Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwanne Ismail Mchemba (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Charles Mwijage, Mbunge na uongozi wote wa Wizara. Pongezi za pekee kwa Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la kufufua viwanda. Naomba Serikali ifufue Kiwanda cha Nyuzi Tabora kwani kiwanda hicho ni cha zamani, pia ni mitambo ya kizamani ambayo imepitwa na wakati. Ni vema Serikali ikamshauri mwekezaji kuagiza mitambo mipya ya kisasa. Serikali ikajiridhishe kuona kama kweli mitambo ipo, isiwe wameihamisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa majengo yaliyojengwa na Serikali ambayo alipewa mwekezaji ameshindwa hata kukarabati, ni vema apewe mwingine. Kukosekana kwa viwanda Mkoa wa Tabora ni kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora, kusababisha ongezeko la uhalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Maziwa, niiombe Serikali kuwawezesha wawekezaji wa ndani ambao uwezo wao ni mdogo kimtaji kama vile mwekezaji anayemiliki Kiwanda cha Nyamwezi. Kukosekana kwa mitaji hiyo, pia kumechangia kufungwa kwa kiwanda hicho mara kwa mara, pia kufanya wafugaji kukosa mahali pa kupeleka maziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kutafuta wawekezaji ambao wanaweza kuweka kiwanda cha kusindika asali kwani Tabora ni centre ya mikoa jirani ambayo nayo wanayo asali kwa wingi kama vile Katavi, Singida na Kigoma. Hivyo basi, ni rahisi kwa mwekezaji kupata mahitaji ya kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Tumbaku, naishauri pia Serikali kuleta wawekezaji Mkoa wa Tabora ili zao la tumbaku lisindikwe kwa urahisi na kuondoa usumbufu kwa wakulima. Pia wananchi wa Mkoa wa Tabora kupata ajira na mikoa jirani kuliko ilivyo hivi sasa ambapo mazao yote hupelekwa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke nguvu zote kwa kuwezesha bajeti ya viwanda vidogo vidogo (SIDO) kupewa fedha za kukuza uchumi kwa wajasiriamali, kwani SIDO imefanya kazi kubwa hapa nchini, imefanikisha kutoa elimu kwa wananchi wengi hapa nchini kwa kada mbalimbali hasa wanawake. Ofisi za SIDO zipewe vitendea kazi kama vile magari, vifungashio vya elimu ambavyo hujifunzia wajasiriamali hapa nchini.
Ombi langu kwa Serikali isaidie kiwanda cha SIDO ambacho hutengeneza sabuni, kusindika karanga, pia mikopo midogo midogo kilichopo Tabora; tumbaku ipewe kipaumbele kwa kutafuta wawekezaji kwani hulimwa Mkoa wa Tabora kwa 60%. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami kwa jioni hii ili niweze kutoa mawili, matatu, lakini ili kuweka record sawa jina langu sahihi naitwa Mwanne Ismail Mchemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo leo wa kuwa hapa na kuweza kupata nafasi ya kuchangia. Naanze na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya kuhusu suala zima la sukari. Nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sukari tusiliangalie hivi hivi tu kwa lele mama, sukari inaathiri jamii nzima ya Kitanzania na ndiyo maana wanakamatwa sasa hivi kwa sababu ya laana ya Mwenyezi Mungu. Sukari hiyo inapofichwa inaathiri watoto, wagonjwa, wazee, wajawazito lakini siyo hilo tu kwamba eti kwa sababu ya mwezi wa Ramadhani, hawazidi kwa sababu ya mwezi wa Ramadhani; mpaka hivi leo ninavyokwambia kuna watu wanafunga. Kwa hiyo, inaathiri sehemu kubwa. Nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri; nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kazi nzuri wanayofanya. Imeonyesha tangu walivyoteuliwa kwamba hawa watu wanatosha. Ni tumaini langu kwamba Wizara waliyopewa ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia. Maradhi ya wanawake yako mengi sana, ni vyema Wizara sasa ikaangalia kutoa kipaumbele kwa maradhi ya akinamama. Kwa mfano, kansa ya mfuko wa uzazi kwa wanawake ni tishio, ni balaa! Kuna kansa ya matiti nayo pia ni balaa! Kuna ugonjwa wa fistula, huo