la DNA. Ni kweli kwamba DNA pia tunaomba ifanye kazi, wataalamu watusaidie. Ninavyofahamu ni kwamba DNA ni mpaka mtoto azaliwe. Je, inawezekana kabla mtoto hajazaliwa ili tuone ni namna gani mtu anapohukumiwa asije akatumikia kifungo wakati hajahusika na kosa lile? Tumeshuhudia China kuna mtu alinyongwa kwa kubaka, lakini baada ya miaka 30 hivi akagundulika kwamba siye yeye aliyebaka na tayari alikuwa ameshanyongwa. Kwa hiyo, naomba hilo sheria itusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilikuwa nataka kuzungumza kuhusu ile Sheria ya Matunzo. Sheria ile ilikuwa inasema kwamba matunzo ni shilingi 100/=. Hivi bado inatumika hiyo shilingi 100/=? Wakati ule shilingi 100/= thamani yake ilikuwa kama shilingi 100/= ya sasa hivi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana sheria hiyo kama haijaletwa, basi iletwe ili iweze kurekebishwa kwa sababu hakuna shilingi 100/= inaweza ikanunua kitu chochote kwa ajli ya matunzo ya mtoto ambaye anakuwa amezaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba elimu itolewe. Sheria hizi tunapopitisha, wananchi wetu vijijini hawapati elimu ya kutosha, matokeo yake wananyanyasika wakati wana haki ya kuweza kutumia hizi sheria ili ziwasaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa naamua kesi moja kwamba mwanamke anataka kumwacha mume kwa sababu tu amemchoka, lakini mwanaume anamwambia ukinipa talaka wewe, wewe ndio unapaswa kunifidia mimi. Yaani sheria za ajabu ajabu kule zinatolewa. Kwa hiyo, naomba sana sheria hizi ziweze kutolewa elimu kwa wananchi wote ili wote wajue waweze ku-enjoy na sheria hizi nzuri ambazo tunazipitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia sheria zifanye kazi. Tunapitisha sheria hapa lakini kuna manyanyaso makubwa sana ambayo yanapita. Kwa sababu juzi tu nilikuwa naangalia kipindi cha TBC namna ambavyo mtoto amenyanyapaliwa na baba yake. Hivi hawa wanaume wanaokataa kuwalea watoto wao, wanawakimbia, wanawatelekeza, sheria inasemaje? Vile vile bado kuna wanawake wanatelekeza watoto wao, sheria inasemaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana pia tuangalie upande huo ili wote waweze kuchukua majukumu yao kwa sababu mtoto yule wameamua kumleta wao duniani na ni lazima alindwe; lakini mtoto wa kike alindwe zaidi na isiwe tu kwa sababu ya wale wanaosoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema chini ya miaka 18, maana sheria naona inamtaja sana matoto aliyeko shule, lakini kuna watoto wengine wanamaliza Darasa la Saba, haendelei, anabaki nyumbani mama au baba wanajitahidi kwamba wanamtafutia mahali pa kwenda, kabla hujapata namna ya kumsaidia, majamaa yameshaingia, wameshampa mimba mtoto na wanaingia mitini. Kwa hiyo, naomba sheria hii imtaje na mtoto ambaye hajafikisha umri hata kama hayupo shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi pia kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu alipolihutubia Bunge letu aliona udhaifu na mapungufu ya sheria hii ya manunuzi na ndio maana leo nashukuru Mawaziri wetu wametuletea ili tuweze kuirekebisha kwa manufaa ya Taifa letu. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa nia yake njema ya kuokoa na kuondoa vichaka maana yake sheria hii ilikuwa ni vichaka kwa watu ambao sio waadilifu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya pongezi hizo mimi sitakuwa na mengi sana kwenye sheria hii kwa sababu sio mtaalamu sana kwenye mambo ya sheria ya manunuzi lakini kuna maeneo mengine ambayo ninaona nitoe ushauri hasa kwenye upande wa afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukachanganya hii Sheria ya Manunuzi pamoja na manunuzi ya dawa za binadamu, huwezi