nao ni muziki! Watu wengi wanaachika kwa sababu hiyo. Bado elimu haijawafikia walengwa hususan vijijini. Vile vile kuna uvimbe kwenye tumbo la uzazi la wanawake; namwomba Mheshimiwa Waziri, magonjwa kama haya yapewe kipaumbele na kutoa elimu hususan vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza MEWATA. Mheshimiwa Waziri naomba Kitengo hiki cha akinamama walionesha ujasiri, MEWATA nadhani Serikali ingewapa support kubwa sana. Wamefika mpaka vijijini; ni Madaktari Bingwa ambao wamejiamini kuwasaidia wanawake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anaye Daktari, anajua umuhimu wa timu ya Madaktari wa MEWATA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, wodi za wazazi haziridhishi. Naomba wodi hizi ziangaliwe, zipewe kipaumbele, kwa sababu kuna matatizo makubwa, hususan vitanda vya kuzalia. Vitanda vya kuzalishia vijijini havipo? Anaambiwa tu kaa hapa, jipange na nini, wewe mama unajua, kwa sababu shule hii umeipitia, ni kiwanda nyeti. Kwa hiyo, naiomba Serikali kupitia mama yangu hapa iliangalia hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende moja kwa moja kwenye ukarabati wa majengo katika Hospitali ya Kitete, Tabora. Tuna matatizo! Kuna miradi ambayo ilishaanza, lakini haijakamilika. Naiomba Serikali ikamilishe miradi hiyo ili angalau sasa madhumuni ya kile chuo kuwepo yaonekane. Kuna wodi ambazo zipo hazijakamilika, nazo ni za akinamama, naomba Mheshimiwa Waziri, nilichangia kwa maandishi, lakini ziangaliwe pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la mashine ya kufulia nguo. Jamani, ile sasa hivi ni Hospitali ya Rufaa, hatuna mashine ya kufulia nguo na iliyopo ni ya zamani ukilinganisha na population ya watu sasa hivi, inahudumia Wilaya saba na wagonjwa wale wanakuwa referred kwenda pale, lakini mashine hakuna. Siyo hilo tu, pia uchakavu wa jiko, miundombinu yake ni ya tangu Ukoloni. Inawezekana hata mimi nilikuwa sijazaliwa bila shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaangalia, kwa sababu kuna watu wengine ambao wanatoka vijijini, hawana ndugu, lakini ameletwa pale kaachwa kwa sababu hakuna sehemu ya kuweza kusubiri wagonjwa. Kama chakula kitaandaliwa vizuri, basi hata wagonjwa wetu watapata nafuu. Kwa hiyo, uchakavu huo ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uchakavu wa jengo la wagonjwa, sijui wanaitwa wagonjwa wa akili, sijui lugha gani nzuri…
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wenye matatizo ya akili, ile wodi ya miaka mingi! Miundombinu yake hovyo, hakuna vyoo, yaani wale tusiwa-dump, wale nao ni wagonjwa kama wagonjwa wengine. Magonjwa haya hayana kuchekwa, mtu unaweza kupata ugonjwa huo au akapata ndugu yako. Kwa hiyo, naomba nchi nzima kuwe na mradi maalum ambao unaweza kutembelea wodi hizo. Ni tatizo kwa kweli! Ukienda pale yaani mpaka utawaonea huruma, wale hawakupenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba na kusisitiza, wodi ya Kitete ya Kichaa, yaani ya wagonjwa wa akili, kwa kweli iangaliwe vizuri ili waweze kupata msaada, hawakupenda. Kwa hiyo, nilikuwa nataka nilisisitize hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuzungumzia makazi ya wazee. Makazi ya wazee, nachukulia ya kwangu Mkoa wa Tabora kwa sababu nimezungukia, hayafai jamani. Tunaita makazi ya wazee lakini yalikuwa ya aina mbili; kuna wale ambao walikuwa na ugonjwa wa ukoma, waliambiwa wasitiriwe wakae mahali pamoja kwa ajili ya matibabu. Kuna wazee ambao hawajiwezi, nao makambi yao yapo, lakini huduma yao hafifu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, huduma kwa wale wa makambi ya wenye ugonjwa wa ukoma, wale jamani vifaa vingine vinafanya kazi. Ni wazima! Wamezaa na wanazaana na kuna watoto na wajukuu. Kwa hiyo, kama mna hesabu ya wazee, basi wapo wengine kwa sababu kazi ile wanafanya bado. Kwa hiyo, wanazidi kuzaana. Ukienda Kambi ya pale Ipuli kuna watoto wadogo, kuna vijukuu vipo mle. Kwa hiyo, naomba wasihukumiwe kwamba ni wazee, lakini bado mambo mengine wanaendelea nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Sheria ya Ndoa. Tumeambiwa kwamba Sheria ya Ndoa inafanyiwa marekebisho, lakini mpaka ikifika kufanyiwa marekebisho, akinamama wameumia, kwa sababu sheria ile inasema unapodai fidia ya mtoto, unalipwa sh. 100/= kwa sheria ya zamani. Kwa hiyo, akinamama wanateseka. Sheria hiyo pia gharama za fidia kwa akinamama wajane napo kuna matatizo wanapokwenda Mahakamani. Kwa hiyo, naomba pia sheria hii iangalie pia na mazingira ya wajane na mazingira ya watoto, kwa sababu ndoa zinapovunjika watoto wa mitaani wanakuwa wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba suala hili la sheria hii ya mwaka 1971, Mheshimiwa Waziri ashirikiane na Mheshimiwa Waziri wa Sheria ili iweze kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Maafisa wa Ustawi wa Jamii. Kwa kweli naomba wapewe vitendea kazi; wanunuliwe basi hata pikipiki ili waweze kuzunguka vijijini. Kama tunasema bajeti finyu, lakini hawa watu hawawezi kufanya kazi inavyotakiwa, inakuwa ni ngumu sana kwa sababu hawa watu ndio tunaowategemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nizungumzie kuhusu Benki ya Wanawake, nawapongeza. Benki ya Wanawake ni mwanzo, tuliianzisha mwaka 2009. Walioanzisha Benki ile kwa kusaidiana na Serikali walikuwa Wabunge wa wakati ule, walichangia sana. Nampongeza Mama Chacha kwa kazi nzuri anayofanya ila tuendelee kumwomba kwanza riba ipungue, lakini waende mikoa yote na ndiyo ilikuwa azma yake, kwamba wafungue madirisha kila mkoa ili angalau watu waende kwenye dirisha kwenye mabenki yale wafaidi, lakini sasa hivi wanafaidi upande mmoja tu na ndiyo ambao wanapata mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo asilimia 10, naomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu nayo hiyo huduma ya wanawake iko kwake, hatupewi, asilimia 10 haifiki! Kwa sababu kinachotakiwa, kweli sisi ni Madiwani kwenye maeneo husika, lakini inapofika kwamba bajeti finyu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitangulize shukurani za pekee kwa kupata nafasi hii kwa muda huu wa asubuhi. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kunifikisha siku hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kwa kutanguliza pongezi lakini nitachangia kwa kuanza na TAMISEMI na badaye Utawala Bora. Tuliponadi sera mwaka 2015 tulikuwa na wasiwasi mkubwa sana kuhusu Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu wakati anazunguka Tanzania nzima alinadi na alikuwa na uhakika bila uwoga. Kwa hiyo, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumpongeza huko niseme alisema hivi, naomba Watanzania wenzangu mnipe nafasi niweze kuongoza nchi hii kwa uchungu niliokuwa nao na Watanzania kwa umaskini wao. Sasa hiyo ilitia mashaka kwamba watu wangemnyima kura kwa sababu alisema atapambana na mafisadi, bandari, rushwa na ubadhirifu wa aina yoyote katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi kwa sasa kiongozi huyo ametimiza matakwa yake kulikuwa na wasiwasi wakati ule kwamba angenyimwa kura lakini alisema itakavyo kuwa na iwe lakini niwatendee haki Watanzania wangu. Hivyo basi, nichukue nafasi hii kumpongeza sana, naomba aendelee hivyo hivyo, jina lake kubwa na Watanzania wana imani kubwa naye.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpongeze Makamu wa Rais, mwanamke anaweza na amejipanga. Pamoja na kwamba ni mwanamke ameweza kuzunguka nchi nzima, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hilo tu, nawapongeza sana Mawaziri pamoja na Manaibu wote wasiogope, kazi wanayofanya wananchi wanaiona na wanamsaidia Rais ipasavyo. Mawaziri hawa wanafanya kazi kiasi ambacho hata sisi tunaona na tunawapenda na tunawaamini kwamba watafanya kazi hiyo hadi miaka mitano na 20 ijayo. Wasiogope kama mahali pa kutumbua majipu watumbue haiwezekani hata kwenye Halmashauri Rais akatumbue majipu wao ndiyo watumbue majipu hayo kama walivyoanza na watumishi hewa, walikuwepo kweli lakini Mheshimiwa Rais anawatumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze Marais waliotangulia wa Awamu zote Nne kazi waliyofanya imeonekana mpaka tumefika hapa leo. Kwa hiyo, nawapongeza sana Marais wote, Rais wa Awamu ya Nne kazi aliyofanya imeonekana na leo Mheshimiwa Rais ameipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia kuhusu TAMISEMI. Kazi kubwa tumeifanya kwenye Kamati kwa sababu na mimi ni Mjumbe wa Kamati hii, kwa hiyo niwapongeze Waziri wa TAMISEMI na Naibu wake kwa ushirikiano waliotuonyesha lakini ninayo machache ya kuongezea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi ya Awamu ya Kwanza na ya Pili ya TASAF ambayo haijakamilika. Kwa sababu iko chini yao naomba waikamilishe ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wenzangu wamezungumzia kuhusu posho ya Madiwani, kweli ni ndogo. Naomba yatolewe maelekezo kwa sababu posho anayolipwa Diwani hailingani na kazi anayofanya, pesa yao ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, hawa nao waangaliwe kwa jicho la huruma. Watu hawa kazi wanazofanya wanatuwakilisha pia sisi Wabunge tuliomo humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 10 inayotengwa na Halmashauri zetu na Manispaa haijatiliwa mkazo pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu aliizungumzia alipokuwa Lindi. Asilimia 10 inatolewa kama zawadi wakati si kweli. Ningemuomba Waziri asichoke, asisitize, atoe waraka mgumu ili watu wajue kwamba ni haki ya Watanzania wote kupata asilimia 10 bila kujali itikadi za watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika vikundi hivyo vinavyopata hiyo asilimia 10 ningeomba Serikali iangalie vikundi vya akina mama wajane. Fedha hii wanapewa tu vikundi vyote lakini kuna vikundi ambavyo vimesajiliwa vya akina mama wajane navyo viangaliwe kwani wanatia huruma kwa sababu wengine wamenyimwa haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, hata hii shilingi milioni 50 ilenge pia kwenye vikundi hivyohivyo ambavyo vipo lakini mkisema kwamba vianzishwe harakaharaka kuna vingine vitaanzishwa ambavyo havistahili kupewa. Ningeweza kuchanganua sana lakini kwa sababu ya muda naomba niseme asilimia 10 haitolewi kama inavyotakiwa. Mtu anatoa asilimia 2, asilimia 3 kama mfano tu. Kwa hiyo, naomba Wizara husika iweze kutia mkazo katika jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu ukusanyaji wa mapato. Tulishazungumzia sana kuhusu masuala ya minara, mabango, ushuru huo umeachiwa tu wananchi, wao wamepata mwanya wa kwenda kukusanya kule kodi zao lakini wanapeana kienyeji mno, sheria ya Halmashauri ingeweza kutumika katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bima ya afya, kuna vituo vingine vya afya na zahanati zake havina umeme na bado REA haijafika. Naomba katika maeneo hayo basi kuwe na utaratibu wa kuweka solar.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Naomba Mheshimiwa Waziri azisaidie ofisi zote ambazo ziko chini yake, Tume ya Utumishi na kadhalika, kwa mfano, Idara ya Kumbukumbu za Nyara za Serikali, asipotimiza hili nalolisema nitaishika shilingi ya mshahara wake. Tulitembelea eneo hilo tukakuta wafanyakazi wako katika mazingira magumu sana, hakuna AC, kuna chombo ambacho kimeharibika takribani miaka miwili inahitajika shilingi milioni 26 tu lakini mpaka leo haijatolewa. Sehemu ile ni nyeti, ina kumbukumbu nzuri za Taifa hili ambazo ni za kizazi na kizazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tulitembelea masuala ya TASAF III, tumekwenda Kigoma, Mwanza, watu waliopewa sio walengwa na hawa wote wako chini ya TAMISEMI. Ofisi zao ziko chini ya TAMISEMI, watendaji wako chini ya TAMISEMI, wamepewa ambao sio walengwa. Kwa hiyo, nashauri pia hili nalo liangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, Tume hizi za chini ya Ofisi ya Rais mpaka leo zinapanga na wanalipa kwa dola, ni hasara. Ni vyema Serikali ikajipanga wawe na majengo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niiombe Serikali inapofanya marekebisho mbalimbali ya kupandisha vyeo, mishahara iende sambamba na kupewa pesa zao. Kuna watu wamepandishwa vyeo lakini mpaka wamekufa hawajapata hela zao na hao walioachiwa sio rahisi kufuatilia. Kwa hiyo, ucheleweshwaji wa ongezeko la mishahara nayo ni kero kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu uhamisho. Uhamisho unapotolewa ni vyema basi uambatane na pesa inayokuwepo kwenye bajeti. Kama tusipofanya hivyo ina maana bado tutaendelea kuwa na madeni na malimbikizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsate kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo hotuba ya Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa siku hii ya leo. Lakini kubwa nimpongeze Waziri wa Fedha na timu zake zote kwa kazi nzuri waliyoifanya. Kwa kweli hotuba nzuri na mwelekeo wa bajeti hii ni mzuri, angalau unaweza ukapunguza makali ya umaskini wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hotuba ya Waziri wa Fedha nimeona kuna asilimia tano ya mapato ya Halmashauri zetu nchini ambao huwa wanatenga asilimia 10 vijana asilimia tano na wanawake asilimia tano.
Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mimi nikuombe, chonde chonde asilimia hii tano ni ya miaka dahari na dahari iko pale pale tunaondoaje umaskini na tunapunguzaje umaskini? Lakini kama tuna nia ya dhati ya kupunguza umaskini; katika hotuba yako umesema ongezeko la makusanyo ya mapato yetu limeongezeka kwa kutokana na haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mianya ya rushwa imezuiliwa, wafanyakazi hewa mshahara wake upo umeingia kwenye mapato, wakwepaji kodi ambao walikuwa wanakwepa mpaka kuingiza makontena hela yake ipo, mapato ya gesi na cement viwanda vyake vipo. Mimi nikuombe Mheshimiwa kwa heshima na taadhima kubwa hebu muangalie sekta hii ya waakina mama na vijana ajira haipo, lakini tunapobana tu asilimia tano umekuwa wimbo wa Taifa na Halmashauri hizo asilimia kubwa hawakidhi viwango vya kupeleke hii asilimia 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri, yeye kwa huruma yake atusaidie kwa hilo ili angalau sasa aongeze kwa njia moja au nyingine anavyoona yeye inafaa kwa mapato haya mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie shilingi milioni 50. Kuna Mbunge mwenzangu hapa amezungumzia; kwa sababu tukiipeleka kwenye SACCOS moja kwa moja yatarudi yale ya Mfuko wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, kwa sababu wajanja wote ndio wenye SACCOS, vijijini kule hawana SACCOS, sasa inakuwa ni masharti makubwa kiasi ambacho watanuafaika watu wachache. Mimi nadhani Serikali ina wataalamu wazuri wa maendeleo ifanye utaratibu isifanye haraka ya kusambaza hela kupitia SACCOS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Wenyeviti wa Mitaa, tuna Makatibu tarafa Wakuu wa Wilaya ndio wanaohodhi eneo la kijiji chote. Mimi ningeomba kabla hamjafanya maamuzi ya kupeleka kwenye SACCOS mimi naomba pesa hizi ziende kwa utaratibu wa vijiji, pia kila Jimbo wapewe maana ndiyo tupo shuleni sasa, ya kwanza ilipita free, sasa hii maadamu tunaipigia sasa; na kwa kuwa Rais hakutoa ahadi mijini, amepita kwenye kampeni yake vijijini kote pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais; isiwe kwa kuwa wale wa mjini kwa sababu ndio wenye SACCOS nyingi wapate, vijijini ambapo hakuna wakose. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba hilo liangaliwe sana kwa sababu tuna mengi ya kuongea, lakini niombe hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine afya. Mheshimiwa Waziri wa Fedha mimi niombe katika fedha za mwaka huu Wizara ya Afya tuna miradi mingi ambayo haijakamilika, tuna zahanati nyingi zimejengwa na zina hospitali ambazo zimejengwa hazina theatre, kuna wafadhili wamekuja wameweka vifaa vyao hivi mnawaambiaje? kwa sababu kila mwaka watafuatilia pesa zao ziko pale lakini mnasema daktari wa usingizi hayupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kama Zahanati ya Bukene Mawaziri wote wamepita pale wameiona waakina mama wanakufa, hivi unapunguzaje vifo wakati ipo tayari vifaa vya kisasa ambavyo hata Muhimbili hawana, Bungando hawana vipo pale kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na mtoto. Kwa hiyo, mimi niombe kipaumbele Wizara ya Afya iangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nimeangalia kitabu hiki katika kupunguza kodi, kuondoa misamaha bado hujatoa misamaha kwa nguo za akina mama, kwa lugha nyingine mataulo yao bado sijaiona. Kuna wanafunzi wanashindwa hata kununua pedi, leo hakuna uondoaji wa kodi. Mimi ningeomba Serikali hata hii inapata kigugumizi gani kutoa iondoe kodi ili angalau viweze kuingia kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nizungumzia tozo nyingi za tumbaku. Hivi unaweka tozo nyingi za tumbaku halafu unasema unamsaidia mkulima? Mheshimiwa Waziri wa Kilimo liangalieni hili mnapokaa kwenye Baraza la Mawaziri, tozo ni nyingi hazifai, wakulima wanazidi kuwa maskini, kilimo chenyewe cha mkono lakini hawapati msaada wowote kutoka Serikalini. Mimi naomba Serikali iangalie sana suala zima la tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pamoja na hayo sekta hii imetengwa haisaidiwi na Serikali, hawa wanunuaji wa tumbaku wanajipangia wenyewe bei, wanaamua juu ya soko wanavyotaka wenyewe. Waziri wa Fedha utapataje ongezeko la pesa ikiwa wakulima wa tumbaku wananyanyaswa ambao asilimia 60 ya tumbaku wanayolima inasaidia mapato ya Serikali? Kwa hiyo, hilo nalo ningeomba Serikali muangalie tuna hali ngumu sana huku wakulima wa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee habari ya maji. Ukigusa umegusa wanawake, akina baba wote humu mnafuliwa nguo na akina mama, mnapikiwa na akina mama, lakini wao ndiyo wanahangaika na maji. Leo hakuna bajeti inayoeleweka ikaambiwa kwamba hii ni bajeti ya maji. Mheshimiwa Waziri, mimi nimesikia sana hotuba zako, umesifia wanawake, umewaonea huruma wanawake, sasa huu Mfuko wa Maji Vijijini toka kwenye 50, weka kwenye 100 hili suala usisumbuke...
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Waziri na Naibu Waziri Engineer Ramo Makani, Katibu Mkuu na watumishi wote kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie uharibifu wa misitu kwa uvamizi wa wafugaji kwani kila wanapofika sehemu hukata miti yote. Kwa mfano, Kizengi, Bukene, Urambo, Bukumbi, Kitundo na kadhalika. Pia ukataji miti kwa kuchoma mkaa ni tatizo hivyo Serikali iangalie upya sheria zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji nyuki, elimu itolewe kwa wajasiriamali ili wafuge kisasa kwa kutumia mizinga ya kisasa. Wajasiriamali hasa wanawake wakopeshwe mizinga ya kisasa kwa bei nafuu. Kuanzisha kiwanda cha kusindika asali kama ilivyokuwa zamani kwani Tabora ina historia ya kurina asali. Pia kiwanda hicho kinaweza kutumika kama Kanda ya Magharibi, Singida, Tabora, Kigoma na kadhalika kwa kusafirisha nje ya nchi pia kusindika nta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Chuo cha Nyuki tuombe chuo hicho kitambuliwe rasmi ili wanafunzi hao wanapohitimu mafunzo haya wapewe ajira kwani mpaka sasa ajira zao ni za kujitegemea, ni vyema sasa ajira hizo zilingane na vyuo vingine. Wanachuo hao wapewe vitendea kazi kama vile mizinga ya kisasa ili wakatoe elimu darasa maeneo mengine. Ukarabati wa chuo hicho niombe uendelee kwani maeneo mengi ni machakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya makumbusho; katika Mkoa wa Tabora katika Kata ya Kwihara kuna makumbusho ya kihistoria ya kumbukumbu za Dkt. Livingstone, Stanley, Said Ibin Batuta, waliokuwa watu maarufu kihistoria. Ni vyema eneo hilo pia likatangazwa kama utalii. Pia kuna majengo ya Ujerumani ambayo yana historia, ni ya maajabu. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWANNE I. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Balozi, Dkt. Augustine Philip Mahiga, Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara yetu iangalie sana mipaka yetu ambayo ina vichocheo vingi na ambavyo wahamiaji haramu hupenya hasa kwenye mipaka ya Kenya na Tanzania kwa kupitia njia za Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko ya ujirani mwema; elimu itolewe. Hapa nchini kuna wafanyabiashara wadogo ambao wanasafirisha bidhaa zao kama mahindi, mpunga, kahawa, chai ili wafanye biashara kwa weledi, kwani mikoani hakuna elimu ya kutosha. Waheshimiwa wetu ambao ni Wabunge wa Afrika Mashariki wapewe uwezo wa kuzunguka nchi nzima kutoa elimu hata mashuleni na vyuoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utumishi; Wizara hii iwasiliane na Wizara ya Mambo ya Ndani kuongeza Watumishi wa Uhamiaji ili ajira iongezeke na kusaidia kulinda mipaka yetu kwani mpaka sasa bado watumishi hao ni wachache. Pia suala la utalii Waheshimiwa Mabalozi watangaze vivutio vyetu vilivyopo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia maneno mawili, matatu hususani kuhusu viwanda na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini nitoe masikitiko yangu makubwa, kama leo Baba wa Taifa ingekuwa kuna jambo la kusema anaweza akasimama akauliza, angeuliza habari ya Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora tuna mateso sana, tulikuwa na viwanda vifuatavyo kwa sababu ni dakika tano lakini nilikuwa nimejipanga kwa dakika kumi ningeeleza nadhani leo Mheshimiwa Waziri yangemuingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tuna Kiwanda cha Nyuzi na Mheshimiwa Riziki amesema, kiwanda hiki kimehujumiwa na wawekezaji. Wamechukua kila kitu hata kama tunakwenda kwa science na teknolojia wameondoa vifaa vyote na wametapeli, mimi ninasema kwa lugha nyepesi, wametapeli. Tangu wamechukua hawajafanya chochote; kwa hiyo hata tukisema zao la pamba liweze kuimarishwa hakuna, tulikuwa tunatengeneza nyuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti lakini tuna Kiwanda cha kusikitisha sana cha Manonga, Mheshimiwa Waziri anajua kipo Igunga. Kiwanda hiki alikuwa amechukua Rajan. Mimi mwaka 2006 nikiwa Mbunge niliwahi kuuliza swali, lakini huyu mwekezaji Rajan amefariki, wamechukua watoto wake, bado kuna usumbufu mkubwa tangu mwaka 1999 kiwanda kile kimefungwa. Ni uchungu mkubwa sana wa unyanyasaji wa Mkoa wa Tabora. Lakini pamoja na hayo, Mheshimiwa Waziri anajua, tulimuomba awakutanishe Rajan pamoja na Igembe Nsabu, hajafanya hivyo na alitoa ahadi ya kwenda kuongea nao, nina uchungu sana, inasikitisha na inakatisha tamaa.
Mheshimiwa mwenyekiti, si hilo tu, Mheshimiwa Waziri alisema katika Bunge lako hili wakati tunauliza swali na alisema wawekezaji wa Kichina wameishia airport, sasa hivi mpaka leo bado wameishia airport? Inasikitisha, leo nipate majibu kama kweli wawekezaji hawa wapo au hawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vya kutafuta wawekezaji Tabora inayo, jinsi ya kuiuza Tabora ipo. Tuna masuala ya tumbaku, tuna masuala ya urinaji wa asali. Hivi asali yote inayotoka nchi nzima hii inatoka Tabora bado hakuna uwezekano wa kuweka kweli? Mheshimiwa Waziri, namheshimu sana naomba aangalie hilo.
Mheshimiwa Mweyekiti, lakini nizungumzie habari ya mazingira. Tabora inalima tumbaku, lakini hawa wanunuzi hawana mpango wa kuhakikisha mazingira endelevu yapo katika Mkoa wa Tabora. Kwa nini nasema hivyo? Wanabeba mbegu za miche, wanatupa kuwapa…….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.