ukalinganisha tender ya pembejeo za kilimo au tender ya kutengeneza barabara au tender ya kuagiza vipuli na dawa ambazo zinatumiwa na binadamu. Ninazungumza hivyo kwa sababu sheria hii imekuwa ikichukua muda mrefu sana katika masuala ya uagizaji wa dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea haya labda nideclare interest kwa sababu mimi nilikuwa mjumbe wa Bodi ya MSD, ninafahamu matatizo makubwa ambayo MSD wanayapata namna ya kuagiza dawa kwa kufuata Sheria hii ya Manunuzi. Tender itatangazwa mwezi wa tatu lakini mpaka sasa ukienda bado hata wale ambao wamepata award kwa ajili ya kuleta labda dawa bado kabisa mlolongo ni mrefu, apate zile awarded letter,aje aende apate mkataba, aende kwa AG maana yake na zile kanuni naona walizirekebisha lakini bado hazisaidii aende kwa AG, atoke pale afanyiwe vetting, akitoka kwenye kufanyiwa vetting arudi sasa aende kutoa order na akitoa order dawa ile ikatengenezwe kule kiwandani ni miezi mitatu, kwa sababu MSD wana nembo yao kwa hiyo ni lazima watoe order kiwandani ili zile dawa zitengenezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri hili mliangalie msichanganye hii Sheria ya Manunuzi ya dawa za binadamu na manunuzi ya vitu vingine, ninaomba sana hili mliangalie. Mnaweza mkawa mmeliweka kama mlivyoliweka, lakini hebu mtakapokwenda nendeni mkaangalie na kama mkiona kuna uzito wala msisite lileteni tena hapa ndani ili tuokoe maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninazungumza hayo kwa sababu mimi ninaelewa kwanza kabisa dawa asilimia 80 zinatoka nje, lakini makampuni mengine yanatoka nje yanakuja ku-register dawa hapa, yanapo- register dawa yanasubiri MSD atangaze tender, MSD anapotangaza tender wao kazi yao ni kuvizia na unakuta wana- tender kwa bei ya chini lakini huwezi kujua hata hizo dawa wanakwenda kuzinunua wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa ninaomba sana tuliangalie suala hili na ushauri wangu ni kwamba kuwe na utaratibu kwanza ninashukuru kwamba makampuni ya ndani yanapewa kipaumbele, mimi kwa kweli ninashukuru. Lakini utekelezaji wake, mimi ninawaamini sana Waheshimiwa Mawaziri na watendaji wenu na ninaamini kupitia ile kauli mbiu ya hapa kazi tu. Lakini ninaamini pia kwa kauli mbiu ya kutumbuliwa majipu, nilikuwa ninaomba sana kauli ya utumbuaji majipu uendelee kuangalia ni namna gani makampuni ya Kitanzania hayanyanyaswi. Kwa sababu makampuni ya Kitanzania yananyanyaswa na makampuni ya nje wanakuja na bei za chini kwa kisingizio kwamba Watanzania wananunua vitu vya bei ya chini. Lakini matokeo yake dawa zinazoletwa zinakuwa ni fake wala sio bora kwa Watanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba sana tuangalie bei, lakini lazima uangalie na ubora wa kile kitu unachompelekea Mtanzania hasa kwa afya yake. Kwa hiyo hilo ninaomba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu hatuna viwanda vya kutosha vya madawa tunategemea viwanda vya nje, nilikuwa naomba makampuni ambayo yanakuwa registered hapa Tanzania ya wazawa au ya nje, wao wawe ni mawakala au ma-agent wa viwanda fulani kule nje ili MSD anapotoa tenda kwa kampuni ile bado atoe copy kwenye kiwanda ambacho yule mtu amesema atatoa zile dawa. Kwa sababu walio wengi wana cheat, watasema kwamba dawa zile wanaenda kuzitoa labda tuseme Malaysia, India au whatever, lakini bado unaweza ukakuta wapo Keko pale wanatengeneza dawa pale, wanaziingiza MSD wakijifanya wamezitoa nje kumbe zile dawa ni fake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilikuwa naomba kuwe na mahusiano kati ya viwanda ambavyo vimetambuliwa na nchi yetu ambavyo vinatu-supply dawa ili wale ma-agent, wale bidders watuambie zile dawa wakipata tender watakwenda kununua wapi lakini bado copy iende ili tupate bei iliyo sahihi ambayo sio ya kudanganya.Kwa hiyo, mimi niliona nizungumze tu kwenye eneo hili wala sikutaka kuzungumzia sana maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba niungane na wale ambao wameendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, pia nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Kabudi pamoja na

Mwanasheria Mkuu ambao kwa kweli wameonyesha uzalendo mkubwa wa kuweza kusimamia mabadiliko na marekebisho haya kwa manufaa ya nchi yetu ambayo Mheshimiwa Rais amekusudia kuwasaidia Watanzania kutoka mahali walipo ili uchumi wa Taifa hili uendelee kupaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana wewe mwenyewe umeona watu wameshindwa kumpa jina Rais wetu, kuna wengine wanaamua kumtoa kwenye Chama cha Mapinduzi wanataka wamweke kama yeye, hii inaonesha ni namna gani wamemkubali na wana imani naye. Nawapongeza sana na tuendelee kumuunga mkono kwa sababu tumekubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inanikumbusha wale wanafunzi walipomtembelea Yohana gerezani, Yohana akauliza aliposikia habari za Yesu nendeni mkamuulize je, ni yeye yule au tumtazamie mwingine? Yesu akawaambia, kamwambieni kwamba matendo na yale yote mnayoyaona nendeni mkamweleze yote. Watanzania wameyaona matendo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wana uhakika kwa matendo tu, inaonesha ndiye ambaye anakuja kulitoa Taifa hili mahali ambapo tumekuwa tukinyonywa hasa kwenye upande wa uchumi na mabepari. Kwa hiyo, tuendelee kumuunga mkono kwa nia yake hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wengine wameonesha wasiwasi wao kwamba, kwa nini mamlaka makubwa yaende kwa Rais, nataka kusema wananchi tayari walishampa mamlaka, lakini kumbukeni yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi letu la Tanzania, tumemwamini kumkabidhi Jeshi hatuwezi kushindwa kumkabidhi rasilimali za nchi yetu, kwa hiyo, lazima tuendelee kuwa na imani naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba nizungumzie kuhusu Madini House; tumeona kwamba pamoja na mrabaha utaokuwa unalipwa bado kutakuwa na dhahabu ambayo itakuwa inapelekwa Benki Kuu. Hii naiunga mkono kwa sababu kwanza itaongezea thamani ya pesa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Madini House naomba madini yote yapite pale, lakini bado naomba wachimbaji wadogo ili waweze kunufaika kama Rais ambavyo amekusudia, pale kuwe na utaratibu wa kwamba Serikali kama ambavyo inaweza ikanunua mahindi kutoka kwa wakulima, ijipange pia kuwe na utaratibu wa kununua yale madini hasa dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo. Hii itawasaidia sana wachimbaji wadogo wasiweze kuibiwa, kwa sababu wanakuja wale wachuuzi wananunua kwa wachimbaji wadogo, wao wanatorosha madini yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii itaisaidia sana nchi yetu kwanza kuhifadhi dhahabu ambayo ni nyingi ambayo itasaidia kukuza uchumi wa Taifa letu. Nikiangalia kuna wakati tulikuwa tunapita kwenye migodi yetu, tunakuta wale wachimbaji wadogo wameshika dhahabu mikononi wanaenda watu wanazinunua ndio hao wanaoenda kupita kwenye njia za panya. Kwa hiyo, naomba sana uwepo utaratibu huo ili wachimbaji wetu waweze kunufaika kama Mheshimiwa Rais ambavyo ameunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hili kwa sababu natambua shida ambazo tunazo kule kwa wananchi wetu; bado tunahitaji maji, bado tunahitaji madawa, bado tunahitaji watoto wetu waweze kukaa kwenye madarasa mazuri na hii itakwenda kusaidia. Nampongeza Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono.